"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, September 11, 2017

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 18



SWALI;-Mwanzo 1:26 ""Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi."" Hapa Mungu alikuwa anaongea na nani?

JIBU: Mara nyingi Mungu alikuwa anatumia neno "sisi" kama wingi kuashiria hakufanya mambo yote peke yake, bali alikuwa na wengine aliowashirikisha mawazo yake, Kumbuka kuumba aliumba yeye peke yake lakini mawazo yake ya kufanya baadhi ya mambo aliwashirikisha wengine, hivyo hapo aliposema na tumfanye mtu kwa mfano wetu alikuwa anaongea na malaika zake, na hakuwa anazungumza na nafsi ya tatu katika uungu wake, Mungu ni mmoja tu na hana nafsi tatu, neno "TUMFANYE" halimaanishi ni watatu tu! bali linaweza likamaanisha wawili, watano, mia au milioni n.k. Hivyo mtazamo wa kusema Mungu ana nafsi tatu kwa kuusimamia mstari huu sio kweli, pale Bwana alikuwa anazungumza na malaika zake ambao walikuwa wameshaumbwa kabla yetu sisi,

Tunaona pia jambo hili linajirudia sehemu nyingine nyingi katika biblia Bwana akizungumza na malaika zake, soma mwanzo 3:22"Bwana Mungu akasema basi huyu mtu amekuwa kama MMOJA WETU, kwa kujua mema na mabaya"..., pia mwanzo 11:6-8"Bwana akasema tazama watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja, na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya na TUSHUKE HUKO, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao." .. sehemu zote hizi mbili Bwana alionekana akijadiliana na malaika zake. Mungu huwa anatenda kazi na malaika zake.

Tukisoma pia Isaya 6:8 Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, nimtume nani? naye ni nani atakayekwenda KWA AJILI YETU? Ndipo niliposema mimi hapa nitume mimi. Naye akaniambia enenda ukawaambie watu hawa fulizeni kusikia lakini msifahamu; fulizeni kutazama lakini msione..." Unaona hapo Bwana alimuuliza nabii Isaya ni nani atakayekwenda kwa ajili ya Mungu na jeshi lake la mbinguni?.

Kwahiyo Mungu kujadiliana na malaika zake sio jambo jipya tunaweza tukaliona pia kwenye ile habari ya mfalme Ahabu na nabii Mikaya ukisoma "2 nyakati 18:15-22" .Kwahiyo pale Mungu alikuwa hazungumzi na YESU wala Roho Mtakatifu bali na malaika zake waliokuwepo kabla yetu sisi.

SWALI 2: Nataka kuuliza je! sadaka ya Habili ilikataliwa kwasababu ipi?

JIBU : Ukisoma mwanzo 4:3-4 sababu kuu iliyomfanya Kaini sadaka yake ikataliwe ni kwasababu hakujua malengo na sababu ya kuitoa hiyo sadaka (kukosa ufunuo)..mwenzake Habili alipata ufunuo wa yeye kwanini atoe mnyama na wala si kinginecho kwani alifahamu baada ya wazazi wao kula tunda na kujiona kuwa uchi kwa aibu walienda kutafuta majani kama njia ya kujisitiri, lakini Mungu aliona hawajasitirika bado hivyo aliamua kuwachinjia wanyama na kuwavisha ngozi zao ndipo walau walipata tena kibali cha kuzungumza na Mungu..

Hii ndio sababu Habili hakwenda tena na sadaka ya majani ili amkaribie Mungu bali alienda na sadaka ya wanyama ndipo Mungu akamtakabari, lakini ndugu yake aliona ni vema kutumia njia ile ile ya kwanza ya kutumia mazao ya ardhi ndipo Mungu akaikataa sadaka yake.

pamoja na hayo Mungu alimshauri afanye kama ndugu yake Habili lakini hakukubali. Ni vema tufahamu kuwa Mungu ana njia yake aliyoichagua yeye ya kumkaribia, Leo hii sadaka inayokubalika mbele za Mungu ni yule mwanakondoo aliyechinjwa kabla kuwekwa misingi ya ulimwengu(Yesu Kristo) hakuna sadaka nyingine inayokubalika mbele za Mungu zaidi ya hiyo kwasababu biblia inasema YESU ndiye njia, na kweli na uzima mtu hafiki kwa Baba ila kwa njia ya yeye, Hivyo usijidanganye kwamba unatoa sadaka sana, au unatenda matendo mema, au unasaidia yatima, au sio mlevi, n.k. na huku haujaoshwa dhambi zako kwa damu ya YESU Kristo hautakuwa na tofauti na Kaini unamtolea Mungu dhabihu ya mazao badala ya mwanakondoo, kumbuka hata wasio wakristo dini nyingine kama waislamu, wahindu,n.k. wanafundishwa kutenda matendo mema, wanatoa sadaka, wanasaidia maskini, sio walevi, sio waasherati, lakini Mungu hawatambui hao kwasababu hawapo chini ya damu ya mwanakondoo YESU KRISTO.

Hivyo mpe Kristo maisha yako ili dhambi zako zisafishwe kwa kubatizwa kwa jina la YESU KRISTO uwe na uhakika na wokovu wako.
 Amen!

No comments:

Post a Comment