"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Friday, December 28, 2018

ROHO MBAYA KUTOKA KWA BWANA.

Umeshawahi kujiuliza pale biblia inaposema ROHO MBAYA KUTOKA KWA BWANA ikamjia Sauli ni roho ya namna gani hiyo? Na ni kwanini Bwana atume roho mbaya kwa mtu, nasi tunajua siku zote Mungu huwa anaachilia roho nzuri, njema na ya amani kwa watu, anasema hapa roho mbaya kutoka kwa Bwana, inakuaje tena anaiachilia roho yake mbaya iende kwa mtiwa mafuta wake, tena inafanya kazi ya kumsumbua kiasi ambacho inataka kufanya uharibifu hata ya kuwadhuru watu wasio na hatia..Tukisoma kitabu cha Samweli inasema:

1Samweli 16:14-23
“14 Basi, roho ya Bwana ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua.
15 Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.
16 Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi
wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa
mkono wake, nawe utapona.
17 Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee.
18 Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese,
Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu
mzuri, ambaye Bwana yu pamoja naye.
19 Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo.
20 Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli
kwa mkono wa Daudi mwanawe.
21 Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa
mtu wa kumchukulia silaha zake.
22 Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu;
maana ameona kibali machoni pangu.
23 Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa
mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha”.

Ili kufahamu vizuri ni kwanini hayo yote yalimpata Sauli, turudi nyuma kidogo tuitazame historia ya Mfalme Sauli jinsi ilivyokuwa. Kama tunavyosoma katika maandiko tunaambiwa kuwa Sauli alikuwa ni kijana mzuri sana, mrefu, mwenye haya ya uso, mlaini, hakuwa hata mtu aliyezaliwa katika mbari za kikuhani au za waamuzi walioamua Israeli wakati ule, hakuwahi hata kupigana vita yeyote, wala hakuwa na dalili ya kuonyesha kama ni mtu aliyeweza kusimama vitani, na ndio maana tunakuja kuona pindi tu siku ile alipokuja kutiwa mafuta na Nabii Samweli na kutangazwa kwa Israeli wote kama mfalme wao, baadhi ya watu walimkebehi kwa kumtazama tu mwonekano wake wa nje na uzoefu wake hafifu, alionekana kama ni mtoto tu, mtu mwenye tabia kama za kitoto, pengine walipomwona sura yake laini na uzuri aliokua nao au mazungumzo yake yasiyo na uzoefu wowote wa uongozi, watu wakamdharau na kumwona kama si kitu hawezi kuongoza taifa kubwa la kishujaa kama Israeli. Na ni kweli ndivyo alivyokuwa, alikuwa hana uwezo wowote ule Sauli.

Lakini siku Mungu alipomtia mafuta biblia inasema Roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu juu yake naye akageuzwa na kuwa mtu mwingine. (1Samweli 10:6). Sasa kumbuku kwasababu mtu kama Sauli alitiwa mafuta ya kuwa mfalme kuongoza taifa kubwa na hodari kama Israeli, ni sharti roho ambayo itaachiliwa juu yake itakuwa ni roho ya uongozi, roho ya ujasiri, roho ya maamuzi magumu, na roho ya udhubutu na roho ya ushujaa. Hivyo jambo ambalo lingemtokea mfalme Sauli hapo ni lazima liwe la namna hiyo.

Lakini Mfalme Sauli hakulitambua hilo vizuri mpaka siku ambayo maadui wa ndugu zao walipotokea na kutaka kuwatawala, tena kwa mapatano ya kila myahudi kung'olewa jicho lake la kuume, vinginevyo watawauawa. Hivyo habari hizo zikafika katika miji mingine yote ya Israeli, watu wote wakalia sana, wakizingatia kuwa huyo adui wa ndugu zao huko Yabesh-gileadi ni mkuu sana, hakuna mtu anayeweza kusimama mbele yake kuwatetea na kushindana naye ili kuwaokoa ndugu zao..Hivyo wakalia sana lakini habari zilimfikia Sauli mwezi mmoja tu baada ya kutiwa mafuta ya kuwa mfalme, Sauli ambaye alidharauliwa na watu, Sauli ambaye hakuwa na uzoefu wowote wa vita ghafla akanyanyuka kwa ushujaa mwingi na HASIRA nyingi, na kusema maneno haya.

1Samweli 11:4 “Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote
wakainua sauti zao wakalia.
5 Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini,
hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi.
6 NA ROHO YA MUNGU IKAMJILIA SAULI KWA NGUVU, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka
sana.
7 Naye akatwaa jozi ya ng'ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote
mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng'ombe
zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa Bwana ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja.
8 Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu.
9 Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua
kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa.
10 Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni
mema.
11 Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago
kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia
wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja.
12 Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu
hao, ili tuwaue.
13 Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo Bwana amefanya wokovu katika
Israeli”.
Sasa tunaweza kuona hapo Roho ya Bwana pindi tu ilipomshukia Sauli alipatwa na Hasira kali. Na Tunafahamu hasira siku zote ikimwaka hata mtu yeyote huwa hajali ni madhara gani atakutana nayo, atapambana nayo kwa hali yoyote ilimradi tu atimize lengo lake, Sasa hii hasira iliyokuwa inamjia Sauli. Inayomfanya ashindwe kujitawala mwenyewe pindi imjiapo ambayo si kila wakati ilikuwa inamjia bali pale tu inapopaswa itimize kusudi fulani, ilitoka kwa Mungu mwenyewe. Hiyo ndio iliyowaokoa wana wa Israeli katika mikono ya maadui zao sikuzote, katika vita vigumu na vizito vilivyokuwa vinawajia waisraeli. Mungu alikuwa anaituma Roho yake kwa hasira nyingi juu ya Sauli, na bila kuogopa wala kujali lolote Sauli alishuka vitani kama simba na kusambaratisha maadui zao wote. Hapo ndipo hata mashujaa hodari wa vita wa Israeli ndipo walipokuwa wanamwogopea Sauli kwa Roho hiyo iliyokuwa juu yake.

Tunaweza pia kuona nyingine katika maandiko roho hiyo hiyo haikuwa tu kwa Sauli peke yake tunaiona pia kwa mtu kama Samsoni. Roho ya Mungu ilipokuwa inamjia kwa nguvu hasira yake ilikuwa inawaka, na hivyo hajali kufanya jambo lolote linaloweza hata kuleta madhara makubwa katika nchi, Tunaona wakati wote alipokuwa anapambana na wafilisti Roho wa Bwana alishuka juu yake kwa hasira nyingi sana.

Waamuzi 14:19 “Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume
thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo.
Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake”.

Na ndivyo ilivyokuwa kwa mfalme Sauli, kwasababu alikuwa ametiwa mafuta na Mungu mwenyewe, Mungu alizielekeza HASIRA zile kwa kusudi maalumu la kuilinda Israeli dhidi ya madui zao, lakini wakati mfalme Sauli alipoacha kufuata njia za Mungu na kufanya vitu ambavyo Mungu hakuwa anamwagiza, ndipo Bwana akaghahiri kumtumia tena, hivyo akauamishia utawala wake kwa jirani yake Daudi. Lakini kumbuka Mungu hakumtoa Roho wake juu ya Sauli, isipokuwa roho ya utawala iliondolewa juu yake.

Hapo tunajifunza nini?. Mungu akishakutia mafuta, amekutia mafuta, hawezi kuyaondoa tena juu yako milele. Isipokuwa yataachwa tu yajiongoze kwa hisia zako na akili zako na sio tena kwa uvuvio au uongozi wa Roho Mtakatifu na hiyo ndiyo mbaya zaidi kwasababu ndio hapo mtu atatumia vipawa Mungu alivyompa kutimiza matakwa yake mwenyewe binafsi. Hilo ndio jambo lililomkuta mfalme Sauli baada ya Mungu kumrarulia ufalme na kumpa Daudi, kuanzia huo wakati mfalme Sauli akapoteza dira kabisa na mwelekeo wa kuitawala Israeli, akaanza kuzitumia nguvu zile za Hasira kuulinda ufalme wake na enzi yake badala ya kuilinda Israeli na ndio hapo akawa anamwinda Daudi siku zote, na hata wakati mwingine akiwa amestarehe tu nyumbani kwake kukiwa na amani, ile Roho pindi imjiapo, anajikuta anarusha rusha tu pasipo kujizuia ili tu amuue Daudi mtu asiyekuwa na hatia. Wakati hasira hizo zingepaswa zielekezwe kwa maadui wa Israeli.

Ni jambo hilo hilo lilimpata na shetani, baada ya shetani kushindwa kuilinda enzi yake Mungu aliyompa. Ambaye alikuwa ni kerubi aliyetiwa mafuta kuliko makerubi wote, yeye hakutaka kuenenda katika utaratibu Mungu aliomuwekea, Hivyo Mungu akaamua kuurarua utawala wake na kuwapa wengine. Lakini kumbuka kama tulivyoona Mungu akishakutia mafuta, hawezi kuyaondoa juu yako. Utaendelea nayo hivyo hivyo lakini yatakuwa hayaongozwi na Roho Mtakatifu bali kwa hisia zako na akili zako kujiundia ufalme wako.

Na ndio maana shetani mpaka sasa hajaondolewa nguvu zake alizopewa na Mungu, lakini sasa anazitumia kujiundia ufalme wake wa giza, ili kutimiza matakwa yake mwenyewe. Na hiyo ndiyo inayoitwa Roho mbaya kutoka kwa Mungu.

Vivyo hivyo na manabii wa uongo,na walimu wa uongo, na wachungaji wa uongo, na waimbaji wa uongo... waliopo leo, jambo ni lile lile, utakuta mwanzoni walitiwa kweli mafuta ya kundi la Mungu, walifundishe, walilishe, waliongoze katika njia njema..Lakini kwa jinsi siku zilivyozidi kwenda wakaanza kuyahalifu maagizo ya Mungu kidogo kidogo kama ilivyokuwa kwa mfalme Sauli. Na mwisho wa siku Mungu akaghahiri kuwaita Watumishi wake, hivyo ile Roho njema ya uongozi kutoka kwa Mungu iliyoachiwa juu yao kulilinda kundi la Mungu inawaacha, wanabakiwa tu na mafuta Mungu aliyowapa ili wajiongoze kwa tamaa zao wenyewe na sio kwa tamaa za Roho Mtakatifu.

Na ndio hapo utamwona mtu anajiita nabii anaona maono sahihi kabisa anatabiria watu mambo yajayo,na kweli yanatokea, lakini bado ni mwasherati, bado anaishi kidunia hawi tena kielelezo cha kuwapeleka watu mbinguni, utakuta badala awaelekeze watu kwa Mungu wao, anawaelekeza kwake, muda wote anajisifia yeye tu, utukufu wote wa Mungu anauchukua yeye, anasahau kuwa mafuta yale aliyopewa hayakuja kwa juhudu zake bali yalitoka kwa Mungu kwa kutimiza kusudi la kundi la Bwana, lakini yeye hajali hilo kwasababu Roho wa Mungu kashamwacha siku nyngi bali ile roho mbaya itokayo kwa Mungu ndiyo inayomwendesha mwisho wa siku anaishia kuleta madhara makubwa kwenye kanisa na kuhusika kuwapeleka watu wengi kuzimu, na kuwapoteza yamkini hata na wale walio wateule wa Mungu. Na siku zinavyozidi kuendelea utakuta yeye ndiye anayekuwa adui wa kwanza wa watumishi wa kweli Mungu kama Sauli alivyokuwa anafanya kwa Daudi.


Ndugu unayesoma, vipawa vya Mungu si vya kuvichezea. Kabisa, Mungu hadhihakiwi, usidhani kunena kwako kwa lugha ni ishara kuwa unaye Roho Mtakatifu, usidhani kuona kwako maono ni dalili kuwa unampendeza Mungu, usidhani kutoa kwako unabii ni ishara madhubuti kuwa upo katika mstari sahihi. Hayo yote hayakusaidii kitu kama hutasimama katika mstari wa Neno la Mungu. Biblia inatuambia

Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu ATAKAYEMWONA BWANA ASIPOKUWA NAO;”

Unaona, utafanya yote lakini kama utakatifu haupo ndani yako, ni mambo machafu tu yamejaa ndani yako, uzinzi,ulevi, anasa, pornography,miziki ya kidunia, mastubation,uchawi,ibada za sanamu, utukanaji n.k hayo yote, hata kama utakuwa unazungumza na malaika kila siku kiasi gani, mbingu hutaiona ndugu.

Embu tusiwe mojawapo ya hao walionza vizuri na kumaliza vibaya, embu tuiruhusu ile Roho njema tu ya Mungu ituongoze na sio fikra zetu ili mwisho wetu upate kuwa mzuri katika safari yetu hapa duniani.Kumbuka Bwana hampi mtu roho mbaya, isipokuwa sisi ndio tunayoitumia roho njema ya Mungu katika ubaya.

Bwana Yesu akubariki sana.

No comments:

Post a Comment