"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, September 30, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 38


 SWALI 1: Katika Mathayo 15:21-28, Yesu alikuwa na maana gani alipomwambia huyu mama kwamba chakula cha watoto hawapewi mbwa?. Pia kwanini alisema hakutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa Israeli.?

JIBU: Tusome, Mathayo 15: 21 “Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni.
22 Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo.
23 Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu.
24 Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
25 Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie.
26 Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.
27 Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao.
28 Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. “

Kumbuka Bwana Yesu alipokuja duniani, hakutumwa kwanza kwa watu wa mataifa, hapana kwasababu wao hawakuwa wanamtazamia mwokozi yeyote, kadhalika watu wa mataifa walikuwa ni watu wasiokuwa ni dini, wapagani, wasiomjua Mungu, walikuwa wanaabudu miungu,na ndio maana Bwana akawafananisha na mbwa katika mfano huo…

Lakini wayahudi ni watu wa Mungu tangu zamani uzao wa Ibrahimu, pamoja na hayo kwa miaka mingi walikuwa wanalitazamia taraja la wokovu wao ambalo lingeletwa tu na MASIHI mwenyewe atakayeshuka kutoka mbinguni, Hivyo kwa kuwa wale ni uzao wa Mungu, uzao wa Ibrahimu, sasa ulipofika wakati wa Mungu kuwatimizia haja yao waliyokuwa wanaisubiria kwa muda mrefu, ndio akamleta Bwana Yesu duniani aje kuwakomboa..

Na ndio maana sasa tunamwona Bwana Yesu alipokuwa duniani, hakuhubiri katika nchi yoyote ya mataifa, kadhalika hakuwatuma hata wanafunzi wake katika mji au kijiji chochote cha mataifa, kwasababu hakutumwa kwao, bali kwa wale waliomtazamia (yaani wayahudi).

Lakini hapa tunamwona huyu mwanamke ambaye ni mtu wa Tiro, (mwanamke aliyekuwa wa kimataifa), asiyekuwa na dini wala Imani katika Mungu wa kweli, alipomwona Bwana akipita kando kando ya miji yao, akamfuata ili ahudumiwe naye, lakini Bwana hakuonyesha kumjali kwa namna yoyote ile, lakini kwa vile alivyokuwa akimsumbua sumbua, ndipo Bwana akamwambia sikutumwa [kwa watu wa mataifa] ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli (yaani wayahudi)..lakini alipozidi kumsumbua sumbua, aliongezea na kumwambia “si vema kutwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa”..yaani akiwa na maana kuwa si vizuri kuiondoa ile neema ya wokovu kwa wale waliostahili kuipokea(yaani wayahudi) na kuwapatia watu ambao hawakustahili kuipokea au kuitazamia(watu wa mataifa).

Lakini pamoja na hayo tunakuja kuona baadaye, ile neema ililetwa kwetu sisi mataifa, baada ya wale ambao waliostahili kuipokea kuikataa, hivyo sisi sasa sio mbwa tena bali tumefanywa kuwa wana wa Mungu kwa damu ya Yesu Kristo.
Hiyo ndio siri iliyokuwa imefichwa tangu zamani kwamba sisi watu wa mataifa tumehesabiwa kuwa warithi wa wokovu sawa na wayahudi kwa njia ya Yesu Kristo. Haleluya. Hivyo ndio maana Mtume Paulo akasema katika..

Waefeso 3: 4 “Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.
5 Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;
6 ya kwamba MATAIFA NI WARITHI PAMOJA NASI WA URITHI MMOJA, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili; “

Hivyo somo la kujifunza, hapo ni lipi?. Tumwendeapo Mungu, kwa haja ihusuyo wokovu wetu, hata kama ni kweli tutakuwa hatustahili mbele za Mungu, pengine njia zetu zimekuwa mbaya sana, na tumeomba mara ya kwanza, na ya pili na ya tatu hatujajibiwa…Hatupaswi kukataa tamaa, tuzidi kuomba tuzidi kuomba kama yule mwanamke..Kwasababu Bwana Yesu alishatupa mfano unaofanana na huo, juu ya yule kadhi dhalimu, aliyekuwa hamchi Mungu, lakini yule mwanamke mjane alivyomwendea mara ya kwanza hakupewa haki yake, lakini kwa jinsi alivyokuwa akimwendea endea mara kwa mara, alimpatia haki yake, japo hamchi Mungu, ili asije akamsumbua daima…(Luka 18:1-8)

Vivyo hivyo na sisi tusiache kumwomba Mungu neema ya wokovu, neema ya uponyaji, mahitaji binafsi, hata kama hatutaona dalili zozote za kujibiwa maombi yetu. Kwasababu Mungu anapendezwa na mtu aombaye kwa bidii.

 SWALI 2: Ndugu zangu Mungu anasababisha AJALI yeyote?.Iwe ya meli,gari,pikipiki,baiskeli,angani ndege,moto n.k?.Mfano wa ajali ya meli ya 'titanic'","mfano wa ajali ya gari lililobeba wale watoto wa shule ya Lucky Vicent(na hizo ajali nyingine)","mfano wa ajali za hosteli/mabweni kuungua moto na watu kufia huko",n.K.K..Ndugu zangu hizi zote zinasababishwa na BWANA wetu YESU KRISTO au ni Shetani.?Karibuni sana ndugu zangu..

JIBU: Mungu hasababishi ajali yoyote ile, japo Mungu anaweza akamwadhibu mtu kwa makosa yake. Shetani ndiye mwenye lengo siku zote la kuangamiza hata wakati ambapo mtu hana makosa, kama alivyofanya kwa Ayubu, kwasababu biblia inasema yeye alikuwa ni muuaji tangu mwanzo.(Yohana 8:44).

Asilimia kubwa ya ajali na majanga yanaletwa na shetani. Na pia biblia inasema yapo majanga mengine yanaletwa na Mungu mwenyewe, na mpaka imefikia hivyo ujue ni adhabu kutokana na makosa ya watu wenyewe, na pia Bwana anasema huwa hafanyi jambo lolote bila kuwafunuliwa hao watumishi wake manabii, kuwaonya kama tunavyoona alivyofanya kwa watu wa Ninawi.

Leo hii mtu anamuudhi Mungu labda ni muuaji, lakini kabla Mungu hajamwadhibu atamwonya pengine kwa kumtumia Mtumishi wa Mungu au kwa kusikia mahubiri, na akajua kabisa Mungu anamwonya atubu utakuta pengine alisikia Neno likisema “Uaye kwa upanga, atauawa kwa upanga”..

Lakini yeye akapuuzia na kuendelea na tabia yake ya kuuiba na kuua watu pasipo hatia.. Sasa mtu kama huyo inatokea mazingira labda siku moja amekutana na kundi la wanyang’anyi usiku, na kwa bahati mbaya wakamvamia na kumchoma kisu, kisha na kufa..Sasa kwa nje unaweza ukasema ni shetani lakini sio shetani bali ni Mungu mwenyewe kamlipizia kisasi juu yake.

Hivyo zipo ajali zinazotoka kwa Mungu mwenyewe. Kadhalika zipo pia zinazotengenezwa na shetani, ambazo hizo ndio nyingi kuliko zile zinazotoka kwa Mungu.

 SWALI 3:Matendo15:37"Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.38"Bali Paulo HAKUONA VEMA kumchukua huyo aliyewaacha huko pamfilia,asiende nao kazini.39"Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana....,swali Kwanini huyu mtume Paulo hakumsamehe huyu Yohana aitwaye Marko hata waende naye wawe watatu yaani Barnaba,Yohana aitwaye Marko,pamoja na yeye Paulo wa tatu.Kwanini walishindana na wao ni Wakristo??

JIBU: Ukisoma kitabu cha matendo 13:13 utaona Yohana, aliwaacha wakina Paulo na Barnaba huko Pamfilia, inaonekana aliogopa dhiki itakayokwenda kuwakuta mbeleni, kwasababu Paulo bado mzigo wa kupeleka injili duniani kote alikuwa nao, hivyo walipomsihi waende pamoja alikataa, lakini sasa baadaye tunakuja kumwona tena akikutana na mtume Paulo na Barnaba na kutaka kujumuika nao katika kwenda kuipeleka injili, na ndio hapo tunaona mtume Paulo hakukubali jambo hilo kwasababu kama alishindwa kuandamana nao wakati wa tabu za awali,

kadhalika hataweza kushikamana nao katika dhiki zinazofuata, hivyo sio kwamba Paulo hakumsamehe, alimsamehe lakini hakutaka kuambatana naye tena ili asiwe kikwazo cha injili kwenda mbele.

Ni mfano tunaopaswa tujifunze na sisi [watumishi wa Mungu], kazi ya Mungu si ya kuifanya kirafiki tu, hapana bali wale watakaoitenda kazi kiuaminifu ndio tuambatane nao na kuwatambua hata kama watakuwa si watu wetu wa karibu sana. Lakini ikiwa ni ndugu halafu anaipuuzia kazi ya Mungu, hapo ni kumweka kando, Biblia ilishasema

Wafilipi 2: 12…utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.
13 Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu,

 SWALI 4: Ni sahihi kwa Mkristo mtakatifu kumwambia BWANA ailaze roho ya mtu aliyekufa mahali pema PEPONI?.Mfano mtu huyu ni Yeze amekufa aidha alikuwa Mwema ama muovu sasa ni sahihi kwa Mkristo mtakatifu kusema "Bwana Yesu Ailaze roho ya marehemu Yeze MAHALA PEMA PEPONI"?..

JIBU: Sio sahihi, kwasababu ameshakufa. Tumepewa amri ya kuombeana sisi kwa sisi, yaani tunapokuwa tunaishi hapa duniani, baada ya kufa hatujapewa amri ya kuombeana. Hakuna maombi yoyote yanayoweza kubadilisha hatima ya mtu aliyekufa, kilichobakia kwa mtu aliyekufa ni hukumu tu! (waebrania 9:27).

Mazishi ya watu wasioamini ni tofauti na mazishi ya watu waliomwamini BWANA wetu Yesu Kristo, wasiomwamini wao hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na mambo yatakayofuata baada ya kifo, ndio maana wanasema maneno hayo, lakini sisi tulioamini ndio tunaoelewa kwamba kama ndugu yetu amekufa katika Bwana, basi tunalo tumaini la kukufuka tena kwasababu ni kama amelala tu!.. Lakini kama mtu amekufa katika dhambi na hakumpokea Kristo basi huyo hana tumaini la uzima wa milele, hivyo hawezi kuokolewa kwa maombi yoyote yale. Kwasababu Bwana Yesu alitupa maagizo ya kuenenda ulimwenguni kote kuihubiri injili, AAMINIYE NA KUBATIZWA ATAOKOKA, hakutupa agizo la kuenenda ulimwenguni kote kuwaombea wafu waokoke au walazwe mahali pema peponi.

Kwahiyo saa ya wokovu ni sasa katika maisha haya, baada ya maisha haya ni hukumu.

Ubarikiwe.

.

Tuesday, September 25, 2018

TANGAZO.


Shalom!

Tangazo.

Ndugu/Dada atakayehitaji kubatizwa, siku ya jumamosi (yaani tarehe 29/09/2018), tutakuwa na huduma ya ubatizo, maeneo ya Ocean road, Dar es salaam. Ubatizo utakuwa ni wa kuzamishwa katika maji mengi kama maandiko yanavyotuagiza na utakuwa ni katika JINA LA YESU KRISTO sawasawa na Matendo 2:38, mdo 8:16,mdo 10:48, na mdo 19:5. 
 

Hivyo ikiwa na wewe ni mmojawapo atakeyekuwa na uhitaji huo wa kubatizwa, tutawasiliana kwa namba zilizohapo chini au kwa inbox. Kadhalika unapopata ujumbe huu mtaarifu na wenzako anayehitaji kufanya hivyo. Hakuna kiingilio, hakuna madarasa ya kupitia kwanza, kwani biblia inatuongoza kuwa pindi mtu anapoamini tu! anapaswa akabatizwe kwa ajili ya ondoleo la dhambi zake.

Kumbuka ili mtu awe amezaliwa mara ya pili ni lazima awe amebatizwa kwa maji na kwa Roho. Hivyo ikiwa ulishaamini na bado haujabatizwa, au ulibatizwa kimakosa utotoni, basi yakupasa ukabatizwe tena kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako. Kumbuka pia ubatizo sio dini mpya au dhehebu jipya bali ni maagizo mwamini yeyote yule anapaswa ayafuate.

Mungu akubariki.

Tuwasiliane kwa namba zifuatazo / 0679804471 au 0787070918.

MANA ILIYOSHUSHWA KUTOKA MBINGUNI.


Katika agano la kale, wakati wana wa Israeli wakiwa safarini kuelekea nchi ya ahadi, walioahidiwa na Mungu mwenyezi, tunaona Bwana Mungu, alijua shida iliyokuwa mbele yao kwamba watapita katika nchi ya jangwa isiyokuwa na kitu, isiyokuwa na kupanda wala kuvuna, nchi kame, hivyo alikuwa ameshawaandalia namna ya kuwalisha kabla hata hawajatoa miguu yao Misri, na ndio tunaona, aliwashushia MANA itokayo juu mbinguni, lakini Bwana alikuwa na sababu kubwa sana ya kufanya vile, kutowapitisha njia yenye chakula tele, au yenye masoko ambayo wangeweza kununua chakula.

Sasa moja ya muujiza mkubwa wa ile mana, ni kwamba haikuwa mikate kama mikate, hapana bali zilikuwa ni chembe ndogo kama za mtama, ambazo walipoamka kila asubuhi walizikuta juu ya ardhi, na walipozikusanya walienda kuzisaga, na kuwa unga kisha kuzitengeneza kuwa mkate.
Wale waliokusanya mana nyingi, waliwapunguzia wale waliokusanya vichache hivyo hakuna aliyemzidi mwenzake…

Kutoka 16:14-18” Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi.
15 Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa ninyi, mle.
16 Neno hili ndilo aliloagiza Bwana, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi,kama hesabu ya watu wenu ilivyo ;ndivyo mtakavyotwaa,kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.
17 Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua.
18 Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa"

Sasa jambo tunaloweza kujifunza hapo, ni kwamba Bwana alitaka kuwafundisha watu wake kwamba waishi kama ndugu, wahudumiane kila mtu na nduguye, mmoja anapokusanya kingi na mwingine anapokusanya vichache, yule mwenye nyingi ampunguzie yule mwenye vichache, kwasababu wamepewa bure.

Jambo hilo hilo linaendelea sasa katika Roho, kama vile wana wa Israeli walipewa mana ya mwilini kuwafanya waishi kule nyikani, leo hii Bwana Mungu ametoa MANA YA ROHONI kutufanya sisi tuishi katika Jangwa hili la Roho, na kama vile mana ile ilishuka tu kwa wana wa Israeli na sio watu wote wa ulimwengu mzima, vivyo hivyo na mana hii ya sasa ya Rohoni, itawafaa wale tu, waliokuwa tayari kuchukua gharama za kutoka Misri(ya rohoni) na kuelekea kaanani.

SASA HII MANA NI IPI?

Hii mana mpya si mwingine Zaidi ya BWANA WA UTUKUFU, YESU KRISTO. Biblia inasema katika…
Yohana 6: 28 “Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?
29 Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.
30 Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani?
31 Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale.
32 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni.
33 Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.
34 Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki.
35 Yesu akawaambia, MIMI NDIMI CHAKULA CHA UZIMA; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe”.

Unaona hapo? Bwana Yesu ndio chakula cha uzima, mfano wa mana, sasa aliposema chakula hakumaanisha vyakula vya kupikwa na wanadamu, hapana! Ukisoma katika tafsiri nyingine za kiingereza tafsiri hapo ya chakula ni “bread” yaani “mkate”John 6: 35”Then Jesus declared, “I am the bread of life. Whoever comes to me will never go hungry”

Hivyo kama vile, MANA ilivyokuwa inaliwa na wana wa Israeli siku kwa siku, vivyo hivyo Mana hii mpya ya rohoni tuliyopewa na Baba, tunaila siku baada ya siku, ikiwa na maana kuwa, tunajifunza maneno ya YESU KRISTO siku kwa siku, hatuachi mpaka siku tutakayoingia kaanani yetu(mbingu mpya na nchi mpya).

Ndio maana tunashiriki meza ya Bwana,(divai na mkate) kipindi baada ya kipindi, kuashiria kuwa katika roho zetu tunakula maneno ya Yesu Kristo siku kwa siku.

Na kama vile ile mana si wote waliokota kwa kipimo kimoja, wengine waliokota kingi wengine pungufu, lakini aliyeokota vingi alimpunguzia yule aliyeokota vichache, vivyo hivyo na katika MANA hii ya rohoni, tumepewa agizo la kukusanyika pamoja ili Bwana atuhudumie Neno lake kila mtu kwa kipimo cha karama alichomkirimia, na ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kukusanyika pamoja.

Tunakuwa tunaula mwili wa Yesu kristo ambaye ndiye chakula kitokacho mbinguni siku baada ya siku. Na ndio maana Bwana aliendelea na kusema ..

Yohana 6: 48 “Mimi ndimi chakula cha uzima.
49 Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa.
50 HIKI NI CHAKULA KISHUKACHO KUTOKA MBINGUNI, KWAMBA MTU AKILA WALA ASIFE.
51 Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.
52 Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, AWEZAJE MTU KUTUPA SISI MWILI WAKE ILI TUULE?
53 Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, MSIPOULA MWILI WAKE MWANA WA ADAMU NA KUINYWA DAMU YAKE, HANA UZIMA NDANI YENU. 
54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 AULAYE MWILI WANGU NA KUINYWA DAMU YANGU HUKAA NDANI YANGU”.

Umeona Umuhimu wa Yesu Kristo kwa wakati huu? Wana wa Israeli wasingeweza KUFIKA KAANANI pasipo kupitia njia ya jangwa Mungu aliyoikusudia wala pasipo kuila MANA chakula Mungu alichokichagua, Kadhalika na wakati huu wa sasa Hutuwezi kufika mbinguni pasipo kupitia njia ya jangwa wala pasipo kuila ile mana ya rohoni Mungu aliyoikusudia (yaani Yesu Kristo).

Njia zipo nyingi ndugu, lakini njia pekee ya kumfikia Mungu ni Yesu Kristo ndiye, na yeye alisema mwenyewe,..
Mathayo 16: 24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.
25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.
26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? “

Chukua gharama ya kutoka katika utumwa wa dhambi (Misri) na ingia gharama za kumfuata Bwana YESU katika njia ya jangwa kama unataka kufika mbinguni. Huko katika kaanani ya watakatifu, hawataingia waasherati, hawataingia walevi, hawataingia wasengenyaji, hawataingia wauaji, hawataingia wavaaji wa vimini wala wapakaji wanja wala watoaji mimba, hawataingia mashoga,wala watazamaji pornography, wala wasiosamehe, hawa wote sehemu yao itakuwa ni katika lile ziwa la moto biblia inasema hivyo. Wanaokuambia utaingia mbinguni kwa kufanya vitu hivyo wanakudanganya hawana haja na roho yako, wanataka vya kwako.

Hivyo geuka leo, ukatwae mkate wa uzima (Yesu Kristo). Mkate unaoshiriki kule kanisani, halafu bado ni muasherati, utapata hatia juu ya mwili wa Yesu Kristo na damu yake, kwasababu unashiriki isivyopasa.

1 Wakorintho 11: 23 “Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate,
24 naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
25 Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.
26 Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.
27 Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana ISIVYOSTAHILI, ATAKUWA AMEJIPATIA HATI YA MWILI NA DAMU YA BWANA.
28 Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.
29 Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili.
30 Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala.
31 Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa”.

Hivyo kula mana sasa, na hii hatuipati pengine mbali na pale wana wa Mungu wakusanyikapo.

Ubarikiwe.

VIGEZO VYA KUWA KARIBU NA YESU KRISTO KATIKA ULIMWENGU UJAO.


Wakati raisi wa Marekani Barack Obama alipokuja Tanzania mwaka 2013, japo wengi walifahamu kuwa ni ngumu kuketi meza moja naye au kumpa mkono lakini pamoja na hayo wengi waliona pia itakuwa ni bahati walau wakiuona msafara wake ukipita barabarani, Hilo tu lingewatosha watu kujiona kuwa ni wenye bahati sana kushuhudua tendo kama lile ambalo watu wachache sana wanaweza kuliona. Na mara nyingine unaweza ukafikiria wale watu wanaoongozana naye kila mahali ni watu ambao wamebahatika kuliko watu wote duniani. Kwasababu kiongozi ambaye ni mkubwa na anayeheshimika duniani kote mahali popote atakapokuwepo yupo nao. Kadhalika wewe nawe ungekuwa katika nafasi ile ungejiona kuwa ni mtu uliyebahatika sana (tunazungumza kwa namna ya kidunia).

