"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, April 26, 2018

YONA: Mlango 1

Yona alikuwa mmoja wa manabii wa Israeli wakati wa utawala wa Yeroboamu Mfalme wa Israeli, ambaye Mungu alimtumia sana kutoa unabii kadha wa kadha katika Israeli, kama tunavyomsoma katika (2Wafalme 14:21-25). Lakini ilifika wakati BWANA akataka kumtuma kwa watu wa Mataifa, Mji wa NINAWI uliokuwa mji mkuu wa Taifa la ASHURU ambalo kwa wakati ule lilikuwa ni moja ya ngome yenye nguvu duniani ndilo lililokuja baadaye kuhusika kuwachukua wana wa Israeli utumwani (2Wafalme 18:11), Mataifa mengine yakiwemo BABELI pamoja na MISRI. Kumbuka taifa la Ashuru liliyachukua yale makabila 10 na kuyapeleka Ashuru, na makabila mawili ya Israeli yaliyosalia (Yaani YUDA na BENYAMINI) Mfalme Nebukadneza, alikuja kuyachukua utumwani Babeli.

Hivyo mji wa NINAWI uliokuwa mji mkuu katika Ashuru ulijaa maovu mengi sana, mfano wa Sodoma na Gomora, mpaka kufikia wakati Bwana kutaka kuuangamiza mji wote na watu wote waliokuwepo kule, lakini Mungu alivyo wa rehema hawezi kufanya jambo lolote kabla hajawaonya kwanza watu wake, ili pengine waghahiri uovu wao wasiangamizwe, na ndivyo alivyofanya kwa kumtuma YONA nabii katika mji ule Mkubwa uliokuwa mbali sana na taifa la Israeli.

Lakini tunasoma habari haikuwa hivyo kwa YONA, badala ya kwenda NINAWI mji wa ASHURU alioagizwa na Bwana, yeye akaamua kuubuni mji wake yeye alioupenda ili akakae huko, ndipo akakimbilia TARSHISHI mji uliokuwa nchi ya Lebanoni ili tu AJIEPUSHE NA MAPENZI YA MUNGU.

Lakini alisahau kuwa ili afikie malengo yake hana budi kupitia “NJIA YA BAHARI”.. Hivyo akaamua kupanda Merikebu zinazoelekea Tarshishi, Na kama tunavyosoma habari alipokuwa katikati ya safari yake bahari ilichafuka na mambo yakaanza kuharibika..


Yona 1: 4 “Lakini Bwana alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.
5 Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.
6 Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.
7 Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.
8 Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani?
9 Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha Bwana, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.
10 Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa Bwana, kwa sababu alikuwa amewajulisha.
11 Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka.
12 Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata.
13 Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana.
14 Basi wakamlilia Bwana, wakasema, Twakuomba, Ee Bwana, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, Bwana, umefanya kama ulivyopenda.
15 Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka.
16 Ndipo wale watu wakamwogopa Bwana mno, wakamtolea Bwana sadaka, na kuweka nadhiri.
17 Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku”.


Bwana aliyaruhusu yote haya yampate YONA ili kutuonya sisi kwamba tusipotaka kuenda katika njia ambayo Mungu kaikusudia tuiendee,yatatukuta kama hayo hayo. Kama biblia inavyosema 1Wakoritho 10: 11 “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ILI KUTUONYA SISI, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.”


SWALI NI JE! NJIA YA BAHARI NI SALAMA?

Kibiblia BAHARI inawakilisha nini?…Ili kufahamu jambo hili ni vizuri tujue ni kitu gani kimo humo ndani yake .tukisoma. Ufunuo 13: 1 “KISHA NIKAONA MNYAMA AKITOKA KATIKA BAHARI, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.
2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.”…………Unaona hapo?.


Kumbuka YONA anawakilisha kundi la wakristo wasiotaka kudumu katika mapenzi ya Mungu (yaani VUGUVUGU).leo wanaenda na Mungu, kesho wanaenda katika akili zao, leo anafanya ibada kesho anakula rushwa. N.k. Sasa Kama vile YONA alivyokimbia uso wa Mungu na kuelekea njia ya BAHARINI na hatimaye kumezwa na yule SAMAKI MKUBWA, vivyo hivyo na kundi hili la wakristo wasiotaka kutengeneza mambo yao sasa vizuri na Mungu, hawajui kama wanakimbilia baharini pasipo wao kujua, ambapo kule kuna Yule mnyama mwenye vichwa saba na pembe kumbi ameandaliwa kuwameza.


Na bahari inawakilisha nini?
 
Tukirudi kusoma Ufunuo 17: 15 Kisha akaniambia, YALE MAJI ULIYOYAONA, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha.” Kumbuka huyu kahaba anayezungumziwa hapa ameketi juu ya Yule mnyama aliyetoka baharini ambaye tumemsoma katika Ufunuo 13.

Kwahiyo bahari au maji mengi inawakilisha mahali penye mkusanyiko wa watu wengi, hivyo Yule mnyama anatoka mahali penye mkusanyiko wa watu wengi, mahali ambapo amekubaliwa na wengi, tukizungumza katika roho leo hii mfumo wa mpinga-kristo unatenda kazi katikati ya mataifa, na dini nyingi za uongo.

Kama vile Yona alivyoiacha njia ya Mungu na kuchagua Njia ya BAHARI akidhani kuwa ni salama, vivyo hivyo na wakristo wa leo walio vuguvugu, wanamsahau Mungu na kushikimana na mambo maovu ya ulimwengu huu, Yona alisinzia pale alipoona kuna utulivu mwanzoni mwa safari yake, kadhalika kundi hili la wakristo vuguvugu wanasinzia kwasababu wanajiona wapo salama, wanaona hata wakifanya hivyo hakuna dhara lolote wanatakalolipata lakini hawajui kuwa kuna mnyama ameshaandaliwa kwa ajili yao chini ya Merikebu yao. Pale PEPO zitakapovuma ndipo watakapotambua kwamba hawapo salama, wakati huo unyakuo umeshapita, ndugu unajiona upo salama katika ulimwengu, hata ukitenda dhambi unaona hakuna dhara lolote linalokupata, angali unafahamu kabisa moyoni mwako umeukimbia uso wa Mungu na unayoyafanya sio sahihi na bado unajiita Mkristo, hujui kwamba ni NEEMA ya Mungu tu, imekushikilia dhidi ya Yule Mnyama utubu, ugeuze njia uepuke madhara yaliyopo mbeleni ambayo yapo karibuni kuupata ulimwengu mzima. Ipo siku NEEMA inayokushikilia itakwisha na moja ya siku hizi PEPO ZITAANZA KUVUMA BAHARINI. Kama biblia inavyosema katika..

Danieli 7: 1 “Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danieli aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.
2 Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, HIZO PEPO NNE ZA MBINGUNI ZILIVUMA KWA NGUVU JUU YA BAHARI KUBWA.
3 Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali”………

Wanyama hao Nabii Danieli alionyeshwa, watatu wa kwanza walishapitia na Yule wa mwisho wanne, ndiye aliyeko sasa chini ya MERIKEBU(NEEMA), na moja ya hizi siku pepo zitamwamsha kutenda kazi tukiendelea kumsoma:

“7 Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama,MNYAMA WA NNE, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi.
8 Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazukia kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang'olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu”.
Kama vile Nabii Yona alikaa ndani ya tumbo la samaki siku tatu usiku na mchana, kadhalika Huyu mnyama atokaye baharini atalimeza hili kundi la watu, kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu ndio kile kipindi cha dhiki kuu, mpinga-kristo atakaponyanyuka na kuanza kuleta dhiki isiyoelezeka kwa wale waliouvuguvugu kwa kuupenda ulimwengu huu, na kuiacha njia Mungu aliyowawekea wao waiendee.

Hichi kipindi kipo karibuni kutokea, Yule mnyama sasa anatenda kazi katika siri na watu wa Mungu wanasinzia hawaoni kuwa wapo katika hatari, wanadanganyika na utulivu uliopo sasa hivi kama vile Yona alivyodhani lakini biblia inasema 1Wathesalonike 5: 2 “Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile MWIVI ajavyo usiku. Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.

Ndugu usileweshwe na ulevi wa hii dunia hata kulala usingizi, Bwana yupo karibu kulichukua kanisa lake BIBI-ARUSI WA KWELI anayedumu katika Neno lake na UTAKATIFU, Na hatua za unyakuo zimeshaanza Bwana anawakusanya watu wake toka kila mahali, watu ambao macho yao yapo mbinguni, duniani wao ni kama wapitaji tu, hao ndio watakaofunuliwa siri za unyakuo lakini wengine wote ikiwemo wakristo vuguvugu, hawatajua lolote isipokuwa kumtazamia Yule mpinga-kristo mnyama atokaye baharini. Utajisikiaje siku ile wenzako wapo mbinguni kwenye KARAMU YA MWANA-KONDOO na wewe upo katika dhiki kuu na zaidi ya yote watakuja kutawala na Kristo milele na milele kama wafalme na makuhani wa Mungu na wewe upo kwenye ziwa la moto??. Ni vizuri utengeneze mambo yako sasa hivi kabla siku ile haijafika. Tubu ukabatizwe kwa Jina la BWANA YESU upate ondoleo la dhambi zako na uanze kuishia wokovu..

Mungu akubariki..


Tafadhali washirikishe na wengine mambo haya...

Usikose mwendelezo wa kitabu cha Yona wa sura zinazofuata.

Wednesday, April 25, 2018

ESTA: Mlango wa 8, 9 & 10. (SIKU KUU YA PURIMU)

Jina la YESU KRISTO BWANA wetu lisifiwe.

Karibu kwenye mwendelezo wa kitabu cha Esta, leo tukiwa katika sura za mwisho, yapo mambo mengi ya kujifunza yahusuyo safari yetu ya ukristo tunapopitia kitabu hichi, tunaona mara baada ya Hamani adui wa watu wa Mungu kuuawa, Malkia Esta ananyanyuka tena kumwomba mfalme ayaondoe madhara aliyokusudia juu ya wayahudi wote waliandikiwa kuuawa, tunasoma;

Mlango 8
1 Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akahudhuria mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu.
2 Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani.
3 Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi.
4 Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme.
5 Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, iandikwe kuzitangua barua za Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika majimbo yote ya mfalme.
6 Kwa maana niwezeje kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au niwezeje kuyatazama maangamizo ya jamaa zangu?
7 Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, kusema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi.
8 Basi waandikieni Wayahudi pia vyo vyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme hakuna awezaye kulitangua.
9 Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na maakida na maliwali, na wakuu wa majimbo toka Bara Hindi mpaka Kushi, majimbo mia na ishirini na saba, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao”.

Kama tunavyosoma ule msiba mkuu na uchungu ambao ulikuwa juu ya wayahudi wote duniani Bwana aliugeuza na kuwa furaha na shangwe kwao, ile nyumba ya Hamani pamoja na cheo chake walipewa Mordekai na watu wake, wale walioonekana hawana heshima katikati ya mataifa Bwana aliwapa heshima kuliko jamii za watu wote duniani. wale walioonekana wadogo wakawa wakuu katikati ya mataifa. Biblia inasema kukawa nuru na furaha kwao;

Hata ile siku waliyopanga kuwaangamiza wayahudi wote tarehe 13 mwezi wa 12, ndio ikawa tarehe hiyo hiyo ya wayahudi wote duniani kuwaangamiza maadui zao waliowazunguka na kuwatawala. Hivyo tarehe 14. na 15 ya mwezi huo huo wa 12 wakaifanya kuwa sikukuu yao ya ushindi Bwana aliowapa dhidi ya maadui zao, wakaifanya kuwa sikukuu ya kupelekeana zawadi, pamoja na karamu na furaha waliyoiita sikukuu ya PURIMU.

Esta 8: 15 "Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawi na nyeupe, mwenye taji kubwa ya dhahabu, na joho ya kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Shushani wakapaza sauti, wakashangilia.
16 IKAWA NURU na FURAHA na SHANGWE na HESHIMA kwa Wayahudi.
17 Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata FURAHA, na SHANGWE, KARAMU na SIKUKUU. HATA WENGI WA WATU WA NCHI WAKAJIFANYA WAYAHUDI, KWA KUWA HOFU YA WAYAHUDI IMEWAANGUKIA. "

Hivyo Bwana akawapa wayahudi wote kustarehe na kufurahi siku zote za ufalme wa Ahasuero.

Kumbuka habari yoyote tunayoisoma katika agano la kale ni kivuli cha mambo yatakayokuja kutokea mbeleni. Wakati wote shetani alipojaribu kuwaletea mateso na dhiki watu wa Mungu, Bwana alitolea wokovu na ushindi mkuu kwao, tunasoma habari ya wana wa Israeli jinsi walivyopiganiwa na Bwana dhidi ya maadui zao walipokuwa wanatoka Misri, wakati wa-Misri walipoona njia pekee iliyosalia ni kuwateketezea katika zile kingo za bahari ya shamu, kinyume chake, wao ndio walioteketezwa katika ile habari, ikawa shangwe kwa wayahudi, huo ulikuwa ni mfano wa PURIMU kwao.

Vivyo hivyo na sehemu nyingine zote, tunaona wakati wa wafilisti walipokuja kupigana na Israeli, wakati wa akina Shedraki, Meshaka, na Abadnego walipotupwa katika tanuru la moto, wakati wa Danieli alipotupwa katika tundu la simba, n.k. hata kwa Bwana wetu Yesu, tunaona jambo lile lile shetani alijaribu kumuua akidhani ameshinda, lakini ufufuo ulidhihirisha ushindi wake, wote hawa maangamizi yao yaligeuka kuwa wokovu mkubwa kwao...ikawa kama mfano wa PURIMU kwao.

Vivyo hivyo katika siku za mwisho shetani anashindana na UZAO wa Mungu, yaani wayahudi wa mwilini na wayahudi wa rohoni (wakristo), kama alivyofanya katika siku za kale, kumbuka HAMANI ni mfano wa mpinga-kristo atakayekuja, na Esta ni mfano wa BIBI-ARUSI wa Kristo. Kama vile HAMANI alivyokusudia kuwaangamiza wayahudi wote duniani, isipokuwa Esta kwasababu yeye alikuwa ni malkia..Vivyo hivyo na mpinga-kristo atakapotafuta kuwaua wayahudi wote (wa-mwilini na wa-rohoni) hatoweza kwa BIBI-ARUSI wa Kristo kwasababu wakati huo atakuwa ameshakwenda katika unyakuo yupo kwenye Jumba la kifalme mbinguni mfano wa Esta. Hivyo hayo madhara hayatamkuta yeye.

Mpinga-kristo (ambaye atakuwa ni PAPA wa wakati huo), atakusudia kuundoa uzao wote wa Mungu duniani kwa njia ya hila, kwa kisingizio cha kuleta amani duniani kama Hamani alivyofanya kuwasingizia wayahudi kwamba wamefarakana na watu wote wa dunia nzima, jambo ambalo si kweli. Hivyo katika siku hizo wayahudi wote, na wale wakristo wote waliokuwa vuguvugu waliokosa unyakuo watagharimika kuingia katika ile dhiki kuu Bwana aliyoizungumzia.

Japokuwa mpinga-kristo atafanikiwa kuua watu wengi, lakini haitakuwa kwa wote, kwasababu biblia inasema wapo watakaofichwa mbali naye,(Ufunuo 12) mpaka siku ile MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA, YESU KRISTO Atakapokuja na mawingu pamoja na bibi-arusi wake, kuwaokoa wateule wake walioko duniani, na kila jicho litamwona, atakaposhuka na kukusanya watu wake(wayahudi) toka pembe nne za dunia, hapo ndipo mataifa yote yatakapoomboleza kwa maana atakuja na upanga kinywani mwake, kama vile maadui wa wayahudi walivyoomboleza siku yao ilipofika, mbele ya Mordekai na Esta ndivyo itakavyokuwa siku ile mbele ya Bwana Yesu na watakatifu wake. Mataifa yaliyowatesa watu wa Mungu yataomboleza sana mbele zake.

Ufunuo 19:11 "Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.
12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.
13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
14 NA MAJESHI YALIYO MBINGUNI WAKAMFUATA, WAMEPANDA FARASI WEUPE, NA KUVIKWA KITANI NZURI, NYEUPE, SAFI.
15 Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.
16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA".

Umeona hapo, ukirudi kwenye Mathayo 24: 29 inasema….; Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;
30 ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.
31 Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu”.

PURIMU KWA WATU WA MUNGU.

Katika sura ya tisa ya kitabu cha Esta, kama vile tulivyoona jinsi wayahudi walivyosheherekea sikukuu ya PURIMU baada ya ushindi dhidi ya maadui zao, mpaka wale wasiokuwa wayahudi walijifanya kuwa kama wayahudi, kadhalika na katika siku hizo mpinga-kristo na mifumo yake yote mibovu pamoja na mataifa yote yaliyosalia wataangamizwa kwa maangamizo makuu katika vita vya Har-Magedoni. Wakati huo wengi watatamani kuwa kama watu wa Mungu lakini haitawezekana tena, kwao itakuwa ni MSIBA mkuu, wakati huo watoto wa Mungu kwao itakuwa ni KARAMU ya PURIMU. Kufarijiwa na kuburudishwa milele, na kufutwa machozi. Pale watakapomwona BWANA wao uso kwa uso akija kuwapigania na kuleta utawala mpya wa AMANI wa miaka 1000 usio wa shida wala uchungu.

Ufunuo 19:17 “Kisha nikaona malaika mmoja amesimama katika jua; akalia kwa sauti kuu, akiwaambia ndege wote warukao katikati ya mbingu, Njoni mkutane KWA KARAMU YA MUNGU ILIYO KUU;
18 mpate kula nyama ya wafalme, na nyama ya majemadari, na nyama ya watu hodari, na nyama ya farasi na ya watu wawapandao, na nyama ya watu wote, waungwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa.
19 Kisha nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake.
20 Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti;
21 NA WALE WALIOSALIA WALIUAWA KWA UPANGA WAKE YEYE ALIYEKETI JUU YA YULE FARASI, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.”

Unaona hapo ndugu hii roho ya mpinga-kristo ilishaanza kutenda kazi tangu zamani, na shabaha yake si kwa kila mtu duniani bali ni kwa wale walio uzao wa Mungu tu.Iliwauwa wakristo wengi wakati wa zama za giza zaidi ya milioni 68, Na chombo chake teule anachotumia na atakachokuja kutumia kuyalaghai mataifa yote ulimwenguni ni dini na madhehebu huku akihubiri injili yake bandia yenye kivuli cha amani lakini nia yake sio kuleta amani bali kuangamiza uzao mteule wa Mungu. Hivyo ndugu ni wakati wa kujitathimini, je! Wewe ni mfuasi wa kweli wa Kristo au mfuasi wa dini au dhehebu?, je! Wewe ni mtakatifu au vuguvugu,.je! unahuakika wa kwenda mbinguni au unahisi tu?. Je! Wewe ni bibi-arusi wa kweli kama Esta au kama Vashti. Jibu lipo moyoni mwako. Kumbuka ndani ya kanisa yapo magugu na ngano, wapo wanawali wapumbavu na werevu..Je! wewe ni yupi kati ya hayo?.

Bwana wetu yuaja.

Mungu akubariki.

Monday, April 23, 2018

ESTA: Mlango wa 5, 6 & 7


Jina la mwokozi wetu YESU KRISTO litukuzwe.

Huu ni mwendelezo wa kitabu cha Esta. Katika sura hizi tatu (5,6 na 7), tunaona Malkia Esta akienda kijihudhurisha mbele ya mfalme kinyume cha taratibu ili awaombee watu wake dhidi ya adui wao Hamani aliyekusudia kuwaangamiza wayahudi wote waliokuwa dunia nzima. Lakini tunasoma badala ya Esta kuuliwa kinyume chake alipata kibali mbele ya mfalme kuwasilisha haja zake, na mfalme alipomuuliza Haja zake, Malkia Esta hakumweleza pale pale bali alimwalika kwanza kwenye karamu alizomwandalia, yeye na Hamani adui wa wayahudi. Tunasoma;

Esta 5: 2 “Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo.
3 Mfalme akamwambia, Malkia Esta, wataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme.
4 Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia.
5 Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyosema. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta.”

Hivyo Mfalme alipofurahishwa sana na sherehe aliyoandaliwa na Malkia Esta, alirudia tena kumuuliza ni nini anachohitaji kufanyiwa?..Lakini Esta hakumweleza mfalme chochote badala yake alimwandalia karamu nyingine nzuri zaidi na kumwalika mfalme pamoja na Hamani. Na Mfalme alipokula na kunywa na kufurahi ndipo akamuuliza kwa mara nyingine tena Esta ni nini haja ya moyo wake. Tunasoma;

Esta 7:2-10 "
2 Mfalme akamwambia Esta tena siku ya pili pale pale penye karamu ya divai, Malkia Esta, dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa.
3 Ndipo malkia Esta alipojibu, akasema, Mfalme, ikiwa nimepata kibali machoni pako, na mfalme akiona vema, nipewe maisha yangu kuwa dua yangu, na watu wangu kuwa haja yangu.
4 Maana tumeuzwa, mimi na watu wangu, ili tuharibiwe, na kuuawa, na kuangamia. Kama tungaliuzwa kuwa watumwa na wajakazi, ningalinyamaza; ila hata hivyo msiba wetu haulinganishwi na hasara ya mfalme.
5 Ndipo mfalme Ahasuero aliponena, akamwambia malkia Esta, Ni nani huyu, tena yuko wapi, ambaye moyoni mwake alithubutu kufanya hivi?
6 Esta akasema, Ni mtesi, tena ni adui, ndiye huyu Hamani, mtu mbaya kabisa. Mara Hamani akaingiwa na hofu mbele ya mfalme na malkia.
7 Mfalme akaondoka katika ghadhabu yake kutoka kwenye karamu ya divai, akaingia bustani ya ngome. Hamani naye akasimama ili ajitakie maisha yake kwa malkia Esta; kwa kuwa aliona ya kwamba amekusudiwa madhara na mfalme.
8 Kisha mfalme akarudi kutoka katika bustani ya ngome hata mahali pa karamu ya divai. Ikawa Hamani amejitupa chini penye kitanda alipokuwapo Esta. Mfalme akasema, Namna gani! Je! Atamfanyia malkia jeuri hata machoni pangu nyumbani mwangu? Na neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, wakamfunika uso Hamani.
9 Ndipo aliposema Harbona, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa wale waliohudhuria mbele ya mfalme, Tazama, basi, mti wa mikono hamsini urefu wake, Hamani aliomwekea tayari Mordekai, ambaye alinena vema kwa ajili ya mfalme, upo umesimamishwa nyumbani kwa Hamani. Mfalme akasema, Mtundikeni juu yake.
10 Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia. ''

Esta kama mfano wa Bibi-arusi wa Kristo, habari yake inatufundisha jinsi ya kumwendea Mfalme wetu (ambaye ni Bwana YESU) pale tunapokuwa na mahitaji yetu. Tunamwona Esta japokuwa alikuwa na uchungu mkubwa na shida kubwa ndani ya moyo wake, hakukimbilia moja kwa moja kuzungumza haja zake, japokuwa mfalme alifahamu kuwa ana mahitaji fulani. Lakini alitumia Hekima kwa kuufurahisha kwanza moyo wa mfalme, kwa kumuandalia karamu mbili, za thamani nzuri. Ndipo baadaye afunue yaliyokuwa ndani ya moyo wake.

