"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, May 3, 2019

MASWALI NA MAJIBU:SEHEMU YA 61


SWALI 1: Shalom Mtumishi naomba kufahamu Mtumishi wa Mungu, Ayubu aliteseka katika majaribu kwa miaka mingapi?.
JIBU: Biblia haijatueleza muda Ayubu aliokaa katika majaribu, Lakini tukisoma baadhi ya vipengele inatupa picha kukisia muda aliodumu, kwa mfano tukisoma ile sura ya Ayubu 7:2-6
Ayubu anasema.. “2 Kama mtumishi atamaniye sana kile kivuli, Kama mwajiriwa anayetazamia mshahara wake; 3 Ni vivyo nami NIMEPEWA MIEZI YA UBATILI iwe fungu langu, NAMI NIMEANDIKIWA MASIKU YENYE KUCHOKESHA.
4 Hapo nilalapo chini, nasema, Nitaondoka lini? Lakini usiku huwa mrefu; Nami nimejawa na kujitupa huku na huku hata kupambazuke. 5 Mwili wangu unavikwa mabuu na madongoa ya udongo; Ngozi yangu hufumba, kisha ikatumbuka tena. 6 Siku zangu hupita upesi kuliko chombo cha kufumia, Nazo zapita pasipokuwa na matumaini.”

Unaona hapo Ayubu anajaribu kujifananisha na mtu aliyeajiriwa ambaye kwa uvumilivu mwingi anasubiri mshahara wake kila mwisho wa kipindi Fulani labda tuseme wiki, au mwezi au mwaka,.apate faraja ya taabu yake, vivyo hivyo Ayubu naye anaonyesha amekaa katika hali hiyo ya kusononeka na kutaabika kwa MIEZI na masiku mengi, kama ya mwajiriwa vile, akisubiria faraja yake kutoka kwa Mungu ni lini atamrehemu na kumtoa katika mateso yale na majonzi yale..

Tunaona hapo Ayubu katamka neno MIEZI na sio MWEZI, hiyo ikiwa na maana ni zaidi ya mmoja, inaweza ikawa ni miwili au mitatu, au mitano au 12, au 20, au 100 hatujui kwasababu biblia haijaeleza jambo lingine la ziada. Halikadhalika Pia hatujui ni muda gani ilimchukua Ayubu kukaa na wale marafiki zake, ambao tunasoma pia waliwasili kwake na kukaa siku 7 bila kuzungumza naye chochote, hivyo tukijumulisha na siku ambazo ziliwagharimu kufika kwa Ayubu kutoka majumbani kwao baada ya kupata taarifa za msiba wake, pamoja na siku ambazo walikuwa wanazungumza naye.. tukijumuisha na wakati ambapo Mungu anamwagiza Ayubu awaombee rehema wale marafiki zake kwa kwenda kuchukua ng’ombe 7 na kondoo 7 kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, tunaweza kukisia ni muda unaoweza kuchukua zaidi ya mwezi..

Lakini pia hatujui, kipindi Mungu alichotumia kumrejeshea Ayubu vitu vyote na mali zote alizozipoteza, je ilikuwa ni mara moja au kidogo kidogo, kama ni kidogo kidogo basi ni muda mrefu ulipita, lakini tunachofahamu ni kuwa Mungu alimburudisha Ayubu mara mbili ya alivyokuwa navyo pale mwanzo. Lakini hiyo ilikuwa ni kwa kusubiri na kwa kustahilimili na kwa kuvumilia.

Yakobo 5.10 “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.11Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”

Hivyo na sisi tunafundishwa tujifunze kuwa wavumilivu maadamu tunajiona bado tupo katika njia sahihi ya wokovu,hatuna budi kuwa hivyo kama Ayubu, tabu, shida, misiba, dhiki, mateso, kupungukiwa, n.k. visituzimishe roho tukamkufuru Mungu kama mke wa Ayubu, hata kama itachukua mwezi, au miezi, au miaka, au miongo, hilo lisituzuie kuangalia ahadi za Mungu, sisi tunachofahamu tu ni kuwa mwisho wa siku tutamwona Mungu jinsi alivyo mwingi wa rehema na huruma…kama alivyokuwa kwa Ayubu.

Ubarikiwe.

SWALI 2: Katika Luka 19:12-27 huu mfano una maana gani ?!!
JIBU: Tusome.. Luka 19:12 “Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.
13 Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja.
14 Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.
15 Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.
16 Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.
17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.
18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.
19 Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.
20 Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso.
21 Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.
22 Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;
23 basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?
24 Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.
25 Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.
26 Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho.
27 Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu”.
Shalom! Mfano huo Bwana aliutoa alikuwa anajizungumzia yeye na kanisa lake.

Huyo Mtu Kabaila aliyesafiri kwenda nchi ya mbali ni BWANA wetu YESU mwenyewe, (KABAILA maana yake ni MTU ALIYEZALIWA KATIKA FAMILIA YA JUU ZAIDI KATIKA JAMII inaweza kuwa familia ya kifalme au kichifu,nk) kama tunavyojua, Bwana Yesu asili yake ni Mbinguni ametoka katika familia ya kimbinguni, na ndio maana hapa anajifananisha na huyu Kabaila, tunaona na baada ya kumaliza tu kazi yake alipaa kwenda mbingu za mbingu..sasa hiyo ndiyo nchi ya mbali inayozungumiwa pale kwenye huo mfano, Na amekwenda kule kwa makusudi kabisa ili kutuandalia sisi makao ili arudi tena kuja kutuchukua.

Na kama mfano unavyosema “akawaita watumwa wake kumi akawapa mafungu 10 ya fedha” maana yake ni kwamba Bwana wakati anaondoka duniani siku ile alituachia sisi Roho wake Mtakatifu..kisha akatugawia majukumu kama agizo kuu, akatuambia tukahubiri injili kwa kila kiumbe ili kuleta faida katika ufalme wa mbinguni, aaminiye na kubatizwa ataokoka, kwahiyo Roho Mtakatifu aliachiliwa juu ya kila mwamini kila mmoja kwa kiwango chake cha neema alichopewa, hilo ndio fungu la fedha kwenye huo mfano (Matendo 2:38)..Ukichunguza pia utaona hawakuambiwa wakafanye biashara moja, hapana kila mmoja alikuwa na uhuru wa kufanya biashara yake, hii ikiwa na maana kila mmoja anayo karama yake Mungu kampa. Na kwa kupitia hiyo utaulizwa uliitumiaje katika mambo yahusuyo ufalme wa mbinguni.

Uwe ni mwinjilisti uwe ni mwalimu uwe ni mchungaji n.k.

Na kama huo mfano unavyosema kwamba kuna siku moja yule kabaila alirudi, na kuanza kuwauliza wale watu aliowapa yake mafungu kila mmoja ameleta faida kiasi gani katika biashara, Ndivyo itakavyokuwa kwetu kila mmoja ataenda kutoa hesabu mbele ya Bwana wetu YESU siku ile. kaitumiaje neema aliyopewa duniani

Ndipo atakapowakusanya watumishi wake wote, na kuanza kumlipa mmoja baada ya mwingine kulingana na jinsi alivyotumika katika huduma, katika nafasi yake ya kuhubiri injili..waliotumika kwa uaminifu watalipwa thawabu kubwa zaidi, lakini waliozembea au waliokuwa wanafanya kazi ya Mungu kwa ulegevu na uvivu, au kinyume cha Neno Bwana anasema atawanyang'anya na thawabu yao na kupewa watu wengine.

Kwahiyo hiyo ndio maana ya mfano huo, unatufundisha kuwa makini sana na Neema Mungu aliyotupa ya Roho wake Mtakatifu, na karama alizotupa, kwamba siku moja tutakwenda kuulizwa, kama umepewa karama ya kuhubiri, au kufundisha halafu haufundishi inavyopaswa au kulingana na Neno, au unakuwa mvivu na kuendelea na mambo yako mengine na kuidharau kazi ya Mungu…Basi siku za mwisho utakwenda kuulizwa..Kama ulipewa karama ya kuhubiri kwa njia ya uimbaji na uimbaji wako hauna tofauti na waimbaji wa miziki ya kidunia, kila mtu akutazamapo anaona kitu tofauti na unachoimba, utakwenda kuulizwa siku ile.

Ndio maana Bwana anasema Ufunuo 22:12 “Tazama, naja UPESI, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho”.


SWALI 3: Tofauti kati ya uzinzi na uasherati ipo wapi?. Pale Bwana Yesu aliposema “Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.(Mathayo 5:32)” Alimaanisha nini?.
JIBU: Neno usherati kama linavyoonekana kwenye kamusi, tafsiri yake ni “kufanya kitendo cha ngono na mtu ambaye bado haujaoana naye”..hii ikimaanisha kuwa inaweza ikawa mtu yupo ndani ya ndoa au nje ya ndoa, tofauti na Neno UZINZI, ambao huo unakuja pale mtu anapofanya kitendo cha ngono na mtu ambaye si mwanandoa mwenzake (yaani kitendo cha kutoka nje ya ndoa na kwenda kufanya ngono).

Hivyo tunaweza kusema Neno Usherati ni Neno la ujumla likimaanisha kitendo chochote cha zinaa kinachofanywa na mtu isivyopaswa yaani nje ya ndoa halali. Kwahiyo Bwana Yesu aliposema pale katika Mathayo 5:32 na Mathayo 19:9, kwamba lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi;.. kitendo kile alikilenga hasa kwa wanandoa, kwasababu habari iliyokuwa inazungumziwa pale ni ya watu ambao wapo katika mahusiano ya mke na mume.

Pia kwa kuongezea hapo, ukisoma sehemu nyingi katika maandiko kwenye agano la kale na jipya, utaona Mungu alilitumia hilo neno Uasherati, kumaanisha uzinzi ambao watu wake walikuwa wanafanya katika roho, soma 2 Nyakati 21:10-14, Ezekieli 16:27, 43, 58, Ezekieli 22:11, Ufunuo 17:1-5, 19:2 n.k. vipo vifungu vingi sana na vyote hivyo vinautaja uzinzi kama uasherati, ambao watu wa Mungu wameufanya na sanamu na machukizo yao…Uasherati ni Neno la Ujumla, ukitaka kushikilia tu Uasherati katika biblia unamaanisha kitendo cha ngono nje ya ndoa takatifu, basi biblia itakuwa haina maana sehemu nyingi, ikiwemo katika hivyo vifungu nilivyovitoa hapo juu.

Hivyo biblia inaposema Ndoa na iheshimiwe na watu wote, ilimaanisha kweli kweli. huwezi kuingia tu kwenye ndoa halafu ukajifanyia tu mambo unayotaka ukaamua kwenda kuzini ukijifariji kuwa hiyo ndoa tayari imeshafungwa haiwezi kuvunjika..Ndugu nataka nikuambie Inaweza kuvunjika kwa kitendo hicho na isiwe makosa mbele za Mungu kwenda kuoa/kuolewa na mwingine.

Lakini ifahamikie pia hilo halikuwa agizo kwamba kila kitendo cha kukosa uaminifu katika ndoa iwe sababu ya mtu kumwacha mkewe na kwenda kuoa mwingine hapana..

Mungu hapendi kuachana biblia imesisitiza hilo, na zaidi ya yote tumefundishwa kusamehe, kwani hata na sisi tunamkosea Mungu kwa mengi. Hivyo kusamehe ni msingi mkubwa sana wa ndoa kusimama. Na zaidi ya yote ni uaminifu na kuwa na hofu kwa Mungu, tukijua kuwa ndiye Mungu aliyeiunganisha, tusigeuke kuwa VIFO katikati yetu. mwanandoa aliweke hilo kichwani kuwa akienda kuzini amestahili kuachwa kibiblia na kusiwe na hatia zozote mbele za Mungu.

No comments:

Post a Comment