Lakini biblia inatuambia YESU KRISTO, Ndiye Mfalme ambaye atakuja kuubatilisha ufalme wote wa hii dunia na kisha atauweka UFALME mpya wa milele usioasika, Biblia inasema yeye atakuwa ni MFALME WA WAFALME, na BWANA WA MABWANA. Ataitawala dunia yote kwa fimbo ya chuma, pale dunia wakati huo itakaporejeshwa katika hali yake ya mwanzo ya uzuri, basi chini yake kutakuwa na wafalme wengi na makuhani wengi, na mabwana wengi sana. Kumbuka wakati huo bahari haitakuwepo, kwani tunajua bahari imechukua asilimia 75% ya dunia, sasa bahari ikiondolewa unaweza ukaona kama ni mabara duniani yatakuwa mangapi?, kadhalika majangwa nayo hayatokuwepo, na wala hakutakuwa na sehemu yoyote ya dunia itakayokuwa ukiwa, sehemu zote zitakuwa zimejaa utukufu wa Mungu na wanadamu.

Kama biblia inavyosema Mfalme wetu YESU KRISTO atatawala na watakatifu wake kwa kipindi cha miaka 1000, kabla ya ule umilele kuanza. Unafahamu sasahivi Kristo ameketi katika kiti cha neema kama mkombozi lakini atakaporudi mara ya pili, sura yake itabadilika hatakuwa tena kama Yesu mwokozi bali YESU MFALME?. Na kama ni mfalme basi na tabia zile zote za kifalme ni lazima ziambatane naye. Na Ndio maana Mungu aliruhusu kwanza tupitie kuziona falme za ulimwengu huu, walau kwa sehemu tupate picha juu ya ule ufalme usiokuwa na mwisho utakavyokuja kuwa huko mbeleni.

Wengi wetu tunadhani, tukienda mbinguni basi watu wote watakuwa sawa kisha tutakuwa usiku na mchana tunamwimbia tu Mungu kama vile malaika. Lakini hiyo sio kweli, huko tunapokwenda biblia inatuambia kuna UFALME, na kuna MBINGU mpya na NCHI mpya. Ikiwa ni Ufalme basi kuna kutawala na kutawaliwa. Na kama vile watu wa ulimwengu huu wanavyoupigania ufalme mpaka waupate, kadhalika na ufalme wa mbinguni unapiganiwa, vinginevyo nguvu yako ikiwa ni ndogo kule hutatawala bali utatawaliwa (hapa tunawazungumzia waliookolewa, na sio watu wote, hao wenye dhambi wakati huo watakuwa katika ziwa la moto).. Na ndio maana Bwana YESU alisema.

Mathayo 11: 12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka”.
 
Unaona hapo?. Kuwa na uhakika wa kwenda mbinguni tu hautoshi, bali nafasi utakayokwenda kuwa nayo huko, na aina gani?
 
Na tena sasa baada ya wanafunzi wake kulisikia hilo, wakijua ya kuwa Kristo ndiye atakayekuwa mmilika wa ufalme wa Mungu, wawili kati ya wanafunzi wake walimwendea kwa siri na kumwomba wafanyiwe jambo kama tunavyosoma katika..
 
Marko 10: 35 “Na Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba.
36 Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini?
37 Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.
38 Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?
39 Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa;
40 lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari.
41 Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana".
Unaona hapo, mfano tu leo hii raisi wa hii nchi angekuwa na rafiki zake wawili ambao tangu zamani walijua kuwa atakuja kuwa raisi, ni wazi kuwa wangemwomba mmojawao awe makamu wake na mwingine waziri mkuu, lakini Raisi asingeweza kuwaambia neno “sawa” kirahisi rahisi tu, ni wazi kuwa yapo masharti yangepaswa wayafuate kutoka kwa raisi tangu kipindi kile kile ambacho kabla hajawa hata Raisi, pengine angewaambia, mkiwa na mimi katika kampeni zangu zote na kunipigia debe, ndipo nitawafanya wote kuwa hivyo, au wahakikishe siku zote wanamletea taarifa zote za maadui zake, kadhalika kwenye shida zote zitakazojitokeza wawe pamoja nye na Zaidi ya yote wawe na angalau na ujuzi Fulani au maarifa Fulani kuhusiana na hayo mambo ya uongozi…Hivyo wakishinda hivyo vigezo, ule wakati ukifika basi atawafanya kuwa viongozi..

Kadhalika na kwa Bwana wetu Yesu Kristo, tunaona wanafunzi wake wawili walimfuata na kumwomba jambo gumu kama lile, kwamba katika ufalme wake awajalie mmoja aketi mkono wake wa kuume na mwingine wa kushoto, lakini yeye akawaambia je! KIKOMBE nikinyeacho mtakinywea?, kadhalika UBATIZO nibatizwao mtabatizwa??.

Hilo ni swali tunauliza hata sisi tunaotamani siku ile YESU KRISTO akiwa kama MFALME atatumbue kama watu wake wa karibu sana wenye heshima kubwa katikati ya wingi wa watakatifu na malaika watakaokuwepo siku zile atakapokuja kutawala dunia…JE! KIKOMBE nikinyeacho mtakinywea?, JE! UBATIZO nibatizwao mtabatizwa??.

Kwa maneno mepesi ni wazi kuwa kila mtu atatamka, Ndio nitaweza! Kama vile wale Yakobo na Yohana walivyotamka,,..Lakini Bwana kwa kuwa alikuwa hajui waliombalo akawaambia ni kweli mnaweza kufanya hivyo lakini yeye hawezi kutamka kuwa mtaketi naye isipokuwa wale Baba aliowaweka tayari..Kuna lugha nyepesi tunaweza kusema “wale ambao Mungu atawapa neema kunywea kukombe kama cha kwake, na kubatizwa ubatizo kama wa kwake hao ndio watakaoketi pamoja naye katika ufalme wake.”.

Swali Kikombe ni nini? Na Ubatizo ni upi?

Kikombe, kama wengi tunavyojua ni mateso kwa ajili ya ushuhuda ulionao, kama tunavyomwona Bwana wetu Yesu alivyopitia yale mateso Makali kama yale mpaka kufikia kufa, kwa kuliona lile kwa uchungu mwingi akatamani hata mateso yale yamwepuke, lakini Mungu alimpa nguvu ya kuyashinda…
 
Mathayo 26: 39 “Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe”.

Lakini UBATIZO ule unaozungumziwa pale haukuwa ubatizo wa maji tena hapana, kwani alikuwa ameshabatizwa wakati huo aliokuwa anazungumza hayo maneno.

Luka 12: 49 “Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi?
50 LAKINI NINA UBATIZO UNIPASAO KUBATIZIWA, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe! “

Kama tunavyofahamu neno Kubatizwa ni kuzamwishwa/kuzikwa, tunapobatizwa ni ishara ya kuwa tunakufa na kufufuka na Kristo katika ubatizo wake. Na ndio maana tunasoma katika

Warumi 6: 3 “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?
4 Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. “

Kwahiyo kama tunavyoona hapo ubatizo Yesu Kristo aliokuwa anauzungumzia hapo ni kile kitendo cha KUFA, KUZIKWA, na KUFUFUKA. Huo ndio ubatizo aliokuwa anaungojea.

Lakini leo hii tunaona wengi tunapenda kumfuata Yesu lakini kuingia gharama hatutaki, Bwana Yesu alisema mtu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama asipoacha vitu vyote na kubeba msalaba wako na kunifuata, na pia kama yeye alivyoutoa uhai wake kwa ajili yetu, na sisi pia imetupasa kutoa uhai wetu kwa ajili ya Kristo , na pia maandiko yanasema hatujapewa kumwamini tu, bali hata kuteswa kwa ajili yake. Njia hiyo hiyo ya msalaba ya kudharauliwa ndiyo iliyowafanya Bwana wetu Yesu Kristo kuwa MFALME,

Waebrania 12: 2 “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake ALIUSTAHIMILI MSALABA NA KUIDHARAU AIBU, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
3 Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu”.


kadhalika pale itupasapo kupitia hayo, basi tujue kuwa Mungu ametuchagua kumkaribia yeye katika ufalme wake, ili siku ile na sisi tuwe na jina mbele zake. Kwanini mitume hawakuona ni kitu kuuliwa kwa ajili ya Kristo ni kwasababu walitamani kumkaribia Kristo katika ufalme wake.

Bwana akubariki.

Thursday, September 20, 2018

VITA VYA KIFIKRA BAADA YA KUZALIWA MARA YA PILI

Yapo mengi ya muhimu mtu anapaswa kufahamu pindi tu anapozaliwa mara ya pili, vinginevyo shetani atatumia nafasi hiyo kumtesa na kumwangaisha mtu huyo kwa lengo tu la kumfanya auache wokovu mara: na moja ya mambo hayo, ni kumfanya mtu KULIHISI LILE DENI LA DHAMBI BADO LIPO NDANI YA MOYO WAKE.

Sasa mtu anapozaliwa mara ya pili [kumbuka, tunaposema kuzaliwa mara ya pili Neno linamaanisha mtu aliyekusudia kutubu kutoka moyoni mwake na kudhamiria kabisa kuacha dhambi zake, kisha akabatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa Jina la YESU KRISTO, kisha akapokea Roho Mtakatifu]. Mtu wa dizaini hiyo anakuwa kuanzia huo wakati amefanyika kiumbe kipya, na deni lote la dhambi liliokuwa juu yake, Mungu anakuwa ameshaliondoa, na anafanyika kuwa mtoto halali wa Mungu.

Lakini tatizo linakuja tu ni pale mara baada ya kuzaliwa mara ya pili vita vya kifikra vinaanza kuibuka ndani, shetani akishajua wewe umeshahesabiwa haki mbele za Mungu, na ile hatia ya dhambi zako haipo tena, kitu atakachofanya baada ya yeye kujua uchanga wako ataanza kuangalia sehemu zilizokuwa dhaifu katika maisha yako ulizokuwa unamwasia Mungu na kwa kupitia hizo atazigeuza kama mwiba wa kukushambulia wewe ujione kama haufai mbele za Mungu.

Jambo la muhimu la kufahamu kwa kila mtu, ni kwamba unapozaliwa mara ya pili hauwi kama robot, ambaye anaweza akaondolewa taarifa zake zote za kumbukumbuku na kuwekewa nyingine mpya (kuwa- formated), na kusahau vyote vya nyuma, pasipo kukumbuka hata kimoja. Hapana haiwi hivyo kwa mkristo pale anapozaliwa mara ya pili.

