"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, December 28, 2018

MOYO ULIOELEKEA KWA MUNGU.


2Nyakati 16: 9 “Kwa maana macho ya Bwana hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake”. 

Tukisoma habari za wafalme katika biblia tunakuja kukutana na mfalme mmoja aliyeitwa ASA. Huyu biblia inasema aliiendea njia ya ukamilifu, alifanikiwa kuwaondoa  watu wote waliokuwa mahanithi (Mashoga) katika nchi ya Yuda, akaondoa maashera yote pamoja na sanamu zote zilizokuwa zimewekwa na baba zake kabla yake. Kwa  ujumbla ni mfalme aliyemtumainia sana Mungu kwa kila jambo na hivyo Mungu akamfanikisha sana(1Wafalme 15:9-15). Ilifikia hatua ambayo baada ya kugundua mama yake mzazi amesimamisha sanamu na kuziabudu, alimwondoa katika kiti chake cha umalkia bila kujali kuwa ni mama yake mzazi yupo hapo. Kwani kipindi kile cha wafalme, ilikuwa ni desturi mahali mfalme anapoketi ni lazima na mama yake awekewe kiti cha enzi kidogo pembeni yake.

 Lakini Mfalme Asa mara baada ya kugundua kuwa mama yake Mzazi anaabudu miungu mingine, bila kujali hisia yoyote ya mtu alimwondoa asionekane tena katika jumba la kifalme daima. Jambo ambalo halikuwahi  kufanywa na mfalme yeyote wa Israeli kabla yake… eti! Kumtoa mama yake aliyekuzaa katika cheo cha umalkia kisa tu kaisujudia miungu mingine?, Hakuna mfalme yeyote aliyedhubutu kufanya kitendo hicho cha kishujaa cha kumvunjia mamaye heshima na kumfanya kuwa kama mtu wa kawaida ili tu ailinde heshima ya Mungu wake japo wengi wao walikuwa wanawaona mama zao wakiwakosesha lakini walikaa kimya kulinda heshma za wazazi wao. Lakini kwa mfalme Asa ilikuwa tofauti, leo hii je! na sisi tunaweza kuyaweka mashauri  ya wazazi wetu chini yale yanayopingana na Mungu na kuyaruhusu yale tu ya Mungu yasimame?. Mungu atusaidie katika hilo na sisi.

Mfalme Asa alisimamia kweli hakubakisha sanamu yoyote katika Yuda na Benjamini, aliingia maagano na Mungu kuwa yeye na watu wote wa Yuda watamtafuta Mungu kwa mioyo yao yote, kwa akili zao zote na kwa nguvu zao zote, akapiga mbiu katika nchi yote ya  Yuda kwamba watu wote wamtufute Mungu muumba wa mbingu na nchi. Na wakakubaliana wote kuwa mtu yeyote ambaye hatamtafuta Mungu wa Mbinguni atauawa bila huruma, si mdogo, si mkubwa, si mwanamke, si mwanaume yeyote yule atauawa.. 
  
Hivyo Mungu akapendezwa sana na Mfalme Asa na hivyo akampa Amani na maadui zake wote waliokuwa wanamzunguka kwa muda mrefu tofauti na wafalme wengine waliosalia, na pindi maadui zake walipokuja kupigana naye Mungu aliwapa ushindi mnono, na nyara nyingi hivyo akaongezeka utajiri, na hofu kubwa ikawaangukia maadui zake wote waliokuwa wanamzunguka. Mungu akamjalia kuijenga Yuda kwa maboma, na minara na malango na makomeo makubwa, Na Hivyo mji ukathibitika na kuimarika kwa miaka mingi katika ufalme wake.

Lakini Bwana alimwambia Asa kwa kinywa cha Nabii Odedi ajitie nguvu wala mikono yake isilegee kwasababu kazi yake itakuwa ina malipo baadaye, haitakuwa bure aendelee hivyo hivyo kuulekeza moyo wake kwa Mungu, aondoe machukizo yote katika nyumba yake na katika Israeli aendelee hivyo hivyo kumtumaini Bwana wala asiwayategemee mataifa.  Tunakuja kusoma ni  kweli Mfalme ASA aliendelea kumsimamia Mungu kwa muda mrefu lakini ilifika wakati akapoa kidogo pindi maadui zake walipokuja kutaka kumzuia asitoke ndani ya mji wake, ndipo badala akimbilie kwa Mungu ambaye amekuwa akimtumainia na kumshindania  kwa muda mrefu, Mungu ambaye amekuwa akimpigania vita vikubwa kwa muda mrefu, na kumfanikisha katika mambo yote siku zote za utawala wake, Mungu ambaye amekuwa akimpa amani pande zote, lakini badala yake akakimbilia kwa mfalme wa Shamu ili amsaidie kufanya vita na maadui zake, hivyo akampelekea na zawadi nyingi kutoka katika hazina ya nyumba ya Mungu, na kweli mfalme wa Shamu alimsaidia kupigana na maadui zake, na wale maadui zake wakaacha kuujengwa uzio wa kuwazuia, Hivyo nchi ikastarehe tena kwa muda mfupi.

Lakini jambo hilo halikumpendeza sana Mungu, kwasababu Mungu alimwona  ASA kama ni mtu ambaye moyo wake ulimwelekea sana zaidi ya wengi waliotangulia, ni mtu ambaye Mungu angeweza kuonyesha uweza na nguvu zake zote kwa mataifa mengine kupitia yeye kama vile alivyoonyesha kwa Daudi na Sulemani, lakini sasa amefanya kitendo cha aibu, moyo wake kuwaelekea wanadamu na sio Mungu wake tena, kwenda kuwaomba wafalme wengine wa kipagani wamsaidie kupigana vita. Na ndio hapo tunakuja kusoma Mungu akimtumia nabii wake na kumwambia maneno haya.

2Nyakati 16: 7 “Wakati ule Hanani mwonaji akamwendea Asa mfalme wa Yuda, akamwambia, Kwa kuwa umemtegemea mfalme wa Shamu, wala hukumtegemea Bwana, Mungu wako, kwa hiyo limeokoka jeshi la mfalme wa Shamu mkononi mwako.
8 Je! Hao Wakushi na Walubi hawakuwa jeshi kubwa mno, wenye magari na wapanda farasi wengi sana? LAKINI, KWA KUWA ULIMTEGEMEA BWANA, ALIWATIA MKONONI MWAKO.
9 KWA MAANA MACHO YA BWANA HUKIMBIA-KIMBIA DUNIANI MWOTE, ILI AJIONYESHE MWENYE NGUVU KWA AJILI YA HAO, WALIOKAMILIKA MOYO KUELEKEA KWAKE. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita”.

Angalia hapo maneno hayo yalimjia mfalme Asa, hakujua kuwa macho ya Mungu yalishazunguka duniani kote kutafuta mtu aliyekamilika moyo ulioelekea kwake, ili Mungu ajionyeshe kuwa mwenye nguvu kwake, na akamwona ASA peke yake, lakini yeye hakulijua hilo, alidhani Mungu hakuwa anauthamini uthabiti wa moyo wake, alidhani Mungu hakumaanisha kumwambia yale maneno kuwa taabu yake kwake itakuwa na malipo (2Nyakati 15:7), yeye alichukulia juu juu tu, mpaka hapo alipoutoa moyo wake kwa Bwana na kuulekeza kwa wanadamu. Ndipo Mungu alipokasirika na kumwambia umefanya upumbavu…Mungu hapendi upumbavu kwa watu wanaomtumainia. Lakini pamoja na hayo yote Mfalme Asa alifanya mema machoni pa Mungu mpaka siku ya kufa kwake, na Bwana hakumwacha kabisa.

Leo hii ndugu yangu biblia inatufundisha na sisi tuwe ni mioyo iliyomwelekea Mungu. Kwasababu macho ya Mungu yanakimbia-kimbia duniani kote,  ikiwa na maana Mungu anaangalia anarudi tena anaangalia, anarudi tena anaangalia aone mtu atakayekuwa na moyo mkamilifu utakaomwelekea yeye kwa kila kitu ili azionyeshe nguvu zake. Kama ilivyokuwa kwa mfalme Asa. Tuweke tegemeo letu lote kwa Mungu, tumtwike yeye fadhaa zetu zote, tusiwe wepesi kuwakimbilia wanadamu, bali mioyo yetu siku zote tuielekeze kwa Mungu muumba wa mbingu na nchi, kwasababu yeye anawaangalia watu kama hao waliokamilika mioyo aonyeshe nguvu zake zote. Tuvumilie na kumtegemea Mungu hatari inapojitokeza mbele yetu..Tusiwapendelee wanadamu hata kama ni ndugu zetu, bali sisi tuangalie tu kile Mungu anachosema basi, tusifanye ibada za sanamu, ambazo biblia inazitaja kama uasherati, na tama mbaya, bali tuvivunje vunje vikae mbali nasi, ndipo hapo Mungu atakapotuona na kazi yetu ikawa na faida kubwa. Na Mungu atatuimarisha.

