"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Sunday, May 26, 2019

MBINGUNI YUPO NANI SASA?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze Biblia, ambapo leo tutajifunza kwa ufupi juu ya upeo wa kimbinguni.

Mungu alipomuumba mwanadamu, alimwumba na vitu vitatu NAFSI, MWILI na ROHO…kwasababu Mungu naye ndio yupo hivyo hivyo, anayo nafsi, mwili na Roho, maana alituumba kwa mfano wake…Nafsi yake ndio yeye mwenyewe, roho yake ndio Roho Mtakatifu, na mwili wake ndio ule Uliokuwepo Pale Kalvari, ukafufuka na kupaa mbinguni…Kwahiyo uhai uliokuwa ndani ya Mwili unaoitwa Yesu ndio Mungu mwenyewe(nafsi yake) ukisoma Wabrania 1:3 utaliona hilo…Na Roho iliyokuwepo ndani ya ule mwili wa Yesu ndiye Roho Mtakatifu mwenyewe. Hilo linatuthibitishia kuwa Mungu ni mmoja, na nafsi yake ni moja na Roho yake ni moja, na mwili wake ni mmoja.
1 Timotheo 3:16 “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu”.
Huyo ni Bwana Yesu anazungumziwa hapo, Mungu katika mwili,aliyehubiriwa katika mataifa na akapaa juu mbinguni…kwasababu hakuna mwingine aliyepaa Mbinguni mpaka kwenye kiti cha enzi zaidi yake yeye..
Yohana 3:13 “Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu”.
Utauliza mbona Biblia inasema Nabii Eliya na Henoko walipaa na kuchukuliwa mbinguni…Ndugu Nabii Eliya hakupelekwa mbinguni Bwana alipo sasa, bali alipelekwa mahali panapoitwa Peponi (paradiso), ndio maana sehemu nyingine biblia inasema Henoko alihamishwa, sio alipaa (Waebrania 11:5)….wakati mwingine biblia inapataja paradiso kama mbinguni, kwasababu ya uzuri uliopo huko…Lakini hao watu hawakupelekwa mbinguni Bwana aliko sasa, kule hakuna mwanadamu ambaye ameshafika, ni makao mapya yanaandaliwa kule kwa watu wote waliookolewa kufika siku moja kwa pamoja…hakuna mwanadamu aliyetutangulia kufika kule…Ni Bwana Yesu tu! Peke yake ndio yupo kule akituandalia makao na malaika watakatifu..Sasa kama Eliya kashafika huko kutakuwaje tena… “sehemu ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia”? unaona?.
Utauliza tena, na hao wanaoona maono wakipelekwa mbinguni, ina maana maono yao ni batili?..Wengi wa wanaosema wamepelekwa mbinguni kiuhalisia hawajapelekwa mbinguni kwasababu huko hakuna mtu ambaye ameshafika…wanachokiona ni Maono ya mbinguni…Bwana anawaonyesha maono ya jinsi mbinguni kunavyofanana fanana, lakini sio kwamba wamefika,..Sasa Bwana anaweza kuwapa maono ambayo wakati mwingine ni dhahiri kabisa mtu anaweza akahisi yupo mahali pengine katika mwili kabisa…lakini yakawa ni maono tu sio sehemu halisi…

Hata katika namna za kawaida mtu anaweza kuota ndoto ambayo ni kama dhahiri kabisa, katika ndoto akahisi kabisa vile vitu kama vile haoti, akasikia harufu, akachoka, akahisi baridi ndani ya ndoto, akahisi jua linampiga, akahisi njaa,wakati mwingine akahisi mpaka maumivu katika ndoto, Lakini si kweli kwamba huyo mtu saa hiyo yupo katika huo ulimwengu…Hizo zinaitwa njozi. Na ndivyo Bwana anavyozungumza na watu, anaweza kuwapa watu wake maono kama vile wapo Mbinguni kabisa, wakaona pengine barabara za dhahabu, au almasi, wakaona bustani nzuri, wakaona Malaika watakatifu, wakaona uzuri usioelezeka wa huko, hisia ambazo wanaweza wakadhani ni kweli wamefika kule..Hapana kule hawajafika isipokuwa wamepewa tu maono ya kule.

Lengo la Bwana kuwaonyesha vile ni kutaka kuwaonjesha watu wake uzuri watakaokwenda kukutana nao kule, na wawafikishie wengine ujumbe. Na Bwana anaweza kumpa mtu yeyote maono hayo. Sasa ukikosa maarifa ya kuyaelewa haya, unaweza ukajipiga kifua mbele na kufikiri kwamba umeshawahi kufika mbinguni kabla ya wengine…Mambo yaliyopo kule wala hatuwezi kuyafikiria wala kuyastahimili katika hii miili yetu na akili zetu, mpaka tubadilishwe ndipo tutakapoweza kuyaelezea.

Na maono haya Bwana anayowapa watu, yanatofautiana mwingine ataonyeshwa hivi mwingine vile…mwingine kwenye maono hayo ataonyeshwa barabara za dhahabu, mwingine almasi, mwingine marumaru, mwingine ataonyeshwa makasri, mwingine mahekalu, mwingine ataonyeshwa tunu za kipekee, mwingine ataonyweshwa malaika wamevaa kanzu nyeupe wameshikilia upanga, mwingine ataonyeshwa wamevaa nyeupe zenye mshipi wa dhahabu na wameshikilia matarumbeta, mwingine ataonyeshwa wamevaa blue n.k Nk kwa jinsi Bwana atakavyopenda kumwonesha mtu. Ndio maana utaona kila mmoja anakuja na ushuhuda wake tofauti na mwingine wa mambo aliyoyaona…

Sasa kama wangekuwa wamepelekwa mahali halisi, wasingekuja kila mmoja na ushuhuda wake? Unaona? Wote wangekuja na ushuhuda unaofanana…Lakini kwasababu ni maono, maono hayawezi kufanana…ndio maana utaona Hata kwenye Biblia Yohana wa Patmo alipewa maono yenye maudhui sawa na yale ya Nabii Danieli lakini yalikuwa hayafanani…utaona Danieli anaonyeshwa wanyama wanne wanatoka baharini, mmoja alikuwa mfano wa simba, mwingine chui, mwingine Dubu na mwingine kiumbe kisichojulikana (Danieli 7:3-7)…Lakini Yohana anaonyeshwa mnyama mmoja akitoka baharini aliye mfano wa chui, miguu yake kama ya dubu na kinywa kama kinywa cha simba..(Ufunuo 13:2). Sasa alichoonyeshwa Yohana wa Patmo na Danieli ni kitu kimoja isipokuwa katika maono tofauti..ndio maana utaona kuna utofauti kidogo huyu kaonyeshwa wanyama wanne, lakini huyu kaonyeshwa mnyama mmoja mwenye maumbile ya wanyama wote wanne.

Utaona tena jambo hilo katika Kitabu cha Ezekieli, yeye alionyeshwa makerubi wana nyuso nne kila upande, uso wa mwanadamu, tai, Ndama, pamoja na simba, yaani kerubi mmoja ana nyuso nne..kwenye maono ndivyo alivyoonyeshwa..

Ezekieli 1: 5 “Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu.
6 Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne.
7 Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana.
8 Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi;
9 mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele.
10 Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng'ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia”.
Lakini Yohana wa Patmo yeye alionyeshwa Kila Kerubi na uso mmoja, yupo aliyekuwa na uso wa Tai, mwingine Uso wa Ndama, mwingine wa Mwanadamu na mwingine wa Simba, lakini hakuoneshwa kuwa kerubi mmoja ana nyuso nne kama alivyooneshwa Nabii Ezekieli.

Ufunuo 4: 6 “Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma.
7 Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye.
8 Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja”.

Sasa Yohana na Ezekieli sio kwamba wameonyeshwa vitu tofauti, hapana..ni kitu kimoja isipokuwa katika maono mawili tofauti.

Kwahiyo Mbinguni hakuna aliyefika sasa, ni sehemu mpya Bwana anayowaandalia watu wake, na watakaofika ni wale tu waliooshwa dhambi zao kwa damu yake, yaani wale waliomwamini yeye na kutubu na kubatizwa, na kuishi maisha ya utakatifu (Waebr 12:14)..Wapendwa wetu waliokufa katika Kristo sasa wapo mahali pa mangojeo panapoitwa Paradiso au peponi (Ni mahali wamehifadhiwa pa raha sana, lakini ni pa muda tu, wakingoja siku ile ifike)..Na sisi tutakapokufa kabla ile siku haijafika tutakwenda kuungana nao kule, ni sehemu nzuri sana, wote tutakuwa tunaingoja ile siku kwa pamoja.

Biblia inasema siku ile itakapofika wafu wote (yaani wale waliokufa katika haki, waliohifadhiwa paradiso sehemu ya raha na mangojeo)..watafufuka (yaani watarudi katika miili hii ya asili kwanza)..na watakatifu walio hai watawaona na kuungana nao, na kwa pamoja kufumba na kufumbua tutabadilishwa miili yetu na kuvaa ya miili ya utukufu..itakayoweza kustahimili hayo mambo mazuri na mapya tutakayokwenda kuyakuta huko juu…Na ghafla tutavutwa juu mbali sana na hii ardhi (Itakuwa ni shangwe kubwa sana siku hiyo) tutaiingia mbingu ya mbingu....(na mambo tutakayoyakuta huko hakuna awezaye kuyasimulia kwasababu hakuna mtu alishawahi kufika huko kabla)…Lakini kwa walio nje ya Kristo itakuwa ni kilio na kusaga meno na maombolezo makubwa…

Siku ya mwisho yaja! Maran atha maana yake “BWANA WETU ANAKUJA” Na watakatifu waliopo paradiso wanaitamani hiyo siku ifike haraka…siku ya kufutwa machozi yao, na taabu zao na kuingizwa katika umilele.
Ufunuo 22: 20 “Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu”.
Mpe Kristo maisha yako leo, ili uwe na uhakika wa kuwepo miongoni mwa watakaokwenda kuyaona mambo mazuri Bwana aliyowaandalia watu wake..

Bwana akubariki sana.

1 comment:

  1. Maono kuwa tofauti kimwonekano huku yakidhihirisha kitu au yakielezea kitu kile kile bila kukosea siyo issue ni sahihi kibaya manabii wa leo ni waongo kila mmoja anaoneshwa vitu tofauti mfn huyu anasema maua ya mbinguni hayachumiki huyu ati yanachumika tumwamini nani?? Hao wote ni manabii wa uongo tusitiane moyo kwa mambo yasiyo na maana
    Manabii wengi utawatambua tu mfano isaya 8:20

    ReplyDelete