"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, April 9, 2018

CHAGUA NI JIWE LIPI LITAKALO KUFAA KWA UJENZI.

Katika ujenzi wa zamani majengo yote ili yasimame IMARA yalikuwa ni lazima lipatikane jiwe kubwa moja la mraba, na kuwekwa katika kona ya kuta mbili mahali zinapokutana, ili ujenzi uendelee katika mtiririko ulio sahihi, hivyo pasipo hilo jiwe kuwepo haiwezekani jengo kusimamishwa kwasababu ili matofali mengine yatakayokuja juu yake yaweze kusimama na kunyooka yalilitegemea sana hilo jiwe, ni sawasawa na pikipiki au baiskeli bila kuwa na ‘stand’ haiwezi kusimama, vivyo hivyo na jengo lolote lililojengwa zamani zile pasipo kuwa na hilo jiwe la pembeni jengo haliwezi kusimama. Na jiwe hilo lilikuwa linachongwa kwa vito tofauti vigumu na imara tofauti na mawe mengine, hivyo kupelekea jiwe hilo kuwa ghali zaidi ya mawe yote. (Tazama picha chini).

Kadhalika katika biblia Jiwe hili la pembeni limefananishwa na BWANA wetu YESU KRISTO.
 
Biblia inasema Waefeso 2: 20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, NAYE KRISTO YESU MWENYEWE NI JIWE KUU LA PEMBENI.
21 Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.
22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu ikatika Roho.”

Hivyo sisi kama kanisa la Mungu (wakristo) tunafananishwa na mawe mengine madogo madogo tunaojengwa juu ya jiwe hilo kuu la pembeni, Kumbuka Bwana Yesu hajafananishwa tu na jiwe la pembeni bali ni kama JIWE ‘KUU’ LA PEMBENI. Ikiwa na maana kuwa ni jiwe la muhimu sana zaidi ya majiwe mengine yote ya pembeni. Kwamba pasipo hilo kazi inayofanyika ni sawa na bure. Ikiwa na maana pia sio kanisa tu peke yake linalohitaji jiwe kuu la pembeni, bali pia maisha ya mtu binafsi ni lazima yajengwe na jiwe kuu la pembeni.

Ndugu kumbuka kila mmoja hapa duniani ni ‘MUASHI’. Muashi maana yake ni ‘MJENZI’..Na je ni mjenzi wa nini?..Ni mjenzi wa MAISHA yake mwenyewe, kila mmoja anajenga maisha yake kwa namna yake mwenyewe, na kama ni mjenzi ni lazima uhitaji JIWE LA PEMBENI kutengeneza jengo lako. Swali Jiwe kuu lako la pembeni ni lipi?

Mawe ya pembeni yapo mengi sana. Shetani ni jiwe la pembeni; wapo wanadamu wanaotumainisha maisha yao yote katika nguvu za giza,uchawi na ushirikina, hivyo shetani ni jiwe kuu lao la pembeni.

Wapo watu ambao sababu ya maisha yao ili yawe na maana ni kuwa na MALI, hivyo mali ni jiwe kuu lao la pembeni.
 
Wengine wamefanya ELIMU kama tumaini la mwisho la maisha yao ya sasa na ya baadaye ni hapo tu, hawapo tayari kusikiliza habari nyingine zihusuzo Mungu au uzima wa milele uliopo katika Kristo Bwana, kwao wao ni kama upuuzi tu. N.k.

Hawa wote ni wajenzi na kila mmoja alichagua jiwe lake la pembeni kwa jinsi apendavyo. Lakini Biblia inasemaje?

1Petro 2: 4 “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, LILILOKATALIWA NA WANADAMU, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima.
5 Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.
6 Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.
7 Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, JIWE WALILOLIKATAA WAASHI [Wajenzi], LIMEKUWA JIWE KUU LA PEMBENI, .
8 Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile,wasiliamini,nao waliwekwa kusudi wapate hayo.”

Unaona hapo ndugu?. Hawa wajenzi wote walikuwa wanajiona wana hekima machoni pao wenyewe na kujichagulia MAWE wanayoyataka wao ili kuyafanya mawe yao makuu ya pembeni, lakini mwisho wao tunasoma walikuja KUJUTA baada ya jengo kukamilika, pale walipogundua kazi waliokuwa wanajitaabisha nayo ni BURE,japo ilikuwa inaonekana ina maana, jengo halifai Halina ubora wowote, baadaye walipopata akili kuwa kuna jiwe moja walilolidharau mwanzoni ndio lingepaswa kuwa jiwe kuu lao la kusimamishia jengo zima hata hivyo walikuwa wameshachelewa. JIWE limegeuka kuwa kwazo kwao (yaani HUKUMU).

Vivyo hivyo na wewe leo hii msingi wa maisha yako unaujenga wapi? je! ni ushirikina unazunguka kwa waganga, pale mambo yako yasipoenda sawa unakimbilia kwa waganga wa kienyeji kwasababu ndio jiwe kuu lako la pembeni, unaelezwa habari za Bwana Yesu kila siku, unazipuuzia kwasababu hazina umuhimu wowote katika maisha yako, lakini siku zinakuja utakapogundua kuwa Yule mwokozi uliyemkataa ndiye angepaswa awe msingi wa maisha yako, kumbuka wakati huo utakuwa umeshachelewa ni jehanamu ya moto itakuwa inakusubiria..

Wewe ambaye kutwa kuchwa ni elimu tu, habari za Yesu kwako ni hadithi za kutunga na zilizopitwa na wakati, lakini siku zinakuja utakapokugundua hukuchagua jiwe sahihi kuwa jiwe kuu la maisha yako...wakati huo utakuwa unalia na kuomboleza ukisema laiti ningejua. hata wale waashi walisema hivyo hivyo "laiti tusingelidharau jiwe lile!!"

Leo hii wewe ambaye pesa ndio kila kitu kwako, hata muda wa Kusikiliza habari za msalaba na neema ya YESU KRISTO hauna, unasema nipo buzy natengeneza maisha..Hakika unajenga kwa kutumia jiwe utakalokuja kulijutia maisha yako yote uliyoishi hapa duniani. Wapo waliotumaini mali kuliko wewe na kumweka Mungu nyuma, wanajuta leo hii katika mateso ya moto wa Jehanamu, soma habari ya tajiri wa Lazaro (Luka 16) utathibitisha jambo hilo.

Unayetumainia kipaji chako, uzuri wako,mitindo yako,afya yako na umaarufu wako kama jiwe kuu la pembeni kwa ajili ya mafanikio ya maisha yako na kuacha kumtazama aliye toa uhai wake kwa ajili ya wote wenye mwili (BWANA YESU KRISTO), nawe pia wakati utafika utakapoona kuwa kazi uliyokuwa unaifanya ni bure..Ndugu yangu usitamani ufikie hiyo hatua ya majuto makuu.

Nakushauri leo hii uchague jiwe lililo bora angali muda upo leo kumbuka hili biblia inasema limedharauliwa na waashi wengi, Lakini Mungu kasema kalifanya kuwa jiwe kuu kuliko yote,..Hayo mengine kwa muonekano yanaweza kuonekana ni mazuri lakini ni batili. Chagua jiwe bora YESU KRISTO, katika hatua uliyopo ya maisha yako sasa hivi JENGA KATIKA VIWANGO vitakavyokubaliwa na Mungu na kukupeleka mbinguni. Tubu mpe Bwana maisha yako ukabatizwe kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, na Bwana atakupokea ikiwa umemaanisha. Na Umuushie Bwana.
 
Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment