"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, November 30, 2018

BARUA INAYOSOMWA

2 Wakorintho 3:2 NINYI NDINYI BARUA YETU, iliyoandikwa mioyoni mwetu, INAJULIKANA NA KUSOMWA NA WATU WOTE;”
Maisha tunayoishi sisi ni BARUA ya Kristo, watu watutazamapo, wanapata ujumbe hata kabla ya sisi kuzungumza lolote,. Na matendo yetu ndiyo maandishi, na siku zetu ndizo kurasa, Tangu tulipompa Bwana maisha yetu, siku hiyo hiyo tunaanza kuandika kurasa njema za barua zetu.

Injili yenye matunda Kristo anayoyataka haihubiriwi kwa maneno matupu! Hapana bali inahubiriwa kwa matendo..Matendo yetu ndiyo yanayohubiri injili kuliko kingine chochote, Matendo yetu ndiyo yanayomtangaza Kristo kuliko kitu kingine chochote. Tunaweza tukawa na uwezo mzuri wa kuhubiri au kuongea lakini kama matendo yetu hayaendani na tunachokizungumza basi injili tunayoihubiri ni BURE!!.

Unaweza ukawa unahudhuria kanisani kila siku, unasaidia watu, lakini kama maisha yako ya siri ni machafu, kama maisha yako ya pembeni ni ya kiasherati, au ni mtazamaji wa pornography, au mfanyaji masturbation au mtukanaji, au mwizi, au mwuaji, au unacheza kamari, au mtu wa hasira usiyesamehe basi wewe ni barua yako ni mbaya, haijalishi unalitaja jina la Kristo mara ngapi..

Maisha yetu yanapaswa yahubiri injili kwa watu wa nje kiasi kwamba mtu akikuona tu anajua moja kwa moja Yule ni Mkristo hata kabla hujazungumza lolote, akikuona juzi, jana na leo maisha yako ni yale yale masafi, hata kabla hajazungumza na wewe Neno moja anakiri moyoni kwamba wewe ni mwanafunzi wa Kristo.
 
Sio lazima tuonekane tumebeba biblia, au tumevaa kanzu, au tumevaa kama watu wa dini au tusikiwe tunaimba mapambio, au tuonekane tunaenda kanisani kila siku, au tusikiwe tukisali kila siku hapana! Hiyo ni vizuri lakini hata pasipo hayo mambo, pasipo watu kutusikia tukisali, au tukiimba, au tukienda kanisani n.k inapaswa wakituona tu, ndani ya muda mfupi wameshajua sisi ni watu wa namna gani, washajua kuwa sisi milki ya Yesu Kristo.

Unaweza usiwe unaongea kama watu wa kidini, lakini inapasa mtu akikutazama tu maisha yako, siku mbili tatu,lazima kuwe kuna kitu ndani yake kinamshuhudia kwamba wewe ni mwana wa Mungu. Kwa jinsi maisha yako yanavyoangaza Nuru, na kuonekana Barua inayosomeka vyema.

Mathayo 5:16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona MATENDO YENU mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni...

Unaona? Kitu Bwana Yesu anachosema hapo ni kwamba nuru ya mtu inaangaza kwa matendo yake, na si kitu kingine na hichi ndicho watu wanachokitazama.

Hebu tujifunze kidogo Kitabu cha ESTA.

Esta alikuwa ni Myahudi lakini alizaliwa katika nchi ya Babeli, wakati wana wa Israeli wapo utumwani, hakuwahi kufika nchi yake Israeli.. aliishi na Kaka yake aliyeitwa Mordekai, baada ya wazazi wake kufa (ambapo Baba yake Esta alikuwa ni mjomba wake Mordekai). Walikuwa wanamcha Mungu yeye na Mordekai, lakini ilipofika wakati Mfalme wa Uajemi anatafuta malkia mwingine sehemu ya Malkia Vashti aliyemvunjia heshima Mfalme, Mordekai alimpandisha Esta kwenda kushindania hiyo nafasi ya umalkia miongoni mwa wanawali watakaochaguliwa na mfalme, Lakini jambo la kimiujiza ni kwamba Mordekai wala Esta hawakujitambulisha kuwa wao ni watu kutoka taifa gani wala Imani yao ni Imani gani...Na chakushangaza ni kwamba japo kuwa Esta hakuidhihirisha Imani yake mbele ya nyumba ya Mfalme wa Uajemi, lakini kwa matendo yake TAYARI WALE WALIOKUWA WANAWACHAGUA WANAWALI, WALISHAMSOMA ESTA NA KUGUNDUA KUWA NI MTU WA KIMUNGU, MWENYE TABIA NJEMA. Na kama ni msomaji wa Biblia utaona kuwa Ni Esta peke yake ndiye aliyepata kibali mbele ya Mfalme kuwa MALKIA kati ya wale wanawali wengine.


Sasa Ni nini tunachoweza kujifunza hapo?? Hata pasipo Kutaja DINI YAKO,WALA DHEHEBU LAKO, WALA IMANI YAKO, watu wanaweza kukusoma tu na kugundua wewe ni mtu wa namna gani? Watu wanaweza wakakusoma tu na kugundua Barua yako ni barua ya namna gani. Kwa mwenendo wako tu hata pasipo kusema BWANA ASIFIWE! au BWANA ATUKUZWE!
Sasa tukirudi kwenye kitabu cha Esta, tunaweza tukajifunza jambo lingine kubwa sana..

JE! Unajua kuwa kitabu cha ESTA ndio kitabu pekee cha Biblia ambacho kuanzia mwanzo wake hadi mwisho wake hakuna Neno “BWANA” wala neno “MUNGU”? Kama hujui hilo nenda kapitie tena biblia yako na utaligundua hilo. Sasa Jambo hilo linafunua nini? Japokuwa kitabu cha Esta hakijamtaja mahali popote Bwana wala neno Mungu halionekani, lakini tukisomapo kile kitabu tunamwona Mungu kwa sehemu kubwa sana na uwezo wake, na bila shaka watu wote tunafahamu kuwa ni kitabu takatifu cha Mungu...ikifunua jambo lile lile kwamba unaweza usionekane unalitaja jina la Bwana Mahali popote pale lakini watu WASOMAPO BARUA YAKO WANAMWONA MUNGU kwa kiwango kikubwa. Na hicho ndicho Mungu anachotaka. Simaanishi kuwa usilitaje jina la Bwana mahali popote hapana, ni wajibu wetu sote kufanya pia na hayo.

Mungu Hataki tuwe kama wanafki kama mafarisayo, ambao kwa nje, tunaonekana ni wakidini lakini kwa ndani ni wachafu. Malkia Esta hakubeba Torati na kuingia nayo kwa Mfalme ndipo akubalike, hakujidhihirisha kwamba yeye ni Myahudi, mwana wa Ibrahimu, na kwamba anamwabudu Mungu wa aliyeziumba Mbingu na nchi..hakufanya hayo yote, yeye aliingia tu mbele ya mfalme na barua ya maisha yake, na utii wake, unyenyekevu wake, upole wake, usikivu wake, na utulivu wake, na tabia yake njema, aliingia na tabia yake ya kuwa na kiasi, ya mtu asiye na majivuno, asiye na kiburi, asiyekuwa na tamaa, aliingia na tabia yake ya kuridhika, na kutotamani mambo makubwa, aliingia na tabia yake ya kutokusengenya, ya kutokuwa mwashetati, hiyo ndiyo iliyomfanya apendwe na Mfalme, hiyo ndiyo iliyomfanya akubalike..Hiyo ndiyo iliyomfanya Barua yake isomeke vyema mbele za Mfalme, na Ufalme wa Uajemi wote, na hiyo ndiyo iliyomfanya KITABU CHAKE JAPOKUWA HAKINA JINA LA BWANA MAHALI POPOTE LAKINI KIMEINGIA KATI YA VITABU 66 VYA BIBLIA.

Kaka/Dada uliye mkristo usomaye ujumbe huu, ifanye barua yako isomeke vyema, kusudi kwamba watu wakishauona mwenendo wako, roho zao zipate kuponywa. Mwenendo tu wa mtu ni nguvu tosha ya kumgeuza mtu kama vile Neno linavyoweza kumgeuza mtu. Wakati mwingine ndoa yako inamatatizo na umehangaika huku na kule, umefunga na kusali, lakini bado mume wako anazidi kuwa mwovu, anazidi kuwa mlevi, mke wako hana nidhamu, hamchi Mungu, watoto wako ni watukutu hawataki kukutii, wazazi wako ni waashirikina, wanagombana, wametengana..Na wewe ni mkristo umejaribu kuomba, hata wakati mwingine kuwashuhudia lakini bado hakuna mabadiliko..Tatizo linaweza kuwepo katika mwenendo wako, wanapokutazama hawaoni kitu cha kuwavutia kuwa kama wewe. Lakini ikiwa mwenendo wako utaubalishwa na kuishi maisha ya nidhamu na utakatifu na kumcha Mungu, basi fahamu kuwa hiyo ni injili tosha ya kuwafanya wao wabadilike. Embu soma vifungu hivi vinavyosema juu ya familia.
1Petro 3:1 “Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;
2 wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.”
Unaona hapo? Hivyo ndugu ikiwa bado hujamkabidhi Bwana Yesu maisha yako, mpe leo, Tubu mgeukie kwasababu yeye ndiye Njia ya kufika mbinguni, hakuna mwingine, njia nyingine za kidini, kidhehebu, mtu binafsi, n.k zote zinaishia mautini..Yesu ndiye mwokozi, Siku tunazoishi ni siku za Mwisho, zilizotabiriwa. Na Neema inakaribia kurudi Israeli, na Kristo kulichukua kanisa lake, je! umo miongoni mwa watakaoenda na Bwana??
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo izidi kuwa nawe!!

Tafadhali “share” kwa wengine,
Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment