Marko 6 :1 ‘Akatoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata.2 Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake?3 Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? WAKAJIKWAA KWAKE’’.
1 Petro 2: 6 ‘Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.7 Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
8 Tena, JIWE LA KUJIKWAZA MGUU, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile,wasiliamini,nao waliwekwa kusudi wapate hayo’’.
Shalom! Mtu wa Mungu, karibu tujifunze Neno la Mungu…ambapo leo kwa neema zake tutajifunza juu ya jiwe la kukwaza..
Ulishawahi kutembea barabarani ghafla ukajikwaa, na ulipotazama chini ukagundua ni kipande kidogo cha jiwe ndicho kilichokukwamisha, ambacho hukutarajia kama kikengeweza kukuweka chini, na wakati mwingine unajikuta umepata jeraha Fulani, au kiatu chako kumeharibika, au kama ulikuwa umevaa sandals unakuta imekatika??..Basi kama tukio kama hilo lilishakutokea basi hiyo ni ajali inayoitwa KUJIKWAA.
Lakini pia kupo kujikwaa kwingine katika roho, ambapo na kwenyewe kuna hasara zake. Kama tunavyojua hakuna mtu yoyote anajikwaa akiwa amesimama, ni sharti awe katika mwendo Fulani…Na sisi wanadamu wote tupo katika mwendo, tupo safarini ndio maana tuna vipindi vya kuzaliwa, na vya kufa..hiyo ni kuonyesha kuwa duniani tunapita tu!.
Lakini Mungu amesema katika Neno lake, kuwa ameweka JIWE katika njia ya safari yetu. Ikiwa na maana kuwa tunaposafiri ni kama tunavyotembea tunapaswa tuwe makini sio tu kuangalia mbele bali pia kuangalia hatua zetu tunazozipiga, na kuangalia njia tunazozipita…Kwasababu wakati tunapita katika haya Maisha kila mtu lazima akutane na hilo JIWE, na sio kubwa kwa macho, linaonekana dogo na lakudharaulika lakini, linaweza kumweka mtu chini, Mtu akilipita pasipo kuliona atajikwaa na kuanguka, na kuumia lakini aliye makini ambaye anapita huku akitazama mbele na chini, atapunguza mwendo.. Maandiko yanasema..
‘Tazama, naweka katika Sayuni JIWE KUU LA PEMBENI, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika….. Tena, JIWE LA KUJIKWAZA MGUU, na mwamba wa kuangusha’’
Ukisoma maandiko utajua kuwa hilo jiwe si linguine Zaidi ya YESU KRISTO.
Yeye ndio JIWE kuu na Teule..Tunasoma katika maandiko…wakati akiwa hapa duniani, watu hawakumjua kama ndiye Masihi aliyetabiriwa…hawakujua kuwe yeye ni chapa ya nafsi ya Mungu, waliona ni mtu wa kawaida tu! Kwasababu walikuwa wanamjua baba yake, mama yake, walikuwa wanamjua tangu utoto wake walikuwa wanamwona jinsi anavyokua, wanapajua kwao,wanawajua wadogo zake, dada zake, wanalikuwa wanajua mpaka kipato chake alichokuwa anakipata katika ajira yake.
Kwahiyo katika kumjua huko, wakamdharau, wakamwona huyu ni Bwana mdogo tu hawezi kufanya lolote,hawakujua kuwa jiwe dogo tu linaweza kumfanya mtu aanguke chini vibaya sana, dharau zile zikasababisha wasimjue kama Mwana pekee wa Mungu, wasimjue kama Mkombozi, wasimjue kama mpatanishi kati ya wanadamu na Mungu, wasimjue kama Bwana, na Masihi, wasimjue kama Adamu wa Pili, bali wamjue tu kama mwana Kijiji au kama mwananchi wa kawaida tu,Kwahiyo Wakajikwaa kwake..Ni kama mtu apite na ghafla akutane na jiwe na kujikwaa..ndicho kilichowatokea hawa watu.
Lakini sio kwamba hao wana bahati mbaya sana, kuliko watu wa kipindi hichi, hapana! hata Hata leo JIWE hilo lipo…Na kila mtu lazima akutane nalo.. Ni jiwe dogo sana mbele za macho ya watu! Lakini ni Teule mbele za Mungu, ni dogo kiasi kwamba barabarani unaweza usilione, lakini ukijikwaa kwa jiwe ni lazima uanguke..
Ndugu unayesoma ujumbe huu, kama hujampa Bwana maisha yako, ni vizuri ukajitathmini mara mbili mbili. Kwasababu katika safari yako ni lazima utasikia injili tu! Itakufikia popote pale..na Kama ukiikataa na kuidharau na kumdharau Yesu Kristo kwako atakuwa ni JIWE LA KUKWAZA. Utaanguka siku na saa usiyodhani, wakati unakazana mbele kukimbilia malengo yako, yatakatika ghafla utakapojikuta upo kaburini na hatimaye kwenye ziwa la moto.Hapa duniani usisafiri kwa kuangalia mbele tu, bali angalia pia njia unazopita…lipo JIWE limewekwa njiani..ni JIWE la KUKWAZA, kwa wale wasioliona. Hivyo usiwe mmoja wao KUKOSANA NA YESU KRISTO, BWANA WAKO aliyetoa uhai wako kwa ajili yako.
Isafishe njia yako kwa kulitii Neno lake leo, anapokwambia mwanangu NJOO!!! Isikie leo sauti yake ukatubu na kubatizwa kwa jina lake, ili upate msamaha wa dhambi zako na ondoleo la dhambi zako, haijalishi ulimkosea kiasi gani, watu wote tulimkosea lakini ametubadilisha, na wewe pia atakubadilisha, usipoteze muda mwingi kuangalia mambo ya ulimwengu huu, wakati hali yako ya kiroho inadorora kila siku, Isafishe njia yako leo.
Zaburi 119: 9 ‘’Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako’’. Bwana akubariki,
Tafadhali ‘share’ ujumbe hu una wengine.
No comments:
Post a Comment