"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, July 25, 2018

UKOMA NA UJANE ULIO NDANI YAKO, UMEUPATIA TIBA?

Luka 4: 22 “Wakamshuhudia wote[YESU KRISTO], wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu?
23 Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe.
24 Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe.
25 Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima;
26 wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni.
27 Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu”.

Neno la Mungu ni mwongozo wa kutufundisha sisi kutokurudia makosa yaliyofanyika nyuma na waliotutangulia, Katika habari hii Bwana Yesu anatuonyesha madhara ya kulinganisha Neno la Mungu, na mazingira ya nyuma ya mtu, Kama tunavyosoma tunaona wale wayahudi baada ya kusikia na kuona maneno mazuri ya wokovu yaliyokuwa yanatoka kinywani mwa Bwana, badala ya kuyasadiki wao moja kwa moja wakaanza kutazama mambo mengine yasiyokuwa na msingi na kurejea kuchunguza ameitolea wapi neema hiyo kwa kuilinganisha na chimbuko lake..

Na ndio maana utaona wanasema..huyu sio yule seremala mwana wa Yusufu, dada zake na kaka zake sio hawa tunao hapa mjini kwetu?, na mama yake sio yule Mariam tunayemfahamu?, n.k. Sasa kama ndivyo katolea wapi ujuzi huu wote na maarifa haya yote,?. Wakahitimisha; hawezi akawa na jipya lolote la kutueleza sisi, tumeshamfahamu tangu zamani huyu ni wa hapa hapa…Kwahiyo kwa kufanya vile ikawapelekea ile neema iliyokusudiwa juu yao kuwapita. Na ule wokovu ambao wangepaswa wapate wao kwanza kutoka kwa Bwana kuupoteza.

Kadhalika na ndivyo ilivyokuwa kwa Nabii Eliya wayahudi hawakuupokea ujumbe aliokuwa anawapelekea siku zote, na badala yake wakayatazama maisha yake ya nyuma, pengine walisema huyu mzee kutoka Gileadi kwanza haijui vizuri Israeli, Ndugu zake si ndo hawa wakulima na wafugaji tunaowaona huku, hawana elimu,?..Hivyo wakahitimisha nao pia kuwa Eliya hawezi akawa na jambo la kuwaongezea kitu, kwasababu historia yake ipo wazi. Lakini wakati Bwana anakaribia kuleta njaa kuu juu ya nchi, Eliya hakutumwa kwa mojawapo ya wajane waliokuwepo Israeli kwa wakati ule badala yake alitumwa kwa mjane mmoja katika nchi ya mbali, asiyemjua hata vizuri Mungu wa Israeli lakini kwa kusikia tu kwamba mtu Yule katumwa na Mungu, alimuheshimu sana. Na kupelekea kupata neema ya chakula tele kipindi chote cha njaa.
 
 
Kadhalika hata katika kipindi cha Nabii Elisha jambo ni lile lile, walikuwepo wakoma wengi katika Israeli lakini wenyewe walimwona Elisha ni kama mtu wa kwao tu, hawezi kuwa mtumishi wa kulibeba Neno la Mungu, hawezi kuundoa ukoma wetu huu, tunamjua ni mfugaji, na baba yake na mama yake ndio wale wale wafugaji wasioijua sheria ya Mungu sana, kaka zake na dada zake kila siku tunawaona huku mtaani kwetu ni watu wa kawaida tu, hivyo tuende kufanya nini kwa mtu kama Yule?? Wakakwazika na maisha ya Elisha. Hivyo kwa dharau zao ziliwafanya wabakie na ukoma wao daima..Lakini mtu mmoja kutoka nchi ya mbali (Iitwayo Shamu) aliposikia habari za Elisha tu kutoka wa kijakazi wake, alimwamini na kuamua kufunga safari kwenda kuomba kuponywa, na ndivyo ilivyokuwa alipokea uponyaji wake wote, na wale wengine wenye kiburi walibakia na ukoma wao siku zote za maisha yao.Swali ni je! Kwanini hakukuwa na mkoma yoyote wa Israeli aliyeponywa?. Au mjane yoyote Israeli aliyepewa chakula na Eliya Na badala yake watu wasiomjua Mungu wa Israeli kutoka mbali kuja kuponywa na kupewa chakula?

Jambo hilo hilo linajirudia leo hii, kwanini wanaojiita wakristo wengi hawataenda mbinguni? Sababu ni ile ile, wanajua historia yote ya Bwana Yesu na biblia yote, wanajua mwanzo wote wa ukristo na utakavyokuwa mwisho wake, lakini bado ni wakoma wa rohoni, bado ni wajane wa rohoni, wasiotaka msaada,.. Wanapoletewa habari ya wokovu, na kuhubiriwa watubu dhambi, na waponywe nafsi zao, wanajiona hawawezi kuongezewa kitu kingine cha ziada, sababu tu wao wamezaliwa katika ukristo, na wamepitia mafundisho yote ya biblia na vyuo vyote vya biblia, lakini ndani yao wanapinga maneno ya neema ya Kristo yahusuyo wokovu, utakuta ni mkristo lakini ni mlevi, ni mkristo lakini ni mzinzi, ni mkristo lakini ni msengenyaji, ni mkristo lakini ni mtazamaji wa pornography na mfanyaji wa mustarbation, ni msagaji, ni mvaaji wa vimini, ni mtukanaji, mtu asiyesamehe n.k. Na akiambiwa habari za kutubu dhambi na kujazwa Roho atasema naifahamu biblia, nilishaenda katika mafundisho hayo zamani, huo ni ulokole tu, atakwambia hayo yote chimbuko lake ni hili au hili n.k. hivyo anakuona huna chochote cha kumwongezea yeye…

Biblia inasema siku zinakuja ambazo Bwana ataleta njaa juu ya nchi Soma

Amosi 8: 11” Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.
12 Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.
13 Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu”.

Hizo siku ndio hizi ndugu, kama zilivyokuwa katika siku za Nabii Eliya..Leo hii duniani kote kuna njaa ya Neno la Mungu, ndani ya Ukristo na nje ya ukristo. Wajane na wakoma walikuwepo ndani ya Israeli na nje ya Israeli, Kadhalika na katika ukristo wenye njaa wapo ndani ya ukristo na nje…Lakini kama vile wale wa ndani waliipinga neema iliyoletwa kwao na Nabii Eliya na Nabii Elisha, na kupelekea watu wengine wa mbali kupewa neema, Vivyo hivyo na katika ukristo wanaoipinga neema hii sasa ihusuyo toba na ondoleo la dhambi, wakati utafika itaondolewa kwao na kuhamishiwa kwa watu wengine wasiomjua Mungu wa kweli na Bwana wetu Yesu Kristo na wao wataponywa roho zao, wakati wanaojiita wakristo watakuwa wanakufa kwa njaa.

Leo hii unajiita mkristo na bado ni mkoma wa rohoni, unajiita mkristo na bado ni mjane wa rohoni mwenye njaa, ni kwasababu gani? Ni kwasababu matendo yako hayaendani na ukristo halisi huku unadai unamfahamu Kristo?..Unakuwa huna tofauti na wale watu waliokuwa wanajua chimbuko la Bwana Yesu, mpaka kazi ya baba yake, na ndugu zake walivyo lakini wasione uzima uliokuwa ndani yake...ndivyo ilivyo kwa wewe unayejiita mkristo, unazini, unakunywa pombe, unatazama pornography, unasengenya, unaenda disco,n.k. Hujui kuwa chakula kile ambacho kingepaswa kije kwako kwanza kinapelekwa kwa mtu mwingine ambaye hata hajawahi kusikia habari za ukristo.

Kila siku unahubiriwa utubu dhambi ugeuke, unakataa, lakini wapo wasiomjua Mungu leo hii wanasikia tu mara moja na kugeuka wakati huo huo, waislamu, wahindu, wabudha, wasio na dini, ndio Bwana anaowaangalia kuwapa chakula chake huu wakati wa njaa..Wewe utaendelea kutangatanga huku na kule, hujui kama Mungu alishakuacha siku nyingi na mwisho wa siku utakufa kwa njaa na kuishia jehanum ya milele kwenye mateso yasiyoelezeka. ..

huu sio wakati wa kujisifia dini au kujisifia kuzaliwa katika ukristo, au ujuzi wa maandiko, au chuo cha biblia ulichopitia ,au vinginevyo, Huu ni wakati wa kunyenyekea na kutafuta wokovu na utakatifu kwa bidii kwasababu biblia inasema .

Waebrania 12: 14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”

Ubarikiwe.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu na wao wapone.

No comments:

Post a Comment