"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, March 14, 2019

NGUVU YA JINA LA YESU.


Katika maisha kuna vitu vikuu viwili vyenye nguvu kubwa sana, cha kwanza ni DAMU na cha pili ni JINA. Damu ni kitu pekee katika mwili wa binadamu kinachoweza kutoa taarifa zote za mtu husika, kwamfano mtu akiumwa ni damu pekee ndiyo inayoweza kueleza tatizo lake, ndugu wa mtu akitafutwa ni damu pekee ndiyo inayoweza kutoa taarifa sahihi za mtu husika. N.k Na damu ndiyo inayotengeneza baadhi ya vitu kama upendo, uvumilivu, huruma n.k kwamfano watu wenye damu moja ni wazi kuwa watapendana zaidi na kuvumiliana na kulindana kuliko watu wasiofanana damu kwasababu ni ndugu, Na jina nalo hivyo hivyo, mtu mwenye Jina kubwa atakuwa na nguvu nyingi za kiutawala na heshima kuliko mwingine, jina la Mfalme ni tofauti na jina la mtu wa kawaida, na mtu akitaka kushushwa anachafuliwa kwanza jina lake, na kwa upande mwingine watu wenye majina yanayofanana ni rahisi kupendana zaidi na kuvumiliana, tofauti na watu wenye majina tofauti.n.k

Na katika mambo ya rohoni na yenyewe ni hivyo hivyo, DAMU na JINA ni vitu vyenye nguvu sana, wachawi wakitaka taarifa za mtu wanatumia damu au jina, karibia mambo yote wanatumia damu,..na shetani anachokiogopa zaidi na anachokichukia ni DAMU yenye nguvu kuliko zote na JINA lenye nguvu kuliko yote. Kwasababu anaelewa nguvu iliyopo katika damu na jina. Na ndio maana hatuwezi na haiwezekani kabisa kumshinda shetani kwa kitu chochote kile isipokuwa kwa damu ya mmoja tu! Yenye nguvu kuliko damu zote (damu ya Imanueli).
Ufunuo 12: 10 “Nikasikia sauti kuu mbinguni,ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.
11 NAO WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa”
Kwahiyo watu walio chini ya Damu ya Imanueli, watapendwa zaidi, watalindwa zaidi, watapendelewa zaidi, watahifadhiwa zaidi, kwasababu damu iliyo juu yao Inawanenea Mema usiku na mchana. Na ni damu iliyo zaidi ya damu zote.
 
Lakini leo hatutazungumzia kwa urefu nguvu iliyopo katika Damu, bali tutaizungumzia ile iliyopo katika JINA. Ambapo kwa kuielewa hiyo tutaona pia umuhimu wa kubatizwa katika jina la Yesu.

Kwanza turudi kujifunza kuhusu Ibrahimu, ambapo kuna maswali tutajiuliza na kisha tutaendelea…Tunasoma Mungu Ibrahimu alimwita atoke Uru ya wakaldayo na aende nchi ya Kaanani, na huko Mungu alimwahidia atakuwa Taifa kubwa, uzao wake utakuwa kama nyota za Mbinguni.
 
Lakini umewahi kujiuliza kwanini Mungu anajiita, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo?, kwanini hajaishia tu kuwa Mungu wa Ibrahimu?..bali akaendelea kuwa Mungu wa Isaka na Kuwa Mungu wa Yakobo?...Na kwanini asiendelee kuwa Mungu wa Yusufu na watoto wake, lakini badala yake akagomea hapo kwa Yakobo?..Umewahi kujiuliza hilo swali?

Ni wazi kuwa kuna kitu hakikukamilika kwa Ibrahimu, ndio maana kikaendelea kwa Isaka na vile vile kuna kitu hakikukamilika kwa Isaka ndio maana kikaendelea kwa Yakobo, lakini kwa Yakobo kikakamilika, na hivyo kulikuwa hakuna haja ya Bwana Mungu kuendelea na mwingine.
Na hicho kitu si kingine zaidi ya “JINA”..Jina la Ibrahimu halikukamilika ndio maana lilibeba mbaraka wa mtoto mmoja tu! Kwa uzao wa Sara, na hivyo watoto wengine ambao Ibrahimu angekuwa nao nje ya Sara, wangekuwa hawana nafasi katika kupokea Baraka za kimbinguni au kuwa warithi wake. Ndio maana unaona Ni Isaka tu ndiye aliyekuwa amebeba Baraka za urithi lakini Ishmaeli hakupata hizo Baraka ingawa alikuwa ni mwana wa Ibrahimu.

Hali kadhalika na Isaka mwana wa Ibrahimu naye pia Jina lake halikukamilika, kwasababu na yeye alikuwa amebeba mbaraka wa mtu mmoja tu! Wa kuzirithi ahadi za Mungu,na Huo mbaraka ulikwenda kwa mmoja tu Yakobo, na ndugu yake Esau akaukosa, watu ambao ni ndugu kabisa, wamezaliwa katika tumbo moja siku moja baba mmoja, mama mmoja lakini bado mbaraka wa urithi ulishuka kwa mtoto mmoja tu Yakobo, Jiulize ni kwanini?.

Lakini ilipofika kwa Yakobo naye kuwa na wana, mambo yaligeuka, yeye alilijua hilo, na hivyo hakutaka mbaraka wake uende kwa mtoto mmoja tu! Kama ilivyokuwa kwa wazazi wake, tunaona Yakobo aliwapenda watoto wake wote, na alikuwa na watoto 12, lakini siku moja alipokutana na Malaika wa Bwana, na kupambana naye mweleka, na kumshinda, kwa kumwambia sitakuacha uondoke mpaka utakaponibariki (Mwanzo 32:25). Na tunasoma mwisho wa siku alimbariki.

Sasa kumbuka Baraka aliyokuwa anaililia Yakobo sio kuwa na Mali, kwasababu mali tayari alikuwa nazo, Baraka aliyokuwa anaililia Yakobo ni Baraka ya “JINA” ..Alitaka jina lake liwe juu ya watoto wake wote 12, na sio mmoja. Yaani kwa ufupi Baraka zake zote ziwe kwa watoto wake 12, na sio kwa mtoto mmoja tu atakayemchagua au mzaliwa wa kwanza kama ilivyokuwa kwa Isaka na Ibrahimu Babu yake.

Na tunasoma baada ya kushindana na Yule malaika, jina lake likabadilishwa siku ile ile na kuwa ISRAELI, maana yake “mshindanaji au mshindi”..Na kuanzia hapo na kuendelea Mungu akawa ni Mungu wa ISRAELI..sio wa Ibrahimu tena. Ikawa ndio mwisho wa Mungu kuhesabu vizazi kuwa yeye ni Mungu wa fulani,fulani na fulani akawa ni Mungu wa ISRAELI, Akaishia hapo kwa Yakobo, na ndio maana unaona Taifa la Mungu linaitwa Taifa la Israeli, watu wa Mungu. Na sio taifa la Ibrahimu wala Isaka. Utaona japo wale watoto walikuwa na wamama tofauti tofauti, lakini Mungu hakumchagua tena mmojawapo kuupitisha urithi wake, bali wote, Benyamini, na Rubeni hawakuwa ndugu wa karibu kama ilivyokuwa kwa Esau na Yakobo, lakini hawa walihesabika ni uzao wa Mungu kuliko uzao wa Esau.
Mwanzo 32: 22 “Akaondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, navijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Yaboki.
23 Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo.
24 Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri.
25 Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye.
26 Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki.
27 Akamwuliza, Jina lako n'nani? Akasema, Yakobo.
28 AKAMWAMBIA, JINA LAKO HUTAITWA TENA YAKOBO, ILA ISRAELI, MAANA UMESHINDANA NA MUNGU, NA WATU, NAWE UMESHINDA.
29 Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko.
30 Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka”.
Sasa nguvu iliyokuwepo katika jina “ISRAELI” ni kubwa mno kwasababu “kila ambaye aliilaani alilaaniwa na kila aliyeibariki naye alibarikiwa”..Hiyo ni nguvu ya Jina. Na jicho la Mungu liliwaelekea watu wote wa Israeli na sio mtu mmoja mmoja tena. Waliitwa watu wa Mungu, Taifa la Mungu.
 
Sasa tukirudi katika Agano Jipya, yupo mmoja tena mwingine mwenye nguvu kuliko Yakobo ambaye alishindana naye akashinda, na hivyo akakirimiwa jina kubwa kuliko lile la Israeli, kwa jina lake hilo, taifa lake lote, linaitwa kwa jina lake. Na huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO.

Wafilipi 2:5 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;
6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;
7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;
8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
9 KWA HIYO TENA MUNGU ALIMWADHIMISHA MNO, AKAMKIRIMIA JINA LILE LIPITALO KILA JINA;
10 ILI KWA JINA LA YESU KILA GOTI LIPIGWE, LA VITU VYA MBINGUNI, NA VYA DUNIANI, NAVYA CHINI YA NCHI;
11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba”

Unaona hapo, Yesu Kristo alikirimiwa jina hilo lipitalo kila jina, hata zaidi ya lile la Israeli, Kama tu kwa kupitia Yakobo wana wake wote waliingizwa katika mbaraka mmoja, kadhalika na Bwana Yesu wale wote watakaompokea wanaingizwa katika mbaraka wake kwa neema.

Kwahiyo Jina la Yesu ndio jina la Urithi wa Taifa la Mungu kwa sasa, yoyote alilaaniye jina la Yesu ameshalaaniwa na yeyote alibarikiye amebarikiwa. Jina la Yesu ndio jina la kimamlaka alilolipokea kutoka kwa BABA, na jina la Yesu hilo hilo ndio jina alilotupa sisi kwa Muhuri wa Roho Wake Mtakatifu..Ndio maana jina la Yesu linajulikana kama jina la BABA, na la MWANA na la Roho Mtakatifu..Kwasababu kalipokea kutoka kwa baba yake, ndipo likawa lake, na kisha likawa letu kwa kupitia Roho Mtakatifu. Kama Yakobo alivyolipokea jina la Israeli kutoka kwa Yule malaika, kisha likawa la kwake na baadaye likawa la uzao wake wote wa Yakobo. Na jina la YESU ndio hivyo hivyo.

Yohana 17: 11 “Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, KWA JINA LAKO ULILONIPA UWALINDE HAWA, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. 12 Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda KWA JINA LAKO ULILONIPA, NIKAWATUNZA; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie”

Yohana 17: 6 “JINA LAKO nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika”.
 
 
 
Yohana 17: 25 “Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma 26 NAMI NALIWAJULISHA JINA LAKO, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao”.

Umeona! Jina la Yesu lilivyo?..lilitoka kwa Baba, likaja kwa Mwana, na sasa lipo kwetu katika Roho Mtakatifu, tumepewa sisi, watu wa Taifa lake,ndio maana kila tunaposali ile sala ya Baba yetu, hatuachi kusema “Jina lako litukuzwe (Mathayo 6:9)”..Ni kwasababu gani?..Ni kwasababu hakuna jina lingine TULILOPEWA WANADAMU LITUPASALO KUOKOLEWA KWALO, isipokuwa jina la YESU (Matendo 4:12). Jina la Yesu ni la kwetu sisi tuliomwamini. Jina la Yesu sio tu la kutolea mapepo kama wengi wetu tunavyodhani, kutoa mapepo na kushindana na wachawi ni elimu ndogo sana ya kulitumia Jina la Yesu. Jina la Yesu ni jina la URITHI.

Sasa utajuaje kama wewe ni mmoja wa warithi wa jina hilo, au utajuaje kuwa umepewa mamlaka ya kulitumia jina hilo?. Jibu lipo kwenye biblia.

Matendo 2: 36 “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.
37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 PETRO AKAWAAMBIA, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU.
39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Umeona hapo, ukitaka uingie katika Taifa la Mungu watu wa Yesu, unachotakiwa kufanya NI KUTUBU KWANZA kwa kudhamiria kuacha dhambi zako na maisha yako ya nyuma yasiyompendeza Mungu, na kumbuka maana ya kutubu sio kuomba tu msamaha bali ni kugeuka au kuacha kile ulichokuwa unakifanya kisichokuwa sahihi, na baada ya kutubu kwa kumaanisha kabisa, na kwa kutokushurutishwa na mtu, hatua inayofuata ni kubadilishwa jina lako kwa KUBATIZWA KWA HILO JINA…Zingatia hilo!! KWA HILO JINA LA YESU, na sio kwa vyeo vyake hapana bali kwa jina la Yesu, kama maandiko yanavyosema hapo juu! Na kama yanavyosema katika sehemu nyingine katika biblia (matendo 8:16, matendo 10:48, na Matendo 19:5).

Shetani anachokifanya sasahivi ni kuwapofusha watu macho wasione umuhimu wa kubatizwa ubatizo sahihi, anatuma majeshi mengi ya mapepo wabaya yenye ushawishi mkubwa, kwa kusudi la kuwapumbaza watu wasione umuhimu wa ubatizo sahihi, waone ni sawa kwenda kujitosa tu baharini ufukweni kuogolea kwenye maji mengi au kwenye ma-swimming pool hata masaa 7 au 8 na kufurahi lakini wasione sawa kuingia kwenye maji hayo hayo mara moja tu! Kubatizwa kwa jina la Yesu Kristo. Jambo hilo shetani atahakikisha analipiga vita kweli kweli, kwasababu anajua endapo mtu huyo akifanya hivyo atakuwa ameshampoteza moja kwa moja, atakuwa ameingizwa kwenye ukuhani wa kifalme.

Ndugu unayesoma ujumbe huu, Dada/kaka maandiko hayo uliyoyasoma hapo juu! Hayajatoka katika kitabu cha dini fulani wala dhehebu fulani, bali yametoka katika kitabu chako biblia yako. Uamuzi ni wako juu ya hatima ya maisha yako. Kuchagua njia ya uzima au ya Mauti. Kuudharau msalaba au kuuheshimu,Lakini natumaini utaichagua njia ya Uzima.
 
Mungu akubariki sana.

3 comments:

  1. Safi, umevhambua vizuri. Ubarikiwe sana. Ndimi Mchg. Pagallo

    ReplyDelete
  2. Hakika huwa nafurahia sana mafundisho haya lakini vipi hamwezi kuyatoa mafundisho haya kwa njia ya PDF ili tuyapate kirahisi na kuyatunza?

    ReplyDelete
  3. mafundisho yetu yote, yanakuwa na PDF chini baada ya somo, kwa mtu anayetaka ku-download,..isipokuwa tu kwenye webiste yetu ile nyingine ambayo link yake ni hii.. >>>> https://wingulamashahidi.org unaweza ukaifungua na kuangalia chini ndugu yangu...Ubarikiwe sana

    ReplyDelete