"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, January 9, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 51


SWALI 1: Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?
JIBU: Kwanza tunapaswa kufahamu kuwa si mapenzi ya Mungu sisi tupitie shida yeyote ile.Lakini zipo shida na dhiki ambazo Mungu huwa anaziruhusu ziwapate wale wateule wake kwa kutimiza kusudi Fulani, aidha kwa kuwafundisha, au kwa kuonyesha utukufu wake, au kwa kuwaonya, lakini mwisho wa siku shida hizi huwa zinaishia na mwisho mwema, na ndio maana mtume Paulo alisema mahali fulani katika

2Wakorintho 12: 9
“Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.
10 Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu. “

kadhalika zipo shida ambazo zinatokana wanadamu wenyewe, au tunaweza kusema zinasababishwa na wanadamu wenyewe na hizo hazipo ndani ya uwezo wa Mungu kuzizua bali kwa mwanadamu mwenyewe unajua ni kwasababu gani? Jaribu kuwazia mfano huu.

Kama vile sisi wanadamu wenyewe kwa wenyewe hatupendi kuchaguliwa baadhi ya mambo kwamfano kijana anapofikia hatua ya kuoa au kuolewa, mzazi mwenye busara hatoweza kwenda kumlazimisha mtoto wake aoe mke amtakaye yeye hata kama msichana huyo atakuwa ni mzuri kiasi gani, au atakuwa na maadili kiasi gani, suala la maamuzi ni la mtu binafsi. Hivyo kitu pekee atakachoweza kufanya kama mzazi mwenye busara ni kumshauri tu, na kumpa mapendekezo mema lakini si kumlazimisha, hata kama anajua huyo mke mtoto wake aliyekwenda kumchagua atakuja kumletea madhara makubwa kiasi gani mbeleni, bado hana uwezo wa kumlazimisha asimwoe.

Na ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu, mara zote anaona madhara yanayokuja mbele yetu, na ni kweli anatamani kuyazuia, lakini jambo analoweza kulifanya yeye kama Mungu wetu, ni kututahadharisha, au kutuonyesha jinsi mwisho wake utakavyokuwa, ili tusipotee au tusidondoke kwenye madhara. Sasa suala la kuamua kuendea au kutokuiendea njia hiyo ni la mtu binafsi. Ikiwa mtu atakubali mashauri ya Mungu basi, Mungu atamwepushia mabaya yale lakini ikiwa hatakubali basi Mungu atamwacha aangamie, hata kama Mungu atakuwa na uwezo mkubwa kiasi gani wa kumwepusha, bado hatoweza kufanya hicho kitu. Kwasababu Mungu katuumbia sisi ndani yetu uwezo wa kuchagua.
Ikiwa mtu ni mzinzi, na huku Mungu alishamwonya kuwa wazinzi hawataurithi ufalme wa mbinguni, na mtu huyo bado anaendelea katika njia zake mbovu, Hapo Mungu hawezi kumzuia japo anajua kabisa njia yake mwisho wa siku ataishia kifo, halafu aende kwenye ziwa la moto.

Alimwonya shetani, hata kabla hajawa shetani, lakini hakumlazimisha asihasi, japo alijua kuwa ataasi na mwisho wa siku kuishia motoni,Mungu alimwonya lakini hakutaka kusimama katika kweli kama malaika wengine watakatifu walivyokuwa. Na ndivyo ilivyo hata kwetu,
Mungu katuwekea maamuzi yetu binafsi. Kukubali au kukataa. Hakuna kulazimishwa.

SWALI 2: Shalom Ndugu zangu, hapa ana maana gani kusema hivi? " Usiseme moyoni mwako,Ni nani atakayepanda kwenda Mbinguni? (yaani ni kumleta Kristo chini), "au,Ni nani Atakayeshuka kwenda Kuzimu? (yaani, ni kumleta Kristo juu,kutoka kwa wafu.). {Warumi10:6-7.}
JIBU: Ukisoma kuanzia hiyo mistari wa kwanza wa kitabu cha Warumi Mlango wa 10, Utaona kuwa Mtume Paulo alikuwa anazungumza habari za juu ya Wayahudi ambao wanaamini katika kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria na wala sio kwa Imani.
 
Sasa Mtume Paulo alichokuwa anataka kuonyesha ni kwamba..Torati Musa aliyopewa na Mungu, imezungumza habari zote mbili yaani habari ya kuishi kwa sheria kwamba Mtu akiitenda sheria zilizoandikwa katika mbao zile ataishi katika hizo..Yaani Mtu akifanya maagizo yote ya torati basi atafanikiwa katika maisha yake..
 