Vivyo hivyo na sisi tunapomwendea Mungu ni vizuri kumfanyia kitu kwanza kinachompendeza moyo wake, kama Esta alivyomfanyia mfalme, swali ni je! katika wingi wa maombi unayompelekea Mungu kila siku je! ulishawahi kumfanyia kitu kinachompendeza kwanza?. Mfano kujitolea kwa ajili ya kazi yake?, au kumtolea Sadaka nzuri katika mali zako? au kuwasaidia wahitaji na maskini au mayatima?, au kuwavuta watu kwa Mungu? au kwenda kuwatazama wagonjwa?hususani wakristo wenzako? kumtolea shukrani kwa kumsifu na kumwabudu kwa bidii? n.k...kisha ndipo upeleke mahitaji yaako?. Kumbuka biblia inasema Mungu anafahamu haja zetu hata kabla hatujamwomba, kama tu vile mfalme alivyokuwa anajua kuwa Esta ana haja kabla hata hajamwomba. Hivyo tunapoenda mbele za Mungu tujifunze kuanza kumwandalia "karamu" impendezayo kwanza, na ndipo tuwasilishe mahitaji yetu. Kama alivyofanya Nuhu baada ya kumtolea Mungu sadaka nzuri Bwana akaibariki tena nchi na kuahidi hataiangamiza tena kwa maji.
 
Jambo lingine tunaona pia Esta hakujiombea ufahari bali alijiombea uhai wake pamoja na ndugu zake wayahudi. Ndipo akapewa alivyoviomba na zaidi ya alivyoviomba. Na sisi pia tunapomwendea Mungu ni vizuri kutanguliza kuwaombea watu wa Mungu na kanisa la Kristo kwa ujumla, kwasababu hao ndio ndugu zako wa daima, shetani akilidhuru kanisa, nawe pia ni lazima udhurike. Mungu anapendezwa na watu wanamwendea kwa namna hiyo, mfano Danieli alipomwendea Mungu kwa ajili ya makosa yake na watu wake Israeli tunaona Mungu alimsikia. Hivyo hivyo hata Bwana wetu Yesu aliomba siku zote kwa ajili yetu sisi na si kwa ajili yake peke yake, kadhalika na sisi tunapaswa tuchukue madhaifu ya wengine. Ili na sisi Bwana ayachukue madhaifu yetu.Wagalatia 6: 2 Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.

Biblia .inasema pia Kisasi ni juu ya Mungu yeye mwenyewe atalipa. Tunaona yule Hamani mti aliouchonga kumtundika Mordekai mtu aliyekuwa na haki ndio uliomtundikia yeye mwenyewe. Cheo alichokuwa anajisifia mbele ya Mordekai ndicho alichopewa Mordekai, Heshima aliyotafuta kutoka kwa Mordekai ndiyo yeye mwenyewe aliyokuja kumpa Mordekai pale alipoambiwa na Mfalme amchukue na kumzungusha mjini,pale alipotaka kumwangamiza Mordekai na watu wake, Mungu akageuza uteka yeye ndiye aliyeangamizwa pamoja na watu wake.

Mthali 26: 27 Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.
 
Kadhalika dhambi atendayo mtu itamrudia mwenyewe wewe unayestarehe katika maisha ya dhambi na anasa, huku unajidhania unanawiri kwa kuwa na afya, mali, cheo au umaarufu, hujui kuwa uharibifu wako utakuja kwa ghafla ndani ya siku moja kama Hamani, leo hii unakejeli injili, unasema wokovu ni kwa watu waliokosa uelekeo wa maisha, biblia ni hadithi zilizotungwa na watu, hakuna mtu kuokoka duniani n.k. Injili inahubiriwa kila mahali lakini unabakia kuwa vile vile kwasababu mafanikio yako yanakudanganya fahamu kuwa utaanguka kama Hamani kama usipotubia uovu wako. Neno la Mungu linasema.

kufanikiwa kwa mpumbavu kutamwangamiza, ziwa la moto lipo halishibi kupokea watu..

Tubu umgeukie Bwana ukabatizwe katika ubatizo sahihi kwa jina lake YESU KRISTO upate ondoleo la dhambi zako.
 
Ubarikiwe.

Thursday, April 19, 2018

ESTA: Mlango wa 4


BWANA wetu YESU KRISTO atukuzwe.

Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha Esta. Leo tukiwa katika sura ya 4, hivyo ni vizuri kama utapitia binafsi kwanza kusoma sura hii na zilizotangulia ili upate picha halisi iliyojificha katika kitabu hichi cha Esta kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Tunaona baada ya Hamani kutoa amri ya wayahudi wote kuuawa katika majimbo yote yaliyokuwa ulimwenguni, ambayo iliwafadhaisha sana wayahudi, na kumbuka hii ilikuwa ni sheria kwa umedi na Uajemi kwamba amri yoyote itakayopitishwa na mfalme isitanguke kwa namna yeyote ile, kama ilivyokuwa katika kipindi cha Danieli ilipotuolewa amri ya yeye kutupwa katika lile tundu la Simba, ilipaswa iwe hivyo hata mfalme mwenyewe alipotaka kujaribu kumwokoa Danieli haikuwezekana,
kwasababu ilikuwa ni sheria kwa Wamedi na Waajemi kwamba Amri yoyote itakayopitishwa na mfalme haiwezi kugeuzwa.

Hivyo kwa kuyafahamu hayo na Kwa tukio hilo Mordekai pamoja na Wayuhudi wote walilia sana na kuomboleza kama biblia inavyosema.

Esta 4: 1 “Basi Mordekai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia pamoja na majivu, akatoka hata kufika katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu.
2 Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme hali amevaa magunia.
3 Na katika kila jimbo, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, palikuwako msiba mkuu kwa Wayahudi, na kufunga, na kulia, na kuomboleza; hata na wengi wakalala juu ya gunia na majivu.”

Hivyo Mordekai akaona mlango pekee wanaoweza kuutumia kutafuta ukombozi wao ni kwa kupitia Malkia Esta, Ndipo akamweleza Esta mambo yote Hamani aliyoyapanga dhidi ya wayahudi wote, na kumsihi akamwombe mfalme ili aweze kugeuze shauri hilo. Lakini jibu la Esta lilikuwa ni tofauti alimwambia hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia katika Ua wa mfalme pasipo kuitwa, na kwamba yeyote atakaye kwenda kinyume na amri hiyo ilikuwa ni kifo.

Esta 4: 10 “Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema,
11 Watumwa wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu ye yote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini”.

Lakini tunasoma Mordekai alizidi kumsisitiza Esta na kumwambia: 14 “Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; WALAKINI NI NANI AJUAYE KAMA WEWE HUKUUJIA UFALME KWA AJILI YA WAKATI KAMA HUO?.

Na ndipo malkia Esta tunasoma akachukua hatua ya kwenda kumuona mfalme kinyume na sheria, lakini kabla ya kufanya hivyo aliwaamuru wayahudi wote wafunge siku tatu kwa ajili yake ili apate kibali cha kusikilizwa. Na tunasoma alipozimaliza zile siku na kwenda kwa mfalme, Mungu alimpa kibali mbele ya mfalme na badala ya kufa alipata kibali kikubwa zaidi kufikia hata kuahidiwa kupewa nusu ya ufalme wa mfalme kama angetaka.

Tunajifunza nini hapo? Esta anayesimama kama Bibi-Arusi wa Kristo, alidhubutu kuhatarisha hata maisha yake kwa ajili ya wokovu wa ndugu zake, hii inatufundisha na sisi wakristo kujitoa kwa ajili ya wokovu wa watu wengine pasipo kujali ni mambo mangapi tutakayoyapoteza kwa kufanya hivyo, Esta alikuwa tayari kupoteza maisha yake, Lakini Bwana Yesu anasema Mathayo 10: 39 “Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”. Mungu ni mwema japo Esta aliyahatarisha maisha yake lakini mwisho wa siku aliyapata kwasababu alifanya hivyo kwa ajili ya ndugu zake.

Kadhalika na sisi tunaojiita bibi-arusi katika nafasi za kiroho Mungu alizotuweka na katika mahali popote tulipo tunapaswa tuwe mashahidi waaminifu wa Kristo pasipo kujali madhara yatakayotukuta, tuwalete watu kwa Kristo ili watoke katika mitego ya mauti ya shetani. Shetani ni mfano wa Hamani amewakusudia mabaya watu wa Mungu, lakini ni nani aliyetayari kujitoa kwa ajili yao? Bila shaka ni wewe uliyepewa hii neema na Bwana ya kumjua yeye.

Mordekai alimwambia Esta “WALAKINI NI NANI AJUAYE KAMA WEWE HUKUUJIA UFALME KWA AJILI YA WAKATI KAMA HUU?”.Vivyo hivyo katika nafasi uliyopo wewe iwe ni katika kanisa, familia, jamii, ofisi, madaraka, uongozi n.k. popote pale , ni nani ajuaye kuwa Mungu kakuweka mahali hapo kwa wakati kama huo kwa ajili ya wokovu wa watu wake?.(nazungumza na wewe uliye mkristo)

Anza kufanya hivyo uone kama hautapa kibali mbele za Mungu, pale ambapo unaona kama ukijaribu kufanya hivyo utapoteza kazi yako, au heshima yako, fahamu tu pale unapomuheshimu Mungu, Mungu naye atakuheshimu na kukutokezea njia pale pasipokuwa na njia., anza leo kuwa shahidi wa Kristo, wahurumie watu wake kwa jinsi wanavyoangamia, naye atakukirimia.

Chochote Mungu alichokupa nacho uwezo kitumie kwa Bwana kwa ajili ya injili, iwe ni cheo, iwe ni mali, iwe ni ujuzi, iwe ni elimu, iwe ni umashuhuri, iwe ni ukubwa, iwe ni kipaji, iwe ni ujana, iwe ni muda, vitumie kwa BWANA maana ni nani ajuaye kuwa umepewa hayo kwa wakati kama huu ili watu wa Mungu waokolewe?.

Unaweza ukasema mahali nilipo hapastahili mkristo kuwepo hapo au hapastahili kufanyia kazi ya Mungu, lakini ni nani ajuaye Mungu kakuweka hapo kwa kusudi maalumu la kuwaokoa watu kwake?. Kumbuka hata Esta mahali alipokuwepo sio kwamba palikuwa ni sehemu nzuri sana inayompendeza Mungu, hapana Torati yao ilishakataza kwa myahudi yoyote kutoa binti yake na kuolewa na watu wa mataifa(watu wasio wayahudi), ni machukizo mbele za Mungu. Lakini ilipotokea kwa Esta ni nani ajuaye ilikuwa vile kwa ajili ya ukombozi wa watu wa Mungu baadaye?.

Hivyo ndugu popote ulipo fanya kitu kwa Mungu, naye atakupa kibali chema.

Ubarikiwe sana.

Usikose mwendelezo wa sura zinazofuata..

Wednesday, April 18, 2018

ESTA: Mlango wa 3

Jina la Bwana wetu YESU KRISTO aliye mkuu wa uzima wote litukuzwe.

Karibu katika kujifunza NENO la Mungu ili tukue toka utukufu hata utukufu mpaka tutakapofikia kile kilele cha kumjua sana huyu mwokozi wetu Yesu. Leo tukiendelea na ile sura ya 3 ni vizuri ukaipitia habari hii kwanza peke yako katika biblia ndipo tuende pamoja.

Kwa maelezo mafupi kitabu hichi kinaelezea unabii wa mambo yatakayokuja kutokea baadaye licha ya kwamba tunaisoma kama hadhithi iliyo nyepesi kuielewa lakini ndani yake imebeba maana kubwa zaidi ambayo kila mkristo ni vema akaifahamu kwa haya majira tunayoishi, kwa mfano laiti ile historia ya YONA ingeeleweka machoni pa watu wengi kwa wakati ule kwamba sio tu ilikuwa ni hadithi ya Yona kutokutii maagizo ya BWANA, bali pia ilikuwa inamwelezea Bwana wetu Yesu kufa na kufufuka kwake, kuwa atakuja kukaa siku tatu kaburini kama vile Yona alivyokaa siku tatu usiku na mchana katika tumbo la samaki. Unaona Hivyo hadithi hizi zote zinaelezea unabii wa mambo yanayokuja kutokea mbeleni na ndivyo ilivyo hata katika kitabu hichi cha Esta.

Katika sura ya 3 tunasoma habari ya HAMANI ambaye alikuja kupandishwa cheo na mfalme Ahasuero na kuwa juu ya maakida wote waliokuwa katika ufalme wake uliotawala dunia nzima, Alitukuzwa sana kiasi kwamba watu wote waliokuwa chini yake waliamiriwa wamsujudie, Lakini tunasoma haikuwa hivyo kwa watu wote, alionekana mtu mmoja myahudi aliyeitwa Mordekai alikataa kuanguka chini yake na kumpa heshima yake. Na habari ilipomfikia Hamani alikasirika sana, na alipomjaribu tena aone kama atamwangukia amsujudie kama wale wengine wanavyofanya, msimamo wa Mordekai ulikuwa ni ule ule hakudhubutu kumsujudia..Hivyo Hamani tunasoma alizidi kuchukia zaidi akaona si shani kumwangamiza Mordekai peke yake bali hata na watu wake wote (yaani WAYAHUDI).

Lakini swali la kujiuliza ni hili; kwanini Mordekai aliyahalifu maagizo ya mfalme juu ya kusujudiwa kwa Hamani angali tunamsoma Mordekai alikuwa ni mtu mkamilifu aliyemuheshimu mfalme na kumtii?. Kumbuka neno kusujudia linavyotumika hapo sio kumsujudia kama Mungu bali ni kuanguka na kumpa Heshima yake kama mkuu wa nchi, ni kama tu vile kwasasa mahali ambapo Raisi anapita watu wote mnapaswa kusimama ili kumpa heshima yake, ndivyo Mordekai alivyokuwa anafanya kwa mfalme na kwa wakuu wote waliokuwa juu yake..lakini haikuwa hivyo kwa Hamani yeye alienda kinyume na wengine, hakumsujudia.


Ni dhahiri kuwa kuna jambo Mordekai aliliona ndani ya HAMANI ambalo sio sawa na ndio maana hakumpa Heshima yake. Biblia haijaeleza moja kwa moja ni mambo mangapi aliyaona kwa yule mtu. Lakini tukichunguza biblia tunaweza tukapata dondoo za kwanini Mordekai asimuheshimu HAMANI kama wakuu wengine wa Uajemi.

Tukirejea nyuma kidogo katika ile ya sura ya pili mwishoni tunaona kulikuwa na watu wawili waliotaka kumfanyia hila mfalme Ahausero na kutaka kumuua. (Esta 2:21-23). Lakini Mordekai alipogundua ya kwamba madhara yamepangwa kinyume cha Mfalme alikwenda kumuarifu jambo hilo na wale watu wakauliwa. Hivyo tukichunguza tunaona kuwa katika ule utawala fitna nyingi zilikuwa zinapangwa dhidi ya mfalme na ufalme wake. Na Mordekai kwasasa tunaweza kusema alikuwa ni mtu wa USALAMA,

Hivyo alichunguza mambo yote waliyokuwa yanaendelea kwa siri pasipo hata wakuu wengine kujua. Hivyo kitendo cha kutokumpa heshima HAMANI ni kwasababu aliziona HILA zake mbaya tokea mbali. Pengine hata wale watu waliotaka kumuua mfalme walikuwa na mahusiano ya karibu na Hamani. Na Mordekai kwa kutokupenda UNAFKI alidhihirisha moja kwa moja kuwa huyu mtu hastahili heshima ya ukuu japokuwa amri imetoka kwa mfalme watu wote wamwangukie.

Lakini tunavyozidi kuendelea kusoma tunakuja kuona jinsi Hamani alivyoomba kibali cha Mfalme kuwateketeza hata watu wasiokuwa na hatia (WAYAHUDI). Aliwachukia mpaka akatenga siku rasmi kuwaangamiza wayahudi wote walioko duniani. Mpaka biblia inamtaja kama "Adui wa wayahudi". Na japokuwa ni mfalme mwenyewe aliyemnyanyua lakini alikuja kuwa adui hata wa mfalme kwa kujaribu kuwaangamiza ndugu wa mke wake (Malkia Esta). Lakini utawala wake wa hila haukudumu kwa muda mrefu tutakuja kuona mbeleni tunavyozidi kusoma..

Habari hii inatoa picha halisi ya mambo yatakayokuja kutokea katika siku za mwisho. Kumbuka moja ya siku hizi atanyanyuka MFALME ambaye Mungu atamruhusu atende kazi kwa kipindi kifupi.

Tukisoma Ufunuo 13:5-7 " 5 Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. AKAPEWA UWEZO wa kufanya kazi yake MIEZI AROBAINI NA MIWILI.
6 Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni.
7 Tena AKAPEWA KUFANYA VITA NA WATAKATIFU na kuwashinda, AKAPEWA UWEZO JUU YA KILA KABILA NA JAMAA NA LUGHA NA TAIFA. "

Hamani ni mfano wa mpinga-kristo atakayeanza kufanya kazi moja ya siku hizi. Yeye alipewa amri kutoka kwa mfalme ahausero naye huyu vivyo hivyo atapewa uwezo kutoka kwa Mungu mwenyewe kutawala dunia kama biblia inavyosema. Na kama vile watu wote wa dunia nzima walimsujudia Hamani isipokuwa Mordekai peke yake. Vivyo hivyo mpinga-kristo atasujudiwa na watu wote wa dunia nzima pale atakapoanza kutenda kazi yake isipokuwa kikundi cha watu wachache sana watakaomdhihirisha maovu yake (miongoni mwao watakuwepo wale mashahidi wawili wa ufunuo 11, pamoja na wale wayahudi 144,000 watakaotiwa muhuri na Mungu katika Ufunuo 7&14.) kumbuka wakati huo kanisa litakuwa limeshanyakuliwa.

Jambo lile lile lililotokea kwa Hamani la kumchukia Mordekai kisa tu hajapendezwa naye na kukusudia kumwangamiza yeye pamoja na watu wake wote (wayahudi), vivyo hivyo MPINGA-KRISTO naye atawaghadhibikia wale MASHAHIDI WAWILI pamoja na wale 144000 na kutaka kuwaua na sio wao tu..bali mpaka wayahudi wengine waliozagaa duniani kote na baadhi ya masalia ya wakristo waliokosa unyakuo. Wote hawa atatafuta kuwaua kwa bidii (Ufunuo 12).

Wale mashahidi wawili wa ufunuo 11 watamhubiri kuwa huyu mfalme anayejitukuza sasa kana kwamba yeye ni Mungu sio rafiki wa Mungu bali ni MPINGA-KRISTO aliyetabiriwa, na watu waache kumwabudu wamgeukia Mungu wa mbinguni, wakithibitisha hilo kwa zile Ishara na yale mapigo yaliyoandikwa kule. Hivyo mpinga-kristo (PAPA kwa wakati huo) ataghadhibika sana na kufanya vita nao. Na kwasababu atakuwa ana nguvu duniani kote, atatoa amri kuundwe ustaarabu mpya wa dunia (NEW WORLD ORDER). Kwa kisingizio cha kuleta amani duniani lakini nia yake sio hiyo bali ni kuwakamata na kuwauwa watu wote watakaenda kinyume na uongozi wake na hawa watakuwa si wengine zaidi ya wayahudi na masalia ya waliokosa unyakuo. kama vile HAMANI alivyofanya.

Kumbuka sio watu wote watajua kuwa ni kiongozi mbaya kama vile Hamani sio watu wote waliojua kuwa ni kiongozi mbaya wengi walijua amepewa heshima na mfalme mpaka mwishoni kabisa walipokuja kujua kumbe alikuwa ni adui wa mfalme pia.

Vivyo hivyo na huyu MPINGA-KRISTO hatajulikana na watu wote, wengi watamwona kama kateuliwa na Mungu kama tu kivuli cha huyu wa sasa watu wasivyoweza kuona ni roho gani iliyopo ndani yake. Biblia inasema watu ambao hawakuandikwa majina yao tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu ndio watakaomsujudia (Ufunuo 17:8). Pale atakapotaka kukaa katika Hekalu la Mungu na kutaka kuabudiwa kama Mungu (2Thesalonike 2).

Hivyo atakuja kwa kivuli cha AMANI, na kuunda chapa yake itakayomtambulisha kila mtu IMANI yake. Vitu kama Micro-chips,lDS, N.k vitatumika kutakuwa hakuna “kujiajiri wala kuajiriwa” bila kuwa na vitambulisho maalumu, hivi vitatumika kutambulisha Dini/ dhehebu lililosajiliwa na UMOJA WAKE ALIOUUNDA (Ekumene). Kumbuka usajili huu hautakwepeka mahali popote usipokuwepo kwenye kitambulisho cha taifa utakutana nao kwenye leseni ya biashara au kitambulisho cha kazi au leseni au ATM card ..Hivyo lile neno hakuna atakayeweza kuuza wala kununua litatimia kwa namna hiyo. Sasa kwa wale ambao watakataa kupokea utambulisho wake ndio watakaopitia DHIKI ambayo haijawahi kuwepo.

Unaona hii roho ya shetani inavyojirudia rudia..ilianzia kwenye utawala wa Babeli wakati wa akina shedraki, Meshaki na Abednego, walipolazimishwa kuabudu ile sanamu, ukaja katika huu utawala wa Uajemi na Umedi, Hamani anataka kuwateketeza tena wayahudi, Ilitokea pia katika utawala wa Uyunani Antiokia IV Epifane alipowauwa baadhi ya wayahudi na kuwaondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima. Na utawala wa mwisho ambao ni RUMI ndio uliopo sasa uliohusika kwa mauaji mengi ya wakristo waaminifu kwa Mungu zaidi ya milioni 68. Umetabiriwa utapata nguvu tena katika siku hizi za mwisho utahusika na mauaji makubwa ambayo biblia inasema haijawahi kutokea mfano wake.

Hivyo ndugu majira haya sio ya kuchezea kabisa Bwana yupo mlangoni kurudi, kulinyakuwa kanisa lake, na siku atakapolinyakua watakaojua ni bibi-arusi tu, lakini wengine haitajulikana kwao. Je! umejiwekaje tayari, Bwana akirudi leo utasema sijasikia?. Mtafute Muumba wako angali muda unao tubu weka mbali uasherati, ibada za sanamu, nguo zisizo na maadili, ulevi, usengenyaji n.k. ukabatizwe upate ondoleo la dhambi zako. Umwishie Mungu ili uwe na uhakika wa maisha yako ya milele.

Ubarikiwe sana.

Usikose mwendelezo wa sura zinazofuata wa kitabu cha Esta.