Karibu katika kujifunza NENO la Mungu ili tukue toka utukufu hata utukufu mpaka tutakapofikia kile kilele cha kumjua sana huyu mwokozi wetu Yesu. Leo tukiendelea na ile sura ya 3 ni vizuri ukaipitia habari hii kwanza peke yako katika biblia ndipo tuende pamoja.
Kwa maelezo mafupi kitabu hichi kinaelezea unabii wa mambo yatakayokuja kutokea baadaye licha ya kwamba tunaisoma kama hadhithi iliyo nyepesi kuielewa lakini ndani yake imebeba maana kubwa zaidi ambayo kila mkristo ni vema akaifahamu kwa haya majira tunayoishi, kwa mfano laiti ile historia ya YONA ingeeleweka machoni pa watu wengi kwa wakati ule kwamba sio tu ilikuwa ni hadithi ya Yona kutokutii maagizo ya BWANA, bali pia ilikuwa inamwelezea Bwana wetu Yesu kufa na kufufuka kwake, kuwa atakuja kukaa siku tatu kaburini kama vile Yona alivyokaa siku tatu usiku na mchana katika tumbo la samaki. Unaona Hivyo hadithi hizi zote zinaelezea unabii wa mambo yanayokuja kutokea mbeleni na ndivyo ilivyo hata katika kitabu hichi cha Esta.
Katika sura ya 3 tunasoma habari ya HAMANI ambaye alikuja kupandishwa cheo na mfalme Ahasuero na kuwa juu ya maakida wote waliokuwa katika ufalme wake uliotawala dunia nzima, Alitukuzwa sana kiasi kwamba watu wote waliokuwa chini yake waliamiriwa wamsujudie, Lakini tunasoma haikuwa hivyo kwa watu wote, alionekana mtu mmoja myahudi aliyeitwa Mordekai alikataa kuanguka chini yake na kumpa heshima yake. Na habari ilipomfikia Hamani alikasirika sana, na alipomjaribu tena aone kama atamwangukia amsujudie kama wale wengine wanavyofanya, msimamo wa Mordekai ulikuwa ni ule ule hakudhubutu kumsujudia..Hivyo Hamani tunasoma alizidi kuchukia zaidi akaona si shani kumwangamiza Mordekai peke yake bali hata na watu wake wote (yaani WAYAHUDI).
Lakini swali la kujiuliza ni hili; kwanini Mordekai aliyahalifu maagizo ya mfalme juu ya kusujudiwa kwa Hamani angali tunamsoma Mordekai alikuwa ni mtu mkamilifu aliyemuheshimu mfalme na kumtii?. Kumbuka neno kusujudia linavyotumika hapo sio kumsujudia kama Mungu bali ni kuanguka na kumpa Heshima yake kama mkuu wa nchi, ni kama tu vile kwasasa mahali ambapo Raisi anapita watu wote mnapaswa kusimama ili kumpa heshima yake, ndivyo Mordekai alivyokuwa anafanya kwa mfalme na kwa wakuu wote waliokuwa juu yake..lakini haikuwa hivyo kwa Hamani yeye alienda kinyume na wengine, hakumsujudia.
Ni dhahiri kuwa kuna jambo Mordekai aliliona ndani ya HAMANI ambalo sio sawa na ndio maana hakumpa Heshima yake. Biblia haijaeleza moja kwa moja ni mambo mangapi aliyaona kwa yule mtu. Lakini tukichunguza biblia tunaweza tukapata dondoo za kwanini Mordekai asimuheshimu HAMANI kama wakuu wengine wa Uajemi.
Tukirejea nyuma kidogo katika ile ya sura ya pili mwishoni tunaona kulikuwa na watu wawili waliotaka kumfanyia hila mfalme Ahausero na kutaka kumuua. (Esta 2:21-23). Lakini Mordekai alipogundua ya kwamba madhara yamepangwa kinyume cha Mfalme alikwenda kumuarifu jambo hilo na wale watu wakauliwa. Hivyo tukichunguza tunaona kuwa katika ule utawala fitna nyingi zilikuwa zinapangwa dhidi ya mfalme na ufalme wake. Na Mordekai kwasasa tunaweza kusema alikuwa ni mtu wa USALAMA,
Hivyo alichunguza mambo yote waliyokuwa yanaendelea kwa siri pasipo hata wakuu wengine kujua. Hivyo kitendo cha kutokumpa heshima HAMANI ni kwasababu aliziona HILA zake mbaya tokea mbali. Pengine hata wale watu waliotaka kumuua mfalme walikuwa na mahusiano ya karibu na Hamani. Na Mordekai kwa kutokupenda UNAFKI alidhihirisha moja kwa moja kuwa huyu mtu hastahili heshima ya ukuu japokuwa amri imetoka kwa mfalme watu wote wamwangukie.
Lakini tunavyozidi kuendelea kusoma tunakuja kuona jinsi Hamani alivyoomba kibali cha Mfalme kuwateketeza hata watu wasiokuwa na hatia (WAYAHUDI). Aliwachukia mpaka akatenga siku rasmi kuwaangamiza wayahudi wote walioko duniani. Mpaka biblia inamtaja kama "Adui wa wayahudi". Na japokuwa ni mfalme mwenyewe aliyemnyanyua lakini alikuja kuwa adui hata wa mfalme kwa kujaribu kuwaangamiza ndugu wa mke wake (Malkia Esta). Lakini utawala wake wa hila haukudumu kwa muda mrefu tutakuja kuona mbeleni tunavyozidi kusoma..
Habari hii inatoa picha halisi ya mambo yatakayokuja kutokea katika siku za mwisho. Kumbuka moja ya siku hizi atanyanyuka MFALME ambaye Mungu atamruhusu atende kazi kwa kipindi kifupi.
Tukisoma Ufunuo 13:5-7 " 5 Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. AKAPEWA UWEZO wa kufanya kazi yake MIEZI AROBAINI NA MIWILI.6 Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni.7 Tena AKAPEWA KUFANYA VITA NA WATAKATIFU na kuwashinda, AKAPEWA UWEZO JUU YA KILA KABILA NA JAMAA NA LUGHA NA TAIFA. "
Hamani ni mfano wa mpinga-kristo atakayeanza kufanya kazi moja ya siku hizi. Yeye alipewa amri kutoka kwa mfalme ahausero naye huyu vivyo hivyo atapewa uwezo kutoka kwa Mungu mwenyewe kutawala dunia kama biblia inavyosema. Na kama vile watu wote wa dunia nzima walimsujudia Hamani isipokuwa Mordekai peke yake. Vivyo hivyo mpinga-kristo atasujudiwa na watu wote wa dunia nzima pale atakapoanza kutenda kazi yake isipokuwa kikundi cha watu wachache sana watakaomdhihirisha maovu yake (miongoni mwao watakuwepo wale mashahidi wawili wa ufunuo 11, pamoja na wale wayahudi 144,000 watakaotiwa muhuri na Mungu katika Ufunuo 7&14.) kumbuka wakati huo kanisa litakuwa limeshanyakuliwa.
Jambo lile lile lililotokea kwa Hamani la kumchukia Mordekai kisa tu hajapendezwa naye na kukusudia kumwangamiza yeye pamoja na watu wake wote (wayahudi), vivyo hivyo MPINGA-KRISTO naye atawaghadhibikia wale MASHAHIDI WAWILI pamoja na wale 144000 na kutaka kuwaua na sio wao tu..bali mpaka wayahudi wengine waliozagaa duniani kote na baadhi ya masalia ya wakristo waliokosa unyakuo. Wote hawa atatafuta kuwaua kwa bidii (Ufunuo 12).
Wale mashahidi wawili wa ufunuo 11 watamhubiri kuwa huyu mfalme anayejitukuza sasa kana kwamba yeye ni Mungu sio rafiki wa Mungu bali ni MPINGA-KRISTO aliyetabiriwa, na watu waache kumwabudu wamgeukia Mungu wa mbinguni, wakithibitisha hilo kwa zile Ishara na yale mapigo yaliyoandikwa kule. Hivyo mpinga-kristo (PAPA kwa wakati huo) ataghadhibika sana na kufanya vita nao. Na kwasababu atakuwa ana nguvu duniani kote, atatoa amri kuundwe ustaarabu mpya wa dunia (NEW WORLD ORDER). Kwa kisingizio cha kuleta amani duniani lakini nia yake sio hiyo bali ni kuwakamata na kuwauwa watu wote watakaenda kinyume na uongozi wake na hawa watakuwa si wengine zaidi ya wayahudi na masalia ya waliokosa unyakuo. kama vile HAMANI alivyofanya.
Kumbuka sio watu wote watajua kuwa ni kiongozi mbaya kama vile Hamani sio watu wote waliojua kuwa ni kiongozi mbaya wengi walijua amepewa heshima na mfalme mpaka mwishoni kabisa walipokuja kujua kumbe alikuwa ni adui wa mfalme pia.
Vivyo hivyo na huyu MPINGA-KRISTO hatajulikana na watu wote, wengi watamwona kama kateuliwa na Mungu kama tu kivuli cha huyu wa sasa watu wasivyoweza kuona ni roho gani iliyopo ndani yake. Biblia inasema watu ambao hawakuandikwa majina yao tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu ndio watakaomsujudia (Ufunuo 17:8). Pale atakapotaka kukaa katika Hekalu la Mungu na kutaka kuabudiwa kama Mungu (2Thesalonike 2).
Hivyo atakuja kwa kivuli cha AMANI, na kuunda chapa yake itakayomtambulisha kila mtu IMANI yake. Vitu kama Micro-chips,lDS, N.k vitatumika kutakuwa hakuna “kujiajiri wala kuajiriwa” bila kuwa na vitambulisho maalumu, hivi vitatumika kutambulisha Dini/ dhehebu lililosajiliwa na UMOJA WAKE ALIOUUNDA (Ekumene). Kumbuka usajili huu hautakwepeka mahali popote usipokuwepo kwenye kitambulisho cha taifa utakutana nao kwenye leseni ya biashara au kitambulisho cha kazi au leseni au ATM card ..Hivyo lile neno hakuna atakayeweza kuuza wala kununua litatimia kwa namna hiyo. Sasa kwa wale ambao watakataa kupokea utambulisho wake ndio watakaopitia DHIKI ambayo haijawahi kuwepo.
Unaona hii roho ya shetani inavyojirudia rudia..ilianzia kwenye utawala wa Babeli wakati wa akina shedraki, Meshaki na Abednego, walipolazimishwa kuabudu ile sanamu, ukaja katika huu utawala wa Uajemi na Umedi, Hamani anataka kuwateketeza tena wayahudi, Ilitokea pia katika utawala wa Uyunani Antiokia IV Epifane alipowauwa baadhi ya wayahudi na kuwaondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima. Na utawala wa mwisho ambao ni RUMI ndio uliopo sasa uliohusika kwa mauaji mengi ya wakristo waaminifu kwa Mungu zaidi ya milioni 68. Umetabiriwa utapata nguvu tena katika siku hizi za mwisho utahusika na mauaji makubwa ambayo biblia inasema haijawahi kutokea mfano wake.
Hivyo ndugu majira haya sio ya kuchezea kabisa Bwana yupo mlangoni kurudi, kulinyakuwa kanisa lake, na siku atakapolinyakua watakaojua ni bibi-arusi tu, lakini wengine haitajulikana kwao. Je! umejiwekaje tayari, Bwana akirudi leo utasema sijasikia?. Mtafute Muumba wako angali muda unao tubu weka mbali uasherati, ibada za sanamu, nguo zisizo na maadili, ulevi, usengenyaji n.k. ukabatizwe upate ondoleo la dhambi zako. Umwishie Mungu ili uwe na uhakika wa maisha yako ya milele.
Ubarikiwe sana.
Usikose mwendelezo wa sura zinazofuata wa kitabu cha Esta.
No comments:
Post a Comment