Je! Unafahamu yatakayotokea muda mfupi sana kabla ya kuondoka kwetu kwenda kumlaki Bwana mawinguni?..Ni kweli unyakuo utakuja tu ghafla kwa watakatifu wa Mungu?, Kama haufahamu Biblia ilishatupa mwangaza juu ya suala hilo tunasoma katika;
1Wathesalonike 5: 1 “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.4 BALI NINYI, NDUGU, HAMMO GIZANI, HATA SIKU ILE IWAPATE KAMA MWIVI.5 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu”.
Unaona hapo maandiko yanaeleza wazi kabisa, siku ile itakuwa kama mwivi kwa wale mataifa(wasio watakatifu) wasiomjua Mungu, kwasababu wao wapo gizani siku zote na usingizi wa mambo ya ulimwengu huu umewalemea, lakini kwa watakatifu wa Mungu, muda mfupi kabla ya siku ya unyakuo kufika watafahamu, na hii ni kutokana na matukio ambayo yatakuwa yanaambatana nao katika siku ile.. Ni kweli biblia haijaeleza siku wala saa lakini imetoa majira(dalili) za kuja kwake, na hizi dalili zipo za ndani na za nje, Sasa za nje ndio kama hizi tunazozifahamu mfano, matetemeko, vita, manabii wa uongo, mji wa Israeli, chukizo la uharibifu n.k…Lakini za ndani zinahusu Ishara inayomuhusu Bibi-arusi wa Kristo peke yake, na hizo zipo tatu,
Leo tutazungumzia moja ya hatua (Ishara) ambayo ni ya mwisho kabisa, itakayowafanya watakatifu sasa wafahamu kuwa siku yao ya kuondoka imefika. Biblia imeeleza wazi unyakuo utaambatana na hatua tatu kuu. 1) MWALIKO WA BWANA, 2) ya pili ni SAUTI YA MALAIKA MKUU, 3) na ya tatu ni PARAPANDA YA MUNGU..
Hatua mbili kati ya hizo tulishazielezea kwa undani katika masomo yaliyotangulia, kama hujazijua unaweza ukazifuatilia kwenye somo linaloitwa UNYAKUO
Lakini leo tutamalizia na hatua ya mwisho ambayo ni PARAPANDA YA MUNGU, hii ni Ishara ya mwisho, kama tunavyoweza kuisoma katika…
1Wathesalonike 4: 13 “Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini.14 Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye.15 Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti.16 Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na MWALIKO, na SAUTI YA MALAIKA MKUU, na PARAPANDA YA MUNGU; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza.17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.18 Basi, farijianeni kwa maneno hayo”.
Sasa wakwanza watakaoisikia sauti ya Bwana hawatakuwa watakatifu walio hai, bali ni wale watakatifu waliotangulia kulala mautini, wakati huo wakiwa huko PEPONI walipo wataisikia sauti ya Bwana ikiwaita kutoka makaburini ikiwaambia wakati umefika wa kutoka huko, kama kipindi kile Lazaro aliposikia sauti ya Bwana ikimwita kutoka makaburini ikimwambia,, “Lazaro njoo huku nje”(Yohana 11) Kadhalika sauti hii hii itasikika tena kwa wale watakatifu waliokuwa wamekufa katika Bwana, kama Bwana Yesu alivyosema katika Yohana 5: 25 “Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.”..Hivyo hiyo itawafanya watoke makaburini na ile miili yao waliokuwa nayo zamani na kutembea duniani.
SASA SWALI KUU UNAPASWA UJIULIZE, BAADA YA HAO WATAKATIFU KUFUFUKA NI KITU GANI KITAFUATA?
Ili kuelewa vizuri mambo mafupi yatakayofuata hapo katikati, inatupasa tujifunze kwanza kwa yaliyotokea katika ufufuo wa kwanza, Kumbuka Bwana aliwafufua watakatifu wa kwanza, lakini hakuwapeleka mbinguni bali mahali panapoitwa (PEPONI/PARADISO). Lakini kabla ya kwenda huko kuna vitu vilionekana.
Tusome kwa ufupi ni vitu gani vilitokea baada ya wale watakatifu kufufuliwa katika ule ufufuo wa kwanza.
Mathayo 27: 50 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.51 Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;52 MAKABURI YAKAFUNUKA; IKAINUKA MIILI MINGI YA WATAKATIFU WALIOLALA;53 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, WAKAUINGIA MJI MTAKATIFU, WAKAWATOKEA WENGI”.
Kumbuka huu ufufuo wa kwanza tunaouna hapo ni kivuli cha ufufuo wa pili, kama vile katika ufufuo wa kwanza kabla ya watakatifu kuingia Peponi waliingia mji mtakatifu na kuwatokea watakatifu wengine waliokuwa hai duniani kwa wakati ule, Vivyo hivyo na katika ule ufufuo wa mwisho wa watakatifu, kabla ya kutoweka duniani kwa watakatifu na kwenda mbinguni kutakuwa na kipindi Fulani kifupi sana ambacho wale watakatifu waliokufa katika Bwana kabla yao, watawatokea wale wanaoishi..
Kumbuka pia walikuwa hawawatokei tu ilimradi,labda kuwafurahisha hapana, bali walikuwa na huduma maalumu ya kuifanya kwa muda mfupi, na hii si nyingine zaidi ya kuwashuhudia wale watakatifu waliokuwa hai kwamba ni kweli wao waliisikia sauti ya waliyemsulibisha YESU KRISTO ikiwaita kutoka katika vifungo vya mauti, na kwamba yeye kweli ndiye MASIHI aliyetabiriwa kuwaokoa watu na uthibitisho ni wao,..
Embu jaribu kutengeneza picha wale wayahudi ghafla wanamwona Baba yao Ibrahimu, na Yakobo na Yusufu wamesimama mbele yao wakiwashuhudia habari za Yesu, unadhani wale watu kuanzia ule wakati walikuwa thabiti kiasi gani?, utawaeleza kitu chochote kuhusu Bwana Yesu?. Ni wazi kuwa yale matukio yaliwapa nguvu wale watakatifu ambao walikuwa wanamtumaini Bwana kama mwokozi wao.
Kadhalika pia na katika ufufuo wa mwisho wa wafu, biblia ilisema hatutawatangulia wale waliolala mautini, kwamba wao ndio watakaofufuliwa KWANZA, ikiwa na maana kuwa wao ndio watakaoisikia sauti ya Mungu kwanza,ikiwaita na kutoka makaburini,. Hivyo kuanzia huo wakati nao pia watawatokea watakatifu wengi watakaokuwa hai duniani. Na hawatawatokea ilimradi kuwafurahisha tu, hapana, bali nao pia watakuwa na hudumu ya muda mfupi sana, watawashuhudia kwamba, ni wameisikia sauti yake ikiwaita watoke makaburini, na ndio maana wapo pale, hivyo ule wakati kwa kwenda KUMLAKI BWANA MAWINGUNI UMEFIKA,
Jambo hilo litawapa nguvu wale watakaokuwa hai,na kwa matukio kama hayo itawaongezea imani kubwa sana ya kuondoka, hii kitakuwa ni kipindi kifupi sana, kumbuka pia watu wengine wasiokuwa watakatifu jambo hili litakuwa haliwahusu, hawatamwona mtu yeyote, hata wale watakatifu waliofufuka kwanza hawakumtokea tu kila mtu Israeli hapana bali watakatifu waliokuwa mji mtakatifu Yerusalemu…Na kwasasa hivi Mji Mtakatifu wa Mungu (Yerusalemu ya mbinguni) ni Kanisa lake takatifu, Hivyo watakao yaona hayo wafu wakipanda makaburini ni watakatifu tu, siku hiyo itakuwa ni furaha kubwa isiyokuwa ya kawaida, na ndio maana biblia inasema siku hiyo haitawajilia kama mwivi kwa kuwa hampo gizani,
Ndipo hapo utashangaa wakati huo, ndugu yako katika Bwana, aliyekufa pengine miaka 20 iliyopita anakutokea na kuzungumza na wewe na kukwambia ule wakati wa kwenda kwa Baba umewadia, wakati huo hata ukijaribu kuwashirikisha watu wengine wasiowatakatifu watakuona kama umerukwa na akili, au umeona mizimu, kwa kipindi hicho kifupi ufahamu wako utakuwa umebadilika na mawazo yako yatakuwa mbinguni,..Pengine utamwona dada aliyekuwa amelala muda mrefu nyuma ambaye alijisitiri kwa usafi wote wa roho na mwili mliokuwa mnafanya wote ushirika kanisani anakujia wakati upo katika shughuli zako za kujipatia rizki, akiwa pamoja na kundi la watakatifu wengine,
Sio hatu tu pia na watakatifu wengine wengi hata wa agano la kale watawatokea wengi…Na kwa muda mfupi sana kuanzia hapo, kufumba na kufumbua miili ya wote itageuka na kuwa ya utukufu, ataungana na wenzako kisha kwa pamoja mtaisikia Parapanda ya Mungu ikiwaita hapo juu, ..HALELUYA hapo tutamwona Bwana.…
Wakati huo dunia yote haitaelewa chochote mambo yanayoendelea, ndio ghafla wale watu ambao ulikuwa unaishi nao watakuona haupo, kumbuka watakaonyakuliwa watakuwa ni wachache sana duniani, hivyo halitakuwa ni jambo la kuishutusha sana dunia, wao wataendelea na shughuli zao kama kawaida wakingojea kufunuliwa kwa mpinga-kristo.
Lakini kama leo hii wewe ni mlevi, ni mwasherati, ni mzinzi, ni mtukanaji, mvaaji wa vimini, mtazamaji wa pornography na bado unajiita mkristo, unategemea mtakatifu gani akutokee siku ile?. Ni dhahiri kuwa haitakuhusu hivyo itakujia kama mwivi tu, kama leo hii tu unajitenga na watakatifu kutokana na uvaaji wako, na ulevi wako, na tabia zako,na anasa zako, kama umeshindwa kuungana nao hapa, utawezaje kuungana nao kule,?, utawezaje siku ile kutokewa na mtume Paulo, mtume Petro, Musa, Stephano, utawezaje siku ile kumwona mchungaji wako aliyekuwa akikufundisha na kukuonya uache dhambi na ukawa unakataa?. hatua ndogo tu kama hiyo ya kuwaona watakatifu ni shida, unategemea vipi kumwona BWANA mwenyewe MFALME WA WAFALME atakapokuja pale mawinguni..????.
Biblia inasema tusilale usingizini kama wengine walalavyo,bali sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu”(1Wathesalonike 5:7-8). Muda umeenda kuliko tunavyodhani Bwana yupo mlangoni kurudi je! Umempa Bwana maisha yako sasa, je! Umebatizwa katika ubatizo utakaokupelekea upate ondolea la dhambi zako na kupokea Roho Mtakatifu?, Kama hujafanya hivyo ni vema ufanye hivyo sasa kabla mlango wa neema haujafungwa, hatimaye siku ile nawe uwe mmojawapo wa watakaokwenda na watakatifu wa Mungu kumlaki Bwana mawinguni.
Biblia inasema Waebrania 12: 14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”;
Ubarikiwe sana.
Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu.