"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, February 1, 2019

TUMEPEWA, SI KUMWAMINI TU KRISTO, ILA NA KUTESWA KWA AJILI YAKE;

Wafilipi 1:29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; ”.
Ni mstari ambao wengi wetu hatuupendi, wala hautufurahishi… na mwingine ni 
1 Wakorintho 14:34 unaosema “Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo
35 Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa.”
Pamoja na 1 Timotheo 2:11 “Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.
12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.
13 Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.”,

Mistari hii kwa mtu ambaye hasomi kabisa biblia akisiisikia kwa mara ya kwanza anaweza akapinga kama vile haipo katika Biblia Takatifu. Ni mistari inayochokiwa na wengi, na huwa haihubiriwi mara kwa mara. Na hata ikihubiriwa inapindishwa pindishwa ikipakwa pakwa rangi, kuipotezea maana halisi ya mistari hiyo.

Lakini Mistari yote hii inapatikana katika Agano jipya na imevuviwa na Roho Mtakatifu, na kuthibitishwa na yeye mwenyewe kwa ajili ya afya ya Roho zetu, na kwa faida zetu. Ndio maana Roho Mtakatifu akaruhusu iwepo katika Biblia Takatifu katika vizazi vyote..Na kama Bwana Yesu anavyosema “Mbingu na Nchi zitapita lakini Maneno yangu hayatapita kamwe”…ndivyo maneno hayo yatakavyodumu siku zote. Na pia inasema maneno ya Mungu yamehakikiwa na ni safi kama fedha iliyosafishwa mara saba (Zaburi 12:6).

Leo kwa Neema za Bwana hatutajifunza hiyo Mistari miwili ya Mwisho bali tutajifunza huo wa Kwanza, unaozungumzia HABARI YA KUTESWA KWA AJILI YA KRISTO.
Ni muhimu kufahamu, chochote Mungu anachotaka tukifanye ni kwa faida yetu, ni kwasababu anatupenda na anataka tupate faida nyingi kwa kupitia hicho…Kwahiyo chochote kile kiwe kibaya au kizuri kitokacho kwa Mungu kinacholetwa juu yetu sisi tuliomwamini yeye, ni kwa ajili ya kutujenga sisi hana lengo la kututesa hata kidogo kwasababu yeye mwenyewe amesema hapendi kuwatesa wanadamu (Maombolezo 3:33.. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha).
Hata mzazi mwenye upendo wa kweli kwa mwanawe,chochote kile akiletacho juu ya mtoto wake kiwe kizuri au kibaya..lengo lake sio kumharibu bali kumfundisha, na wala lengo lake sio kumhuzinisha, bali kumjenga..ndivyo ilivyo kwa Baba yetu wa mbinguni.

Kwahiyo maandiko yanasema, hatujapewa kumwamini tu!!...yaani ikiwa na maana hatujapewa kumwamini tu Bwana Yesu na kusali na kuomba, na kutenda mema na kuishia hapo! Hapana! Bali tumepewa pia kuteswa kwa ajili yake.
Hivyo Kwanini Bwana anataka tuendelee mbele hatua ya kuteswa kwa ajili yake?..ina maana hiyo ya kumwamini tu haitoshi?!!.. Jibu ni kwamba haitoshi ndio maana anataka tuendelee mbele.

Lengo la kufanya vile ni ili ATUFANANISHE NA YESU KRISTO, MWANA WAKE. Ili kwamba turithi kama Kristo alivyorithi, kwasababu yeye ili aweze kuzirithi mbingu za mbingu, kikombe cha mateso hakukiepuka…ingawa kuna wakati aliomba “Baba ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke”…Lakini Baba hakumwepushia lengo lilikuwa sio kumtesa bali ni kumpa sababu ya kupata zile mbingu za mbingu alizomwahidia kumpa sababu ya yeye kwanini awe juu ya malaika wote.