Na pia torati hiyo hiyo mahali pengine pia imezungumzia kuhusu haki ipatikanayo kwa njia ya Imani kwamba..Sheria za Mungu zikiandikwa ndani ya moyo wa mtu basi naye pia atabarikiwa zaidi..Kwasababu maana halisi ya agano jipya ni kuwa zile zile sheria za Mungu zinakuwa zinaandikwa ndani ya Moyo wa Mtu.
Sasa ukisoma Kitabu cha kumbukumbu utaona Mungu anaizungumzia hiyo Mtume Paulo aliyoinukuu..
Kumbukumbu 30: 11 “Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.
12 Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?
13 Wala si ng'ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?
14 Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.
15 Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya”

Unaona Haki ipatikanayo kwa njia ya Imani kwamba sheria za Mungu zitakuwa karibu sana na mtu mahali alipo, hazipo mbinguni kwamba Bwana Yesu aende akatuchukulie atuletee katika gari la moto, au hazipo kuzimu kwamba Bwana Yesu azifuate atuletee katika mbao kama Musa alivyozileta katika mbao kwa wana wa Israeli ili wazishike.. Hapana sheria zake ataziandika ndani yetu (ndani ya mioyo yetu)..zipo karibu sana na sisi, hakuna haja ya kwenda milimani kuzitafuta kama alivyofanya Musa, wala hakuna haja ya kusubiria mtu atoke mbinguni au kuzimu kutufundisha…yeye Bwana ataziandika mioyoni mwetu kutufundisha mwenyewe.. 
 
Hiyo ndiyo maana ya huo mstari..
 
"Usiseme moyoni mwako,Ni nani atakayepanda kwenda Mbinguni? (yaani ni kumleta Kristo chini), "au,Ni nani Atakayeshuka kwenda Kuzimu? (yaani, ni kumleta Kristo juu,kutoka kwa wafu.) Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo”
Mtume Paulo alielezea vizuri zaidi juu ya agano hilo jipya katika kitabu cha Waebrania
Waebrania 8:8 “…Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, Nami nitawatimizia nyumba a Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya;
9 Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, Katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali asema Bwana.
10 Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli Baada ya siku zile, asema Bwana; NITAWAPA SHERIA ZANGU KATIKA NIA ZAO, NA KATIKA MIOYO YAO NITAZIANDIKA; Nami nitakuwa Mungu kwao, Nao watakuwa watu wangu.
11 Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake, Na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; Kwa maana wote watanijua, Tangu mdogo wao hata mkubwa wao.
12 Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena”

SWALI 3: Je!,Inakubalika kumtolea mtu mwengine damu?(blood transfusion).
JIBU: Ikiwa Bwana alituagiza tupendane sisi kwa sisi hata tufikie hatua ya kuweza kutoa uhai wetu kwa ajili ya wengine wapone kama yeye alivyofanya kwetu sisi, Sasa! damu itakuwa ni kitu gani kwetu?. Tumeambiwa tusipende kwa neno au kwa ulimi tu bali kwa tendo.

Biblia inatuambia 1Yohana 3:16 "Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.
17 Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?
18 Watoto wadogo, TUSIPENDE KWA NENO, wala kwa ulimi, BALI KWA TENDO NA KWELI".

Ni sawa na kumwona ndugu yako amepungukiwa damu na, hivyo asiposaidiwa atakwenda kufa muda si mrefu, na wewe angali unao uwezo huo wa kumsaidia na hautaki unasema sitoi damu yangu ni dhambi, hivyo nakuombea tu,kisha Mungu akupumzishe salama, je! hapo utakuwa umeonyesha upendo gani kwa ndugu yako huyo?. Huoni kama utakuwa umependa kwa Neno na wala si kwa tendo?.

Lakini wapo watu wanafanya hivyo kama biashara kwa kisingizio cha kuwa wanasaidia watu, wanatoa damu zao, wanatoa figo zao, si kwa lengo la kumsaidia ndugu yake, bali kwa lengo la kufanya biashara. Hiyo ni dhambi mbele za Mungu na wanaofanya hivyo siku zinakuja watuvuna walichokipanda.

SWALI 4: Je! Ni vizuri kwa wakristo kutumia msalaba katika maombi?.
JIBU: Hapana sisi kama wakristo hatupaswi kuhusisha kitu chochote chenye mfano wa kiungu katika ibada zetu, kwani hizo ni sawa na ibada za sanamu, Mungu hana mfano wa kulinganishwa na kitu chochote ili kuabudiwa kwani yeye ni Roho nao wamwabuduo imewapasa kuabudu katika roho na kweli.

Na ndio maana alisema katika Kumbukumbuku 16: 21 Usipande mti uwao wote kuwa Ashera kwako kando ya madhabahu utakayofanya ya Bwana, Mungu wako.
22 Wala usisimamishe nguzo; ambayo Bwana, Mungu wako, aichukia.

Hivyo kitu chochote kile iwe ni msalaba, au sanamu, au mti au picha, au pambo, au chochote kile ikiwa kipo kwa ajili ya matumizi mengine au kumbukumbuku, haina shida ili kikiwa kinahusianishwa na masuala mengine ya ibada hayo ni makosa makubwa sana mbele za Mungu kwani hivyo utakuwa utakuwa unamwabudu shetani moja kwa moja badala ya Mungu, wapo watu wanaoachukua misalaba na rozari, na masanamu na kufanya kama sehemu za ibada zao za kila siku, wanazisujudia, na kumwombea Mungu kupitia hivyo.
Sasa Hiyo ni dhambi kubwa sana kwa mkristo. Na ni machukizo mabaya yanayoweza kupelekea hata Mungu kukuua kwa wivu wake.

Ubarikiwe sana.

No comments:

Post a Comment