"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, April 19, 2018

ESTA: Mlango wa 4


BWANA wetu YESU KRISTO atukuzwe.

Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha Esta. Leo tukiwa katika sura ya 4, hivyo ni vizuri kama utapitia binafsi kwanza kusoma sura hii na zilizotangulia ili upate picha halisi iliyojificha katika kitabu hichi cha Esta kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Tunaona baada ya Hamani kutoa amri ya wayahudi wote kuuawa katika majimbo yote yaliyokuwa ulimwenguni, ambayo iliwafadhaisha sana wayahudi, na kumbuka hii ilikuwa ni sheria kwa umedi na Uajemi kwamba amri yoyote itakayopitishwa na mfalme isitanguke kwa namna yeyote ile, kama ilivyokuwa katika kipindi cha Danieli ilipotuolewa amri ya yeye kutupwa katika lile tundu la Simba, ilipaswa iwe hivyo hata mfalme mwenyewe alipotaka kujaribu kumwokoa Danieli haikuwezekana,
kwasababu ilikuwa ni sheria kwa Wamedi na Waajemi kwamba Amri yoyote itakayopitishwa na mfalme haiwezi kugeuzwa.

Hivyo kwa kuyafahamu hayo na Kwa tukio hilo Mordekai pamoja na Wayuhudi wote walilia sana na kuomboleza kama biblia inavyosema.

Esta 4: 1 “Basi Mordekai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia pamoja na majivu, akatoka hata kufika katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu.
2 Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme hali amevaa magunia.
3 Na katika kila jimbo, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, palikuwako msiba mkuu kwa Wayahudi, na kufunga, na kulia, na kuomboleza; hata na wengi wakalala juu ya gunia na majivu.”

Hivyo Mordekai akaona mlango pekee wanaoweza kuutumia kutafuta ukombozi wao ni kwa kupitia Malkia Esta, Ndipo akamweleza Esta mambo yote Hamani aliyoyapanga dhidi ya wayahudi wote, na kumsihi akamwombe mfalme ili aweze kugeuze shauri hilo. Lakini jibu la Esta lilikuwa ni tofauti alimwambia hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia katika Ua wa mfalme pasipo kuitwa, na kwamba yeyote atakaye kwenda kinyume na amri hiyo ilikuwa ni kifo.

Esta 4: 10 “Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema,
11 Watumwa wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu ye yote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini”.

Lakini tunasoma Mordekai alizidi kumsisitiza Esta na kumwambia: 14 “Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; WALAKINI NI NANI AJUAYE KAMA WEWE HUKUUJIA UFALME KWA AJILI YA WAKATI KAMA HUO?.

Na ndipo malkia Esta tunasoma akachukua hatua ya kwenda kumuona mfalme kinyume na sheria, lakini kabla ya kufanya hivyo aliwaamuru wayahudi wote wafunge siku tatu kwa ajili yake ili apate kibali cha kusikilizwa. Na tunasoma alipozimaliza zile siku na kwenda kwa mfalme, Mungu alimpa kibali mbele ya mfalme na badala ya kufa alipata kibali kikubwa zaidi kufikia hata kuahidiwa kupewa nusu ya ufalme wa mfalme kama angetaka.

Tunajifunza nini hapo? Esta anayesimama kama Bibi-Arusi wa Kristo, alidhubutu kuhatarisha hata maisha yake kwa ajili ya wokovu wa ndugu zake, hii inatufundisha na sisi wakristo kujitoa kwa ajili ya wokovu wa watu wengine pasipo kujali ni mambo mangapi tutakayoyapoteza kwa kufanya hivyo, Esta alikuwa tayari kupoteza maisha yake, Lakini Bwana Yesu anasema Mathayo 10: 39 “Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”. Mungu ni mwema japo Esta aliyahatarisha maisha yake lakini mwisho wa siku aliyapata kwasababu alifanya hivyo kwa ajili ya ndugu zake.

Kadhalika na sisi tunaojiita bibi-arusi katika nafasi za kiroho Mungu alizotuweka na katika mahali popote tulipo tunapaswa tuwe mashahidi waaminifu wa Kristo pasipo kujali madhara yatakayotukuta, tuwalete watu kwa Kristo ili watoke katika mitego ya mauti ya shetani. Shetani ni mfano wa Hamani amewakusudia mabaya watu wa Mungu, lakini ni nani aliyetayari kujitoa kwa ajili yao? Bila shaka ni wewe uliyepewa hii neema na Bwana ya kumjua yeye.

Mordekai alimwambia Esta “WALAKINI NI NANI AJUAYE KAMA WEWE HUKUUJIA UFALME KWA AJILI YA WAKATI KAMA HUU?”.Vivyo hivyo katika nafasi uliyopo wewe iwe ni katika kanisa, familia, jamii, ofisi, madaraka, uongozi n.k. popote pale , ni nani ajuaye kuwa Mungu kakuweka mahali hapo kwa wakati kama huo kwa ajili ya wokovu wa watu wake?.(nazungumza na wewe uliye mkristo)

Anza kufanya hivyo uone kama hautapa kibali mbele za Mungu, pale ambapo unaona kama ukijaribu kufanya hivyo utapoteza kazi yako, au heshima yako, fahamu tu pale unapomuheshimu Mungu, Mungu naye atakuheshimu na kukutokezea njia pale pasipokuwa na njia., anza leo kuwa shahidi wa Kristo, wahurumie watu wake kwa jinsi wanavyoangamia, naye atakukirimia.

Chochote Mungu alichokupa nacho uwezo kitumie kwa Bwana kwa ajili ya injili, iwe ni cheo, iwe ni mali, iwe ni ujuzi, iwe ni elimu, iwe ni umashuhuri, iwe ni ukubwa, iwe ni kipaji, iwe ni ujana, iwe ni muda, vitumie kwa BWANA maana ni nani ajuaye kuwa umepewa hayo kwa wakati kama huu ili watu wa Mungu waokolewe?.

Unaweza ukasema mahali nilipo hapastahili mkristo kuwepo hapo au hapastahili kufanyia kazi ya Mungu, lakini ni nani ajuaye Mungu kakuweka hapo kwa kusudi maalumu la kuwaokoa watu kwake?. Kumbuka hata Esta mahali alipokuwepo sio kwamba palikuwa ni sehemu nzuri sana inayompendeza Mungu, hapana Torati yao ilishakataza kwa myahudi yoyote kutoa binti yake na kuolewa na watu wa mataifa(watu wasio wayahudi), ni machukizo mbele za Mungu. Lakini ilipotokea kwa Esta ni nani ajuaye ilikuwa vile kwa ajili ya ukombozi wa watu wa Mungu baadaye?.

Hivyo ndugu popote ulipo fanya kitu kwa Mungu, naye atakupa kibali chema.

Ubarikiwe sana.

Usikose mwendelezo wa sura zinazofuata..

No comments:

Post a Comment