"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, June 20, 2017

BASI MUNGU AKAMUADHIMISHA SANA..

Waefeso 1:20 ".......akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; 21 juu sana kuliko UFALME WOTE, na MAMLAKA, na NGUVU, na USULTANI, na KILA JINA LITAJWALO, wala si ulimwenguni humu tu, BALI KATIKA ULE UJAO PIA; 22 AKAVITIA VITU VYOTE CHINI YA MIGUU YAKE, akamweka awe KICHWA juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo 23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote. 
Pia 1Timotheo 6:16".....yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, MFALME WA WAFALME, BWANA WA MABWANA; 16 ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, AMEKAA KATIKA NURU ISIYOWEZA KUKARIBIWA; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. HESHIMA NA UWEZA UNA YEYE HATA MILELE. Amina. "



Ndugu Bwana YESU KRISTO alivyokuja hapo mwanzo, sio sawa na sasa hivi alivyo, mwanzoni alikuja katika hali ya utumwa akaishi kama sisi tulivyo, lakini alijinyenyekeza akawa mtii kama maandiko yanavyosema, hivyo basi Mungu alimwadhimishia akamweka juu ya vitu vyote, kwahiyo tufahamu tu jambo moja yule sio mtu wa KAWAIDA KABISA, NI MIALE YA MOTO!!!, toa yale mawazo unayodhania kuwa ni mtu fulani wa kuchukuliwa kawaida, Malaika wenye nguvu na wakuu wa mbingu wanatetemeka mbele yake, ameketi katika mbingu za mbingu asikoweza kufika mtu huko hata malaika!! unaweza ukatengeneza picha ni mtu wa dizaini gani huyo??..Hivyo tuwe makini sana tunapomzungumzia au tunapomtaja huyu MFALME MKUU WA KUTISHA, tuwe MAKINI, tuwe makini!!!.. sio mtu wa kawaida ni MUNGU YULE! 

Wafilipi 2:7 "bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; 8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. 9 Kwa hiyo tena MUNGU ALIMWADHIMISHA MNO, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; 10 ILI KWA JINA LA YESU KILA GOTI LIPIGWE, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; 11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba. "

Tunaona  maandiko hayo yote yanadhihirisha ukuu alionao Bwana Yesu Kristo sasa hivi, usikae ufikirie kuwa ni mtu wa kawaida kama wengi wao wanavyomwona kwenye maigizo na tamthilia. Kumbuka VITU VYOTE na SHUGHULI ZOTE za MBINGUNI, DUNIANI na KUZIMU zipo chini yake, Hakuna chochote kinachofanyika bila idhini kutoka kwake, liwe ni jambo zuri au baya.

Tena Hakuna malaika yoyote anayeweza akaamua jambo lolote kwa namna yoyote pasipo idhini yake aidha awe mbinguni au duniani, wala hakuna chochote kinachoendelea sasa hivi mbinguni kama hakitoki kwake.

Vivyo hivyo shetani naye hawezi kufanya jambo lolote dunia isipokuwa kwanza amepata idhini kutoka kwake yeye HUYO MKUU WA WAKUU(YESU KRISTO), Kumbuka shetani hajiamulii kufanya jambo lolote jinsi apendavyo, yote uyaonayo anayoyafanya karuhusiwa kuyafanya kwa kibali maalumu kutoka kwa Bwana, Na pia kuzimu hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kumtoa mtu kuzimu wala kumpeleka. Ni YESU peke yake ndiye anayewamiliki walio hai na walio kufa. yeye ndiye anayeamua aidha akupandishe juu au akushushe, shetani hana mamlaka yoyote juu ya wafu.(warumi 14:9). Mganga yoyote asikudanganye kwamba anaweza akamleta ndugu yako aliyekufa(mzimu) kuzungumza nawe, huo uwezo hana ukiona mzimu ujue ni pepo hilo limevaa sura ya huyo mtu. Uwezo huo anao MFALME TU (YESU KRISTO).

VIvyo hivyo na wanadamu wote pia hakuna mwanadamu anayeishi kwa nafsi yake mwenyewe, hakuna mamlaka inayojiamulia mambo yake tu yenyewe, kila kitu kipo chini ya utawala wa BWANA YESU KRISTO, hata wafalme waliopo leo duniani hawakuwekwa na watu bali ni MFALME MKUU(yaani YESU KRISTO) ndiye aliyewaweka kwa makusudi yake,Huwezi kufanya jambo lolote liwe baya au zuri kama halikupitishwa kwanza kwenye utawala mkuu wa Bwana YESU, mithali 16:3" Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.  Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; NAAM, HATA WABAYA KWA SIKU YA UBAYA. " ..soma pia maombolezo 3:37 "Ni nani asemaye neno nalo likafanyika, Ikiwa Bwana hakuliagiza?  Je! Katika kinywa chake Aliye juu HAYATOKI MAOVU NA MEMA? ".
Hivi ndugu hauogopi unaposikia mambo haya yote halafu hautetemeki mbele ya hili JINA. 

Vivyo hivyo hata vitu vya asili kama wanyama, ndege, samaki, milima, mimea, bahari n.k. Hivi vyote vinatetemeka na kungojea maagizo kutoka kwa Bwana YESU, na vyote vinamjua kama vile wewe unavyomjua haviwezi vikajiamulia mambo, mvua haiwezi kunyesha au nchi kuzaa kama hazijapokea amri kutoka kwa BWANA YESU KRISTO.

Na pia katika utawala unaokuja wa miaka 1000 BWANA YESU atakaposhuka kuja kutawala na watu wake hapa duniani, dunia itabadilishwa kuwa kama Edeni bahari itaondolewa, kwahiyo sehemu kubwa ya nchi kavu itaongezeka, kumbuka leo hii robo tatu ya dunia ni maji, kwahiyo bahari ikiondolewa mabara tuliyonayo leo yataongezeka mpaka kufikia 28 au zaidi unaweza ukajenga picha kutakuwaje?, Hivyo wafalme na watawala watakuwa wengi sana kupita kiasi, dunia itajaa utukufu na ustaarabu wa hali ya juu ambao haujawahi pata kuonekana, matatizo hayatakuwepo huko, njaa, shida, umaskini na magonjwa hayatakuwepo, na YESU KRISTO ndiye atakayekuwa BWANA WA MABWANA, na MFALME WA WAFALME na kiti chake cha enzi kitakuwepo huko Yerusalemu na watu wote wa ulimwengu mzima watakusanyika kwenda kumwabudu huko. 

Kama tu huu ulimwengu wa leo wenye dhambi na utawala wake, na wafalme wake unamantiki (unaonekana wa kuvutia) si zaidi huo utakaokuja? huo hauelezeki ni raha zisizo na kifani, kutakuwa na shughuli nyingi na teknolojia kubwa zinazotoka kwa Mungu ambazo kwasasa hazipo, wala haziwezi kufananishwa na hizi, wanyama na wanadamu wataishi kwa amani, watu wa Mungu watajenga na kupanda na hakuna mtu atakayebomoa au kuharibu kwasababu shetani wakati huo atakuwa amefungwa.

Kumbuka ndugu haya mamlaka yote yapo mkononi mwa Bwana YESU KRISTO. Naye aliahidi kumiliki nao wale wote watakaoshinda kama yeye alivyoshinda, soma ufunuo 3:20 -21" Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, NITAMPA KUKETI PAMOJA  NAMI KATIKA KITI CHANGU CHA ENZI, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. ". Hatuwezi kumiliki na Bwana haya yote kama hatutapita katika njia aliyopitia yeye.  "Yohana 14:6.. Yesu akamwambia, Mimi ndimi NJIA, NA KWELI NA UZIMA; mtu haji kwa Baba, ila kwa NJIA YA MIMI. ". Hapo aliposema NJIA alikuwa anamaanisha MAISHA, na wala sio kumpokea YESU kuwa Bwana na mwokozi wako tu! bali ni maisha yako yanapaswa yapite katika ile ile NJIA ya Yesu Kristo aliyopita.

Je! Njia ya Yesu Kristo ni ipi?

Luka 9:23 "Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, AJITWIKE MSALABA WAKE KILA SIKU, anifuate.
 
24 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. 25 Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe? 26 Kwa sababu kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu. 

Ishara kuu ya kukutambulisha kwamba unamfuata YESU ni MSALABA WAKO. na msalaba ni nini?. Tunajua YESU alibeba msalaba wake ikiashiria kwenda mautini. Vivyo hivyo na sisi pia tunapaswa kubeba misalaba yetu ikiashiria tunapaswa kufa kila siku kwa mambo ya ulimwengu, na pia tunakuwa tayari kufa katika mwili kwa ushuhuda wa YESU KRISTO. Kumbuka wakati YESU alipobeba msalaba wake, alipitia fedheha, alitemewa mate, aliaibishwa kwa ajili ya ushuhuda wa baba yake. kama yeye alivyopitia hiyo NJIA  na sisi tunapaswa tupitie vivyo hivyo kwa ajili ya jina lake, kudharauliwa, kuchekwa, kutukanwa, kufungwa, hata kuuliwa pasipo kuuweka chini msalaba wetu. wafilipi 1:29 "Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ILA NA KUTESWA KWA AJILI YAKE;”

Kwa yeye kuwa mtii vile katika maisha yake na msalaba wake, ndipo tunaona Mungu akamwadhimisha sana kuwa juu ya vitu vyote vya mbinguni na duniani, Na kama kwa njia hiyo ya kuvumilia Baba alimpa vyote, unadhani ili na wewe uwe kama yeye utapitia NJIA nyingine yoyote tofauti na hiyo ya MSALABA??. Usidanganyike kimbia injili za mafanikio na tamaa za ulimwengu huu tu na za sifa za kutiana moyo na majigambo! yasiyoweza kumzalia mtu matunda ya wokovu, injili zinazokufanya ujione upo sawa na Mungu katika hali yako ya uvuguvugu angali ukijua moyoni mwako hata BWANA akarudi leo utabaki! kimbia ndugu.

 Bwana alisema mwenyewe mtumwa sio mkubwa kuliko Bwana wake ikiwa yeye walimuita beelzebuli si zaidi watumwa wake?. Ikiwa yeye alikataliwa na viongozi wakubwa wa dini wakati ule kwa ajili ya ushuhuda wa baba yake, inakuwaje wewe unasifiwa na ulimwengu mzima?. Jiulize! jiulize! msalaba wako ni upi?  mitume wote na manabii walioifuata njia yake waliishia msalabani, au kama sio msalabani maneno yao yalikataliwa na wakuu wa dini wasiompenda Mungu. Jua tu ukienda katika njia iliyosahihi lazima upitie udhia soma..2 Timotheo 3:12 “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa. “

Unaogopa kumkiri Kristo kwasababu unaogopa utatengwa na dhehebu lako. mwanamke unaogopa kuacha kuvaa suruali na vimini na make-up na fashion kwasababu unaogopa marafiki zako watakuonaje!. Umeujua ukweli kwamba hupaswi kuabudu sanamu, au kusujudia vinyago na dhamiri yako inakushuhudia unachofanya sio sahihi lakini kwasababu unamwogopa mama yako au baba yako au ndugu zako, unaendelea kufanya hivyo, ili usionekane mtu wa ajabu. Bwana Yesu (MFALME WA WAFALME )alisema :

Mathayo 10:32 "Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33 Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 34 Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga. 35 Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; 36 NA ADUI ZA MTU NI WALE WA NYUMBANI MWAKE.37 APENDAYE BABA AU MAMA KULIKO MIMI , HANISTAHILI; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. 38 WALA MTU ASIYECHUKUA MSALABA WAKE AKANIFUATA, HANISTAHILI.39 Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. "

Je! msalaba wako ni nini katika ukristo wako??..je! ni Yesu kukufanikisha katika biashara yako au kazi yako huku ukiendelea kuwa vuguvugu? au kuponywa ugonjwa wako huku ukiendelea kuvaa nusu uchi? au kukupa familia nzuri huku ukiendelea  kuabudu sanamu?..au kujitoa kikamilifu kwa Bwana na kupita katika njia yeye aliyoipitia bila kujali dunia inasema nini juu yako?. jibu unalo! maombi yangu ni sisi sote tushinde ili siku ikifika tukaketi pamoja naye katika kiti chake cha enzi kama alivyoshinda yeye. (yaani yule MFALME MKUU BWANA WETU NA MWOKOZI WETU YESU KRISTO). 

SIFA NA HESHIMA NA UTUKUFU VINA YEYE MILELE NA MILELE. HALELUYA!.

Mungu akubariki!.

Tuesday, June 13, 2017

TUTAWEZAJE KUMZALIA MUNGU MATUNDA?:


Kuna hatua za kupitia, ambazo ni lazima kila mkristo azipitie ili aweze kumzalia Bwana matunda, Bwana alizifananisha hatua hizi na ule mfano wa MPANZI;

Tukisoma Mathayo 13:2-9 " Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. 3 Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. 4 Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; 5 nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; 6 na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. 7 Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; 8 nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. 9 Mwenye masikio na asikie. "


Katika mfano huu tunaona huyu mkulima alienda kupanda mbegu, kumbuka hizi hazikuwa mbegu za kuchimbiwa ardhini, bali zilikuwa ni mbegu nyepesi ndogo za kurusha, na alipokuwa akizirusha alizielekeza zote ziende kwenye udongo mzuri, ili zikue na kuzaa matunda, hizi tofauti na mbegu zile za kupanda ambapo mkulima huenda moja kwa moja kwenye udongo mzuri na kuzifukia ardhini, lakini hizi ni tofauti, tunaona zilipewa nguvu ya kutembea kwa kurushwa ili zifike katika eneo lililokusudiwa la udongo mzuri. Lakini  kuna nyingine zilikwama kwenye hatua tofauti tofauti katika safari zao kuelekea kwenye udongo mzuri.

Katika mfano huu hapa mbegu zilipitia katika hatua kuu NNE (4), ambazo ni; NJIANI, kwenye MIAMBA, Kwenye MIIBA, na kwenye UDONGO MZURI. Na hizi ndizo hatua NNE za mkristo katika safari ya maisha yake tangu siku ile ya kwanza anayompa Bwana maisha yake. Tuzitazame hatua hizi kwa ufupi;



HATUA YA KWANZA: NJIANI


Unaposikia injili (NENO) kwa mara ya kwanza, wewe unakuwa ni mbegu iliyorushwa na mkulima ambaye ni YESU KRISTO katika shamba lake, Kumbua Bwana alikusudia wewe ufike kwenye udongo mzuri, lakini mbeleni kuna vikwazo sasa hatua ya kwanza ni wewe kurushwa kutokea NJIANI, hapa unajikuta umeshapokea neno la Mungu (yaani kumpokea Kristo) katika namna ya kawaida unajikuta bado haulielewi lile NENO vizuri, ndani yako unasikia kiu ya kutaka kuendelea kumjua Mungu, hivyo unajikuta hauridhiki katika hali uliyopo ndani kunachemka kutaka kuendelea kujua zaidi, unaenda huku na kule kutafuta majibu ya maswali yako ya rohoni, na unakuwa na kiu pia ya kusoma NENO la Mungu.

Ukiona hali kama hiyo ujue ni ile nguvu ya Roho wa Mungu inakusukuma kusonga mbele kuelekea kwenye udongo mzuri ili ukamee. Lakini kwa upande mwingine unakuta mtu amesikia injili na ile nguvu ya kumfanya aendelee kusonga mbele yaani kutaka kumjua Mungu zaidi haipo ndani yake. anaridhika na hali aliyopo, akikuta kitu kwenye NENO la Mungu asichokielewa hajishuhulishi kutafuta jibu la maswali yake , hivyo anatulia njiani, hapo ndipo shetani anapopata nafasi kuchukua kile kilichopo ndani yake, hapo ndipo linakuja lile neno "aliyenacho ataongezewa na asiyenacho hata kile kidogo alichonacho atanyang'anya".

 Hivyo unamkuta mtu anajiita mkristo lakini matendo yake hayaendani na ukristo, hanufaiki na jambo lolote katika NENO la Mungu ,japo anaenda kanisani kila siku, anaimba kwaya, anasema ameokoka pasipo kujua ibilisi ameshamwondolea ile nguvu ya Roho Mtakatifu na kiu ndani yake imekufa, anakuwa hana tofauti na mtu asiyeamini.

Na ndio maana Bwana Yesu alisema mathayo 13: 19" Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia."



HATUA YA PILI: KWENYE MIAMBA
Mathayo 13:20-21 "Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa. "
Kumbuka hii ni hatua ya pili, ambayo inakuja baada ya kushinda ile hatua ya kwanza, shetani akishaona una kiu, hamu, shauku na bidii nyingi ya kutaka kumjua Mungu, na  kutafuta kuujua ukweli na hatma ya maisha yako ya milele, na maisha ya kumpendeza Bwana, hapo ndipo majaribu yanapoanza, Kumbuka kila mkristo lazima ajaribiwe imani yake, Mungu mwenyewe ndiye aliyeruhusu iwe hivyo, maana ndivyo wana wa Mungu wote walivyopitia huko nyuma.

 Sasa katika hali hii, ile nguvu ya Roho Mtakatifu inakusukuma uikabili hatua inayofuata, hapo ndipo unakutana na majaribu kwa ajili ya NENO la Mungu, pengine utapitia, kuchukiwa na ndugu, kutengwa na marafiki, misiba, magonjwa, kufungwa kwa ajili ya Neno la Mungu, kudharauliwa, kuchukiwa kisa tu umeamua kuifuata hiyo imani, wakati mwingine mambo yako mengine kuharibika kwahiyo hali hii inapotokea usiogope ni IMANI yako inajaribiwa ni uthibitisho kwamba ile mbegu bado ipo safarini kuelekea kwenye udongo mzuri, usichukizwe, shika sana ulichonacho, Bwana hatakuacha hali hii inaweza ikadumu kwa muda mrefu lakini usikate tamaa Bwana hatakuacha yupo nawe. Kumbuka jambo hili litakuja kwa yule tu mtu ambaye hatua ya kwanza ameivuka kikamilifu. lakini safari bado inaendelea.

Lakini wapo watu wengi wakifika kwenye hii hatua wanaizimisha ile nguvu ya kuendelea mbele kwa kuogopa udhia na dhiki na aibu hivyo wanakwazika na kuiacha imani, hawa ndio wale waliokwama katika miamba natamani ndugu yangu wewe usiwe hivyo. kumbuka Bwana Yesu alisema mtu yeyote akitaka kunifuata ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.



HATUA YA TATU: KWENYE MIIBA
Mathayo 13:22 "Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. "
Shetani akishajua bado unang'ang'ana na NENO na kuzidi kutamaini kufikia utimilifu, na kumtumaini Bwana kuelekea udongo mzuri, japo kuwa unapitia dhiki, udhia, lakini bado upo na Bwana, safari hii hatumii nguvu tena, anakuja na ushawishi, na anafahamu ni mahali gani pa kumkamatia mtu na si pengine zaidi ya Tamaa ya mambo ya ulimwengu huu..hivyo atakuletea nguvu kubwa ya ushawishi ili utamani kuwa kama watu wa ulimwengu huu, kupenda kuwa mali nyingi, kuubadilisha muda wako wa kuwa karibu na Mungu na u-bize, mihangaiko, anasa, Starehe, biashara, ili tu uridhike  na hali uliyopo umzimishe Roho,  Hali kama hii inapokuja wewe umtazame Bwana na ahadi zake usitamani kufanana na watu wa ulimwengu huu, yeye mwenye alisema "sitakuacha wala kukupungukia kabisa" kumbuka Bwana Yesu alichokisema katika mathayo 6.

Hivyo usipunguze muda wako wa kusoma NENO, kusali, kumtafakari Mungu, kutangaza Neno la Mungu, kisa tu! ya kusongwa na mahangaiko ya maisha, bali kinyume chake uongeze muda wako na Bwana, hayo mengine yaweke kando utafute kwanza ufalme wake na haki yake na hayo mengine yote utazidishiwa.

Lakini katika hatua hii wakristo wengi ndipo waliponasiwa na mwovu, walianza vizuri lakini pesa, shughuli, mahangaiko, yamewasonga wamwache Mungu na kupoa hivyo ile Nguvu ya ROHO wa Mungu ndani yao inapoa, wanaacha kutazamia mambo ya ulimwengu ujao badala yake wanaangalia mambo ya ulimwengu huu, wakidhani katika hali yao ya uvuguvugu ya ukristo waliyopo ndiyo wanamzalia Mungu matunda kumbe bado hawajafika.



HATUA YA NNE: UDONGO MZURI
Luka 8:15 "Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa KUVUMILIA. "
Hatua hii ndipo mtu anapokamilishwa kwenye udongo mzuri ili kumzalia Mungu matunda. Kumbuka hatua hii mtu ataifikia kwa KUVUMILIA hari zote tatu zilizopita nyuma, yaani njiani,kwenye miamba, na kwenye miiba, pale mkristo anapolipokea NENO kwa uthabiti wa moyo, kila siku akiendelea kutafuta na kumjua Mungu bila kuchoka japo kuwa adui yupo njiani na majaribu yote, dhiki, udhia, shida, taabu, misiba, kuvunjwa moyo, kukatishwa tamaa, kutengwa, ukame, kufungwa, kuchukiwa kwa ajili ya Kristo, kukana mambo yote ya ulimwengu, naam hata nafsi yake mwenyewe, kwa ajili ya Bwana akizidi kuvumilia hayo yote anakuwa dhahabu iliyosafishwa kwenye moto tayari kwa kusudi na kazi ya Mungu aliyomweka duniani. Mtu huyu anakuwa ameingia KAANANI yake, Utukufu wa Mungu unafunuliwa juu yake, ili kumzalia Bwana matunda ya haki yaliyokubaliwa. kama alivyosema huyu thelathini, huyu sitini, huyu mia, kulingana na kipimo cha neema alichopimiwa huyo mtu. Wakati huu pia Bwana anambariki kwa vitu vyake vyote alivyovipoteza kwa ajili yake mara mia zaidi kama alivyoahidi katika NENO lake. Na mtu wa namna hii anakuwa na uhusiano wa kipekee na Mungu, na kupewa nafasi za kipekee katika ufalme wa Mungu angalia akiwa hapa hapa duniani.

Kumbuka kuhubiri au kufanya kazi yoyote ya Mungu, kama haujazivuka hizi hatua NNE, hauwezi kumzalia Mungu matunda maana sasa utakuwa umepandwa kwenye udongo gani?. Yatupasa tuyashinde ndipo tumzalie Mungu matunda, kumbuka Yesu alishinda hivyo na sisi pia yatupasa tushinde. BWANA anasema ufunuo 3:21 "Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. "
Hivyo ndugu tujitahidi mimi na wewe, tufikie hapo ili tumzalie Bwana wetu matunda, tujiangalie maisha yetu tujiulize je tupo katika hatua gani?. je ni njiani? au kwenye kwenye miamba,? au kwenye miiba? au kwenye udongo mzuri?. tupige mbio tuufikie utimilifu na jambo lolote lisitusonge au lisitutenge sisi na upendo wa Mungu, iwe ni njaa, dhiki, udhia, taabu, raha, uzima, mauti, lolote lile, TUZIDI KUIITI ILE NGUVU YA ROHO MTAKATIFU ITAKAYOTUFIKISHA KATIKA UDONGO MZURI. Naye Bwana ataturuzukia baraka zake tukishinda.

Mungu akubariki!.