"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, November 19, 2018

FAHAMU KINACHOMGHARIMU MUNGU, KUTOA URITHI WAKE.

Kamusi inatoa tafsiri ya neno “KURITHI” kwamba ni kitendo cha kupokea mali baada ya kifo cha mmiliki wa mali hiyo. Hii ikiwa na maana kuwa mali inapopaswa kurithishwa haiwezi kutoka mikononi mwa mrithishaji mpaka siku atakapokufa mwenyewe. Hivyo yule atakayerithishwa siku zote hapaswi kujimilikisha mali zile hata kama atakuwa anazihudimia kwa kiasi gani, mpaka siku atakapokufa mmiliki mwenyewe ndipo ziwe zake moja kwa moja kihalali.

Na ni lazima pia mrithishaji na mrithishwaji wawe na mahusiano ya kibinafsi na ya kipekee na kama hiyo haitoshi, ni lazima pia waingie katika makubaliano ya kimaagano au ya ki-waraka ili kutambulisha kuwa walidhiana katika mapatano hayo. Haiwezekani mtu kutokea siku ya kifo na kudai urithi kama mmojawapo wa warithishwaji angali hakuwa na mahusiano yoyote na mwenye mali au makubaliano.

Biblia nayo inakubaliana na tafsiri hiyo,Tukisoma:
Waebrania 9:16 “Maana agano la urithi lilipo, lazima IWEPO MAUTI YAKE ALIYELIFANYA.
17 Kwa maana agano la urithi lina nguvu palipotukia kufa kwa mtu; kwa kuwa halina nguvu kabisa, akiwa yu hai yeye aliyelifanya”.
Unaona hapo?. Ni kwanini KIFO kitokee? Ni kwasababu moja tu ili kwamba ile mali iwe ni milki halali ya yule mrithishwaji MILELE. Kwasababu kifo kisipokuwepo inaweza kutokea siku moja pengine yule aliye hai akadai tena mali zake, na kugeuka kuwa sio urithi tena..

Kwasababu sheria moja ya urithi ni lazima uwe ni wa milele.. Na kifo tu pekee ndio kinaweza kuleta hilo jambo. Hivyo tunaweza kusema nguvu ya urithi ni KIFO.

Hayo mambo yanafunua nini rohoni? Kumbuka Mungu alitoa ahadi kuu za urithi kwa watoto wake juu ya nchi aliyowaandalia itakayokuja huko mbeleni. Na tunafahamu kuwa mbingu hizi na dunia hii ni mali ya Mungu sasa?, milima, sayari, nyota, mito , habari mabara n.k vyote hivi ni mali yake.


(Kutoka 19:5).Na mwanadamu aliwekwa ndani yake pale Edeni lakini kwa kutokutii kwake akamruhusu shetani ainyakue mikononi kwake, mpaka kupelekea kuingia katika matatizo tuliyonayo sasa hivyo ikamgharimu Mungu amtume mwanawe mpendwa Yesu Kristo ili aje kuukomboa tena ulimwengu uliokuwa umepotea. Na tunafahamu kuwa ushindi huo ulipatikana pale Kalvari miaka 2000 iliyopita hapo ndipo umiliki wa mbingu hizi na nchi hizi ziliporudi tena kwa Mungu baba kwa kupitia YESU mwokozi wetu.

Hivyo, vitu vyote vilivyopo ulimwenguni sasa vinamilikiwa na YESU KRISTO mwenyewe, isipokuwa huu mfumo wa utawala mbovu wa shetani unaoiharibu dunia sasa kwa kitambo ndio upo mikononi mwa shetani. Lakini kwa kuwa YESU ni mshindi alishapanga siku ya maangamizi ya vitu vyote ili kuitengeneza upya dunia na kuifanya kuwa bustani ya Mungu yenye makao mazuri yasiyoneneka. Matengenezo hayo yataanza katika ule utawala wa miaka 1000, ambapo kila kitu kiovu kitasafishwa na YESU KRISTO atakapokuja kutawala na watakatifu wake hapa duniani.

Sasa hapo ndipo Mungu atakapoutoa ule urithi alioutunza kwa ajili ya watoto wake ambao tangu zamani aliundaa kwa ajili yao, urithi ambao Ibrahimu aliuona tokea mbali ukamfanya mpaka aishi kama mpitaji hapa duniani.
Waebrania 11:8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.
9 Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.
10 MAANA ALIKUWA AKIUTAZAMIA MJI WENYE MISINGI, AMBAO MWENYE KUUBUNI NA KUUJENGA NI MUNGU.
Unaona hapo Yatafakari maneno hayo vizuri “10 MAANA ALIKUWA AKIUTAZAMIA MJI WENYE MISINGI, AMBAO MWENYE KUUBUNI NA KUUJENGA NI MUNGU.

kama biblia inavyosema katika Mathayo 5: 5 “Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi”.

Ndugu Ipo nchi tutakayokuja kuirithi sisi watoto wa Mungu baada ya utawala huu mbovu wa shetani kuharibiwa kabisa hapo dunia itakapofanywa kuwa upya tena wakati huo ndipo urithi wetu utaachiliwa. Hapo ndio kila mtoto wa Mungu ambaye alijiona kuwa yeye si kitu alipokuwa duniani, aliyejinyima nafsi yake na mambo ya ulimwengu mpaka kuonekana kama ni takataka ya dunia sasa kwa mambo ambayo atakutana nayo huko katika siku hizo, hata kumbuka tena taabu yake aliyoipitia, biblia inasema kama vile mwanamke aliyetoka kujifungua anavyosahau uchungu aliopitia baada ya kuona kiumbe kipya kuja duniani.Ndivyo itakavyokuwa kwa watoto wa Mungu siku ile.
1Petro 1:3 “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;
4 TUPATE NA URITHI USIOHARIBIKA, USIO NA UCHAFU, USIONYAUKA, ULIOTUNZWA MBINGUNI KWA AJILI YENU.”
Sasa swali linakuja je! ili Mungu atupe huo urithi wa mbingu mpya na nchi mpya, ambao ametuahidia inampasa na yeye afe ili tuwe na umiliki halali wa urithi huo milele?

Jibu ni hapana, kama tunavyojua kuwa Mungu anaishi milele, hafi, sasa kitakachofanyika ni kuwa MUNGU ATAKUFA KWA HABARI YA UMILIKI WA NCHI HIYO INAYOKUJA, ikiwa na maana kuwa dunia ijayo itakuwa ni MILKI HALILI YA MWANADAMU MILELE.. Yaani mwanadamu atakuwa na maamuzi ya kufanya jambo lolote katika nchi hiyo aliyoandaliwa na Mungu.. Unajua kwasasa huwezi kufanya lolote kwasababu dunia hii ni mali ya Mungu, embu jaribu kufikiria mfano ingekuwa ni mali yako, ungeamua kufanya nini?. Unaona ni kama jambo ambalo haliwezekani lakini itakuwa hivyo.

Mungu wakaandalia watakatifu wake urithi wa milele, siku hiyo Mungu hatawauliza chochote juu ya urithi huo, kana kwamba sio yeye aliyeiumba dunia bali wao..

Jambo pekee litakalofanyika ni kwamba tutamjua yeye katika viwango vingine, Tutamwabudu Mungu katika viwango vingine , mbali ni hivi tunavyovijua mbali na masuala ya mbingu na nchi, mambo ambayo kwasasa hatuwezi kuyastahimili mpaka tutakapofika kule kwanza…siku hizo hatutamwabudu yeye kama tunavyomwabudu sasa, Huko tutakapomjua Mungu kwa mapana na marefu, huko ndiko tutakapomjua Mungu kuwa ni zaidi ya mbingu na nchi, na vitu tunavyoviona Haleluya!.

Ni vizuri tukiyafahamu hayo, ili kusudi kwamba mambo ya ulimwengu huu mabovu ya kitambo tuyaonapo tuone kuwa ni takataka tukifananisha na urithi usioharibika Mungu aliotuandalia huko mbeleni na ndio maana biblia ilikazia sana kusema maneno haya:

Waefeso 1.18 macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; NA UTAJIRI WA UTUKUFU WA URITHI WAKE KATIKA WATAKATIFU JINSI ULIVYO;.


Pia Kumbuka biblia inaposema mbingu mpya na nchi mpya, inamaanisha jambo zaidi ya hii sayari yetu inayojulikana kama dunia..Inamaanisha kuwa ni pamoja na sayari zote, na nyota zote na magimba yote yaliyopo angani. Yote yatakuwa ni makao na urithi Mungu aliwaandalia wanadamu watakatifu.

Sayari hii yetu ni kama makao makuu tu, wanasayansi wanafanya utafiti wa kupata uwezekano wa makazi mapya ya wanadamu katika sayari nyingine, na kweli wameziona lakini hawawezi kuzifikia, kwasababu ni mbali na upeo wa kibinadamu kufika huko. Wanachunguza chunguza uwezekano wa kuishi katika sayari zilizo kando kando ya dunia lakini bado hawataweza kwasababu huo sio urithi wao. Huo ni urithi wa wana wa Mungu Bwana aliowaandalia wale wazishikao amri zake.
Ayubu 9: 7 “Aliamuruye jua, nalo halichomozi; Nazo nyota huzipiga muhuri”.Na pia inasema..
Zaburi 147: 4 “Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina”.
Kitu kikishapewa jina na Mungu mwenyewe inamaanisha kuwa kitu hichi kina uhai, na pia kinakaliwa. Sasa kama nyota zote kazipa majina na kazipiga muhuri itafika wakati kama ilivyokuwa pale mwanzo Nchi ilikuwa ukiwa lakini Roho wa Mungu alipotujua juu ya dunia hii , pakawa mahali pa kukaliwa na watu. Ndivyo itakavyokuwa kwa sayari nyingine na magimba mengine yaliyopo angani.
  

Ili kusudi kwamba Mungu awe wa milele na asiyeisha, ni lazima awe na urithi ambao kuisha kwake unahitaji umilele. dunia pekee hii haitaweza kustahimili umilele, kwani kuna wakati itafika tutajua kila kitu kilichopo duniani.

Na ndio maana pale anasema macho ya mioyo yetu yatiwe nuru ili tujue utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;…Zingatia hilo neno UTAJIRI WA UTUKUFU WA URITHI WAKE.. yaani utukufu wa urithi wake una TAJIRI usiopunguka..

Hayo ni machache tu yapo mambo mengi yahusuyo urithi Mungu aliowaandalia watoto wake. Leo hii watu wanajiona kuwa hii dunia ni ya kwao japo si ya kwao, wanajiona kuwa wanaweza kufanya kila kitu, wanajiona kuwa wapo huru kana kwamba hakuna anayewamiliki.. Sasa kama wao kwasasa wanajiona hivyo na hawajijui kuwa wanamilikiwa pasipo wao kujijua kwasababu hii nchi hawajarithishwa wao. Itakuwaje siku hiyo pale Mungu atakapomaliza kuitengeneza upya hii dunia na kuwapa watoto wake..

WATAKUWA HURU KIASI GANI?..NI ZAIDI YA UHURU unaweza kuudhani. Kwa Mungu hakuna utumwa.

Lakini leo hii tusipoyaona hayo na kuupenda huu ulimwengu uliojaa utumwa wa kila namna, ulimwengu wa kitambo, ambao mwisho wake upo karibu, hatutaki kutazama mambo ya milele yanayodumu, tunapuuzia wokovu, tunadhani kuwa Mungu ni mtu wa kando wa sisi kujiamulia mambo tu, kana kwamba tusipompokea yeye kuna kitu anapungukiwa…Hapana ndugu siku ile tutajuta pale tutakapoona tumekosa urithi huo ulio bora, na wenzetu wanaingia katika raha ya milele na sisi tunaenda katika ziwa la moto.

Siku ile ya hukumu Bwana atakapotenga mbuzi na kondoo, kondoo wake wakiwa upande wake wa kiume na mbuzi (waovu) wakiwa upande wa kushoto atawaambia maneno haya:

Mathayo 25:34 “Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, URITHINI UFALME MLIOWEKEWA TAYARI TANGU KUUMBWA ULIMWENGU;”

Unaona? Wataurithi ufalme Mungu aliwaandalia tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.Lakini waliosalia wote sehemu yao itakuwa katika lile ziwa la moto. Kama biblia inavyoeleza katika..

1Wakorintho 6:9 "Au hamjui ya kuwa wadhalimu HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,
10 wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi."


Hivyo tuyachunguze maisha yetu leo kama je! kweli tunastahili kupewa urithi huo? Je! tumeshaingia katika agano hilo la kufanyika kuwa warithi wa Baba yetu wa mbinguni?. Kumbuka Agano hilo halifanyiki nje ya Damu ya YESU Kristo. Ikiwa bado haujaokolewa fanya hivyo sasa maadamu neema ipo, uoshwe dhambi zako kwa kutubu na kubatizwa katika ubatizo uliosahihi wa maji mengi katika jina la YESU ili upate ondoleo la dhambi zako. Na ikiwa bado unasua sua njia panda upo vuguvugu ni wakati sasa wa kufanya imara wito wako na uteule wako. Ili urithi huo usikupite.

Bwana akubariki.

Tafadhali Washirikishe wengine habari njema za Yesu Kristo, popote pale ulipo.

No comments:

Post a Comment