"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Saturday, July 20, 2019

WEWE SI MALI YAKO MWENYEWE!


1 Wakorintho 6: 19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? WALA NINYI SI MALI YENU WENYEWE;”
Ukilijua Neno hili utauheshimu mwili wako, kuliko hapo kwanza. Kitu kikubwa kisichofahamika na wengi ni kuwa Miili hii tuliyonayo sio mali yetu..hatujapewa dhamana ya kuitawala asilimia 100. Kama ingekuwa ni mali yetu asilimia mia moja, tungekuwa na uwezo wa kuzisimamisha nywele zetu zisiote kwa amri zetu, tungekuwa tunaweza kuiambia mioyo yetu isimame kusukuma damu na ingetutii kama tu vile tunavyoamua kusimama au kukaa…
Kwahiyo unaweza kuona miili hii, tunamamlaka nayo sehemu ndogo sana, tena sana….huwezi kukiongoza chakula tumboni, kinajiongoza chenyewe, huwezi kuuongoza mwili wako utoe jasho unajitoa wenyewe, au kucha kukua…mwanamke hawezi kutengeneza kiumbe ndani ya tumbo lake, kiumbe kinajitengeneza chenyewe ndani kwa ndani, anajikuta tu, uchungu umemfikia na anajifungua mtoto… kadhalika hatuwezi kujifanya tukue..tangu tulipokuwa Watoto tunajikuta tu tunaongezeka kimo na ukubwa bila idhini yetu, vitu kama ini, figo,kongosho, seli zinafanya kazi pasipo hiyari zetu nk…chunguza utagundua kuwa hii miili yetu, tuna mamlaka nayo sehemu ndogo sana, karibia kila kitu kinaongozwa na nguvu nyingine..

Mamlaka tuliyopewa sisi ni uwezo wa kusogeza viungo vyetu vya nje kama miguu, mikono, macho, na uwezo wa kujisogeza kutoka sehemu moja hadi nyingine..basi hakuna kingine cha ziada...Hii yote ni kuonyesha kuwa HII MIILI SI MALI YETU NI MALI YA MWINGINE.

Ni kama tu mtu unapofungua account ya Facebook au ya Bank au anapoisajili laini ya simu…Unapofungua account ya facebook kwa mfano, account hiyo inakuwa ni ya kwako ina jina lako na password yako, kiasi kwamba hakuna mtu anayeweza kujua kinachoendelea ndani ya account hiyo, isipokuwa wewe umwonyeshe… kila kitu unaweza ukakifanya private mtu yeyote asijue unafanya nini, na unaweza kuitumia utakavyo…lakini pamoja na kwamba unao uwezo wa kuitumia utakavyo, bado kuna vitu utakuwa huwezi kufanya…kwamfano ukikiuka sheria za wamiliki wa facebook wanakunyanganya hiyo account, aidha wanakufuta kabisa au wanakublock kwa muda…na huwezi kuirudisha kwa namna yoyote ile,

Hiyo yote ni kuonyesha kwamba hiyo account si yako bali ni yao. Hata kama unauwezo wa kuweka password ngumu kiasi gani, lakini wenyewe wakitaka kujua kinachoendelea ndani ya account hiyo huwezi kuwazuia, wakitaka kukupokonya vile vile huwezi kuwazuia.
Na Zaidi ya yote, jinsi account za facebook na nyinginezo zinavyofanyiwa marekebisho, huwa mwenye account hahusiki, anajikuta tu kuna kitu Fulani kimeongezeka kipya, au kuna kitu Fulani kimeondolewa..Hiyo yote ni kuonyesha kuwa hiyo account ni ya kwako lakini bado sio ya kwako. Ni watu Fulani walikupa tu..

Na hii miili tuliyopewa ni hivyo hivyo, ni Mali ya Mungu…Si mali yetu kabisa, na ilivyowekwa hapa duniani na aliyeiweka (yaani Mungu) kaiwekea sheria na utaratibu wake, namna inavyopaswa iwe…Hakutupa kwa lengo la kuigeuza bango la matangazo, au chombo cha kuharibu wengine, au kituo cha roho nyingine chafu zinazoharibu kukaa…Mwili unaofanya hivyo utafungiwa haki ya kuishi (maana yake utakufa).

Ndio maana kuna umuhimu sana wa kuitunza hii miili tuliyopewa, na kuelewa kwa undani masomo kuhusu NAFSI, MWILI na ROHO.. kwasababu si MALI YETU WENYEWE…Ukiuchora mwili wako tattoo isingekuwa shida endapo ingekuwa ni mali yako…lakini kwasababu si mali yako ni ya mwingine usifanye hivyo, utajitafutia mabaya badala ya mazuri….Ni sawa sasahivi uanze kutumia hiyo account ya facebook vibaya, ukaanza kuitumia kuweka picha chafu na zisizofaa na kuharibu jamii, na kufanya uhalifu, wamiliki wakiligundua hilo unafungiwa mara moja na wala hutapata nafasi ya kuongea nao..kwasababu hata hawajawahi kuzungumza na wewe hapo kabla…password haimaanishi kuwa ndio umepata uhalali wa kuimiliki hiyo account asilimia 100. Kadhalika sio kwasababu unauwezo wa kusitiri siri ndani ya mwili wako kiasi kwamba hakuna mtu awezaye kujua kinachoendelea ndani mwako, na una uwezo wa kutembea kutoka sehemu moja hadi nyingine kama utakavyo, ndio iwe sababu ya kusema huo ni mwili wako…Huo sio wako ni mali ya Mungu, akiutaka anauchukua siku yoyote, na huwezi kumwuliza kwanini.

Hivyo ili tuweze kuishi ndani ya hii miili kwa muda mrefu na kwa kheri hatuna budi kuishi kwa kuzifuata sheria zake, Neno lake linasema…mwanamke avae mavazi ya kujisitiri (1 Timotheo 2:9) basi ni vizuri kutii…usiseme una uhuru juu ya mwili wako, na kuvaa utakavyo, kumbuka huo si wako…
Biblia inasema usichanje chale wala usichore alama (tattoo) katika mwili wako ni machukizo, basi usijifanye wewe ni mgunduzi wa huo mwili, yupo mwenye huo mwili ambaye akiutaka anao uwezo wa kuutahifisha muda wowote.
Walawi 19: 28 “Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana”.
Biblia inasema uashareti hata usitamkwe kamwe kwenu (Waefeso 5:3)…Usiseme mwili wangu, nina uhuru wa kufanya nitakalo, Hivyo Mungu hawezi kunihukumu kwa kitu ambacho ni mali yangu…Ndugu huo sio mali yako, ingekuwa hii miili ni mali yetu katupa moja kwa moja, wala asingetusumbua kutuwekea sheria sheria,… tungekuwa na uhuru wa kila mtu kufanya atakalo…mtu angeamua kujirefusha kuwa kama mlingoti, ni sawa, mwingine angetaka kujifanya kuwa tembo pia ni sawa…lakini kwasababu ni mali yake, wote anatuweka kwenye kimo Fulani karibia kinachofanana na maumbile yanayofanana, kutimiza kusudi lake yeye na si la kwetu…Kwahiyo Uasherati ni moja ya dhambi mbaya sana ambayo inaweza kusababisha kifo cha ghafla kuliko dhambi nyingine zote..
1 Wakorintho 6: 18 “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe”.
Na dhambi nyingine ambazo ni mbaya zinazopelekea kuharibu mwili ni Ulevi, uvutaji sigara, matumizi ya madawa ya kulevya na matumizi ya vipodozi na utoboaji mwili.

Kama uliyafanya hayo pasipo kujua, na ulikuwa hujui kuwa mwili huo ulionao sio mali yako, basi hii ndio nafasi yako ya kutubu, unatubu na kumwambia Bwana hutaki tena hayo mambo na hivyo unataka kutimiza kusudi lake alilolikusudia juu ya mwili wako, baada ya kutubu katafute ubatizo sahihi popote pale, kama hujafanya hivyo, ubatizo sahihi ni wa umuhimu kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako (Matendo 2:38) na ubatizo sahihi ni wa kuzama mwili wote katika maji na kwa jina la Yesu, na baada ya hapo Bwana mwenyewe atakupa Roho Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya Biblia. Hakuna mtu awezaye kushinda dhambi kwa nguvu zake mwenyewe, wote tunamtegemea Roho Mtakatifu kutuwezesha, hivyo Roho Mtakatifu ni wa muhimu sana baada tu ya kumwamini na kubatizwa, maana yeye ndio Muhuri wa Mungu (Waefeso 4:30)

Bwana akubariki.

No comments:

Post a Comment