"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, April 29, 2019

NI WAKATI GANI SHETANI ANAPENDA KUMSHAMBULIA MWAMINI?


Kama umechunguza utagundua kuwa Wanajeshi vitani sikuzote huwa hawakimbii tu ovyo ovyo kila mahali na kuanza kurusha mabomu na silaha kwa maadui zao kama wanavyojisikia tu hapana, mambo hayawi hivyo vinginevyo wanaweza wakajikuta wao ndio wanakuwa shabaha ya maadui zao, bali huwa wanatulia kwanza na kutafuta mahali pazuri ambapo maadui zao hawatawaona na pia mahali ambapo patakuwa ni rahisi kwao, hapo watapiga maadui zao vizuri na kwa upesi, hata simba porini huwa halikimbilii tu bila malengo kundi la nyumbu analoliona mbele yake na kwenda kumrukia yoyote tu ampendaye hapana, vinginevyo hataambulia chochote lakini kinyume chake utamwona anatulia katika eneo zuri la utulivu na la maficho ambalo litamsaidia kuchora mpango wake kichwani na pia litakalompa wigo wa kuchomoka kwa kasi na haraka kumrukia mnyama kabla hata hajaanza kuongeza kasi ya kukimbia..

Na ndivyo ilivyo hata kwa shetani, si kila eneo atakujaribu tu mwaminio, Mtume Paulo aliwaandikia wakorintho maneno haya 2Wakorintho 2.11 ‘Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake...’

Hii ikiwa na maana kuwa kama tukikosa kuzifahamu fikira zake, basi itakuwa ni ngumu sana sisi kumshinda yeye. Hivyo leo tutazama baadhi ya vipengele vikuu muhimu ambavyo shetani anapenda sana kuvitumia kumshambulia mkristo. Kwa kuyatazama maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo tunaweza kuvibainisha vipengele hivyo vikuu.
 
 

1) Wakati unaingia katika maisha mapya ya rohoni: Hii ipo wazi kabisa wakati tu Bwana Yesu anakuja duniani pale pale shetani alinyanyua vita vikubwa kutaka kumwangamiza mtoto Yesu kwasababu alijua akimwacha baadaye atakuja kuleta madhara makubwa sana katika ufalme wake, kwasababu aliiona nyota yake, na aliufahamu unabii wa kuja kwake, hivyo jambo analohakikisha ni kumwondoa Yule mtu tangu akiwa mchanga..Na mambo kama hayo hayo yatajirudia kwa mtu yeyote atayeingia katika wokovu leo. Hivyo usishtuke kuona mambo yanakubalikia, usishtuke kuona ndugu wanakugeuka au kukuchukia wakati mwingine, usishtuke kupitia majanga kwasababu ya imani yako.. hilo lisikusababishe kuwachukia ndugu zako au jamii, wala kuwalaani fahamu kuwa ni shetani ndiye anayeyasababisha hayo yote kutaka kukuzuia usiupende wokovu. Unachopaswa tu kufanya ni kudumu katika imani kwasababu Bwana atakuwa pamoja na wewe kukulinda na kila aina na madhara atakayojaribu kukuleta kama alivyomlinda mtoto YESU kipindi kile anazaliwa. Kadhalika pia tunaweza kujifunza katika Wanyama wawindao, Watoto wadogo wa Wanyama ndio wanaowindwa sana kuliko Wanyama waliokomaa…utaona mtoto wa tembo au mtoto wa twiga ni rahisi kuwa chaguo la Wanyama kama fisi au chui kuliko twiga mzima au tembo mzima…

2) Wakati ukiwa peke yako: Sehemu nyingine unayopaswa uwe makini nayo sana ni pale unapokuwa peke yako. Mtu aliye peke yake siku zote nguvu yake inakuwa ni ndogo kuliko anapokuwa na wenzake, hiyo ipo wazi.Hivyo shetani akishagundua kuwa kuna wakati upo peke yako, hapo ndipo anaanza tena kuamsha majaribu yake. Bwana Yesu alipojitenga peka yake kule jangwani siku 40, tunaona shetani ndipo alipomtokea na kumjaribu. Tunaweza kumwona tena Daudi alipokuwa peke yake nyumbani ndipo shetani alipomjaribu na kufanikiwa kumdondosha katika dhambi ya uzinzi. Hivyo chukua tahadhari mara mbili, na ndio maana biblia inatuonya na kutushauri kila wakati katika Muhubiri..
Mhubiri 4: 9 ‘‘Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. 10 Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! 11 Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto? 12 Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi
Hata Wanyama wanaowinda kama chui au fisi au simba, huwa wanapenda kumvizia yule mnyama aliye peke yake Zaidi ya kulivamia kundi zima…Na shetani naye ndio yupo hivyo hivyo.

3) Wakati upo katika hali ya udhaifu: Fursa nyingine shetani anayopenda kuitumia ni pale mkristo anapokuwa katika hali ya udhaifu, shetani anapapenda sana hapo. Wakati Bwana alipofunga siku zile 40 hakumwona adui lakini alipoona tu njaa, ndipo hapo hapo adui akatokea na kuanza kumjaribu, shetani anapenda kutumia madhaifu, njaa, magonjwa, shida, tabu ili kukunaswa kwenye mitego yake.. Ayubu wakati wote hakuwahi kukutana na shetani akizunguza naye kumlaumu kuwa yeye kamkosea Mungu, siku zote hizo hakumwona shetani lakini alipoanza kupitia majanga yale ndipo shetani akamjia kwa vinywa vya wale marafiki zake watatu kumvunja moyo, na kumtaabisha wakimwambia kuwa yeye amemkufuru Mungu ndio maana yamemkuta yale yote..

Vivyo hivyo na wewe unayejijua ni mkristo, kumbuka shetani atakusubiria katika engo hiyo pia, wakati unapitia mazingira magumu, hatakuja wakati upo kwenye raha, au mafanikio, atakutafuta kwenye shida, na misiba, huko ndipo atakapokuletea hata vipengele vya maandiko kichwani mwako, ili tu kukutoa katika mstari wa imani, atakuleta vishawishi vingi, wa watu wengi wa ajabu, atakupa mpaka njia mbadala ya kufanya kama vile alivyomshauri Bwana Yesu ageuze jiwe liwe mkate.Lakini nataka nikuambie kupitia shida, au udhaifu au taabu ya kitambo fahamu kuwa sio uthibitisho kuwa Mungu amekuacha maadamu unafahamu kuwa uhusiano wako na Mungu bado upo, usiikate imani ndugu..kuwa kama Daudi aliposema Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu nijapopita katika bonde la uvuli wa Mauti, sitaogopa kwa maana wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji.(Zaburi 23). Tukirudi pia katika mifano ile ile ya Wanyama wawindao kama simba au chui huwa wanapenda kumvamia yule aliye dhaifu, wakishakosa aliye peke yake katika kundi, au aliye mtoto katika kundi, huwa wanatafuta aliyedhaifu, au mgonjwa, kwasababu hawatasumbuka sana katika kumkamata..shetani naye ni kama simba angurumaye akitafuta mtu ammeze..maandiko yanasema hivyo… 1 Petro 5:8

4) Eneo lingine analolipenda kulitumia ni wakati unahama kutoka kiwango kimoja cha utukufu hadi kingine: Kuna wakati Mungu atayaongeza mafuta yake kwako, kwa ajili ya utumishi wake, hapo napo shetani hatataka atulie kukuangalia tu unakwenda kufanikiwa kuutangaza ufalme wa Mungu, ni lazima alete mawimbi yake. Tunaona Bwana siku ile tu alipokwenda kubatizwa kule Yordani na Roho wa Mungu kushuka juu yake na kumtia mafuta yale ya utumishi mkuu kama ule, tunaona shetani akajidhihirisha kwake alipokwenda kule jangwani..Hii ni kawaida, kwa watumishi wa Mungu kukumbana na mkono wa shetani uso kwa uso safarini katika kuineza kazi ya Mungu. Lakini mwisho wa siku ataishia kushindwa tu, kwasababu vita ni vya Bwana.

