Shalom karibu tujifunze Neno la Mungu, Maandiko yanatuambia
“kumcha Bwana ni chanzo cha Maarifa”… Maneno ya Yesu Kristo yanafaida kubwa
katika maisha zaidi hata tunavyofikiri. Kwa jinsi tunavyozidi kumcha Bwana maarifa
yetu ndivyo yanavyozidi kuongezeka siku baada ya siku, mpaka tunapofikia
kiwango kile cha Maarifa cha kumfahamu yeye anachotaka tukifikie sisi kama
tunavyosoma katika Waefeso 4:13.
Nilipita sehemu Fulani, nikapisha na dada mmoja aliyekuwa
anaongea na mwenzake, walikuwa wanatembea kwa kasi kidogo lakini nilifanikiwa
kusikia moja ya kauli zake akisema
“tumepewa mamlaka ya kukanyaga nge na nyoka”…akaendelea kumwambia mwenzake
“adui yako akija mbele yako usimsubirishe we mkanyage..kwa maana tumepewa
mamlaka hayo ”…Akiwa na maana kuwa mtu akija mbele yako ambaye yupo kinyume
chako mdhuru kabla yeye hajakudhuru biblia imeturuhusu kufanya hivyo, tena
hakikisha unammaliza kweli kweli.
Niliposikia hivyo nilisikitika sana, nikasema Bwana
atusaidie kweli kweli,
Ndugu yangu nataka nikwambie..katika Agano jipya hatuna adui
yoyote ambaye ni Mwanadamu…Adui yetu ni Shetani na majeshi yake, kwa maana
kupigana kwetu sisi si juu ya damu na nyama, maandiko yanatuambia hivyo… Vita
juu ya damu na nyama vilikuwa katika Agano la kale, ndio maana tunawaona watu
kama wakina Daudi, Sulemani, Sauli na wengine wote ndio waliokuwa na maadui
ambao ni wanadamu kwasababu, bado walikuwa hawalijui agano lililo bora zaidi.
Kwa neema Mungu aliyowapa aliwaruhusu wawaone maadui zao kwa njia ya kibinadamu,
lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Tangu Edeni adui wa kwanza wa mwanadamu
alikuwa ni shetani.
Kwahiyo baada ya dhambi Mungu aliruhusu tuishi katika
vipengele pengele Fulani vya maisha ambavyo vingi havikuwa ni njia kamili au
mpango kamili wa Mungu japo aliviruhusu, kwamfano aliruhusu talaka, aliruhusu
ndoa za wake wengi. N.k lakini ulipokuja
utimilifu wote ulioletwa wa lile Neno lililofanyika mwili ambaye ni Bwana wetu
Yesu Kristo, kwa Neema aliweka mambo yote kama yanavyopaswa yawe katika
utimilifu wote..ndio maana Bwana aliwaambia “watu haikuwa hivyo tangu mwanzo”,..wao
walikazana kumwambia Bwana mbona Musa alifanya hivi, alisema vile…lakini Kristo
alizidi kuwaambia haikuwa hivyo tangu mwanzo..
Na leo jambo ni lile lile watu tunaweza kujiuliza mbona
Daudi alikuwa na maadui na aliwaua na aliwalaani… na sisi tufanye hivyo hivyo, lakini
Kristo anatuambia haikuwa hivyo tangu mwanzo…haikuwa hivyo tangu mwanzo
kujilipiza kisasi, haikuwa hivyo tangu mwanzo kumlaani mwanadamu mwenzako
(ambaye tunaona roho ya uadui ipo ndani yake)…Utauliza hayo maneno yanatoka
wapi kwenye biblia?..soma
Luka 6:28 "wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi."
Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi”..
38 Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho,na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume,mgeuzie na la pili”
Hayo ni maneno
ya Bwana Yesu mwenyewe..anasema “mmesikia imenenwa….”
Sasa swali
wamesikia kutoka kwa nani? Jibu ni wamesikia kutoka Kwa mababa waliowatangulia ambao
ndio hao wakina Musa, Daudi, Eliya na wengine wote…
Ndugu yangu
unaposoma kitabu cha Zaburi, pasipo uongozo wa Roho Mtakatifu wa kujua nyakati
Mungu alizokuwa anatembea kwa kila nyakati itakupoteza kwasababu ndani ya
Zaburi hiyo hiyo kuna sehemu imehalalisha mvinyo, Ndani ya zaburi hiyo hiyo
usipokuwa na msaada wa roho kuielewa unaweza ukajifunza chuki na visasi, ndani
ya sheria za Musa na torati pasipo msaada wa roho unaweza kujifunza mauaji na kiburi…Na
ndani ya hiyo hiyo biblia unaweza kujifunza uasherati kama wengi sasahivi wanavyoitumia
kuhalalisha ndoa za mitara.
Sasa tukirudi
kwenye suala la “Maadui zetu”…swali ni je! Maadui wetu ni wakina nani sasa?
Kumbuka Tangu
mwanzo adui ni Ibilisi biblia inasema hivyo, yeye ndiye atushitakiaye mbele za
Mungu mchana na usiku, na ni mfano wa simba angurumaye atafutaye mtu wa kummeza
(1 Petro 5:8). Huyo ndio adui yetu wa kwanza na wa mwisho, hivyo kwa kutumia
majeshi yake ya mapepo wabaya..ndio anafanya vita na sisi.
Anayatuma
mapepo yake yanawaingia watu, kwahiyo Yule mtu anageuka kuwa ofisi ya shetani
kwa kujua au pasipo kujua..ndio hapo unakuta mtu anakuchukia ghafla pasipo
sababu, au anakutafutia hila, anaanza kukupiga vita, au kukutafutia madhara, au
wivu au anafurahia kuanguka kwako!…au anatafuta namna ya wewe kuiacha imani, sasa
chanzo sio Yule mtu, bali ni roho iliyoko ndani yake…roho iliyoko ndani yake
ndio roho ya uadui.
Sasa sio jukumu
letu sisi kupambana na Yule mtu, kama watu wa agano la kale walivyokuwa
wanafanya bali ni jukumu letu kupambana na ile roho inayotenda kazi ndani yake, Yule mtu yeye ni kama ofisi tu!! Awe anajua au asiwe anajua.. Watu
wa agano la kale kama wakina Daudi walikuwa wanapambana na watu kwasababu bado
walikuwa hawajapewa neema ya kujua chanzo cha mambo yote ni wapi lakini sisi
tumepewa….
Ndio hapo
biblia inatuambia katika Wafilipi 6:11 “ Vaeni silaha zote za Mungu, mpate
kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama;
BALI NI JUU YA FALME NA MAMLAKA, JUU YA WAKUU WA GIZA HILI, JUU YA MAJESHI YA
PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO”
Hapo Neno
linatuambia “tuweze kuzipinga hila za shetani na sio mwanadamu”.
Sasa namna ya
kuipiga na kuikanyaga hii roho ya adui iliyopo ndani ya ndugu zetu!! Namna ya
kuitowesha kabisha, na kuiharibu tumepewa silaha madhubuti za kuiangusha,
pasipo kuidhuru ile ofisi shetani anayoitumia, maana nia na madhumuni ni
kuipiga ile roho na kuiacha ile ofisi huru iokoke ili itumiwe na Mungu kama
ofisi ya Nuru. Haleluya!!, sasa silaha za kuipiga ile roho ndio hizi zifuatazo.
Wafilipi 6:13 “Kwa
sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu,
na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama..
1)
Basi simameni, hali mmejifunga KWELI
VIUNONI- Hakikisha unaifahamu kweli yote ya biblia, unamfahamu Yesu Kristo
katika ukweli wote,Maneno ya Mungu kama haya.
2)
Dirii ya Haki kifuani- Hakikisha
unauelewa vizuri ufunuo wa kuhesabiwa haki kwa Imani, kwamba sio kwa matendo
tunaokolewa bali kwa neema, sio kwa matendo tunaponywa bali kwa neema, si kwa
matendo tunapata ulinzi kutoka kwa Mungu bali kwa neema, sio kwa matendo tunampendeza
Mungu bali kwa Neema kupitia Yesu Kristo. Hiyo itakusaidia shetani anapoleta
mashtaka yake ya kukuhukumu ndani ya moyo wako, au nje unakuwa na mafuta ya kutosha
kumshinda hoja zake, na kutokupepeswa na maneno ya mwovu yanapokuja juu yako.
3)
kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya
amani- Hii ni silaha ya tatu madhubuti kabisa ya kuiharibu ile roho ya uadui
ndani ya mtu, hatua hii ni ile mtu anapochukua hatua ya kwenda kumhubiria INJILI
Yule mtu ambaye roho ya uadui ipo ndani yake, na kumhubiria sio tu kwa maneno
bali kwa kielelezo cha matendo, unakwenda kumhubiria habari njema za wokovu,
una mwombea, unaonyesha upendo, akikuomba chakula unampa,akikuomba nguo mvike, na
hiyo inapelekea Ile roho iliyoko ndani
yake inapungua nguvu kwa kasi sana, na kutengeneza njia ya ushindi wa vita.
4)
Ngao ya Imani –Imani ni kuwa na
uhakika wa mambo yatarajiwayo, kwa lolote lile shetani atakalolileta, una imani
kuwa halitafanikiwa, na zaidi ya yote una Imani kuwa wewe ni mwana wa Mungu
mrithi wa ahadi zake, na hakuna chochote kitakachokudhuru, hata jeshi la mapepo
kiasi gani,hata waganga wote duniani wakiungana kupambana wewe hakuna jambo
lolote litakalofanikiwa kwasababu upo chini ya damu. Na unaimani kuwa lolote umwombalo Baba atakutendea
5)
Tena ipokeeni
chapeo ya wokovu- Chepeo ni HELMET kwa kiingereza, kazi yake ni kulinda sehemu
ya kichwa..Na sisi tunaposimama mbele ya Adui yetu shetani, silaha yetu
nyingine ni tumaini la Wokovu tulionao, kwamba tumemwamini Yesu Kristo
aliyetukomboa kwa damu yake, na kutuahidia ukombozi wa miili yetu, kwahiyo
hakuna chochote kitakachoweza kututoa kwake kwa kupitia Roho wake Mtakatifu
tumetiwa Muhuri mpaka siku ya ukombozi wetu (Waefeso 4:30). Na huko huko ndio
unajifunza kusamehe. Kwasababu unajua na wewe ulisamehewa deni kubwa kushinda
hilo la ndugu yako.
6) Upanga wa Roho
ambao ni neno la Mungu- Hii ndio silaha ya mwisho na ya umuhimu kuliko zote..
ukilifahamu Neno la Mungu, hakuna elimu yoyote ya shetani itakayokupiga chenga,
kwasababu shetani naye anayo injili yake ambayo inafanana sana na injili ya
Kweli, ambayo kwake nayo ni kama UPANGA anayokatakata nayo watu, ndio ile
aliyokuwa anataka kumkata nayo Bwana kule jangwani injili ya
“imeandikwa”..lakini Bwana alimshinda kwasababu Neno la Mungu lilikuwa limekaa ndani
yake kuliko shetani. Upanga wa Kristo ulikuwa mkali kuliko wa shetani aliweza
kumkata shetani kwa kumjua hila zake na njama zake na mawazo yake… Waebrania
4:12 “ Tena Neno la Mungu li hai tena lina nguvu tena lina ukali kuliko upanga
uwao wote ukatao kuwili tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo
na mafuta yaliyomo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya
moyo”.alimshinda kwa Neno.
Hizo ndizo silaha 6 Muhimu na pekee
za kushindana na Adui yetu shetani. Sasa kumbuka katika vita adui yako na yeye
kavaa kama wewe, na yeye ana kweli yake kiunoni, ana dirii yake kifuani, ana
chepeo yake kichwani ana injili yake miguuni, na ana upanga wake mkononi
amepewa na shetani. Hivyo Ndivyo alivyo shetani ana injiili yake ya uongo ana
imani yake ya uongo, ana wokovu wake wa uongo, ana haki yake ya uongo...yote
hayo ni kwaajili naye kujilinda,lakini kwasababu sisi tunavyo vya ukweli na
vyenye nguvu kuliko vyake tunamshinda. Lakini kama hatuna hata kimoja cha
ukweli atatukatakata na upanga wake na kutuweka chini.
Sasa tutajuaje kwamba tumeshinda
vita? Tutajua tumeshinda vita vizuri kama tutakuwa tumefanikiwa kumleta Yule mtu
kwa Kristo, au tumempandia mbegu ya Kristo ndani yake, Kwasababu Yule ni mtu wa
Mungu, anayestahili wokovu kama wengine tu! Kama sisi, naye pia Mungu hapendi kumwona anakwenda
kwenye ziwa la moto, naye anasikia maumivu kama sisi, na anahisia zote kama
sisi tulizonazo.
Lakini endapo tukikosa shabaha! Na
kuanza kupambana na Yule mtu badala ya kupambana na roho iliyopo ndani yake, na
kuanza kumrudishia ubaya, kuanza kumlaani, kuanza kumwombea afe…na kusema Bwana
katupa mamlaka ya kukanyaga nge na nyoka kwahiyo tumkanyage yeye kweli kweli, hapo
tutakuwa hatujashinda vita bali tumeshindwa vita!! Na kugeuka kuwa vyombo vya
shetani.
Na unajua ni sisi tu wakristo ndio
hatuna hekima katika ukristo wetu, lakini watu wa ulimwengu huu kama biblia
inavyosema wana hekima katika mambo yao…Kwamfano serikali inapotangaza vita
dhidi ya UMASKINI, MARADHI na UJINGA..Huwezi kuona inakwenda kupambana na
wagonjwa hospitalini, huwezi kuona inaenda kuua wagonjwa na kusema tunapapambana
vita dhidi ya maradhi, au huwezi kuona inakwenda kuwaua maskini wa nchi na
kusema tunapambana vita dhidi ya umaskini, au huwezi kuona serikali inakwenda
kuwaua au kuwafukuza watu wasio na elimu kwa kisingizio cha kupambana vita
dhidi ya Ujinga, badala yake utaona itaenda kutafuta suluhisho na tiba kwa watu
wake waondokane na umaskini, maradhi na kukosa elimu..Lakini sisi wakristo ndio
namba moja kuuwa watu wenye magonjwa ya kiroho, umaskini wa kiroho na ujinga wa
kiroho na kusema ni maadui zetu! Yaani Inaonyesha ni jinsi gani hatujielewi!!!
Wakati Fulani Bwana alipokuwa
anakwenda Samaria kuhubiri, wenyeji wa mji ule walimkataa, ndipo wanafunzi wake
wakamwambia tushushe moto kama Eliya uwaangamize..lakini Bwana hakufanya vile
kwasababu alijua tatizo sio hao watu bali ni roho iliyo ndani yao..akawaambia
wanafunzi wake Mwana wa Adamu hakuja kuangamiza roho bali kuokoa.
Luka 9: 52 “akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu.54 Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?55 Akawageukia, akawakanya. [AKASEMA, HAMJUI NI ROHO YA NAMNA GANI MLIYO NAYO.]56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine”
Sasa kama Bwana hakufanya hivyo
kwanini sisi tufanye hivyo?? Tutakuwa na roho gani ndani yetu??..bila shaka
itakuwa ni roho ya Ibilisi!! Roho ya kuangamiza badala ya kuokoa…
Nataka nikuambie tu ndugu, nge wetu
ni shetani na nyoka wetu ni shetani, hao ndio tuliopewa mamlaka ya
kuwakanyaga..na hatuwakanyagi kwa maneno bali kwa hizo silaha 6 hapo juu!!..Maombi
ya kuwatakia shari ndugu zako acha kuanzia leo, maombi ya kuwalaani wale
wanaokuudhi acha kuanzia leo, muhubiri au mwalimu anayekufundisha hivyo anakufundisha
uongo na anakuhubiria uongo!! Tena wengine wanaaambiwa watu kabisa waandike
majina ya maadui zao wayaweke kwenye maboksi wayaombee wafe!! HAYO NI
MAFUNDISHO YA MASHETANI!!..Kwanini usiweke jina la adui yako kwenye boksi
umwombee ampe Kristo maisha yake? Kuliko kumwombea afe!!.Fikiria ni mama yako
anaombewa afe na mtu mwingine wewe utafurahia kitendo hicho?. Mambo yale
tunayotaka tutendewe sisi ndio tutendee wengine Bwana alitufundisha hivyo.
Warumi 12:14 “Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.”
Ni maombi yangu kuwa Bwana
atakujalia kuyaona hayo na zaidi ya hayo.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa
wengine na Bwana atakubariki.
Kwa mpangalio mzuri wa masomo haya tembelea website yetu. |www.wingulamashahidi.org|
No comments:
Post a Comment