Na kama alimpitisha mwanawe mpendwa Yesu Kristo katika mateso yale, pia atawapitisha wanawe wengine wote katika njia ile ile, ili kwamba na sisi nasi tuwe tumestahili kuzirithi zile ahadi kubwa namna ile Yesu alizozirithi. Na yeye ni mwaminifu kama alivyokuwa na Bwana Yesu ndivyo atakavyokuwa na sisi wakati wa mateso..na atatupa ushindi kama alivyompa BWANA Yesu.
Ufunuo 3:21 “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.”
Unaona nafasi ya kuketi na Bwana katika kiti cha enzi, ni lazima tushinde kama yeye alivyoshinda.
Yeye alipigwa pasipo sababu, na sisi hatuna budi kupitia wakati mwingine kupigwa pasipo sababu, yeye alichukiwa bure biblia inasema hivyo (Yohana 15:24-25), na sisi hatuna budi wakati mwingine kupitia kuchukiwa Bure kwasababu ya Imani yetu au mienendo yetu inayompendeza Mungu, yeye aliishinda hasira pale alipotemewa mate bila kosa lolote, na sisi hatuna budi kushinda hasira na ghadhabu tutakapozalilishwa pasipo sababu yoyote.

Yeye walimsimamishia mashahidi wa uongo lakini alishinda kwa kujinyenyekeza kama kondoo apelekwaye machinjoni wala hakupaza sauti yake kushindana na mtu, Isaya 53: 7 “Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, HAKUFUNUA KINYWA CHAKE”. Na sisi tunatakiwa tushinde vile vile,kwa kufumba vinywa vyetu tunapoonewa, na kusingiziwa mambo mabaya na kusimamishiwa mashahidi wa uongo.

Yeye alishinda kwa kuwaombea msamaha wale waliomsulibisha katika hatua yake ya mwisho ya uhai wake, na sisi tunapaswa tushinde kwa kuwasamehe wale wote wanaotutesa au kutuonea, au kutuumiza hata katika hatua ya mwisho ya uhai wetu.
Hiyo ndio maana ya kuteswa kwa ajili ya Kristo na kila mkristo wa kweli lazima apitie, kwasababu hatuwezi kusema tunafanana na Kristo, wakati historia za maisha yetu hazifanani na historia ya maisha yake. Ndio maana Bwana Yesu alituambia… “mtu yoyote akitaka kumfuata, sharti kwanza ajikane nafsi yake na ajitwike msalaba wake kisha amfuate”…Na zaidi ya yote apige gharama kwanza kabla ya kumfuata…Kwasababu njia ya Kristo ni njia ya Msalaba, ambayo mwisho wake ni KALVARI. Lakini mwisho wake una matunda makubwa sana.
Na tukishinda kama yeye basi tutarithi kama yeye alivyorithi…kama Mtume Paulo anavyosema mahali fulani..

2Timotheo 2.9 “Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi.
10 Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.
11 Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia;
12 Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi;”
Lakini pia biblia imetuonya tusiteswe kwajili ya matendo mabaya..hatupaswi kuteswa kwajili ni wezi, au watukanaji, au wasengenyaji, au wakorofi au waasherati, au wala rushwa au mafisadi, au wachokozi… na kusema tunateswa kwa ajili ya Kristo, Hapo tutakuwa hatuteswi kwa ajili ya Kristo bali kwa ajili ya shetani.

1 Petro 4:12 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.
13 Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
14 Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.
15 Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.
16 Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.
17 Kwa maana wakati umefika wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii injili ya Mungu utakuwaje?
18 Na mwenye haki akiokoka kwa shida, yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi ataonekana wapi?
19 Basi wao wateswao kwa mapenzi ya Mungu na wamwekee amana roho zao, katika kutenda mema, kama kwa Muumba mwaminifu”.

Bwana atujalie sote, kuyaelewa maandiko na kuyatendea kazi. Tutakapokutana na hayo basi tusizimie mioyo tukidhani kuwa Mungu hatupendi au tuna bahati mbaya..Kwani tukumbuke kuwa hata watakatifu waliotutangulia walipitia mambo kama hayo hayo, na hata sasa wengine wanaendelea kupitia.
Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment