"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, April 29, 2019

NI WAKATI GANI SHETANI ANAPENDA KUMSHAMBULIA MWAMINI?


Kama umechunguza utagundua kuwa Wanajeshi vitani sikuzote huwa hawakimbii tu ovyo ovyo kila mahali na kuanza kurusha mabomu na silaha kwa maadui zao kama wanavyojisikia tu hapana, mambo hayawi hivyo vinginevyo wanaweza wakajikuta wao ndio wanakuwa shabaha ya maadui zao, bali huwa wanatulia kwanza na kutafuta mahali pazuri ambapo maadui zao hawatawaona na pia mahali ambapo patakuwa ni rahisi kwao, hapo watapiga maadui zao vizuri na kwa upesi, hata simba porini huwa halikimbilii tu bila malengo kundi la nyumbu analoliona mbele yake na kwenda kumrukia yoyote tu ampendaye hapana, vinginevyo hataambulia chochote lakini kinyume chake utamwona anatulia katika eneo zuri la utulivu na la maficho ambalo litamsaidia kuchora mpango wake kichwani na pia litakalompa wigo wa kuchomoka kwa kasi na haraka kumrukia mnyama kabla hata hajaanza kuongeza kasi ya kukimbia..

Na ndivyo ilivyo hata kwa shetani, si kila eneo atakujaribu tu mwaminio, Mtume Paulo aliwaandikia wakorintho maneno haya 2Wakorintho 2.11 ‘Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake...’

Hii ikiwa na maana kuwa kama tukikosa kuzifahamu fikira zake, basi itakuwa ni ngumu sana sisi kumshinda yeye. Hivyo leo tutazama baadhi ya vipengele vikuu muhimu ambavyo shetani anapenda sana kuvitumia kumshambulia mkristo. Kwa kuyatazama maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo tunaweza kuvibainisha vipengele hivyo vikuu.
 
 

1) Wakati unaingia katika maisha mapya ya rohoni: Hii ipo wazi kabisa wakati tu Bwana Yesu anakuja duniani pale pale shetani alinyanyua vita vikubwa kutaka kumwangamiza mtoto Yesu kwasababu alijua akimwacha baadaye atakuja kuleta madhara makubwa sana katika ufalme wake, kwasababu aliiona nyota yake, na aliufahamu unabii wa kuja kwake, hivyo jambo analohakikisha ni kumwondoa Yule mtu tangu akiwa mchanga..Na mambo kama hayo hayo yatajirudia kwa mtu yeyote atayeingia katika wokovu leo. Hivyo usishtuke kuona mambo yanakubalikia, usishtuke kuona ndugu wanakugeuka au kukuchukia wakati mwingine, usishtuke kupitia majanga kwasababu ya imani yako.. hilo lisikusababishe kuwachukia ndugu zako au jamii, wala kuwalaani fahamu kuwa ni shetani ndiye anayeyasababisha hayo yote kutaka kukuzuia usiupende wokovu. Unachopaswa tu kufanya ni kudumu katika imani kwasababu Bwana atakuwa pamoja na wewe kukulinda na kila aina na madhara atakayojaribu kukuleta kama alivyomlinda mtoto YESU kipindi kile anazaliwa. Kadhalika pia tunaweza kujifunza katika Wanyama wawindao, Watoto wadogo wa Wanyama ndio wanaowindwa sana kuliko Wanyama waliokomaa…utaona mtoto wa tembo au mtoto wa twiga ni rahisi kuwa chaguo la Wanyama kama fisi au chui kuliko twiga mzima au tembo mzima…

2) Wakati ukiwa peke yako: Sehemu nyingine unayopaswa uwe makini nayo sana ni pale unapokuwa peke yako. Mtu aliye peke yake siku zote nguvu yake inakuwa ni ndogo kuliko anapokuwa na wenzake, hiyo ipo wazi.Hivyo shetani akishagundua kuwa kuna wakati upo peke yako, hapo ndipo anaanza tena kuamsha majaribu yake. Bwana Yesu alipojitenga peka yake kule jangwani siku 40, tunaona shetani ndipo alipomtokea na kumjaribu. Tunaweza kumwona tena Daudi alipokuwa peke yake nyumbani ndipo shetani alipomjaribu na kufanikiwa kumdondosha katika dhambi ya uzinzi. Hivyo chukua tahadhari mara mbili, na ndio maana biblia inatuonya na kutushauri kila wakati katika Muhubiri..
Mhubiri 4: 9 ‘‘Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. 10 Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! 11 Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto? 12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi
Hata Wanyama wanaowinda kama chui au fisi au simba, huwa wanapenda kumvizia yule mnyama aliye peke yake Zaidi ya kulivamia kundi zima…Na shetani naye ndio yupo hivyo hivyo.

3) Wakati upo katika hali ya udhaifu: Fursa nyingine shetani anayopenda kuitumia ni pale mkristo anapokuwa katika hali ya udhaifu, shetani anapapenda sana hapo. Wakati Bwana alipofunga siku zile 40 hakumwona adui lakini alipoona tu njaa, ndipo hapo hapo adui akatokea na kuanza kumjaribu, shetani anapenda kutumia madhaifu, njaa, magonjwa, shida, tabu ili kukunaswa kwenye mitego yake.. Ayubu wakati wote hakuwahi kukutana na shetani akizunguza naye kumlaumu kuwa yeye kamkosea Mungu, siku zote hizo hakumwona shetani lakini alipoanza kupitia majanga yale ndipo shetani akamjia kwa vinywa vya wale marafiki zake watatu kumvunja moyo, na kumtaabisha wakimwambia kuwa yeye amemkufuru Mungu ndio maana yamemkuta yale yote..

Vivyo hivyo na wewe unayejijua ni mkristo, kumbuka shetani atakusubiria katika engo hiyo pia, wakati unapitia mazingira magumu, hatakuja wakati upo kwenye raha, au mafanikio, atakutafuta kwenye shida, na misiba, huko ndipo atakapokuletea hata vipengele vya maandiko kichwani mwako, ili tu kukutoa katika mstari wa imani, atakuleta vishawishi vingi, wa watu wengi wa ajabu, atakupa mpaka njia mbadala ya kufanya kama vile alivyomshauri Bwana Yesu ageuze jiwe liwe mkate.Lakini nataka nikuambie kupitia shida, au udhaifu au taabu ya kitambo fahamu kuwa sio uthibitisho kuwa Mungu amekuacha maadamu unafahamu kuwa uhusiano wako na Mungu bado upo, usiikate imani ndugu..kuwa kama Daudi aliposema Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu nijapopita katika bonde la uvuli wa Mauti, sitaogopa kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji.(Zaburi 23). Tukirudi pia katika mifano ile ile ya Wanyama wawindao kama simba au chui huwa wanapenda kumvamia yule aliye dhaifu, wakishakosa aliye peke yake katika kundi, au aliye mtoto katika kundi, huwa wanatafuta aliyedhaifu, au mgonjwa, kwasababu hawatasumbuka sana katika kumkamata..shetani naye ni kama simba angurumaye akitafuta mtu ammeze..maandiko yanasema hivyo… 1 Petro 5:8

4) Eneo lingine analolipenda kulitumia ni wakati unahama kutoka kiwango kimoja cha utukufu hadi kingine: Kuna wakati Mungu atayaongeza mafuta yake kwako, kwa ajili ya utumishi wake, hapo napo shetani hatataka atulie kukuangalia tu unakwenda kufanikiwa kuutangaza ufalme wa Mungu, ni lazima alete mawimbi yake. Tunaona Bwana siku ile tu alipokwenda kubatizwa kule Yordani na Roho wa Mungu kushuka juu yake na kumtia mafuta yale ya utumishi mkuu kama ule, tunaona shetani akajidhihirisha kwake alipokwenda kule jangwani..Hii ni kawaida, kwa watumishi wa Mungu kukumbana na mkono wa shetani uso kwa uso safarini katika kuineza kazi ya Mungu. Lakini mwisho wa siku ataishia kushindwa tu, kwasababu vita ni vya Bwana.

Hivyo pia katika eneo hilo zingatia sana, tarajia kukutana naye na hakikisha umwachi atoke salama.

5) Eneo lingine ni Wakati upo katikati ya watu ambao unadhani wanaweza kuwa faraja au msaada mkubwa sana kwako katika imani: Hii inatokea hususani kwa watu wa imani moja na wewe…Hichi ni chanzo ambacho Mtu hawezi kukitazamia kama shetani anaweza kupitia kukujaribu lakini biblia imekithibitisha chanzo hichi, na kinakuwa na matokeo makubwa sana kwa mtu kama asipokuwa makini. na hivyo tunapaswa tuwe makini katika eneo hilo pia. Hilo tunalithibitisha kwa Bwana wetu Yesu yeye ndiye aliyewachagua mitume wake 12, na yeye ndiye aliyewatenga kwenda kufanya kazi ya kutangaza ufalme wa mbinguni pamoja naye,.na wakati mwingine aliwasifia kwa utumishi wao kwa mfano Petro alipopokea ufunuo wa kuwa yeye ni nani (Mathayo 16) alimsifia lakini mbele kidogo shetani alimtumia kupitisha hila zake..Lakini Bwana alilitambua hilo haraka kwa mafuta yaliyopo ndani yake na kumwambia Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.(Marko 8:33).

Hali kadhalika tunaona baadaye kwa mwingine aliyeitwa Yuda,alikuja kumsaliti, yeye ndio aliyeifanikisha kazi ya shetani kwa ufasaha zaidi mambo ambayo mafarisayo pamoja na wingi wao na utajiri wao walishindwa kumwangamiza Yesu lakini Yuda mmoja tu alifanikiwa kumweka Bwana mikononi mwa maadui zake. Hivyo ukiwa katika ukristo au katika utumishi hilo usilisahau akilini mwako, usiweke asilimia zako zote kwa mwanadamu mwenzako, kwasababu siku akikusaliti unaweza ukavunjika moyo kiasi cha kufa, jambo hilo lilishawahi kunikuta pia mimi, sipendi likukute na wewe, wewe kaa nao karibu, ombeaneni, pia aminianeni lakini usilitoe hili akilini kuwa inaweza kutokea nafasi shetani kumtumia kukushambulia wewe, Lakini kama ukiwa umelijua hilo mapema halitakusumbua na hivyo mishale hiyo ya shetani kwako ikija itakuwa si kitu. Bwana atakuwa upande wako.

Jambo la mwisho la kufahamu ni kuwa shetani akishaona umezijua njama zake hizi zote, na amezilita kwako na umezishinda, hatakuacha moja kwa moja, fahamu kuwa atatulia tu kwa muda fulani, halafu atarudi tena, Kama tunavyoona kwa Bwana wetu Yesu Kristo tukisoma katika
Luka 4.13 ‘Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda’’.
Hivyo biblia inatuambia mambo hayo yaliandikwa ili kutuonya sisi…Na sehemu nyingine Bwana anasema “Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele”. (Mathayo 24.25).

Kwahiyo hatupaswi kulala, wala kusinzia, kwasababu adui yetu yeye hakati tamaa, na hiyo inatufundisha tuwe watu wa kukuesha katika roho kila wakati. Kumbuka shetani hawezi kutushinda, pindi tu tunapotaka kutulia katika Neno la Mungu, Hivyo usiogope ikiwa umeyakabidhi maisha yako kwa Bwana kweli kweli na umesimama basi fahamu USHINDI NI LAZIMA.

Bwana akubariki.
Tafadhali "share" ujumbe huu na wengine.
.

Saturday, April 27, 2019

JIWE LA KUKWAZA


Marko 6 :1 ‘Akatoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata.
2 Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake?
3 Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? WAKAJIKWAA KWAKE’’. 
1 Petro 2: 6 ‘Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.
7 Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
8 Tena, JIWE LA KUJIKWAZA MGUU, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile,wasiliamini,nao waliwekwa kusudi wapate hayo’’.
Shalom! Mtu wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu…ambapo leo kwa neema zake tutajifunza juu ya jiwe la kukwaza..

Ulishawahi kutembea barabarani ghafla ukajikwaa, na ulipotazama chini ukagundua ni kipande kidogo cha jiwe ndicho kilichokukwamisha, ambacho hukutarajia kama kikengeweza kukuweka chini, na wakati mwingine unajikuta umepata jeraha Fulani, au kiatu chako kumeharibika, au kama ulikuwa umevaa sandals unakuta imekatika??..Basi kama tukio kama hilo lilishakutokea basi hiyo ni ajali inayoitwa KUJIKWAA.
 

Lakini pia kupo kujikwaa kwingine katika roho, ambapo na kwenyewe kuna hasara zake. Kama tunavyojua hakuna mtu yoyote anajikwaa akiwa amesimama, ni sharti awe katika mwendo Fulani…Na sisi wanadamu wote tupo katika mwendo, tupo safarini ndio maana tuna vipindi vya kuzaliwa, na vya kufa..hiyo ni kuonyesha kuwa duniani tunapita tu!.

Lakini Mungu amesema katika Neno lake, kuwa ameweka JIWE katika njia ya safari yetu. Ikiwa na maana kuwa tunaposafiri ni kama tunavyotembea tunapaswa tuwe makini sio tu kuangalia mbele bali pia kuangalia hatua zetu tunazozipiga, na kuangalia njia tunazozipita…Kwasababu wakati tunapita katika haya Maisha kila mtu lazima akutane na hilo JIWE, na sio kubwa kwa macho, linaonekana dogo na lakudharaulika lakini, linaweza kumweka mtu chini, Mtu akilipita pasipo kuliona atajikwaa na kuanguka, na kuumia lakini aliye makini ambaye anapita huku akitazama mbele na chini, atapunguza mwendo.. Maandiko yanasema..

‘Tazama, naweka katika Sayuni JIWE KUU LA PEMBENI, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika….. Tena, JIWE LA KUJIKWAZA MGUU, na mwamba wa kuangusha’’
Ukisoma maandiko utajua kuwa hilo jiwe si linguine Zaidi ya YESU KRISTO.

Yeye ndio JIWE kuu na Teule..Tunasoma katika maandiko…wakati akiwa hapa duniani, watu hawakumjua kama ndiye Masihi aliyetabiriwa…hawakujua kuwe yeye ni chapa ya nafsi ya Mungu, waliona ni mtu wa kawaida tu! Kwasababu walikuwa wanamjua baba yake, mama yake, walikuwa wanamjua tangu utoto wake walikuwa wanamwona jinsi anavyokua, wanapajua kwao,wanawajua wadogo zake, dada zake, wanalikuwa wanajua mpaka kipato chake alichokuwa anakipata katika ajira yake.

Kwahiyo katika kumjua huko, wakamdharau, wakamwona huyu ni Bwana mdogo tu hawezi kufanya lolote,hawakujua kuwa jiwe dogo tu linaweza kumfanya mtu aanguke chini vibaya sana, dharau zile zikasababisha wasimjue kama Mwana pekee wa Mungu, wasimjue kama Mkombozi, wasimjue kama mpatanishi kati ya wanadamu na Mungu, wasimjue kama Bwana, na Masihi, wasimjue kama Adamu wa Pili, bali wamjue tu kama mwana Kijiji au kama mwananchi wa kawaida tu,Kwahiyo Wakajikwaa kwake..Ni kama mtu apite na ghafla akutane na jiwe na kujikwaa..ndicho kilichowatokea hawa watu.

Lakini sio kwamba hao wana bahati mbaya sana, kuliko watu wa kipindi hichi, hapana! hata Hata leo JIWE hilo lipo…Na kila mtu lazima akutane nalo.. Ni jiwe dogo sana mbele za macho ya watu! Lakini ni Teule mbele za Mungu, ni dogo kiasi kwamba barabarani unaweza usilione, lakini ukijikwaa kwa jiwe ni lazima uanguke..

Ndugu unayesoma ujumbe huu, kama hujampa Bwana maisha yako, ni vizuri ukajitathmini mara mbili mbili. Kwasababu katika safari yako ni lazima utasikia injili tu! Itakufikia popote pale..na Kama ukiikataa na kuidharau na kumdharau Yesu Kristo kwako atakuwa ni JIWE LA KUKWAZA. Utaanguka siku na saa usiyodhani, wakati unakazana mbele kukimbilia malengo yako, yatakatika ghafla utakapojikuta upo kaburini na hatimaye kwenye ziwa la moto.Hapa duniani usisafiri kwa kuangalia mbele tu, bali angalia pia njia unazopita…lipo JIWE limewekwa njiani..ni JIWE la KUKWAZA, kwa wale wasioliona. Hivyo usiwe mmoja wao KUKOSANA NA YESU KRISTO, BWANA WAKO aliyetoa uhai wako kwa ajili yako.

Isafishe njia yako kwa kulitii Neno lake leo, anapokwambia mwanangu NJOO!!! Isikie leo sauti yake ukatubu na kubatizwa kwa jina lake, ili upate msamaha wa dhambi zako na ondoleo la dhambi zako, haijalishi ulimkosea kiasi gani, watu wote tulimkosea lakini ametubadilisha, na wewe pia atakubadilisha, usipoteze muda mwingi kuangalia mambo ya ulimwengu huu, wakati hali yako ya kiroho inadorora kila siku, Isafishe njia yako leo.

Zaburi 119: 9 ‘’Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako’’. Bwana akubariki,

Tafadhali ‘share’ ujumbe hu una wengine.

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:


Shalom! Mtu wa Mungu, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo litukuzwe daima, karibu tujifunze Neno la Mungu, na leo tutaenda kuona tabia za wanawake hawa wawili na naamini tutakwenda kujifunza kitu kikubwa hususani kwa upande wa wanawake wakristo. Watu hawa ambao tunakwenda kutazama tabia zao wa kwanza ni MKE WA HERODE, na wa pili ni Yule MKE WA PILATO.

Tunafahamu katika maandiko hawa wote walikuwa ni wake wa viongozi wakubwa waliokuwa wanaongoza Taifa la Israeli kipindi cha Bwana wetu Yesu Kristo, Herode alikuwa ni mtawala wa Galilaya upande wa kaskazini na Pilato alikuwa ni akida wa Yudea upande wa kusini wa taifa la Israeli, hawa wote hawakuwa wayahudi, walikuwa ni WARUMI. Kumbuka wakati ule Dola ya kiRumi ndio iliyokuwa inatawala karibu dunia nzima, hivyo kama ngome yenye nguvu ilikuwa ni sharti iwe na majimbo mengi au makoloni mengi chini yake ya kuyaamrisha. Kama tu tunavyofahamu kipindi kile cha ukoloni katika nchi yetu hii ambayo mwanzo iliitwa Tanganyika lilikuwa ni koloni la wajerumani, na ndivyo ilikuwa katika kipindi kile cha Bwana Yesu nchi ya Palestina (yaani Israeli), ilikuwa ni moja ya koloni la Warumi, hivyo sheria zote, na maagizo yote yahusuyo utawala pamoja na kodi zote zilikuwa zikisanywa na kupelekwa Rumi makao makuu.

Sasa kipindi kifupi kabla ya kuzaliwa Bwana Yesu KAISARI AUGUSTO ambaye tunamsoma habari zake katika Luka 2:1, ndiye aliyekuwa mtawala mkuu wa Dola hii ya Kirumi huko RUMI. Hivyo yeye pamoja na baraza lake chini yake likamweka Herode kuwa kama mfalme wa taifa lote la Palestina na nchi zilizokuwa kando kando yake. Herode huyu mkuu ndiye anayesifika kwa kulikarabati lile Hekalu lililokuwa limebomoka, (Yohana 2:22) na huyu ndiye aliyetaka baadaye kuja kumwua Yesu pindi anazaliwa mpaka kupelekea Yusufu na familia yake kukimbilia uamishoni Misri.

Sasa baada ya kufa kwake, ilipasa awepo mtu wa kumrithi ufalme wake, hivyo aliacha waraka wa urithi na kusema nchi ile ya Palestina igawanywe kwa watoto wake wote, kwahiyo alipokufa waraka ule ulipelekwa Rumi makao makuu ili kuombwa uthbitishwe na Kaisari, hivyo kaisari akathibitisha migawanyo ile na Palestina ikagawanywa kwa watoto wa Herode mkuu, sasa sehemu zile unazoziona zinatajwa sana katika agano jipya (Ndani ya taifa la Israeli) walipewa watoto wake wawili, ambapo mmoja alipewa atawale Galilaya na mwingine akapewa atawale (Samaria, Yudea na Idumea) karibu nusu ya Taifa zima la Israeli, na watoto wake wengine wawili waliosalia walipewa nchi za kando- upande wa Yordani ng’ambo, Iturea na trakoniki na Dekapoli.(Luka 3:1).

Sasa huyu mtoto mmoja wa Herode ambaye alipewa Galiliya ndio Herode Yule tunayemsoma aliyekuja kumuua Yohana Mbatizaji, na ndio huyu huyu alikuwa anamwinda Bwana Yesu baadaye aje kumuua alipokuwa anahubiri lakini Bwana alimwita Mbweha..Na ndio Yule Yule siku ile ya kusulibiwa kwake Pilato alimpeleka kwake ili ahukumiwe,lakini yeye akamrudisha kwa Pilato tena.

Lakini tukirudi kwa Yule mtoto wa pili wa Herode mkuu, ambaye alipewa kutawala upande wa chini wa taifa la Israeli ambayo ni YUDEA NA SAMARIA yote sehemu kubwa ya Israeli historia inaonyesha naye alikuwa ni mkatili vile vile kama ndugu zake, awali ya yote yeye ndio alikuwa akimtafuta mtoto Yesu, ili amwangamize Yesu aliporudi kutoka Misri na wazazi wake hata baada ya baba yake kufa.
Mathayo 2:19 “Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri,
20 akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto.
21 Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.
22 Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya,
23 akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo".
Huyu alizidi kuwa mbaya sana, Historia inaonyesha alifikia hatua hata ya Kaisari kule Rumi kutopendezwa naye, na kumwondoa kwa nguvu madarakani na kumpeleka uamishoni huko ufarasa na kukaa huko mpaka kufa kwake. Ndipo sasa akahitajika mtu wa kuijaza nafasi yake na ndio tunakuja kuona nafasi yake ikachukuliwa na huyu liwali mpya aliyejulikana kama PONTIO PILATO…atawale miji yote ile ya upande wa kusini.

Sasa mpaka hapo natumai utakuwa umepata picha kidogo, jinsi utawala huo ulivyokuwa umejiganyika, hivyo kipindi kile cha Yohana mbatizaji, na Bwana Yesu, hawa viongozi wawili yaani Herode na Pontio Pilato ndio waliokuwa wanalishikilia taifa la Israeli.

Kwahiyo turudi katika kiini cha Somo letu, tunaona viongozi hawa ambao hata hofu ya Mungu haikuwa ndani yao, watu ambao walikuwa sio wayahudi bali wapagani walikuwa na wake zao kila mmoja na mahali pake. Lakini tunaona tabia za hawa wanawake zilitofautiana sana, hususani pale lilipotokea suala la kuwaangamiza watu wa Mungu. Kama tunavyofahamu habari mke wa Herode japo alifahamu kabisa kuwa Yohana alikuwa ni nabii wa Mungu kweli, lakini yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kukitaka kichwa cha Yohana, zaidi hata ya wale mafarisayo ambao hao ndio wangestahili kukiomba kichwa cha Yohana lakini sio Yule mwanamke. Yeye alimshawishi mume wake amuue Yohana mbatizaji kwa faida zake mwenyewe..Na Herode naye kwa kutomwogopa Mungu akasikiliza viapo vya mke wake na kwenda kumwangamiza Yohana kule gerezani kwa kumkata kichwa.

Lakini tukirudi kwa mwanamke mwingine pili, ambaye naye pia alikuwa katika kiti cha kifalme, aliketi kama malkia, Tunaona Mume wake alipotaka kwenda kuwapa wayahudi amri ya kumuua Bwana Yesu, yeye alikuja na ushawishi mwingine tofauti na Yule wa kwanza, yeye alimwonya sana mume wake asidhubutu kufanya vile kwani ni mtumishi wa Mungu. Anaeleza jinsi alivyoteswa sana katika ndoto usiku kabla ya Yesu kusulibiwa, embu jaribu kutengeneza picha analala mara ya kwanza, anaota kama yeye ndio anayemngongelea misumari mtu asiye na hatia, anashtuka anaona ni ndoto tu, halafu analala tena, anaota kitu kile kile, anaamka tena, analala jambo lile lile tena linajirudia, hata mara 10, halafu asubuhi anakutana na mtu Yule Yule aliyekuwa anamwona kwenye ndoto analetwa mbele yake…Sura ile ile ya upole inakuja mbele zake,..


Hakika huyu mwanamke Mungu alimwekea kitu kingine cha ziada ndani yake.
Unaweza ukajiulizwa kwanini mambo kama haya hayakumtokea na Yule mke wa Herode? Pengine Yohana angekuwa mzima mpaka wakati wa Kristo kufa kwake,. Kwasababu kumbuka huyu hana chochote cha kumshinda Yule, wala Yule hakuwa na cha ziada cha kumshinda huyu lakini kwanini haikutokea kwa Yule mwanamke mwingine?.

Kaka/dada Kuna wakati unajiuliza maswali mengi lakini unakosa majibu, kwamfano utakutana na dada mmoja mkristo atakwambia anajisikia aibu kuvaa nguo zinazobana, na zaidi atakwambia ninajisikia kuhukumiwa ndani yangu pale ninapojaribu kudhubutu kuvaa sketi fupi, atakwambia ninajiona kama ninajidhalilisha pale ninapovaa suruali na kutembea nayo barabarani mbele za watu na bado mpendwa huyo huyo atakwambia ninaona kama bado sijawa mkristo pale ninapovaa vimini na kuweka ma-make up usoni na kwenda kanisani au kutembea mbele za watu…

Lakini wakati huo huo utakutana na dada mwingine naye anasema ameokoka atakwambia mbona mimi ninaona kawaida tu, Mungu haangalii mavazi anaangalia moyo..Utamkuta yupo confortable kutembea na vimini na suruali zinazobana barabarani, na wala hasikii chochote kinachomuhukumu ndani yake na bado anaona hakuna tatizo lolote ni sawa tu..

Embu jiulize ni roho ya aina gani ipo ndani yako?, Jichunguze ujiulize kama ni Roho wa Mungu mbona basi haiugui kwa namna moja na ya Yule mwenzako anayejisitiri?..Au unadhani ile ni roho ya shetani au ni mawazo yake tu yanampelekea kuwa vile? Na ya kwako ndio Roho ya Mungu?..Embu nenda kawaulize kabla ya kukutana na Kristo walikuwa wanavaaje watakueleza...watakuambia tofauti yao kabla ya kukutana na baada ya kukutana na Yesu.

Hujui kuwa unamsulibisha Kristo kwa matendo yako, tufauti yako na Yule mke wa Herode haipo, Roho ya Mungu imeshakufa ndani yako, HAIUGUI tena, unaona kila kitu ni okay!!. Utajitetea nipo katika mazingira magumu ya kuacha, lakini nataka nikuambie hawa wanawake wote wawili walikuwa katika mazingira ya level moja, walikuwa wake wa wakuu, tena wa kidunia, tena sio hata wayahudi, lakini mmoja alikuwa na hofu ya Mungu ndani yake na mwingine hakuwa nayo…Vivyo vivyo na wewe usidhani ni wewe peke yako upo katika mazingira magumu ya kuacha hivyo vitu..Wapo wengi tu, tena zaidi yako wewe lakini kwasababu wao wamekubali kuitii hiyo sauti inayougua ndani yao kila siku. Wamekuwa kama walivyokuwa leo hii..ambaye wewe unawaona washamba wamepitwa na wakati.

Ni maombi yangu utabadilisha mwenendo wako dada yangu, shetani anapenda kuwatumia wanawake, kuunyanyua ufalme wake, ni chombo chepesi cha shetani, alikitumia Edeni anakitumia na sasa..Hivyo wewe dada usifanyike kuwa chombo hicho chepesi chepesi tu cha shetani kukutumia anavyotaka. Sio kila mtindo wa dunia hii unaokuja mbele zako unakufaa.. mingi asili yake ni kuzimu,Biblia inasema unapaswa utufute mwenendo wa wanawake wacha Mungu mfano wa wakina Sara na Rebeka na Hana na sio wasanii wa nyimbo za kuzimu.

1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;
10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.
11 Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna”….Unaona??.

Halikadhalika na kwa mwanaume unayeweka mlegezo, unanyoa kama jogoo, unachora mwili wako tattoo, na huku unajiita ni mkristo..Jiulize ni kwanini wewe unaonaekana tofauti na wacha Mungu wengine?. Au Roho iliyo ndani yako ni bora zaidi kuliko ya wale wengine..Jiulize ndugu, jitathmini…Tumeambiwa tuzijaribu hizi roho, tunapenda injili za “haijalishi”..Na huku nyuma roho zetu zinaangamiia.

Ni maombi yangu, na matumaini yangu injili itatubadilisha, na kuanza kuenenda katika njia kamilifu za Mungu huku tukitii ile sauti ya Roho Mtakatifu inayougua ndani yetu kila siku kutukumbusha namna kuenenda katika utakatifu wote, mpaka kufikia kuja kwa Kristo Bwana wetu na wote kwenda mbinguni bila hila wa mawaa.

Mungu akubariki sana.

Friday, April 26, 2019

KWANINI NABII ISAYA ALIAGIZWA KUHUBIRI UCHI.?

Habari hiyo tunaipata katika kitabu cha Isaya 20: 1-6
 
1 Katika mwaka ule jemadari Yule alipofika Ashdodi,alipotumwa na Sargoni mfalme wa Ashuru;naye alipigana na Ashdodi akautwaa.
2 wakati huo Bwana alinena kwa kinywa cha Isaya,mwana wa Amozi, akisema, Haya, uvue nguo ya magunia viunoni mwako, na viatu vyako miguuni mwako.
3 Naye akafanya hivyo akaenda UCHI, miguu yake haina viatu. Bwana akasema, Kama vile mtumishi wangu Isaya anavyokwenda UCHI, hana viatu, awe ishara na ajabu kwa muda wa miaka mitatu juu ya Misri na juu ya Kushi;
4 vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi waliohamishwa, watoto kwa wazee, hawana viatu, MATAKO YAO WAZI, Misri iaibishwe.
5 Nao watafadhaika, na kuona haya kwa ajili ya Kushi, matumaini yao, na Misri, utukufu wao.
6 Na mwenyeji wa nchi ya pwani atasema katika siku hiyo, Angalia, haya ndiyo yaliyowapata watu wale tuliowatumaini, ambao tuliwakimbilia watuokoe na mfalme wa Ashuru; na sisi je! Twawezaje kupona?”.

Misri wakati huo wa kipindi cha nabii Isaya ilikuwa ni moja ya mataifa matatu makuu yenye nguvu duniani, ikitanguliwa na Ashuru pamoja na Babeli, lakini kutokana na majivuno yake kuzidi na maovu yake kuwa mengi kwa sanamu zake, Mungu alikusudia kuuangamiza, tena sio kwa maangamizi ya kawaida tu bali ya aibu, pamoja na nchi ya kando yake iliyoitwa kushi (ambayo ni nchi ya Ethiopia kwa sasa) lakini kabla ya Mungu kufanya hivyo alimtuma kwanza nabii Isaya awatolee unabii na kuwaonya , ndio hapo tunaona Isaya anaambiwa avue nguo zake na viatu vyake atembee uchi katika hiyo miji awahubirie kuwa wasipotubu, basi mfalme wa Ashuru atakuja kuwafanya hivyo watu wote wa Misri na Kushi, yaani ataipiga miji yao na kisha hataishia hapo tu atawachukua watu mateka wao wakiwa uchi wa mnyama, kutoka Misri mpaka Ashuru.

Tunafahamu kabisa kitendo cha kutembea uchi ni kitendo cha aibu kubwa sana, kwanza utaanzaje anzaje kutembea barabarani uchi,.Nakumbuka wakati Fulani nyuma kabla sijampa Bwana maisha yangu niliota ndoto ambayo siwezi kuisahau nilipoamka nilimshukuru Mungu haikuwa kweli. Niliota nimejikuta ghafla nipo katikati ya mji, nikiwa uchi wa mnyama,sasa kwa kupaniki nikaanza kutafuta nguo au kitu chochote cha kujifunika lakini nilikosa, nikaanza kutumia mikono kujisitiri, huku nikijibanza kwenye vikona kona vya kuta ili watu wasinione, ikawa nikiona watu wamepungua kidogo ninatokea pale na kwenda kukimbilia kujificha sehemu nyingine, mpaka ikafanikiwa kuwa usiku, ndipo nikakimbia moja kwa moja nyumbani, nikapata unafuu kidogo,.

Nikadhani imeishia hapo hakuna mtu aliyejua, lakini baada ya muda kidogo rafiki yangu mmoja wa kike akaja kunifuata, akaniambia mbona tumeona picha zako za uchi zimezagaa mtandaoni kila mahali? Yule ni wewe kweli au ni mwingine?..Niliposikia vile nilitamani nife palepale ili aibu ile inipotee!, maana picha ikishaingia mitandaoni haitakaa ifutike milele, vizazi na vizazi wataona..na hapo hapo likaja neno la kiingereza mbele yangu ambalo nilikuwa sijawahi kulisikia sehemu yoyote likisema “NUDE”. Halafu saa hiyo hiyo nikashutuka usingizini..Nikaenda moja kwa moja kutazama kwenye dictionary ya kingereza lile neno lina maana gani..nikakuta linamaanisha UCHI wa mnyama.. Hapo ndipo nikajua nilikuwa uchi katika roho.

Nimetoa mfano huo kuonyesha ni hali mbaya kiasi gani mtu kujikuta upo uchi halafu isitoshe mbele za watu wengi, Kulikuwa kuna sababu kubwa kabisa Mungu kumruhusu Nabii Isaya atembee vile kwa miaka 3 ili watu wa Misri na Kushi waogope kwa mambo yatakayowakuta miaka michache mbeleni.

Kwahiyo ni kawaida ya Mungu, kuzungumza na mtu au watu wake kupitia ishara fulani, tunamsoma pia Nabii Ezekieli, Bwana Mungu alimwambia ale kinyesi, kuwaonyesha wana wa Israeli kuwa wasipotubu, watapelekwa utumwani na watakula chakula kilichotiwa unajisi kwa kinyesi kwa namna hiyo. Na kwasababu wana wa Israeli hawakutaka kusikia jambo hilo lilikuja kutimia kama lilivyo siku walipokuja kuchukuliwa mateka kupelekwa utumwani.

Vivyo hivyo tunamsoma nabii mwingine, ambaye ndiye NABII MKUU , naye Mungu aliruhusu atoe ujumbe wake katika hali kama hiyo hiyo ya kuwa tupu ili watu wake wajiulize ni nini maana ya mambo hayo, watu waogope, watubu, lakini wasipotaka kutubu hali kama hiyo hiyo itakuta huko mbeleni, na huyu si mwingine zaidi ya BWANA wetu YESU KRISTO. Yeye alitundikwa uchi pale msalabani, mataifa yote yalikuja kuitazama aibu yake, mpaka watu wakasema amelaaniwa huyu..japo kuwa vile hakukuwa kwa ajili yake bali kwa ajili yetu sisi lakini Mungu aliruhusu aenende vile kama ishara ya yatakayowakuta watu wasipotubu huko mbeleni..Wakati ule wanawake walikuwa wanamlilia Bwana, lakini yeye aliwaambia msinililie mimi, hii ni ishara kwa ajili yenu, jililieni ninyi na nafsi zenu, na watoto wenu. (Luka 23:28), Na kwasababu hawakutubu kama Bwana alivyowaonya na kuwaambia ..“ni mara ngapi amejaribu kuwakusanya pamoja kama kuku akusanyavyo vifaranga vyake lakini mlikataa” hivyo nyumba yao imeachiwa hali ya ukiwa…Mnamo mwaka AD 70, Jeshi la kirumi chini ya Jenerali Titus liliizunguka Yerusalemu, na kuliteketeza hekalu na kuwaua watu kwa kuwachicha kama kuku..

Kulingana na mwanahistoria JOSEPHUS, aliyeandika historia nyingi katika usahihi za kuhusiana na matukio ya nyakati za kale za biblia, anaeleza kuwa, wakati Jeshi la Rumi limeuzunguka mji wa Yerusalemu, walikuwa wanakamata wayahudi kila siku na kuwasulibisha uchi kama walivyomsulibisha Bwana Yesu, anasema ilifika mpaka idadi ya watu 500 kwa siku waliokuwa wanasulibiwa nje ya ukuta wa Yerusalemu, na wote walikuwa wanasulibiwa uchi wa mnyama, anasema ilikuwa ni idadi kubwa mpaka kufikia MTI ya kusulibishia watu maeneo yale ikawa inakosekana …Jeshi la Rumi lilifanya vile kuwahimiza Wayahudi (Waisraeli) wasalimu amri, na wanawake na watoto wauawa kikatili sana.

Kwahiyo Bwana kuangikwa msalabani akiwa tupu (licha ya kuwa msalaba unabeba ufunuo mwingi na tofauti tofauti wa kinabii) lakini pia ile ilikuwa ni ishara kwa Wana wa Israeli kwamba wasipotubu mambo hayo hayo na zaidi ya hayo yatawakuta mbeleni…Bwana alifanyika ishara kama Isaya alivyofanyika Ishara.

Kumbuka Pia Bwana wetu huyo huyo alisema maneno haya katika Ufunuo 16:15 (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na KUYATUNZA MAVAZI YAKE, ASIENDE UCHI HATA WATU WAKAIONE AIBU YAKE.)..

Unaona hapo kwa bahati mbaya siku Bwana atakapokuja atakuta kuna watu ambao wapo UCHI rohoni, (YAANI HAWAJASITIRIWA DHAMBI ZAO)..Hao ndio wale siku ile ya hukumu watasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu na ndipo jambo lao moja baada ya lingine liwe la siri lisiwe la siri, lilifanyika gizani, litachambuliwa mbele ya mataifa yote, na mbele ya malaika wote wa Mbinguni..hatua baada ya hatua, tukio baada ya tukio, ulizini kwa siri, ulitazama pornography kwa siri, ulitoa mimba siri, uliua kwa siri, ulitukana kwa siri, ulikula rushwa kwa siri, yote yatawekwa wazi pale, ndipo hapo mtu atakumbana na aibu isiyoelekeza ambayo hajawahi kuiona katika maisha yake yote, na moja kwa moja atatupwa katika lile ziwa la moto..Lakini kwa mtu Yule ambaye sasa maisha yake yamefichwa na Kristo, siku ile vivyo hivyo dhambi zake zitafichwa na hivyo hatapita hukumuni bali atavuka na kwenda moja kwa moja uzimani.
Warumi 4: 6 “Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,
7 Heri waliosamehewa makosa yao, NA WALIOSITIRIWA DHAMBI ZAO.
8 Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi”.
Hilo ndilo vazi ndugu..Hiyo DAMU YA YESU…Lakini kwa bahati mbaya kanisa tunaloishi sisi, ambalo ndio kanisa la mwisho kati ya yale saba, limetabiriwa kuwa kanisa baya kuliko yote, na katikati ya ujumbe wetu tuliopewa, tumeonekana kuwa tu UCHI, tofauti na makanisa mengine ya nyuma yaliyopita..Hiyo ni kuonyesha kuwa tupo katika hali mbaya sana.
Tusome.

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na UCHI.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, NA MAVAZI MEUPE UPATE KUVAA, AIBU YA UCHI WAKO ISIONEKANE, na dawa ya macho ya kujipakamacho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
22Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”.
 
 

Unaona hapo?. Huu ni wakati wa kugeuka na kumaanisha kabisa kumfuata Bwana, tuhakikishe uhusiano wetu na Mungu upo sawa kila siku ili siku ile tuwe na ujasiri wa kusimama mbele zake. Ndugu Kudumu katika dhambi hakuna manufaa yoyote, zaidi ni kila siku kuishi katika maisha ya mashaka na hofu, usiikatae neema ya Kristo maishani mwako hiyo ni kwa faida yako mwenyewe. Tubu sasa umaanishe kumfuata Kristo naye atakupokea, naye atakupa VAZI, lililochovywa katika damu yake liwezalo kusitiri aibu yako yote ya rohoni.Na siku ile hutakuwa uchi mbele zake, bali utaweza kuvuka kutoka mautini kwenda uzimani…

Damu ya Bwana wetu YESU KRISTO itukuzwe milele.Amina
 
Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.

Sunday, April 21, 2019

AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA!


Luka 24:1 ‘‘Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari.
2 Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi,
3 Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu.
4 Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumeta-meta;
5 nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hata nchi, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?
6 Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya,
7 akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya tatu’’. 
Mambo yote yalimalizika siku ile Bwana aliyokata roho, pale aliposema IMEKWISHA!!..Hapo ndio ilikuwa mwisho wa mambo yote, ni sawa na mwanafunzi aliyemaliza mtihani wake wa mwisho wa kuhitimu siku ile anapoweka kalalmu yake chini ..Siku hiyo ndio mwisho wa mambo yake yote yahusuyo shule.

Na Bwana katika siku ile ya Ijumaa, ndio ulikuwa mwisho wa Majaribu yake yote, mwisho wa kazi yake yote, Hivyo mwisho wa majaribu yake ndio ulikuwa mwanzo wa ukombozi wetu! NA Heshima yetu sisi..Haleluya. Siku ile alimaliza yote aliyopaswa kufanya, maumivu, dhiki, taabu, uchungu na kila kitu! Ndio vilikuwa mwisho pale…akaweka rekodi ulimwenguni ya kuwa mwanadamu aliyeishi mpaka kufa bila kutenda dhambi hata moja!..Na kuthibitisha mbele za Mungu kuwa mwanadamu anaweza kuishi pasipo dhambi, Maisha yake yote mpaka kufa, Na ndio maana maandiko yanasema ‘amefanyika bora kupita malaika.
Waebrania 1:4 '…Ikiwa na maana kuwa Hakuna malaika yoyote ambaye alishawahi kuwa mkamilifu kama yeye.
Wengi hatujui kuwa malaika nao walijaribiwa kama tunavyojaribiwa sisi, na wapo walioshinda na wapo walioshindwa, walioshinda ndio hao wapo mbinguni sasa, na walioshindwa ndio hao ambao wapo upande wa shetani..Kwahiyo miongoni mwa walioshinda pia wametofautiana ngazi, wapo waliofanya vizuri Zaidi ya wengine..sisi wanadamu hatuwajui ni yupi aliyefanya vizuri Zaidi ya mwingine, pengine tutajua tukishafika huko juu, tutakapopewa miili ya utukufu ya kufanana na wao. Sasa miongoni mwa hao waliofanya vizuri,
 hakuna aliyefanya vizuri Zaidi ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Na kwasababu Mungu hana upendeleo, yeyote aliyefanya vizuri ndiye atakayepewa thawabu kubwa Zaidi. Kwahiyo kwasababu Bwana alifanya vizuri kuliko malaika wote wa mbinguni basi,Mungu akampa Jina ambalo, hakuna mtu aliyewahi kuwa nalo tangu ulimwengu kuumbwa, na Zaidi ya yote akapewa vitu vyote vya mbinguni na vya duniani..Akakabidhiwa mamlaka yote ya mbinguni na duniani juu ya watu wote..kwamba kila goti lipigwe mbele zake. Utasema ni wapi kwenye biblia jambo hilo lipo..soma.

Wafilipi 2: 5 ’Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;
6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;
7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;
8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
9 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;
11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba’’.
Na kwasababu sisi tuliomwamini ni ndugu zake, hivyo hawezi kutuacha chini, ni lazima nasi pia tutamiliki naye, malaika watakuwa chini yetu, kwasababu yeye yupo juu ya malaika wote sharti na sisi tuliokolewa tuwepo naye..Ni sawa na kijana apambane mpaka aipate nafasi ya uraisi, ndugu zake kwa namna moja au nyingine watafika tu ikulu mahali anapokaa..mama yake na baba yake watamtembelea hata ikiwezekana kulala kule,na hiyo ni kwasababu tu wale ni ndugu zake! na si kingine kingine..

Kadhalika na Bwana Yesu kwa Haki yake ambayo imemfanya kupewa mamlaka yote ya mbinguni na duniani, na kupewa enzi yote na kuketi katika kile kiti cha enzi, sasa sisi ndugu zake (ambao ni wanadamu na si malaika) hawezi kututupa, kwa namna moja au nyingine tutafika tu pale alipo haleluya!! Ndio maana kuna umuhimu sana wa kuwa ndugu wa damu wa Bwana wetu Yesu Kristo nikimaanisha ndugu wa kuzaliwa mara ya pili. Kwasababu hakuna njia yoyote ya kumkaribia yeye kama hatutazaliwa mara ya pili kwa damu yake!! Kumbuka si kwa damu ya mwanadamu bali kwa damu yake, sio kwa mapenzi ya mwili bali kwa mapenzi yake..wengi wanatenda mema na kufanya mambo mazuri na kusema kwa matendo yangu haya lazima nitamwona Mungu, ndugu yangu usidanganyike…

Unaweza ukatenda matendo mazuri kuliko mkristo yeyote duniani na bado usimkaribie Mungu hata kidogo…kwanini iwe hivyo? Jibu ni rahisi ni kwasababu wewe sio ndugu wa damu wa yule mhusika, kwahiyo matendo yako mazuri ni bure!.

Ndugu yangu kama wewe ni muislamu unasoma ujumbe huu, au mkristo ambaye bado hujayajua vizuri mamlaka Bwana Yesu aliyopewa na vigezo vya kuwa mrithi pamoja naye, na unasema moyoni ninasaidia masikini, ninawaheshimu wazazi, sidhulumu, sifanyi hichi sifanyi kile, ukijidanganya kuwa kwa mambo hayo tu upo karibu na Mungu na huku umemweka Kristo nyuma…Hujazaliwa mara pili katika damu yake, napenda nikuambie ndugu yangu UNAPOTEZA MUDA!!!! Matendo yako ni mazuri lakini hayatakusaidia huko mbeleni. Huko mbeleni ni UNDUGU ndio utakaojalisha kwanza na kisha ndio matendo yafuate!..Ni sawa na kwenda kumfanyia boss wako mema yote unayoyajua duniani na kumpendeza kwa viwango vyote ukitumai kuwa siku moja atakurithisha kampuni lake!!...hilo katika akili yako lifute, kwasababu hawezi kuacha kumrithisha mtoto wake (damu yake) akurithishe wewe?..hata kama mwanawe hana tabia nzuri kama za kwako, hata kama wewe ni mchapa kazi kuliko yeye, siku moja huyo mtoto atakuja kuwa boss wako tu…kwanini?? Kwasababu ya uhusiano wa kidamu uliopo kati ya yule mtoto na baba yake!!.

Na ufalme wa Mbinguni ndio upo hivyo hivyo, ndio maana ufalme wa mbinguni unaitwa URITHI, sio UTAHIFISHWAJI, hapana bali URITHISHWAJI, wanarithishwa WANA WA MUNGU tu. Kumbuka pia ufalme wa mbinguni haukuanza siku ile Bwana Yesu aliposulibiwa, ufalme wa mbinguni ulikuwepo kabla hata ya dunia kuumbwa, ni kitu kinachoendelea, kwahiyo kitakachotokea ni urithishwaji, Na wana wa Mungu ndio watakaourithi, na wana wa Mungu ni wale wote waliomwamini Yesu Kristo na kumpokea kwa kuzaliwa mara ya pili.
Yohana 1:12 ‘Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;.
Kwahiyo ndugu yangu, siku ya leo (SIKU YA BWANA KUFUFUKA). Ni siku ya muhimu sana,Bwana anapowatembelea wengi duniani kuwapa wokovu asikupite na wewe. Kama hujazaliwa mara ya pili, huu ni wakati mzuri wa kufanya hivyo…Utauliza unazaliwaje mara ya pili?...Biblia imetupa majibu, kuwa hatuwezi kurudi tena kwenye matumbo ya mama zetu na kuzaliwa tena!!..Kuzaliwa mara ya pili ni lugha ya rohoni, yenye maana ya kufanyika upya kwa Maisha yako ya kiroho, yaani kugeuzwa na kuwa mwingine katika mwelekeo wako wa kiimani. Hiyo ndio maana ya kuzaliwa mara ya pili. Tunasema Taifa ya Tanganyika lilizaliwa mwaka 1961, haimaanishi liliingia tumboni kwa mama yake na kuzaliwa hapana! Bali ni lugha tu inayomaanisha, kuwa lilifanyika upya kidemokrasia na kuwa taifa huru linalojitegemea mwaka huo. Na katika Imani ya kikristo ndio hivyo hivyo, unapofanyika upya kifikra kwa nguvu za kiMungu, unakuwa umezaliwa mara ya pili. Na zipo hatua chache za kufanyika upya huko…
Yohana 3:1 ''Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi.
2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye.
3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, MTU ASIPOZALIWA MARA YA PILI, HAWEZI KUUONA UFALME WA MUNGU.
4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?
5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, MTU ASIPOZALIWA KWA MAJI NA KWA ROHO, HAWEZI KUUINGIA UFALME WA MUNGU.
6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili".
Kwahiyo hatua za kufuata ili uwe umezaliwa mara ya pili baada ya kumwamini Bwana Yesu Kristo kuwa ni mkombozi wa ulimwengu, na kuwa yeye ndiye aliyeshinda kila kitu, na kukabidhiwa mamlaka yote ya mbinguni na duniani, hatua inayofuata ni kwenda kubatizwa katika maji mengi na kwa jina lake (Yesu Kristo), kuwa kwako kama ishara ya kufa na kufufuka na Kristo, (huko ndio kuzaliwa kwa maji Bwana alikokuzungumzia) na baada ya kubatizwa Bwana Mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu ndani yako atakayekusaidia kushinda dhambi, na kukuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko, na kukulinda, (Huko ndiko kuzaliwa kwa Roho).

Sasas ukikamilisha hatua hizo tatu, yaani kuamini, kubatizwa kwa maji, na kubatizwa kwa Roho Mtakatifu…Utakuwa tayari umezaliwa mara ya pili, umefanyika kiumbe kimpya , nawe unakuwa ni mwana wa Mungu, mrithi wa Mungu.ya kale yote yamepita, Tazama yamekuwa mapya,(2 Wakoritho 5:17) Unakuwa ni NDUGU wa Bwana WETU YESU KRISTO, wa Damu kabisa…Unakuwa mrithi wa ahadi za Mungu, hakuna atakayeweza kukushtaki kuanzia wakati huo, wala hakuna atakayeweza kukutenga na upendo wake…

Ndugu Kwasasa hatuujui vizuri kwa mapana na marefu urithi huo, tunajua kwa sehemu tu! Lakini baada ya maisha haya kuisha, ndipo tutakapomfurahia Mungu, tutamjua kwa mapana na marefu utajiri aliotupa na heshima aliyotuheshimu nayo, kwa kupitia mwanawe mpendwa YESU KRISTO.

Ni maombi yangu kuwa katika msimu huu wa pasaka, Utatambua maana yake katika maisha yako, na pia utafanya maamuzi Mema na ya Busara na Bwana akusaidie.