"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, June 30, 2019

UFUNUO: Mlango wa 11


Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha Ufunuo, biblia inasema Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu,. Heri maana yake ni amebarikiwa, hivyo umebarikiwa wewe ambaye unakiu ya kufahamu maarifa yaliyomo katika kitabu hichi cha Ufunuo, wengi hawakipendi, wengine wanakiogopa kwasababu kimebeba hukumu nyingi lakini pia wafahamu kitabu hiki kimebeba Baraka nyingi kwa yeye asomaye na kuyashika yaliyoandikwa humo.. leo tukiwa katika ile sura ya 11, Kama hujapitia sura zilizotangulia, ni vizuri ukazipitia kwanza taratibu kisha kwa Neema za Bwana tuendelee pamoja katika sura hizi za mbeleni. Kupata maelezo ya ufunuo sura ya 10 bofya hapa ⏩ ufunuo 10......Tusome:
Ufunuo 11:1 “Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, Inuka, ukalipime hekalu la Mungu, na madhabahu, na hao wasujuduo humo.
2 Na behewa iliyo nje ya hekalu uiache nje wala usiipime, kwa maana Mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili”.
Hapa tunaona Yohana akipewa ono lingine likiwa baada ya Ono la yule Malaika Mkuu, maono haya yalifuatana lakini katika Ono hili aliona anapewa Mwanzi kama fimbo, na Mmoja akamwambia ainuke akalipime hekalu la Mungu na madhabahu, na hao wasujuduo humo..

Sasa katika Ono hili Yohana anapelekwa moja kwa moja katika mji mtakatifu, yaani YERUSALEMU, Na anafika anaonyeshwa Hekalu la Mungu, ambalo lipo Yerusalemu na anaambiwa alipime, Kumbuka hekalu la kwanza lililojengwa na Mfalme Sulemani, lilibomolewa na Mfalme Nebukadneza, Na baada ya wana wa Israeli kutoka utumwani Babeli, walijenga tena Hekalu lingine la pili mahali pale pale lilipokuwa limejengwa hekalu la kwanza…lakini nalo baada ya miaka kadhaa kama 585 hivi lilikuja kubomolewa tena na jeshi la Warumi (mwaka 70BK), Hivyo Israeli ikabaki bila hekalu tangu huo mwaka wa 70BK mpaka Leo…Takribani miaka 1949 mpaka sasa..

Sasa maandiko yanatabiri kuwa siku za mwisho, Hekalu hili litajengwa tena kwa mara ya tatu, na litakapojengwa, wayahudi watarejea katika desturi zao kama za kwanza za utoaji wa sadaka za kuteketezwa na kufanya ibada za upatanisho. Na hiyo yote inatokana na Wayahudi macho yao kufumbwa kutomjua kuwa YESU KRISTO waliyemkataa ndiye Masihi wao aliyetabiriwa na yeye ndiye Hekalu la Mungu, na yeye ndiye Sadaka iliyobora, kwamba wangemjua yeye kwa namna hiyo basi wasingekuwa na haja ya kurejea tena kufukiza uvumba na kuchinja sadaka za Wanyama na kushughulika na hekalu la kimwili…Lakini biblia inatabiri wataendelea na huo upofu hata mpaka watakapolijenga tena Hekalu la Tatu, na kipindi kifupi sana baada ya kumaliza kujilenga hekalu hili, baadhi yao watafumbuliwa macho na kuigundua sadaka ya kweli ni ipi na hekalu la kweli ni lipi kuwa ni YESU KRISTO, Hivyo hao watakaojua ndio watatiwa muhuri na Roho Mtakatifu mwenyewe..Ndio wale 144,000 tunawasoma katika Ufunuo 7..

Sasa kwasababu ni Mungu mwenyewe ndiye kawafumba macho wasimjue Kristo, hivyo bado yupo nao hajawaacha kabisa…Bado analipenda Taifa lake Israeli na kulilinda, aliahidi kutokuliacha kwa namna yoyote ile.
Isaya 44:21 “Kumbuka haya, Ee Yakobo; nawe Israeli, maana wewe u mtumishi wangu; nimekuumba; u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi”. Soma pia 
Isaya 49:16-26.
Kwasababu hiyo basi hata katika Ujenzi wa Hekalu hilo la tatu watakalokuja kulijenga bado Bwana atakuwa pamoja nao..atawapigania na kuwatetea katika ujenzi huo, maadamu hawamjengei baali wala miungu migeni bali wanamjengea Mungu wa mbinguni hivyo Bwana atawaheshimu hata katika Imani hiyo. Kwahiyo biblia inatabiri watafanikiwa katika hilo, na watalisimamisha hekalu la tatu..

Sasa mahali ambapo Hekalu hili la tatu, linapaswa lijengwe leo pamesimamisha Msikiti wa Waislamu. Ingawa wapo watafiti wa kiyahudi ambao Wamejaliwa akili na Bwana wanasema…Hekalu la kwanza la Sulemani lilikuwa limejengwa futi 150, kutoka mahali Msikiti huo ulipojengwa..kwahiyo endapo wakitaka kulijenga tena Hekalu inaweza kufanyika hivyo pasipo kuugusa huo msikiti. Lakini kwa vyovyote vile mahali pale lazima pasafishwe kupisha ujenzi wa tatu wa Hekalu hilo, hivyo kama ni eneo la kwenye huo msikiti, itahitajika muujiza kuuondoa. Na maandalizi ya ujenzi huo yapo tayari sasa hivi tunavyozungumza…kila kitu kipo tayari ghafla tu! Siku sio nyingi kutasikika ujenzi umeanza huko. Na hiyo itakuwa ni ishara kubwa ya siku za mwisho, kwani ndio utakuwa mwanzo wa kufunguliwa kwa lile juma la 70 la mwisho la Danieli lililosalia. Ambayo ni miaka 7 tu.

Sasa wakati wa ujenzi wa Hekalu hili, shetani naye atajaribu kuingilia kwa namna zote, kuzuia au kujipendekeza kama alivyokuwa anataka kujiingiza na kujipendekeza wakati wa ujenzi wa Hekalu la pili, pale walipotaka kujiingiza katika kuchangia ujenzi wa hekalu lile…
Ezra 4:1 “Basi adui za Yuda na Benyamini, waliposikia ya kuwa wana wa uhamisho wanamjengea Bwana, Mungu wa Israeli, hekalu,
2 wakamkaribia Zerubabeli, na wakuu wa mbari za mababa, wakawaambia, Na tujenge sisi nasi pamoja nanyi; kwa maana tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi, nasi twamtolea dhabihu tangu zamani za Esarhadoni, mfalme wa Ashuru, aliyetupandisha mpaka hapa.
3 Lakini Zerubabeli, na Yoshua, na wakuu wengine wa mbari za mababa katika Israeli, wakawaambia, Ninyi haiwahusu kushirikiana nasi katika kumjengea Mungu wetu nyumba; bali sisi wenyewe peke yetu tutamjengea Bwana, Mungu wa Israeli, nyumba, kama mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi, alivyotuamuru.
4 Ndipo watu wa nchi wakaidhoofisha mikono ya watu wa Yuda, wakawasumbua, walipokuwa wakijenga”.
Na kadhalika katika ujenzi huu wa hekalu la Tatu, Mpinga-Kristo (Papa wa wakati huo) atataka kuingiza ushirika na Wayahudi kulijenga, na hivyo wayahudi watafanya kosa kubwa sana la kukubali kushirikiana naye (Na mwisho wa siku ataingia Agano na Taifa la Israeli), kama Danieli 9:27 inavyotabiri…atataka kuweka mchango wake mkubwa sana katika kazi hiyo, kwa njia ya mkataba..Kwani wakati huo pia atakuwa ameshapewa nguvu na mataifa yote ulimwenguni na kuaminiwa kuwa ni mtu wa Amani (Man of peace), mkataba huo au makubaliano hayo atakaoingia na Taifa la Israeli utakuwa ni wa miaka saba..kwamba ndani ya hiyo miaka saba tutafanya hichi na hichi kwa pamoja.Wayahudi pasipo kujua kuwa yule ndiye Mpinga-Kristo aliyetabiriwa katika Kitabu cha Danieli kuwa malengo yake ni kuabudiwa kama Mungu ndani ya hekalu la Mungu, watakubaliana naye…Sasa kumbuka Kanisa katoliki ndio kanisa lenye utajiri mkubwa kuliko taasisi zote za kidini na kisiasa ulimwenguni…

Huo utajiri lilianza kuupata wakati wa kipindi cha giza, watu walipoambiwa watoe michango ili wafanyiwe ibada Fulani za ukombozi, ilikuwa ili mtu wabarikiwe ni lazima utoe kiasi Fulani cha fedha, ili ndugu zao wapate kuokolewa kutoka toharani lazima utoe kiasi Fulani cha fedha n.k sasa kuanzi hicho kipindi mpaka leo, limekusanya utajiri mkubwa usioelezeka. Limejenga ngome kubwa duniani kote, Ukienda leo Israeli, kila mahali utakapoingia kuanzia Goligotha mpaka Galilaya na Yerusalemu ni Taasisi za kikatoliki tu zimefurika, kama hujui jambo hilo fuatilia utaona..Tunaishi ukingoni mwa muda sana.

Hivyo huyu Mpinga-Kristo atafanikiwa mpaka kujipenyeza katika Hekalu la Mungu, kwa nguvu zake za ushawishi na za kifedha..na hivyo kuwa CHUKIZO KUBWA SANA MBELE ZA MUNGU, Hilo ndilo chukizo la Uharibifu. Lililotabiriwa na Nabii Danieli na Bwana Yesu pia kulirudia tena kuwa litasimama patakatifu.. Na Mtume Paulo pia alikuja kulitilia msisitizo tena.
2Wathesalonike 2:3 “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu;
4 yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe KUKETI KATIKA HEKALU LA MUNGU, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.
5 Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?”
Huyo mtu wa kuasi ni Mpinga-kristo, ukiendelea kusoma hiyo mistari utaona Paulo anamwelezea, hivyo huyu mpinga-kristo atajiingiza katika hekalu la Mungu, na ghafla ataanza kubadilika Tabia na kutaka kuabudiwa, na watu baadhi kutoka duniani kote wataanza kumwabudu na kumsujudia…

Sasa tukirudi kwenye lile ono ambalo Yohana anaambiwa alipime Hekalu la Mungu, utaona aliambiwa apime vitu vikuu vitatu..1) Alipime Hekalu lenyewe 2) Aipime madhabahu 3) Awapime watu wanaoabudu humo…Na behewa iliyokuwa nje aliiambiwa asiipime.

Sasa vipimo vinavyozungumziwa hapo sio vipimo vya kimwili..hapana bali ni vipimo vya kiroho, hata sasa sisi wakristo tunapimwa kuangaliwa tumesimamaje! Wale malaika wawili waliotumwa Sodoma walitumwa wakapime kiwango cha uovu na utakatifu kilichopo Sodoma na ghomora na kurudisha majibu, Ufalme wa Mfalme Belshaza ulipimwa kwenye mizani na kuonekana kuwa umepunguka n.k.

..Kadhalika hapa Yohana anaambiwa akalipime Hekalu la Mungu…maana yake akatazame mambo yanayoendelea kule katika Roho je yapo sawa kama yanavyopaswa yawe? Hiyo ndio maana ya kupima… Na pia anaambiwa apime madhabahu je! Vinavyofanyika vipo sawa? Na pia anaambiwa awapime hao wasujuduo humo? Je! Wanayemwabudu ni nani ndani ya hilo Hekalu? ni Mungu kweli wa Israeli? Na sasa tunajua ni lazima kasoro zionekane kwasababu anayeabudiwa ndani ya hilo hekalu ni Mpinga-Kristo Papa-wa-wakati huo na si Mungu..

Utaona pia alikatazwa asiipime behewa iliyo nje ya Hekalu, kumbuka behewa/ uwa wa nje ilikuwa ni sehemu ya hekalu la Mungu, ambalo watu wasio wayahudi waliompenda Yehova walimwabudia Mungu hapo, hawakuruhusiwa kufika uwa wa ndani..Lakini hapa anaambiwa hata asihangaike kuipima behewa iliyo nje ya madhabahu, kwasababu kwasasa haina kazi tena, jicho lake halipo kwao tena (yaani watu wa mataifa)..

Hii ni kuonyesha kuwa, mpaka hayo mambo yaanze, Mungu atakuwa kashamalizana na sisi watu wa Mataifa, neema itakuwa Imehamia Israeli, Hivyo kama hujatengeneza mambo yako sawa na Mungu sasa, usitazamie wakati huo kutakuwa na neema kwako..

Sasa tukirudi kwa Wayahudi ambao sasa, Mungu anawanyoa kwa vipimo vyake, na kuonekana kuwa wamepunguka, maneno haya ndio yaliyofuata…
Ufunuo 11: 3 “Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia.
4 Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi.
5 Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka katika vinywa vyao na kuwala adui zao. Na mtu akitaka kuwadhuru, hivyo ndivyo impasavyo kuuawa”.
Bwana atawanyanyua mashahidi wake wawili, watakaokuwa na Neema ya Mungu ya kipekee sana juu yao…Hawa watakuwa na kazi mbili tu! Ya kwanza ni kwenda kumfunua Yule Mpingamizi ajiinuaye nafsi yake na kutaka kuabudiwa ndani ya Hekalu la Mungu, kana kwamba yaye ndiye Mungu..Na pia watakuwa na kazi ya kuwafundisha wayahudi, Hekalu halisi ni lipi, na madhabahu ya kweli ni ipi, kuwa hekalu halisi na madhabahu halisi ni KRISTO YESU. watu hawa watakuwa ni Manabii…
Watawaambia wayahudi kuwa HUYU MTU NDANI YA HEKALU Ndiye Mpinga-Kristo mwenyewe. Ni shetani katika kiti cha enzi cha kibinadamu. Na pia watawaambia kuwa Yesu Kristo waliyemkataa miaka 2000 iliyopita ndiye Masihi mwenyewe… sasa kutokana na Ishara kubwa watakazokuwa wanafanya hawa manabii wawili, wayahudi wengi wataamini…Kumbuka kigugumizi kikubwa walichonacho wayahudi sasa ni ISHARA, siku zote huwa wanataka ishara ili waamini,tangu kipindi cha Yesu ilikuwa hivyo, na ndio maana hata leo ukienda kuwauliza ni kwanini hawamwamini Yesu Kristo, watakwambia ikiwa huyu Yesu wenu ni Masihi basi tumwone leo akifanya ishara za manabii kama vile Musa na Eliya kushusha moto n.k.
Sasa Mungu atawapa wanachokitafuta, kwa kupitia injili za manabii hawa wawili ambao wanamtukuza Kristo,
 
Ndipo watakapojua na kutubu na kulia na kuomboleza na kusema hakika tulifanya makosa kumwua mwokozi wetu, Bwana wetu mwenyewe na kumwuza kwa watu wa mataifa…macho yao yatafumbuliwa watamwombolezea yeye waliomchoma kama Biblia inavyotabiri katika Zekaria 12:10.

Wale watakaoamini ushuhuda wa manabii hawa wawili watatiwa muhuri, ambaye ni Roho Mtakatifu…Kwa maelezo juu ya hili tafadhali rejea ufunuo, mlango wa saba katika mfululizo huu wa kitabu hichi.

Na Hawa manabii wawili ndio watakaotimiza sehemu ya zile baragumu nne za kwanza,kama tulizojifunza katika Ufunuo Mlango wa 8. Watafanya ishara kama zile za Musa, alizofanya ili kuwatoa wana wa Israeli kwenye Kamba za Farao, kadhalika na hawa watafanya ishara kama zile zile, bahari kuwa damu, jua kutiwa giza lengo ni kuwatoa wana wa Israeli katika kifungo cha Mpinga-Kristo..Na pia manabii hawa watafanya ishara kama zile za Eliya kufunga mbingu mvua isinyeshe, lengo ni kuigeuza mioyo ya watu imgeukie Mungu wa Israeli, kadhalika na hawa watafunga mbingu mvua isinyeshe na kuipiga dunia kila wanapotaka ili tu kuwageuza wana wa Israeli mioyo yao imgeukie Mungu, na kama ilivyokuwa kwa Eliya mtu yeyote aliyekuja kwa lengo la kumdhuru moto ulishuka ukawateketeza, vivyo hivyo na hawa manabii wawili itakuwa ni kitu kile kile, moto utashuka kuwateketeza maadui zao, Kumbuka shughuli yote hii ya itakapotokea Kanisa litakuwa limeshakwenda kwenye unyakuo.
Ufunuo 11:16 “Hao wana amri ya kuzifunga mbingu, ili mvua isinyeshe katika siku za unabii wao. Nao wana amri juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuipiga nchi kwa kila pigo, kila watakapo.
7 Hata watakapoumaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika kuzimu atafanya vita nao, naye atawashinda na kuwaua.
8 Na mizoga yao itakuwa katika njia ya mji ule mkuu, uitwao kwa jinsi ya roho Sodoma, na Misri, tena ni hapo Bwana wao aliposulibiwa.
9 Na watu wa hao jamaa na kabila na lugha na taifa waitazama mizoga yao siku tatu u nusu, wala hawaiachi mizoga yao kuwekwa kaburini
10 Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi.
11 Na baada ya siku hizo tatu u nusu, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama.
12 Wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, Pandeni hata huku. Wakapanda mbinguni katika wingu, adui zao wakiwatazama.
13 Na katika saa ile palikuwa na tetemeko kuu la nchi, na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka; wanadamu elfu saba wakauawa katika tetemeko lile. Na waliosalia wakaingiwa na hofu, wakamtukuza Mungu wa mbingu”.
Wakati huo Papa-mpingakristo atapata jeraha kubwa sana kwa mahubiri ya hawa mashahidi wawili…na mahubiri ya hawa manabii wawili yatamwuzunisha sana na kumwumiza kichwa kama vile zile taarifa za mamajuzi zilivyomhuzunisha Herode kipindi cha kuzaliwa Bwana Yesu…tutazidi kuielewa habari hii vizuri katika sura inayofuata…lakini kwa ufupi Manabii hawa wawili watatoa unabii kwa muda wa miaka mitatu na nusu, na watakapomaliza ushuhuda wao yule mnyama atokaye baharini (Yaani mpinga-Kristo,PAPA) Atafanya vita nao, atatangaza kwenye vyombo vyote vya habari kuwa kuna baadhi ya watu wanachafua amani ya dunia, na wanakwenda kinyume na makubaliano, atatuma vyombo vya usalama viwafuatilie lakini haitasaidia, mpaka watakapomaliza ushuhuda wao, Bwana ataruhusu wauawe kama ilivyokuwa kwa Bwana alivyomaliza ushuhuda wake. Na watauawa mahali palepale Bwana wao alipouawa Yerusalemu, Golgotha..Ndio mji ambao kwa jinsi ya roho unaitwa Sodoma na Misri.

Ni Sodoma kwasababu ya mambo yatakayokuwa yanaendelea pale Yerusalemu wakati huo, na Misri kwa utumwa waliokuwa wanapitishwa katika roho na Mpinga-kristo. Na baada ya siku tatu na nusu watafufuka na kupaa juu adui zao wakiwatazama…wataingiwa na hofu kuu, na saa hiyo hiyo tetemeko kubwa la nchi litatokea na wanadamu 7,000 watakufa kwa tetemeko lile. Naam! Hata Kristo alipofufuka kulitokea tetemeko kubwa la nchi. Na wayahudi wachache watakaoiona hiyo ishara wataingiwa na hofu, na watazidi kumtukuza Mungu. Kumbuka baada ya hawa manabii wawili kuondoka ndipo Papa atavunja agano aliloingia na wayahudi na dhiki kuu kuanza kwa miaka mingine mitatu na nusu iliyosalia.

Tukiendelea na mistari unaofuata Biblia inasema…
Ufunuo 11:14 “Ole wa pili umekwisha pita, tazama ole wa tatu unakuja upesi.
15 Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele.
16 Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vya enzi vyao wakaanguka kifulifuli, wakamsujudia Mungu.
17 wakisema, Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi, uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umeutwaa uweza wako ulio mkuu, na kumiliki.
18 Na mataifa walikasirika, hasira yako nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na wa kuwapa thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu, na hao walichao jina lako, wadogo kwa wakubwa, na wa kuwaharibu hao waiharibuo nchi.
19 Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua ya mawe nyingi sana”.
Ole ya tatu ndio ole ya mwisho, na inahusu Baragumu la saba. Na baragumu hili lilipopigwa zikasikika sauti mbinguni zikisema…Ufalme wa duniani umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu Yesu Kristo, sauti hizi utaona zinatoka mbinguni na sio sauti ya mtu mmoja bali za wengi…na hao si wengine Zaidi ya watakatifu walionyakuliwa…maana hao Kristo ndio Bwana kwao. Hao ndio watakaorithi na Bwana katika Mbingu mpya na nchi mpya..ndio watakaokuwa wafalme katika nchi mpya.

Na katika Baragumu hili inaelezea SIKU YA BWANA..Siku ambayo Bwana atashuka kutoka mawinguni kuyahukumu mataifa, siku ambayo kila jicho litamwona..siku ambayo atakuja kuanza utawala mpya wa amani wa miaka 1000 hapa ulimwenguni.

Mstari wa mwisho unasema “Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake”..Tunajua kuwa mbinguni hakuna hekalu kama haya ya kiduniani…Hekalu la Mungu ni wale watakatifu walionyakuliwa…wale ndio hekalu la Mungu, Mungu anakaa katikati yao, na mbinguni pia hakuna sanduku la agano..Kwahiyo sanduku la agano hapo linafunua agano Mungu aliloingia na watu wake (Yeremia 31:33 “siku hiyo watakuwa watakuwa watu wangu na mimi nitakuwa Mungu wao”).Hivyo utakuwa ni wakati wa kufunuliwa wana wa Mungu, mbingu zitafunguka na watu wote waliosalia wa mataifa wasiokufa katika siku ya Bwana watamwona Bwana na watakatifu wake wakishuka mbinguni, waking’aa kama jua! Oo haleluya! Hao ndio hakalu la Bwana lililofunguliwa mbinguni.

Baada ya hayo kutakuwa hakuna tena muda, kama biblia inavyosema…Ufunuo 10:6 “akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya; 7 “..isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu;..”

Embu angalia mambo haya yalivyojibinja ndani ya kipindi kifupi, baragumu zote sana zitakuwa ndani ya miaka 7 tu ya mwisho, dhiki kuu, mapigo vya vitasa yote hayo ni ndani ya huo muda mfupi sana Je! Umempa Bwana Maisha yako? Je! Maisha yako yanastahili wokovu?..una uhakika Bwana akija leo utakwenda naye kwenye unyakuo?.Jibu unalo ndani ya moyo wako, ni maombi yangu, uchukue uamuzi sasa wa kumruhusu Bwana ayatawale maisha yako ndani ya hichi kipindi kifupi kilichobakia,

Neema ya Bwana iwe pamoja nawe.
 
Usikose mwendelezo huu wa sura inayofuata ya 12, bofya hapa.⏩ Ufunuo 12
 Bwana akubariki sana.

No comments:

Post a Comment