"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, January 31, 2019

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 53


SWALI 1: Je!Mungu anaweza kuleta majibu kupitia nguvu za giza maana nashindwa Kuelewa ninaposoma habari za Mfalme Sauli kupata majibu kwa mwanamke mwenye pepo.

JIBU:Shalom!. Ni vizuri tuifahamu sifa ya Mungu, ili tusiishie tu kumchukulia yeye yupo mbinguni kaketi kwenye kiti cha Enzi, mahali pengine popote palipo pachafu hawezi kuingia wala kukanyaga, wala kujua kinachoendelea huko.

Zaburi 139:7 “Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?
8 Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya ku
zimu kitanda changu, Wewe uko.
9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari;
10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika.
11 Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku;
12 Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.”

Na ndio maana ukisoma ule mstari ule mstari wa 6 juu yake kidogo unasema hivi.. “Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.” Hii Ikiwa na maana kuwa uweza wa Mungu hautambulikani, na njia zake hazitafutikani hata tukijaribu kumtafakari Mungu vipi, hatuwezi kumpima kwa akili zetu hizi za kibinadamu kwa jinsi alivyoenea kila mahali.

Hiyo Inatuthibitishia kuwa Mungu pekee ndiye anayeweza kuwepo kila mahali, na ndio pekee mwenye funguo za makao ya viumbe vyote ulimwenguni,..hakuna mwingine yeyote mwenye uwezo huo.Kama tunavyofahamu..Zipo falme Kuu tatu zinazotembea katika duara lote la uumbaji wa Mungu, Ufalme wa kwanza ni ufalme wa Mungu mwenyewe ambao huo upo katika ulimwengu wa roho, na ufalme wa pili ni ufalme wa giza nao pia upo katika ulimwengu wa roho, na ufalme ya tatu ni ufalme ya wanadamu ambao ndio huu tunaouona katika mwili na ndio huu tunaoishi mimi mimi na wewe.

Na falme hizi zote kila mmoja inayo utendaji kazi wake wenyewe, na nguvu zake, na mamlaka yake yenyewe, na kama zilivyojipanga ile Falme ya kwanza ndiyo yenye nguvu zaidi mbali na nyingine zote ndiyo ya Mungu wetu, kisha hapo chini unafuata ufalme wa giza ambao ndio shetani anaumiliki, na wa mwisho ndio huu wa kwetu sisi wanadamu.

Sasa Yule mwenye nguvu zaidi ndiye mwenye uwezo wa kuingia na kutoka kwenye ufalme wa chini yake. Kwa mfano ufalme wa mbinguni ambao ndio wa Mungu wetu, unaouwezo wa kuamua lolote juu hizi falme mbili za chini, unaouwezo wa kuzitumia au kuziamurisha lolote la kufanya, zinaweza kutumiwa pia kutimiza kusudi Fulani la Mungu kwa muda kwa kipindi fulani. Vivyo hivyo na ufalme wa pili ambao ni wa giza unao nguvu wa kuumurisha ufalme wa chini yake (yaani sisi tunaouishi), kamwe mwanadamu hata afanyaje hawezi kuushinda ufalme wa ibilisi kama hana Mungu, atatawaliwa tu na falme hizo mbili, na ndio maana shetani naye alikuwa na ujasiri wa kujigamba mbele ya Yesu na kumwambia hivi vyote ni vyangu nami humpa yeyote nimtakaye na huku sisi tunajua kuwa dunia na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu. Unadhani shetani alikuwa anajisifia bure?, hapana kwasababu ufalme wake ni kweli una nguvu zaidi ya ufalme wa wanadamu..Hivyo alikuwa na haki ya kusema vile. Hali kadhalika ule ufalme ulio dhaifu hauwezi kuelewa mambo yanayoendelea katika ufalme ulio juu yake wenye nguvu hata uwe na bidii kiasi gani.

Hivyo ufalme wa ibilisi hauwezi kujua lolote linaloendelea katika ufalme wa Mungu, hata atafute kiasi gani hawezi kujua chochote.

Sasa Tukirudi kwenye swali lililoulizwa Je!Mungu anaweza kuleta majibu kupitia nguvu za giza maana nashindwa Kuelewa ninaposoma habari za mfalme Sauli .kupata majibu kwa mwanamke .mwenye pepo.nisaidie hapo.

Jibu ni Ndio Mungu anaoweza kuleta majibu sio tu kupitia ufalme wa giza, bali pia kupitia ufalme wa kibinadamu, Kwasababu yeye yupo mahali popote,.kama hapo juu anavyosema “Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; 10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika".


Lakini yeye kuwa uwezo huo wa kupitisha ujumbe wake kupitia falme hizo zote mbili haimaanishi kuwa unampendeza au umemfikia Mungu kinyume chake ni hukumu inafuata…Pia hiyo haimaanishi kuwa mtu anapokwenda kwa mganga kumtafuta Mungu atamwona, kumbuka wote wanaokwenda kwa waganga hawana lengo la kumtafuta Mungu, hakuna hata mmoja, huwa wanakwenda kutafuta njia za kutatuliwa matatizo yao na wala sio kumtafuta Mungu,kama wangekuwa na lengo la kumtafuta Mungu wasingedhubutu kutumia njia hizo ambazo wanajua kabisa Mungu amezikataa. Hata Sauli mwenyewe hakwenda kumtafuta Mungu kule kwa mganga,bali samweli amsaidie kutatua ufumbuzi wa shida iliyo mbele yake..

Na ndio huko huko Mungu wakati mwingine anatokea kuzungumza na watu, na ikishafika hatua kama hiyo basi ujue kuwa kinachofuata ni hukumu tu kwa kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

Hata wachawi wenyewe huwa wanakutana na sauti ya Mungu huko huko katika shughuli zao zikiwaonya matendo yao, lakini hawawezi kusema siri hizo wanazo wao wenyewe, wale ambao wanakuja kuokolewa ukiwauliza watakuthibitishia hilo kwamba kuna wakati Fulani ambao Mungu alishawahi kuwaonya.

Sio tu Sauli alikwenda kwa waganga..Yupo ambaye alikuwa ni mchawi kabisa biblia inamtaja naye ni Balaamu, nabii wa uongo, huyu naye Mungu alikuwa anazungumza naye akimwonya asiwalaani Israeli, lakini yeye hakusikia sauti ile ya Mungu akatia ukwazo kwa wana wa Israeli, Mungu baadaye akaja kumuua.

Hivyo huo uwezo Mungu anao,lakini sio njia Mungu anayoitumia kuleta majibu ya maombi wa watu. Njia yoyote nje ya Yesu Kristo, yaani njia ya sanamu, njia ya uganga, njia ya sayansi, hakuna hata moja yenyewe uwezo wa kufikisha maombi kwa Mungu, wala usijaribu kufanya hivyo utaangukia hukumu, isiyoponyeka. japo Mungu anaweza kuzitumia hizo kuleta majibu kwa watu tena majibu yaambatanayo na hukumu wala sio jambo jema.

ubarikiwe.
 SWALI 2: Ndugu zangu kwenye biblia kuzaliwa kwa mtu Utaratibu wa Mungu ni mimba inatungishwa kwenye TUMBO LA UZAZI LA MWANAMKE. Swali ni kwamba mtu anayetungisha mimba kwenye "CHOMBO(CHUPA)MAABARA",Huyu ana hatia mbele za Bwana Mungu?
JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu nini maana ya watoto wa kwenye chupa...ikitokea mama anakuwa ana mayai lakini anapata shida kushika mimba huwa kuna uwezekano wa kuyatoa mayai yake kutoka kwenye uzazi na kuyaweka kwenye kifaa maalum kinachoitwa test tube au kwa kiswahili chupa, sasa wakishaliweka hilo yai la mwanamke mule huwa wanachukua mbegu za mwanamume na kuziweka kule kitaalamu ili kurahisisha lile yai kurutubishwa kirahisi...na baada ya lile yai kurutubishwa ndani ya ile chupa wanalichukua lile yai na kulirudisha kwenye tumbo la yule mama na kuendelea na hatua nyingine za ukuaji wa yule mtoto kwenye tumbo la mama yake...hiyo ndio maana ya mtoto wa kwenye chupa, sio kwamba yule mtoto anawekwa kwenye chupa maisha yake yote hapana....ni yai tu ndio linalorutubishiwa kule na kurudishwa mahali husika…kwahiyo hakuna mazingira yoyote nje na tumbo la mama mtoto anaweza kukua..wanadamu hawajafikia huo uwezo. Tumbo la mama ndio sehemu pekee mtoto anaweza kukua mpaka kufikia hatua ya kuzaliwa.

Sasa tukirudi kwenye swali je! ni dhambi yai kurutubishiwa kwenye chombo hicho maalumu nje na tumbo la mama?? Jibu ni kwamba Mungu anaangalia nia ya mtu kufanya vile ni ipi, wengi wanaofanya hivyo unakuta wana matatizo ya kutokushika mimba, kwahiyo njia rahisi wanayoshauriwa na madaktari ni kutumia hiyo njia, hivyo sio dhambi kwasababu nia yao ni kutafuta mtoto sio kuua mtoto. Na hatua hiyo ya kurutubisha yai kwenye chupa ni hatua ya awali kabisa hata mtoto hajaanza kutengenezwa. Ingekuwa kufanya hivyo ni dhambi basi pia kuzaa kwa operation ingekuwa ni dhambi kwasababu sio njia ya asili Mungu aliyoiumba kwa kuzalia watoto. Kwahiyo inategemea na sababu ya mtu kufanya hivyo ni nini?, kama mtu anafanya kwa nia nyingine tofauti na hiyo basi ni dhambi, Lakini ingekuwa ni vizuri zaidi kumtegemea Mungu kuliko madaktari yaani kumwamini Mungu kuliko kutafuta njia mbadala, lakini pia hatuna imani zinazofanana…wako wenye imani kuwa Mungu atawapa watoto pasipo njia hizo na wapo wasio na imani hiyo…Lakini mtu akitumia hiyo njia hafanyi dhambi endapo tu atakuwa na nia njema.

 SWALI 3: Napenda kujua maana na tofauti kati ya MYUNANI, MFARISAYO NA MSADUKAYO.

JIBU: Mafarisayo na Msadukayo chimbuko lao ni moja dini zao zimeegemea katika Torati ya Musa, wote hawaamini maagizo mengine nje ya torati isipokuwa tofauti inakuja katika kuamini kiama cha wafu.. Mafarisayo wanaamini kuwa kuna kiama cha wafu (yaani maisha baada ya kufa, wanaamini yote yaliyoandikwa katika torati hata tumaini ya kuja kwa Masihi duniani) lakini masadukayo hawaamini kama kuna kufufuliwa kwa wafu, wanaamini kuwa mtu akishakufa, amekufa hakuna chochote baada ya hapo, wala hakuna malaika wala ulimwengu wa roho wala mbingu.

Ukisoma Mathayo 22:24-34 utaona Bwana Yesu akiwajibu hao mafarisayo kuhusu mitazamao wao hafifu ya maandiko Na kuwaambia kuwa Mungu asingesema yeye ni Mungu wa Ibrahimu, na Isaya na Yakobo kama watu hao ni wafu sasa. Kwasababu siku zote Mungu si Mungu wa wao bali wa wanaoishi..Hivyo Neno hilo linathibitisha kuwa kiama kipo.

Ukisoma tena Matendo 23 Utaona Mtume Paulo akiyagonganisha madhehebu hayo mawili.

Matendo 23: 23.6 Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo,
akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi
ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu.
23.7 Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina
ya Mafarisayo na Masadukayo,
mkutano ukafarakana.
23.8 Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali
Mafarisayo hukiri yote.
23.9 Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama,
wakateta
, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema
naye, ni nini?
23.10 Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru
askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumle
ta ndani ya ngome.”

Hivyo kwa maandiko hayo utapata kuelewa tofauti ya watu hawa ipo wapi..

MYUNANI: Sio dini au imani, bali ni watu wa taifa la uyunani, kwasasa ni Ugiriki.Hivyo katika agano jipya mahali popote anapotajwa myunani, linalenga watu wa aina mbili, aina ya kwanza ni aidha wayahudi wanaotokea katika nchi za wayunani, na hivyo wanajulikana kama wayunani lakini kiasili ni wayahudi, kwa mfano wale watu waliotaka kumwona Bwana zamani zile ni wayahudi lakini sio wa kuzaliwa Israeli. tunasoma:.

Yohana 12:20 Palikuwa na WAYUNANI kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.21 Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya,wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu

Unaona? Kadhalika pia wale watu waliokuwa Yerusalemu siku ile ya Pentekoste, (Matendo 2) wakishangaa matendo makuu ya Mungu, biblia inasema walikuwa Warparthi na Wamedi na Waelami,n.k. wote hawa hawakuwa watu wa mataifa mengine (yaani watu wasio wayahudi) hapana bali walikuwa ni Wayahudi waliotoka katika hayo mataifa yaliyotajwa hapo,
Na aina ya pili: ni Wayunani ambao asili yao ni Uyunani kabisa, watu wa mataifa. Mfano tunaweza kumwona mwanamke huyu aliyezungumziwa hapa ni myunani lakini hana uyahudi wowote ndani yake:

Marko 7:24 “Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba,akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika.
25 Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake,
akaja akamwangukia miguuni pake.
26 Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika
binti yake.
27 Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto,
na kuwatupia mbwa.
28 Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.
29 Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako.
30 Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo
amekwisha kumtoka.”

Kadhalika tunaona watenda kazi wa Mungu wengine kama Tito, mwanafunzi wa Paulo (Wagalatia 2:3).Na Timotheo (Matendo 16:1) hawa wote biblia inawataja kama ni Wayunani, na sio wayahudi.

Wednesday, January 30, 2019

VITA DHIDI YA MAADUI


Shalom karibu tujifunze Neno la Mungu, Maandiko yanatuambia “kumcha Bwana ni chanzo cha Maarifa”… Maneno ya Yesu Kristo yanafaida kubwa katika maisha zaidi hata tunavyofikiri.  Kwa jinsi tunavyozidi kumcha Bwana maarifa yetu ndivyo yanavyozidi kuongezeka siku baada ya siku, mpaka tunapofikia kiwango kile cha Maarifa cha kumfahamu yeye anachotaka tukifikie sisi kama tunavyosoma katika Waefeso 4:13. 

Nilipita sehemu Fulani, nikapisha na dada mmoja aliyekuwa anaongea na mwenzake, walikuwa wanatembea kwa kasi kidogo lakini nilifanikiwa kusikia moja ya kauli zake  akisema “tumepewa mamlaka ya kukanyaga nge na nyoka…akaendelea kumwambia mwenzake “adui yako akija mbele yako usimsubirishe we mkanyage..kwa maana tumepewa mamlaka hayo ”…Akiwa na maana kuwa mtu akija mbele yako ambaye yupo kinyume chako mdhuru kabla yeye hajakudhuru biblia imeturuhusu kufanya hivyo, tena hakikisha unammaliza kweli kweli.

Niliposikia hivyo nilisikitika sana, nikasema Bwana atusaidie kweli kweli,  
Ndugu yangu nataka nikwambie..katika Agano jipya hatuna adui yoyote ambaye ni Mwanadamu…Adui yetu ni Shetani na majeshi yake, kwa maana kupigana kwetu sisi si juu ya damu na nyama, maandiko yanatuambia hivyo… Vita juu ya damu na nyama vilikuwa katika Agano la kale, ndio maana tunawaona watu kama wakina Daudi, Sulemani, Sauli na wengine wote ndio waliokuwa na maadui ambao ni wanadamu kwasababu, bado walikuwa hawalijui agano lililo bora zaidi. Kwa neema Mungu aliyowapa aliwaruhusu wawaone maadui zao kwa njia ya kibinadamu, lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Tangu Edeni adui wa kwanza wa mwanadamu alikuwa ni shetani.
Kwahiyo baada ya dhambi Mungu aliruhusu tuishi katika vipengele pengele Fulani vya maisha ambavyo vingi havikuwa ni njia kamili au mpango kamili wa Mungu japo aliviruhusu, kwamfano aliruhusu talaka, aliruhusu ndoa za wake wengi. N.k  lakini ulipokuja utimilifu wote ulioletwa wa lile Neno lililofanyika mwili ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo, kwa Neema aliweka mambo yote kama yanavyopaswa yawe katika utimilifu wote..ndio maana Bwana aliwaambia “watu haikuwa hivyo tangu mwanzo”,..wao walikazana kumwambia Bwana mbona Musa alifanya hivi, alisema vile…lakini Kristo alizidi kuwaambia haikuwa hivyo tangu mwanzo..

Na leo jambo ni lile lile watu tunaweza kujiuliza mbona Daudi alikuwa na maadui na aliwaua na aliwalaani… na sisi tufanye hivyo hivyo, lakini Kristo anatuambia haikuwa hivyo tangu mwanzo…haikuwa hivyo tangu mwanzo kujilipiza kisasi, haikuwa hivyo tangu mwanzo kumlaani mwanadamu mwenzako (ambaye tunaona roho ya uadui ipo ndani yake)…Utauliza hayo maneno yanatoka wapi kwenye biblia?..soma
Luka 6:28 "wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi."
Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi”..
38 Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho,na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume,mgeuzie na la pili” 

Hayo ni maneno ya Bwana Yesu mwenyewe..anasema “mmesikia imenenwa….” 

Sasa swali wamesikia kutoka kwa nani? Jibu ni wamesikia kutoka Kwa mababa waliowatangulia ambao ndio hao wakina Musa, Daudi, Eliya na wengine wote…
Ndugu yangu unaposoma kitabu cha Zaburi, pasipo uongozo wa Roho Mtakatifu wa kujua nyakati Mungu alizokuwa anatembea kwa kila nyakati itakupoteza kwasababu ndani ya Zaburi hiyo hiyo kuna sehemu imehalalisha mvinyo, Ndani ya zaburi hiyo hiyo usipokuwa na msaada wa roho kuielewa unaweza ukajifunza chuki na visasi, ndani ya sheria za Musa na torati pasipo msaada wa roho unaweza kujifunza mauaji na kiburi…Na ndani ya hiyo hiyo biblia unaweza kujifunza uasherati kama wengi sasahivi wanavyoitumia kuhalalisha ndoa za mitara.

Sasa tukirudi kwenye suala la “Maadui zetu”…swali ni je! Maadui wetu ni wakina nani sasa?

Kumbuka Tangu mwanzo adui ni Ibilisi biblia inasema hivyo, yeye ndiye atushitakiaye mbele za Mungu mchana na usiku, na ni mfano wa simba angurumaye atafutaye mtu wa kummeza (1 Petro 5:8). Huyo ndio adui yetu wa kwanza na wa mwisho, hivyo kwa kutumia majeshi yake ya mapepo wabaya..ndio anafanya vita na sisi. 

Anayatuma mapepo yake yanawaingia watu, kwahiyo Yule mtu anageuka kuwa ofisi ya shetani kwa kujua au pasipo kujua..ndio hapo unakuta mtu anakuchukia ghafla pasipo sababu, au anakutafutia hila, anaanza kukupiga vita, au kukutafutia madhara, au wivu au anafurahia kuanguka kwako!…au anatafuta namna ya wewe kuiacha imani, sasa chanzo sio Yule mtu, bali ni roho iliyoko ndani yake…roho iliyoko ndani yake ndio roho ya uadui.

Sasa sio jukumu letu sisi kupambana na Yule mtu, kama watu wa agano la kale walivyokuwa wanafanya bali ni jukumu letu kupambana na ile roho inayotenda kazi ndani yake,  Yule mtu yeye ni  kama ofisi tu!! Awe anajua au asiwe anajua.. Watu wa agano la kale kama wakina Daudi walikuwa wanapambana na watu kwasababu bado walikuwa hawajapewa neema ya kujua chanzo cha mambo yote ni wapi lakini sisi tumepewa….

Ndio hapo biblia inatuambia katika Wafilipi 6:11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA, JUU YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO”

Hapo Neno linatuambia “tuweze kuzipinga hila za shetani na sio mwanadamu”.
Sasa namna ya kuipiga na kuikanyaga hii roho ya adui iliyopo ndani ya ndugu zetu!! Namna ya kuitowesha kabisha, na kuiharibu tumepewa silaha madhubuti za kuiangusha, pasipo kuidhuru ile ofisi shetani anayoitumia, maana nia na madhumuni ni kuipiga ile roho na kuiacha ile ofisi huru iokoke ili itumiwe na Mungu kama ofisi ya Nuru. Haleluya!!, sasa silaha za kuipiga ile roho ndio hizi zifuatazo.

Wafilipi 6:13 “Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama..

1)   Basi simameni, hali mmejifunga KWELI VIUNONI- Hakikisha unaifahamu kweli yote ya biblia, unamfahamu Yesu Kristo katika ukweli wote,Maneno ya Mungu kama haya.

2)   Dirii ya Haki kifuani- Hakikisha unauelewa vizuri ufunuo wa kuhesabiwa haki kwa Imani, kwamba sio kwa matendo tunaokolewa bali kwa neema, sio kwa matendo tunaponywa bali kwa neema, si kwa matendo tunapata ulinzi kutoka kwa Mungu bali kwa neema, sio kwa matendo tunampendeza Mungu bali kwa Neema kupitia Yesu Kristo. Hiyo itakusaidia shetani anapoleta mashtaka yake ya kukuhukumu ndani ya moyo wako, au nje unakuwa na mafuta ya kutosha kumshinda hoja zake, na kutokupepeswa na maneno ya mwovu yanapokuja juu yako.


3)    kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani- Hii ni silaha ya tatu madhubuti kabisa ya kuiharibu ile roho ya uadui ndani ya mtu, hatua hii ni ile mtu anapochukua hatua ya kwenda kumhubiria INJILI Yule mtu ambaye roho ya uadui ipo ndani yake, na kumhubiria sio tu kwa maneno bali kwa kielelezo cha matendo, unakwenda kumhubiria habari njema za wokovu, una mwombea, unaonyesha upendo, akikuomba chakula unampa,akikuomba nguo mvike, na hiyo inapelekea  Ile roho iliyoko ndani yake inapungua nguvu kwa kasi sana, na kutengeneza njia ya ushindi wa vita.

4)   Ngao ya Imani –Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, kwa lolote lile shetani atakalolileta, una imani kuwa halitafanikiwa, na zaidi ya yote una Imani kuwa wewe ni mwana wa Mungu mrithi wa ahadi zake, na hakuna chochote kitakachokudhuru, hata jeshi la mapepo kiasi gani,hata waganga wote duniani wakiungana kupambana wewe hakuna jambo lolote litakalofanikiwa kwasababu upo chini ya damu. Na unaimani kuwa  lolote umwombalo Baba atakutendea

5)   Tena ipokeeni chapeo ya wokovu- Chepeo ni HELMET kwa kiingereza, kazi yake ni kulinda sehemu ya kichwa..Na sisi tunaposimama mbele ya Adui yetu shetani, silaha yetu nyingine ni tumaini la Wokovu tulionao, kwamba tumemwamini Yesu Kristo aliyetukomboa kwa damu yake, na kutuahidia ukombozi wa miili yetu, kwahiyo hakuna chochote kitakachoweza kututoa kwake kwa kupitia Roho wake Mtakatifu tumetiwa Muhuri mpaka siku ya ukombozi wetu (Waefeso 4:30). Na huko huko ndio unajifunza kusamehe. Kwasababu unajua na wewe ulisamehewa deni kubwa kushinda hilo la ndugu yako.

6)   Upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu- Hii ndio silaha ya mwisho na ya umuhimu kuliko zote.. ukilifahamu Neno la Mungu, hakuna elimu yoyote ya shetani itakayokupiga chenga, kwasababu shetani naye anayo injili yake ambayo inafanana sana na injili ya Kweli, ambayo kwake nayo ni kama UPANGA anayokatakata nayo watu, ndio ile aliyokuwa anataka kumkata nayo Bwana kule jangwani injili ya “imeandikwa”..lakini Bwana alimshinda kwasababu Neno la Mungu lilikuwa limekaa ndani yake kuliko shetani. Upanga wa Kristo ulikuwa mkali kuliko wa shetani aliweza kumkata shetani kwa kumjua hila zake na njama zake na mawazo yake… Waebrania 4:12 “ Tena Neno la Mungu li hai tena lina nguvu tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo”.alimshinda kwa Neno.

Hizo ndizo silaha 6 Muhimu na pekee za kushindana na Adui yetu shetani. Sasa kumbuka katika vita adui yako na yeye kavaa kama wewe, na yeye ana kweli yake kiunoni, ana dirii yake kifuani, ana chepeo yake kichwani ana injili yake miguuni, na ana upanga wake mkononi amepewa na shetani. Hivyo Ndivyo alivyo shetani ana injiili yake ya uongo ana imani yake ya uongo, ana wokovu wake wa uongo, ana haki yake ya uongo...yote hayo ni kwaajili naye kujilinda,lakini kwasababu sisi tunavyo vya ukweli na vyenye nguvu kuliko vyake tunamshinda. Lakini kama hatuna hata kimoja cha ukweli atatukatakata na upanga wake na kutuweka chini.

Sasa tutajuaje kwamba tumeshinda vita? Tutajua tumeshinda vita vizuri kama tutakuwa tumefanikiwa kumleta Yule mtu kwa Kristo, au tumempandia mbegu ya Kristo ndani yake, Kwasababu Yule ni mtu wa Mungu, anayestahili wokovu kama wengine tu! Kama sisi,  naye pia Mungu hapendi kumwona anakwenda kwenye ziwa la moto, naye anasikia maumivu kama sisi, na anahisia zote kama sisi tulizonazo.

Lakini endapo tukikosa shabaha! Na kuanza kupambana na Yule mtu badala ya kupambana na roho iliyopo ndani yake, na kuanza kumrudishia ubaya, kuanza kumlaani, kuanza kumwombea afe…na kusema Bwana katupa mamlaka ya kukanyaga nge na nyoka kwahiyo tumkanyage yeye kweli kweli, hapo tutakuwa hatujashinda vita bali tumeshindwa vita!! Na kugeuka kuwa vyombo vya shetani.

Na unajua ni sisi tu wakristo ndio hatuna hekima katika ukristo wetu, lakini watu wa ulimwengu huu kama biblia inavyosema wana hekima katika mambo yao…Kwamfano serikali inapotangaza vita dhidi ya UMASKINI, MARADHI na UJINGA..Huwezi kuona inakwenda kupambana na wagonjwa hospitalini, huwezi kuona inaenda kuua wagonjwa na kusema tunapapambana vita dhidi ya maradhi, au huwezi kuona inakwenda kuwaua maskini wa nchi na kusema tunapambana vita dhidi ya umaskini, au huwezi kuona serikali inakwenda kuwaua au kuwafukuza watu wasio na elimu kwa kisingizio cha kupambana vita dhidi ya Ujinga, badala yake utaona itaenda kutafuta suluhisho na tiba kwa watu wake waondokane na umaskini, maradhi na kukosa elimu..Lakini sisi wakristo ndio namba moja kuuwa watu wenye magonjwa ya kiroho, umaskini wa kiroho na ujinga wa kiroho na kusema ni maadui zetu! Yaani Inaonyesha ni jinsi gani hatujielewi!!!

Wakati Fulani Bwana alipokuwa anakwenda Samaria kuhubiri, wenyeji wa mji ule walimkataa, ndipo wanafunzi wake wakamwambia tushushe moto kama Eliya uwaangamize..lakini Bwana hakufanya vile kwasababu alijua tatizo sio hao watu bali ni roho iliyo ndani yao..akawaambia wanafunzi wake Mwana wa Adamu hakuja kuangamiza roho bali kuokoa.
Luka 9: 52 “akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.
53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu.
54 Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?
55 Akawageukia, akawakanya. [AKASEMA, HAMJUI NI ROHO YA NAMNA GANI MLIYO NAYO.]
56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine”

Sasa kama Bwana hakufanya hivyo kwanini sisi tufanye hivyo?? Tutakuwa na roho gani ndani yetu??..bila shaka itakuwa ni roho ya Ibilisi!! Roho ya kuangamiza badala ya kuokoa…

Nataka nikuambie tu ndugu, nge wetu ni shetani na nyoka wetu ni shetani, hao ndio tuliopewa mamlaka ya kuwakanyaga..na hatuwakanyagi kwa maneno bali kwa hizo silaha 6 hapo juu!!..Maombi ya kuwatakia shari ndugu zako acha kuanzia leo, maombi ya kuwalaani wale wanaokuudhi acha kuanzia leo, muhubiri au mwalimu anayekufundisha hivyo anakufundisha uongo na anakuhubiria uongo!! Tena wengine wanaaambiwa watu kabisa waandike majina ya maadui zao wayaweke kwenye maboksi wayaombee wafe!! HAYO NI MAFUNDISHO YA MASHETANI!!..Kwanini usiweke jina la adui yako kwenye boksi umwombee ampe Kristo maisha yake? Kuliko kumwombea afe!!.Fikiria ni mama yako anaombewa afe na mtu mwingine wewe utafurahia kitendo hicho?. Mambo yale tunayotaka tutendewe sisi ndio tutendee wengine Bwana alitufundisha hivyo.
Warumi 12:14 “Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.”
Ni maombi yangu kuwa Bwana atakujalia kuyaona hayo na zaidi ya hayo.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na Bwana atakubariki.
Kwa mpangalio mzuri wa masomo haya tembelea website yetu. |www.wingulamashahidi.org|

Tuesday, January 29, 2019

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:

Shalom! Karibu tujifunze Neno la Mungu,leo tutajifunza siri mojawapo ya kipekee iliyolala katika kitabu cha cha Ruthu. Kitabu hichi ni chepesi kukisoma, kwasababu ni kitabu kinachoelezea historia ya maisha ya watu zaidi kuliko unabii, hivyo nakushauri mahali ulipo chukua biblia yake ukipitie kwanza binafsi,kisha tuendelee ni kitabu chenye sura 4 fupi zinazoeleweka, hivyo ni vema ukafanya hivyo ili tuende pamoja.

Kitabu hichi kinaanzana na habari ya mtu anayeitwa Elimeleki, ambaye huyu alikuwa akiishi Israeli zamani kipindi cha Waamuzi, na biblia inatuambia siku njaa ilipokuja katika mji ule, Elimeleki alifunga safari kwenda nchi ya jirani kuishi huko yeye pamoja na mke wake aliyeitwa Naomi pamoja na wana wake wawili wa kiume..Lakini baada ya Muda kidogo mambo yalibadilika Elimeleki alikufa na kumwacha mke wake akiwa mjane na watoto wake wawili katika nchi ya ugenini..Na Baadaye kidogo watoto wake wote wawili walibahatika kupata wake wazuri tu, lakini kwa bahati mbaya, nao pia walifariki wakiwa bado hawajapata watoto na wale wanawake, Hivyo yule mwanamke mjane Naomi hakufanikiwa kuambulia chochote, si mume, si watoto, wala si wajukuu, na hapa sasa ameshakuwa mzee sana hawezi kubeba mimba tena, hata angesema azae asingeweza tena kwani muda umeshakwenda amekaa ugenini zaidi ya miaka 10, hata hana wa kumsaidia tena, nguvu zake zimeisha kilichobakia ni kurudi tu katika nchi yake Israeli kwenda kumalizia siku zake za kuishi.

Kabla hatujaendelea mbele Embu jiulize, zamani zile za kipindi cha waamuzi kulikuwa na watu wengi mashujaa tu kama tunavyokisoma, kulikuwa na wajane wengi tu, kulikuwa na watu wengi wema tu, Hivyo habari zao zingeweza kuandikwa kama mojawapo ya kumbukumbuku nzuri kama funzo kwa ajili ya vizazi vya mbeleni, lakini ni kwanini habari za watu wengine hazijaandikwa isipokuwa za huyu mtu mmoja tu Elimeleki na familia yake ndizo zimenakiliwa hapa, na kuwekwa kama vitabu vitakatifu?.. Njia za Mungu sio njia zetu, Naomi hakufahamu kuwa japo maisha yake yalionekena kuwa ni ya bahati mbaya mbele za watu, maisha ya kusahauliwa, mtu ambaye sasa hana kumbukumbu tena, ambaye aliyekuwa amefanikiwa sana lakini sasa si kitu, hana mume,wala watoto,wala wajukuu, wala mali, wala chochote kile..hakujua kuwa kumbe Mungu alikuwa anaandika kwa kupitia maisha yake ufunuo mzito ambao ndio huo unakuja kutusaidia hata sisi watu ambao hatukustahili kupata neema za kumjua Kristo. Kwahiyo wakati mwingine maisha ya mtu yanaweza kubeba ufunuo Fulani wa Roho.

Lakini tukiendelea kusoma habari tunaona Naomi sasa anakusudia kurudi katika nchi yake mpweke,mwenye uchungu mwingi, na hapa tunaona anawaambia wale wakwe zake, ambao mwanzoni walikuwa wameolewa na watoto wake wawili kwamba kila mmoja sasa awe na amani kurudi kwa jamaa zake wakaolewe na kufanikiwa na kuishi maisha ya furaha siku zote za maisha yao. Lakini tunaona wale wanawake wawili mwanzoni wote walikataa kumwacha Naomi peke yake, Lakini hilo halikumfanya Naomi aache kuwasihi wasifuatane naye, kwani hakutaka mtu yeyote abebe wake wowote kwa kulazimishwa, hivyo aliwabariki na kuwaomba warudi kwa jamaa zao wenyewe, lakini kama tunavyosoma habari, moyo wa Ruthu ulikuwa thabiti kuliko wa Orpa, Yeye Orpa baadaye alikubali kurudi kwa jamaa zake lakini Ruthu hakutaka kinyume chake alikuwa tayari kuambatana na Naomi popote aendapo kwa gharama zozote, alikubali kuchukuliana na gharama zote.

Tunasoma:

Ruthu 1: 11 “Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu?
12 Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume;
13 je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa Bwana umetoka juu yangu.
14 Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthuu akaambatana naye.
15 Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako.
16 Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu;
17 Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami.
18 Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye”.
Sasa ukiendelea kusoma habari huko mbeleni utaona Ruthu alikubali kuondoka na Naomi katika umaskini wao, Ruthu asijue anapoelekea, asijue wakifika watapokelewa na nini, Ruthu akimtazama mwanamke yule kashakuwa mzee, na yeye bado ni binti kijana, ambaye anao uwezo wa kwenda kuolewa tena, ameacha vijana wazuri wenye mali katika nchi yake mwenyewe, pengine mabinti wenzake wanamkebehi wakimwambia hivi wewe umelogwa na kale kabibi? Kwani katakupa nini? mwangalie mwenzako Orpa, aliona mbele kuwa huko hakuna tena uelekeo wa maisha, zaidi ni kuzeeshwa tu akili za wazee na kuwahudumia tu, na mwisho wa siku kuwa kama mjakazi wao..Isitoshe anakwenda mahali asipopajua, wala hajawahi kuwafahamu watu wa huko, pengine walimwambia Unakwenda kupotea tu huko na mwisho wa siku utajuta..Wewe bado binti mdogo hata bado hujazaa, unakwenda wapi?

Lakini Ruthu hakujali kuipoteza nafsi yake kuwa ni kitu cha maana sana, kuliko kujitenga na mama wa mume wake marehemu, hivyo aliendelea kufuatana naye tu katika taabu zote kama alivyoapa.

Kumbuka ni sheria iliyokuwa imetolewa na Mungu katika Israeli, kwamba mtu yeyote aliye myahudi asioe mwanamke ambaye si myahudi, kadhalika ni mwiko pia kwa mwanamke wa Kiyahudi kuolewa na mtu wa mataifa, Lakini hapa tunaona Naomi akirudi katika nchi yake mwenyewe akiwa amemwambulia mtu mmoja tu.. Pengine wale ndugu zake waliokuwa wamebaki Israeli walitazamia Elimeleki pamoja na Naomi watarudi na mali nyingi, kondoo, mbuzi, ngamia pamoja wa watoto wao na wajukuu wengi, na wajakazi wengi. Lakini hapa anaonekana Naomi peke yake, na binti mmoja wa kimataifa, na tena kibaya zaidi ni heri angekuwa kijakazi wake, lakini kumbe ni mke wa mtoto wake, jambo ambalo ni machukizo makubwa kwa Israeli.

Lakini kwa jinsi Ruthu tabia yake ilivyokuwa njema, na ya kupendeza watu wote, na kwa ukarimu wake wote aliomfanyia Naomi bibi yake,basi habari zake zikasikika katikati ya jamaa za Naomi. Na siku moja alipokuwa anakwenda kuokota masazo ya nafaka kwenye mashamba ya watu matajiri, aliingia katika shamba la mtu mmoja mkuu sana wa mji huo jina lake Boazi, ndipo Boazi akamwona na kuulizia habari zake, na kuambiwa kuwa huyu ni binti wa Naomi. Wakati huo huo Boazi na Elimeleki mumewe Naomi walikuwa ni mtu na kaka yake. Hivyo ukiendelea kusoma habari hiyo mpaka mwisho kwa kuwa sasa hatuna nafasi ya kueleza habari yote, utaona kuwa mwisho wa siku Ruthu ambaye ni mwanamke wa kimataifa anakuja kuolewa na Boazi mtu mkuu wa Uzao wa kifalme, na ndiye kwa kupitia huyu Mfalme Daudi alitokea. Daudi ni kitukuu cha RUTHU.

Sasa kama tunavyojua mambo yote yanayotokea katika agano la kale ni kivuli cha mambo yanayoendelea katika agano jipya, habari yote ya Naomi na Ruthu, ni habari ya Kristo na bibi-arusi wake ambayo Mungu alikuwa anaichora kwa kupitia maisha ya hawa watu.

Kumbuka YESU Kristo alishuka kutoka mbinguni na utajiri mkubwa, kama Mfalme, aliyeacha enzi na mamlaka juu mbinguni, alikuja kwa watu wake Wayahudi, na hivyo alikaa nao, alikula nao,mfano tu wa Naomi jinsi alivyotoka Israeli na mumewe na watoto wake, na mali zao nyingi na kukaa katika nchi ya ugenini Moabu. Lakini haikuwa vile kwa Naomi kama alivyotarajia, Mungu alimpiga na kumwacha pasipo kitu chochote na kubakia yeye tu alivyo. Picha kamili ya Bwana wetu Yesu kristo jinsi alivyopitia, ilimpasa yeye awe mfalme kwa wakati ule aliokuja ulimwenguni kwa mara ya kwanza lakini Mungu hakufanya hivyo kwa wakati ule, kinyume chake, alikataliwa, watu walimwona kuwa si kitu, walimtupa, walimtemea mate, walimpiga mijeledi, walizipiga kura nguo zake, walimsulibisha jaribu kufikiria mtu ambaye angepaswa awe mfalme lakini sasa anakuwa kituko kitu cha kuchekesha hana lolote tena..

Biblia inasema hivi juu yake: 
“2 Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.
3 ALIDHARAULIWA NA KUKATALIWA NA WATU; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; NA KAMA MTU AMBAYE WATU HUMFICHA NYUSO ZAO, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.(Isaya 53)”….

8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; NA MAISHA YAKE NI NANI ATAKAYEISIMULIA? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
9 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
10 Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake;
11 Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao.
12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji…

Unaona biblia inasema maisha yake Bwana Yesu ni nani awezaye uyasimulia?..Jinsi yalivyoonekana kuwa ya ajabu mbele za watu waliomwona kama vile maisha ya Naomi. Lakini kumbe Mungu alifanyia vile Naomi kwa makusudi ili ampate RUTHU haleluya..

Angalia ni upendo mkuu namna gani huo, kumgharimu Mungu kwenda kuyaharibu maisha na raha ya mwingine, kwa ajili ya mtu mmoja asiyestahili kupata lolote asiyekuwepo hata katika mzao wa kiyahudi huko mbali katika nchi za wachawi na waabudu masanamu…Kwani hakukuwa na wanawake wazuri Israeli, wenye kumcha Mungu wakati ule, walikuwepo, lakini kwa jinsi Rehema za Mungu zilivyokuwa nyingi, alikwenda kumtafutia Boazi mke mwema katika nchi za mataifa mabovu, tena kwa kuyaharibu kwanza maisha ya Naomi kwa kunyang’anya kila kitu pamoja na watoto wake ili tu Ruthu apate mlango wa kumwendea BOAZI.

Ndugu yangu, mimi na wewe hatukustahili kuitwa bibi-arusi wa Kristo hata kidogo..Wayahudi walistahili heshima hiyo, kwani wao ndio waliochanguliwa na Mungu tangu awali, Lakini Mungu alituhurumia sisi zaidi, na kuja kutuchagua kututoa sisi katikati ya mataifa, Na zaidi ya yote hakuja kututwaa pasipo gharama, hapana bali alimtoa mwanawe wa pekee ambaye ndiye kama Naomi wetu, kuja kuteseka kupoteza kila kitu alichokuwa nacho, kupigwa, kutemewa mate kudharauliwa, kwa ajili yetu, na mwisho wa siku kufa, na kufufuka na alipofufuka alitaka sasa kurudi kwa Baba yake juu mbinguni, katika makao yake aliyotoka huko kama vile Naomi alivyotaka kurudi kwa watu wa jamaa zake.

Lakini sasa tendo la sisi kumfuata Kristo lipo mikononi mwetu, na si mikononi mwake,..Je! tutaamua kuanza naye safari ya kwenda kwa BOAZI wetu mbinguni? Au tutataka kuwa kama Orpa, kuona kuwa Naomi hana faida yoyote kwetu, Yesu Kristo hana chochote cha kutugawia, tukimfuata tutaendelea kuwa maskini, tukimfuata tutakuwa washamba, tukimfuata kampani zetu za Disco na vilabuni zitatuacha, tukimfuata vimini vyetu tutavitupa, tukimfuata, tutaonekana vibibi,. tukimfuata tutakwenda kupotea moja kwa moja na kuwa vichaa..

Ndugu fahamu kuwa huu wakati ambao Bwana ameshakulipia gharama zote, hatakuja tena kukulazimisha, bali kinyume chake atakupa uhuru wa kuchagua, je! utakuwa tayari kujitwika msalaba wako kumfuata kama Ruthu au kuendelea kubaki katika dunia kama Orpa. Ukitaka kubaki kama Orpa ni sawa lakini kumbuka BOAZI yupo Israeli anamsubiria yule aliyetayari kumtii NAOMI, na maagizo yake yote.

Hivyo huu ni wakati wako wa kupiga gharama, mambo ambayo Wayahudi wameyakosa japo walikuwa wanayatazamia tangu zamani yamepewa wewe, mfano tu wa wale wajakazi wa Boazi waliokuwa wanafanya kazi shambani mwake miaka yote, hata mmoja hakuna aliyekuja kuolewa na Boazi isipokuwa mgeni wa mbali wa Ruthu. Ni kwasababu gani?..Ni kwasababu NAOMI ndiye aliyekuwa na SIRI ya jinsi ya kumwingia BOAZI na siri hiyo alipewa Ruthu peke yako.
Na ndio maana Bwana alimaanisha kuwaambia makutana maneno haya..

Luka 9.23 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.
24 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.
25 Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?”.
Na alisema “Mimi ndimi njia na kweli na Uzima mtu hafiki kwa Baba ila kwa njia yake yeye”
Je! leo hii utachukua uamuzi wa kumfata Kristo? kama vile Ruthu alivyojitoa kikamilifu mpaka kuwa tayari kuacha vyote alivyonavyo kwa ajili ya mkwe wake?.

Hizi ni siku za mwisho Tubu ukabatizwe, moja ya hizi siku bibi-arusi wa Kristo atanyakuliwa kwenda kwenye karamu iliyoandaliwa huko juu ya Mungu mwenyewe, watakaofika huko ndugu si kila mtu anayejiita ni mkristo halafu maisha yake yanaonyesha kabisa hajachukua msalaba wake kumfauta Kristo, mguu mmoja upo nje, mwingine ndani, watakaokwenda kwenye unyakuo ni wachache sana, ni kikundi kidogo sana mfano wa Ruthu pekee yake, wale walioamua kumfuata Kristo kikweli kweli pasipo kuangalia mbele wala nyuma, Nawe usiwe ni mmojawapo wa watakaokosa karamu hiyo. Ni heri upoteze kila kitu sasa kuliko kuikosa karamu ya mwana-kondoo.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.