"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, May 13, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 62


SWALI 1:  2Wafalme2:12; `Naye Elisha akaona,akalia,Baba yangu,baba yangu,GARI LA ISRAELI NA WAPANDA FARASI WAKE! Asimwone tena kabisa;' '' Hapo anaposema "Gari la Israeli na wapanda farasi wake!-Anamaana gani?"

JIBU: Hilo ni swali la kujiuliza ni kwanini mwisho wa safari ya Eliya linatokea gari kutoka mbinguni na wapanda farasi wake, na si isiwe kitu kingine labda ngazi, au upepo au aishie kutoweka tu asionekane mpaka litokee gari la vita?, Hizi ishara zinazotokea mwisho za washindania Imani, zinakuwa na maana kubwa sana kwetu, ni sawa na Bwana wetu Yesu alivyoondoka tujiulize ni kwanini WINGU lilimpokea na si gari au malaika..lipo jambo Mungu anatuonyesha katika haya matukio.

Lakini tukirudi kwenye tukio la Eliya, Kulitokea gari la Vita, Elisha ndio alivyoliona, hii kuonyesha kuwa Eliya alikuwa vitani Duniani anapigana, na sasa mwisho wa vita vyake umefika, Ushindi ameshaupa, vita kavipiga, mwendo kaumaliza, Umefika wakati wa kuondoka, Hivyo ni wajibu lile jeshi lililokuwa linapigana naye yeye kama Jemedari wao siku zote za maisha yake, lije kumchukua na kumpeleka nyumbani kwa vishindo vikuu vya ushindi.

Vivyo hivyo hata leo kwa mtakatifu yoyote atakayemaliza kazi yake duniani kwa ushindi , siku ile anayokufa, katika Ulimwengu wa Roho lile Gari la Israeli [yaani Jeshi la ki-mbinguni] ambalo siku zote za maisha yake amekuwa akitembea nalo kupigana vita litamchukua moja kwa moja mpaka Paradiso kule watakatifu wengine walipo.

Lakini hiyo ni mpaka mtu apigane na ashinde, asiposhinda hakuna atakayekuja kumchukua, huyo atabakia kaburini, Na ndio maana Mtume Paulo mwisho wa safari yake aliandika hivi:

2Timotheo 4:6 "Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika.
7 Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda;
8 baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake".

Hivyo na sisi pia tujitahidi tukaze mwendo, siku ile tuondoke na ushindi mnono duniani. Kwasababu yapo mema mazuri Mungu ametuandalia huko tuendako.

Ubarikiwe.


SWALI 2: Biblia inaposema kwamba ..kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo lakini utauwa wafaa kwa mambo yote..inamaana gani? (1Timotheo 4:8).
JIBU: Kama ukisoma vifungu vya juu katika hiyo habari utaona, ni kuwa kulikuwa na baadhi ya watu wanawashurutisha watu kwa kuwaambia kushika mambo ya mwilini ndio bora na kunafaa kwa uzima wa mtu, kwa mfano kuzingatia aina Fulani ya vyakula, kwamba usile kambale, au usile nguruwe, au ni lazima utahiriwe unapozaliwa, au ni lazima unawe mikono pale unapokula, au kutawadha, au ni lazima mtu afanye mazoezi ya mwili, au mtu ili awe mtakatifu ni lazima mtu asioe,… n.k...

Na huku wamesahau au wamepuuzia kabisa mambo ya muhimu ya rohoni yaani kumcha MUNGU na utakatifu wa roho zao....

Na ndio hapa Paulo anamwambia Timotheo Ni kweli kwa namna moja au nyingine vinaweza vikampa mtu uzima wa mwili wake, na afya njema, hapa duniani lakini haviwezi kumpa uzima huko anapokwenda…Vitu kama hivyo haviwezi kumpa mtu daraja la moja kwa moja kwenda mbinguni, haviwezi kuzuia vitu kama tamaa za mwili n.k.

Wakolosai 2:20 "Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani,
21 Msishike, msionje, msiguse;
22 (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu?
23 Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; LAKINI HAYAFAI KITU KWA KUZIZUIA TAMAA ZA MWILI".

Unaona?. Na ndio maana Paulo anamshauri Timotheo jambo jema la kuchagua…Nalo ni Utauwa, (Utakatifu), kuwa mtu wa rohoni, au kwa namna nyingine ni KUWA NA HOFU YA MUNGU ambalo hilo tu ndio linaweza kuyadhibiti mambo yote ya mwilini na rohoni….Ukiwa na hofu ya Mungu, ukimcha Mungu hata usipozingatia mlo kamili, bado Mungu atakulinda tu na kukupa afya, na bado juu yake utakuwa na ahadi ya uzima wa milele..Tofauti na Yule mtu anayezingatia lishe bora na huku maisha yake ya rohoni yapo chini, anaweza kweli akapata afya njema, na mwonekano mzurimkwa kitambo tu lakini siku akifa atakuwa wapi kama moyo wake ni mchafu..

Unaweza ukawa umehangaika kujipatia mali ili uwe na maisha bora hapa duniani, ni kweli hapo ni sawa na umejipatia nguvu za mwilini, kwani mali ni ulinzi, zinaweza kukulinda kwa sehemu Fulani, lakini roho yako haiwezi kulindwa na mali…lakini ukiwa ni mtu wa rohoni, mtauwa, mtakatifu, unayemcha Mungu, unayeyajua maandiko, anayezijua ahadi za Mungu, analisimama imara katika Imani,..Mali ameahidiwa kuzipata halikadhalika uhakika kwa maisha ya milele upo. Sasa Kwanini na sisi tusichague fungu hilo?

1Timotheo 4:8 "Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye".

Hivyo tusipoteze muda mwingi kwa vitu vya muda tu, bali tujishuhulishe zaidi na vile vitakavyotusaidia kwa mambo yote..Hiyo ni hesabu rahisi sana na inayoeleweka.

SWALI 3: Katika Biblia tunaona, ni Makuhani tu peke yao ndio walioruhusiwa kuhudumu katika Hema ya Mungu, na ndio walioruhusiwa kuingia ndani ya nyumba ya Mungu,ambao walikuwa ni wa kabila la LAWI mwingine yeyote akiingia kule anakufa, lakini katika biblia hiyo hiyo tunamwona mtoto Samweli ambaye hakuwa Mlawi aliwekwa ndani ya ile hema mbele ya lile sanduku la agano, na hakufa na tunasoma Baba yake aliyeitwa ELKANA alikuwa anatokea katika kabila la EFRAIMU, ukisoma 1 Samweli 1 utaona jambo hilo. Hapo nahitaji ufafanuzi kidogo.

JIBU: Tukisoma 1Samweli 1:1 inasema “ Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, MWEFRAIMU”.

Ni kweli kabisa kwa sentensi hiyo inaonyesha dhahiri kuwa Baba yake Samweli alikuwa ni Mwefraimu, lakini ukijifunza maandiko kwa undani! Utagundua kuwa Elkana Baba yake Samweli hakuwa Mwefraimu bali alikuwa Mlawi. Kumbuka wakati wa agano la kale, Kipindi ambacho Yoshua anaigawanya nchi ya Kaanani kwa makabila yote ya Israeli, Kabila la LAWI halikuwa na urithi wowote, Mungu aliwaweka wawe wakfu kwake kwa ajili ya shughuli ya madhabahuni tu, hivyo walipovuka Yordani walitawanywa na kukaa katikati ya makabila yote kuwahudumia watu katika masuala ya Torati na Ibada,..Hivyo walawi waliokuwa wanakaa Dani, waliitwa wanadani, walawi waliokuwa Rubeni waliitwa warubeni, vivyo hivyo walawi waliokuwa wanakaa Efraimu waliitwa waefraimu.

Kumbukumbu 18: 1 “Makuhani Walawi, kabila yote ya Lawi, wasiwe na fungu wala urithi pamoja na Israeli; watakula sadaka za Bwana zifanywazo kwa moto, na urithi wake.
2 Wala wasiwe na urithi kati ya ndugu zao; Bwana ndiye urithi wao, kama alivyowaambia”

Sasa kuthibitisha jambo hilo kuwa Samweli alikuwa ni mlawi, turudi katika kitabu cha Mambo ya Nyakati..Tusome.

1 Nyakati 6: 33 “Na hawa ndio waliofanya huduma pamoja na wana wao. Katika wana wa Wakohathi; Hemani mwimbaji, mwana wa Yoeli, MWANA WA SAMWELI;
34 MWANA WA ELKANA, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu;
35 mwana wa Sufu, mwana wa Elkana, mwana wa Mahathi, mwana wa Amasai;
36 mwana wa Elkana, mwana wa Shauli, mwana wa Uzia, mwana wa Urieli;
37 mwana wa Tahathi, mwana wa Asiri, mwana wa Ebiasafu, mwana wa Kora;
38 mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, mwana wa Israeli.
39 Na nduguye Asafu, aliyesimama upande wake wa kuume, huyo Asafu alikuwa mwana wa Berekia, mwana wa Shimea;
40 mwana wa Mikaeli, mwana wa Baaseya, mwana wa Malkiya;
41 mwana wa Yeatherai, mwana wa Zera, mwana wa Ido;
42 mwana wa Yoa, mwana wa Zima, mwana wa Shimei;
43 mwana wa Yahathi, mwana wa Gershoni, mwana wa Lawi.
44 Na upande wa kushoto ndugu zao, wana wa Merari; Ethani, mwana wa Kishi, mwana wa Abdi, mwana wa Maluki;
45 mwana wa Hashabia, mwana wa Amazia, mwana wa Hilkia;
46 mwana wa Amzi, mwana wa Bani, mwana wa Shemeri;
47 mwana wa Mali, mwana wa Mushi, mwana wa Merari, MWANA WA LAWI.
48 Na ndugu zao, Walawi, ndio waliowekwa ili kufanya huduma yote ya maskani ya nyumba ya Mungu”.

Unaona hapo? Ukiufuatilia huo uzao wa Elkana baba yake Samweli utaona unakuja kuishia kwa LAWI. Kwahiyo ni wazi kuwa Baba yake Samweli, Elkana hakuwa Mwefraimu bali Mlawi..Mungu asingeweza kuruhusu mtu yeyote asiyekuwa mlawi kuhudumu katika nyumba yake au hema yake.

Kwahiyo Samweli alikuwa ni Mlawi, Mlawi mwenye asili ya Efraimu

Ni sawa na leo Mchaga aliyezaliwa Kenya aje kuishi Tanzania, moja kwa moja atajulikana kama ni Mkenya..kwasababu amezaliwa Kenya na si Tanzania, ingawa asili yake na kabila lake ni Tanzania.

Kwahiyo hiyo ndio sababu Elkana baba yake Samweli aliitwa Mwefraimu, ni kutokana na mahali alipotokea na sio kutokana na kabila lake.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment