"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, December 3, 2018

HUIJUI KAZI YA MUNGU, AFANYAYE MAMBO YOTE.

Ni kweli sisi kama wakristo tunaomngojea Bwana ni wajibu wetu kila siku kuelekeza macho yetu mbinguni, tukichunguza katika maandiko yale yatupasayo kufahamu juu ya siku hizi za mwisho na kuangalia dalili zote zinazoeleza kuja kwa pili kwa Kristo, Na kama utakuwa ni mfuatiliaji mzuri wa maandiko utagundua kuwa hichi kizazi tunachoishi ndio kile kizazi kilichotabiriwa na Bwana kushuhudia kuja kwa pili kwa Kristo. Kwasababu kuu mbili kwanza ni kizazi kilichoshuhudia kuchipuka tena kwa “mtini” (yaani Taifa la Israeli), Pili: Tunaishi katika kanisa la 7, na la mwisho, ambalo ni moja ya yale makanisa 7 tunayasoma katika kitabu cha (Ufunuo 2&3), litaisha na unyakuo. Na hakutakuwa na kanisa lingine zaidi ya hilo. Na kanisa hili lilianza mwanzoni mwa karne ya 20, (yaani mwaka 1900) na litaisha na kunyakuliwa kwa kanisa.

Kadhalika biblia inatabiri pia katika wakati wa mwisho, kabla ya kuondoka kwa bibi-arusi wa Kristo na kwenda mbinguni kwenye karamu ya mwanakondoo, ni sharti kwanza IMANI ionekane ndani ya huyu bibi-arusi (Luka 18:8). Ni imani itakayomfanya anyakuliwe, vinginevyo kanisa halitaweza kuenda mahali popote kama halitafikia viwango hivyo vya ukamilifu Mungu analotaka liwe nalo. Hivyo ili hayo yote yatokee ni sharti kuwepo na uamsho na uvuvio mkubwa sana wa Roho Mtakatifu kabla ya huo wakati kufika ili wateule wawezi kufikia kiwango hicho cha ukamilifu Bwana anachotaka kukiona katika kanisa.

Na ndio ukija kusoma katika kitabu cha Yoeli 2: 23 utaona Inasema hivi;
“Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie Bwana, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi MVUA YA MASIKA, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na MVUA YA VULI, kama kwanza.”

Unaona hapo? Biblia inazungumzia juu ya MVUA YA MASIKA na MVUA YA VULI au kwa tafsiri nyingine mvua hizi zinajulikana kama MVUA ZA KWANZA, na MVUA ZA PILI. Au mvua za sasahivi na mvua za baadaye..Sasa mvua ya kwanza Bwana aliiachilia katika ile siku ya Pentekoste, mwanzo kabisa wa kanisa na mwanzo wa ukristo, (Matendo 2), lakini ipo mvua ya mwisho ambayo Bwana ataiachilia tena katika dunia nayo itakuwa ni kwa ajili ya kulitimiliza kanisa, kwa ajili ya kuondoka hapa duniani. Na utukufu wake ni sharti uwe mkubwa kuliko ule utukufu wa lile kanisa la kwanza. Biblia imetabiri hivyo. Katika Hagai 2:9 
“Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi…”
Hivyo mambo yatakayoambatana na uamsho huo mkubwa ambao upo mbio kutokea ni mambo ambayo hayajazoeleka kuyaona katika wakati wowote wa kanisa tangu lianze siku ile ya Pentekoste hadi sasa. “Zile nguvu za zamani zijazo” za utendaji kazi wa Roho Mtakatifu ndio zitaonekana hicho kipindi, Sehemu ya pili ya ule unabii wa Yoeli aliotabiri juu ya siku za mwisho zitakavyokuwa ndio zitakwenda kuonekana katika kipindi cha majira hayo kama tunavyosoma:

Matendo 2:16-21.
“16 lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,
17 Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.
18 Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri.
19 Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi.
20 Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri.
21 Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.”

Ukisoma katika maandiko hayo sehemu moja ya unabii huo utaona umetimizwa, kwamfano sehemu ya ndoto, maono, kutabiri, lakini sehemu nyingine bado yaani sehemu ya ishara za juu mbinguni, na nchi, damu, moto,jua kuwa giza n.k.. Sasa hicho kipengele kilichobakia, kitatimizwa katika kipindi hicho cha uamsho huo wa mwisho wa kanisa. Kadhalika ukisoma kitabu cha Ufunuo 10, utaona pia zipo ngurumo 7 ambazo sauti zake hazijiandikwa mahali popote katika biblia nazo hizi zitafunuliwa katika hicho kipindi karibu na ukamilifu wa kanisa takatifu la Mungu. Ujumbe utakaotolewa na hizo ngurumo 7, utakuwa ni ujumbe wa kumkamilisha bibi-arusi wa Kristo tu peke yake, na si mtu mwingine aliye nje ya mpango wa wokovu. Kwao jumbe hizo zitasikika kama ngurumo tu, hawatuaelewa chochote.

Hivyo tukiyafahamu hayo, tunajua kabisa huu ni wakati wa kujiweka tayari na kwamba mambo hayo siku yoyote yanatokea. Lakini Sasa embu turudi katika kiini cha somo letu la leo.
Kuna wakati wanafunzi wa Bwana baada ya kuona kuwa Kristo sasa ameshashinda na kupewa mamlaka juu ya vitu vyote baada ya kufufuka kwake kutoka katika wafu, wanafunzi wake wakatanuka vichwa vyao wakidhani kuwa ule ndio wakati Mungu aliokuwa anauzungumzia tangu zamani wa Bwana kuwapigania Israeli na kuwarudishia ufalme wao ambao ulikuwa umetwaliwa na wapagani kuwa muda mrefu ndio wakati sasa umefika Israeli watapata raha, na kwamba Bwana atakwenda kuwaangamiza watu wote na mataifa yote yasiyomcha Mungu.

Hivyo hiyo ikawafanya wale wanafunzi wahamishe mawazo yao yote katika kutafuta kufanya mapenzi ya Mungu kwa wakati waliokuwepo na kuwafanya wafikirie mambo ya mwisho wa dunia. Walitaka mambo yaishe haraka haraka, hawakutaka kusikia kitu kingine chochote kinachohusu wokovu, hawakuwa na muda wa kufikiria kuokoa nafsi za watu ili zisiangamie huo muda utakapofika, wao walifikiria juu ya jamii ya watu wao tu, hawakujali na watu wengine ambao hawakuwahi kuisikia kweli, watu wa mataifa ambao laiti na wao wangeijua kweli ya wao wasinge abudu sanamu.

Kumbuka Mitume waliyajua maandiko na kuelewa kuwa siku masihi wao atakapokuja kuuchukua ufalme basi atawaokoa na maadui zao wote waliokuwa waliowatesa kwa miaka mingi. Ni kweli kabisa hilo jambo lilitabiriwa na ni lazima lije kutokea, katika siku hizi za mwisho lakini lile lilikuwa sio jukumu lao kuliharakisha.

Matendo 1:6-8
6 Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?”

Unaona walijua kabisa hilo. Lakini jibu lake lilikuwa ni hili..

7 Akawaambia, SI KAZI YENU kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.
8 LAKINI MTAPOKEA NGUVU, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa MASHAHIDI WANGU katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Ndugu tukiyaelewa hayo maneno vizuri yatatusaidia sisi tunaoishi katika kipindi hichi ambacho tunaona kweli wakati wa mavuno upo karibu, na siku yoyote Bwana anarudi kama walivyoona mitume kwa kipindi chao. Je! na sisi kwa kulijua hilo tutahamisha mawazo yetu ya kumtumika Mungu, mawazo yetu ya kumzalia Mungu matunda ya kazi, na kustarehe na kusema tunangojea huo uamsho wa mwisho ufike sisi tuondoke?. Tuna relax tukingojea hizo sauti za ngurumo 7 zifunuliwe?. Tunangojea mpaka Mvua ya pili ishuke ndio tuanze kumtumika Mungu? Na huku hatutaki kutazama hali za watu waliokatika dhambi huu wakati, hatutaki kuyajua mapenzi ya Mungu kwetu sisi sasa hivi ni nini?..Sisi muda wote Ngurumo 7 zitafunuliwa,..ngurumo 7 zitafunuliwa.

Lakini Bwana Yesu vivyo hivyo anatuambia na sisi watu wa leo “Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.
8 LAKINI MTAPOKEA NGUVU, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

Ndugu, njia za Mungu HAZITAFUTIKANI, hujui leo na kesho Mungu kaipanga vipi, au kaamua kipi kianze au kipi kiishe, Mfalme Sulemani alijaribu kufanya hivyo kuzichunguza njia za Mungu ajue mwanzo wake na mwisho wa njia zake, lakini alishindwa na mwisho wa siku alimalizia na kusema:

Mhubiri 9: 17 basi, niliiona kazi yote ya Mungu, ya kuwa haitafutikani na mwanadamu kazi inayofanyika chini ya jua; kwa sababu mwanadamu na akijisumbua kadiri awezavyo kuitafuta, hata hivyo hataiona; naam, zaidi ya hayo, mwenye hekima ajapodhania ya kuwa ataijua, lakini yeye hataweza kuiona.
Pia Mtume Paulo anasema:

Warumi 11:33 Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala NJIA ZAKE HAZITAFUTIKANI!.

Mwisho kabisa ikiwa Bwana ametupa na sisi nguvu ya kuwa mashahidi wake, hatuna budi sasa kufiria kumzalia Mungu matunda kwa wingi iwezekanavyo, na kuacha kupoteza muda mrefu kungojea mambo ambayo huna uhakika ni muda gani yatatokea. Kumbuka watu wengi wanaokaa katika hali hiyo ya kusubiria kipindi Fulani cha uvuvio kifike na huku hawana muda na shamba la Mungu sasa huwa hawafiki mbali. Kwasababu wanaishi kama watu waoteaji tu, na si kama watu wa Imani. Soma.
Mhubiri 11: 4 “Mwenye kuuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna.
5 Kama vile wewe usipojua njia ya upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadhalika huijui kazi ya Mungu, afanyaye mambo yote.
6 Asubuhi panda mbegu zako, Wala jioni usiuzuie mkono wako. Kwa maana wewe hujui ni zipi zitakazofanikiwa,kama ni hii au hii,au kama zote zitafaa sawasawa.”
 Tenda kazi ya Mungu bila kuangalia msimu, au wakati unaofaa Bwana huwa analaani miti ile inayosubiria msimu ndio izae, kumbuka ule mtini Bwana Yesu alioulaani ambao alitarajia akute matunda juu yake na akakosa hivyo akaulani. Biblia inasema haukuwa umezaa kwasababu ulikuwa sio msimu wake wa kuzaa, kama Bwana angeenda katika kipindi cha msimu wake ni wazi kuwa angekuta matunda, lakini njaa ilimshika kabla ya msimu kufika. Hivyo usitegemee msimu, mwisho wa siku utajikuta huzai chochote. Anza kutafuta kufanya mapenzi ya Mungu sasa angali LEO IPO, KWASABABU KESHO SI YAKO.

Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment