"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, May 31, 2018

KITABU CHA UFUNUO: Mlango wa 2.

(Sehemu ya 1)
Jina kuu la BWANA wetu YESU KRISTO litukuzwe milele yote. Karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo, Leo tutaitazama ile sura ya pili. Kama tulivyotangulia kusoma katika ile sura ya kwanza, Tuliona Yohana akionyeshwa Sura na umbo la YESU KRISTO , na wasifa wake ambao alionyeshwa kwa lugha ya picha,(Kumbuka Bwana Yesu kiuhalisia hana muonekano kama ule), jinsi alivyokuwa anaonekana na nywele nyeupe kama sufu, macho ya moto, miguu ya shaba, upanga unaotoka kinywani mwake, mwenye sauti kama maji mengi, aendaye katikati ya vile vinara 7 n.k. hizo zote zilisimama kama viashiria (Nembo) vya tabia yake, ambayo kila moja ina nafasi yake katika hichi kitabu cha Ufunuo na ndio maana zilitangulizwa kuelezwa mwanzoni kabisa mwa kitabu hichi.

Hivyo katika sura ile ya kwanza mwishoni tuliona jinsi Yohana anaambiwa ayaandike yale aliyoyaona na ayapeleke kwa yale makanisa saba. Ufunuo 1: 19 Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.
20 Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba."

Ni muhimu kufahamu Barua hizi Yohana alizopewa hazikuyahusu tu yale makanisa 7 yaliyokuwa Asia ndogo kwa wakati ule, bali pia na kwa makanisa yatakayokuja huko mbeleni na ndio maana hapa anaambiwa ayaandike mambo hayo YALIYOPO na YATAKAYOKUJA baada ya hayo. Ikiwa na maana kuwa yale yaliyoko ndio yale makanisa 7 yaliyokuwa Asia katika wakati wa Yohana, na yale yatakayokuja ni Makanisa 7 tuliopo sisi baada ya Yohana kuondoka. Kwahiyo Tunaposoma leo hii kitabu cha ufunuo tunajua kuwa yale makanisa 7 yaliyokuwa katika kipindi cha Yohana yameshapita. Na tangu kipindi cha Bwana YESU kuondoka hadi sasa ni takribani miaka 2,000 na kanisa la Kristo limekuwa likipita katika vipindi tofauti tofauti saba ndani ya huo muda wa miaka 2000, vijulikanavyo kama NYAKATI SABA ZA KANISA.

Sasa tukirudi katika sura ya pili. Tunaona Bwana Yesu akianza kutoa ujumbe kwa kanisa moja baada ya lingine, Kuanzia kanisa la Efeso mpaka Laodikia ambalo ndio la mwisho. Tunasoma;

KANISA LA EFESO:
Ufunuo 2:1 "Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu".

Awali ya yote tunaona Bwana Yesu anajitambulisha hapa kama "yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu na aliyeshika zile nyota saba". Kumbuka hapa hajajitambulisha yeye kama yeye mwenye macho ya moto au uso ung'aao kama jua. Lakini alisema yeye aendaye katikati ya vile vinara saba ikiwa na maana kuwa uelekeo wake wote utakuwa katika kuchunguza kinara cha hilo kanisa na yale makanisa mengine. Kumbuka kinara ni taa iliyokuwa inawekwa katika nyumba ya Mungu (Hekaluni) Kwa ajili ya kutia Nuru kule ndani (Patakatifu) ili shughuli za kikuhani ziende sawasawa (Kutoka 27:20), na kilikuwa hakizimwi muda wote, sharti ni lazima kimulike daima usiku na mchana pasipo kuzimwa. Vivyo hivyo hapa Bwana alipoanza kwa kujitambulisha hivyo alikuwa anatazamia nuru isiyozimika ndani ya hilo kanisa husika (nyumba yake) ambalo analitolea habari zake hapo chini.
(katika nyumba ya Bwana kinara cha taa kilikuwa na mirija/matawi saba, na kilikuwa kinatia nuru nyumba ya Mungu daima)
  

Na NURU hii ni ipi Bwana aliyokuwa aliitazamia kuiona inaangaza?. Biblia inatuambia

1Yohana 2: 8 Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu; kwa kuwa giza linapita na ile nuru ya kweli imekwisha kung'aa.
9 Yeye asemaye kwamba yumo NURUNI, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.
10 Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.
11 Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.

Na pia tukisoma 1Wakorintho 13 inasema Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote, Upendo haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli n;k. Hivyo kwa ujumla NURU ni UPENDO. Ambao huo unaanza kwanza kwa KUMPENDA BWANA MUNGU WAKO kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote,na kwa nguvu zako zote, (Kwa kuzishika na kuzifuata amri zake) na pia kumpenda jirani yako kama nafsi yako. Kwa kuzingatia hayo mawili KINARA CHAKO kitakuwa kinatoa Nuru ya kutosha.

Sasa tukirudi katika Kanisa lile la EFESO, tunaona Bwana aliendelea kulitolea habari zake na kusema:

Ufunuo 2:2-5 "Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo;
3 tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka.
4 Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.
5 Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.
6 Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia."
Kwanza kabisa maana ya neno EFESO ni "Kuacha mema yaondoke". Hivyo hili kanisa kama jina lake lilivyo mwanzoni lilianza kuenenda katika Nuru ya Neno ambao ni UPENDO wa kiungu, lilikuwa japokuwa linapitia majaribu mengi liliendelea kumpenda Mungu, lilivumilia mabaya,Hii tunaona katika utawala wa Rumi chini ya kiongozi mkatili Nero, aliyewaua wakristo wengi wakati ule kwa kuwasingizia kuwa wameuchoma mji na hali sio wao. Kanisa hili pia mwanzoni lilijiweka katika utakatifu wa hali ya juu, liliwapima manabii wa uongo na kugundua kuwa sio, kwa muda mrefu sana. Walikuwa na uwezo pia wa kuyagundua matendo ya WANIKOLAI na kuyapinga katikati ya Kanisa. Kumbuka neno "Nikolai" tafsiri yake ni "Kuteka madhabahu" Hivyo kulikuwa na tabia zilizokuwa zimeanza kujitokeza katikati ya baadhi ya makanisa, watu(wasio wa Mungu) walianza kijipachikia vyeo vilivyoua uongozi wa Roho Mtakatifu. kwamfano watu badala ya kwenda kumuomba Mungu msamaha, walianza kuwafuata wanadamu wenzao wawaombee au wawaondolee dhambi zao kwa niaba ya Mungu, Badala karama za roho ziongoze kanisa, vyeo vya kibinadamu vikaanza kuongoza kanisa n.k. Huku ndiko kuteka madhabahu na hayo ndiyo yaliyokuwa matendo ya Wanikolai, ambayo kanisa la Kristo la kweli lilichukizwa nayo na Bwana vilevile.

Lakini Kanisa hili la Efeso lilifikia kipindi ule upendo waliokuwa nao hapo kwanza ukaanza kupoa (wakaanza kuacha mema yaondoke katikati yao kama vile Jina la kanisa lao lilivyo), uvumilifu kwa ajili Imani, utakatifu na subira vikaanza kupoa, zamani walikuwa wanawajaribu manabii wa uongo na kuwaondoa katikati yao lakini sasa hawafanyi hivyo tena.. Na ndio maana Bwana hapa anatokea na kuanza kukichunguza kinara chao na kuwaambia NURU yao imeanza kufifia na kukaribia kuzima Ukiendelea kusoma utaona Bwana anawaambia watubu " 5 Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye MATENDO YA KWANZA. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu."

Kama tulivyoona Pale mwanzoni katika ile sura ya kwanza juu ya ule mwonekano wake, jinsi alivyoonekana akipita katikati ya vile vinara vya taa, ikiwa na maana kuwa anapeleleza na kufanya masahihisho, kinara kilichofifia na kukaribia kuzima anakiondoa na kile kinachozidi kuwaka anakiongezea nuru, kwasababu biblia inasema "mwenye nacho ataongezewa asiye nacho hata kile kidogo alicho nacho atanyang'anywa" Hivyo kama wasingeimarisha matendo yao, hata ile nuru waliyokuwa nayo kidogo ingeondolewa kwao. Na ile taabu yao ya mwanzo waliyoisumbukia ingekuwa ni sawa na bure.

Sasa kanisa hili la Efeso lenye tabia hizi lilianza kati ya kipindi cha 53WK hadi mwaka 170WK. Na Malaika wa kanisa hilo alikuwa ni Mtume Paulo. Kumbuka Neno "malaika" tafsiri yake ni "mjumbe"  hivyo wapo wajumbe wa kimbinguni(ndio malaika wa rohoni) na wapo wajumbe wa duniani. Hawa wanaotajwa katikati ya haya makanisa saba ni wajumbe wa kiduniani (yaani wanadamu). Kwahiyo malaika wa Kanisa hili la Efeso alikuwa ni Mtume Paulo. Kwasababu yeye ndiye mtume aliyepewa neema ya kupeleka Injili kwa mataifa. Na mafunuo mengi aliyopewa yalikuwa ni msingi katika makanisa ya wakati ule, na hata sasa.

Kadhalika na sisi tuliopo katika Kanisa la mwisho (Laodikia) ambalo tutakuja kusoma habari zake hapo baadaye na sisi pia tunaonywa tusipotubu kinara chetu kitaondolewa.. Kumbuka BWANA pale anaonekana akipita katikati ya vile vinara 7 na sio "Kinara kimoja". Hivyo anavichunguza vyote kuanzia cha kwanza mpaka cha mwisho. Na kama asipoiona ile nuru aliyoikusudia iwepo katika kinara chetu vile vile kitaondolewa.. Na tunafahamu madhara ya Nuru kuondolewa, anamaanisha giza linaachiliwa liingie ndani yako.

Ndugu Mwanzoni ulipoanza kuamini ulikuwa mtakatifu lakini sasa hivi utakatifu wako umepoa, ulikuwa unasali, ulikuwa unavaa vizuri, ulikuwa na huruma kwa ndugu, ulikuwa na upendo, ulikuwa na uvumilivu juu ya imani yako hata kama watu wanaokuzunguka wanakudhihaki, ulikuwa huwezi kuabudu sanamu au kuchukuliana na mafundisho ya uongo lakini sasahivi unayapokea mafundisho ya uongo na kuyafurahia, Injili zisizokufanya utazama ufalme wa mbingu ndio unazozipenda, huwezi tena kusali, kujisitiri huwezi tena, hukutazamii tena kuja kwa Bwana umechoka na kuishiwa nguvu. Hizo ni dalili za Kinara chako kuzima..Jitahidi kabla hakijaondolewa. Maana siku kitakapoondolewa ndugu hali yako ya mwisho itakuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Ule upendo uliokuwa nao kwanza wa Mungu unaondoka kabisa ndani yako, unafanana tena na watu wasiomjua Mungu, au unakua kama vile mtu ambaye hajawahi kumjua Mungu kabisa.

Hivyo tujitahidi na sisi TAA zetu ziwe zinawaka katika hizi siku za kumalizia kwasababu Bwana hivi karibuni anarudi.. yeye mwenyewe alisema; katika Luka 12: 35 Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA; 36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara."

Ubarikiwe sana.

Usikose sehemu ya pili ya sura hii ya pili ya kitabu cha Ufunuo,.ambapo tutakuja kuona ujumbe wa kanisa la pili (SMIRNA).

Tafadhali "Share" kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki.

Wednesday, May 30, 2018

MASWALI NA MAJIBU:SEHEMU YA 27

SWALI: Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?
JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu kwamba ziwa la moto  wameandaliwa shetani na malaika zake,(wale walioasi pamoja naye), kutokana na makosa waliyoyafanya huko nyuma kabla ya mwanadamu kuumbwa, ambapo shetani pamoja na kuonywa  na Mungu abaki katika kweli lakini hakutaka, akaandaliwa adhabu hiyo,Na vivyo hivyo wanadamu ambao hawataki kukaa katika ile kweli, wao pia watatupwa katika lile ziwa la moto.

lakini pia ni muhimu kufahamu kuwa Mungu hamchomi shetani au mwanadamu kwenye ziwa la moto kama kuwakomoa au kuwakomesha au kuwalipizia kisasi, hapana! bali Bwana anafanya vile ili kuondoa uovu karibu naye kwasababu yeye ni mtakatifu, ili kuelewa zaidi tafakari mfano ufuatao,

Wewe ni msafi hupendi uchafu halafu inatokea kuna uchafu umejitengeneza pembeni yako au karibu na makazi yako, uchafu huo unakuletea harufu mbaya, na kichefuchefu, na kukufanya ujisikie vibaya sana, dawa pekee ya kuutoa uchafu huo ni lazima itakuwa ni kuukusanya pamoja na kwenda kuuchoma moto? swali ni je! umeuchoma uchafu huo kwasababu unakisasi nao? au kwasababu unataka kuukomoa? jibu ni hapana!! unauchoma uchafu kwasababu umekaa mahali pasipo upasa na wewe huwezi kuchangamana na uchafu, kwahiyo itabidi utengeneze tanuru ili kuuondoa uchafu huo, na kama unavyojua takataka iliyo ngumu zaidi itachelewa kuteketea kuliko takataka illiyo laini, karatasi litawahi kuteketea kuliko mpira,

Kadhalika na Mungu pia, yeye ni mtakatifu na hachangamani na uchafu, biblia inasema tutakuwa watakatifu kwasababu yeye Mungu ni mtakatifu (1 Petro 15: 15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
16 kwa maana imeandikwa, MTAKUWA WATAKATIFU KWA KUWA MIMI NI MTAKATIFU.
17 Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. )

Unaona hapo sababu pekee ya Mungu kuuteketeza Roho zote zilizoasi katika ziwa la moto ni kwasababu yeye ni MTAKATIFU na hawezi kuchangamana na uchafu, hawezi kukaa mahali pamoja na uchafu, watu waovu hawawezi kurithi ahadi za Mungu, hawawezi kuketi pamoja naye, na kama unavyojua takataka ngumu ndiyo inayochelewa kuteketea zaidi kuliko ile laini kadhalika nafsi iliyojichafua sana na mambo maovu ndiyo itakayoadhibiwa sana kuliko ile iliyojichafua kidogo.

Luka 12: 47 "Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.
48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi". Hivyo adhabu ya shetani haiwezi kuwa sawa na ya mwanadamu, yeye atapigwa zaidi, na adhabu ya aliyeua watu 100 haiwezi kuwa sawa na aliyeua watu 10 n.k

Lakini mwisho wa yote roho zote zilizoasi(shetani na wanadamu walioasi) zitakufa katika lile ziwa la moto, kwasababu hazina uzima wa milele, hiyo ndiyo mauti ya pili biblia inayoitaja katika (ufunuo 2:11,ufunuo 20:14).

SWALI : Kwa nini Mungu hakumuua shetani.?

JIBU: Tunaweza tukajiuliza pia, kama Mungu anafahamu mambo yote na anajua pia yatakayokuja kutokea mbeleni ni kwanini basi arusuhusu mabaya yatokee mpaka kufikia kiwango cha roho ya mtu kupotea kwenda kuzimu?..Lakini biblia inatuambia (..AKILI ZAKE HAZICHUNGUZI Isaya 40:28)..Ni kweli tutajua mambo mengi kumuhusu Mungu na uweza wake wa kiungu, na mamlaka yake, na nguvu zake, lakini hatuwezi kabisa moja kwa moja kufahamu mipango yake aliyojiweka ndani ya uumbaji wake.

Sisi tunazo taratibu zetu, Mungu naye anazotaratibu zake. Anavyofikiri yeye ni mbali sana na tunavyofikiri sisi, biblia inasema kama mbingu zilivyo mbali sana, unaweza ukajiuliza mbingu ukitazama hauoni mwisho, kadhalika na mipango yake ilivyo mbali sana na mipango yetu. Isaya 55: 8 Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.
9 Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

Lakini sisi tuliookolewa tunafahamu jambo moja ambalo katika Ahadi zake alituambia ; Yeremia 29:11 "Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.". Hivyo lolote linalotokea tunaliona tunajua kabisa kuna wakati utafika tutagundua kuwa Mpango wa Mungu juu ya kumwacha shetani aendelee kuuharibu ulimwengu ulikuwa na busara mara milioni moja zaidi kama angemuondoa mapema. Na kwamba tutapewaje tuzo iliyo bora kama hatujashindana? Tiara itapaaje juu sana kama hakutakuwa na upepo wa kuikabili? tutashindaje kama hakuna vita? unaona? ipo sababu kwa kila kusudi. Na ndio maana hata sasa tunasema NJIA ZAKE NI KAMILIFU siku zote kama biblia inavyosema katika (Zaburi 18:30).

Lakini kumbuka pia shetani kuendelea kuishi mpaka sasa, sio kwamba bado hajahukumiwa bado hapana! Yeye alishahukumiwa tangu zamani, isipokuwa adhabu ya mauti ndio haijaja bado ambayo kwasasa ndio inakaribia kumfikia kwasababu siku alizobakiza kuendelea kufanya maovu zimebaki chache sana Ufunuo 12: 12 Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, AKIJUA YA KUWA ANA WAKATI MCHACHE TU. "

SWALI: Mtumishi. Ninaswali Hapa Kwenye UFUNUO 20:7 "Na Hiyo Miaka Elfu Itakapokwisha, Shetani Atafunguliwa, Atoke Kifungoni Mwake", Je, Hiyo Miaka Elfu Imeshapita Au Bado Au Ndo Wakati Huu Wa Sasa?
JIBU: Utawala wa miaka 1000 bado haujaanza, utakuja kuanza baada ya dhiki kuu kuisha, na baada ya ile SIKU KUU YA BWANA kupita, Pale Bwana atakapokuja na watakatifu wake kutoka mbinguni ambapo kila jicho litamwona. Katika siku hiyo ndio Bwana atakapokuja kuyahukumu mataifa na kuleta utawala mpya wa amani wa miaka 1000 (soma ufunuo 19 na 20 yote utaona jambo hilo), kwahiyo shetani sasa hivi hajafungwa, yupo? anatenda kazi kwa kasi sana, akijua kwamba muda wake ni mchache..huoni maasi yanavyozidi kuongezeka, mauaji, vita, anasa, ananyanyua manabii wa uongo wengi, analeta magonjwa mengi n.k huo ni uthibitisho tosha kwamba yupo na anafanya kazi kwa viwango vingine, na anapenda watu wajue kwamba yeye kafungwa ili wadanganyike siku ile iwajie ghafla. .

Ubarikiwe sana.

Ukiwa na swali lolote lihusulo biblia ..tutumie  (kwa e-mail/whatsapp/namba za simu )na kwa neema za Bwana litajibiwa.

Tuesday, May 29, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 26

 SWALI:Barikiwa sana swali langu je mwanadamu wa kwanza kuumbwa.ni yupi mzungu mwafrika au mchina na kama ni mmojawapo kati ya hao je hao wengine wametoka wapi ? By lucas
JIBU: Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu aliiumba jamii moja tu ya watu..Hakuumba jamii nyingi za watu pale Edeni na hii jamii tunaipata kutoka kwa Adamu na Hawa (Mwanzo 1: 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba ). Watu Hawa wawili ndio Mungu aliowaumba kwa ukamilifu wote bila kasoro kubwa wala ndogo,sasa Adamu na mke wake hawakuwa wazungu hapo mwanzo, kama wengi wanavyodhani, au waafrika au wachina au wahindi au jamii nyingine yeyote ya watu tunayoiona leo. la! Adamu na Hawa walikuwa ni watu wenye upekee wao ambao leo hii hatuwezi kuuona kwa mtu yeyote aliyeko duniani, wala hakuna mfano wa kulinganishwa nao kwa uzuri na mvuto waliokuwa nao kwasababu Mungu aliwaumba wakamilifu sana pasipo mapungufu yeyote. Lakini baada ya wao kumkosea Mungu na kuasi ule ndipo utukufu waliokuwa nao ukaanza kuondoka kidogo kidogo na mauti kuingia ndani yao.Siku baada ya siku wakaanza kubadilika mionekano yao ikaanza kuwa kama yetu sisi tunavyoonekana sasa hivi.
Hivyo miili yao ikaanza kubadilika ghafla kutokana na kwamba Utukufu wa Mungu umewaondokea, ardhi ikalaaniwa kama tunavyosoma, jua likaanza kuwa kali, mimea ikaanza kukauka baadhi ya maeneo, na kusababisha majagwa kutokea duniani, jasho likaanza kuwatoka kutokana na jua kuwa kali, ngozi zikazidi kubadilika, makovu yakaanza kutokea..Watu wakaanza kuzaliana kwa kasi na baada ya gharika dunia ilipozidi kuharibika zaidi na kupoteza taswira iliyokuwa nayo kwanza, tunakuja kuona watu wakaanza kuweka tena ustaarabu mpya duniani wakaanza kujenga ule mnara wa Babeli ili wamfikie Mungu..Lakini Mungu alipoona matendo yao ndipo akawatawanya waende katika pembe zote za dunia..
Sasa kuanzia hapo jamii ya watu walikwenda zile sehemu zenye majangwa, wakakaa huko, wengine walikimbilia nchi za baridi, wakaa kaa huko, wengine sehemu za barafu, wengine visiwani, wengine misituni n.k...Hivyo walipoendelea kukaa kwa muda mrefu kutokana na mazingira waliyopo, wakaanza kuendana na yale mazingira, ndipo watu wakaonekana tofuati zao kulingana na mahali walipotokea.. Kwa mfano watu waliokuja pande za Afrika, mazingira ya huku tunafahamu ni ya joto, hivyo ni dhahiri kuwa ngozi ikipigwa na jua kwa muda mrefu inakuwa nyeusi, na pia nywele zinapungua..kwahiyo hatushangai kuona watu wa Afrika ni weusi, kadhalika na watu waliopo nchi za baridi miili yao kwa kawaida itahitaji joto, hivyo nywele zitalazimika kukua na kuwa ndefu huko ndipo tunapowaona watu jamii ya wazungu, ukitazama nchi kama ya India, wahindi waliopo pande za kaskazini za baridi kama DELHI n.k utaona ngozi yao ni nyeupe, kadhalika waliopo pande za kusini(mf. Sri Lanka) ambako kuna joto kali utaone ngozi yao umefifia kidogo(inakuwa nyeusi) n.k. Na kumbuka hii sio tu kwa wanadamu..bali hata kwa wanyama..Kama ukichunguza wanyama kama kondoo,ng'ombe au mbuzi mwitu, au farasi,mbwa,tembo n.k wanaotoka nchi za baridi utawaona wana manyoya mengi zaidi, kuliko wale wanaotokea nchi za joto. Hivyo kwa ufupi mazingira ndiyo yaliyowabadilisha watu, na si kingine.
SWALI:: Hivi wakati Yohana akiwa kule kisiwa cha Patmo alivyopewa ule Ufunuo wale mitume wenzake walikuwepo duniani au walikuwa wameshaondoka duniani.??Na kama walikuwepo je! walikifundisha?? Swali:Kule Yohana alisema alikuwa kisiwa cha Patmo.kisiwa cha Patmo kipo Nchi gani ndugu?? .

JIBU: Kitabu cha Ufunuo kulingana na Historia kiliandikwa kati ya mwaka AD 90 na AD 96..Wakati huo yeye(Yohana) alikuwa ni mzee sana na mitume wengine walikuwa wameshakufa.. Na aliyekipeleka katika yale makanisa saba yaliyokuwa Asia ndogo ni yeye mwenyewe. Na kuhusu kisiwa cha Patmo kilikuwa Maeneo kando kando ya Uturuki ni kisiwa kidogo sana kilichokuwa umbali kama wa km 60 mpaka 120km kutoka Uturuki (Asia ndogo) mahali makanisa yalipokuwepo.

SWALI: Ndugu Hivi yale makanisa 7 halisi aliyoonyeshwa Yohana yaliyokuwepo Asia ndogo ambayo Yohana alionyeshwa yalikuwa ni ya watu waliookoka kwa kuhubiriwa injili na mitume ndugu?!
JIBU: Kwanza ni vizuri kufahamu yale ni maeneo tofauti tofauti kama vile ilivyo leo Tanzania..kuna moshi, arusha, tanga n.k. Ndivyo ilivyokuwa pia kwa Asia ndogo (Uturuki) kulikuwa na maeneo tofauti tofauti kama Efeso, smirna, Laodikia n.k. Sasa katikati ya hayo maeneo kulikuwa na wakristo waliohubiriwa injili na mitume na kuamini. Hivyo zile barua zilipelekwa kwa wakristo waliokuwepo katika hayo maeneo husika, kila kanisa na barua yake...ukisoma kitabu cha matendo utaona ziara za mitume katikati ya baadhi ya hayo makanisa. Tazama picha chini ya hayo makanisa na kisiwa cha Patmo yalipokuwepo.
 (Ramani ya Asia ndogo(Uturuki) kipindi cha kanisa la kwanza)  (nchi ya Uturuki kwa sasa hivi ilivyo)
Ubarikiwe.

Monday, May 28, 2018

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 25

SWALI 1: Nina swali kidogo wapendwa , hivi roho ya sauli (sauli asiye paulo ) ilienda wapi baada ya kufa?(KUZIMU au PEPONI?) maana bwana alimuacha?
JIBU: Ukisoma kwenye biblia kuna kitu kinachoitwa DHAMBI YA MAUTI na DHAMBI ISIYO YA MAUTI. (1Yohana 5:16)..Sasa Hii dhambi isiyo ya mauti mtu anaweza akaitenda na ndugu wakamuombea kwa Mungu akamsamehe kutokana na maombi yao na akapata neema ya akaendelea kuishi..Lakini ipo nyingine hiyo hata mtu aombeweje, ndio utasamehewa lakini adhabu ya kifo ipo pale pale..hii inakuja pale mtu wa Mungu anapofanya dhambi ya makusudi angali anafahamu kabisa anachokifanya sio sawa. Mfano wa watu kama hawa ndio kama SAULI.

Sauli Kwanza Alimkosea Mungu kwa kwenda kinyume na maagizo yake ya kutokutii masharti aliyopewa (maana Bwana alimwambia akawaue waamaleki wote asiache kitu chochote binadamu wala mfugo, {1samweli 15} lakini yeye alikaidi, badala ya kuangamiza kila kitu yeye akaacha hai kondoo,ng'ombe na kuteka nyara baadhi ya vitu) hiyo ilimsababishia Mungu kuukataa ufalme wake, Hivyo hata angeombewaje, Mungu asingeweza kumkubali tena, kama ukisoma biblia utaona Samweli alijaribu kumwombea sana kwa Mungu ili apewe rehema lakini Bwana alichokisema juu yake alishakisema "Kwamba ufalme wake umeraruliwa amepewa mtu mwingine" (Soma 1 wafalme 16:1)..

Pili, Sauli alimkosea Mungu kwa kwenda kwa wapunga pepo kutafuta majibu ya maswali yake kitu ambacho anafahamu kabisa ni kinyume na TORATI, isitoshe yeye ndio aliyekuwa wa kwanza kuwaondoa wachawi wote katika Israeli lakini hapa ndiye anayekuwa wa kwanza kuwafuata..Sasa kitendo kama hicho ni sawa na kutenda DHAMBI YA MAUTI. Hata angelia vipi asingeweza kusamehewa aendelee kuishi..Japo baada ya kufa angeweza kuokolewa.

Na ndio maana Sauli Alipomwendea yule mchawi, Samweli alimwambia ..
1Samweli 28: 16 "Samweli akasema, Kwa nini kuniuliza mimi, AKIWA BWANA AMEKUACHA, naye amekuwa adui yako?17 Yeye Bwana amekutendea kama alivyosema kwa kinywa changu; Bwana amekurarulia ufalme mkononi mwako, na kumpa jirani yako, yaani, Daudi.18 Kwa sababu wewe hukuitii sauti ya Bwana, wala hukumtimilizia hasira yake kali juu ya Amaleki; kwa sababu hii Bwana amekutendea hili leo.19 Tena pamoja na wewe Bwana atawatia Israeli mikononi mwa Wafilisti; HATA NA KESHO WEWE NA WANAO MTAKUWAPO ""PAMOJA NAMI""; tena Bwana atawatia jeshi la Israeli pia mikononi mwa Wafilisti. "

Unaona hapo adhabu yake ilikuwa ni ufalme wake kuchukuliwa na mwingine, pamoja na kifo basi!!. Lakini baada ya kufa Samweli anamwambia, Kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Neno pamoja nami linamaanisha, Sauli atakuwepo pamoja na Samweli katika sehemu ya wenye haki, Hivyo Sauli yupo Paradiso na akina Samweli sasa, kwasababu pia kumbuka alikuwa ni mtiwa mafuta na BWANA na ndio maana Daudi hakudhubutu kumwangamiza popote pale. Ila kwasababu ya uzembe wake mwenyewe alijiondolea thawabu zake alipokuwa duniani
. Kwa maelezo marefu kuhusu "dhambi ya mauti" soma kupitia linki hii>>> https://wingulamashahidiwakristo.blogspot.com/2017/07/dhambi-ya-mauti.html#links

SWALI 2: Ufunuo Yohana 16:5 anasema "Nikamsikia malaika wa maji akisema",...Huyu malaika wa maji Yohana aliyesema alimsikia akisema "Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako,Mtakatifu, kwakuwa umehukumu hivi" ndugu tunaweza tukamfahamu huyu malaika ni nani?
JIBU: Ulimwengu wa malaika ni mkubwa/Mpana sana kama vile ulivyo ulimwengu wa wanadamu, Kama vile Mungu alivyotoa vipawa tofauti tofauti kwa wanadamu, vivyo hivyo alitoa vipawa tofauti tofauti kwa malaika zake,..wapo malaika wa maji, wapo malaika wa moto (ufunuo 14:18), wapo malaika wa vita, mfano Mikaeli na wenzake, wapo wajumbe kama Gabrieli na wenzake, na wapo pia wa sifa (makerubi na maserafi) na shetani naye alikuwa kwenye hili kundi kabla ya kuasi, n.k. kwahiyo wapo wengi hata wengine hatuwajui, na wala hatujawahi kuwaona, wapo walinzi, wapo malaika wa kila nchi, wapo wa kila mkristo mmoja mmoja, na wapo wanaosimama kwa kila huduma, n.k kila mmoja anatenda kazi kulingana na alipopangiwa na Mungu mwenyewe....Hawaonekani kwa macho, ni viumbe wa rohoni, isipokuwa mara chache chache sana, wanaonekana kama Bwana akipenda kukufunulia uwaone, Hivyo ukimwomba Mungu akufunulie hata mmoja, siku moja ikimpendeza atakuonyesha, nakumbuka sisi siku moja tulikuwa tunamtafakari Mungu mida ya usiku, kama saa 1:45 jioni, umeme ulikuwa umekatika tunatazama nyota juu tukaona kitu  mfano wa mwanga mkali sana unaofanana na ule wa kuchomelea kama wa blue hivi, tulimwona kama kwa muda wa sekundi 2, tatu hivi akatoweka, eneo lote liliangaza ule mwanga, tuliogopa sana, lakini baadaye tukajua ni Mungu alikuwa anatuonyesha utukufu wake...ndio maana MUNGU WETU ANAITWA BWANA WA MAJESHI! unaweza ukajiuliza hayo majeshi ni akina nani??? sio wanadamu kwasababu wanadamu sisi tunaitwa WANA WA MUNGU (Waebrania 1:5) bali ni malaika ndio wanaoitwa MAJESHI ya BWANA...yapo MAELFU kwa MAELFU ya malaika wanazunguka kila siku duniani kuwahudumia watu wa Mungu(Waebrania 1:13-14).

SWALI 3: Ndugu nielewesheni hapa wapenzi? Ile SANAMU YA MNYAMA ya ufunuo kumi na tatu. Tunajua ni Muungano wa madhehebu yote ulimwenguni kuwa dini moja.ndugu sasa maswali ya ni haya 1.Huu muungano wa madhebu yote na dini zote ulimwenguni yakiungana kuwa KITU KIMOJA (yaani DINI MOJA).sasa watakaokuwa wanahudumu kanisani hilo la DINI MOJA ni mapadre tu? ama watakuwa ni akina nani?.

JIBU: hapana muungano wa madhehebu na dini zote, hautakuwa muungano wa kiimani na kutengeneza kanisa moja,hapana!! bali utakuwa ni muungano wa kiitikadi, kila mtu atabaki na dini yake na dhehebu lake isipokuwa wote watakubaliana katika katiba moja. kwa mfano tanganyika ilivyoungana na zanzibar haikulazimisha watu wote tufanane, kidini, kiutamaduni n.k hapana kila nchi ilibaki na tamaduni zake na sera zake na dini yake isipokuwa mambo ya itikadi ndiyo yaliyoungana kwamfano jeshi moja,lugha moja n.k au vyama vya siasa vinapoungana, mfano kwa hapa Tanzania UKAWA, ni vyama vingi vimeungana kwa lengo fulani, lakini kila chama kina itikadi zake na desturi zake,  wameungana kwa lengo la kutimiza kusudi Fulani, lakini kila chama kinajitegemea, kwahiyo yoyote atakaye kuwa mmoja wa chama hicho automatically atakuwa ameshajiingiza moja kwa moja katika muungano huo hata kama hataki...Na ndio maana yule mwanamke anaitwa mama wa makahaba, ikiwa na maana atakuwa na mabinti anaowaendesha chini yake.. kwahiyo hapo baadaye wakishirikiana pamoja wafikie muafaka wa ustaarabu mpya wakiongozwa na Kanisa lao mama Katoliki, ambao utafanana kwa dini zote, na mtu yoyote asipoufuata, madhara yatamkuta. na hii itagusa karibu dini zote na madhehebu yote duniani..
SWALI 4: Wale mitume wa BWANA wote walikuwa wasomi?
 JIBU: Hapana sio wote walikuwa wasomi, maana biblia kuna sehemu imewataja kuwa ni watu wasio na  Elimu (Matendo 4:13 " 13 Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu WASIO NA ELIMU,WASIO NA MAARIFA , wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.") Hivyo walikuwa ni watu wa kawaida, isipokuwa yule mathayo mtoza ushuru( kwasababu mtoza ushuru ni lazima awe mtu aliyesoma).. labda pengine na mwingine ni Yuda iskariote aliyekuwa anashikilia mfuko wa hazina..lakini wengine wote walikuwa ni watu tu wa kawaida wasio na elimu wengi wao walikuwa ni wavuvi

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 24

SWALI 1: marko2:18"Nao wanafunzi wa Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwani wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga bali wanafunzi wako hawafungi? SASA BWANA ALIKUSUDIA Nini kuwajibu hivi?19"Yesu akawaambia, WALIOALIKWA HARUSINI WAZAJE KUFUNGA maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao?(BWANA ALIKUWA ANAMAANISHA NINI KUSEMA HIVYO?
JIBU: shalom! Mfano huo sawa tu, na mwanafunzi aliye na mwalimu wake, pindi anapokuwa naye anao uwezo wa kumuuliza swali lolote na likajibiwa, au akampelekea mwalimu wake maswali yote magumu yanayomsumbua na yakatatuliwa pindi wakati yupo naye, lakini kikifika kipindi cha mitihani, labda mtihani wa NECTA, pale ambapo anawajibika kuketi mwenyewe kwenye chumba cha mtihani mahali ambapo mwalimu wake hawezi kuwepo tena hapo ndipo itampasa atumie nguvu na jitihada ya ziada kutatua maswali yote peke yake anayokutana nayo kwa maarifa aliyopewa na mwalimu wake, lakini hapo mwanzo angeweza kumpelekea tu kila swali linalokuja mbele yake na akasaidiwa pasipo hata kujishughulisha...

Na ndivyo ilivyokuwa kwa mitume wa BWANA wetu YESU KRISTO wao walipewa neema ya kipekee kutembea na Mungu( BWANA YESU) duniani tofauti na wanafunzi wa Yohana au masadukayo, sasa unategemea vipi watu kama hao wafunge, au kujisumbua kwa lolote, wakati wanayemwomba wapo naye hapo hapo...wakiwa wanahitaji ufunuo wa jambo fulani si wanamkimbilia BWANA  na kumuuliza kwasababu yupo nao hapo?!!!...Na ndio maana akasema wakati utafika Bwana arusi atakapoondolewa...hapo ndipo watalazimika kufunga kama wenzao. Wakitaka ufunuo wa jambo fulani sasa itawapasa wafunge, wakitaka kutatua au kujua jambo fulani itawapasa wafunge kwanza na kuomba,Kwahiyo kile kitendo cha wao kutembea, kula, kuishi na kufundishwa na BWANA ndio kualikwa kwenyewe Harusini.

SWALI 2: SASA BWANA ALIMAANISHA NINI MSTARI WA MARKO 2:21-22? 21"Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kukuu,na pale palipotatuka huzidi. 22"Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikukuu;ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. BALI HUTIA DIVAI MPYA KATIKA VIRIBA VIPYA.JIBU: Mfano huo..unawalenga watu wanaojiita wakristo..Viriba ni vyombo maalumu vilivyokuwa vinatumika kuwekea divai wakati wa zamani, vilikuwa ninatengenezwa kwa ngozi, sasa nadhani utakuwa unafahamu pombe huwa inafura wakati inapoanza kukaribia kuchacha, na pombe zote ndivyo zilivyo, sasa, kwa wayahudi walikuwa wanatumia viriba vya ngozi ambayo bado ni mbichi, hivyo wakiweka divai ambayo bado inaendelea kuchachuka wakati ikiendelea kuvimba basi ile ngozi kwasababu bado ni laini, na mbichi, hutanuka pamoja na divai, kama vile kiatu cha ngozi, unaweza ukanunua mwanzoni kikakubana lakini baadaye kikakuenea vizuri ni kwasababu ni ngozi ambayo haijakakamaa haijawa ngumu bado...vivyo hivyo na kwa divai pia,..kwahiyo mfano ile pombe ikiwekwa kwenye kiriba ambacho kimeshakauka au kukaa sana inamaanisha kuwa ile ngozi itakuwa ishakuwa ngumu, kwahiyo ukiweka pombe changa mule ndani ni lazima kipasuke kwasababu ile pombe itavimba na kwa vile hakiwezi kutanuka mwisho wa siku kitapasuka tu...kwahiyo kiriba kipya, ni kwa divai mpya, huwezi kuweka divai mpya kwenye kiriba cha kale.

Hiyo inafunua tabia za wakristo wa leo, ambao roho zao zimegandishwa na mafundisho ya kale, wasiotaka kubadilika kwa kumruhusu Roho wa Mungu kutenda kazi ndani yao, hao ni sawa ni viriba vya kale visivyoweza kutanuka, Hivyo mfano ukija ufunuo wa kweli wa Roho Mtakatifu, ufunuo mpya mbele yao ambao hawajawahi kuusikia katika dini zao, au maisha yao, kwasababu ni viriba vya kale visivyotaka kutanuka basi vinapasuka..na ndio maana watu kama hao hawawezi kuupokea Ufunuo wa Roho wa Mungu hata kama ni kweli vipi au upo dhahiri kiasi gani, wanaishia kupinga tu kama mafarisayo kwasababu hawana uwezo wa kuchukuliana na ufunuo mpya wa Roho wa Mungu wao wataaishia kupinga tu, na kibakia katika dini zao, na ndivyo walivyokuwa mafarisayo na masadukayo wakati wa Bwana, Yeye alipowaletea kitu kipya hawakuweza kukipokea kwasababu roho zao zilikuwa zimegandishwa na mafundisho yao ya kale. Lakini wale wote waliokubali na kuilainisha mioyo yao kwa Bwana. Basi waliweza kuupokea ndio wale waliokuwa Mitume wa Bwana baadaye. Na ndio maana Bwana akawapa mifano hiyo....Hivyo ni vizuri kila siku kumruhusu Roho wa Mungu kututengeza kwa jinsi apendavyo ili kutambua ujumbe wa wakati tunaoishi...tusije tukawa tunaishi wakati wa ujumbe wa kanisa la kwanza wakati tupo katika kanisa la mwisho la Laodikia.

SWALI 3: Ndugu ninawaombeni msaada wenu mnieleewesheni ufunuo wa hivi vifungu? na unabii wake utatimia lini? Mathayo 24:29"Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile,jua litatiwa giza,na mwezi hautatoa mwangaza
wake,na nyota zitaanguka mbinguni,na nguvu za mbinguni zitatikisika;30"ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; NDIPO MATAIFA(haya mataifa baada ya kumuona kwanini yaliomboleza? na baada ya kumuona yalikwenda na wapi?) YOTE YA ULIMWENGU* watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.31"Naye atawatuma "malaika" wake pamoja na SAUTI KUU YA PARAPANDA, NAO WATAWAKUSANYA WATEULE WAKE TOKA PEPO NNE,TOKA MWISHO HUU WA MBINGU MPAKA MWISHO HUU.

JIBU: Hiyo itakuwa ni mwisho kabisa, pale mataifa yote yatakapojikusanya katika vita ile kuu ya Har magedoni, wataomboleza kwasababu Bwana hatakuja kuwafariji, Bali Atakuja na  UPANGA kutoka kinywani mwake(ufunuo 19:11-16), watajutia maisha yao ya nyuma walioishi, watahuzunika pale watakapogundua kuwa wamedanganyika na huu ulimwengu, na dini za uwongo, na kamba za mpinga-kristo na kwamba KRISTO ndiye aliyekuwa njia pekee ya uzima na kwamba anakuja na hasira kali...Maana ukisoma pale kwenye ufunuo utaona anashuka akiwa amepanda farasi mweupe, ..sasa farasi anaashiria vita, hatakuja tena amepanda punda kama kile kipindi alichokuwa anaingia Yerusalemu kuashiria amani,..La! bali atakuja na upanga, kuteketeza mataifa yote, yaliyomkataa yeye, maelfu ya watu wataomboleza watakapogundua kuwa walikuwa wanapoteza muda maisha yao yote na kwamba hakuna tena maisha waliyoyazoelea, na wala hakuna nafasi ya pili,na Bwana ataleta utawala mpya wa Amani duniani...lakini watakaookoka ni wateule wachache sana watakaokuwa duniani wakati huo, ambao ni wayahudi na watu baadhi waliokuwa wanawasaidia wayahudi, tena ni wachache sana, hivyo, kutakuwa na maafa makubwa kutoka kwa Bwana sio kipindi cha kutamani kuwepo, na watu watu wote watamwona watakaokuwepo watamwona, na kuomboleza..

SWALI 4: Ufunuo 18:11"Nao wafanya biashara wa nchi walia na kuomboleza,kwasababu hapana mtu anunuaye bidhaa yao tena;..sasa hawa wafanya biashara waliolia kwa kuangamizwa kwa KANISA KATOLIKI NA MAKAO YAKE MAKUU VATIKANI kulingana na kile kitabu cha ufunuo 18 hii babeli ya kiroho inawasaidiaje sasa katika biashara zao ndugu? mpaka walie nakuomboleza? ebu nieleweni hapo ndugu?

JIBU: Hazina yote ya dunia leo hii inashikiliwa na Vatican,(fuatilia utajua hilo), ipo Vatican ambapo ndipo makao makuu ya kanisa katoliki utajiri wote upo kule, wala usifikirie ni Marekani, jaribu tu, kuangalia miradi mikubwa kama mahospitali, mashule, taasisi za kijamii, nk. zinafadhiliwa na kumilikiwa na nani?..au chunguza karibu kila kata utakuta kanisa kubwa la katoliki, chunguza hata hapo mahali unapoishi, utaona,na ndivyo ilivyo katika sehemu kubwa za dunia.. uchumi wote wa dunia unaongozwa na huo mfumo..Na sasa kanisa hilo linaongeza nguvu kuleta madhehebu yote pamoja na dini zote, kuiunda ile chapa ya mnyama, dini na serikali itakuwa ni kitu kimoja, Papa akisema ni sawa na serikali  imesema, itafika wakati kutakuwa hakuna kuuza wala kununua pasipo kuwa na utambulisho wa dhehebu fulani au dini iliyojiunga kwenye umoja huo wa dini na madhehebu.

Ubarikiwe sana.

Ukiwa na swali lolote lihusulo biblia ..tutumie  (kwa e-mail/whatsapp/namba za simu )na kwa neema za Bwana litajibiwa.

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 23

SWALI 1: Ndugu zangu tunaweza kufahamu wale wajumbe 5 wa kanisa kila mmoja katoka Nchi gani? "Ninafahamu ndugu Paulo katoka Israel na ndugu Branham katoka marekani(ni kweli ndugu?)" je,hao 5?

JIBU: Paulo mjumbe wa kanisa la kwanza kama ulivyosema alikuwa ni MUISRAELI, IRENIO mjumbe wa kanisa la pili alizaliwa mji uliloitwa SMIRNA kwasasa ni UTURUKI ya magharibi, MARTIN Mjumbe wa kanisa la tatu alizaliwa nchi ya HUNGARY isipokuwa sehemu kubwa ya huduma yake ilikuwa ni Ufaransa, COLUMBA mjumbe wa kanisa la nne alitokea nchi ya IRELAND huko ulaya, MARTIN LUTHER mjumbe wa kanisa la tano alikuwa ni MJERUMANI, JOHN WERSLEY mjumbe wa kanisa la sita alitokea nchi ya UINGEREZA(UNITED KINGDOM)...na WILLIAM BRANHAM nabii wa Bwana kama ulivyosema alitokea Marekani, umeona injili inaenda na jua, kutokea mashariki mpaka magharibi, ilitokea israeli mashariki na inaishia marekani magharibi. kwahiyo tupo wakati wa jioni sana.


SWALI 2: Wale wajumbe ...5 waliomtangulia ndugu Mjumbe wa kanisa la saba(Branham) walibatiza ubatizo sahihi wakuzamishwa kwenye maji mengi na iwe Katika Jina La YESU KRISTO Kama alivyofanya mjumbe wa kwanza (Paulo wa kanisa la kwanza Efeso na mjumbe wa 7 ndugu Branham???...) Na Kama hawakufanya hivyo je,unaniambia hao wakristo waliowaamini tutakuwa nao kule ng'ambo kwa BWANA (nakusudia hawataenda motoni?) na kama hawataenda motoni hauoni hata hawa ambao sasa hawabatizwi katika jina la Yesu Kristo badala yake Baba,Mwana na Roho mtakatifu nao watakwenda mbinguni?

B.na kama hawa wajumbe 5 walihitilafiana na mjumbe 1 na wa7 hauoni tunawezakusema hawakuwa na Roho mtakatifu???Je kama hawakuwa naye kwanini???Na wote tunafikiri walitumwa na Mungu?(sio kama ninapinga sio wajumbe wa BWANA ndugu).

 JIBU: Ubarikiwe ndugu swali zuri sana, ni kweli wajumbe waliotangulia sio wote waliobatiza ubatizo sahihi wa kwa jina la Yesu, nyakati za Paulo na Irenio wa kanisa la pili watu ndio waliobatizwa sahihi kwa ubatizo wa jina la Yesu lakini baada ya kanisa katoliki kuoana na ukristo mwaka 325AD(katika baraza la Nikea) ndipo ubatizo sahihi wa kwa jina la Yesu Kristo, ukauliwa(ukapindishwa) hivyo wajumbe waliofuata hawakupata ufunuo huo, kwasababu ile roho ilikuwa imetafuna mafundisho ya ukweli kwa sehemu kubwa, isipokuwa kikundi kidogo sana cha watu wachache Bwana aliopenda kuwafunulia, Hivyo Bwana alianza kuwatumia wale kurejesha nuru ya  kweli kidogo kidogo, ila hawakufanikiwa kuirejesha yote. Hivyo kama waliokolewa au la! ni wazi kuwa wote waliokolewa hata kama hawakubatizwa kwa ubatizo sahihi,kwasababu kulingana na kiwango cha nuru Mungu alichowapa kwa wakati ule, kiliwatosha kuokolewa. hivyo Mungu ni Mungu wa rehema hawezi kumuhukumu mtu kwa jambo asilolijua, wataokolewa kama tu watu wa agano la kale walivyookolewa pasipo damu kumwagika kwani muda ulikuwa bado, wataokolewa kama Daudi, Samweli, Musa n.k sasa watu wa kizazi hiki cha mwisho wote ambao wamesikia ufunuo wa ubatizo sahihi na bado hawataki kubatizwa watahukumiwa kwasababu wameisikia kweli, na wameikataa, hivyo inakuwa ni dhambi kwao, jambo ambalo watu wa kanisa la tatu, la nne na la tano, hawakuipata hii neema. Na kuhusu wajumbe kuwa na Roho au la! Bwana pia anaweza kumpa mtu Roho hata kabla hajabatizwa kwamfano Kornelio alipokea ROho kabla ya kubatizwa lakini hiyo ni neema na inatokea mara chache sana, hivyo wakina luther japokuwa hawakubatizwa katika ubatizo sahihi lakini walikuwa na Roho Mtakatifu ndani yao,

SWALI 3:Mfano mtu alikuwa anafanya maovu alafu ikafika wakati wa kufa kwake akatubu, mfano saa 3:00 jioni alafu akafa saa 3:01jioni atakuwa na uzima wa milele?(mfano kuna bibi mmoja hapa kwetu alikuwa mkatoliki mnyenyekevu tu kama alivyokuwa anapenda alipenda kusali wakatialivyokuwa anaumwa sasa akasema alikufa akarudi wakati alipokuwa anaumwa sana akasema aliona nafiri kuzimu akasema nikubaya sana wale watu aliokuwa nao akawaambia wasali sana huko ni kubaya "nadhani lilikuwa ni ono" sasa hakuchukua siku nyingi akafa).


JIBU: Kwanza ni vizuri kufahamu TOBA ni neno pana kuliko wengi tunavyofikiri. Huwezi kusema leo hii naamua kutubu, kwasababu naenda kufa na sitaki niende kuzimu, Hapana TOBA ni kitu ambacho Mungu mwenyewe anakileta ndani ya moyo wa mtu ( Yohana 6: 44 "Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho". )..Unaona hapo? Hivyo toba inatokea pale Mungu mwenyewe anapougusa moyo wa mtu, kisha yule mtu anajikuta anaona kila sababu ya yeye kubadilisha maisha yake ya kale, sasa kuanzia huo wakati na kuendelea aidha awe hai, au aende kufa anakuwa mtu mwingine.. Mtu kama huyo anajikuta anaingia katika majonzi ya kuyachukia maisha yake ya kale, pengine kwa kulia na kutubu kwa kumaanisha kabisa kuacha mambo ya nyuma aliyokuwa anayaishi. Kisha baada ya Mungu kuona kumaanisha kwake, anamjibu TOBA yake kwa kumpa Amani isiyo ya kawaida. Na hii ndiyo inayompa uhakika kwamba dhambi zake zimesamehewa.


Lakini hii TOBA haiji kwasababu mtu anaona anakaribia kwenda kufa, kwasababu anaogopa kwenda kuzimu, au anataka kwenda mbinguni ndio anatubu..Watu wengi wa dizaini hiyo ni dhahiri kuwa huko nyuma walishawahi kusikia injili ya neema na kuipuuzia. Na hata wakitubu wanafanya kama kubahatisha, hivyo hawawezi kuwa na ule uhakika (ambayo ni AMANI ya kiMUNGU ndani yao) kuwathibitishia  kwamba wamesamehewa dhambi zao, labda neema ya Mungu iwe kubwa sana juu ya watu kama hao.


Kwahiyo safari ya wokovu sio  ya bahati nasibu, kwamba naikataa injili sasahivi ili kipindi fulani kikifika ndipo nitubu.Hapana, Bwana kwa wakati huo hatakusikia ..kwa maana biblia inasema katika 2Wakoritho 6: 2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa.)SWALI 4: Ndugu mzee mmoja alinihoji nakuniambia "kuna wazee wengi waliokufa kabla hata injili haijafika Tanzania akasema hata hawakubatizwa ama hawakujua kitu kinachoitwa injili n.K...Ndugu naomba nijibuni hili swali lake akaniambia "Hao watu hawatakwenda mbinguni???..Ndugu hili nilishindwa kulijibu..swali langu watu hawa wanateseka kuzimu sasa hivi au???au wako wapi kwasababu hawakupata injili?! mbarikiwe ndugu zangu wapendwa.JIBU: Hao watu ambao hawajasikia injili  kila mmoja atahukumiwa kulingana na maisha aliyoishi, kwa kawaida kila mwanadamu duniani anayo sheria ndani yake inayomuongoza huku DHAMIRA yake ikimshuhudia kabisa kwamba jambo analolifanya ni sahihi au sio sahihi(totauti na wanyama). Sasa (Hiyo ndiyo inayoitwa INJILI YA MILELE. ni tofauti na injili ya MSALABA. (Warumi 1&2)) . Watu wa kipindi cha Nuhu, Torati ilikuwa bado haijaja duniani, lakini walihukumiwa kwasababu walikuwa wanajua kabisa, uuaji, ni makosa, ushoga ni makosa, wizi ni makosa, ufiraji ni makosa, utoaji mimba ni makosa, kuzini na wanyama ni makosa, kuzini na wazazi wako ni makosa, kutukana ni makosa  n.k. Hiyo ndio Injili ya milele ambayo mtu hahitaji kuhubiriwa na yeyote ili ahifahamu, ni injili  iliyokuwepo tangu enzi na enzi, kwamba kila mwanadamu anaifahamu na anapaswa kuishi katika hiyo. Kwahiyo wale wote wasioijua torati ya Musa, au Injili ya msalaba..basi watahukumiwa kwa hiyo Injili ya milele..

Lakini kwa sasa Injili ya Msalaba imesambaa ulimwenguni kote. Hivyo sidhani kama kutakuwa na udhuru kwamba mtu yeyote  kusema hajasikia.


Ubarikiwe.

Ukiwa na swali lolote lihusulo biblia ..tutumie  (kwa e-mail/whatsapp/namba za simu )na kwa neema za Bwana litajibiwa.

Saturday, May 26, 2018

KITABU CHA UFUNUO: Mlango wa kwanza

Jina la BWANA wetu YESU KRISTO lihimidiwe daima. Karibu katika uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo leo tukianza na ile sura ya kwanza.; Tunasoma...
1 Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa malaika akamwonyesha mtumwa wake Yohana; 2 aliyelishuhudia Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu Kristo, yaani, mambo yote aliyoyaona.”

Awali ya yote tunaona hapa Yohana akiandika na kusema "Ufunuo wa Yesu Kristo" akimaanisha kuwa alichokipokea sio ufunuo wake bali ni wa Yesu mwenyewe. Kumbuka Yohana ndiye Mtume pekee aliyekuwa karibu sana na Bwana, na aliyependwa na Bwana kuliko mitume wote, Kiasi kwamba hata siri za karibu sana za Bwana alikuwa anazipokea kwanza yeye ndiye ndipo wengine wafuate, ni mtume pekee aliyekuwa akiegema kifuani mwa Bwana muda wote (Yohana 13:23, na Yohana 21:20), Na ndio maana tunaona wakati ule wa jioni wa kuumega mkate, Bwana aliposema mmoja wenu atanisaliti, Petro alimpungia mkono Yohana amuulize Bwana ni nani atakayemsaliti, na Bwana akamfunulia Yohana ni yule atakaye mmegea tonge na kumpa, kwasababu Petro alijua Yohana ndiye  kipenzi wa Bwana.
Kwasababu ya uhusiano wake wa kipekee na Bwana, ilimpelekea, mpaka kufikia hatua ya kupewa neema hii ya MAFUNUO na Bwana mwenyewe, mambo ambayo yatakuja kutokea katika siku zake na siku za mwisho. Yohana ni mfano wa Danieli ambaye naye alikuwa ni mtu aliyependwa sana na Mungu, Ikapelekea yeye naye kupewa mafunuo yanayofanana na ya Yohana. Kwahiyo kama ukichunguza utagundua watu wanaofunuliwa Mafunuo makuu kama haya sio tu kila mkristo, au mwamini yoyote bali ni mtu yule anayependezwa na Mungu, Vivyo hivyo na sisi tukimpendeza Bwana atatupa siri zake za ndani zaidi.
Mstari wa 3 unasema; "Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu". Hapa Biblia inasema heri ikiwa na maana kuwa amebarikiwa mtu yule ASOMAYE, ASIKIAYE, na AYASHIKAYE ..Na kusikiwa kunakozungumziwa hapo ni kusikia kwa masikio ya ndani (yaani kupata Ufunuo ) na sio masikio ya nje, na kuyashika ikimaanisha kuyaishi uliyoyasikia. Hivyo Mtu yeyote afanye hivyo biblia inasema amebarikiwa. Kumbuka Si watu wote wanapata neema hii ya kikielewa kitabu hichi, kwasababu ni kitabu kilichofungwa hivyo kinahitaji kufunguliwa na Roho mwenyewe. Kwahiyo kama wewe umepata neema, jitahidi kuyaishi yaliyoandikwa humo ili na wewe uitwe HERI.
Tukiendelea mistari inayofuata;
"4 Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi;
5 tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,
6 na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina".
Tunasoma hapa Yohana anaanza na salamu kwa yale makanisa 7 aliyopewa kuyaandikia maneno hayo. Anasema neema iwe kwenu na amani zitokazo kwa yeye "aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja", Hii inafunua umilele wa Mungu Elohimu, Yeye pekee ndiye asiyekuwa na mwanzo wala mwisho. Tena zitokazo kwa Roho saba walioko mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Sasa kumbuka Mungu hana Roho 7, Tunajua wote Mungu mwenyewe ni Roho(1),na nafsi moja, hapo anaposema hapa roho 7 haina maana kuwa anazo roho 7, bali anaonyesha jinsi Roho ya Mungu ilivyokuwa inatenda kazi katika yale makanisa 7 ambayo tutasoma habari zake hapo baadaye. Na pia anasema Neema na Amani zitakazo kwa Yesu Kristo aliyeshahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa. Kama tunavyojua Mungu alitoka katika UMILELE akaingia katika MUDA ili kumkomboa mwanadamu. Hivyo akaundaa mwili ili akae ndani yake. Na huo mwili ukawa YESU. 

 Kwahiyo Mungu alikuwa ndani ya Yesu akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake (2Wakorintho 5:18-19). Kwahiyo hapa haizungumzii UTATU, hapana Mungu ni mmoja anayo nafsi moja, na Roho moja. Kwa mfano mimi nazungumza na wewe kwa kutumia account ya facebook, yenye jina, picha na utambulisho wangu. Ninazungumza, ninaongea na wewe ninajibu maswali, lakini haimaanishi sisi tupo wawili. kwamba wa kwanza ni mimi  na wapili yule wa mtandaoni hapana mimi ni yule yule mmoja isipokuwa nimeingia ndani ya facebook ili  nikutane na jamii ya watu fulani. vivyo hivyo na Mungu ambaye hana mwanzo wala mwisho aliingia ndani ya mwili wa kibinadamu (1Timotheo 3:16) ili tu kutupata sisi wanadamu..Na kama vile ile account yangu siku moja  ilikuwa na mwanzo wake vivyo hivyo Bwana Yesu alikuwa na mwanzo, na ndio maana atakuja kuona kuna mahali anasema yeye ni ALFA NA OMEGA. Lakini haimaanishi kuwa Mungu(ELOHIM) ni mwanzo na mwisho..hapana Yeye hana mwanzo wala mwisho.

"7 Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina.
8 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi".


Sasa Biblia inasema upo wakati Bwana aliouweka wa yeye kurudi tena ambao kila jicho litamwona na hao waliomchoma mkuki pale Kalvari (yaani wayahudi na watu wa mataifa) watamwombolezea, kumbuka hapa sio ule wakati wa kulichukua kanisa lake, hapana bali utakuwa ni ujio wa Bwana Yesu kuja duniani na watakatifu wake waliokuwa wameshanyakuliwa muda wa miaka 7 iliyopita tangu tukio hilo litokee. Hapo ndipo kila jicho la watu waliosalia ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu watamwona na kumuombolezea..

Mathayo 24: 29 "

Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;
30 ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. (soma pia Yuda 1:14 na Ufunuo 19:11-21,)

Tukiendelea mistari inayofuata....

" 9 Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika MATESO na UFALME na SUBIRA ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu.
10 Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,
11 ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia."
Yohana anasema "mimi ndugu yenu mwenye kushiriki pamoja nanyi"...Ikiwa na maana kuwa kile alichokuwa anakipitia, ndugu wengine walikuwa wanakipitia pia.mateso, dhiki,vifungo, na subira ya Yesu Kristo. Hii inaonyesha kabisa mojawapo ya utambulisho wa mkristo kwamba yupo katika safari ya Imani ni kupitia hayo kwa ajili ya Bwana.(Kumbuka ni kwa ajili ya Bwana, na si kwasababu nyingine zozote)

Lakini tunapokuwa wakristo lakini hatuna subira, kwa ajili ya Bwana, inaonyesha kabisa hatupo miongoni mwa hao ndugu waaminio.. Yohana anasema alikuwa katika kisiwa kiitwacho PATMO.Hichi  ni kisiwa kilichokuwa maeneo ambayo sio mbali sana na yale makanisa 7 yaliyokuwepo Asia ndogo (ambayo kwasasa ni maeneo ya UTURUKI) umbali wa takribani km 60-120.

Ni kisiwa ambacho wafungwa walikuwa wanaenda kuachwa huko wafe, ni kisiwa kilichokuwa na mawe mawe tu, mijusi nyoka na kenge, na nge. Hakuna mimea kumezungukwa na maji kote, hivyo ni mahali pasipokuwa na jinsi yoyote ya kuishi au kutoroka mtu utaishia kufa kwa njaa au kuuawa na wanyama wakali. Hivyo Yohana naye alitupwa kule kama mmojawapo wa wafungwa. Na ndipo huko huko Bwana akamfunulia mambo ya siri kama tunavyoyasoma. Nasi pia tunajifunza wakati mwingine tukitupwa katika majaribu mazito (maadamu ni wakristo) tujue ni Bwana anaruhusu mwenyewe ili kutupa mafunuo zaidi.

Hivyo maono hayo Yohana aliyoonyeshwa hayakuwa ndani ya siku moja yote..Bali ulikuwa ni mfululizo wa maono kwa kipindi cha muda fulani.Ndipo akapewa maagizo kwamba ayaandike mambo yote anayoyaona na ayapeleke kwa yale makanisa saba yaliyopo Asia, yaani  Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.

 MTU MFANO WA MWANADAMU.
"12 Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu;
13 na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini.
14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto;
15 na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi".
 Tunaona Yohana alipogeuka aisikie ile sauti akaona mtu "MFANO" wa mwanadamu. aliyevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini. Kumbuka Yohana kuonyeshwa vile haikuwa na maana kuwa Bwana Yesu anataka kuonyesha mwili wake jinsi ulivyo na utukufu au unavyotisha mbele za wanadamu, hapana, bali kila kitu alichokuwa anakiona katika mwili wake kilikuwa kina maana fulani.. Kumbuka lile lilikuwa ni ONO sio kitu halisi.

Tukisoma tunaona Mtu yule alikuwa na nywele kama sufu nyeupe. Ikiashiria kuwa ni HAKIMU. (Kumbuka mahakimu huwa ni desturi yao kuvaa wigi nyeupe kichwani) Hivyo yule ni Muhukumu wa mambo yote, na weupe wake inaashiria usafi na haki ya hukumu yake. Atakapokuja kuketi katika kiti chake cha enzi cheupe, atawahukumu kwa haki watu wote. Tutakuja kuona vizuri katika sura 20.
Na pia mtu huyu alionekana ana macho kama mwali wa moto, na miguu iliyosuguliwa kama shaba. Ikifunua hukumu yake juu ya waovu katika kanisa na wasiomcha yeye ulimwenguni kote,.Kumbuka na macho kazi yake ni kuona, na miguu ni kukanyaga. Hivyo anapoonekana na macho ya moto inamaanisha kuwa anaona mambo yote yanayopaswa kuhukumiwa kwa moto. Tutakuja kuona pia katika kanisa la tatu la Thiatira (jinsi Bwana alivyojionyesha kwao kama miale ya moto na miguu ya shaba, kutokana na maovu yaliyojificha ndani ya kanisa hilo,).

Na kama miguu yake ilivyokuwa  ya SHABA atakanyaga mambo yote maovu ndani ya kanisa lake kwanza kisha baadaye atamalizia na kwa ulimwengu mzima tutakapofika  katika  sura ya 14 tutaona pia jinsi atakavyokuja kukanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu mwenyezi(Ufunuo 19:15).


Tukizidi kuendelea kusoma mistari inayofuata..;
16 Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake.
17 Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,
18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. 19 Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.
20 Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba”.

Tunaona pia mtu huyu anaonekana akiwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume. Hizi nyota saba tafsiri yake kama inavyoelezwa ni malaika saba, mkono tunajua  kazi yake ni kubeba, na ukiwa wa kuume, inamaana unabeba kitu stahiki, hivyo wale malaika (wajumbe 7) watakuwa wamebeba ujumbe stahiki kwa kanisa husika. na pia alionekana akitembea katikati ya vile vinara 7 vya taa ambavyo ndiyo yale makanisa 7. Jiulize ni kwanini hakuonekana akiwa katikati ya madhabahu, au katika birika ya shaba Katika Hekalu la Mungu?, bali anaonekana katikati ya vile vinara 7 vya Taa akitembea katikati yake?. Inamaana kuwa makao yake ni katikati ya yale makanisa saba. Huko ndipo jicho lake lilipo na Roho yake ilipo.

Mtu huyu pia alionekana na Upanga mkali ukatao kuwili unaotoka kinywani mwake. Kwa  kawaida mtu hawezi kutoa upanga mdomoni, Tunafahamu Neno la Mungu ndio upanga wa Roho (soma waefeso 6:17) na pia waebrania  4: 12 inasema …“Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo”.


Hivyo upanga huo ambao ni NENO lake ameuandaa tayari kwa ajili ya vita kwa watu wote wanaokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Na kama anavyosema ni upanga ukatao kuwili anamaanisha kuwa ni upanga unaokata pande zote yaani watu walioko ndani ya kanisa na watu walioko nje ya Kanisa.
Jambo hili tutakuja kuliona jinsi Bwana alivyojifunua kwao(Kanisa la pili Pergamo) kwamba yeye ndiye mwenye ule upanga mkali ukatao kuwili…aliasema "anayajua matendo yao na kwamba watubu na wasipotubu  atakuja kufanya vita nao kwa huo upanga wa kinywa chake.(Ufunuo 2:16).
Kadhalika na kwa watu wa mataifa wasiomjua Mungu wao nao Bwana atakuja kufanya nao vita kwa huo upanga, jambo hili tutakuja kuliona katika ile sura ya 19:15 katika siku ile atakapokuja mara ya pili na watakatifu wake.

Utaona pia baada ya Yohana kuuona muonekana wa nje wa yule mtu alianguka chini kwa hofu na kutetemeka, Tunasoma " 17 Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,
18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. "
Ndipo baada ya hayo yule mtu akajitambulisha kwa tabia zake za ndani ambazo Yohana hakuziona kwa macho..nazo ni 
1)yeye ni wa kwanza na wa mwisho,

2) aliye hai,aliyekuwa amekufa na sasa yu hai milele na milele na ambaye 

3) anazo funguo za Kuzimu.


Sasa kwa tabia hizo TATU Yohana ndipo alipojua kuwa yule MTU ni YESU KRISTO mwenyewe. Hivyo ule muonekano wa Nje ni msingi utakaotusaidi kuelezea  ujumbe na kuelewa utendaji kazi wa Yesu katika habari husika zinazofuata. Ni muhimu kuzingatia hivyo vipengele, mfano tunaweza kuona katika kila kanisa anaanza kwa kujitambulisha kwa kipengele kimoja wapo cha mwili wake au tabia zake.

Hivyo kwa ufupi Alichoonyeshwa Yohana ni mfano wa ile sanamu aliyoonyeshwa Nebukadreza juu ya zile Falme 4 zitakazokuja kutawala mpaka mwisho wa dunia. Na kwamba kila sehemu ya ile sanamu (Kichwa cha dhahabu, kifua cha fedha, kiuno cha shaba na miguu ya chuma) ilikuwa na maana, na ndio iliyounda msingi wa kuelewa undani wa kitabu cha Danieli katika sura za mbeleni.Kadhalika na hichi kitabu cha Ufunuo, sura hii ya kwanza (Ambayo Inayoonyesha muonekano na tabia za Yesu Kristo ) ni msingi wa sisi kuelewa ujumbe katika sura zinazofuata za kitabu cha Ufunuo.
Hivyo usikose mwendelezo wa sura zinazofuata..

Ubarikiwe sana.


Washirikishe na wengine habari hizi na Mungu atakubariki.