"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, March 18, 2017

MEZA YA BWANA, NA KUTAWADHANA MIGUU.

Moja ya maagizo muhimu ambayo Bwana wetu Yesu Kristo aliyatoa kwa wanafunzi wake na kwa kanisa kwa ujumla ni kitendo cha kushiriki meza ya Bwana, pamoja na wakristo kutawadhana miguu na mengineyo yakiwemo ubatizo , na wanawake kufunika vichwa vyao wakiwemo ibadani. lakini leo tujifunze  hayo mawili ya kwanza.

MEZA YA BWANA:
mathayo 26:26-28" Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu
27 Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;
28 kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. "
Tukisoma pia...
 Yohana 6:52-56" Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?
53 Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.
54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.
57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.  "
Tunaona kuwa haya ni maagizo ya Bwana kwa kila mkristo kushiriki meza ya Bwana kikamilifu.

FAIDA ZA KUSHIRIKI MEZA YA BWANA IPASAVYO:
 
1. Kuitangaza mauti ya Bwana hata ajapo; 
1wakoritho 11:26 inaeleza umuhimu wa jambo hili kwamba tunapoumega mkate na kukinywea kile kikombe tunaitangaza mauti ya Bwana katika miili yetu wenyewe, hii inamaana kuwa tunakubaliana na lile jambo la kufa na kufufuka kwa Bwana Yesu pale msalabani vivyo hivyo na sisi tunayachukuwa yale mateso ya Bwana Yesu katika miili yetu( kwamba tunakubali kudharauliwa, kuchukiwa na hata kuuawa kwa ajili ya yake kama yeye alivyouawa).hivyo picha ya Kristo inajengwa ndani yetu wafilipi 1:29"Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; "2timotheo 2:12" Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; " Kwahiyo Huko pia ndiko kutangaza mauti ya Kristo.

2. Tunauimarisha uhusiano wetu na Mungu:
 1wakoritho 10:16" Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?
17 Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.
18 Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu?
19 Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu?
20 Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani.
21 Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani. "
kwa mistari hii inaonyesha kabisa kuna mahusiano makubwa ya rohoni kati ya mtu na Bwana, pale anaposhiriki meza ya Bwana. Kama tu vile mtu anapokwenda katika madhabahu za mashetani na kula vitu vya mashetani ni dhahiri kabisa nguvu za giza zitamwandama huyo mtu, vivyo hivyo pia na kwa mtu anayeshiriki meza ya Bwana anashiriki pia neema ya Bwana na baraka za Bwana, na roho za unyemelezi za shetani kama roho za magonjwa, hofu, n.k. Mungu anazifukuzia mbali maana Bwana Yesu alisema mtu asipokula mwili wangu na kuinywa damu yangu hana uzima ndani yake.(yohana 6:53). kwahiyo tunapoula mwili wake na kuinywa damu yake tunakuwa na uzima ndani yetu kila siku.

3. Kupokea ufahamu wa kulielewa NENO la Mungu zaidi:
luka 24:13"
13 Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili.
14 Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia.
15 Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.
16 Macho yao yakafumbwa wasimtambue.
17 Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.
18 Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?
19 Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;
20 tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha.
21 Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo;
22 tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema,
23 wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai.
24 Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona.
25 Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!
26 Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?
27 Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.
28 Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele.
29 Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao.
30 Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
31 Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao.
32 Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko? "
tunaona hapa umuhimu wa jambo lingine tena kuwa  watu hawa wasingemtambua Bwana kama wasingeumega mkate, vivyo hivyo na sisi kwa kufanya hivyo Mungu anaachilia Roho ya kumjua yeye na Neno lake vizuri siku baada ya siku pale ambapo tulikuwa hatumuelewi vizuri tunapata ufahamu mpya wa kumwelewa vizuri, hivyo ni muhimu kwa kila mkristo kushiriki meza ya Bwana.

JINSI YA KUANDAA:

Vitu vinavyohitajika ni  mkate usiotiwa chachu( yaani usiotiwa hamira), na uwe ni unga wa ngano, Ni vizuri kutumia ngano ambayo haijakobolewa iliyosagwa japo kwa mazingira ya sasa hivi ni ngumu kupata ngano ambayo haijakobolewa isiyochanganywa na chochote hivyo unaweza ukaenda tu masokoni kununua ngano na kwenda kuisaga mwenyewe mashineni kama wanavyosaga unga wa mahindi nusu kilo/kilo moja inatosha kwa matumizi ya muda mrefu, kwahiyo wakati unaanza kuandaa chukua unga mkono mmoja(sasa inategemea na idadi mnaokutanika kushiriki) idadi inapaswa iwe ni watu wawili na kuendelea haiwezekani kushiriki peke yako, kanisa ni kuanzia watu wawili na kuendelea.
ukishapima unga mkono mmoja, tia mafuta yoyote mazuri ya kupikia kama kijiko kimoja (wengi wanapenda kutumia mafuta ya mizeituni), lakini kwa huku kwetu yanayopatikana sana ni ya alizeti, kisha tia chumvi kidogo, kisha weka maji kidogo halafu kanda kama vile unavyokanda chapati, (angalizo : usitie hamira wala vyombo unavyotumia visiwe na hamira vioshe kabla haujatumia).

ukishamaliza kukanda sukuma kama unavyosukuma chapati, usipoteze muda mwingi katika kukanda na kutengeneza umbo, maana unavyozidi kukawia unga utaumuka kutokana na hamira ya asili hivyo jitahidi kuwa haraka kidogo. ukishamaliza tia jikono usiweke chochote tena baada ya kuuweka jikoni, acha kama dakika mbili tatu, ili uwe mgumu wa kuvunjika ukishaiva toa. Na mkate wako utakuwa upo tayari.

Divai inayohitajika ni ile ya mzabibu, na sio fruto au juisi ya zabibu hapana, kilichotumika kushiriki kwa mitume na kanisa la kwanza ni divai(yenye kiwango fulani cha kileo ndani yake). Kama utahitaji divai hizi zinapatikana kila mahali hapa nchini kwetu, zinaitwa "Alter wine". zimetengenezwa maalumu kwa ajili ya kushiriki meza ya Bwana, ukinunua utaona zimechorwa alama ya msalaba na zimeandikwa "Alter wine".
Kwahiyo baada ya kuandaa mkate wako na divai mkishakwisha kushukuru mnaweza mkaumega kama Bwana alivyoagiza muda wa jioni ni mzuri zaidi.(tazama picha yake hapa chini)


KUTAWADHANA MIGUU:
Yohana 13:3-17" Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu,
4 aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni.
5 Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga.
6 Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi?
7 Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye.
8 Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami.
9 Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia.
10 Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote.
11 Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi.
12 Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea?
13 Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo.
14 Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.
15 Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.
16 Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka.
17 Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda. "
Maagizo hayo yanajitosheleza kabisa kwamba yatupasa sisi kutawadhana miguu hii inaonyesha picha ya unyenyekevu na kujishusha jambo hili linapuuziwa sana na watu wengi na katika makanisa lakini ni la muhimu sana na faida zake ni nyingi, unaposhika miguu ya mwenzako na kuiosha mambo yote na sababu zote mbaya ambazo shetani ameziweka za uadui baina yako na ndugu yako zinayeyuka, utashangaa ghafla chuki na ndugu yako inapotea, wivu, masengenyo, kutokumjali kunapotea na jinsi utakavyofanya mara kwa mara ndivyo upendo na mahusiano yanavyozidi kuongezeka zaidi na zaidi.
si ajabu leo tunakosa umoja wa Roho kanisani baina ya ndugu, kwasababu tumeyaacha maagizo kama hayo kila mmoja na mambo yake, mkristo mmoja hamjui mwumini mwenzake kanisani. matabaka kati ya maskini na matajiri yanakuwepo kanisani ni kwasababu hakuna mtu anayetaka kujinyenyekeza kwa mwenzake, Bwana Yesu alisema mkiyajua hayo heri ninyi mkiyatenda, kama Bwana wetu alituosha sisi miguu inatupasaje sisi?? tunapaswa tufanye haya zaidi na zaidi.
Kwahiyo mambo haya mawili makuu (kushiriki meza ya Bwana na kutawadhana miguu), sio lazima yatendeke tu kanisani hata nyumbani tunapokusanyika katika Bwana iwe ni wawili au watatu au wanne, n.k. jambo hili linaweza likatendeka. Na tukizingatia haya hali zetu za kiroho zitazidi kuimarika pamoja na upendo kati ya ndugu na ndugu.

Mungu akubariki.