Mtu anapozaliwa mara ya pili kitu anachokifanya Roho Mtakatifu baada ya kumsamehe dhambi zake ni kuondoa ile kiu ya kutenda dhambi ndani ya mtu [anampa kila sababu ya kuona madhara ya dhambi], ndio hapo unakuta kama mtu alikuwa anakunywa pombe anaacha, alikuwa mvutaji sigara anaacha, alikuwa mwasherati hataki kufanya tena vile, alikuwa mwizi hofu ya Mungu inamwingia haibi tena, alikuwa mtukanaji ile kiu ya kutukana inakufa…

Lakini tatizo linalojitokeza ni pale anafanikiwa kweli kufanya hivyo lakini bado anaona kuna vitu havijaisha vizuri ndani yake..Kwamfano wapo watu wengi wanasema nimeacha uasherati lakini ndoto za uasherati zinanisumbua, mwingine anasema nimeacha uzinzi lakini na mawazo machafu yananisumbua, nashindwa kutawala mawazo yangu, kila ninapojaribu ninajikuta nimezama huko tena jambo ambalo linanikosesha raha, mwingine anasema nimeacha usengenyaji lakini kuna muda ninajikuta nimesengenya jambo ambalo baada ya hapo ninajisikia vibaya sana.

Mwingine anasema nimeacha kusikiliza miziki ya kidunia lakini zile nyimbo bado zinajirudia rudia kichwani mwangu, zinajiimba na sipendi zijirudie kwasababu nafahamu MUNGU hapendezwi nazo,,nifanyeje?. Mwingine atakwambia niliwahi kutoa mimba, nikatubu lakini ndani bado kuna kitu kinaniambia sijasamehewa jambo ambalo linanifanya nijihisi kama Mungu ananichukia,
mwingine anasikia wazo linamwambia amemkufuru Roho Mtakatifu hivyo dhambi yako hata atubuje hatasemehewa kwasababu alifanya dhambi Fulani zamani kwa makusudi.

Mwingine atakwambia baada ya kumpa Bwana maisha yangu na kuacha ushirikina, bado wachawi wananijia usiku, n.k. 
Kumbuka hawa wote ndani ya mioyo yao wanatamaini na wanadhamira safi ya kuwa wasafi na watakatifu lakini wanashindwa. Kwa Nje wanajitahidi kweli kuishinda dhambi lakini ndani ni vita vikali kweli vya kimawazo, n.k.

Sasa hawa wote kazi anayoifanya shetani ni kuzidi kuwakandamiza na kuwakandamiza kwasababu ya uchanga wao. Kwasababu hawajui kuwa tangu siku ile ya kwanza walipoamua kutubu na kufuata hatua zote za wokovu, Mungu alishawasamehe dhambi zao pasipo matendo yoyote. Mungu hakuangalia uelekevu wao, au utakatifu wao ndipo awasamehe, hapana aliwasamehe bure tu kwa neema yake. Hivyo walipofanyika kuwa wana wa Mungu tu, walihesabiwa kama watakatifu wa Mungu..

Lakini sasa jambo linaloendelea katikati yao ni kama vile gari lilokuwa katika mwendo kasi lililopigwa breki ghafla, haliwezi likasimama hapo hapo, hapana bali litaendelea na mwendo kidogo, japo kuwa matairi yatakuwa hayazunguki, vivyo hivyo hali yake mtu anayezaliwa mara ya pili,.Anakuwa ametoka kwenye dhambi fresh, ametoka kwenye dunia fresh, anatoka kwenye uasherati, anatoka kwenye matusi n.k.

Sasa Roho Mtakatifu anapopiga breki ghafla kwenye maisha yake ya dhambi, na kukata kiu yote ya dhambi ndani yake, kweli matairi yatasimama, ndio hapo yule mtu utakuta hataki kuendelea mbele na maisha ya dhambi tena, lakini kwasababu alikuwa kwenye mwendo kuna nguvu ya zamani iliyokuwa ndani yake iliyokuwa ikimsukuma kufanya zile dhambi haiwezi kusimama saa hiyo hiyo, itachukua muda kidogo ndio iondoke kabisa.. Na ndio maana Biblia inasema “kile apandacho mtu ndicho atakachovuna”, hapo ndipo utakapojua kuwa dhambi ina madhara makubwa, ina maumivu makali, inalipiza kisasi, na kuindoa itampasa mtu aingie gharama yake binafsi mbali na ile breki ya Roho Mtakatifu..

Ushahidi utakaokuonyesha kuwa wewe ni mtoto wa Mungu ni kwamba utaona unayachukia yale mambo ya kale lakini baadhi bado utayaona unayatenda pasipo wewe mwenyewe kupenda. Tofauti na hapo mwanzo ulipokuwa kwenye dunia, uliyatenda wala hakukuwa na kitu ndani kikikuhukumu, Na ndio maana Mtume Paulo aliandika..

