"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, May 30, 2018

MASWALI NA MAJIBU:SEHEMU YA 27

SWALI: Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?
JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu kwamba ziwa la moto  wameandaliwa shetani na malaika zake,(wale walioasi pamoja naye), kutokana na makosa waliyoyafanya huko nyuma kabla ya mwanadamu kuumbwa, ambapo shetani pamoja na kuonywa  na Mungu abaki katika kweli lakini hakutaka, akaandaliwa adhabu hiyo,Na vivyo hivyo wanadamu ambao hawataki kukaa katika ile kweli, wao pia watatupwa katika lile ziwa la moto.

lakini pia ni muhimu kufahamu kuwa Mungu hamchomi shetani au mwanadamu kwenye ziwa la moto kama kuwakomoa au kuwakomesha au kuwalipizia kisasi, hapana! bali Bwana anafanya vile ili kuondoa uovu karibu naye kwasababu yeye ni mtakatifu, ili kuelewa zaidi tafakari mfano ufuatao,

Wewe ni msafi hupendi uchafu halafu inatokea kuna uchafu umejitengeneza pembeni yako au karibu na makazi yako, uchafu huo unakuletea harufu mbaya, na kichefuchefu, na kukufanya ujisikie vibaya sana, dawa pekee ya kuutoa uchafu huo ni lazima itakuwa ni kuukusanya pamoja na kwenda kuuchoma moto? swali ni je! umeuchoma uchafu huo kwasababu unakisasi nao? au kwasababu unataka kuukomoa? jibu ni hapana!! unauchoma uchafu kwasababu umekaa mahali pasipo upasa na wewe huwezi kuchangamana na uchafu, kwahiyo itabidi utengeneze tanuru ili kuuondoa uchafu huo, na kama unavyojua takataka iliyo ngumu zaidi itachelewa kuteketea kuliko takataka illiyo laini, karatasi litawahi kuteketea kuliko mpira,

Kadhalika na Mungu pia, yeye ni mtakatifu na hachangamani na uchafu, biblia inasema tutakuwa watakatifu kwasababu yeye Mungu ni mtakatifu (1 Petro 15: 15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
16 kwa maana imeandikwa, MTAKUWA WATAKATIFU KWA KUWA MIMI NI MTAKATIFU.
17 Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. )

Unaona hapo sababu pekee ya Mungu kuuteketeza Roho zote zilizoasi katika ziwa la moto ni kwasababu yeye ni MTAKATIFU na hawezi kuchangamana na uchafu, hawezi kukaa mahali pamoja na uchafu, watu waovu hawawezi kurithi ahadi za Mungu, hawawezi kuketi pamoja naye, na kama unavyojua takataka ngumu ndiyo inayochelewa kuteketea zaidi kuliko ile laini kadhalika nafsi iliyojichafua sana na mambo maovu ndiyo itakayoadhibiwa sana kuliko ile iliyojichafua kidogo.

Luka 12: 47 "Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.
48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi". Hivyo adhabu ya shetani haiwezi kuwa sawa na ya mwanadamu, yeye atapigwa zaidi, na adhabu ya aliyeua watu 100 haiwezi kuwa sawa na aliyeua watu 10 n.k

Lakini mwisho wa yote roho zote zilizoasi(shetani na wanadamu walioasi) zitakufa katika lile ziwa la moto, kwasababu hazina uzima wa milele, hiyo ndiyo mauti ya pili biblia inayoitaja katika (ufunuo 2:11,ufunuo 20:14).

SWALI : Kwa nini Mungu hakumuua shetani.?

JIBU: Tunaweza tukajiuliza pia, kama Mungu anafahamu mambo yote na anajua pia yatakayokuja kutokea mbeleni ni kwanini basi arusuhusu mabaya yatokee mpaka kufikia kiwango cha roho ya mtu kupotea kwenda kuzimu?..Lakini biblia inatuambia (..AKILI ZAKE HAZICHUNGUZI Isaya 40:28)..Ni kweli tutajua mambo mengi kumuhusu Mungu na uweza wake wa kiungu, na mamlaka yake, na nguvu zake, lakini hatuwezi kabisa moja kwa moja kufahamu mipango yake aliyojiweka ndani ya uumbaji wake.

Sisi tunazo taratibu zetu, Mungu naye anazotaratibu zake. Anavyofikiri yeye ni mbali sana na tunavyofikiri sisi, biblia inasema kama mbingu zilivyo mbali sana, unaweza ukajiuliza mbingu ukitazama hauoni mwisho, kadhalika na mipango yake ilivyo mbali sana na mipango yetu. Isaya 55: 8 Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.
9 Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

Lakini sisi tuliookolewa tunafahamu jambo moja ambalo katika Ahadi zake alituambia ; Yeremia 29:11 "Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.". Hivyo lolote linalotokea tunaliona tunajua kabisa kuna wakati utafika tutagundua kuwa Mpango wa Mungu juu ya kumwacha shetani aendelee kuuharibu ulimwengu ulikuwa na busara mara milioni moja zaidi kama angemuondoa mapema. Na kwamba tutapewaje tuzo iliyo bora kama hatujashindana? Tiara itapaaje juu sana kama hakutakuwa na upepo wa kuikabili? tutashindaje kama hakuna vita? unaona? ipo sababu kwa kila kusudi. Na ndio maana hata sasa tunasema NJIA ZAKE NI KAMILIFU siku zote kama biblia inavyosema katika (Zaburi 18:30).

Lakini kumbuka pia shetani kuendelea kuishi mpaka sasa, sio kwamba bado hajahukumiwa bado hapana! Yeye alishahukumiwa tangu zamani, isipokuwa adhabu ya mauti ndio haijaja bado ambayo kwasasa ndio inakaribia kumfikia kwasababu siku alizobakiza kuendelea kufanya maovu zimebaki chache sana Ufunuo 12: 12 Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, AKIJUA YA KUWA ANA WAKATI MCHACHE TU. "

SWALI: Mtumishi. Ninaswali Hapa Kwenye UFUNUO 20:7 "Na Hiyo Miaka Elfu Itakapokwisha, Shetani Atafunguliwa, Atoke Kifungoni Mwake", Je, Hiyo Miaka Elfu Imeshapita Au Bado Au Ndo Wakati Huu Wa Sasa?
JIBU: Utawala wa miaka 1000 bado haujaanza, utakuja kuanza baada ya dhiki kuu kuisha, na baada ya ile SIKU KUU YA BWANA kupita, Pale Bwana atakapokuja na watakatifu wake kutoka mbinguni ambapo kila jicho litamwona. Katika siku hiyo ndio Bwana atakapokuja kuyahukumu mataifa na kuleta utawala mpya wa amani wa miaka 1000 (soma ufunuo 19 na 20 yote utaona jambo hilo), kwahiyo shetani sasa hivi hajafungwa, yupo? anatenda kazi kwa kasi sana, akijua kwamba muda wake ni mchache..huoni maasi yanavyozidi kuongezeka, mauaji, vita, anasa, ananyanyua manabii wa uongo wengi, analeta magonjwa mengi n.k huo ni uthibitisho tosha kwamba yupo na anafanya kazi kwa viwango vingine, na anapenda watu wajue kwamba yeye kafungwa ili wadanganyike siku ile iwajie ghafla. .

Ubarikiwe sana.

Ukiwa na swali lolote lihusulo biblia ..tutumie  (kwa e-mail/whatsapp/namba za simu )na kwa neema za Bwana litajibiwa.

No comments:

Post a Comment