"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, June 17, 2019

NITAONGEZAJE NGUVU ZANGU ZA ROHONI?

Hapo nyuma, kabla sijampa Kristo maisha yangu, na wakati ambao bado ni mchanga kabisa wa masuala ya wokovu, niliaminishwa kuwa kigezo kikuu kinachomtambulisha mtu huyu kuwa anazo nguvu nyingi za rohoni ni kiwango chake cha UPAKO, pengine na wewe ulifahamu hivyo au unafahamu hivyo, yaani mtu kuwa na uwezo wa kufanya miujiza,au kuona vitu katika ulimwengu wa roho kama vile mapepo, wachawi,majini, kuona maono, kuota ndoto, kunena sana kwa lugha, au kufanya sana ishara.n.k. Kwamba mtu kama huyo ni mtu mwenye nguvu nyingi sana rohoni na hivyo shetani anamwogopa sana. Jambo hili lilinifanya nione shauku kutatufa Upako kuliko kitu kingine chochote.

Lakini je! Kwa mujibu wa biblia hizo ndizo nguvu za rohoni?. Leo tutajifunza juu ya hilo, na ni kitu gani tufanye ili nguvu zetu za rohoni ziongezeke. Sasa Ili kuelewa nini maana ya nguvu za rohoni, ni vizuri tujifunze kwanza juu ya nguvu nyingine, Tunajua siku zote kitu chochote chenye nguvu huwa kinakuwa na uwezo wa “kuteka na kutawala”, Simba ni mnyama mwenye nguvu na ndio maana ameteka pori lote, hivyo nguvu ya aina yoyote ile huwa inateka na kutawala, tunafahamu pia mtu mwenye nguvu ya kiuchumi huwa anatawala, mwenye nguvu ya kisiasa huwa anateka na kutawala, mwenye nguvu ya kiteknolojia huwa na uwezo pia wa kuteka na kutawala, na ndio maana tunaona mataifa kama Marekani na Ulaya, yanatawala dunia sio kwasababu ni makubwa hapana, bali kwasababu yana nguvu Fulani zinazowazidi wengine.

Vivyo hivyo na kwa mwenye nguvu za Rohoni, ni lazima mtu awe na uwezo wa kuteka na kutawala, na ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya.
Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.”,
 Unaona nguvu anazozizungumzia sasa hapo ni NGUVU ZA ROHONI. Ikiwa na maana kuwa mtu mwenye nguvu nyingi za Rohoni ndiye atakayeweza kuuteka ufalme wa mbinguni, ukiwa na nguvu chache utakuwa mnyonge tu. Na leo nataka ujue hizi nguvu za Rohoni zinapatikana wapi.

Sasa tukirudi kwenye huo huo mstari hapo juu, lazima tujiulize swali moja, ni kwanini Bwana alisema “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa”, kwanini hakusema tangu siku za Ibrahimu au za Musa hadi sasa? Badala yake anasema “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa”, . Utagundua kuwa Bwana alitaka tujifunze kitu Fulani kwa Yohana mbatizaji katika masuala ya kupata nguvu za rohoni. Hivyo embu tumwangalie kidogo Yohana alikuwa ni mtu na namna gani tangu utoto wake.

Maandiko yanatuambia:
Luka 1:80 “Yule mtoto akakua, AKAONGEZEKA NGUVU ROHONI, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli”.
Unaona kumbe Yohana tangu utoto wake alikuwa akiongeza nguvu rohoni kwa kasi sana, mpaka alipokuwa mtu mzima alipoanza huduma yake. Lakini hakuwahi kufanya muujiza hata mmoja, wala kutoa ishara yoyote kutoka mbinguni kama vile Eliya, Biblia inasema hivyo (Yohana 10:41), Na ndio maana tunasema Upako wowote kulingana na maandiko sio kitambulisho kuwa mtu huyo anazo nguvu za rohoni. Mtu unaweza akawa na uwezo wa kuona maono yote duniani lakini rohoni ukawa mdhaifu kuliko hata mtu aliyempa Kristo maisha yake leo.
Sasa tunaona Yohana alipoteza muda wake mwingi kukaa mbali na makazi ya watu ili tu kuongeza nguvu zake rohoni tangu utoto wake,(baadaye kidogo tutaona ni kitu gani alichokuwa anakifanya alipokuwa anakwenda kule jangwani) mpaka kufikia kilele cha nguvu za rohoni mpaka Bwana Yesu Kumshuhudia vile katika: 
Mathayo 11:11 “Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; 
12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.”.
Kwa Nguvu alizokuwa nazo rohoni, hakukuwahi kutokea nabii au mtu yoyote katika agano la kale aliyeweza kumfikia, sio Ibrahimu, sio Musa, sio Eliya, sio Daudi sio mtu yoyote Yule aliyefanya mambo makubwa unayemsoma katika agano la kale aliyeweza kuwa na nguvu zaidi yake (Yohana) kuuteka ule ufalme. Lakini Leo utafahamu SIRI imelala wapi nawe uanze kujishughulisha nayo.

Sasa kumbuka Yohana tangu utoto wake hakuwahi kujishughulisha na jambo lingine zaidi ya kutafuta kumjua huyu MASIHI ALIYETABIRIWA NI NANI?. Ambaye ndiye kiini cha dini yao kiyahudi, ndiye kiini cha wokovu uliokuwa unatarajiwa wa ulimwengu mzima, wakati wengine wanang’ang’ania kukariri torati huyu aling’ang’ania kumtafuta Kristo ambaye Mungu alimshuhudia tangu enzi za kale za manabii. Na hiyo ndiyo iliyomfanya mbinguni aonekane kila siku nguvu zake za rohoni kuongezeka kwa kasi sana.

Alianza kutafuta kwa bidii katika torati habari zake, tangu mwanzo mpaka mwisho, kwa jinsi alivyokuwa anamtafuta kwa bidii akachunguza akaona kuwa kumbe kwa mfano ule ule wa wana wa Israeli walivyookolewa utumwani Misri ndivyo mwokozi atakavyouokoa ulimwengu wote kwa jinsi hiyo hiyo..

Kwa hatua zile tatu, ambapo hatua ya kwanza, ilikuwa ni Yule mwanakondoo kuchinjwa, ili damu ipatikane kwa pigo la mzaliwa wa Kwanza Misri, akajua kumbe damu ilihitajika kufungua vifungo. Na pigo lile lililegeza kweli vifungo vya maadui zao kuwapa ruhusu wa kutoka Misri, lakini lile halikutosha kuwafanya maadui zao wasiwafuatilie, hivyo ilihitajika hatua nyingine ya pili na ndio ile ya nguzo ya moto, ambayo ilikuwa inawatangulia mbele yao sasa ilibidi irudi nyuma yao kuweka wigo wasiwafuate.. Yohana akagundua kumbe moto ulipitia juu yao kuwatakasa pasipo wao kujijua.
Lakini moto ule haukutosha kumaliza kabisa adui yao ulipoondolewa, bado walitaka kuwafuata na ndipo tunaona maji yalifuata kuwatakasa tena, nako ndiko kule kuvuka bahari ya shamu Kubatizwa, na hapo ndipo maadui zao walipomalizwa moja kwa moja walipotoswa na yale maji.

Hatua hizo tatu (yaani damu ya mwana-kondoo, moto-wa-Roho Mtakatifu, na Maji), ndizo Yohana alitambua kuwa Masihi ajaye atazitumia kumkamilisha mwanadamu kwa wokovu wake.

Sasa hapo ndipo Yohana alipopatia ufunuo wa ubatizo wa Maji akaanza kuufundisha na kuwaambia watu wabatizwe, huku akitazamia kuwa mwanakondoo atakajua ambaye atakamilisha yaliyobakia yaani maji na moto wa Roho Mtakatifu,
Yohana 1:26 “Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi.
27 Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake.
28 Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza.
29 Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, MWANA-KONDOO WA MUNGU, AICHUKUAYE DHAMBI YA ULIMWENGU!
30 HUYU NDIYE NILIYENENA HABARI ZAKE YA KWAMBA, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.
31 Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji.
32 Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake.
33 Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.
34 Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.
35 Tena siku ya pili yake Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake.
36 Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!
37 Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu”.
(Soma pia Mathayo 3:11)..

Unaona hapo Yohana alimtambua YESU na Kazi yake atakayokuja kuifanya kabla hata hajawasili, alimtengenezea njia, Hivyo mbinguni akaonekana mtu mkuu sana, mwenye nguvu nyingi za rohoni japo duniani watu walimwona maskini amerukwa na akili.

Leo hii nataka nikuambie ndugu usifurahie tu kuwa YESU ameyaokoa maisha yako, halafu ukaridhika, mahali ulipo, unaendelea na mambo yako, YESU KRISTO ni zaidi ya unavyomfikiria, Mungu kaweka Heshima yake yote pale, ndio hekima ya Mungu na NGUVU YA MUNGU (1Wakorintho 1:24), na ndipo utajiri wote, na hazina zote za maarifa zilipolala. Hapo ndipo Yohana alipopatia heshima yake na ukuu wake.

Wakolosai 2:2 “….wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo;
3 ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika.”
Kwa mtu Yule leo hii anayejishughulisha kutafuta kumjua YESU usiku na mchana, mtu huyo nguvu zake za rohoni zinaongezeka kwa kasi sana pasipo hata yeye kujijua. Na mwisho wa siku anajikuta anauteka ufalme wa Mbinguni kirahisi kabisa kwasababu amefahamu mahali lulu ya thamani ilipo.

Itafute hii LULU ndugu. Nataka nikuambie vita kubwa ya shetani ipo hapo, watu wasimjue Kristo ni nani hasaa na uweza wake, yeye anataka watu wamwone kama mtu wa kawaida tu, kwasababu anafahamu mtu akishamwelewa vizuri Bwana Yesu ni nani, basi atajijengea daraja zuri mbinguni na atamsababishia madhara makubwa sana katika ufalme wake.

Anza leo mwanzo mpya, maanisha kumfauta Kristo…usitafute upako wala miujiza..Bwana akikujalia hizo ni vizuri lakini sio jawabu la kuwa na nguvu za rohoni…Ikiwa unapenda kuwa mkuu hata zaidi ya Yohana, machoni pa Mungu,wala usijishughulishe na jambo lingine lolote, JISHUGHULISHE KATIKA KUMTAFUTA KRISTO, acha kuzisumbukia karama, acha kutafuta maombezi, acha kukesha kwa ajili ya upako, kesha kwa ajili ya KUMSOMA KRISTO. Sisemi usizitumie hizo karama, hapana zitumie maadamu Mungu kakupa, lakini huku nyuma usisahau kuwa ufalme wa mbinguni unatekwa na wenye nguvu za mafunuo ya YESU Kristo. Tumeaswa tumjua sana Yesu Kristo, Mwana wa Mungu mpaka tufikie kimo cha utimilifu wake.
Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani NA KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”
Unapoyatafakari maandiko, jenga mtazamo wa Kristo ndani yake, wengi wakifungua maandiko wanayatazama kwa sura ya mafanikio ya kidunia, hivyo wanapata ufunuo kulingana na walichokitazamia, lakini ukimsoma Kristo kwa lengo la kutaka kumjua zaidi…atakujaza maarifa na nguvu za rohoni, atajifunua kwako na kuanza kukufundisha kanuni zake zote kwa namna ya ajabu sana.

Ubarikiwe sana.

6 comments:

  1. Replies
    1. Some zuri Saana, Hakika nimebatikiwa na kuelewa
      Mungu akubariki mtumishi

      Delete
    2. Oooh amen amen SoMo zuri Sana Sana linatoa mtazamo mpya Sana kwa habari ya kitofauti karama na nguvu za Rohoni wengi wetu tulikuwa tunajua kwa mtu anayefany miujiza mingi ndiye ana nguvu zaidi kumbe sivyo ilivyo ...amen amen. Ubarikiwe Sana mtumishi wa Mungu

      Delete
  2. I am blessed may God bless you

    ReplyDelete
  3. SoMo zuri Mungu akubariki sana

    ReplyDelete