"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, July 14, 2019

USIWE SABABU YA WATU KUMKUFURU MUNGU.


2 Samweli 12:9 “Kwa nini umelidharau neno la Bwana, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni.
10 Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako.
11 Bwana asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili.
12 Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya Israeli wote na mbele ya jua.
13 Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa.
14 Lakini, KWA KUWA KWA TENDO HILI UMEWAPA ADUI ZA BWANA NAFASI KUBWA YA KUKUFURU, MTOTO ATAKAYEZALIWA KWAKO HAKIKA YAKE ATAKUFA”.
Shalom! Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.
Leo tutajifunza, madhara ya kuruhusu dhambi katika maisha yetu!..Tukijifunza kwa Daudi, ambaye Mungu alimpaka mafuta awe Mfalme juu ya Israeli, kama wengi wetu tunavyojua, alikwenda katika njia za Mungu kwa ukamilifu wote isipokuwa katika habari za Mke wa Uria.
1 Wafalme 15:5 “kwa sababu Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana, wala hakukosa katika yote aliyomwamuru, siku zote za maisha yake, isipokuwa katika habari ya Uria, Mhiti”.
Kosa la Daudi kumchukua mke wa Uria na kumwua Uria mwenyewe, ndio lililotia doa haki yake…Lilikuwa ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu, mpaka Daudi alikuwa hatiani kufa…kwasababu alistahili kufa…Lakini kwasababu pia alikuwa ni mwepese wa kujirudi na kukimbilia kutubu, Bwana alimhurumia na akaghairi kumwua, lakini hakumwacha bila adhabu.
Unajua wengi wetu tunadhani madhara ya dhambi ni kumwudhi Mungu tu basi..si zaidi ya hapo…lakini kiuhalisia madhara ya dhambi ni marefu sana, hayaishii tu kumwudhi Mungu bali yanakwenda mpaka kuathiri kazi ya Mungu.
Unaweza ukatenda sasahivi jambo, wewe ukaliona ni dogo tu! Lakini hilo jambo ulilolifanya likaenda kusababisha madhara mengine makubwa huko, ya jina la Mungu likatukanwa..kwahiyo ukawa umemletea mazao mengi shetani. Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kujiepusha na dhambi za makusudi.
Tukirudi kwa Daudi tunaona alifanya nayeye dhambi kama hiyo ya makusudi, yeye alifanya kwa siri, akijua ni dhambi ndogo, lakini mbele ya jicho la Mungu ilikuwa ni dhambi yenye kuleta madhara makubwa katika Israeli..Kwa maana kwa kitendo kile Daudi alichokifanya, watu wote ambao walikuwa wanamsifia Daudi kuwa ni Mtumishi wa Mungu mkamilifu, waliposikia kamwua mtu asiye na hatia na kumwibia mke wake, walimdharau Mungu wake,…Hayo ndiyo madhara ambayo Mungu yanamchukiza zaidi.

Ndio maana Bwana alimwambia katika ule mstari wa 14 maneno yafuatayo.. “14 Lakini, KWA KUWA KWA TENDO HILI UMEWAPA ADUI ZA BWANA NAFASI KUBWA YA KUKUFURU, MTOTO ATAKAYEZALIWA KWAKO HAKIKA YAKE ATAKUFA”.

Mtoto Yule Mungu alimwua sio kwasababu ya makosa ya huyo mtoto, ni kwasababu ya Daudi, na aliadhibiwa hivyo kwasababu ALIWAPA ADUI ZA BWANA NAFASI YA KUKUFURU.
Hivyo na sisi tunajifunza hapo, tusipime kimo cha dhambi kwa jicho la juu juu tu! Kwamba nitatenda dhambi na kutubu! Tambua kuwa dhambi za makusudi zina madhara makubwa sana, sio kwako tu bali pia katika kuidhoofisha kazi ya ufalme wa mbinguni. Kwasababu zinasababisha jina la Mungu linatukanwa.
Warumi 2:21 “basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?
22 Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?
23 Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?.
24 KWA MAANA JINA LA MUNGU LATUKANWA KATIKA MATAIFA KWA AJILI YENU, kama ilivyoandikwa”.
Hatupaswi kufanya watu wamkufuru Mungu wetu kwa tabia zetu za ubishi, mashindano, wizi, kwa uasherati, uzinzi, wizi na utukanaji na mambo mengine yote machafu, Ni heri useme wewe sio mkristo kuliko useme ni mkristo halafu mtu asiyeamini akukute unafanya hayo mambo, utakuwa umemfanya aamini kuwa Ukristo ni unafki na uongo, jambo ambalo si kweli. Utakuwa unamsulibisha Kristo mara ya pili.

Daudi alimsababishia Yule mke wa Uria uchungu mwingi, kwa kumwulia mumewe na pamoja na huyo mtoto aliyemzaa Bwana alimwua… lakini Bwana alimfariji baadaye, Mama yake Sulemani alikuwa ni huyu mke wa Uria, ingawa Daudi alikuwa na wake wengi wenye watoto wengi lakini wana wao hawakuketi mahali pa Daudi isipokuwa mwana wa huyu mke wa Uria ambaye alikuwa ni Sulemani, mfalme mkuu.

Kwahiyo tunaonywa tujichunguze mienendo yetu, na tuyajue madhara ya dhambi kuwa hayaishii tu kutuletea sisi madhara, bali pia yanaathiri kazi za Mungu za kuwavuta watu kwake.

Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment