"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, March 20, 2019

JE! NI KWELI AMERUKWA NA AKILI?

Marko 3:21 Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili.
Huyu ni YESU ambaye leo hii tunamwita Bwana na mwokozi wa maisha yetu, ambaye sasa amekuwa ni tegemeo na mwamba kwa kila mtu duniani apendaye maisha, ambaye mpaka sasa ni maarufu kuliko wote kwa vizazi vyote, takwimu zinaonyesha ni mtu anayezungumiziwa sana kuliko watu wote duniani kwa kwa wakati wote, na vizazi vyote ni mtu anayependwa zaidi ya watu wote duniani hana mfano, Huyo ni mwokozi wetu, ambaye tunamshuhudia hakuwahi kutenda dhambi hata moja, lakini biblia kwa huzuni inatuambia ..

Ni nani aliyesadiki habari alizozileta yeye? Alidharauliwa na watu, na maisha yake ni nani atakayeyasimulia? (Isaya 53). Kwa jinsi mwenendo wake ulivyokuwa wakitofauti kabisa na jinsi watu walivyokuwa wakimtazamia.
 
Embu tufikirie, Bwana anatoka kushuhudiwa na mbingu, kuwa yeye ndiye mwana mpendwa wa Mungu aliyependezwa naye, Roho wa Mungu naye anashuka juu yake kumtia mafuta ya utumishi, mafuta ya shangwe kuliko wote..( Waebrania 1.9 Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio.)
 
Ili kuwaganga watu mioyo, na kuwahubiria habari njema..Anakwenda nyikani kufunga siku arobaini shetani na mapepo yake yote yakiacha shughuli zao na kwenda kumjaribu ili amkosee Mungu, lakini wakashindwa, mapepo yote yakawa yanamkiri kuwa yeye ni mwana wa Mungu aliye hai kila mahali alipokwenda…Lakini tunakuja kusoma habari ya kusikitisha sana, kumbe wale watu waliomzunguka walimwona kama mwendawazimu karukwa na akili, na wengine wakamwona kama ana PEPO. Na kibaya zaidi wale walio ndugu zake wa karibu ndio waliokuwa kipaumbele kumtangaza vile.

Ikafikia mpaka hatua ya wale watu kutaka kwenda kumkamata na kumfunga, aache kuhubiri, aache kuwadanganya watu..waliona kama akili zake hazipo sawa kwa mtu kuonyesha tabia kama zile..lakini huyo ndiye MWOKOZI WA ULIMWENGU.
 
Kaka/dada, mtu aliyemwamini Kristo na kumfuata, si jambo la kushangaza kuonekana amerukwa na akili, si jambo la kushangaza, kuitwa mtu mwenye stress za maisha, lakini unaogapa nini kuitwa mkoloni kwa uvaaji wako mzuri binti wa Mungu, unavaa sketi, unapokataa suruali na kaptura na kupaka mawanja usoni, unaogopa nini kuitwa mshamba unajali nini?....Hujafikia hatua ya kuonekana kichaa kiasi cha kutaka kwenda kukamatwa na kufungwa kama YESU,..hata kama maisha yako hayasimuliki, yamepoteza ladha mbele ya ulimwengu, unahofu gani? Bwana Yesu alikuwa zaidi ya hapo, lakini sasa tunamwona jinsi Mungu alivyomtukuza na kumfanya kuwa mkuu wa wote, anatawala mbinguni na duniani. Wewe songa mbele, faida yake utakuja kuiona maisha baada ya hapa, wacha udharauliwe kwa uamuzi wako wa kumfuata Kristo, ondoa hofu ulimwengu ukikupa mgongo wewe nawe upe mgongo songa mbele fainali ni maisha baada ya hapa..

Hata watu wasipotaka kukusikiliza unapowaeleza juu ya tumaini ulilonalo juu ya Mungu wako, visikuumize kichwa, umekuwa mtu wa kutokusikilizwa tena kama ilivyokuwa hapo mwanzo, endelea kumtumikia Bwana, siku ile Bwana Yesu atakapoketi kama mfalme wa wafalme, ni sharti na yeye achukue watu waliopitia kama yeye ili wawe wafalme pembeni yake.

Hivyo nakutia moyo wewe ndugu ambaye unapitia changamoto nyingi kwasababu ya imani yako kwa Mungu..wewe unayepitia njia kama zile za Yesu, Zipo nyakati za wewe kufarijiwa hivyo endelea kujipa moyo sasa na Bwana atakuangazia neema zake.

Zaburi 31:24 “Iweni hodari, mpige moyo konde, Ninyi nyote mnaomngoja Bwana”.
Zaburi 27: 14 “Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.”

Isaya 40: 26 “Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake.
27 Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie?
28 Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.
29 HUWAPA NGUVU WAZIMIAO, HUMWONGEZEA NGUVU YEYE ASIYEKUWA NA UWEZO.
30 HATA VIJANA WATAZIMIA NA KUCHOKA, NA WANAUME VIJANA WATAANGUKA;
31 BALI WAO WAMNGOJEAO BWANA WATAPATA NGUVU MPYA; WATAPANDA JUU KWA MBAWA KAMA TAI; WATAPIGA MBIO, WALA HAWATACHOKA; WATAKWENDA KWA MIGUU, WALA HAWATAZIMIA”.

Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment