"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, June 29, 2018

UFUNUO: Mlango wa 4

Shalom! Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo tukiendelea na ile sura ya 4, tulishakwisha kuona katika sura zilizotangulia jinsi Mungu alivyotembea katika yale makanisa 7 yaliyokuwa Asia ndogo, yaliyowakilisha makanisa 7 katika nyakati saba tofauti tofauti kuanzia wakati wa Pentekoste hadi wakati wa kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo mara ya pili, na tuliona pia sisi tunaishi katika kanisa la mwisho, linalojulikana kama Laodikia, na kwamba baada ya hili hakutakuwa na kanisa lingine la nane, kadhalika pia kila kanisa lilikuwa na mjumbe wake, na kanisa hili la mwisho mjumbe wake alikuwa ni Ndugu.William Branham ndiye Mungu aliyemnyanyua kubeba ujumbe wa nuru ya wakati huu wa mwisho. Hivyo ukiwa haujapitia sura zilizotangulia ni vizuri ukazipitia kwanza , ili tuende pamoja.

Sasa katika sura hii ya nne tunasoma..

"1 Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo".
 
Hapa tunaona Mtume Yohana ambaye anamwakilisha bibi-arusi wa Kristo (Kanisa), akisikia sauti ambayo ndio ile iliyokuwa inazungumza naye hapo kwanza kutoka mbinguni, na sauti hiyo sio ya mwingine zaidi ya sauti ya Bwana wetu YESU, ikimwambia "Panda hata huku nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo ". Unaona hapo kabla Yohana hajajua lolote mlango ulimfungukia kwanza mbinguni, ikimaanisha kuwa hakuna mtu yeyote atakayeweza kupokea ufunuo wowote ule wa Roho kama mlango wa mbinguni haujamfungukia,.Kanisa/mtu ni lazima awe wa rohoni kwanza ndipo liweze kuelewa mambo ya mbinguni, vinginevyo halitaweza kuyaona yaliyo juu likitegemea mifumo au mapokeo ya kibinadamu peke yake.

Na tunasoma pia ile sauti ikamwambia "Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi KUWAKO BAADA YA HAYO". Ikiwa na maana kuwa, yale maono aliyoonyeshwa kwanza, kama tulivyotangulia kusoma huko nyuma, Yohana alivyomwona YESU KRISTO katika ule mwonekano mwingine, mwenye uso kama jua, macho kama miale ya moto, miguu kama ya shaba n.k. alimwona akitembea katika vile vinara saba, pamoja na nyota saba katika mkono wake, n.k. haya yote yalifunga sehemu ya kwanza ya maono...Na sasa hapa anafungua sehemu ya pili ya maono mengine ambayo yatakuwa pia ni msingi wa mambo mengine tutakayokuja kuyaona huko mbeleni yahusuyo mihuri saba, kama tu vile yale maono ya kwanza yalivyokuwa msingi wa kufahamu tabia za makanisa saba. Na ndio maana hapo anasema " Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo. "..Hivyo ni muhimu kuyazingatia haya maono pia kwasababu tusipoyaelewa hapa mwanzoni basi sehemu zinazofuata za kitabu cha Ufunuo zitakuwa ni ngumu kuelewa,..

Tuliona kila kitu Yohana alichoonyeshwa katika lile ono la kwanza linalohusu mwili, tabia na mwonekano wa Kristo(Ufunuo 1) vilikuwa na maana kubwa katika yale makanisa 7 yaliyofuata(Ufunuo 2&3), Kwamfano ile miguu ya shaba ilikuwa na sehemu yake katika ujumbe wa kanisa husika, kadhalika na yale macho kama mwali wa moto, na ule upanga utokao kinywani mwake, na vile vinara saba na zile nyota saba zilizokuwa mkononi mwake n.k. yote haya tuliona jinsi yalivyokuwa na mahusiano makubwa sana katika kuelezea nyakati saba za kanisa..Vivyo hivyo na hapa pia katika hii sehemu ya pili ya maono, ambayo Yohana aliitwa juu kuonyeshwa mambo mengine tofauti na aliyoyaona hapo kwanza..Tusome;

Ufunuo 4:2 “Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti;
3 na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi.
4 Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu.
5 Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.
6 Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma.
7 Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye.
8 Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.
9 Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele,
10 ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema,
11 Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa”.

Mstari wa pili unasema.."2 Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti;
3 na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi".

Hapa Yohana anaonyeshwa kiti cha Enzi na "MMOJA" Kumbuka sio watatu, ameketi katika Kiti hicho, na anaonekana pia mithili ya jiwe la yaspi na akiki,. Sasa kumbuka mawe haya kwa wakati wa agano la kale yalikuwa ni mawe yenye uzuri wa kipekee na ya thamani kubwa sana,yalitumiwa na makuhani katika kifuko cha kifuani (Kutoka 28:15), ni mawe 12 yaliyotumika kama Urimu na thimimu na mojawapo ya hayo mawe ndio Yaspi na akiki, Hivyo hapo mawe hayo yanafunua UZURI wa Mungu, na thamani ya Uzuri wake kwetu sisi wanadamu pia Yohana aliona kile kiti kimezungukwa na upinde wa mvua ikifunua rehema na neema za Mungu pamoja na uthabiti wa maagano yake, Kumbuka baada ya Gharika Mungu kwa rehema zake aliuweka ule upinde wa mvua kama Ishara ya kughahiri hasira yake itakapokuja kutokana na maovu ya watu.


Tukiendelea tunaona pia, Yohana alionyeshwa wazee 24 wamekizunguka kile kiti cha Enzi, wamevikwa mavazi meupe na juu ya vichwa vyao walikuwa na mataji ya dhahabu, pamoja na taa 7 mbele ya kile kiti cha enzi ambazo ndio Roho 7 za Mungu, Kadhalika pia alionyeshwa wale wenye uhai 4 wamekizungu kiti cha enzi wote kwa pamoja wakimpa Mungu utukufu
Kwahiyo Mungu alikuwa anamuonyesha Yohana, mahali kiti chake cha enzi kilipo,kwamba ni lazima kiwe kimezungukwa na wale wazee 24, pili kiwe kimezungukwa pia na wale wenye uhai 4 Na tatu kiwe na Taa saba mbele yake...Hapo kiti cha enzi cha Mungu kimekamilika..hakuonyeshwa kama kimezungukwa na miji au makasri na magorofa ya dhahabu hapana.
 
Sasa huyu aliyeketi katika kiti cha enzi ni nani?
 
Kwa maelezo yake marefu tutakuja kumuona vizuri katika sura inayofuata ya tano.
 
Lakini sasa tuwatazame wale wazee 24 ni akina nani?.
 
Kwanza ni vizuri kufahamu mbinguni hakuna wazee 24, walioketi kando kando ya Mungu hapana, kumbuka yale ni maono, na wale wazee 24 ni ROHO 24 za Mungu zinazotengeneza ufalme wake katikati ya wanadamu, na ndio maana zimechukua taswira ya mwanadamu. Sasa hizo roho 24 ziliachiwa ulimwenguni kulitengeneza taifa la Mungu katikati ya wanadamu,.Na tunafahamu kuwa ufalme wa Mungu(KANISA) umeundwa na mataifa mawili,nayo ni Wayahudi na Wakristo.

Hivyo mwanzo kabisa Bwana alipoanza kuunda ufalme wake alianza na taifa la mwilini (yaani Israeli), na tunajua taifa la Israeli limegawanyika katika makabila 12, Mungu aliruhusu hivyo makusudi ili kulitengeneza taifa lake. Hivyo Bwana aliachia hizi roho 12 za kwanza kukaa juu ya kila kabisa ili kulijenga taifa la Israeli ambalo ni sehemu moja ya ufalme wake. Ndipo hizi roho zikaanzia kwa wana 12 wa Yakobo na kuendelea.

Lakini baadaye Mungu alipokusudia kuunda sehemu ya pili ya ufalme wake, ndipo akawajia watu wa mataifa (sisi), hivyo kama tu alivyoanza na misingi 12 katika taifa la Israeli kadhalika na huku pia alianza na misingi 12, kujenga sehemu ya pili ya ufalme wake, hivyo akaachia Roho nyingine 12 zilizokuja kukaa juu ya wale mitume 12 wa Bwana Yesu. 
 
Wefeso 2: 20 " Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni". 
 
Ile injili tuliyoipokea sisi kwa mikono ya mitume wa Bwana ndio imekuwa chachu mpaka leo hii ukristo umeenea duniani kote, Hizo ndio zile Roho 12 nyingine zilizoifanya hiyo kazi, kwahiyo kwa ujumla watakatifu wote wa agano la kale na wa agano jipya ndio wanaokizunguka kiti cha enzi cha Mungu katika roho, ndio wale wazee 24...Na ndio maana utaona wamevikwa mavazi meupe kuashiria usafi na weupe wa watakatifu na mataji kuashiria mamlaka ya kifalme kwa ushindi waupatao kutoka kwa yule adui.

Kadhalika na wale wenye uhai wanne, ni Roho nne za Mungu zinazowakilishwa na tabia za wale wanyama wanne. Utaona pia walikuwa wamejaa macho mbele na nyuma, ikiashiria kuwa wapo kwa kazi ya ulinzi, wanaona vitu vitakavyokuja kabla hata havijawasili, wanaona mambo yaliyopita na yanayokuja.
 
Kwamfano mwenye uhai wa kwanza alionekana akiwa na mfano wa simba, inamaanisha kuwa ni Roho ya Mungu iliyokuwa ikililinda (Kanisa la Mungu), kwa wakati husikia ikijifunua kama tabia ya Simba. Tunajua simba siku zote sio mwoga, ni jasiri, hivyo tutakuja kuona huko mbeleni ni wakati gani hii Roho ilijidhihirisha hivyo katikati ya watu wa Mungu.Kadhalika na yule mwenye uso kama wa ndama, na yule mwenye uso mfano wa Tai arukaye n.k. wote hawa wanabeba tabia fulani inayoendana na maumbile yao..hizi roho zimechukua mfano wa malaika zina mabawa na kupaa tofauti na wale wazee 24, zenyewe zilikuja kwa mfano wa wanadamu,..

Kadhalika tunaona pia Taa saba za moto mbele ya kile kiti cha enzi. Hizo ni roho saba za Mungu, ambazo tulishakwisha kuziona zenyewe kwenye sura zilizotangulia zikitembea katika yale makanisa saba ya Mungu.

Kwahiyo kwa ujumla katikati ya vitu hivyo vyote ndipo kiti cha enzi cha Mungu kilipo, yaani ndani ya kanisa lake (Israeli na Mataifa), linaloongozwa na hizo Roho saba, na Roho za wenye uhai wanne, Hivyo ni muhimu kufahamu ni roho gani inayoliongoza kanisa ulilopo sasa, kadhalika na ni Roho ya mwenye uhai yupi aliye juu yako na juu ya wakati wa kanisa ulilopo vinginevyo hutaweza kukiona kiti cha enzi cha Mungu au kumshinda shetani kwa namna yoyote ile katika wakati huu unaoishi.

Kumbuka shetani naye anacho kiti chake cha enzi, na chenyewe pia kimezungukwa na roho chafu nne, ndio wale wapanda farasi wanne ambao tutakuja kuwaona katika sura ya 6, na anazo roho nyingine chafu saba, ndizo zilizokuwa zinatembea pia katika makanisa saba ya Mungu kulichafua kanisa la Mungu na kupoteza watu Ndio zile Bwana Yesu alizozizungumzia katika..
 
Mathayo 12: 43 " Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.
44 Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.
45 Mara huenda, akachukua pamoja naye PEPO WENGINE SABA walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa KIZAZI HIKI kilicho kibaya. "
 
Unaona hapo katika ile siku ya Pentekoste Bwana alilijenga tena kanisa kwa kulitakasa kwa Roho wake, kwa wakati ule Kanisa lilikuwa kamilifu lakini mitume wa kweli walipoondoka,mitume wa uongo wakanyanyuka kuunda misingi ya kanisa lingine la uongo na kuanza kuchanganya kweli ya Mungu na mafundisho ya kibinadamu, hivyo ikapelekea ile roho (pepo) ambalo Bwana Yesu alilitoa pale Kalvari kurudi tena katika kanisa la Mungu kwa taswira mbaya zaidi, lilirudi katika mwishoni wa kanisa la kwanza, kadhalika na katika kanisa la pili likaongezeka lingine la pili, na katika kanisa la tatu, na la nne, mpaka kanisa la saba, mapepo yote saba maovu yakalivaa kanisa, na ndio maana hali ya kanisa hili la Laodikia ni mbaya kuliko makanisa yote yaliyotangulia...Lakini siku zote mbegu halisi haiwezi changanyikana na ya uharibifu Bwana alishalianza kuwatenga watu wake na kanisa hilo la uharibifu tangu zamani.
 
Hivyo ni muhimu kufahamu pia kiti cha enzi cha shetani kilipo, kwasababu yeye naye anachokiti chake cha enzi Soma Ufunuo 2: 13 " Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; ...." Unaona hapo?

Ikiwa na maana kuwa hata yeye naye analo kanisa lake aliloliunda ndipo aketipo yeye. Na kanisa hilo ni Kanisa Katoliki. Hilo ndilo linaloongozwa na (mapepo) yale saba maovu, na wale wapanda farasi wanne, ambao kwa ujumla roho hizi zilishughulika sana kupambana na uzao wa Mungu na kuuharibu kama tutakavyokuja kuona katika sura ya sita.

Kama vile Mungu alivyotwaa mwili na kuishi katikati yetu na kufanyika mfalme wa kanisa la Mungu, kadhalika shetani naye amemtia mtu mafuta akae badala yake katika kiti chake cha enzi, na si mwingine zaidi ya mpinga-kristo (PAPA atakayekuja) aliye kichwa cha kanisa hilo la uongo.

Hivyo ndugu jiulize je! umeketi katika kiti cha enzi cha Mungu au cha shetani??..Kama unadai umeketi katika kiti cha enzi cha Mungu, na bado haupo katika misingi ya mafundisho ya mitume 12(BIBLIA), na haufahamu kanisa unaloishi!, na hauifahamu Roho inayoliongoza kanisa lako? basi ni dhahiri kabisa kwamba unaketi katika kiti cha enzi cha shetani pasipo hata wewe kujijua, kwasababu ile roho ya uhai yenye macho mbele na nyuma ambayo ingepaswa ikuongoze haipo juu yako ambayo ingekupa wewe uhai na macho ya kuweza kuona mambo ya mbele na ya nyuma na kukuwezesha wewe kuzijua fumbo za shetani imeondoka. Na pia kumbuka viti vyote vya enzi (cha MUNGU na cha shetani) vinaundwa hapa hapa duniani..Hivyo jitathimini maisha yako. je! umeoshwa kwa damu ya YESU KRISTO na kujazwa Roho Mtakatifu? Huyo tu ndiye atakayekuongoza katika kweli yote na sio dini au dhehebu. Mkumbuke muumba wako siku za ujana wako kabla haijakaribia miaka utakayosema sina furaha katika hiyo(Mhubiri 12).

Ubarikiwe.

Tafadhali "share" kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki.

Thursday, June 21, 2018

INJILI YA MILELE.

Licha ya kuwa na INJILI YA MSALABA,ambayo ndio kiini cha kila mwanadamu ipo injili nyingine pia ijulikanayo kama INJILI YA MILELE, hii ni tofauti na injili ya msalaba. Injili ya msalaba yenyewe inatangaza wokovu kwa mwanadamu tu, kwa kupitia mmoja naye ni YESU KRISTO BWANA wetu. Kwahiyo injili nyingine yeyote inayodai kumkomboa mwanadamu na haimweki Bwana Yesu kama kiini cha injili yenyewe, basi injili hiyo ni batili, kwasababu yeye pekee ndiye Njia, kweli na uzima, hakuna mtu yeyote atakayemwona Mungu, pasipo kupitia kwake yeye biblia inasema hivyo(Yohana 14:6).. Kwahiyo zipo injili nyingi zinazodai zinaweza kumkomboa mwanadamu lakini kati ya hizo ni moja tu itakayoweza kumkomboa mwananadau! Nayo ni Kwa kupitia Yesu Kristo, na ndio maana Mtume Paulo alisema|:

2Wakoritho 11: 4 “Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au INJILI NYINGINE msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!”

Unaona hapo? Biblia inasema kuna Yesu mwingine, roho mwingine na injili nyingine tofauti na ile iliyohubiriwa na mitume. Kwahiyo injili yoyote inayohusishwa na ukombozi wa mwanadamu inapaswa imlenge YESU KRISTO ALIYESULIBIWA,akafa na kufufuka kama kiini cha Ukombozi wenyewe, kwa asilimia mia yeye peke yake na sio pamoja mtu mwingine.

Lakini leo kwa ufupi tutaitazama INJILI YA MILELE ambayo ipo na imezungumziwa katika biblia..kama tunavyosoma katika;
Ufunuo 14: 6 “Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye INJILI YA MILELE, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa,
7 akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji”.

Sasa hii injili ya milele ni ipi?

Kama jina lake lilivyo “Milele” inamaana kuwa ni injili ambayo Ipo milele yote, ilikuwepo kabla ya mwanadamu kuumbwa, ipo sasa, na itaendelea kuwepo milele na milele, Kumbuka INJILI YA MSALABA ilikuwa na mwanzo, na itakuwa na mwisho, mwanzo wake ilikuwa ni Kalvari, na mwisho wake itakuwa katika Unyakuo. Baada ya hapo hakutakuwa na nafasi tena ya ukombozi, kwasababu mlango wa neema utakuwa umefungwa. Kitakachokuwa kimebaki ni ile ile injili ambayo ilikuwepo milele na milele.

Na ndio maana ukisoma mstari huo hapo juu utaona kuwa yule malaika(mjumbe) anapita kuitangaza hiyo injili ambapo kwa wakati huo unyakuo wa kanisa utakuwa umeshapita na mlango wa neema ya kuokolewa utakuwa umefungwa kwa watu wa mataifa.

Kwahiyo injili hii ni tofauti na ya msalaba tuliyonayo sasa, hii ya msalaba tunaifahamu kwa “kuhubiriwa”. Hatuwezi kuifahamu pasipo kuhubiriwa ndio maana biblia inasema katika;

Warumi 10: 13 “kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana{YESU KRISTO} ataokoka.
14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? TENA WAMSIKIEJE PASIPO MHUBIRI?
15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!{INJILI YA MSALABA}”

Kwahiyo unaona hapo, ni lazima awepo mtu wa kuihubiri ndipo watu waokolewe.

Tofauti na ilivyo INJILI YA MILELE. Injili hii haisambazwi kwa kuhubiriwa na mtu yeyote, Ni Mungu mwenyewe anaiweka ndani ya mtu, katika eneo maalumu la moyo wa mwanadamu linaloitwa “DHAMIRA”..ambayo kila mtu anazaliwa nayo. Na inafanya kazi ya kuhukumu njia zote mbaya zinazokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu ndani ya mtu..Na Injili hii haipo tu kwa wanadamu, ilikuwepo hata kwa malaika, kwasababu ni ya milele, ilikuwepo huko enzi na enzi, ipo na itakuwepo.

Kwahiyo sasa kitendo tu cha mtu kuwa mwanadamu, tayari moja kwa moja kuna kitu ndani yake kitakuwa kinamshuhudia mambo yanayofaa na yasiyofaa, bila hata kuhubiriwa au na mtu yeyote, au kukumbushwa na mtu yeyote, kwamfano, kila mtu anafahamu kuwa uuaji sio sawa, iwe anayo hofu ya Mungu au hana hofu ya Mungu, kila mtu anafahamu kuwa dhuluma ni mbaya, hata kama sheria isingesema hivyo, ndani ya moyo wake dhamira inamuhubiria kuwa kitendo hicho ni kibaya, Kadhalika haihitaji kuifahamu biblia kujua kuwa uonevu ni makosa, wizi ni makosa, utukanaji, ubakaji, rushwa ni makosa hayo yote hata kama mtu hajawahi kumsikia Mungu, au chochote kinachoitwa Mungu anajua kabisa hayo mambo hayafai kufanya, pia haihitaji kwenda katika vyuo vya biblia kutambua kuwa kulala na ndugu yako wa damu ni makosa, kadhalika na ushoga au usagaji ni makosa, utajikuta tu wewe mwenyewe unachukia kufanya hivyo au unalipinga hilo wazo ndani yako pale linapokuja kwasababu unajua kabisa kuwa hayo ni makosa. Sasa hiyo ndio inayoitwa INJILI YA MILELE, Mungu anayoihubiri ndani ya moyo wa mtu. Na ndiyo hiyo siku za mwisho itakuja kukumbushwa kwa watu, wamche Mungu.wakati huo unyakuo utakuwa umeshapita.

Kwahiyo usidhani kuwa wale watu ambao hajasikia habari za YESU(Injili ya msalaba) mahali popote, hawatahukumiwa. Hapana Watahukumiwa tu kama wale wengine kwa injili hiyo. Watu wa kipindi cha Nuhu hawakuwa na sheria waliyopewa na Mungu kama watu wa Musa na kuendelea,Na ndio maana Mtume Paulo alieleza habari za watu hawa kama tunavyosoma katika...

Warumi 1: 17 Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.
18 Kwa maana GADHABU YA MUNGU imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.
19 Kwa kuwa MAMBO YA MUNGU YANAYOJULIKANA YAMEKUWA DHAHIRI NDANI YAO, KWA MAANA MUNGU.
20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; YAANI, UWEZA WAKE WA MILELE NA UUNGU WAKE; hata wasiwe na UDHURU;
21 kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.
22 Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika;
23 wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.
24 Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.
25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.
26 Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;
27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.
28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.
29 Wamejawa na UDHALIMU, UOVU na TAMAA na UBAYA; wamejawa na HUSUDA, na UUAJI, na FITINA, na HADAA; watu wa NIA MBAYA, wenye KUSENGENYA,
30 wenye KUSINGIZIA, wenye KUMCHUKIA MUNGU, wenye JEURI, wenye KUTAKABARI, wenye MAJIVUNO, wenye KUTUNGA MABAYA, WASIOTII WAZAZI WAO,
31 wasio na UFAHAMU, wenye KUVUNJA MAAGANO, WASIOPENDA JAMAA ZAO, WASIO NA REHEMA;
32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.
Umeona hapo ndugu, biblia inasema wakijua kabisa watendao mambo kama hayo wamestahili mauti lakini bado wanayatenda. Dhamira zao zikiwashuhudia ndani kuwa wanayoyafanya sio sahihi lakini wanaendelea kuyafanya, Na wewe je! Ambaye upo kwenye dhambi utahitaji mhubiri siku moja aje kukuthibitishia kwenye biblia kwamba, uvutaji sigara ni dhambi, au uasherati ni dhambi?? Angali ndani ya moyo wako dhamira inakushuhudia kabisa unachofanya ni makosa?..hakika unaweza usilione lakini fahamu kuwa hukumu inakungojea.!

Wewe unayevaa vimini, na kutembea nusu uchi barabarani unasema Mungu haangalii mavazi lakini moyo wako unakuambia kabisa hayo ni makosa unayoyafanya na bado unaweka moyo mgumu, wewe unayevaa suruali,unayepaka wanja, na kupaka lipstick, na kuvaa wig na hereni, Hukumu ipo mbeleni dada!, wewe unayesengenya, wewe ambaye ni shoga, wewe unayejisaga, wewe unayetoa mimba, wewe uliye mwasherati, wewe uliye mlevi, wewe unayetazama pornography, wewe unayefanya masturbation, wewe unayeabudu sanamu za watakatifu waliokufa zamani angalia biblia inavyokuambia hapo juu < wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu(sanamu), na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo >..Unaona unajua kabisa Mungu hawezi kufananishwa na mfano wowote wa kinyago cha kuchonga lakini wewe bado unakwenda kuvipiga magoti na kuviabudu..

2Wakorintho 6: 16 inasema “Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu?”..

Lakini biblia inaendelea kusema kwa jinsi utakavyozidi kuweka moyo wako mgumu, kuna kipindi kitafika Mungu anakuacha uendelee hivyo hivyo kwasababu umekataa kuitii hiyo sauti inayosema ndani yako, mpaka ile siku ya hukumu ije na utaingia kuzimu!! Alisema “”28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa”. 
Kwahiyo dada/kaka hukumu ya Mungu haikwepeki hata uwe nje ya kanisa, njia pekee ni kujisalimisha maisha yako kwa BWANA YESU ambaye yeye ndiye aliyetoa uhai wake ili akuokoe, Tubu geuka, ukapewe uwezo wa kushinda dhambi. Muda umekwenda kuliko unavyodhani, na Injili ya msalaba sio ya milele utafika wakati utatamani uingie utakosa, muda ndio huu, mpe Bwana maisha yako tangu sasa.

Ubarikiwe.
Tafadhali “Share” kwa wengine na Mungu atakubariki.

JE! UMEYABATILISHA MAMBO YA KITOTO?

1Wakoritho 13: 11 “Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto”.

Katika maisha ya kawaida, mwanadamu ni lazima apitie katika hatua hizi mbili; UTOTO na UTU UZIMA. Na kila hatua ni lazima iwe na uongozi juu yake, Kwamfano mtoto mdogo hawezi kujiongoza mwenyewe kwasababu akili yake haijakomaa kuweza kutambua jema na baya au kupambanua kanuni za maisha hivyo ni lazima aandaliwe na mzazi wake au mlezi wake kanuni fulani za kufuata aidha apende au asipende kwake huyo zinakuwa ni sheria na amri, na ndio maana tunaweza kuona mtoto anapofikisha umri fulani labda miaka 6/7, anapelekewa shule sio kwa mapenzi yake, hapana, pia analazimishwa kuamshwa asubuhi kila siku ili aende shule na tunafahamu hakuna mtoto anayependa kuamshwa asubuhi apige mswaki na kwenda shule, yeye atatamani tu acheze cheze na kurukaruka,

Kadhalika akirudi baadaye nyumbani, atalazamishwa alale mchana, atalazimishwa aoge, atalazimishwa afanye homework,atachaguliwa nguo za kuvaa, na wakati mwingine atachaguliwa mpaka na marafiki wa kucheza naye, n.k. Hivi vyote atafanya tu hata kama hataki, na wakati mwingine akikosea mojawapo ya hizo kanuni alizowekewa itamgharimu adhabu. Hivyo ukichunguza kwa undani utaona kuwa sio kwamba Yule mtoto anatimiza zile sheria kwa kupenda la! Bali anafanya vile kwa kutimiza tu matakwa ya baba / mama yake basi, laiti angepewa uhuru kidogo tu! Asingedhubutu kufanya mojawapo ya hayo, angeenda kufanya mambo yake mengi kuzurura zurura tu.

TABIA YA MTU MZIMA.

Lakini Yule mtoto atakapokuwa mtu mzima kidogo kidogo mabadiliko yataanza kutokea ndani yake, ataanza kuona umuhimu wa yeye kuamka asubuhi na mapema na kupiga mswaki mwenyewe, na umuhimu wa kwenda shule , ataona umuhimu wa kuoga, ataona umuhimu wa kuwa na marafiki wazuri, n.k. Lakini ni kwasababu gani anafanya hivyo?. Ni kwasababu ameshakuwa mtu mzima na anajua kufanya hivyo ni kwa faida yake mwenyewe na sio kwa faida ya mzazi. Na hiyo ndiyo dalili kubwa ya kuonyesha kuwa mtu huyo amekuwa. Kwasababu ile sheria na maagizo aliyopewa na wazazi wake sasa anayatimiza mwenyewe ndani ya moyo wake pasipo kushurutishwa. Na ndipo mzazi anapoona sababu ya kumwamini na kumwacha huru kabisa kabisa ayaongoze maisha yake mwenyewe.

Mfano mwingine tunaweza tukajifunza kwa mwanafunzi: alipokuwa shule ya msingi ni tofauti na atakapokuwa chuo kikuu, kule nyuma alikuwa analazimishwa kuwepo shule kila siku alfajiri, ahudhurie kila kipindi cha darasani, alilazimshwa avae sare, alichapwa alipokosea, alikaguliwa notes alizoandika n.k.. Lakini alipofika chuo hakuna tena sheria ya kumwambia aamke alfajiri kila siku aende chuo, ni kwasababu gani? Ni kwasababu chuo kinatambua kwamba Yule mtu anajielewa, hivyo hata asipohudhuria leo atakuwa na sababu za msingi za kutokufanya hivyo tofauti na alipokuwa shule ya msingi, mfano angepewa uhuru tu! Angeutumia katika michezo na utoro, kadhalika pia akiwa chuo hapewi sare, hashikiwi kiboko kulazimishwa kusoma, hakaguliwi notes n.k. lakini japokuwa hakuna sheria zote hizo, mwisho wa siku utakuta Yule mwanafunzi anafaulu. Unaona hapo? hayo yote haimaanishi kuwa chuo hakikuwa na sheria hapana, kilikuwa nayo sana tu, bali kimemweka huru mbali na ile sheria kwasababu kilitambua aliyefika chuo ameshajitambua vya kutosha na anajua jukumu lake kama mwanafunzi.

Kadhalika na katika KANISA LA MUNGU nalo pia limepitia katika hatua zote mbili: UTOTO na UTU UZIMA. Hatua ya utoto ni pale Mungu alipolizaa kanisa kwa mara ya kwanza kule jangwani, hivyo kama lilikuwa ni changa ni dhahiri kuwa lingehitaji kupewa sheria ya kuliongoza kwasababu halijaweza bado kupambanua mema na mabaya. Na ndio tunaona sheria/ Torati ilikuja na zile amri zote kutolewa kwa mkono wa Musa na kupewa watu, kwamba waishi katika hizo. Na kama tunavyojua sheria kwa mtoto inakuwa ni AMRI na sio OMBI, kadhalika na hawa nao (kanisa-jangwani waisraeli) ilikuwa ni AMRI kuzitimiza sheria za Mungu zilizotolewa, ndio maana ilikuwa ni amri mtu asiibe, asizini, asiue, aishike sabato, asiabudu sanamu n.k.na kwa yeyote asiyefanya aliadhibiwa vikali. Na kwasababu walikuwa ni watoto walifanya vile kwaajili ya kumridhisha tu baba yao (MUNGU), Walitimiza zile sheria sio kwasababu wanapenda hapana, ni kwasababu baba yao hapendi dhambi, laiti wangeachiwa uhuru kidogo wasingezishika.

Lakini ulipofika wakati wa KANISA LA MUNGU KUKUA, Ilipasa zile sheria ziingizwe ndani ya moyo wa kanisa ili zitimizwe kwa mapenzi ya mtu mwenyewe na sio mapenzi ya Mungu na bila shuruti. Kama biblia ilivyotabiri zamani za manabii tukisoma.

Yeremia 31: 31 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.
33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; NITATIA SHERIA YANGU NDANI YAO, NA KATIKA MIOYO YAO NITAIANDIKA; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
34 Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”.

Jambo hili lilikuja kutimia siku ya PENTEKOSTE, pale ROHO wa Mungu alipomiminwa juu ya mioyo ya watu kwa mara ya kwanza na kuwafanya wavuke daraja la utoto na kuingia katika daraja la UTU UZIMA. Sasa kuanzia huo wakati Roho alipomshukia mtu, kitu cha kwanza alichokuwa anafanya ni kuiingiza ile sheria ndani ya moyo wake, kiasi kwamba Yule mtu ile sheria anakuwa anaitimiza kwa mapenzi yake mwenyewe na sio kwa mapenzi ya Mungu. Kama vile mwanafunzi aliyeko chuo anasoma kwa mapenzi yake na sio kwa mapenzi ya Baba yake au mama yake tofauti na alivyokuwa akifanya shule ya msingi. Hicho ndicho alichokifanya Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Na ndio anachoendelea kukifanya mpaka sasa hivi.

Sasa kuanzia ule wakati wote walioshukiwa na Roho wa Mungu, wakawa hawazini, sio kwasababu Mungu kawakataza bali ni kwasababu waliona ni kwa faida yao wenyewe, wakawa hawaabudu sanamu sio kwasababu Mungu kawakataza hapana bali ni kwasababu wanajua Mungu pekee ndiye anayestahili kuabudiwa, wakawa wanaomba sio kwasababu Mungu kawaagiza lakini kwasababu waliona umuhimu wa kuomba kama Mkristo ili kuepukana na majaribu, hawakuishika sabato kama amri, kwamba tumwabudu Mungu tu katika siku fulani, hapana bali sabato yao ilikuwa kila siku, kwasababu walijua Mungu haabudiwi katika siku Fulani bali katika Roho na Kweli.Kadhalika na zile sheria zote walizopewa walipokuwa wachanga walikuwa wanazitimiza pasipo AMRI bali kwa moyo na kwa uelewa. Kwasababu hiyo basi Mungu akawacha huru kabisa mbali na SHERIA na TORATI. Na ndio maana biblia inasema:

Wagalitia 5: 18 “Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria”. Na pia inasema…
Warumi 8: 2 “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti”.
Warumi 8: 4 “ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho”.

Kwahiyo unaona hapo? Umuhimu wa kuwa na Roho Mtakatifu?..Ni kukufanya wewe utoke katika hali ya utoto wa kiroho(utumwa) na uingie katika hali ya utu uzima(Uhuru) na hiyo ndiyo neema. Ukiona mtu pale unapomuuliza ni kwanini huzini, au huibi? Na anakwambia ni kwasababu Mungu kanikataza, moja kwa moja unajua huyo bado ni mtoto yupo chini ya Sheria hata kama atajifanya yupo chini ya neema. Ukiona mtu anakwambia mimi nashikilia siku moja ya kuabudia sabato, unajua huyo naye yupo chini ya sheria ya utoto, au mtu akikuambia mimi sivai vimini, sinywi pombe, sivuti sigara kwasababu Mungu kakataza, ujue huyo pia ni mtoto bado hajawekwa huru na sheria ya dhambi, Ukiona mtu anasema mimi siabudu sanamu kwasababu amri ya 2 inasema hivyo, unajua kabisa huyo bado ni mtoto Roho wa Mungu bado hajamfanya kuwa huru nk....

Lakini wale wote waliowekwa huru na ROHO, hawataona mzigo wowote kuishi maisha ya utakatifu wataona kutokuzini, kutokuvaa vimini, kutokuweka make-up, kutokuvaa suruali, kutokusengenya, kutoiba, kutokwenda disco, n.k. wataona kuwa hayo ni majukumu yao na ni kwa faida ya Roho zao na sio kwa faida ya Mungu, au sio kwasababu Mungu kawaambia. Watafanya yote yawapasayo kufanya iwe ni Mungu kawaagiza, au hajawaagiza.. Na hiyo ndio DALILI ya mtu kuwa amepokea kweli kweli Roho Mtakatifu…Utakatifu anautimizwa kwa kupenda na sio kwa maagizo Fulani.

Warumi 8: 9 “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake”.

Hivyo ndugu, na wewe upo katika uchanga au utu uzima?. Umejazwa Roho Mtakatifu au bado unaongozwa na dini?. Tafuta Roho Mtakatifu kumbuka Roho Mtakatifu ndio muhuri wa Mungu (Waefeso 4:30) pasipo huyo hakuna UNYAKUO.

Ubariwe

Wednesday, June 20, 2018

CHUKIZO LA UHARIBIFU


Jina la Bwana wetu YESU KRISTO libarikiwe sana. Karibu tuongeze maarifa katika kulichambua Neno la Mungu leo tutajifunza juu ya chukizo la uharibifu, natumai ujumbe huu utakutoa sehemu moja ya kiroho hadi nyingine, sasa ili tuweze kwenda kwa uzuri ni vema uwe na biblia pembeni ili kukusaidia kufuatilia baadhi ya mistari tutakayokuwa tunaipitia katika somo hili.

Kwa kuanza ni vizuri tukifahamu nini maana ya “chukizo la uharibifu”: Kwa lugha nyepesi tunaposema chukizo la uharibifu ni sawasawa na kusema “chukizo linaloleta uharibifu” au “Chukizo linalopelekea uharibifu”..Kwahiyo hapo kuna mambo mawili, la kwanza ni CHUKIZO, na la pili ni UHARIBIFU. Sasa chukizo ni nini? Na uharibifu ni nini?.

CHUKIZO: Kwa tafsiri ya kibiblia hilo neno chukizo maana yake ni kuudhi/kuleta hasira, hususani pale panapohusishwa na uzinzi, Hivyo mambo yote yaliyokuwa yanafanywa na watu wa Mungu ambayo yalikuwa kinyume na sheria zake mfano kuabudu miungu mingine, kujichongea sanamu, kufanya uchawi, n.k. hayo yote mbele za Mungu yalijulikana kama MACHUKIZO (mambo ya kuudhi au kukasirisha).

Kwa mfano tunaweza kuona Bwana aliwaambia wana wa Israeli katika Kumbukumbu 18: 9-13 akisema:

"9 Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa MACHUKIZO ya mataifa yale.
10 Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,
11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.
12 KWA MAANA MTU ATENDAYE HAYO NI CHUKIZO KWA BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.
13 Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako”.

Unaona hapo mambo waliowafanya wafukuzwe (“mataifa yaliyokuwa Kaanani”) na kuondoshwa kabisa ni MACHUKIZO yao mbele za Mungu, hivyo Mungu akatangulia kuwaonya mapema watu wake kwamba watakapofika katika hiyo nchi ya Ahadi wasijaribu kutenda mfano wa mambo hayo. Kwani Watu wa mataifa walikuwa wana loga, wanaabudu miungu mingi, wanaabudu masanamu, wanapitisha watoto wao kwenye moto, wauaji, n.k. Kwasababu hiyo basi wana wa Israeli walionywa sana wakae mbali na hivyo vitu, kwani vitawasababisha wao nao yawapate yale yale yaliyowapata mataifa mengine.

UHARIBIFU: Kama tulivyoona hapo juu, sababu kubwa iliyowapelekea mataifa yale makubwa yafukuzwe na KUHARIBIWA kabisa haikuwa kwasababu ya kwamba Mungu anawachukia tu!au anawapenda Israeli kuliko wao hapana bali ni kwasababu ya machukizo yao na ndiyo ikawapelekea kuharibiwa na kutolewa katika ile nchi ya Kaanani na kupewa wana wa Israeli. Na kama tunavyojua siku zote kitu kikiwa kinachukiza mara kwa mara kinachofuata ni kuangamizwa au KUHARIBIWA kabisa.

Bwana aliwaaonya tena wana wa Israeli na kusema:

Mambo ya walawi 18: 24 “Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote;
25 na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa.
26 Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye MACHUKIZO hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu;
27 (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya MACHUKIZO HAYA YOTE, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;)
28 ili kwamba hiyo nchi isiwatapike na ninyi pia, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu.
29 KWANI MTU AWAYE YOTE ATAKAYEFANYA MACHUKIZO HAYO MOJAWAPO, NAFSI HIZO ZITAKAZOFANYA ZITAKATILIWA MBALI NA WATU WAO.
30 Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi ZICHUKIZAZO mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”

Unaona hapo, machukizo yote yaliyokuwa yanazungumiziwa mwisho wake yote yalipelekea UHARIBIFU kwa namna moja au nyingine kwa hilo taifa au mtu mmoja mmoja aliyeyafanya.. Sasa kumbuka vitu hivi kama uchawi, ulawiti, uuaji, uongo n.k. haya yote yalikuwa ni machukizo yanayoleta uharibifu lakini LIPO CHUKIZO MOJA, lililozungumziwa na BWANA YESU, na katika kitabu cha DANIELI, ambalo litakuja kusimama sehemu patakatifu na kuleta uharibifu mkubwa kwa watu wengi wa Mungu litakalosababisha kuwepo na dhiki kubwa ambayo haijawaki kutokea tangu ulimwengu kuwako, na ndilo litakalopelekea hata uharibifu wa dunia.

Kumbuka wakati wana wa Israeli walipokuwa wanaingia katika nchi ya Kaanani, Mungu hakuteua mahali popote katikati ya miji yao pa kuliweka jina lake, na kuwa sehemu takatifu, hivyo wakati huo wote waisraeli walipokuwa wanafanya machukizo Bwana aliwaharibu mara nyingine kwa kuwatia katika mikono ya maadui zao kama wafilisti na walipotubu Bwana aliwanyanyulia waamuzi ambao waliwaokoa na mikono ya maadui zao lakini hawakuwa wanaondolewa taifa lao. Lakini ulipofika wakati Bwana alipojiteulia mahali PATAKATIFU pake pa kuwekea Jina lake yaani YERUSALEMU, zamani za mfalme Daudi, mambo yalianza kubadilika, siku ile HEKALU LA MUNGU lilipokamilika kujengwa kwa mikono ya Sulemani mwana wa Daudi, Baraka na bila kusahau LAANA pia ziliongezwa makali, Na ndio maana Bwana alimwambia Sulemani baada ya kuijenga ile nyumba maneno haya..

1Wafalme 9: 6 “Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, TENA MKIENDA NA KUITUMIKA MIUNGU MINGINE NA KUIABUDU,
7 BASI NITAWAKATILIA ISRAELI MBALI NA NCHI HII NILIYOWAPA na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa MITHALI NA NENO LA TUSI KATIKA MATAIFA YOTE.
8 Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atasituka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini Bwana ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya?
9 Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu Bwana ameleta mabaya haya yote juu yao”.

Unaona hapo?. Baada ya Mungu kuichagua YERUSALEMU, kama mahali pake patakatifu na HEKALU kama mahali atakapoweka Jina lake alitarajia muda wote Israeli wakae katika hali ya usafi wa hali ya juu kuliko hapo kwanza, kwamba wakifanya machukizo mbele za Patakatifu pa Mungu, wakatakatiliwa mbali, na kutawanywa katika mataifa yote, na watakuwa mithali kwa kila wawatazamao.

Lakini tukirudi katika kitabu cha Wafalme tunaona hawakuisikia hiyo sauti ya Mungu, badala ya kudumu katika usafi kwa Mungu wakaanza kidogo kidogo kuingiza ibada nyingine katika Israeli na katika nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu, licha ya kwamba Mungu aliwatumia manabii wengi kuwaonya lakini hawakutaka kubadilika (Kuyaacha machukizo yao mbele za Mungu) ikapelekea Mungu kutamka UHARIBIFU WAO. Kama alivyoahidi katika NENO lake, pale Nebukadneza Mfalme wa Babeli Bwana alipomruhusu kwenda kuuteketeza mji wa Yerusalemu, na kuliharibu kabisa lile hekalu la Sulemani, wakauawa majemedari wengi wa Israeli kwa upanga, wengine njaa, na wengine magonjwa, Dhiki ilikuwa kubwa sana, wakachukuliwa utumwani na Israeli ikabaki kama ukiwa, Kutokana na MACHUKIZO waliyoyasimamisha wao wenyewe hivyo yakawapelekea UHARIBIFU MKUBWA namna hiyo.. Naamini kidogo kidogo utakua umeanza kuelewa nini maana ya chukizo la uharibifu.

2Mambo ya nyakati 36:14 “Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na MACHUKIZO YOTE YA MATAIFA; WAKAINAJISI NYUMBA YA BWANA ALIYOITAKASA KATIKA YERUSALEMU.
15 Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;
16 lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, HATA ILIPOZIDI GHADHABU YA BWANA JUU YA WATU WAKE, HATA KUSIWE NA KUPONYA.
17 Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo{Wa-babeli}, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake.
18 Na vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, vikubwa kwa vidogo, na hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za mfalme, na za wakuu wake; vyote pia akavileta Babeli.
19 WAKAITEKETEZA NYUMBA YA MUNGU, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, WAKAVIHARIBU vyombo vyake vyote vya thamani.
20 Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi;

Tukio hili lililiathiri Taifa la Israeli kwa vizazi vingi, Kama ukifuatilia historia utaona kuwa Israeli halikuwahi kuwa tena taifa huru kwa muda wa miaka 2500, tangu ule wakati walipopelekwa Babeli mpaka juzi juzi tu mwaka 1948, ndio wamekuwa taifa huru tena, siku zote hizo walikuwa wanaishi kama wageni mahali popote walipopelekwa au kukaa. Na hata walipotoka Babeli walikuwa chini ya mataifa yaliyokuwa yanamiliki dunia kwa wakati huo. Unaweza ukaona ni MACHUKIZO MAKUBWA kiasi gani yaliyowasababishia kupitia uharibifu na adhabu kali kaisi hicho… Mungu ni Mungu mwenye WIVU hapendi mahali pake patakatifu panajisiwe kwa namna yoyote ile..

Na tunaona baada ya kutoka Babeli, Bwana aliwarehemu akawajalia kujenga tena hekalu la pili baada ya lile la kwanza lililotengenezwa na Sulemani kubomolewa na mfalme Nebukadneza wa Babeli. Kadhalika Mungu aliwaonya pia yale masalia ya wayahudi waliorudi wasifanye machukizo kama waliyoyafanya mababa zao. Mwanzo walitii lakini kilipopita kipindi Fulani walikengeuka, wakaanza kufanya mfano wa machukizo ya mataifa. (Kumbuka wakati huu Israeli ilikuwa haijiongozi yenyewe kama hapo kwanza) ilikuwa chini ya utawala wa wafalme wengine. Hivyo njia pekee shetani aliyoitumia kusimamisha machukizo katika nyumba ya Mungu kiurahisi sio kuwatumia wayahudi peke yake, bali alianza kuwatumia pia wafalme wa mataifa kwasababu wao ndio waliokuwa na nguvu juu ya taifa la Israeli,

Tukisoma katika kitabu cha Danieli tunaona Danieli akionyeshwa katika maono juu ya mfalme atakayenyanyuka katika utawala wa Umedi & Uajemi ambao ndio kwa wakati huo ulikuwa unatawala dunia, alionyeshwa kiongozi mkatili akilisimamisha chukizo la uharibifu tena katikati ya wayahudi na patakatifu na huyu hakuwa mwingine zaidi ya ANTIOKIA IV EPIFANE (Kumbuka mpaka Antiokia kuja kulitia unajisi hekalu ilikuwa ni matokeo ya kukengeuka kwa wana wa Israeli,mfano wasingeasi Bwana angewaepusha na hayo mambo) Tukisoma

Danieli 11: 31 Na wenye silaha watasimama upande wake, nao watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku, NAO WATALISIMAMISHA CHUKIZO LA UHARIBIFU..

Kulingana na historia inavyoeleza, kiongozi huyu alinyanyuka na kuingia katika hekalu la Mungu na kufanya maasi yote ambayo hayapaswi kuwepo katika nyumba ya Mungu, aliweza kusitisha sadaka zote za kuteketezwa ambazo zilikuwa zinafanywa na makuhani katika nyumba ya Mungu, na kuiweka sanamu ya ZEU mungu ambayo ilikuwa inamwakilisha yeye, kadhalika akawa anatoa dhabihu ya viumbe najisi kwa wayahudi kama nguruwe katika madhabahu iliyokuwa ndani ya Hekalu la Mungu na kuwalazimisha wanywe damu zao hivyo viumbe, mambo ambayo yalikatazwa katika Torati ya Musa, hakuishia hapo tu, aliwaua wayahudi wengi sana na kuwakosesha kuabudu katika dini yao, hivyo ikawa ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu…Lakini Mungu alikuja kumuua Antiokia, kwa mambo hayo lakini hekalu halikubomolowa,(Ni sadaka tu ya kuteketezwa ndio iliyokomeshwa) kwahiyo kile kitendo cha yeye kwenda pale pamoja na majeshi yake na kutia unajisi patakatifu pa Mungu, ni CHUKIZO LA UHARIBIFU,.kama Danieli alivyolinena.

Sasa huyu Antiokia alikuwa anatimiza sehemu ya kwanza ya chukizo la uharibifu juu ya Hekalu la pili..Sehemu ya pili ambayo ilipelekea tena Uharibifu mkubwa mpaka Hekalu la Mungu kubomolewa na wana wa Israeli kutawanya katika mataifa yote ilitokea mwaka wa 70WK. Wakati jeshi la Rumi chini ya jenerali TITO alipouzunguka mji wa Yerusalemu na kuuchoma moto, na kulibomoa hekalu na kuliteketeza kabisa, na kuwatawanya wana wa Israeli kutoka katika nchi yao, hii ikawa ni mara ya pili ya hekalu la Mungu kuteketezwa baada ya lile la kwanza lililobomolewa na mfalme Nebkadreza wa Babeli.

Na kama vile lile la kwanza lilivyoteketezwa kwasababu ya maovu na maasi ya wana wa-israeli kadhalika na hili la pili lilibomolewa kwasababu hiyo hiyo,? Tunasoma wana wa Israeli walianza kwa kumkataa Yohana mbatizaji kisha wakaja kumkataa BWANA YESU mwenyewe, na kibaya zaidi wakamsulibisha, Bwana aliwaambia katika Yohana 8: 24 “Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu”..Na ni kweli hawakumsadiki Bwana, na ndio maana siku ile alipoukaribia mji wa Yerusaleu aliulilia na kusema.

Luka 19: 41 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,
42 akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.
43 Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;
44 watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako”.

Unaona hapo? Sababu ya kwanza iliyowapelekea wana wa Israeli mpaka kuharibiwa mji wao tena pamoja na Hekalu na jeshi la Rumi ni zile zile kwani waliwakataa manabii wa Mungu kwa kuwaua (soma Luka 13:34) na kuwasulibisha na zaidi ya yote walimkataa aliyemkuu wa uzima wakamkataa mfalme wao (ambaye ni Yesu) wakamkubali mfalme mwingine wa kidunia (KAISARI) na kumkiri hadharani kuwa huyo ndiye mfalme wao.

Yohana 19: 15 “Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari”.

Hivyo wakaendelea na maovu yao, pamoja na wafalme wao wa kipagani, Ndipo wakati wa mapatilizo ulipofika mji kuteketezwa na watu kuuawa na dhiki kubwa ikatokea. Lakini kabla ya huo wakati kufika Bwana alishawaonya wale waliokuwa tayari kumsikiliza kwamba watakapoona ishara Fulani (Yaani majeshi ya Rumi) kuuzunguka Yerusalemu waondoke katikati ya mipaka ya Yerusalemu. Hivyo wale waliomwamini Bwana Yesu na maneno yake (yaani Wakristo) waliepuka hiyo dhiki kwa kuondoka Yerusalemu lakini wale waliosalia waliangamia wote, Yerusalemu iligeuka kuwa ziwa la damu. Jeshi la Rumi liliwaua watu wote na kubomoa Hekalu la Mungu.

Na ndio maana Bwana alisema hivi.

Luka 21: 20 “Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba UHARIBIFU wake umekaribia.
21 Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.
22 Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.
23 Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.
24 Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia”.

Kwahiyo yale maasi waliokuwa wanayafanya katika (nyumba ya Mungu) pamoja na kuwaua manabii wa Mungu kadhalika na kumkataa Masihi wao, ndio lililokuwa CHUKIZO lililopelekea UHARIBIFU wao.

Baada ya hapo wayahudi wote walitapanywa katika mataifa mengi duniani, pasipo kuwa na makao maalumu kama hapo mwanzo, lakini tunaona Bwana aliwakumbuka tena, akawahurumia mwaka 1948, pale Mungu alipowarudishia taifa lao tena. Na sasa wameshaanza kujitambua wao ni wakina nani mbele za Mungu ile neema imeshaanza kuwarudia kidogo kidogo Hivi karibuni wataenda kujenga HEKALU LA TATU, na hili litakuwa ni la mwisho. Maandalizi yote ya kulijenga yapo tayari, kinachongojewa ni kujengwa tu, na zile dhabihu walizokuwa wanatoa kama zamani, zitaanza kutolewa tena. Na mahali patakatifu pa Mungu patawekwa wakfu tena, Na Mungu ataikumbuka Israeli tena kama zamani.
 

Lakini kumbuka shetani yupo katika kazi siku zote,..Alilokuwa analifanya nyuma ndilo atakalokuja kulifanya katika siku za mwisho, tena na zaidi ya pale. Kumbuka “machukizo ya uharibifu” yote ya nyuma yaliyotangulia yalikuwa ni kivuli tu cha CHUKIZO LA UHARIBIFU hasaa litakalokuja katika siku hizi za mwisho.

Bwana Yesu alisema katika Mathayo 24: 15 “Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (ASOMAYE NA AFAHAMU),
16 ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;
17 naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake;
18 wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake.
19 Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!
20 Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.
21 KWA KUWA WAKATI HUO KUTAKUWAPO DHIKI KUBWA, AMBAYO HAIJATOKEA NAMNA YAKE TANGU MWANZO WA ULIMWENGU HATA SASA, WALA HAITAKAKUWAPO KAMWE.
22 Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo”.

Kumbuka kutakuwepo CHUKIZO LA UHARIBIFU la tatu na la mwisho litakalokuja kusimamishwa huko Yerusalemu katika Hekalu la TATU. Wakati ule wana wa Israeli kwasababu ya makosa yao Ikasababisha Nebukadneza kuja kuliteketeza hekalu la kwanza, na kwasababu ya makosa yao tena ya kumkataa Masihi ndipo Jeshi la Rumi likaja kuuteketeza mji na Hekalu la pili. Kadhalika na kwa makosa yao tena ndiyo yatakayokuja kupelekea Mpinga-kristo kunyanyuka na kupatia unajisi patakatifu na kuleta uharibifu, pamoja na dhiki kuu katika hekalu la tatu.

Sasa kosa lenyewe litakuwa ni lipi?

Danieli alionyeshwa kosa hilo, tunasoma katika Danieli 9:26 “27 NAYE {mpinga-kristo} ATAFANYA AGANO THABITI NA WATU WENGI KWA MUDA WA JUMA MOJA; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama CHUKIZO LA UHARIBIFU; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu”.

Kwahiyo unaona hapo kuna AGANO ambalo mpinga-kristo ataingia na watu wengi, na hawa watu si wengine zaidi ya wayahudi ambao wataingia agano hilo na huyu mpinga-kristo ambalo litakuwa kwa kipindi cha miaka 7, agano hili litahusisha kupewa nafasi mpinga-kristo katika Hekalu la Mungu, jambo ambalo Mungu alishalikataza kwamba kisionekane kitu chochote katika hekalu la Mungu isipokuwa wayahudi tu tena makuhani wa uzao wa Walawi, lakini hawa wayahudi baadhi watampa heshima mpinga kristo wakijua tu ni mtu anayeheshimika duniani, hivyo anastahili kuwa na sehemu katika hekalu la Mungu, kama tu wale wa wayahudi wa kipindi cha Bwana Yesu walivyompa Heshima Kaisari, lakini hawatajua kama Yule ndio mpinga-kristo mwenyewe (ambaye atakuwa ni PAPA wa wakati huo) , na hiyo itapelekea kuwa CHUKIZO KUU kuliko yote, na ndipo Mungu ataruhusu hili agano livunjwe, lakini Yule mpinga-kristo ataghadhibika na kuleta dhiki kuu, ambayo haijawahi kuwako tangu ulimwengu kuumbwa.

Na ndio maana biblia inamtaja..katika 2Thesalonike 2: 3 “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi{MPINGA-KRISTO}, mwana wa uharibifu;
4 yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe KUKETI KATIKA HEKALU LA MUNGU, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.
5 Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?
6 Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.
7 Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.{kumbuka bibi-arusi wa Kristo ndiye azuiaye mpaka atakapoondolewa kwa kwenda kwenye unyakuo}
8 Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;
9 yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo;
10 na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa”.

Hivyo huyu mpinga-kristo ataleta dhiki duniani kwa kuihimiza chapa ya mnyama kutenda kazi,ataua wayahudi wengi sana, japokuwa sio wote kwasababu wapo ambao wataiepuka ile dhiki kwa kupitia ile injili ya manabii wawili (Ufunuo 11),na kwenda kujificha hawa watakuwa ni wale wayahudi 144,000 wanaozungumziwa katika (Ufunuo 7), lakini waliosalia wote wataungana na wale wanawali wapumbavu (yaani watu wa mataifa ambao hawakwenda kwenye unyakuo) kwa pamoja watapitia dhiki kuu ambayo itakudumu kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Kama inavyosema katika Danieli:

Danieli 12:11 “Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini”.
 
Kwahiyo hilo chukizo ni pale wayahudi watakapokuja kuingia agano na mpinga-Kristo, ambaye atataka kuja kuabudiwa kama Mungu..Hayo ni Machukizo makubwa ambayo yatasababisha Uharibifu kwa Wayahudi na kwa Dunia nzima, na kwa mpinga-kristo mwenyewe kwa kupatia unajisi patakatifu pa Mungu.( kumbuka pia Msikiti wa OMAR(Al-aqsa) uliopo pale Yerusalemu sio chukizo la uharibifu kama inavyodhaniwa na wengi .)

Kwahiyo ndugu hili chukizo la uharibifu sio tu kwa Yerusalemu peke yake hapana hata kwa KANISA, maana Kanisa ni HEKALU la Mungu biblia inasema hivyo. Na hili chukizo pia limesimama patakatifu pa Mungu, mahali ambapo pangepaswa YESU KRISTO peke yake aabudiwe, pamekuwa sehemu ya kuabudiwa sanamu pamoja na wanadamu. Bwana anasema Ufunuo 18: 4 “……..Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake. Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake”.

Tukijua kuwa tunaishi katika siku za hatari ni wakati wa kujiweka sawa, je! Bwana akija leo utaenda nae kwenye unyakuo?. Umeamini na kubatizwa?, je! wewe Ni miongoni mwa watakatifu?. Kama sivyo fanya hima katika muda huu wa nyiongeza tuliopewa. Weka mambo yako sawa siku ile isije ikakujia kama mwivi.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki..