"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, July 13, 2018

MASWALI NA MAJIBU:SEHEMU YA 33


SWALI 1: Habari nilikuwa naomba unifafanulie maandiko kutoka katika Marko 2:2-12 Kwanini pale Bwana Yesu alichukua hatua ya kusamehe dhambi kwanza badala ya kumponya yule kiwete?.

JIBU: Ubarikiwe dada tuisome kwanza habari yenyewe..

Marko 2: 1 “Akaingia Kapernaumu tena, baada ya siku kadha wa kadha, ikasikiwa ya kwamba yumo nyumbani.
2 Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake.
3 Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne.
4 Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza.
5 Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.
6 Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao,
7 Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?
8 Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu?
9 Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?
10 Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza),
11 Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.
12 Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote,wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe”

.....Kama ukichunguza utaona kuwa jambo la kwanza Bwana aliloliona ni ile Imani yao kwake, aliona ndani yao walikuwa na kitu cha ziada zaidi ya imani ya kuponywa, nayo ni Imani kwa Yesu Kristo.....Na tunajua kitu cha kwanza kilichomleta Bwana Yesu duniani ni kuokoa dhambi za watu, na vitu vingine baadaye… Ukisoma Yohana 8:24 Bwana aliwaambia makutano ..“Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu”....Unaona hapo?...Inakupasa uamini kwanza. Na ndio maana jambo la kwanza alilolitamka yeye kama mkuu wa uzima wa roho za watu mara baada ya kuona Imani yao kwake, akamwambia yule aliyekuwa amepooza..UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO…..Ni Neno zuri na la neema kiasi gani!!!

Lakini wale wengine mawazo yao yalikuwa tofauti, wao walitazamia tu, Bwana amponye yule mtu kisha amwambie nenda zako, halafu yule mtu akaendelee kuishi maisha ya dhambi kisha mwisho wa siku afe aishie kupata hasara ya nafsi yake!..na uponyaji wake wa mwili usimfaidie kitu baada ya maisha ya hapa.

Sasa Ukiendelea kusoma pale utaona Bwana anawauliza tena wale watu, Marko 2:9 “Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?, Sasa kwa namna ya kawaida kwa mtu mwenye akili za rohoni atagundua kuwa ni afadhali usipone ugonjwa wako, lakini dhambi zako ziwe zimesamehewa…kuliko kuponywa halafu dhambi zako ziendeleee kubaki! Na ndio maana Bwana alimchagulia fungu lililo jema la kusamehewa dhambi zake kwanza, kisha baadaye amponye…

Na ndivyo tunavyopaswa na sisi kama wakristo kufanya sasahivi, tunakimbilia kuwaombea watu magonjwa ,wapokee miujiza, na mafanikio na huku tunasahamu kuwafundisha watu habari za msamaha wa dhambi ambao ndio msingi wa Imani ya kikristo.. vyepesi ni vipi??? Ni heri tukamuhubirie mtu habari za msamaha na toba, aokolewe roho yake hata kama hatapokea uponyaji kuliko kuhubiri kila siku mimbarani miujiza na uponyaji na huku bado watu wanakufa katika dhambi zao. Au ni afadhali kufanya vyote kuliko kutupilia mbali habari za msamaha wa dhambi, na kushikamana na miujiza tu.

SWALI 2: Bwana Yesu Kristo asifiwe mtumishi. Nina swali kama ifuatavyo, Katika Biblia neno MASHEHE limetanjwa zaidi ya mara 16 katika kitabu cha Joshua, Samweli, Ezra na Nehemia, katika kitabu cha Joshua na Samweli MASHEHE wameoneshwa kama viongozi wa nchi za kigeni yaani tofauti na Israel, kama vile, Wafilisti, Wagaza, Waashkeloni, Wagati, Waekroni, na Waavi, (Joshua:13:3). Lakini tunawaona tena wakitanjwa ndani ya taifa ya Israel (Pengine kama viongozi), (Nehemia:2:16).


Maswali.. 1.Mashehe walikuwa wahusika na nini katika uongozi wao? 2. Kwa nini mwanzo katika kitabu cha Joshua na Samweli wanatanjwa kama viongozi wa nje, lakini katika kitabu cha Ezra na Nehemia wanatanjwa kama viongozi ndani ya Israel? 3. Kwa nini katika agano jipya hatuwaoni au hawatajwi waliishia wapi? Ahsante sana Mungu akubariki.

JIBU: Ubarikiwe ndugu...Hilo neno SHEHE lisikusumbue sana..kama tunavyofahamu lugha yetu ya Kiswahili maneno mengi yametoholewa kutoka katika lugha ya kiharabu..kwamfano neno shukrani, marhaba, salamu, sultani, sadaka, simba, msalaba,jehanamu, sheria, raisi,uasherati, hekalu, adhabu, adui, askari, lawama, dhamira,roho,damu, giza, tufani n.k. theluthi ya Lugha ya Kiswahili ni kiharabu.

Sasa kwasababu waarabu walikuwepo katika nchi yetu huku zamani zile na lugha yetu ilikuwa bado haijajitosheleza hivyo tukajikuta tunatumia maneno yao katika lugha zetu, na sio kiharabu tu hata na lugha nyingine za kigeni za watu waliotawala nchi yetu... Kwahiyo hilo neno SHEHE asili yake ni kiharabu, likiwa na maana ya Kiongozi, au mwalimu hususani anayehusiana na mambo ya kidini..na ndio maana ukisoma katika tafsiri nyingine za biblia mfano za kiingereza utaona linatumiwa neno Lords, or rulers badala yake...Hivyo kwasababu ni Neno la kiharabu viongozi wa dini ya kiislamu walilitumia sana katika dini yao na ndio maana linaonekana kama ni neno la kiislamu lakini kiuhalisia sio..

kadhalika kama tu neno Rabi ni neno linalomaanisha mwalimu kwa kiyahudi, lakini kwasababu ni neno la lugha ya kiyahudi na linatumiwa sana na viongozi wa dini ya kiyahudi basi inachukuliwa hivyo mtu yeyote anayejiita Rabi yeye ni kiongozi wa dini ya kiyahudi lakini kiukweli sio hivyo hata kiongozi wa dini nyingine yoyote tofauti na ya kiyahudi anaweza kuitwa Rabi kwasababu maana halisi ya neno Rabi ni mwalimu…

Kadhalika na Neno Mchungaji limezoeleka kutumiwa na viongozi wa dini ya kikristo, na halitumiwi na wengine lakini kiuhalisia hata kiongozi wa dini ya kibuddha anaweza kuitwa mchungaji.. Na ndivyo ilivyo hata kwa Neno shehe, kwahiyo pale katika maandiko neno hilo linasimama kama kiongozi wa imani wa dini husika kwa wayahudi na kwa wasio wayahudi.…

Na pia katika agano jipya halijatumika sana hilo neno lakini badala yake yametumika maneno kama waalimu na wachungaji lakini kwa lugha ya kiharabu ndio hao hao.

 SWALI 3: SAYUNI ni nini ndugu zangu?.


JIBU: Tukirudi Mwanzo kabisa Daudi alipoenda kuiteka Yerusalemu,na kufanikiwa eneo lile liliitwa ngome ya SAYUNI (2Samweli 5:7).Hivyo Sayuni kwenye biblia imetumika kama Mji wa Daudi au Mji wa Mungu (YERUSALEMU)..

Kadhalika na lile eneo la mlima ambalo hekalu la Mungu lilijengwa liliitwa pia mlima Sayuni, ambalo lipo hapo hapo Yerusalemu (Yeremia 31:6,12). Sehemu nyingine biblia imetaja Sayuni kama watu wa Mungu yaani wayahudi;

Isaya 60: 14 “Na wana wa watu wale waliokutesa Watakuja kwako [Israeli] na kukuinamia; Nao wote waliokudharau Watajiinamisha hata nyayo za miguu yako; Nao watakuita, Mji wa Bwana, Sayuni wa Mtakatifu wa Israeli”

Unaweza kuona hapo. Kadhalika ukisoma pia (Zakaria 9:9, Sefania 3:14-19),biblia inamtaja Israeli kama binti Sayuni. Yote haya yanaonyesha pia Wayuhudi mbele za Mungu ni sawa na SAYUNI yake. Lakini tukirudi katika agano jipya neno Sayuni limezungumziwa kama ufalme wa watu wa Mungu wa rohoni.

Waebrania 12: 22 “Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, 23 mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika,”

Hapo Mtume Paulo kwa ufunuo wa Roho anaonyeshwa Sayuni hasaa ambayo Mungu aliikusudia kwa watu wake tangu zamani yaani hiyo Yerusalemu ya mbinguni kanisa la Mungu. Mtume Petro pia aliandika katika…

1Petro 2: 6 “Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika. 7 Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni. 8 Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile,wasiliamini,nao waliwekwa kusudi wapate hayo.”

Habari hiyo nayo inathibitisha kuwa kanisa ndiyo Sayuni ya Mungu na ndio pia Yerusalemu ya mbinguni,..na tunafahamu Kanisa msingi wake ni Yesu Kristo, na hapo hiyo Sayuni jiwe kuu lake la pembeni linaonekana ni YESU KRISTO BWANA WETU. Kwahiyo na sisi pia tujitahidi tuwe na sehemu katika hiyo SAYUNI/ YERUSALEMU mpya ya Mungu ambayo Mungu alishaanza kuiandaa na anaendelea kuiandaa hapa hapa duniani.
Ubarikiwe!


No comments:

Post a Comment