Wakati tunakaribia kumaliza Mwaka ni kipindi maalumu sana cha kukaa na kutafakari na kuchukua hatua ya kumshukuru Mungu kwa Mengi aliyotutendea...Jambo kubwa la kuweza kumshukuru Mungu, ni juu ya pumzi aliyotupatia mwaka mzima, Katika safari ya mwaka mzima, kuna vipindi vingi tumepita lakini bado tunaishi..jua linachomoza na kuzama kila siku, hatujapitia matetemeko ya ardhi mwaka mzima, hatujapigana vita mwaka mzima, Mungu katuepusha na majanga mengi, katuepusha na magonjwa mengi, na hata tulipopata ugonjwa Bwana alituponya n.k Unafikiri ni kwasababu ya nani? Mpaka Mungu atuepushe na hayo yote?
si kwasababu tuna unafuu mbele zake, au kwasababu tunazingatia mlo kamili, wala si kwasababu tunajitunza sana na kujipenda, wala si kwasababu tunaustaarabu mzuri wa maisha, wala si kwaajili ya haki yetu sisi, wala si kwasababu sisi ni watakatifu, wala sio kwasababu tunabidii ya kumtafuta yeye, wala si kwasababu tunatenda mema sana, wala si kwasababu tunafunga sana, wala si kwasababu tunaomba sana, wala si kwasababu ni washirika wazuri wa kanisani au watoaji sadaka wazuri au wenye upendo sana.. Hakuna hata jambo moja kati ya haya ambayo Baba yetu wa mbinguni anayaangalia ili kutunyeshea sisi mvua yake, au kutupa pumzi, au kutupatia mema, au kutupatia uzima au kutuangazia jua lake, Hakuna hata moja!!
Sasa swali linakuja kama sio kwa ajili ya hayo yote, tunaumaliza mwaka salama..basi ni kwasababu gani? Kama si kwaajili ya utakatifu wetu, au bidii zetu, au juhudi zetu, au matendo yetu, au utakatifu wetu ni kwasababu gani basi tunapokea neema hii?.
Jibu ni rahisi, ni kwasababu ya haki ya mtu mmoja, ni kwasababu ya utakatifu wa mtu mmoja, ni kwasababu ya bidii ya mtu mmoja, ni kwasababu ya juhudi ya mtu mmoja, ni kwasababu ya matendo ya mtu mmoja, ni kwasababu ya maombi ya mtu mmoja, na huyo mtu ni BWANA YESU KRISTO, kwa huyo Baba wa mbinguni ndiye aliyependezwa naye.
Baba wa mbinguni hakupendezwa na maelfu waliopo duniani, hakuona mwenye haki hata mmoja duniani, wote tulikuwa tumetenda dhambi, tunakasoro nyingi, zisizokuwa na hesabu.
Zaburi 14: 2 “Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja”.
Unaona! Sasa kama hakuna hata mmoja aliyemwona duniani mwenye haki??..unadhani vipi kama kuna ambaye angestahili kupokea baraka yoyote kutoka kwake?..hakuna hata mmoja..angestahili kupata pumzi kwa haki yake,wote tumestahili hukumu ya milele, Ndio maana inapasa atoke mtu mwingine kutoka mbinguni mwenye haki ambaye angestahili kupokea baraka kutoka kwa Mungu, kwasababu duniani hakuna hata mmoja mwenye akili, wote tumepungukiwa na utukufu wa Mungu..Hakuna hata mmoja mwenye unafuu.
Kwasababu hiyo basi kwa kuwa Yesu Kristo pekee ndiye aliyekuwa mkamilifu, ambaye hakutenda dhambi tangu kuzaliwa kwake mpaka ameondoka, yeye peke yake ndiye aliyehesabiwa haki kwa matendo yake binafsi, yeye peke yake ndiye Baba wa mbinguni aliyemwona mwenye AKILI anayemtafuta Mungu, alimchungulia toka juu akamwona akamtangaza “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” ...hakusema hawa ndio wanangu wapendwa wangu..hapana bali “huyu ndiye”..maana yake yupo mmoja tu!! kwa haki yake amestahili kubarikiwa kwa kila namna. Ndugu mtu asikudanganye kwamba kuna wabarikiwa wengi..Mbarikiwa ni mmoja tu! Yesu Kristo.. Maandiko yanasema hivyo..
Mathayo 21:5 “Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda,Na mwana-punda, mtoto wa punda.6 Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru,7 wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake.8 Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi yamiti, wakayatandaza njiani.9 Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, HOSANA , MWANA WA DAUDI; NDIYE MBARIKIWA , yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni”.
Sasa basi kwasababu ni mmoja tu! Ndiye aliyestahili baraka, Yesu Kristo pekee asiyestahili kufa wala kuangamizwa milele...Yeye Yesu Kristo Bwana wetu alitununua sisi tusiokuwa wakamilifu kwa Baba wa mbinguni, akatushirikisha baraka zake alizobarikiwa na Baba wa mbinguni, akatuhusisha katika fadhili zake alizofadhiliwa na Baba, japokuwa sisi hatukustahili kubarikiwa, wala kupewa uzima, wala kuangaziwa jua..lakini sasa tunayapata hayo yote kupitia Yesu Kristo.
Kwasababu hiyo basi hata kipindi hichi tunachomaliza mwaka, kama bado tunaishi...tusijisifu ni kwa matendo yetu, sio kwa matendo yetu hata kidogo, bali kwa ajili ya matendo ya Yesu Kristo aliyoyaishi hapa duniani yaliyompendeza Baba..si kwa ajili tuna bidii za kujitunza hapana...wapo waliokuwa na bidii ya kujitunza sana lakini wameondoka..ni kwaajili ya Huruma ya Yesu Kristo juu yetu.
Sio kwasababu ya juhudi zetu, ndio tumebarikiwa na kupata mema ya nchi hapana ni kwasababu ya Mbaraka Bwana Yesu aliobarikiwa na Baba yake kwa haki yake..na sisi ndio tunaoushiriki . Yesu Kristo pekee yake ndiye Mbarikiwa, sisi ni kama waalikwa tu! Tumealikwa kwenda kula baraka za Yesu Kristo..Ndio maana na sisi tunajumuishwa kama miongoni mwa waliobarikiwa, lakini Mbarikiwa ni mmoja tu!
Kwahiyo ndugu, tukimfahamu Yesu Kristo kwa namna hiyo, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa ajili yake, hatuna budi kunyenyekea sana na kumwambia Bwana Ahsante...Ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa jambo moja moja alilotutendea kuanzia mwanzo wa mwaka huu hata mwisho. Hata kama bado ni mgonjwa mshukuru sana! Hata kama bado hukupata mwaka huu ulichokitamani, mshukuru tu Maadamu bado unaishi...Kwa wakati wake ukifika, atakutimizia matakwa yako.
Mshukuru kwasababu bado upo kwenye Imani, hujaanguka, shetani alikutafuta mwaka mzima kama simba angurumaye..Mshukuru kwasababu amekuepusha na yule mwovu..mshukuru kwasababu kama sio yeye kukubaliwa na Baba wa mbinguni usingekuwa hapo ulipo..kama sio yeye kuishi maisha makamilifu tangu anazaliwa mpaka anakufa usingepata hata hiyo pumzi, kama sio yeye kuwa mwenye akili ya kumtafuta Mungu, kwa kufunga na kuomba, na dua na sala nyingi...leo hii dunia pengine isingekuwepo, wote tungekuwa ni wana wa Jehanum ya moto.
Mshukuru kwa kila nyanja ya maisha yako, na pia mwombe Neema zaidi kwa Mwaka unaokuja, ukazidi kumtafuta yeye na kumsogelea zaidi, na kumjua yeye zaidi na uwezo wake, Akakupe Neema zaidi ya kuushinda ulimwengu na mambo yake, maana mambo ya ulimwengu huu yanapita, na yeye yupo mlangoni kurudi, na maandiko yanasema atakuja kama mwivi usiku wa manane!..Siku moja inapopita ndivyo tunavyokaribia mwisho, mwaka mmoja unapopita ndivyo siku ile tunavyozidi kuikaribia. Tumwombe Bwana neema na yeye atatusaidia.
Bwana akubariki sana!
No comments:
Post a Comment