Warumi 7: 14 “Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi.
15 MAANA SIJUI NIFANYALO, KWA SABABU LILE NILIPENDALO, SILITENDI, BALI LILE NILICHUKIALO NDILO NINALOLITENDA.
16 Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema.
17 Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu
18 Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati.
19 Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.
20 Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, SI MIMI NAFSI YANGU NILITENDAYE, BALI NI ILE DHAMBI IKAAYO NDANI YANGU.”
Unaona hapo? Ukiona hayo mambo yanakujia ujue kuna gharama ya kuziondoa hizo, hiyo ni kazi yako binafsi, na njia pekee ya kuviondoa ni kujitenga na kukaa mbali na vichocheo vya hizo dhambi, kwamfano, hapo mwanzo maisha yako yalikuwa ni ya uzinzi, ya kutazama pornography, na kufanya uasherati, na mustarbation zile picha na mawazo na kumbukumbu za yale matukio haziwezi kuisha mara, zitachukua muda kukutoka, unachotakiwa kufanya ni siku baada ya siku kuzidi kukaa mbali na azingira yote yanayokupelekea wewe kuingia katika hayo mambo,

Kaa mbali na makundi yenye mazungumzo yasiyokuwa na maana muda wote yanazungumzia habari za uasherati, biblia inasema..

Waefeso 5: 3” Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;
4 wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. ”

Kadhalika biblia inasema pia..1Wakorintho 15: 33”Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema”.
Sasa ukiendelea kudumu katika hali ya kuwa mbali navyo, kidogo kidogo vinaanza kuzikwa ndani yako na hatimaye kupotea kabisa, ile hali ya mawazo mabaya kukutumikisha inapotea, unakuwa na uwezo wa kutawala mawazo yako, zile ndoto ulizokuwa unaota kila siku unafanya uasherati hatimaye zinapotea kabisa.

Ulikuwa unasikiliza miziki ya kidunia, unachopaswa kufanya ili hayo mambo yazikwe kwenye akili yako, ni kufuta miziki yote kwenye simu yako au kompyuta yako, na wakati zile nyimbo zinapotaka kuanza kuja kichwani, weka nyimbo za injili za kumtukuza Mungu badala yake..jizoeshe kuzisikiliza hizo mpaka zenyewe zitakapochukua nafasi ya zile nyimbo za kidunia.

Kadhalika ulikuwa na tabia za kwenda kwa waganga wa kienyeji, na baada ya kumpa Kristo maisha yako bado zile nguvu za giza zinakujia jia, endelea kudumu katika maombi, na kujifunza Neno la Mungu, visikuogopeshe wewe tayari ni mwana wa Mungu haviwezi kukudhuru, ni vitisho tu vya shetani, kwa jinsi unavyoendelea kukaa katika kujifunza Neno la Mungu na kukusanyika na watakatifu wengine vile vitu vinaondoka vyenyewe kidogo kidogo mpaka kufikia kutoweka kabisa, hutakaa uone mambo hayo yote tena..

Unajikuta umeingia katika usengenyaji, na hali hupendi kufanya hivyo, unachopaswa kufanya ni kukaa mbali na mazingira yote yatakayokupelekea kumzungumzia mtu mwingine vibaya, vikao vya kwenye masaluni, marafiki wasio kujenga, vijiwe n.k. unakata, sasa ukiendelea kujizoesha hivyo ile hali ya kusengenya inaondoka yenyewe ndani yako, baada ya kipindi fulani hata ukija kukaa katikati ya hao watu, utajikuta huwezi kusengenya kwasababu hiyo tabia imeshakufa tayari ndani yako..

Na mambo mengi yote, unayoshindwa kufanya kwa nguvu zako, usianze kuwaza kushindana nayo, hutaweza kwa siku moja ,huo ni ukumbi wa shetani,utajikuta unatazama matendo kuhesabiwa haki mbele za Mungu, badala ya kusonga mbele katika Imani. wewe kimbilia chanzo cha hayo mambo kisha kaa nayo mbali, kwa muda Fulani utaona matokeo mazuri, hutajisikia kuhukumiwa, wala kujilaumu, mawazo yako yatakuwa safi, ndoto zako zitakuwa sio za uchafu kila wakati, n.k..

Kadhalika shetani anapokuletea mawazo ya kukuhukumu kwa madhaifu yako, unayakataa. Ukijua kuwa Mungu ndiye aliyekuchagua wewe, na sio wewe uliyemchagua Mungu. Na hatuhesabiwi haki kwa matendo bali kwa neema yake.

Pia ni jukumu la kila mtakatifu kujitakasa kila siku kama maandiko yanavyosema. (Ufunuo 22:10 )Na tutajitakasa tu pale tutakapozidi kukaa mbali na mambo yote yanayochochea uovu ndani yetu.

Lakini kumbuka mambo haya yote mtu hawezi kuyashinda kama hajazaliwa mara ya pili. Na kuzaliwa mara ya pili ni kwa njia ya kutubu, na kubatizwa katika ubatizo sahihi, na kupokea Roho mtakatifu. Hivyo kama haujafanya hivyo ni vema uchukue uamuzi sasa kwasababu majira haya sio ya kukawia tena..Bwana yu karibu kurudi.


Ukipenda kujifunza Zaidi juu ya somo hili soma hapa kupitia link hii>>>http://wanatai.wingulamashahidi.org/2018/04/moto-hufa-kwa-kukosa-kunina-ndivyo.html#links

Pia Kwa mpangilio mzuri wa masomo haya  tembelea website yetu >>> www.wingulamashahidi.org.

Tafadhali “share/print” ujumbe huu na kwa wengine. Mungu atakubariki.

Ubarikiwe sana.