Hivyo pia katika eneo hilo zingatia sana, tarajia kukutana naye na hakikisha umwachi atoke salama.

5) Eneo lingine ni Wakati upo katikati ya watu ambao unadhani wanaweza kuwa faraja au msaada mkubwa sana kwako katika imani: Hii inatokea hususani kwa watu wa imani moja na wewe…Hichi ni chanzo ambacho Mtu hawezi kukitazamia kama shetani anaweza kupitia kukujaribu lakini biblia imekithibitisha chanzo hichi, na kinakuwa na matokeo makubwa sana kwa mtu kama asipokuwa makini. na hivyo tunapaswa tuwe makini katika eneo hilo pia. Hilo tunalithibitisha kwa Bwana wetu Yesu yeye ndiye aliyewachagua mitume wake 12, na yeye ndiye aliyewatenga kwenda kufanya kazi ya kutangaza ufalme wa mbinguni pamoja naye,.na wakati mwingine aliwasifia kwa utumishi wao kwa mfano Petro alipopokea ufunuo wa kuwa yeye ni nani (Mathayo 16) alimsifia lakini mbele kidogo shetani alimtumia kupitisha hila zake..Lakini Bwana alilitambua hilo haraka kwa mafuta yaliyopo ndani yake na kumwambia Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.(Marko 8:33).

Hali kadhalika tunaona baadaye kwa mwingine aliyeitwa Yuda,alikuja kumsaliti, yeye ndio aliyeifanikisha kazi ya shetani kwa ufasaha zaidi mambo ambayo mafarisayo pamoja na wingi wao na utajiri wao walishindwa kumwangamiza Yesu lakini Yuda mmoja tu alifanikiwa kumweka Bwana mikononi mwa maadui zake. Hivyo ukiwa katika ukristo au katika utumishi hilo usilisahau akilini mwako, usiweke asilimia zako zote kwa mwanadamu mwenzako, kwasababu siku akikusaliti unaweza ukavunjika moyo kiasi cha kufa, jambo hilo lilishawahi kunikuta pia mimi, sipendi likukute na wewe, wewe kaa nao karibu, ombeaneni, pia aminianeni lakini usilitoe hili akilini kuwa inaweza kutokea nafasi shetani kumtumia kukushambulia wewe, Lakini kama ukiwa umelijua hilo mapema halitakusumbua na hivyo mishale hiyo ya shetani kwako ikija itakuwa si kitu. Bwana atakuwa upande wako.

Jambo la mwisho la kufahamu ni kuwa shetani akishaona umezijua njama zake hizi zote, na amezilita kwako na umezishinda, hatakuacha moja kwa moja, fahamu kuwa atatulia tu kwa muda fulani, halafu atarudi tena, Kama tunavyoona kwa Bwana wetu Yesu Kristo tukisoma katika
Luka 4.13 ‘Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda’’.
Hivyo biblia inatuambia mambo hayo yaliandikwa ili kutuonya sisi…Na sehemu nyingine Bwana anasema “Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele”. (Mathayo 24.25).

Kwahiyo hatupaswi kulala, wala kusinzia, kwasababu adui yetu yeye hakati tamaa, na hiyo inatufundisha tuwe watu wa kukuesha katika roho kila wakati. Kumbuka shetani hawezi kutushinda, pindi tu tunapotaka kutulia katika Neno la Mungu, Hivyo usiogope ikiwa umeyakabidhi maisha yako kwa Bwana kweli kweli na umesimama basi fahamu USHINDI NI LAZIMA.

Bwana akubariki.
Tafadhali "share" ujumbe huu na wengine.
.

No comments:

Post a Comment