"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, April 27, 2019

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:


Shalom! Mtu wa Mungu, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo litukuzwe daima, karibu tujifunze Neno la Mungu, na leo tutaenda kuona tabia za wanawake hawa wawili na naamini tutakwenda kujifunza kitu kikubwa hususani kwa upande wa wanawake wakristo. Watu hawa ambao tunakwenda kutazama tabia zao wa kwanza ni MKE WA HERODE, na wa pili ni Yule MKE WA PILATO.

Tunafahamu katika maandiko hawa wote walikuwa ni wake wa viongozi wakubwa waliokuwa wanaongoza Taifa la Israeli kipindi cha Bwana wetu Yesu Kristo, Herode alikuwa ni mtawala wa Galilaya upande wa kaskazini na Pilato alikuwa ni akida wa Yudea upande wa kusini wa taifa la Israeli, hawa wote hawakuwa wayahudi, walikuwa ni WARUMI. Kumbuka wakati ule Dola ya kiRumi ndio iliyokuwa inatawala karibu dunia nzima, hivyo kama ngome yenye nguvu ilikuwa ni sharti iwe na majimbo mengi au makoloni mengi chini yake ya kuyaamrisha. Kama tu tunavyofahamu kipindi kile cha ukoloni katika nchi yetu hii ambayo mwanzo iliitwa Tanganyika lilikuwa ni koloni la wajerumani, na ndivyo ilikuwa katika kipindi kile cha Bwana Yesu nchi ya Palestina (yaani Israeli), ilikuwa ni moja ya koloni la Warumi, hivyo sheria zote, na maagizo yote yahusuyo utawala pamoja na kodi zote zilikuwa zikisanywa na kupelekwa Rumi makao makuu.

Sasa kipindi kifupi kabla ya kuzaliwa Bwana Yesu KAISARI AUGUSTO ambaye tunamsoma habari zake katika Luka 2:1, ndiye aliyekuwa mtawala mkuu wa Dola hii ya Kirumi huko RUMI. Hivyo yeye pamoja na baraza lake chini yake likamweka Herode kuwa kama mfalme wa taifa lote la Palestina na nchi zilizokuwa kando kando yake. Herode huyu mkuu ndiye anayesifika kwa kulikarabati lile Hekalu lililokuwa limebomoka, (Yohana 2:22) na huyu ndiye aliyetaka baadaye kuja kumwua Yesu pindi anazaliwa mpaka kupelekea Yusufu na familia yake kukimbilia uamishoni Misri.

Sasa baada ya kufa kwake, ilipasa awepo mtu wa kumrithi ufalme wake, hivyo aliacha waraka wa urithi na kusema nchi ile ya Palestina igawanywe kwa watoto wake wote, kwahiyo alipokufa waraka ule ulipelekwa Rumi makao makuu ili kuombwa uthbitishwe na Kaisari, hivyo kaisari akathibitisha migawanyo ile na Palestina ikagawanywa kwa watoto wa Herode mkuu, sasa sehemu zile unazoziona zinatajwa sana katika agano jipya (Ndani ya taifa la Israeli) walipewa watoto wake wawili, ambapo mmoja alipewa atawale Galilaya na mwingine akapewa atawale (Samaria, Yudea na Idumea) karibu nusu ya Taifa zima la Israeli, na watoto wake wengine wawili waliosalia walipewa nchi za kando- upande wa Yordani ng’ambo, Iturea na trakoniki na Dekapoli.(Luka 3:1).

Sasa huyu mtoto mmoja wa Herode ambaye alipewa Galiliya ndio Herode Yule tunayemsoma aliyekuja kumuua Yohana Mbatizaji, na ndio huyu huyu alikuwa anamwinda Bwana Yesu baadaye aje kumuua alipokuwa anahubiri lakini Bwana alimwita Mbweha..Na ndio Yule Yule siku ile ya kusulibiwa kwake Pilato alimpeleka kwake ili ahukumiwe,lakini yeye akamrudisha kwa Pilato tena.

Lakini tukirudi kwa Yule mtoto wa pili wa Herode mkuu, ambaye alipewa kutawala upande wa chini wa taifa la Israeli ambayo ni YUDEA NA SAMARIA yote sehemu kubwa ya Israeli historia inaonyesha naye alikuwa ni mkatili vile vile kama ndugu zake, awali ya yote yeye ndio alikuwa akimtafuta mtoto Yesu, ili amwangamize Yesu aliporudi kutoka Misri na wazazi wake hata baada ya baba yake kufa.
Mathayo 2:19 “Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri,
20 akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto.
21 Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.
22 Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya,
23 akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo".
Huyu alizidi kuwa mbaya sana, Historia inaonyesha alifikia hatua hata ya Kaisari kule Rumi kutopendezwa naye, na kumwondoa kwa nguvu madarakani na kumpeleka uamishoni huko ufarasa na kukaa huko mpaka kufa kwake. Ndipo sasa akahitajika mtu wa kuijaza nafasi yake na ndio tunakuja kuona nafasi yake ikachukuliwa na huyu liwali mpya aliyejulikana kama PONTIO PILATO…atawale miji yote ile ya upande wa kusini.

Sasa mpaka hapo natumai utakuwa umepata picha kidogo, jinsi utawala huo ulivyokuwa umejiganyika, hivyo kipindi kile cha Yohana mbatizaji, na Bwana Yesu, hawa viongozi wawili yaani Herode na Pontio Pilato ndio waliokuwa wanalishikilia taifa la Israeli.

Kwahiyo turudi katika kiini cha Somo letu, tunaona viongozi hawa ambao hata hofu ya Mungu haikuwa ndani yao, watu ambao walikuwa sio wayahudi bali wapagani walikuwa na wake zao kila mmoja na mahali pake. Lakini tunaona tabia za hawa wanawake zilitofautiana sana, hususani pale lilipotokea suala la kuwaangamiza watu wa Mungu. Kama tunavyofahamu habari mke wa Herode japo alifahamu kabisa kuwa Yohana alikuwa ni nabii wa Mungu kweli, lakini yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kukitaka kichwa cha Yohana, zaidi hata ya wale mafarisayo ambao hao ndio wangestahili kukiomba kichwa cha Yohana lakini sio Yule mwanamke. Yeye alimshawishi mume wake amuue Yohana mbatizaji kwa faida zake mwenyewe..Na Herode naye kwa kutomwogopa Mungu akasikiliza viapo vya mke wake na kwenda kumwangamiza Yohana kule gerezani kwa kumkata kichwa.

Lakini tukirudi kwa mwanamke mwingine pili, ambaye naye pia alikuwa katika kiti cha kifalme, aliketi kama malkia, Tunaona Mume wake alipotaka kwenda kuwapa wayahudi amri ya kumuua Bwana Yesu, yeye alikuja na ushawishi mwingine tofauti na Yule wa kwanza, yeye alimwonya sana mume wake asidhubutu kufanya vile kwani ni mtumishi wa Mungu. Anaeleza jinsi alivyoteswa sana katika ndoto usiku kabla ya Yesu kusulibiwa, embu jaribu kutengeneza picha analala mara ya kwanza, anaota kama yeye ndio anayemngongelea misumari mtu asiye na hatia, anashtuka anaona ni ndoto tu, halafu analala tena, anaota kitu kile kile, anaamka tena, analala jambo lile lile tena linajirudia, hata mara 10, halafu asubuhi anakutana na mtu Yule Yule aliyekuwa anamwona kwenye ndoto analetwa mbele yake…Sura ile ile ya upole inakuja mbele zake,..


Hakika huyu mwanamke Mungu alimwekea kitu kingine cha ziada ndani yake.
Unaweza ukajiulizwa kwanini mambo kama haya hayakumtokea na Yule mke wa Herode? Pengine Yohana angekuwa mzima mpaka wakati wa Kristo kufa kwake,. Kwasababu kumbuka huyu hana chochote cha kumshinda Yule, wala Yule hakuwa na cha ziada cha kumshinda huyu lakini kwanini haikutokea kwa Yule mwanamke mwingine?.

Kaka/dada Kuna wakati unajiuliza maswali mengi lakini unakosa majibu, kwamfano utakutana na dada mmoja mkristo atakwambia anajisikia aibu kuvaa nguo zinazobana, na zaidi atakwambia ninajisikia kuhukumiwa ndani yangu pale ninapojaribu kudhubutu kuvaa sketi fupi, atakwambia ninajiona kama ninajidhalilisha pale ninapovaa suruali na kutembea nayo barabarani mbele za watu na bado mpendwa huyo huyo atakwambia ninaona kama bado sijawa mkristo pale ninapovaa vimini na kuweka ma-make up usoni na kwenda kanisani au kutembea mbele za watu…

Lakini wakati huo huo utakutana na dada mwingine naye anasema ameokoka atakwambia mbona mimi ninaona kawaida tu, Mungu haangalii mavazi anaangalia moyo..Utamkuta yupo confortable kutembea na vimini na suruali zinazobana barabarani, na wala hasikii chochote kinachomuhukumu ndani yake na bado anaona hakuna tatizo lolote ni sawa tu..

Embu jiulize ni roho ya aina gani ipo ndani yako?, Jichunguze ujiulize kama ni Roho wa Mungu mbona basi haiugui kwa namna moja na ya Yule mwenzako anayejisitiri?..Au unadhani ile ni roho ya shetani au ni mawazo yake tu yanampelekea kuwa vile? Na ya kwako ndio Roho ya Mungu?..Embu nenda kawaulize kabla ya kukutana na Kristo walikuwa wanavaaje watakueleza...watakuambia tofauti yao kabla ya kukutana na baada ya kukutana na Yesu.

Hujui kuwa unamsulibisha Kristo kwa matendo yako, tufauti yako na Yule mke wa Herode haipo, Roho ya Mungu imeshakufa ndani yako, HAIUGUI tena, unaona kila kitu ni okay!!. Utajitetea nipo katika mazingira magumu ya kuacha, lakini nataka nikuambie hawa wanawake wote wawili walikuwa katika mazingira ya level moja, walikuwa wake wa wakuu, tena wa kidunia, tena sio hata wayahudi, lakini mmoja alikuwa na hofu ya Mungu ndani yake na mwingine hakuwa nayo…Vivyo vivyo na wewe usidhani ni wewe peke yako upo katika mazingira magumu ya kuacha hivyo vitu..Wapo wengi tu, tena zaidi yako wewe lakini kwasababu wao wamekubali kuitii hiyo sauti inayougua ndani yao kila siku. Wamekuwa kama walivyokuwa leo hii..ambaye wewe unawaona washamba wamepitwa na wakati.

Ni maombi yangu utabadilisha mwenendo wako dada yangu, shetani anapenda kuwatumia wanawake, kuunyanyua ufalme wake, ni chombo chepesi cha shetani, alikitumia Edeni anakitumia na sasa..Hivyo wewe dada usifanyike kuwa chombo hicho chepesi chepesi tu cha shetani kukutumia anavyotaka. Sio kila mtindo wa dunia hii unaokuja mbele zako unakufaa.. mingi asili yake ni kuzimu,Biblia inasema unapaswa utufute mwenendo wa wanawake wacha Mungu mfano wa wakina Sara na Rebeka na Hana na sio wasanii wa nyimbo za kuzimu.

1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;
10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.
11 Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna”….Unaona??.

Halikadhalika na kwa mwanaume unayeweka mlegezo, unanyoa kama jogoo, unachora mwili wako tattoo, na huku unajiita ni mkristo..Jiulize ni kwanini wewe unaonaekana tofauti na wacha Mungu wengine?. Au Roho iliyo ndani yako ni bora zaidi kuliko ya wale wengine..Jiulize ndugu, jitathmini…Tumeambiwa tuzijaribu hizi roho, tunapenda injili za “haijalishi”..Na huku nyuma roho zetu zinaangamiia.

Ni maombi yangu, na matumaini yangu injili itatubadilisha, na kuanza kuenenda katika njia kamilifu za Mungu huku tukitii ile sauti ya Roho Mtakatifu inayougua ndani yetu kila siku kutukumbusha namna kuenenda katika utakatifu wote, mpaka kufikia kuja kwa Kristo Bwana wetu na wote kwenda mbinguni bila hila wa mawaa.

Mungu akubariki sana.

No comments:

Post a Comment