"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, August 13, 2018

TWEKA MPAKA VILINDINI.

Luka 5: 1 “Ikawa makutano WALIPOMSONGA wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti,
2 akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao.
3 Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni.
4 Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.
5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.
6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;
7 wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama”.

Tukio hilo lililowapata wakina Petro linaweza likaonekana ni dogo lakini linabeba siri kubwa sana ya mafanikio hususani kwa wale watu ambao shughuli zao za kujipatia kipato haziendi sawa. Hivyo kama wewe ni mmoja wapo somo hili litakufaa sana. Soma hadi mwisho, lakini kama mambo yako yanaenda vizuri basi halitakuhusu sana., Zidi tu kuendelea kujifunza masomo mengine yahusuyo utakatifu na ufalme wa mbinguni.

Ukitafakari hiyo habari utaona Bwana Yesu, alikuwa akihangaika sana katika kuwafundisha makutano, yale mazingira yalikuwa ni magumu sana kutokana na kwamba watu wengi walimsonga na yeye alitaka kuwafundisha zaidi katika utulivu, hivyo hakuona kama akiendelea katika hali ile ile atatimiza kusudi lake, ndipo akaamua atafute madhabahu ya kuwakutanisha wale watu pamoja, mahali atakapotulia ili awafundishe wale watu katika ustaarabu na utaratibu ambao Mungu ameukusudia..

Na alipogeuka akaona vyombo viwili vimeegeshwa pwani na wenye navyo wametoka, ndipo akikichagua cha mmojawapo na kukigeuza kuwa madhabahu yake ya muda.

Sasa Chombo kinawakilisha nini katika mazingira tuliyopo leo?. Chombo kinawakilisha kitu chochote cha kujipatia kipato, kumbuka chombo hicho Bwana alichokitumia kilikuwa ni cha akina Petro cha kuvulia samaki, kwasasa hivi chombo kinaweza kikawa, elimu ya mtu, ujuzi wa mtu, biashara ya mtu, fremu ya mtu, shamba la mtu, kiwanja cha mtu,n.k.

Lakini tunasoma katika habari hiyo, tunaona Bwana alipotazama hakuchagua vyombo vilivyokuwa kando kando vyenye wavuvi au samaki, kumbuka vilikuwepo tu vingi vizuri zaidi ya hivyo vilivyokuwa vinazungukazunguka maeneo yale, lakini yeye hakuchagua chochote kati ya hivyo bali alivichagua vile visivyokuwa na kitu ndani yake…(Na ndio maana somo hili linawahusu sana wale ambao shughuli zao haziendi sawa),

Sasa kilichotokea ni kwamba wakina Petro walifanya kazi ya kuchosha usiku kucha wakihangaika kutafuta samaki ukanda mzima wa ziwa la Genesareti kwa shida, na kujitoa kweli kweli lakini wasipate kitu, mpaka kulipokucha wakakata tamaa ya kuendelea kuvua tena, wakaona kilichobakia tu ni kukipumzisha chombo na kuzitengeneza nyavu zao tena, kisha kuzihifadhi mpaka wakati mwingine,

Lakini baadaye kidogo ndio tunamwona Bwana Yesu akisumbuka na wale makutano, ndipo wao wakamruhusu Bwana kutumia vile vyombo ili kutimiza kusudi lake la kuhubiri,. Na baada ya Bwana kumaliza kuhubiri, sasa wakati makutano yote wameshaondoka ndipo akawageukia wale wamiliki wa vile vyombo, na kuwaambia NENDENI VILINDINI MKASHUSHE NYAVU ZENU, MVUE SAMAKI.

Lakini wao walimwambia, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha pasipo mafanikio, na walipokubali tu kwenda kuvua walipata matokeo makubwa ya kushangaza, mpaka nyavu zao kuanza kukatika, mpaka kufikia hatua ya kuomba msaada kwa wingi wa Baraka hizo, maana rizki imekuwa nyingi na kuwalemea mpaka hawawezi tena kuimaliza wao wenyewe ikawabidi wawaite na marafiki zao na maadui zao waokote na wao pia wapate kidogo..

Bwana Yesu hajabadilika, ni yeye Yule jana, na leo na hata milele, njia aliyotumia kumbarikia Petro ndiyo hiyo hiyo atakayoitumia sasahivi kukubariki na wewe uliyefanya kazi ya kuchosha miaka na miaka bila mafanikio yoyote. Umejaribu kufanya kwa bidii kazi lakini unachokipata hakijitoshelezi…

Leo hii hicho chombo chako kigeuze kuwa MADHABAHU YA KRISTO kwasababu anakitafuta hicho ili ilifanye kusudi lake, kumbuka pale Bwana hakutafuta sinagogi la kuwakusanya wale makutano waliokuwa wanamsonga, hakutafuta hekalu, wala hakutafuta mahali patakatifu bali alitafuta MAHALI PA KUJIPATIA KIPATO KWA MTU, mahali ambapo mtu anapopategemea kujipatia mkate wake wa kila siku, na pia fahamu tu, siku zote Bwana anapaangalia mahali ambapo palipo patupu kama kwako wewe, Mahali ambapo pamefanyika kazi ya kuchosha miaka mingi, miezi mingi pasipo mafanikio yoyote, hapo ndipo anapopataka kwa ajili ya kazi yake, na akishamalizana napo hapo, ndipo atakwambia nenda katupe nyavu zako kilindini uvue samaki, kwa wingi wa atakachokupa Bwana utaita mpaka na marafiki na zako na maadui zako waje nao kushiriki Baraka zako Mungu alizokuandalia.

Leo Kazi yako wewe ni ya ufundi, una ujuzi wa kutosha kuhusu masuala ya ujenzi, na unaona mahali unapokusanyikia pengine ni kanisani kuna kasoro Fulani ya ujenzi, na shughuli zako za kijenzi haziendi sawa, umekuwa ukipata mapato kidogo kupitia hiyo,wakati mwingine unakosa kabisa kazi, huo ndio wakati wa kwenda kumruhusu Bwana atumie hicho chombo chako (ujuzi),
nenda mahali unapokusanyika (kanisa), kazi ya Mungu inapofanywa, angalia kasoro zinazohusiana na taaluma yako, na utumie ujuzi wako kurekebisha tatizo hilo bila kutazamia malipo yoyote, pengine umeona ukuta wa kanisa umebomoka au una ufa, uzibe, umeona mfumo wa maji haujakaa sawa na una ujuzi wa kufanya hivyo, urekebishe hata kama hauna chochote, umeona kanisa halina choo kinachostahili, na wewe una ujuzi wa namna ya kutengeneza vizuri, nenda kafanye hivyo, kajenge kwa ustadi wote, na maarifa yako yote, umeona kuna kasoro ya umeme na mfumo wa nyaya, na una ujuzi huo nenda karekebishe usisubiri hata mtu akamwambie, mruhusu Bwana atumie hicho chombo, na mwisho wa siku utaona tofauti yako na mtu asiyefanya hivyo wakati Fulani ukifika.

Au wewe ni polisi au mlinzi, anza kutoa mchango katika sekta hiyo ndani ya kazi ya Mungu..Usiseme Mungu kweli ataweza kutumia taaluma hii/ujuzi huu kwenye kazi yake??..kumbuka Bwana Yesu alitumia mtumbwi wa wavuvi kuwapelekea maelfu ya watu katika ufalme wa mbinguni…Na wewe vivyo hivyo mpe Bwana chombo chako.

Au wewe unafanya kazi ya upishi, na unaona kazi zako haziendi sawa, faida ndogo, na unaona kuna uhitaji mkubwa wa wapishi ndani ya nyumba ya Mungu, labda kwa ajili ya wazee wasiojiweza (wakristo), au wageni, au wenye mahitaji na mayatima (walio wakristo), ndani ya kanisa n.k usingoje uambiwe au uwe na kitu kwanza ndio ufanye, wewe mwenyewe anza kuchukua hatua ya kujitolea kwenda kuifanya, tena pasipo hata kuombwa.

Wewe ni mtengeneza bustani, na ndiyo kazi yako umekuwa ukifanya kwa ajili ya kujipatia kipato..Lakini mazingira ya kanisani ni machafu au hayavutii, panaonekana ni mahali pasipo tofauti na sehemu nyingine yoyote, Tumia chombo chako (ujuzi) kurekebisha mazingira ya Mungu, pakavutia kama vile unavyopendezesha bustani za watu wengine,..unaweza ukaona ni jambo dogo lakini linamaana kubwa na Bwana akisharidhika atakuambia shuka vilindini..utaona milango Mungu anayokufungulia katika hiyo hiyo kazi yako ilivyo ya ajabu.

Wewe ambaye ulikuwa unatafuta kazi,na bado hujapata, angali unao ujuzi Fulani, usiuache ulale utumie huo ujuzi katika kazi ya ufalme wa mbinguni, kwamfano labda wewe ni “ IT ” (mjuzi wa katika teknolijia ya Kompyuta), unaweza uka unda wavuti na tovuti kwaajili ya kutangaza ufalme wa mbinguni, unaweza ukabuni programu za kutangaza kazi ya Mungu kirahisi katika mitandao fanya kiuaminifu kabisa..Na Bwana akishamaliza kutenda kazi kwa kutumia chombo chako, atakuambia shuka vilindini…Utaona nafasi ambayo ulikuwa unaitafuta kwa kuhangaika kwa muda mrefu pasipo mafanikio kama wakina Petro walivyokuwa..unaipata ndani ya kipindi kifupi tena chenye faida mara 100 zaidi ya kile cha mwanzo ulichokuwa unakihangaikia..

Lakini hizo zote zinakuja kwanza kwa kumtolea Bwana chombo chako akitumie, kwa ajili ya kazi yake, lakini kuna wengine hawapendi kumpa Bwana nafasi lakini wanataka Baraka za Bwana, utakuta mtu analo eneo kubwa limekaa pasipo matumizi yoyote, hataki hata kukaribisha watu wafanyie kazi za mikutano ya injili hapo, na bado anataka Mungu ambariki, ndipo hapo zile roho za udanganyifu zilizoachiliwa katika siku za mwisho zinaanza kumdanganya na kumshawishi, akanunue mafuta ya upako, anunue chumvi na maji ya Baraka akanyunyuzie kwenye kiwanja chake na kwenye biashara yake, aanze kukemea roho za laana katika kiwanja chake, au biashara zake, ili mambo yake yaanze kwenda vizuri.

Utamkuta mwingine anazo fremu za vyumba na zimekosa mpangaji wa kufanyia biashara au tution,..na wakati huo huo kuna wakristo wenzake wamekuja kumwomba awape angalau fremu moja wawe wanafanyia bible study au maombi wakati wa jioni kwa muda huku wanatafuta eneo lingine..lakini kwasababu hajui uweza wa Mungu, anawazuilia na kuona bora tu ziendelee kuwa zimefungwa.na wakati huo huo anazunguka kutafuta kuombewa na kununua maji na mafuta ya upako huku na kule hata wakati mwingine nchi na nchi..Mtu wa namna hii hawezi kutazamia miujiza kama waliofanyiwa wakina Petro.

Bwana anasema nikaribieni, nami nitawakaribia… Wakati mwingine hilo pigo unalolipata la kuvuna haba, ni kwasababu kazi ya Mungu inakaa katika hali ya kusongwa songwa na wewe hutaki kulitazama hilo kwa kumzuilia Bwana chombo chako..(Soma Hagai 1:1-12). Anza leo kufanya kama akina Petro walivyofanya na Mungu atakubariki. Mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.

Ubarikiwe.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu.

Kwa mpangilio mzuri wa masomo haya tembelea website yetu >>> www.wingulamashaidi.org

No comments:

Post a Comment