"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, December 13, 2017

MAELEZO JUU YA "UFUNUO 12"


Ufunuo 12

1 Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili.
2 Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa.
3 Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba.
4 Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.
5 Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi.
6 Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko muda wa siku elfu na mia mbili na sitini.
7 Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;
8 nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.
9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.
10 Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.
11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.
12 Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.
13 Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.
14 Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo.
15 Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule.
16 Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake.
17 Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.

Ukisoma Ufunuo mlango wa 11, utaona habari ya wale MASHAHIDI WAWILI wakifanya kazi ya kuwahubiria injili wale Wayahudi 144,000 na kutiwa muhuri (Ufunuo 7). Na tunaona walifanya kazi yao miezi 42, (yaani miaka mitatu na nusu) na baada ya kumaliza ushuhuda wao yule mnyama atokaye kuzimu atawaua lakini baada ya siku tatu na nusu tunaona Mungu atawafufua.

Kumbuka baada ya kanisa kunyakuliwa, injili itahamia Israeli na itakuwa imebakia miaka 7 tu mpaka mwisho wa dunia utakapofika kulingana na unabii wa Danieli 9:27, kwenye lile juma moja la mwisho kati ya yale majuma 70 aliyoonyeshwa.

Hivyo ndani ya hii miaka 7, nusu yake yaani miaka mitatu na nusu ya kwanza, hawa manabii wawili watafanya kazi ya kuwahubiria wayahudi, na nusu ya pili iliyobaki itakuwa ni kipindi cha ile DHIKI KUU (yaani miaka 3.5 ya mwisho).

Sasa tukiendelea kusoma kitabu cha Ufunuo 12 tunaona Yohana akiona ishara kuu mbinguni, yule mwanamke aliyevikwa jua na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake na juu ya kichwa chake taji ya nyota 12.

Ukiangalia huyu mwanamke anawakilisha taifa la Israeli, ukisoma mwanzo 37:9 utaona ile ndoto aliyoota Yusufu aliona jua na mwezi na zile nyota 11 zikimwinamia ambayo tafsiri yake tunafahamu ilikuwa ni Yakobo kama jua, mwezi kama mama zake, na wale wana 11 wa Israeli kama zile nyota. Hivyo yule mwanamke ni taifa la Israeli.

Ukiendelea kusoma mstari wa pili utaona yule mwanamke alikuwa na mimba, na katika hali utungu wa kutaka kuzaa, na akamzaa mtoto mwanamume ambaye atawachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Maana ya ule utungu ni unabii au matarajio ya kuzaliwa masiya katika Israeli ambaye alikuwa akisubiwa kwa muda mrefu, Na huyu mtoto mwanamume si mwingine zaidi ya BWANA YESU KRISTO yeye ndiye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma katika ule utawala wa miaka 1000 (Ufunuo 2:27).

Ukizidi kusoma utaona pia katika mstari wa 3-6, utaona ishara nyingine ilionekana lile joka kubwa jekundu (ambalo ni shetani) likiwa limejiandaa pale atakapozaliwa yule mtoto limmeze, lakini halikufanikiwa, jambo hili tunaliona lilitimia wakati Bwana YESU anazaliwa Mfalme Herode, alipopata habari kuwa mfalme aliyetabiriwa kazaliwa katika Israeli alifadhaika na kutaka kumwangamiza mtoto YESU, Lakini hakufanikiwa mpaka Mungu alipomchukua juu mbinguni katika kiti chake cha enzi.

Tukiendelea kusoma kuanzia ule mstari wa 7-12, Tunaona habari nyingine inayohusu vita iliyopiganwa mbinguni kati ya Malaika watakatifu na shetani pamoja na malaika zake, na tunaona aliposhindwa alitupwa chini ili afanye vita na watu wanaozishika amri za Mungu.

Lakini tukiendelea mstari wa 13 tunaona baada ya yule mtoto kunyakuliwa juu (yaani Yesu kupaa AD 30) yule joka aliendelea kumuudhi yule mwanamke,tunaona katika historia alizidi kumuudhi kwa takribani muda wa miaka 2000 mpaka sasa, aliwatesa na kuwaua wayahudi katika nyakati tofauti tofauti, mfano wakati wa utawala wa Adolf Hitler aliwaua wayahudi zaidi ya milioni 6, katika historia tunaona wayahudi ni watu wamekuwa wakichukiwa na mataifa mengi n.k.

Mstari wa 14, tunasoma mwanamke yule baada ya kuudhiwa muda mrefu akapewa MABAWA MAWILI YA TAI yule mkubwa ili aruke aende mbali na yule Joka aliyetupwa chini ili kufanya vita na watakatifu kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Yale mabawa ya Tai ni injili ya wale manabii wawili wa ufunuo 11, watakaowahubiria wayahudi ili kuwafanya wamjue yule joka ni nani (MPINGA-KRISTO), na utendaji kazi wake na namna ya kumuepuka, na ndiye anayetaka kukaa katika Hekalu la Mungu kuabudiwa kama Mungu.

Kumbuka wale manabii wawili katika injili yao ndio watakaomfunua yule mpinga-kristo kwa wayahudi kuwa si mwingine zaidi ya kiongozi maarufu anayetoka katika utawala wa RUMI, mwenye kivuli cha Amani kumbe ndani yake ni joka linalotaka kuabudiwa, Kama tu vile lile joka lilivyokuwa ndani ya HERODE-Mrumi kutaka kumwangamiza YESU vivyo hivyo hilo joka litakuwa ndani ya mpinga-kristo atakayetoka katika utawala ule ule wa Rumi kutaka kuwaangamiza wayahudi.

Hivyo wale wayahudi 144,000 (ufunuo 7), watakapoamini ile injili ya wale manabii wawili watakayoihubiri ile miaka mitatu na nusu ya kwanza, pamoja na zile ishara na yale mapigo yatakayofuatana nao, Hawa wayahudi wachache 144,000 watafahamu kuwa yule joka anawawinda, na kwamba DHIKI KUU itaanza hivi karibuni, hivyo Mungu atawafungulia mlango wa kuwaficha mbali na yule JOKA pale dhiki itakapoanza,

Kwahiyo hili kundi dogo litaondoka ISRAELI, Mungu atawapeleka mahali alipowaandalia mahali ambapo yule mpinga-kristo hataweza kuwafikia (hii ndio maana ya kupewa mabawa ya Tai), lakini kumbuka sio wayahudi wote wataikubali ile injili ya wale manabii wawili bali ni wale tu 144,000 tu.

Watakaosalia ile miaka mitatu na nusu ya mwisho itakapoanza (ambacho ndio kipindi cha dhiki kuu), watapata mateso mengi yasiyokuwa na mfano tangu ulimwengu kuumbwa na hayatakuwepo hata baada ya hapo, kumbuka dhiki hii itajumuisha pia watu wote wa mataifa watakaokataa kuipokea ile chapa ya mnyama wakati huo unyakuo utakuwa umeshapita.

Kama tu vile kipindi cha kuzaliwa kwa YESU wale mamajusi walipomletea Herode habari ya kuzaliwa mfalme Israeli, malaika walimwonya Mariamu na mwanawe waondoke Israeli kwasababu mpinga-kristo(Herode) anakwenda kuleta dhiki, walikimbilia Misri kabla ya ile dhiki kuanza, lakini yule Herode alipoona kuwa wale mamajusi wamemlaghai, alikasirika akaenda kufanya vita na uzao wote uliobakia wa watoto wa Israeli,

Tunaona kulikuwa na maombolezo makuu Yerusalemu watoto wote walichinjwa. Vivyo wale manabii wawili (Ufunuo 11) wanafananishwa na wale MAMAJUSI ambao walimtangazia Herode habari mbaya za kuzaliwa mfalme, na wakati wa mwisho wale MANABII WAWILI pia watamtangazia mpinga-kristo kwamba mfalme kazaliwa tena mioyoni mwa WAISRAELI na kwamba anayepaswa kuabudiwa ni yule mtoto na sio yeye, na kama vile Herode alivyowakasirika mamajusi pamoja na Mariamu na mtoto vivyo hivyo mpinga-kristo wakati wa mwisho atawakasirikia wale MASHAHIDI WAWILI na kuwaua, lakini baadaye hakufanikiwa kuwaangamiza kabisa kwani walifufuka kama vile wale mamajusi walivyopewa njia ya kumtoroka Herode,

Na kama vile ni mwanamke mmoja tu (Mariamu) kati ya wanawake wote wa Israeli ndiye aliyekuwa na mimba ya mwokozi ndani, vivyo hivyo ni lile kundi dogo tu (144000) ndio litakalokuwa na ufunuo wa YESU mioyoni mwao utakaoletwa na wale manabii wawili wanaofananishwa na mamajusi.

Na pia kama tunavyoona Mariamu alipelekwa peke yake Misri mbali na Herode vivyo hivyo na wale 144,000 ndio tu watakaopelekwa mbali na mpinga-kristo wakati wa dhiki itakapoanza walioabakia wote yaani mamilioni ya waisraeli itawapasa wapitie DHIKI KUU kama tu wale wanawake wengine wa Israeli walivyouliwa wana wao.

Kwahiyo hawa 144,000 hawataguswa na yule joka na ndio maana tunawaona katika Ufunuo 14 wakiwa wamesimama na mwanakondoo juu ya mlima Sayuni, bikira safi wa Mungu, hawa wataingia katika ule utawala wa miaka 1000, pasipo kupitia madhara yoyote.

Kwa ujumla Ufunuo sura ya 12, inaelezea ISRAELI na jinsi yule mwanamke alivyofananishwa na taifa la Israeli.

Kwahiyo ndugu tazama ni wakati gani tunaishi, je! umepokea kweli Roho Mtakatifu? umebatizwa katika ubatizo sahihi? Maisha yako yanastahili unyakuo?. Kumbuka sasa Taifa la Israeli linanyanyuka, dalili zote zinaonyesha kuwa unyakuo upo mlangoni na injili inakaribia kurudi Israeli, Maombi yangu utubu,
Fahamu tu yule JOKA alishatupwa chini akiwa na ghadhabu nyingi akijua muda wake umebaki mchache, Hivyo utendaji wake wa kazi wa sasa sio kama ule wa zamani anatafuta kukupeleka kuzimu kwa gharama zozote, hivyo ni wakati wako wewe kusimama imara na kuuthibitisha wokovu wako.

Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment