"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, December 3, 2018

NYOTA YA ASUBUHI.

Ulishawahi kuitazama kwa ukaribu ile nyota ya asubuhi? Kama ulishawahi kuifuatilia na ukaona tabia yake utagundua ni ya kipekee sana, kwasababu ndio nyota pekee inayochelewa kupotea asubuhi na ndio nyota pekee inayotangulia kuonekana wakati wa jioni kabla ya nyingine… Ukiifuatilia kwa makini utagundua kuwa hii nyota ya asubuhi ndio ile ile nyota ya jioni na iko moja tu!.

Sasa jambo la kipekee sana kuhusu hii nyota ni kwamba licha tu ya kuwa inachelewa kupotea asubuhi na kuwahi kuchomoza jioni…lakini pia HUWA INAONEKANA MCHANA. Mchana kweupe wakati kukiwa hakuna mawingu nyota hii inaonekana, Mimi binafsi nikiwa na watu kadhaa tuliwahi kulithibitisha hilo..Wakati juu kukiwa hakuna mawingu, anga la Blue tumewahi kuiona hii nyota zaidi ya mara moja.
Kwa kawaida unaweza ukadhani ni jambo lisilowezekana lakini lipo!..kwasababu hata mimi mwanzo sikuwahi kutegemea kuona nyota yoyote mchana saa saba…lakini ilitokea nikaiona siku hiyo, na sikuwa mwenyewe tulikuwa wengi nao pia waliiona, na siku inayofuata iliendelea kuonekana. Sasa hii nyota kulingana na dunia inavyosogea na yenyewe huwa inasogea…asubuhi inaweza ikaonekana mashariki, mchana ikaonekana juu ya utosi jioni ikaonekana magharibi..inabadili eneo kulingana na mzunguko wa dunia. Ukipata muda ifuatilie nyota hii, utagundua haya yote na mengine zaidi ya haya.

Sasa katika maandiko Bwana amefananishwa na hii NYOTA YA ASUBUHI. Kutokana na tabia ya nyota hiyo ilivyo…Kama tu vile sehemu nyingine Bwana Yesu alivyofananishwa na SIMBA WA YUDA, alifananishwa na simba kutokana na tabia ya samba ilivyo, kwanza Simba ni mnyama aliye na nguvu kuliko wanyama wengi, na mwenye ujasiri kuliko wanyama wote, na sehemu nyingine anajulikana kama Mfalme wa mwituni..kadhalika na Bwana wetu Yesu Kristo, aliposhinda mauti pale Kalvari, alipewa nguvu, na heshima na uweza na ufalme wa dunia yote na mbingu zote, kama vile Simba alivyo mfalme wa mwituni, kadhalika na Bwana wetu Yesu Kristo alifanyika Mfalme wa ulimwengu wote.

Sasa tukirudi katika ILE NYOTA YA ASUBUHI, utaona kuwa licha tu ya kung’aa asubuhi na jioni, lakini pia inang’aa mchana, hivyo inang’aa katika vipindi vyote vya siku, yaani asubuhi, mchana na jioni na usiku. Biblia inasema:
Ufunuo 22:16 “Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ILE NYOTA YENYE KUNG'AA YA ASUBUHI.
Ikimfunua BWANA wetu YESU KRISTO, ambaye yeye ameshinda na kukaa katika NURU ISIYOWEZA KUKARIBIWA, aling’aa milele iliyopita, anang’aa nyakati hizi na atang’aa milele…

1 Timotheo 6: 14 “..hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo;
15 ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana;
16 ambaye yeye PEKE YAKE HAPATIKANI NA MAUTI, AMEKAA KATIKA NURU ISIYOWEZA KUKARIBIWA; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina”. 


Wakati nyota nyingine zote zinang’aa jioni na asubuhi kufifia, Nyota ya Yesu Kristo haififii kamwe, NURU YAKE HAIHARIBIKI, (Haifunikwi) wakati wanadamu mashuhuri, watu maarufu, watu wakuu, na wafalme wa dunia wanakuja na kuondoka, lakini Yesu Kristo Mfalme wa Wafalme na Bwana wa mabwana anadumu milele, vizazi na vizazi hapungui nguvu, wala uweza, wala mamlaka..ANANG’AA HATA MCHANA KWEUPE..anatoa NURU isiyoweza kufunikwa na nuru nyingine, Je! Unajua kuwa mtu pekee anayeshikilia namba moja kwa umaarufu duniani kwa wakati wote ni YESU KRISTO??...Kama hujui hilo nenda kasome kwenye vitabu vya rekodi ya dunia,.. (hata mambo ya ulimwengu huu tu yanamtangaza) Ndio maana Bwana Yesu alisema yeye ndiye NURU YA ULIMWENGU. Ikiwa na maana kuwa hakuna Nuru nyingine zaidi yake. Mbingu na nchi zitapita lakini Yesu ni yeye yule jana na leo na hata milele. Haleluya!
Yohana 1: 9 “Kulikuwako NURU HALISI, amtiaye NURU KILA MTU, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua”.
Umeona hapo? Anasema kulikuwako na NURU halisi, ikiwa na maana kuwa zilikuwepo nuru nyingine lakini hazikuwa halisi, na Nuru hii halisi, ina uwezo wa kumtia Nuru kila mtu , ikiwa na maana kuwa ina uwezo wa kumfanya kila mtu kuwa kama yeye alivyo.
Ndugu yangu, Yesu Kristo Mkuu wa Uzima anataka watu wote, tuwe kama yeye, anataka wote tung’ae kama yeye, anataka tuangaze hata mchana kweupe, kusiwepo na chochote kinachoweza kutuzima, milele na milele, na ndio maana maandiko pia yanasema katika..

Mithali 4:18 “Bali njia ya wenye haki ni kama NURU ING'AAYO, Ikizidi kung'aa HATA MCHANA MKAMILIFU”.

Unaona hapo wenye haki, yaani wote waliyoikubali NURU HALISI (YESU KRISTO), biblia inasema watang’aa hata mchana Mkamilifu. Siku ile watakapomaliza kazi yao hapa ulimwenguni, ndio watadhihirika mng’ao wa utukufu wao ulivyo. Watakuwa kama miale ya Moto, watang’aa kuliko jua. Bwana hataki maisha yako leo yawe hivi kesho yanyauke, anataka uishe milele. 

Danieli 12:3 “Na walio na hekima WATANG'AA KAMA MWANGAZA WA ANGA; na hao waongozao wengi kutenda haki WATANG'AA KAMA NYOTA MILELE NA MILELE”.

Mathayo 13: 40 “Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia.
41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi,
42 na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
43 Ndipo wenye HAKI WATAKAPONG'AA KAMA JUA katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie”.
Je! Na wewe leo umetiwa nuru na ile Nuru halisi (Yesu Kristo)? Je! Umemkabidhisha maisha yako leo? Siku tunazoishi ni za hatari, Kristo anakaribia kurudi kulichukua kanisa lake, na kukusanya ngano ghalani na makapi kuyakusanya kwenda kuchomwa moto. Yesu Kristo ndiye Nuru ya ulimwengu, na ukombozi kwa mwingine yoyote isipokuwa yeye..Tubu leo, ukabatizwe kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, naye Bwana atakutia Muhuri wa Roho wake Mtakatifu.

Ubarikiwe!

No comments:

Post a Comment