"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, July 8, 2017

DHAMBI YA MAUTI


1Yohana 5:16 "Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. IKO DHAMBI ILIYO YA MAUTI. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo.Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti."


Biblia inaeleza wazi kuwa kuna DHAMBI ZA MAUTI na DHAMBI ZISIZO ZA MAUTI:




DHAMBI ISIYO YA MAUTI:

Hii ni dhambi ambayo mtu akiifanya anaweza akatubu na kusamehewa, na dhambi hii ni ile inayotokana na aidha kutenda pasipo kukusudia, au inatendeka kutokana na uchanga wa kiroho, au kwa kukosa maarifa  au jambo lingine lolote linaloweza kutendeka ambalo halijavuka mipaka ya neema. Dhambi  ya namna hii biblia inasema mtu anaweza akatubu au akamuungamania mwenzake na akasamehewa, akaendelea kuishi na asife. Lakini kuna dhambi mtu akiitenda hiyo hata huyo mtu aombeje, anaweza akasamehewa kosa tu lakini adhabu ya mauti ipo pale pale, je! hii dhambi inasababishwa na nini?



DHAMBI YA MAUTI:

Dhambi hii ipo kwa namna mbili, ya kwanza kwa wale watoto wa Mungu (watumishi wake) na ya pili ni kwa watu wengine ambao neema ya Mungu inalilia masikioni mwao lakini wanaichezea. Namna hizi mbili tunaweza tukaona zimefananishwa  na Musa na wana wa Israeli kule jangwani, Musa akiwa mfano wa "watumishi wa Mungu", pamoja na kwamba Mungu alitembea nae kwa namna ya tofauti hata kuliko manabii wote, lakini alitenda dhambi kwa kosa kutokutii maagizo ya Mungu na kuchukua utukufu wa Mungu, alifanya vile akijua kabisa kuwa ni kosa ikampelekea kutenda DHAMBI YA MAUTI, 


Musa kwa kweli alisamehewa lile kosa lakini adhabu ya mauti ilikuwa pale pale iliyomsababishia apoteze hata zile ahadi zote Mungu alizomuahidia za kuiona nchi ya Ahadi. Hata leo hii wapo watumishi wanatenda hii dhambi, wanachukua utukufu wa Mungu na kutokutii maagizo yake, inapelekea Mungu kuwaadhibu huduma zao zinakatishwa kama ilivyotokea kwa Anania na Safira walipomdanganya Roho Mtakatifu na kupokea adhabu ya kifo pale pale japo walikuwa ni watoto wa Mungu. Hizo zote ni DHAMBI ZA MAUTI.

Vivyo hivyo na wana wa israeli ni mfano kamili wa "wakristo vuguvugu" wa leo kumbuka wana wa israeli ijapokuwa waliuona utukufu wote wa Mungu, na maajabu yote na miujiza yote lakini mioyo yao haikuwa mikamilifu  ijapokuwa Mungu aliwavumilia kwa muda mrefu watubu lakini hawakutaka wakaanza kuabudu sanamu, wakafanya uasherati, wakawa wakimnung'unikia Mungu na kumjaribu ikafika wakati neema ya Mungu juu yao ikakoma Mungu akaapa kwamba wote wangekufa nyikani ijapokuwa walitubu kwa kulia na kuomboleza hata hivyo hakuna hata mmoja wao aliyeiona nchi ya ahadi isipokuwa wale wana wao tu!, unaona hiyo ndiyo DHAMBI YA MAUTI. unajisikiaje pale ambapo unaona ungestahili kupata baraka fulani halafu unazikosa, hautakaa uzipate tena milele? fikiri juu ya hilo, na ndio maana maandiko yafuatayo yanatuonya..tusome.


1 wakorintho 1 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;
2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;
3 wote wakala chakula kile kile cha roho;
4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.
5 Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.
6 Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani.
7 Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.
8 Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.
9 Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.
10 Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.
11 Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.
12 Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. 

Mfano kamili wa kanisa la leo lililo vuguvugu kupita kiasi" linaona utukufu wa Mungu karibu kila mtu anafahamu kabisa kuwa KRISTO ni mwokozi, mponyaji, na wengi wao wamebatizwa wanaenda kanisani, wanaujua ukweli wote lakini utakuta bado mtu ni mwasherati, mlevi, mtukanaji, anaenda disco, msengenyaji, anatazama pornography, anavuta sigara, anavaa mavazi ya kiasherati n.k. angali akifahamu Mungu hapendezwi na watu wa namna hiyo. Anaiona neema ya Mungu lakini bado anaidharau mfano ule ule wa wana wa Israeli, Lakini watu kama hawa hawajui kuwa wapo hatarini kutenda DHAMBI YA MAUTI. kama tu Mungu hakuweza kumwachilia mtumishi wake Musa kwa kosa dogo tu la kutokutii wewe unadhani utaponea wapi ikiendelea na maisha yako ya dhambi?..Ni kweli Musa alisamehema lakini adhabu ya kutokuiona nchi ya ahadi kwa njia ya Mauti ilikuwa pale pale.


Kwa namna hiyo hiyo unahubiriwa injili leo umgeukie Mungu, uache dhambi utubu usamehewe unasema hapana ngoja nile maisha nitakuja kutubu baadaye unaweza usiseme kwa mdomo lakini moyo wako unasema unaendelea kuwa mwasherati pale unapopata ugonjwa usiokuwa na matumaini mfano ukimwi unaona ndio sababu ya kumgeukia Mungu angali wakati ulipokuwa mzima hukufanya hivyo? Ni kweli ukitubu unaweza ukasemehewa lakini adhabu ya mauti ipo pale pale ndio maana utaona watu wa namna hiyo hata waombeweje hawaponi, sababu ni kwamba wameshatenda DHAMBI YA MAUTI. Sisemi hili kwa kukutisha lakini ndio ukweli tuyachunguze maisha yetu.


Mara nyingine sauti ya Mungu inakulilia uache dhambi ya ulevi na uvutaji sigara ili usafishwe maisha yako lakini unaziba masikio yako hutaki kusikia. Mungu anaruhusu pepo la Kansa linakuingia unapata kansa ya koo au mapafu au ini hapo ndipo unapoona sababu ya kumrudia Mungu ni kweli ukitubu Mungu anaweza kukusamehe lakini adhabu ya kifo ipo pale pale Kwasababu apandacho mtu ndicho atakachovuna. Mungu sio wa kumtegea kwamba niache nifanye mambo yangu kisha nikishafika mzee au wakati fulani ndipo nimgeukie, Mungu hadhihakiwi.


MADHARA YA DHAMBI YA MAUTI:

Madhara yake makubwa ni kwamba utapoteza thawabu yako katika ule ulimwengu ujao kwasababu umelikatisha kusudi la Mungu juu yako, ndio hapo kama Mungu alikupa huduma au anataka uwe na huduma haiwezekani tena kuendelea nayo kwasababu ulishatenda DHAMBI YA MAUTI, huna budi kuondoka nafasi yako anapewa mtu mwingine kama ilivyomtokea Yuda nafasi yake ilichukuliwa na mtu mwingine. wakati wengine wakipewa mataji yao mbinguni siku ile kwa kazi nzuri walizotaabika nazo duniani wewe utakuwa huna lolote, utabaki mtu wa kawaida milele.


Hivyo ndugu, biblia inasema 1petro 1:10 " KWAHIYO NDUGU, JITAHIDINI ZAIDI KUFANYA IMARA KUITWA KWENU NA UTEULE WENU; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe. " .


Itikia wito wa Mungu ulio ndani yako sasa kabla hazijaja siku zilizo mbaya utakazosema ee! Mungu wangu nisamehe nataka kuishi lakini usiweze kusikilizwa dua zako kwa upumbavu wako mwenyewe. Ndugu Tukisikia hili tuogope kwasababu imeandikwa..


Wafilipi 2:12 "Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, UTIMIZENI WOKOVU WENU WENYEWE KWA KUOGOPA NA KUTETEMEKA.KWA MAANA NDIYE MUNGU ATENDAYE KAZI NDANI YENU, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. "

AMEN!


1 comment: