"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, February 26, 2018

"Ni heri nimuishie Mungu nikiwa na maji na mkate tu, kuliko kumuishia shetani pamoja na kuku wa kukaanga, na lamba lamba kutwa mara tatu..."

William Branham.
(53-0831 Mungu alizungumza na Musa)
 "Kama unataka kuzungumziwa vizuri , mzungumzie kwanza vizuri mtu mwingine, na ndipo na wewe utazungumziwa vizuri na watu wengine, Mhubiri 11:1 Tupa chakula chako usoni pa maji; Maana utakiona baada ya siku nyingi."

William Branham (48-0302 Uzoefu)

Saturday, February 24, 2018

DANIELI: Mlango wa 8

Jina la YESU KRISTO, BWANA wetu libarikiwe.

Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha Danieli, Kama tulivyoona katika sura iliyotangulia Danieli akionyeshwa wale wanyama 4 waliotoka baharini, wa kwanza mwenye mfano wa simba, wa pili kama Dubu, watatu kama Chui na wanne alionekana kuwa mbali sana na wale wengine kwa muonekano wake ikiashiria utendaji wake ulikuwa ni wa tofauti, na tuliona wanyama wale waliwakilisha zile FALME 4 zitakazotawala mpaka mwisho wa Dunia, wa kwanza ukiwa ni Babeli, wapili, Umedi & uajemi, watatu Uyunani na wanne ambao ni wa mwisho ni RUMI.

Lakini tukiendelea na mlango huu wa 8, tunaona Danieli akionyeshwa maono mengine ya kipekee yanayohusiana na mambo yatakayokuja kutokea huko mbeleni kuhusiana na hizo falme kama Danieli 8:19 inavyosema.." Akaniambia, Tazama, nitakujulisha yatakayokuwa wakati wa mwisho wa ghadhabu; maana, ni ya wakati wa mwisho ulioamriwa. "

Tusome.
Danieli 8:1-4"
1 Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake mfalme Belshaza maono yalinitokea mimi, naam, mimi Danieli, baada ya hayo yaliyonitokea hapo kwanza.
2 Nami naliona katika maono; ilitukia, nilipoona, nalikuwako huko Shushani ngomeni, katika wilaya ya Elamu; nikaona katika maono, nami nalikuwa karibu na mto Ulai.
3 Ndipo nikainua macho yangu nikaona, na tazama, mbele ya mto alisimama kondoo mume, mwenye pembe mbili; na pembe zile mbili zilikuwa ndefu; lakini moja ilikuwa ndefu kuliko ya pili, na ile iliyokuwa ndefu zaidi ilizuka mwisho.
4 Nikamwona huyo kondoo mume akisukuma upande wa magharibi, na upande wa kaskazini, na upande wa kusini; wala hakuna mnyama ye yote awezaye kusimama mbele yake, wala hakuna mnyama ye yote awezaye kupokonya mkononi mwake; lakini alitenda kama alivyopenda mwenyewe, akajitukuza nafsi yake.

Danieli katika maono haya alimwona kondoo mume mwenye pembe mbili, kumbuka ukiendelea mbele kwenye mstari wa 20 utaona tafsiri yake kuwa huyo kondoo anawakilisha ufalme wa UMEDI & UAJEMI,..
"20 Yule kondoo mume uliyemwona, mwenye pembe mbili, hizo ndizo wafalme wa Umedi na Uajemi. "

Na kama tunavyosoma hapo pembe moja ilikuwa ndefu kuliko nyingine na ndio iliyozuka mwishoni hii ikiwa na maana kuwa mfalme mmoja atakuwa na nguvu kuliko mwingine na huyu sio mwingine zaidi ya Koreshi mfalme wa UAJEMI ambaye tunaona alinyanyuka mwishoni baada ya Dario ambaye alikuwa ndugu yake mfalme wa Umedi kufa, Hivyo Ufalme wa Uajemi chini ya Koreshi uliimarika sana, mpaka ulipofikia wakati wa utawala wa Mfalme Ahasuero aliyemtwaa Esta kuwa malkia.

Na pia tunaona kondoo huyu akisukumu pande zote nne za nchi ikiashiria kuwa alifanikiwa kuteka sehemu kubwa ya dunia na mataifa makubwa, kuanzia India mpaka Ethiopia, jambo hili tunaweza tukalisoma katika kitabu cha Esta 1:1..." Zamani za Ahasuero; naye huyu Ahasuero alimiliki toka Bara Hindi mpaka Kushi, juu ya majimbo mia na ishirini na saba; "

Alionekana pia akijitukuza nafsi yake, ni dhahiri kuwa milki kubwa aliyokuwa nayo ni rahisi kujinyanyua moyo hivyo pengine alifikiri kuwa hakuna taifa lolote lingeweza kumwangusha. lakini kama tunavyoendelea
  
Mstari wa 5-8" unasema...

5 Nami nilipokuwa nikifikiri, tazama, BEBERU akatoka upande wa magharibi, juu ya uso wa dunia nzima, bila kuigusa nchi; na beberu yule alikuwa na pembe mashuhuri kati ya macho yake.
6 Naye akamwendea huyo kondoo mume mwenye pembe mbili, niliyemwona akisimama karibu na mto, akamshambulia kwa ghadhabu za nguvu zake.
7 Nikamwona akimkaribia kondoo mume, akamwonea hasira kali, akampiga kondoo mume, akazivunja pembe zake mbili; na huyo kondoo mume alikuwa hana nguvu kusimama mbele yake; bali akamwangusha chini, akamkanyaga-kanyaga; wala hapakuwapo awezaye kumwokoa kondoo mume katika mkono wake.
8 Na yule beberu akajitukuza sana; na alipokuwa na nguvu, pembe ile kubwa ilivunjika; na badala yake zikazuka pembe nne mashuhuri zilizoelekea pepo nne za mbinguni.

Vivyo hivyo ukienda mbele kusoma mstari wa 21-22 utaona tafsiri ya yule beberu kuwa ni Ufalme wa UYUNANI, ambao ndio ulioungusha ufalme wa Umedi na Uajemi,...{"21 Na yule beberu, mwenye manyoya mengi, ni mfalme wa Uyunani; na ile pembe kubwa iliyo kati ya macho yake ni mfalme wa kwanza.22 Tena katika habari ya pembe ile iliyovunjika, ambayo badala yake zilisimama pembe nne, falme nne zitasimama kutoka katika taifa lile, lakini si kwa nguvu kama zake. "}

Kumbuka kama tulivyosoma katika milango iliyopita, ufalme wa tatu uliokuja kutawala dunia ulikuwa ni UYUNANI na ndio unawakilishwa na yule chui mwenye vichwa 4 katika Danieli sura ya 7,

Hivyo Danieli anaonyeshwa tena jambo lile lile katika ono tofauti lakini kwa undani zaidi, na Beberu huyu anaonekana akija akiwa na PEMBE MOJA MASHUHURI katikati ya macho yake naye akaenda kumvamia yule kondoo mwenye pembe mbili na kumwangamiza kabisa.

"Alexanda Mkuu" ndio ile pembe mashuhuri iliyozuka, Historia inasema mtu huyu alifanikiwa kuteka falme nyingi kwa kipindi cha muda mfupi sana, ndani ya miaka 12 alikuwa ameshaitiisha sehemu kubwa ya dunia kuanzia makedonia, India, hadi Misri na ilipofika 331 KK aliidondosha ngome ya Umedi na Uajemi (ndio yule kondoo) na kuiangamiza kabisa.

Na kama tunavyosoma mstari wa 8, tunaona ile pembe ilipokuwa na nguvu ilivunjika ghafla, na badala yake zikazuka pembe nyingine 4 mashuhuri. Historia inaonyesha Alexandra Mkuu, ambaye ndio ile pembe, alikufa ghafla na ugonjwa akiwa bado kijana wa miaka 31, Hivyo baada ya kufa hakuonekana wa kumrithi, hivyo wale majenerali wake 36 waliokuwa chini yake walianza kuupigania ufalme, hakuonekana aliyekuwa na nguvu kama za Alexanda hivyo mwishoni walikuja kuishia wanne tu, na kuugawanya ufalme katika pande nne sawasawa na biblia ilivyotabiri. Na majenerali hao walikuwa ni:

1)Cassander - Alitawala pande za magharibi ambazo ni Makedonia na Ugiriki
2)Lysimachus -Alitawala pande za kaskazini ambazo ni Bulgaria na maeneo ya Asia ndogo
3)Ptolemy - Alitawala pande za kusini ambayo ni Misri
4)Seleucus - Alitawala pande za Mashariki ambazo zilikuwa Israeli, Syria na mashariki yake.

Kumbuka hizi Pembe NNE ndio vile Vichwa vinne Danieli alivyoonyeshwa katika yule mnyama wa tatu, aliyefanana na CHUI katika Danieli sura ya 7.

Lakini tukiendelea kusoma kuanzia ule mstari wa 9 hadi wa 14 tunaona PEMBE nyingine NDOGO, ikizuka katikati ya moja ya zile pembe nne.

Tusome..
"9 Na katika moja ya pembe hizo ilitokea pembe ndogo, iliyokua sana, upande wa kusini, na upande wa magharibi, na upande wa nchi ya uzuri.
10 Nayo ikakua, kiasi cha kulifikilia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota, ikazikanyaga.
11 Naam, ikajitukuza hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo, ikamwondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini.
12 Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.
13 Ndipo nikamsikia mtakatifu mmoja akinena, na mtakatifu mwingine akamwuliza huyo aliyenena, Haya maono katika habari ya sadaka ya kuteketezwa ya daima, na lile kosa lifanyalo ukiwa, yataendelea hata lini, kukanyagisha patakatifu na jeshi?
14 Akamwambia, Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa. "

PEMBE NDOGO

Hii Pembe ndogo iliyozuka kati ya zile nne, historia inaonyesha ni mtawala aliyezuka katika ufalme wa Seleucus mmoja wa wale watawala wanne ambaye alikuwa wa mashariki, na tunaona ilizidi kujiimarisha mpaka kufikia NCHI YA UZURI (AMBAYO NI ISRAELI), Na mtawala huyu si mwingine zaidi ya ANTIOKIA IV, EPIFANE. Aliyetawala kuanzia 175-164 KK ..alijiita EPIFANE, akiwa na maana kuwa yeye ni "MUNGU ALIYEDHIHIRIKA", huu ni mfano wa kile kile cheo cha mpinga-kristo atakayenyanyuka siku za mwisho. Kumbuka mambo yanayoandikwa, au yaliyotokea katika historia ni kivuli cha mambo yatakayokuja kutokea siku za mwisho.

Lakini tukisoma mstari wa 10 tunaona "Nayo ikakua{PEMBE}, kiasi cha kulifikilia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota, ikazikanyaga.

Kumbuka nyota za mbinguni zinafananishwa na makuhani wa Mungu, au viongozi wa watakatifu wa Mungu, ukisoma (Danieli 12:3., na ufunuo 2 & 3)utaona hilo jambo. Hivyo historia inaeleza huyu mtawala katili ANTIOKIA alishuka Yerusalemu na kuanza kuua wakuhani wa Mungu walokuwa wanahudumu katika nyumba ya Mungu na kuzuia watu wasitoe dhabihu katika nyumba ya Mungu( Hekaluni) na ndio maana ukisoma mstari wa 11 unasema " Naam, ikajitukuza{hiyo pembe} hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo, IKAMWONDOLEA SADAKA YA KUTEKETEZWA YA DAIMA, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini".

Hivyo kuanzia huo wakati wayahudi wote walikatazwa kufanya ibada yoyote katika nyumba ya Mungu, badala yake Antiokia akawalazimisha wayahudi wafuate tamaduni za kipagani za kigiriki badala ya sheria ya Musa.

Alizidi hata kufikia hatua ya kuiba vyombo vya hekaluni na kutengeneza madhabahu ya mungu wake wa kipagani-ZEU ndani ya HEKALU la Mungu, Hilo ni chukizo kubwa sana kwa Mungu na kwa Wayahudi, aliendelea kwa kuchinja vitu haramu kama nguruwe na kunyunyiza damu juu ya madhabahu ndani ya hekalu la Mungu. Na wayahudi walipojaribu kwenda kinyume naye juu ya kulichafua hekalu la Mungu aliwaua wengi kikatili na wengine kuwauza utumwani, alikataza wayahudi kutahiriwa, yeyote atakayekiuka adhabu yake ilikuwa ni kifo, wayahudi walilazimishwa kula nyama za nguruwe na kutolea dhabihu miungu migeni ya kigiriki mambo ambayo ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu. Lakini kumbuka haya yote yaliwapata wayahudi kwasababu ya MAKOSA YAO, kama mstari wa 12 unavyoeleza...."12 Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, KWASABABU YA MAKOSA; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa. "

Wayahudi walimsahau Mungu na kuacha kuzishika sheria zake hivyo Mungu akaruhusu kiongozi mbaya na mkatili kama huyu anyanyuke dhidi yao. Lakini baadaye Mungu alikuja kumuhukumu na kufa ghafla.

Kumbuka Antiokia ni kivuli cha mpinga-kristo atakayekuja, biblia inasema atajiinua nafsi yake na kutaka kuabudiwa kama Mungu tunasoma.1Wathesalonike 2:3 Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; 4 yule mpingamizi, AJIINUAYE NAFSI YAKE JUU YA KILA KIITWACHO MUNGU, AMA ; hata yeye mwenyewe KUKETI KATIKA HEKALU LA MUNGU, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu. "

Na kama vile Antiokia aliwalazimisha wayahudi waikane imani yao na kuabudu miungu ya kipagani, vivyo hivyo na mpinga-kristo (PAPA) atawalazimisha watu wa ulimwengu mzima kupokea dini yake inayotambulishwa na ile chapa, na yeyote atakayepinga adhabu yake itakuwa ni kifo cha mateso kama ilivyokuwa kwa Antiokia kumbuka wakati hayo yanatokea kanisa litakuwa limeshanyakuliwa.

Tukiendelea mstari wa 13-14 inasema..
"13 Ndipo nikamsikia mtakatifu mmoja akinena, na mtakatifu mwingine akamwuliza huyo aliyenena, Haya maono katika habari ya sadaka ya kuteketezwa ya daima, na lile kosa lifanyalo ukiwa, yataendelea hata lini, kukanyagisha patakatifu na jeshi? 14 Akamwambia, Hata nyakati za jioni na asubuhi ELFU MBILI NA MIA TATU (2300); ndipo patakatifu patakapotakaswa. "

Hizi siku 2300 ni sawa na miaka sita na theluthi moja hivi, ndipo uovu wote utaondolewa katika hekalu la Mungu, na Historia inaonyesha tangu kipindi Antiokia kuzuia sadaka za kuteketezwa mpaka siku ziliporejeshwa tena, ilikuwa ni siku 2300 kamili kama unabii ulivyotabiri.

Hii ilitokea pale baadhi ya wayahudi kutokuvumiliana na vitendo vya Antiokia na kuamua kuasi kwa kuingia vitani hivyo wakanyanyuka wana wa Matthatias mmoja wao akiwa YUDA MAKABAYO, na kwenda porini kumpinga Antiokia siku zote za utawala wake, walifanikiwa kumshinda na kuichukua tena YERUSALEMU na KULIWEKA TENA WAKFU Hekalu la Mungu baada ya kuchafuliwa kwa muda mrefu, hivyo wakatimiza unabii wa siku 2300 hii ilikuwa ni mwaka 164 KK. Siku hiyo wayahudi wakaanza tena kutoa sadaka za kuteketezwa, Na ndipo ile sikukuu ya KUTABARUKU ilianzia hapo {KUTABARUKU ni kuweka wakfu} (Yohana 10:22).

Kumbuka ndugu Danieli alionyeshwa mambo hayo kwa ajili ya SIKU ZA MWISHO, kwa sehemu yametimia kama KIVULI TU, lakini matukio halisi yenyewe yatakuja katika vizazi hivi vya siku za mwisho siku mpinga-kristo atakaposimama na kuwakosesha watu wengi.

Hivyo ndugu biblia inasema 2Thesalonike 2:
7 Maana ILE SIRI YA KUASI HIVI SASA INATENDA KAZI; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.

Biblia inasema ni SIRI, hivyo inahitaji hekima kuigundua, utendaji kazi wake ni katika SIRI, na JINA lake pia lipo katika SIRI, BABELI MKUU MAMA WA MAKAHABA NA MACHUKIZO YA NCHI!(Ufunuo 17:5). ni roho ile ile iliyokuwa kwa Antiokia, ndio ipo mpaka sasa hivi, IBADA ZA SANAMU katika nyumba ya Mungu(KANISA), pombe kanisani, uasherati kanisani, ushoga kanisani, vimini kanisani, burudani kanisani, sanaa & siasa kanisani, mizaha kanisani, biashara kanisani n.k. haya yote ni machukizo kama aliyofanya Antiokia na Belshaza juu ya nyumba ya Mungu. Ni roho ile ile.

2Wakoritho 6:15 Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?
16 Tena pana mapatano gani kati ya HEKALU LA MUNGU NA SANAMU? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
17 Kwa hiyo, TOKENI KATI YAO, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.
18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, "

EPUKA ROHO YA UDHEHEBU NA DINI ZA UONGO MGEUKIE KRISTO AYASAFISHE MAISHA YAKO KWA NENO LAKE NA UZALIWE MARA YA PILI ILI UWE MTAKATIFU. Kwasababu biblia inasema pasipo huo UTAKATIFU hakuna mtu atakayemwona Mungu(Waebrania 12:14).

Mungu akubariki.

Tuesday, February 20, 2018

DANIELI: Mlango wa 7

Jina la BWANA wetu YESU KRISTO lihimidiwe.

Katika sura zilizotangulia (yaani ya 1-6), tuliona zikielezea sana sana historia za maisha ya watakatifu waliyopitia zaidi kuliko unabii lakini kuanzia Mlango huu wa 7 na kuendelea tunaona Danieli akionyeshwa maono ya mambo yatakayokuja kutokea katika siku za mwisho. Tukisoma..

Danieli 7:1-8" Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danieli aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.
2 Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa.
3 Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali.
4 Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake yakafutuka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu.
5 Na tazama, mnyama mwingine, wa pili, kama dubu, naye aliinuliwa upande mmoja, na mifupa mitatu ya mbavu ilikuwamo kinywani mwake katika meno yake; wakamwambia mnyama huyo hivi, Inuka, ule nyama tele.
6 Kisha nikatazama, na kumbe! Mnyama mwingine, kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka.
7 Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama, mnyama wa nne, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi.
8 Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang'olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu.

Tukirejea kwenye ile sura ya pili tunaona jinsi Mfalme Nebudreza akionyeshwa katika ndoto Falme nne zitakazotawala dunia mpaka hapo ALIYE JUU(YESU KRISTO) atakapochukua Falme zote za dunia, hivyo Danieli alimpa tafsiri yake, Ufalme wa kwanza ukiwa ni Babeli, wa pili ukiwa ni Umedi na uajemi, wa tatu ukiwa ni ufalme wa uyunani na wa nne ni Rumi. Jambo hili hili tunaona linajirudia tena katika sura hii ya 7, Danieli akifunuliwa zile zile Falme 4 zitakazotawala ulimwengu wote mpaka mwisho wa dunia isipokuwa hapa anaonyeshwa kwa undani zaidi.

Hapa aliona wanyama 4, wakitoka baharini, kumbuka bahari inawakilisha mikusanyiko ya watu wengi(makutano){ufunuo 17:15, } hivyo hizi falme zitanyanyuka kutoka katikakati ya watu.Kumbuka wanyama hawa 4 Danieli aliowaona ndio yule yule mnyama Yohana alioonyeshwa akitoka Baharini mwenye vichwa 7 na pembe 10, wa kwenye Ufunuo 13 isipokuwa hawa wameunganishwa wote pamoja..

"ufunuo 13:1 Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa MFANO WA CHUI, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya DUBU, na kinywa chake kama kinywa cha SIMBA, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi. "
Tutazame wanyama hawa.
 

MNYAMA WA KWANZA:

Kama tunavyosoma yule mnyama wa kwanza alionekana kama mfano wa SIMBA na akiwa na mabawa ya tai, kumbuka utawala wa kwanza Babeli ndio uliohusika kuwapeleka wana wa Israeli utumwani, ulifananishwa na simba ukisoma Yeremia 4:5-6 inaelezea kuwa watu walioichukua Israeli mateka na kuwapeleka Babeli walifananishwa na kama simba aangamizaye mataifa. Na pia kama anavyoonekana na mabawa ya tai hii inaashiria uharaka wake katika kuteka, kitu kinachopaa siku zote kina kasi kuliko vinavyokwenda kwa miguu hivyo Babeli ulikuwa mwepesi wa kuteka.

Habakuki 1:6" Kwa maana, angalieni, nawaondokesha Wakaldayo {wakaldayo ni wa-babeli}, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao."
7 Hao ni watu wa kutisha sana, wa kuogofya sana; hukumu yao na ukuu wao hutoka katika nafsi zao wenyewe.
8 Farasi zao ni wepesi kuliko chui, ni wakali kuliko mbwa-mwitu wa jioni; na wapanda farasi wao hujitapa naam, wapanda farasi wao watoka mbali sana; HURUKA KAMA TAI AFANYAYE HARAKA ALE. "

Kwahiyo tunaona hapo yule mnyama wa kwanza ni ufalme wa Babeli ambao ulikuja kuanguka baadaye na kunyanyuka mwingine wenye nguvu kushinda huo.
 

MNYAMA WA PILI:

Mnyama huyu anaonekana akifanana na Dubu, na pia anaonekana kama ameinuliwa upande mmoja ikiwa na maana kuwa anazo pande mbili na upande mmoja imezidi mwingine, na tunafahamu utawala huu si mwingine zaidi ya ufalme wa UMEDI na UAJEMI, na historia inaonyesha ufalme wa Uajemi ulikuwa na nguvu zaidi kuliko Umedi , hivyo zilipoungana zikaja kuundoa ufalme wa Babeli katika mamlaka yake na kuimiliki dunia upya, na pia yule Dubu anaonekana akiwa na MIFUPA MITATU ya mbavu kinywani mwake hizi ni ngome tatu walizoziangusha hawa wafalme wa Umedi na Uajemi, nazo ni Lidya, Misri na Babeli.

Ukisoma Isaya 13:15 ilishatabiri ukatili wake hata kabla ya utawala huo kunyanyuka.inasema ..
 
"15 Kila mtu atakayeonekana atatumbuliwa, na kila mtu atakayepatikana ataanguka kwa upanga.
 16 Na watoto wao wachanga watavunjwa-vunjwa mbele ya macho yao, nyumba zao zitatekwa nyara, na wake zao watatendwa jeuri.
17 Tazama, nitawaamsha WAAMEDI juu yao, ambao hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu.
18 Na nyuta zao zitawaangusha vijana; wala hawatahurumia mazao ya tumbo; jicho lao halitawahurumia watoto.
19 Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza."

ukizidi kusoma utaona huyu mnyama anaambiwa "ainuke ale nyama tele" ikiwa na maana kuwa atapewa uwezo wa kuteka mataifa mengi, na ndivyo ilivyokuja kuwa, katika historia inaonyesha Umedi na Uajemi uliteka na kutawala mataifa mengi Kuanzia India mpaka Ethiopia majimbo 127 (Esta 1:1) inaelezea vizuri.

MNYAMA WA TATU:

Mnyama huyu wa tatu Danieli alimwona akiwa mfano wa chui mwenye vichwa vinne, tukisoma.."6 Kisha nikatazama, na kumbe! Mnyama mwingine, kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka."

Huu ni utawala wa UYUNANI (UGIRIKI) ambao ulikuja kunyanyuka baada ya mtawala wa Uyunani "Alexander the great" kuiangusha ngome ya Umedi na Uajemi, ni mtawala aliyekuwa na nguvu sana, kama chui alivyo mwepesi wa kushika mawindo yake, ndivyo ilivyokuwa kwa huyu mtawala mdogo, kila alipokwenda kupigana na maadui zake alifanikiwa, kwa muda wa miaka 12 tu alikuwa tayari amekwishafanikiwa kuiteka dunia nzima. Lakini naye pia hakudumu sana katika utawala wake, alipokuwa na miaka 31 alipata ugonjwa na kufa, hivyo hakuacha mtu wa kumrithi baada yake, Hivyo ikasabisha wale majemedari waliokuwa chini yake kupigania ufalme lakini hakufanikiwa kutokea mwenye nguvu kama za Alexander hivyo ufalme ule ukagawanyika katika pande NNE, Ambavyo ndio vile vichwa vinne vya yule mnyama; Cassander, Lysimachus ,Ptolemy na Seleucus
 
 

MNYAMA WA NNE:

"7 Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama, mnyama wa nne, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi.

Mnyama huyu ni utawala wa RUMI, ndio ile miguu ya chuma kwenye yale maono aliyoyaona Mfalme Nebukadreza kwenye Danieli 2, na mnyama huyu hapa anaonekana akiwa na meno ya chuma, ikiashiria ana nguvu nyingi za kuharibu na kusagasaga, na pia hapa anaonekana na pembe 10, ambavyo ndio vile vidole 10 vya kwenye ile sanamu ya Nebukadreza. Kumbuka utawala huu ndio uliokuwa utawala katili kuliko yote iliyotangulia, na ndio unaotawala hata sasa katika roho,Lakini Katika historia, utawala wa Rumi ya magharibi ulikuja kugawanyika katika mataifa 10 yanayojitegemea AD 476, ambayo ni

1) Alemanni- kwa sasa ni Ujerumani
2) Franks - kwa sasa ni Ufaransa
3) Burgundians-Kwa sasa ni uswizi
4) Visigoths -Hispania
5) Lombards-Italia
6) Anglo-Saxons- Uingereza
7) Suevi- Ureno
8) Vandals -iling'ofolewa na ile pembe ndogo iliyozuka
9) Ostrogoths-ilingom'ofolewa na ile pembe ndogo iliyozuka
10) Heruli- iling'ofolewa na ile pembe ndogo iliyozuka

Lakini tukiendelea kusoma mstari wa 8 tunaona kuna PEMBE nyingine ndogo ikizuka

“8 Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake PEMBE TATU katika zile za kwanza zikang'olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu.

Hivyo baada ya Danieli kuona haya alitamani kufahamu ile pembe ndogo maana yake ni nini??, Kama tunavyosoma Danieli 7:19 Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake;
20 na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake.

Kumbuka Pembe zinawakilisha ufalme au mfalme, Hivyo zile pembe 10 zinasimama kama wafalme wenye falme, vivyo hivyo na ile pembe ndogo ya 11 iliyoonekana kuzuka na kung'oa pembe nyingine tatu ni mfalme atakayenyanyuka na kuangusha wafalme wengine watatu. Historia inaonyesha mara baada ya utawala wa RUMI kugawanyika katika zile Falme 10, utawala wa KIPAPA ulizuka na kungusha tatu ya hizo ngome 10, pale zilipotaka kushindana na utawala wa PAPA aliziharibu kabisa na kuzishinda na hizo si nyingine zaidi ya Vandals, Ostrogoths na Heruli.

Na kama tunavyosoma pembe hiyo ilijitukuza sana na kunena maneno makuu ya makufuru, tunafahamu cheo pekee kinachosimama kama Mungu duniani ni cheo cha UPAPA, leo hii katika enzi yake yeye anasimama kama " badala ya Kristo duniani", anao uwezo wa kusamehe dhambi, anafahamika kama mtawala wa mbinguni, duniani, na chini ya nchi, N.K. hayo yote ni maneno ya makufuru mbele za Mungu. watu wanamtazama duniani yeye kama Mungu.

Lakini Mstari wa 21 unasema. " Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; " hakuishia tu katika kujitukuza lakini aliendelea hata kufanya vita na watakatifu Hili ni jambo limekuwa likijirudia katika historia tangu utawala wa KIPAPA chini ya Kanisa Katoliki uanze, wakristo wengi wamekuwa wakiuliwa kikatili pindi tu pale walipoonekana wanaenda kinyume na Dini hiyo. Wakristo zaidi ya milioni 68 waliuawa kikatili walipoonekana tu wanalishika Neno na kupinga mafundisho ya uongo ya kanisa hilo. Kumbuka wakatoliki sio wapinga-kristo isipokuwa ule mfumo wa lile kanisa na kile cheo anachokikalia kiongozi wa lile kanisa ndio cha MPINGA-KRISTO MWENYEWE.

Mstari wa 25 unasema " Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa WAKATI, NA NYAKATI MBILI, NA NUSU WAKATI ". Hii inafunua siku mpinga-Kristo yule PAPA wa mwisho atakaposimama kutenda kazi.

Kumbuka hawa PAPA waliopo sasa hivi na waliopita wamekaa katika viti vya mpinga-kristo lakini yupo MMOJA atakayesimama na kubadilisha majira, na sheria, biblia inasema 
 
( 1Yohana 2:18 "Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba MPINGA KRISTO YUAJA , hata sasa WAPINGA KRISTO WENGI wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho).

Na siku sio nyingi atasimama atawale na kuitesa dunia kwa nyakati na nyakati mbili na nusu wakati, ambayo ni miaka mitatu na nusu, kwasababu kibiblia nyakati moja ni mwaka mmoja.

Hivyo hiyo itakuwa ni miaka mitatu na nusu ya dhiki kuu,. labda anaweza akawa ndio huyu PAPA aliyepo sasa au mwingine muda utaeleza yote.. Huu ni wakati wa kujiweka tayari muda wowote mambo yanabadilika, Hauoni sasa hivi anavyozunguka kuleta DINI zote pamoja, akiwa kama mtu mwenye wafuasi wengi kuliko wote duniani. Kilio chake ni AMANI! AMANI! kwa kivuli hicho anatafuta ufalme ili baadaye aje kupambana na uzao wa Mungu.

Biblia inasema..1Wathesalonike 5:1-3" Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.Wakati wasemapo, KUNA AMANI NA SALAMA, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. "
 
Ndugu wakati umeisha usidanganyike na watu wanaosema dunia haishi leo wala kesho, geuka weka mambo yako sawasawa yahusuyo wokovu.Huu ulimwengu unapita na mambo yake yote.

Mstari wa 9-10. unasema..." Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao.10 Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na VITABU VIKAFUNULIWA.

Hapa tunaona mwisho wa yote vitabu vitafunguliwa vihusuvyo maisha yetu, kila mtu na kitabu chake na utahukumiwa katika hicho, je! kitabu chako unakiandikaje? Biblia inasema sisi ni barua, na kila siku tunafungua kurasa mpya wa vitabu vyetu, na siku ile utakapokufa kitafungwa kikingojea kufunguliwa tena katika siku ile ya HUKUMU.

Hivyo tukiona mambo haya tunajua kabisa ule mwisho umekaribia UTAWALA USIOWEZA KUHARIBIKA wa mwokozi wetu ,hivi karibuni utakuja hapa ulimwenguni,.BWANA wetu YESU KRISTO MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA, atamiliki pamoja na watakatifu wake milele tunasoma..
27 Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; UFALME WAKE NI UFALME WA MILELE, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii.

2Petro 1:10" Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe."

AMEN!

Monday, February 19, 2018

DANIELI: Mlango wa 6


Jina KUU la Bwana wetu YESU KRISTO libarikiwe.
 
Ndugu mpenzi karibu tujifunze Neno la Mungu na leo tukiwa katika mwendelezo wa kitabu cha Danieli, kama Biblia inavyosema, katika 2 Timotheo 3:16" Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa MAFUNDISHO, na kwa kuwaonya watu makosa yao, NA KWA KUWAONGOZA, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema."

Hivyo kila habari tunayoisoma katika biblia kwa namna moja au nyingine ina mafunzo tosha ya kutufanya sisi tuenende kiukamilifu katika safari yetu hapa duniani pasipo kukwazwa na majaribu ya aina yoyote ya shetani, na ndio maana maandiko yanasema " Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. (1Wakoritho 10:11) ". Kwahiyo mambo yote waliyoyapitia watakatifu wa kale ni kwa ajili ya kutuonyesha sisi njia ya kupita tunapokumbwa na majaribu kama ya kwao. 
 
Katika sura hii ya sita Danieli licha ya kwenda katika ukamilifu wake wote lakini bado tunaona akiingizwa katika majaribu mazito, kama tunavyoweza kusoma habari hii:

Danieli 6:1-18"

1 Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote;
2 na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara.
3 Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote.
4 Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake.
5 Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, TUSIPOIPATA KATIKA MAMBO YA SHERIA YA MUNGU WAKE.
6 Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele.
7 Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.
8 Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.
9 Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.
10 Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.
11 Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.
12 Ndipo wakakaribia, wakasema mbele ya mfalme katika habari ya ile marufuku ya mfalme; Je! Hukuitia sahihi ile marufuku, ya kwamba kila mtu atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme, atatupwa katika tundu la simba? Mfalme akajibu, akasema, Neno hili ni kweli, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi isiyoweza kubadilika.
13 Basi wakajibu, wakasema mbele ya mfalme, Yule Danieli, aliye mmoja wa wana wa wale waliohamishwa wa Yuda, hakujali wewe, Ee mfalme, wala ile marufuku uliyoitia sahihi, bali aomba dua mara tatu kila siku.
14 Basi mfalme aliposikia maneno haya alikasirika sana, akakaza moyo wake ili kumponya Danieli; akajitaabisha kumwokoa hata jua likachwa.
15 Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme.
16 Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya.
17 Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli.
18 Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa.

Kama tukifuatilia habari hii tunaona Danieli alitumika kikamilifu katika kazi zote za uliwali pasipo dosari yoyote, alikuwa mwaminifu, hakuruhusu jambo lolote ovu limkoseshe katika kazi zake za uliwali siku zote za maisha yake, hakuwa anakula rushwa, wala kuwa na matumizi mabaya ya fedha za ufalme katika mamlaka aliyopewa, na ndio maana mfalme ilibidi atafute watu watatu waaminifu ambao wataweza kuzisimamia hizo hazina kubwa za fedha ili mfalme asipate hasara katika mahesabu yake na mmojawao alikuwa ni Danieli.

Lakini haikuwa hivyo kwa wale wakuu wenzake waliokuwa na Danieli, wao walikuwa wanatafuta faida zao wenyewe, mambo kama ufisadi, rushwa, na ubadhilifu wa fedha vilikuwa ni sehemu ya maisha yao, Hivyo mtu kama Danieli alikuwa ni kikwazo kikubwa kwao. Pengine walipojaribu kuhujumu fedha za nchi Danieli aliwakemea na kuwashitaki kuwa wanachokifanya sio sawa, Hivyo ikawapelekea kumchukia Danieli sana na kuanza kumuundia visa, kwasababu nuru na giza haviwezi kuchangamana.

Kumbuka huo ulikuwa ni mpango wa shetani ndani ya watu, alipoona kuwa Danieli ni mkamilifu na hawezi kuuacha ukamilifu wake, akaamua kubadilisha kinyago chake na kuja na mbinu mpya, isipokuwa hii ni katika IMANI YAKE. Na hapo ndipo vita vinapokuwa vikali, pale unapolazimika kuchukua maamuzi ya NDIO AU HAPANA juu ya IMANI yako.

Na ndio maana ukisoma pale kwenye ule mstari wa 5 "Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, TUSIPOIPATA KATIKA MAMBO YA SHERIA YA MUNGU WAKE".

Kwahiyo wale wakuu tunaona waliunda SHERIA moja madhubuti ihusuyo IMANI katika DUNIA YOTE ili tu kumnasa mtu mmoja wapate kumuangamiza. Lakini Danieli alipoona kuwa ile amri imeshapitishwa hakuacha msimamo wake zaidi ya yote alifungua madirisha yake kuelekea YERUSALEMU na kuendelea kusali kutwa mara tatu kama ilivyokuwa desturi yake, alichukua uamuzi wa kukubali kufa kwa ajili ya imani yake, na walipomwona bado anashikilia uamuzi wake wakamtupa katika Tundu la Simba, lakini tunaona Bwana ni mwaminifu alikuja kumwokoa.

Vivyo hivyo mambo hayo waliyoyakuta akina Danieli na sisi pia yatatukuta kwa namna moja au nyingine, Kama hao walikuwa ni watoto wa Mungu waliopendwa wameyapitia hayo vivyo na sisi pia tutayapitia kama hayo. Kumbuka ikiwa wewe ni mkristo na unajiona umesimama katika imani yako, fahamu kuwa shetani anakuchunguza maisha yako kila siku, ni kweli unaweza ukawa hauli rushwa kazini kwako, au haufanyi uasherati, au haunywi pombe, au hauvai mavazi ya kikahaba au hauabudu sanamu au haukosi kwenda ibadani au kusali n.k. Hivyo vyote shetani anaviangalia na atakapokujaribu kwa ushawishi wa muda mrefu ili uache msimamo wako na kuona unazidi tu kuvishinda, atatafuta njia mbadala ambayo moja kwa moja itaathiri UHUSIANO wako wewe na Mungu, aidha ukiache uishi au uendelee nacho uangukie MATATIZO MAKUBWA.

Kwamfano umekuwa mwaminifu kwa bosi wako kazini kwa muda mrefu na anafahamu kuwa wewe ni mkristo, lakini hapa ghafla anakuletea ripoti ya kukulazimisha usaini mapatano ya rushwa, kumbuka yule ni bosi wako na ukimkatalia utafukuzwa kazi,mkumbuke Danieli,

Au wewe wewe desturi yako ni kujisitiri lakini ghafla sheria mpya inakuja ofisini ni lazima kuvaa suruali au vimini, na usipofanya hivyo ni kuhatarisha kazi yako, sasa hilo ni jaribu shetani anakuletea la kutumia nguvu ili umtendee Mungu wako dhambi kwamaana ameona kwa utaratibu huwezi, hivyo anakuja kwa nguvu. 
 
Au pengine kiongozi/mwalimu wako anakulazimisha ufanye naye uasherati usipokubali anakufelisha mitihani, au anakuzushia mabaya yatakayokupelekea hata pengine kufungwa. Katika mazingira kama hayo mkumbuke Yusufu, Kimbia! ni heri upoteze kila kitu kuliko kuipoteza nafsi yako.

Au wewe ni mwombaji mzuri, unasoma Neno, unafunga lakini unashangaa ghafla mzazi anatoa sheria nyumbani hakuna kuomba muda mrefu tena, hakuna kufunga, au hakuna kusoma NENO, unalazimishwa kurudia ibada za sanamu ambazo hapo mwanzo ulishaziacha, na ukijaribu kukataa tu, unatengwa na wazazi au unafukuzwa nyumbani. Usiogope kufukuzwa wala kutengwa hayo ni mapito ya muda tu! Bwana anakuwazia yaliyo mema.

Fahamu tu yatakapokutokea hayo yote usione kama Mungu amekuacha, wewe mkumbuke Danieli, mkumbuke Yusufu, mkumbuke Shedraka, Meshaki na Abednego, mkumbuke na Ayubu, mkumbuke Mordekai, hawa wote baada ya kuonekana wamesimama katika imani yao, shetani aliwaletea SHERIA ZA MASHARTI YA NGUVU. aidha ukubali kuabudu sanamu au ufe, aidha ukubali kuzini au uende gerezani, aidha ukuendelee kumtumikia Mungu wako kwa dua na sala au uishie kwenye matundu ya simba na moto. Lakini kumbuka mwisho wao hawa wote ulikuwa ni wa faraja, badala ya kuangamia kabisa walinyanyuliwa mara dufu. Hivyo usiogope yatakapokupata.
Na mambo hayo hayatamkuta kila mtu isipokuwa ni wale tu watoto wa Mungu waliosimama imara katika Imani ya YESU KRISTO, haya hayana budi kuja na ndio maana Bwana Yesu mwenyewe alisema.

Yohana 16:1-4 ” Maneno hayo nimewaambia, MSIJE MKACHUKIZWA.
2 Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.
3 Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi.
4 Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi.

Unaona hapo, shetani hatoweza kuvumulia kumuona mtoto wa Mungu anadumu katika utakatifu wakati wote hivyo ni lazima ameletee majaribu yatakayohusu imani yake na wakati mwingine Mungu anaruhusu kama vile Ayubu kwasababu biblia inasema. Wafilipi1:29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; “

Na pia inasema kwenye 2 Timotheo 3:12 "Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa."

Kumbuka pia jambo kama hili hili litajitokeza tena wakati wa kipindi cha dhiki kuu pale mpinga-kristo atakaponyanyuka na kuunda SHERIA MOJA YA SHARTI inayohusu IMANI, na shabaha yake itakuwa sio kila mtu aliye duniani bali ni kwa wale waliobaki (wasiokwenda kwenye unyakuo) wakristo vuguvugu wanawali-wapumbavu ambao watajaribu kutoshirikiana naye hao ndio watakaopitia dhiki kuu kwa kuteswa kwa mateso ambayo hayajawahi kuwako tangu ulimwengu kuumbwa. Na sheria itakuwa ni moja tu aidha uisujudie sanamu yake na kupokea chapa yake, ili uendelee kuisha au ukatae kuisujudia na kuteswa na kuuawa kikatili.

Kumbuka lile neno : Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. (1Wakoritho 10:11) ". Mambo ya kale ni kivuli cha mambo yanayokuja.

Hivyo ndugu kuna wakati unakuja mbeleni ulio mgumu sana, wa ulimwengu mzima kujaribiwa na yule mwovu shetani( katika dhiki kuu), Na huu ndio wakati wa kuziweka taa zetu sawa kwa kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu ili Bwana atuepushe na hiyo saa itakapofika (kwa kutunyakua). Kwasababu muda umeisha na wakati wowote Bwana anakuja kulichukua kanisa lake. NI WATAKATIFU TU! NDIO WATAKAOEPUKA HIYO DHIKI KAMA BWANA ALIVYOSEMA..

Ufunuo 3:10-11" Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, UTOKE KATIKA SAA YA KUHARIBIWA ILIYO TAYARI KUUJILIA ULIMWENGU WOTE, KUWAJARIBU WAKAAO JUU YA NCHI. Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako."

Kama bado haujatubu ndugu, ni vema ukafanya hivyo leo angali muda upo.

Ubarikiwe.