Ikiwa haujampa Bwana maisha yako, mlango wa neema bado upo kwa ajili yako, damu ya thamani ya Yesu Kristo bado inafanya kazi hata sasa hivi, imebaki kipindi kifupi sana isimame kufanya kazi yake. Usisubiri kipindi Fulani kifike , hicho hakitafika ndugu yangu, hiyo ni injili ya shetani anayokuhubiria moyoni mwako.. muda wa wokovu ni sasa biblia inasema hivyo. Chukua uamuzi sasa wa kuyakabidhi maisha yako kwa Bwana Yesu kikamilifu, na utakapofanya hivyo kwa kudhamiria kabisa kutoka ndani ya moyo wako, kutubu kwa kuacha dhambi na maisha yako ya kale, basi yeye mwenye atakupa uwezo wa kuzishinda dhambi. Na haraka mara baada ya kuamini kwako unapaswa ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwa jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako. Kisha Roho wa Mungu ataachiliwa juu yako kukulinda na kukuongoza katika kweli yote. Na baada ya hapo utakavyozidi kuuelekeza moyo wako kwa Mungu na kumtegemea yeye siku zote ndivyo utakavyouona mkono wake katika maisha yako, Na Mungu atakutumia wewe kuonyesha nguvu zake kwa wengine.

Ni matumaini yangu utafanya hivyo. Na Bwana akubariki sana.

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 48


SWALI 1: HOSEA 3 Kwa nini MUNGU Anampa Nabii Hosea maagizo ya Kumuoa mwanamke kahaba?

 JIBU: Mungu alimpa maagizo nabii Hosea kuoa mke aliye kahaba, sio kwasababu Mungu, anahalalisha usherati, hapana! Kusudi la Mungu kufanya vile ni kutaka kuwaonyesha wana wa Israeli ni jinsi gani wao wanavyofanya uasherati katika roho zao mbele zake kwa kuyaacha maagizo  yake..

Kwahiyo nabii Hosea alipooa mke wa uzinzi, ilikuwa kama ishara ya Bwana kutaka kuwaonyesha wana wa Israeli mambo wanayoyafanya mbele zake…Sasa Bwana alitaka endapo watu watakapomwuliza Hosea kwanini ameoa mke ambaye ni mzinzi…ndipo Hosea awajibu, kama mimi ninavyoudhiwa na huyu mwanamke mzinzi ndivyo na ninyi (wana wa Israeli) mnavyomuudhi Bwana kwa kufanya uzinzi mbele zake kwa kulihalifu agano lake na kuabudu miungu migeni, ukisoma habari ile yote kwa urefu utaona jambo hilo.


Sio mara ya kwanza Bwana kutoa ishara kupitia maisha ya watu, ukisoma biblia mahali pengine utaona Nabii ezekieli Bwana anamwagiza ale kinyesi, mahali pengine akate nywele zake kwa upanga azigawanye sehemu tatu….sehemu nyingine anaambiwa ahame nyumba yake kwa kutoboa ukuta, huku amejifunika macho kumwonyesha Mfalme wa Yuda Sedekia kwamba wakati majeshi ya wakaldayo yatakapouzingira mji kwa miaka miwili, yeye atatoroka kwa njia ya kutoboa ukuta wa mji, na hatimaye watamkamata na kumtoboa macho yake sawasawa na nabii Ezekieli alivyoonyesha…


Ezekieli 12:1-15

"1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema,

2 Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi.

3 Basi, mwanadamu, funga tayari vyombo kwa uhamisho, ukahame wakati wa mchana mbele ya macho yao; nawe utahama toka mahali pako hapa mpaka mahali pengine mbele ya macho yao; labda watafahamu, wajapokuwa ni nyumba iliyoasi.

4 Nawe utatoa vyombo vyako, wakati wa mchana, mbele ya macho yao, kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa; nawe mwenyewe utatoka, wakati wa jioni, mbele ya macho yao, kama watu watokavyo katika kuhamishwa.

5 Toboa mahali ukutani mbele ya macho yao, ukachukue vitu kwa kuvipitisha pale.

6 Mbele ya macho yao utajitwika begani pako, na kuvichukua nje gizani; utafunika uso wako, hata usiione nchi; kwa maana nimekuweka uwe ishara kwa nyumba ya Israeli.

7 Nikafanya vile vile kama nilivyoamriwa; nalitoa vyombo vyangu wakati wa mchana kana kwamba ni vyombo vya kuhamishwa, na wakati wa jioni nikautoboa ukuta kwa mkono wangu; nikavitoa gizani, nikavichukua begani, mbele ya macho yao.

8 Asubuhi neno la Bwana likanijia, kusema,

9 Mwanadamu, nyumba ya Israeli, je! Nyumba ile iliyoasi, hawakukuambia, Unafanya nini wewe?

10 Waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Ufunuo huu wamhusu mkuu wa Yerusalemu, na nyumba yote ya Israeli walio kati yao.

11 Sema, Mimi ni ishara kwenu; kama mimi nilivyotenda, wao nao watatendwa vile vile; watahamishwa, watakwenda kufungwa.

12 Naye mkuu aliye kati yao atachukua begani katika giza; naye atatoka kwenda zake; watatoboa mahali ukutani, wapate kuvichukua vyombo vyao nje; atafunika uso wake, kwa sababu hataiona nchi kwa macho yake.

13 Tena wavu wangu nitautandika juu yake, naye atanaswa kwa mtego wangu; nami nitampeleka Babeli, mpaka nchi ya Wakaldayo; lakini hataiona, angawa atakufa huko.

14 Nami nitawatawanya kwa pepo zote wote wamzungukao ili wamsaidie, na vikosi vyake vyote; nami nitaufuta upanga nyuma yao.
15 Nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; nitakapowatawanya kati ya mataifa, na kuwatupa-tupa katika nchi zote”
  *Ukizidi kusoma utaona mahali pengine Nabii mmoja Bwana alimwagiza amwambie mtu ampige mpaka atoke majeraha.

1 Wafalme 20: 35 “Basi, mtu mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake kwa neno la Bwana, Nipige, nakusihi. Akakataa yule kumpiga.

36 Akamwambia, Kwa sababu hukuisikiliza sauti ya Bwana, angalia, mara ukitoka kwangu simba atakuua. Na mara alipotoka kwake, simba alimwona, akamwua.
37 Ndipo akaona mtu mwingine, akasema, Nipige, nakusihi. Yule mtu akampiga, hata kumpiga na kumtia jeraha.”

Sasa mambo haya yote ni ishara ya Bwana kutaka kuzungumza na wana wa Israeli kwa kupitia maisha ya watu, kwahiyo hiyo ndio sababu ya Mungu kumwambia Nabii Hosea akaoe mke wa kikahaba..na pia kumbuka Hosea mwenyewe hakuwa mzinzi ni yule mwanamke aliyeambiwa amwoe ndiye aliyekuwa ni kahaba. Kwa jinsi hiyo hiyo mambo hayo yanavyochukiza mbele za watu ndivyo hivyo hivyo yanavyochukiza mbele za Mungu, pale watu wanapoasi maagano yake.


Ubarikiwe!



SWALI 2: Milele tunafahamu ni kitu ambacho hakina mwisho.Swali ni kwamba Yuda1:6"Na Malaika wasiolinda enzi yao wenyewe,lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu,amewaweka katika VIFUNGO VYA MILELE CHINI YA GIZA kwa hukumu ya siku ile...

Swali hapo ndugu zangu hiyo LUGHA iliyotumika hapo"VIFUNGO VYA MILELE"hapo inamaana gani..Kwanini imesema vya "milele" badala ya kusema vya daima au vya Muda fulani?.



JIBU: Nafikiri hili swali tulishalijibu kipindi fulani nyuma...Lugha yetu ya kiswahili ina mipaka, au tunaweza tukasema haijitoshelezi kwa baadhi ya tafsiri, kwahiyo inagharimu kutumia neno la ujumla kumeza tafsiri mbili au zaidi..kwamfano ukitaka kutafsiri neno la kingereza linalosema  “she came here yesterday” tafsiri yake ni  “alikuja hapa jana”…kadhalika ukitaka kutafsiri neno “he came here yesterday”..utaona ni kitu kile kile “alikuja hapa jana”…kwahiyo utaona kwamba lugha yetu katika kutafsiri inameza baadhi maneno, unakuta hatuna tafsiri ya neno kama “he” au “she” katika sentensi zetu na maneno mengine mengi ni ivyo hivyo.

Kadhalika  ukirudi katika biblia yetu ya kiswahili imetafsiriwa kutoka katika lugha ya kigiriki ambayo ndio iliyoandikia biblia..sasa kuna baadhi ya maneno hatuna tafsiri nayo katika lugha yetu..

Kwamfano tuchukue maneno la kingereza “everlasting” na “eternity”..Haya maneno mawili yanatafsiri zinazokaribia kufanana sana, lakini hayafanani...everlasting maana  yake “kwa muda mrefu sana” na “eternity” maana yake “milele isiyokuwa na mwisho”..Sasa katika biblia ya kigiriki tafsiri hizi za maneno haya mawili zimetofautishwa…lakini kwa katika tafsiri yetu hayajatofautishwa..mahali panapopaswa patumike kama “everlasting” pametumiwa “eternity” na mahali pa pa eternity pametumika ivyo hivyo eternity. Kwasababu lugha yetu haijitoshelezi.

Sasa wote waliomwamini Kristo hao Bwana kawaahidia uzima wa milele yaani “eternal life” na sio “everlasting life”..lakini wote ambao hawajampokea yeye biblia inasema watahukumiwa kwa moto wa milele..sasa huo umilele uliozungumziwa kwa wote ambao hawajampa Bwana maisha yao sio umilele wenye tafsiri ya “eternity” hapana bali ni wenye tafsiri “everlasting” yaani “moto wa muda mrefu”..lakini kwa kuwa lugha yetu neno “everlasting na eternity” ina tafsiri moja “milele” ndio maana unaona kote biblia inataja watakaohukumiwa watahukumiwa kwa moto wa milele lakini sio sahihi…Uzima wa milele upo kwa Yesu tu peke yake!! Hakuna  mtu au kiumbe chochote kitakachopata uzima wa milele nje ya Yesu Kristo..vingine vyote vitaadhibiwa kwa moto wa kudumu muda mrefu sana na hatimaye baada ya kipindi fulani kirefu sana vitapotea kabisa milele..kwasababu havina uzima wa milele..

Ubarikiwe!

SWALI 3: Waebrania1:5"Kwamaana(Bwana Yesu)alimwambia MALAIKA YUPI wakati wowote,NDIWE MWANANGU,..? Tunaona hapo Roho akituuliza ni Malaika yupi ambaye Mungu amemuita Mwanangu?.akasema kwa habari ya Malaika kwamba "Hao ni roho watumikao,wakitumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu[Hapo anapinga kuwaita Malaika wa mbinguni Wana wa Mungu.Waebrania1:14]".


Tukirudi agano la kale anasema"Ilikuwa,siku moja ambayo hao WANA WA MUNGU walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA[Ayubu1:6]:.. 

Ndugu zangu kama mlivyofundisha leo[Kwenye lile somo la HUDUMA YA MALAIKA WA MBINI] kwamba hao wana wa Mungu wanaotajwa hapo(Ayubu1:6)ni Malaika wa mbinguni".Nilikuwa silifahamu hilo ndugu zangu.Sasa nikawa na swali mbona katiki hicho kitabu cha Waebrania anapinga kuwaita hao malaika wa mbinguni WANA WA MUNGU Lakini Kama mlivyofundisha leo kwenye kitabu cha Ayubu anawaita Malaika wa mbinguni WANA WA MUNGU?.


JIBU: Ni kweli maandiko yanasema Malaika sio wana wa Mungu, lakini hiyo ilikuwa ni maana kwa ujumla..inategemea mahali neno hilo wana wa Mungu linapotumika..katika kitabu cha mwanzo wana wa Mungu waliozungumziwa pale ni wanadamu, lakini katika kitabu cha Ayubu ni malaika...
Kwahiyo Hiyo hilo neno wana wa Mungu..wakati mwingine linatumika kama neno la ujumla kuwakilisha familia ya Mungu..ambayo ni wanadamu na malaika. Ubarikiwe! Mfano mzuri ni neno Malaika lenyewe...mahali pengine katika maandiko malaika wanatumika kama wajumbe wa kiroho kutoka mbinguni...lakini ukirudi kwenye kitabu cha ufunuo sura ya 2 na ya 3 utaona malaika wanaozungumziwa pale wa yale makanisa saba ni wanadamu...kwahiyo wana wa Mungu na malaika ni majina yanaoingiliana na wanadamu na malaika.

 Ubarikiwe!

ROHO MBAYA KUTOKA KWA BWANA.

Umeshawahi kujiuliza pale biblia inaposema ROHO MBAYA KUTOKA KWA BWANA ikamjia Sauli ni roho ya namna gani hiyo? Na ni kwanini Bwana atume roho mbaya kwa mtu, nasi tunajua siku zote Mungu huwa anaachilia roho nzuri, njema na ya amani kwa watu, anasema hapa roho mbaya kutoka kwa Bwana, inakuaje tena anaiachilia roho yake mbaya iende kwa mtiwa mafuta wake, tena inafanya kazi ya kumsumbua kiasi ambacho inataka kufanya uharibifu hata ya kuwadhuru watu wasio na hatia..Tukisoma kitabu cha Samweli inasema:

1Samweli 16:14-23
“14 Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua.
15 Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.
16 Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi
wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa
mkono wake, nawe utapona.
17 Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee.
18 Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese,
Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu
mzuri, ambaye Bwana yu pamoja naye.
19 Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo.
20 Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli
kwa mkono wa Daudi mwanawe.
21 Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa
mtu wa kumchukulia silaha zake.
22 Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu;
maana ameona kibali machoni pangu.
23 Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa
mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha”.

Ili kufahamu vizuri ni kwanini hayo yote yalimpata Sauli, turudi nyuma kidogo tuitazame historia ya Mfalme Sauli jinsi ilivyokuwa. Kama tunavyosoma katika maandiko tunaambiwa kuwa Sauli alikuwa ni kijana mzuri sana, mrefu, mwenye haya ya uso, mlaini, hakuwa hata mtu aliyezaliwa katika mbari za kikuhani au za waamuzi walioamua Israeli wakati ule, hakuwahi hata kupigana vita yeyote, wala hakuwa na dalili ya kuonyesha kama ni mtu aliyeweza kusimama vitani, na ndio maana tunakuja kuona pindi tu siku ile alipokuja kutiwa mafuta na Nabii Samweli na kutangazwa kwa Israeli wote kama mfalme wao, baadhi ya watu walimkebehi kwa kumtazama tu mwonekano wake wa nje na uzoefu wake hafifu, alionekana kama ni mtoto tu, mtu mwenye tabia kama za kitoto, pengine walipomwona sura yake laini na uzuri aliokua nao au mazungumzo yake yasiyo na uzoefu wowote wa uongozi, watu wakamdharau na kumwona kama si kitu hawezi kuongoza taifa kubwa la kishujaa kama Israeli. Na ni kweli ndivyo alivyokuwa, alikuwa hana uwezo wowote ule Sauli.

Lakini siku Mungu alipomtia mafuta biblia inasema Roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu juu yake naye akageuzwa na kuwa mtu mwingine. (1Samweli 10:6). Sasa kumbuku kwasababu mtu kama Sauli alitiwa mafuta ya kuwa mfalme kuongoza taifa kubwa na hodari kama Israeli, ni sharti roho ambayo itaachiliwa juu yake itakuwa ni roho ya uongozi, roho ya ujasiri, roho ya maamuzi magumu, na roho ya udhubutu na roho ya ushujaa. Hivyo jambo ambalo lingemtokea mfalme Sauli hapo ni lazima liwe la namna hiyo.

Lakini Mfalme Sauli hakulitambua hilo vizuri mpaka siku ambayo maadui wa ndugu zao walipotokea na kutaka kuwatawala, tena kwa mapatano ya kila myahudi kung'olewa jicho lake la kuume, vinginevyo watawauawa. Hivyo habari hizo zikafika katika miji mingine yote ya Israeli, watu wote wakalia sana, wakizingatia kuwa huyo adui wa ndugu zao huko Yabesh-gileadi ni mkuu sana, hakuna mtu anayeweza kusimama mbele yake kuwatetea na kushindana naye ili kuwaokoa ndugu zao..Hivyo wakalia sana lakini habari zilimfikia Sauli mwezi mmoja tu baada ya kutiwa mafuta ya kuwa mfalme, Sauli ambaye alidharauliwa na watu, Sauli ambaye hakuwa na uzoefu wowote wa vita ghafla akanyanyuka kwa ushujaa mwingi na HASIRA nyingi, na kusema maneno haya.

1Samweli 11:4 “Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote
wakainua sauti zao wakalia.
5 Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini,
hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.
6 NA ROHO YA MUNGU IKAMJILIA SAULI KWA NGUVU, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka
sana.
7 Naye akatwaa jozi ya ng'ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote
mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng'ombe
zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa Bwana ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja.
8 Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu.
9 Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua
kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa.
10 Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni
mema.
11 Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago
kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia
wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja.
12 Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu
hao, ili tuwaue.
13 Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo Bwana amefanya wokovu katika
Israeli”.
Sasa tunaweza kuona hapo Roho ya Bwana pindi tu ilipomshukia Sauli alipatwa na Hasira kali. Na Tunafahamu hasira siku zote ikimwaka hata mtu yeyote huwa hajali ni madhara gani atakutana nayo, atapambana nayo kwa hali yoyote ilimradi tu atimize lengo lake, Sasa hii hasira iliyokuwa inamjia Sauli. Inayomfanya ashindwe kujitawala mwenyewe pindi imjiapo ambayo si kila wakati ilikuwa inamjia bali pale tu inapopaswa itimize kusudi fulani, ilitoka kwa Mungu mwenyewe. Hiyo ndio iliyowaokoa wana wa Israeli katika mikono ya maadui zao sikuzote, katika vita vigumu na vizito vilivyokuwa vinawajia waisraeli. Mungu alikuwa anaituma Roho yake kwa hasira nyingi juu ya Sauli, na bila kuogopa wala kujali lolote Sauli alishuka vitani kama simba na kusambaratisha maadui zao wote. Hapo ndipo hata mashujaa hodari wa vita wa Israeli ndipo walipokuwa wanamwogopea Sauli kwa Roho hiyo iliyokuwa juu yake.

Tunaweza pia kuona nyingine katika maandiko roho hiyo hiyo haikuwa tu kwa Sauli peke yake tunaiona pia kwa mtu kama Samsoni. Roho ya Mungu ilipokuwa inamjia kwa nguvu hasira yake ilikuwa inawaka, na hivyo hajali kufanya jambo lolote linaloweza hata kuleta madhara makubwa katika nchi, Tunaona wakati wote alipokuwa anapambana na wafilisti Roho wa Bwana alishuka juu yake kwa hasira nyingi sana.

Waamuzi 14:19 “Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume
thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo.
Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake”.

Na ndivyo ilivyokuwa kwa mfalme Sauli, kwasababu alikuwa ametiwa mafuta na Mungu mwenyewe, Mungu alizielekeza HASIRA zile kwa kusudi maalumu la kuilinda Israeli dhidi ya madui zao, lakini wakati mfalme Sauli alipoacha kufuata njia za Mungu na kufanya vitu ambavyo Mungu hakuwa anamwagiza, ndipo Bwana akaghahiri kumtumia tena, hivyo akauamishia utawala wake kwa jirani yake Daudi. Lakini kumbuka Mungu hakumtoa Roho wake juu ya Sauli, isipokuwa roho ya utawala iliondolewa juu yake.

Hapo tunajifunza nini?. Mungu akishakutia mafuta, amekutia mafuta, hawezi kuyaondoa tena juu yako milele. Isipokuwa yataachwa tu yajiongoze kwa hisia zako na akili zako na sio tena kwa uvuvio au uongozi wa Roho Mtakatifu na hiyo ndiyo mbaya zaidi kwasababu ndio hapo mtu atatumia vipawa Mungu alivyompa kutimiza matakwa yake mwenyewe binafsi. Hilo ndio jambo lililomkuta mfalme Sauli baada ya Mungu kumrarulia ufalme na kumpa Daudi, kuanzia huo wakati mfalme Sauli akapoteza dira kabisa na mwelekeo wa kuitawala Israeli, akaanza kuzitumia nguvu zile za Hasira kuulinda ufalme wake na enzi yake badala ya kuilinda Israeli na ndio hapo akawa anamwinda Daudi siku zote, na hata wakati mwingine akiwa amestarehe tu nyumbani kwake kukiwa na amani, ile Roho pindi imjiapo, anajikuta anarusha rusha tu pasipo kujizuia ili tu amuue Daudi mtu asiyekuwa na hatia. Wakati hasira hizo zingepaswa zielekezwe kwa maadui wa Israeli.

Ni jambo hilo hilo lilimpata na shetani, baada ya shetani kushindwa kuilinda enzi yake Mungu aliyompa. Ambaye alikuwa ni kerubi aliyetiwa mafuta kuliko makerubi wote, yeye hakutaka kuenenda katika utaratibu Mungu aliomuwekea, Hivyo Mungu akaamua kuurarua utawala wake na kuwapa wengine. Lakini kumbuka kama tulivyoona Mungu akishakutia mafuta, hawezi kuyaondoa juu yako. Utaendelea nayo hivyo hivyo lakini yatakuwa hayaongozwi na Roho Mtakatifu bali kwa hisia zako na akili zako kujiundia ufalme wako.

Na ndio maana shetani mpaka sasa hajaondolewa nguvu zake alizopewa na Mungu, lakini sasa anazitumia kujiundia ufalme wake wa giza, ili kutimiza matakwa yake mwenyewe. Na hiyo ndiyo inayoitwa Roho mbaya kutoka kwa Mungu.

Vivyo hivyo na manabii wa uongo,na walimu wa uongo, na wachungaji wa uongo, na waimbaji wa uongo... waliopo leo, jambo ni lile lile, utakuta mwanzoni walitiwa kweli mafuta ya kundi la Mungu, walifundishe, walilishe, waliongoze katika njia njema..Lakini kwa jinsi siku zilivyozidi kwenda wakaanza kuyahalifu maagizo ya Mungu kidogo kidogo kama ilivyokuwa kwa mfalme Sauli. Na mwisho wa siku Mungu akaghahiri kuwaita Watumishi wake, hivyo ile Roho njema ya uongozi kutoka kwa Mungu iliyoachiwa juu yao kulilinda kundi la Mungu inawaacha, wanabakiwa tu na mafuta Mungu aliyowapa ili wajiongoze kwa tamaa zao wenyewe na sio kwa tamaa za Roho Mtakatifu.

Na ndio hapo utamwona mtu anajiita nabii anaona maono sahihi kabisa anatabiria watu mambo yajayo,na kweli yanatokea, lakini bado ni mwasherati, bado anaishi kidunia hawi tena kielelezo cha kuwapeleka watu mbinguni, utakuta badala awaelekeze watu kwa Mungu wao, anawaelekeza kwake, muda wote anajisifia yeye tu, utukufu wote wa Mungu anauchukua yeye, anasahau kuwa mafuta yale aliyopewa hayakuja kwa juhudu zake bali yalitoka kwa Mungu kwa kutimiza kusudi la kundi la Bwana, lakini yeye hajali hilo kwasababu Roho wa Mungu kashamwacha siku nyngi bali ile roho mbaya itokayo kwa Mungu ndiyo inayomwendesha mwisho wa siku anaishia kuleta madhara makubwa kwenye kanisa na kuhusika kuwapeleka watu wengi kuzimu, na kuwapoteza yamkini hata na wale walio wateule wa Mungu. Na siku zinavyozidi kuendelea utakuta yeye ndiye anayekuwa adui wa kwanza wa watumishi wa kweli Mungu kama Sauli alivyokuwa anafanya kwa Daudi.


Ndugu unayesoma, vipawa vya Mungu si vya kuvichezea. Kabisa, Mungu hadhihakiwi, usidhani kunena kwako kwa lugha ni ishara kuwa unaye Roho Mtakatifu, usidhani kuona kwako maono ni dalili kuwa unampendeza Mungu, usidhani kutoa kwako unabii ni ishara madhubuti kuwa upo katika mstari sahihi. Hayo yote hayakusaidii kitu kama hutasimama katika mstari wa Neno la Mungu. Biblia inatuambia

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu ATAKAYEMWONA BWANA ASIPOKUWA NAO;”

Unaona, utafanya yote lakini kama utakatifu haupo ndani yako, ni mambo machafu tu yamejaa ndani yako, uzinzi,ulevi, anasa, pornography,miziki ya kidunia, mastubation,uchawi,ibada za sanamu, utukanaji n.k hayo yote, hata kama utakuwa unazungumza na malaika kila siku kiasi gani, mbingu hutaiona ndugu.

Embu tusiwe mojawapo ya hao walionza vizuri na kumaliza vibaya, embu tuiruhusu ile Roho njema tu ya Mungu ituongoze na sio fikra zetu ili mwisho wetu upate kuwa mzuri katika safari yetu hapa duniani.Kumbuka Bwana hampi mtu roho mbaya, isipokuwa sisi ndio tunayoitumia roho njema ya Mungu katika ubaya.

Bwana Yesu akubariki sana.