"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Wednesday, January 31, 2018

NJIA MUNGU ALIYOIWEKA KWA KILA JAMBO:

Kuna NJIA za kufikia kila jambo, ambayo Mungu tayari alishaziweka tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, kwa mfano ili mwanadamu amfikie Mungu, tayari njia ilishaandaliwa, nayo ni YESU KRISTO, (Yohana 14:6" Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi". ), watu wengi wanapotea wakidhani au wakijifariji kuwa zipo njia nyingi mbalimbali za kumfikia Mungu na zote zinaishia sehemu moja, kwamba unaweza ukawa muhindu, au m-muhamedi au m-budha n.k. na bado ukafika kwa Mungu. Huo ni uongo NJIA ni moja tu (nayo ni YESU KRISTO) na Mungu alishaitengeneza na hakuna mikato. Hivyo kama unataka kumfikia Mungu ni sharti upitie hiyo, nyingine zote zinapotosha.


Vivyo hivyo pia katika kufikia BARAKA fulani za MAISHA, Kuna njia ambazo Mungu alishaziweka zifuatwe hapa duniani, kwamfano ili kupata afya, ili kupata maisha marefu, ili kupata mafanikio, ili kupata cheo, ili kupata amani,n.k. ni lazima uzingatie njia hizo ambazo Mungu alishaziweka vinginevyo utajikuta unakosa shabaha na kuona kama Mungu hana msaada wowote kwako kwasababu tu ulikosa kujua njia sahihi ya kupita ili kufikia malengo yako ni ipi.


Kwa mfano Njia ambayo Mungu aliiweka kwa mtu apate kuishi maisha marefu na ya kheri biblia inasema katika Mithali 10:27 "Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa. Na pia ukisoma.." Waefeso 6:2-3 inasema " Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia."

Kwahiyo kama ungependa uwe na maisha marefu hapa duniani kwanza ni UMCHE BWANA, na lingine ni kuwaheshimu wazazi, lakini njia nyingine zinazoonekana kuwa ni sawa kama vile kuzingatia MLO KAMILI, kuzingatia MAZOEZI, au Kupata muda mrefu wa kupumzika, au kuzingatia vyakula vya asili, vyote hivyo ni sawa lakini Havikuongezei maisha marefu na ya Kheri duniani. Kumbuka kosa la kwanza lilofanya maisha ya wanadamu kupunguzwa kutoka miaka 1000 mpaka miaka 120 ilikuwa sio kutokuzingatia mlo kamili bali ni kwasababu ya kutokushika maagizo ya Mungu. Hivyo kama unalegalega na njia zako hazimpendezi Mungu badilika sasa ishi maisha ya kumpendeza Mungu kama Mkristo na zingatia pia kuwaheshimu wazazi Mungu aliokupa hapa duniani. Kwa kufanya hivyo Mungu atakuongezea maisha marefu na sio tu marefu bali pia na ya Kheri.


Vivyo hivyo ili kupata afya, ni vizuri ukafahamu njia ya Mungu ni ipi aliyoiweka yeye, Mithali 3:7 Usiwe mwenye hekima machoni pako; MCHE Bwana, ukajiepushe na uovu. Itakuwa AFYA MWILINI PAKO, Na mafuta mifupani mwako. " Ukisoma pia. Kutoka 15:26 "akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye. ".


Mara nyingi tunajiuliza kwanini kila kukicha magonjwa yanatuandama, nimezunguka kutoka kwa mtumishi huyu hadi mtumishi huyu, nimeombewa na kila mtu lakini hali inazidi kuwa mbaya unaona kama vile Mungu hayupo pamoja nawe, Lakini hujui kuwa wewe ndio umemwacha Mungu na shetani ndipo anapopata nafasi ya kukutesa kwasababu umeiacha njia ambayo Mungu aliiweka tangu mwanzo tuiendee na kuwa na afya zetu, huwezi ukawa mwasherati, mlevi, mvutaji sigara, msengenyaji, fisadi, mwizi, au mtukanaji n.k halafu hayo yote yasikupate. Kumbuka biblia inasema KUMCHA BWANA ni KUCHUKIA UOVU (Mithali 8:13). Jifungue mwenyewe kwanza katika hivyo vifungo vya uovu kwa kuacha kutenda dhambi, kumpoke Yesu Kristo, ndipo Bwana akulinde na maradhi kwasababu yeye anasema "ndiye Bwana akuponyaye", Kwahiyo hauhitaji nguvu nyingi kujinyima kula vyakula vya aina fulani, au kuzunguka kwenda kuombewa na watumishi wakati wewe mwenyewe unaweza kujifungua..KUMCHA BWANA ndio msingi wa kila kitu!!

Vivyo hivyo ili kupata mafanikio ya kimwili ipo njia ambayo Mungu alishaiweka ukiikosa hiyo utaona kama vile Mungu kakuacha kwasababu Mungu siku zote anatembea katika kanuni zake na si katika kanuni zetu sisi tunazotaka yeye azitembelee. Tumekuwa tukimkumbusha Mungu kila siku tukisema "Mungu umesema; Utatubariki mijini, utatubariki mashambani, utatubariki tuingiapo utatubariki tutokapo, utatubariki kapu letu, na vyombo vyetu vya kukandia unga, atatufanya kuwa vichwa wala si mikia, atatubariki mifugo yetu na uzao wa matumbo yetu n.k."


Ni wimbo ambao tumekuwa tukiuimba pengine pasipo kuona matokeo yoyote, na kufanya watu waishie kuzunguka kutoka kwa nabii huyu hadi nabii huyu,.Nataka nikuambie tu ndugu yangu mtu anayekutamkia kwamba "pokea baraka mwaka huu", ki-uhalisia ni kwamba huyo mtu hajakubariki bali "AMEKUTAKIA TU KHERI"..kama vile tu mtu anavyokutakia Kheri ya mwaka mpya, au kheri ya maisha marefu.


BARAKA HALISI INATOKA WAPI?

Tumesahau Neno moja katika hiyo mistari ambalo ni la muhimu sana nalo ni "IKIWA".."IKIWA UTAKAPOSIKIA SAUTI YA BWANA MUNGU WAKO"

Kumbukumbu 28:1 inasema; ITAKUWA UTAKAPOSIKIA SAUTI YA BWANA, MUNGU WAKO, KWA BIDII, KUTUNZA KUYAFANYA MAAGIZO YAKE YOTE NIKUAGIZAYO LEO, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;
2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.
3 Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.
4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.
5 Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.
6 Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo...."

Kwahiyo unaona hapo NJIA Mungu aliyoiweka ili kupokea hizo baraka, ni KWA KUYATUNZA NA KUYAFANYA MAAGIZO YOTE YA MUNGU, ambayo ki uhalisia ni wachache wanafanya hivyo, utakuta mtu ni fisadi au mla rushwa bado anakwenda mbele za Mungu na kumwomba baraka, utakuta mtu anaishi maisha ya anasa halafu anamfuata mtumishi amwombee abarikiwe, utakuta mtu hata hana mpango na Mungu na yeye pia anakimbilia kwenda kununua mafuta ya upako, hiyo ni sawa na uganga wa kienyeji tu, ni vyema ukaacha na kutubu. Njia pekee Mungu aliyoiweka ni KUMCHA yeye na kuyashika aliyokuagiza, kwa kuzingatia hivyo hautahitaji kwenda kwa mtumishi yoyote akuombee, au kukesha kuomba, au kutumia mafuta au chumvi vinavyoitwa vya upako, ili kufanya mambo yabadilike, Mungu mwenyewe atakutengenezea njia, kwa wakati wake, kwasababu anasema yeye mwenyewe anajua kuwa tunahaja na hayo yote.


Na ndio maana biblia inasema..Mathayo 6:32-33 "...kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa." Usihangaike huku na huko, hakutakusaidia chochote MCHE MUNGU.

Vivyo hivyo ukitaka CHEO (ukubwa mahali popote), njia ipo nayo ni "kuwa mdogo kuliko wote" jinyenyekeze kwa maana ajishushaye atakwezwa na ajikwezaye atashushwa,usitumie njia za kujipendekeza kwa watu ili upate kibali wewe jishushe kuwa mnyenyekevu hakuna mtu yeyote asiyependa mtu mnyenyekevu..hizo ndio NJIA zilizowekwa na Mungu, ukitaka kupokea vitu kutoka kwa watu, Bwana Yesu alisema.. katika Luka 6:38 "Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. " Hata siku zote ili bomba litoe maji ya kujaza vyombo vingi ni sharti lifunguliwe, lakini likifungwa litabakia na maji yake ya ndani tu..vivyo hivyo ukitaka upokee "favour" inakupasa utoe kwa wengine na kwa Mungu.

Ukitaka furaha, amani na watu, mche Bwana kwa kuzishika amri zake,Mithali 16:7 " Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye."

Sulemani mtu aliyekuwa na mafanikio na mwenye utajiri mwingi kuliko watu wote waliomtangalia na waliokuja baada yake, japo katika ufahari wake wote alihitimisha na kusema..Mhubiri 12:13-14" Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; MCHE MUNGU, NAWE UZISHIKE AMRI ZAKE, Maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu. Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya. "

Sisi ni akina nani tusimche Bwana?.

Ubarikiwe sana na Bwana wetu YESU KRISTO.

Tuesday, January 30, 2018

FUVU LA KICHWA.


Luka 23:32 "Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye.
33 Na walipofika mahali paitwapo FUVU LA KICHWA, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. "

Zamani zile tunafahamu utawala wa kikatili wa kirumi, uliua watu wengi kwa kuwatundika katika miti na misalaba, ni utawala uliokuwa umesambaa karibia ulimwenguni kote, na Israeli pia, Lakini tunaona wakati wa kumsulibisha Bwana wetu Yesu Kristo walimchukua na kumpeleka mahali panapoitwa FUVU LA KICHWA, Lakini swali la kujiuliza ni kwanini asipelekwe mahali pengine kama vile bethania, au Emau, badala yake walimpeleka mahali panapoitwa FUVU LA KICHWA.? Ipo sababu.

Vitu hivi vinafunua mambo ya rohoni, kama vile tu biblia inasema wana wa Israeli ule mwamba waliounywea maji kule jangwani, haukuwa tu ni mwamba wa kawaida, bali katika roho ulikuwa unamfunua Kristo, (1Wakorintho 10:4) Kadhalika na katika tukio hili.

Ni kiashirio cha wazi  kuwa kabla Kristo hajapandishwa msalabani tayari walikuwa wameshamsulibisha katika VICHWA vyao wenyewe, Kitendo cha kumpandisha msalabani ni matokeo tu ya kitu kilichokuwa kimeshatendeka  ndani , walishamkataa tangu siku nyingi na ndio maana biblia inasema Yohana 3:19 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. " unaona hapo NURU ilikuja lakini waliipinga tangu mwanzo. Bwana alikataliwa tangu kuzaliwa kwake kama tunavyosoma katika maandiko habari hizo zilimfadhahisha Herode pamoja na Israeli yote. Alipingwa na viongozi wa dini pamoja na jamaa zake wakaribu,wengine walimsaliti, wengine walikuwa wanamjaribu kwa maneno ili wapate jambo la kumshitaki, sasa huko ndiko kumsulibisha Kristo katika vichwa vyao.

Isaya 53:3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.

Ni rahisi kusema mimi ningekuwepo  kipindi kile cha Bwana Yesu kamwe nisingeshirikiana nao kumsulibisha Bwana, Lakini ukweli ni kwamba Kristo anasulibishwa mpaka leo, na jambo hili linaanzia katika VICHWA VYA WATU.

huwezi kusema moja kwa moja unamsulibisha Kristo lakini ulishamsulibisha Katika KICHWA CHAKO, kwa kulikataa Neno La Mungu lilipokuwa linalia ndani ya moyo wako kwa mara ya kwanza na ukakataa kutubu, Ulipenda Giza kuliko Nuru.
Unakuwa ni mtu wa kutoa  maneno ya kijeli na mizaha juu ya jina la Bwana( maneno kama " eti unakuja umekuwa Yesu?), ni kumsulibisha Kristo, unapoambiwa ukweli na moyoni mwako unajua kabisa ni kweli lakini unapinga kama walivyofanya wale mafarisayo na masadukayo ni sawa na kumsulibisha Kristo huna tofauti na watu wa kipindi kile, n.k.

Huu ni wakati wa kufungua moyo wako, Kristo ayafanye maisha yako kuwa mapya, badilisha fikra zilizo ndani ya fuvu la kichwa chako, kwa kulitii NENO la Mungu uokolewe, ukabatizwe katika ubatizo sahihi utakaokuwezesha kuwa na uhakika wa kuondolewa dhambi zake, nao si mwingine zaidi ya kuzamishwa kwenye maji tele katika Jina la YESU KRISTO, na kuanzia hapo uishie maisha ya yakumpendeza yeye, ili jambo lile lisikutokee kama lilivyowatokea wale watu wa wakati ule.
 

Wanaomsulibisha Kristo mara ya pili, biblia inasema ni vigumu kufanywa upya tena, kwasababu WANAMFEDHEHI Bwana kwa DHAMIRA ZAO, (Waebrania 6:5)..Hivyo tukiyajua hayo tumwombe Mungu tusifike huko, tuwe tayari kugeuka, kwa kumaanisha kutubu dhambi zetu,  ili Bwana atuponye.

Ubarikiwe

Monday, January 29, 2018

ANGALIA JINSI USIKIAVYO:

Bwana alituweka duniani kila mmoja wetu tumzalie matunda, na kuna matunda ya aina mbili

1) Matunda ya Haki: (wafilipi 1:11, wagalatia 5:22) nayo ni upendo, furaha, utu wema, kiasi, uvumilivu, upole, amani, fadhili, n.k. ambayo kwa ujumla tunaita ni UTAKATIFU.

2) Matunda ya kazi ya Mungu: Ambayo ni kuwavuta watu wa Kristo, kwa njia mbalimbali za kuhubiri, kufundisha, na kuhudumu, nk.


Biblia mahali pengine imefananisha matunda haya yote kama "TALANTA". Tukisoma mfano Bwana Yesu aliowapa wanafunzi wake kwenye
 Mathayo 25:14-30"
14 Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.
15 Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.
16 Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano.
17 Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida.
18 Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.
19 Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.
20 Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.
21 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
22 Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.
23 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
24 Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;
25 basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.
26 Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;
27 basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.
28 Basi, mnyang'anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.
29 KWA MAANA KILA MWENYE KITU ATAPEWA, NA KUONGEZEWA TELE; LAKINI ASIYE NA KITU, HATA KILE ALICHO NACHO ATANYANG'ANYWA.
30 Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno."


Mfano huu ni dhahiri unajulikana kuwa moja kwa moja unalenga katika kuifanya kazi ya Mungu kwa karama mtu aliyopewa, kama amepewa karama ya aulimu, au amepewa karama ya kichungaji, au karama ya kinabii au uinjilisti au nyingine yoyote ni jukumu lake kuitumia kuwavuta watu kwa Kristo ili siku ile Bwana atakapokuja na kumuuliza mtu huyo umemzalishia vingapi aweze kumpa vya kwake na vya ziada.


Lakini pia tafsiri kuu ya mfano huu, TALANTA haimaanishi karama peke yake, bali pia hata KILE MTU ANACHOSIKIA ni talanta. Unapohubiriwa NENO la Mungu hiyo ni talanta imepandwa moyoni mwako na Bwana ataihitaji ya kwake pamoja na ya ziada katika siku ile ya hukumu kwa yote uliyoyasikia.

Kama ukisoma kwa makini mstari wa 29 unasema "Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa."

Mstari huu huu umejieleza zaidi kwenye 
Mathayo 13:2-13" unasema..."Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani.
3 Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.
4 Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;
5 nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina;
6 na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka.
7 Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga;
8 nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.
9 Mwenye masikio na asikie.
10 Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano?
11 Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.
12 KWA MAANA YE YOTE MWENYE KITU ATAPEWA, NAYE ATAZIDISHIWA TELE; LAKINI YE YOTE ASIYE NA KITU, HATA KILE ALICHONACHO ATANYANG'ANYWA.
13 Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. "

Bwana Yesu mara nyingi alipokuwa akiwafundisha makutano, hakuzungumza nao moja kwa moja, kwa kufafanua mambo, bali kama kwa njia ya mafumbo, hivyo wengi walikuwa wakitoka na maswali mengi kichwani, au wengine hawakumuelewa kabisa, na wengine walimwona kama vile mtunga hadhithi tu zisizo na maana, lakini alifanya hivyo kwa makusudi ili ajue ni wangapi walio tayari kujifunza , na ndio maana tunaona baada ya kumaliza ile mifano ni kikundi cha watu wachache tu(wanafunzi wake) kati ya maelfu kilichoenda kumuuliza tafsiri ya ile mifano yote aliyokuwa anazungumza, na ndipo hapo anapowafunua macho yao na kuwaelewesha tafsiri ya mifano ile na kuponyeka roho zao, bali wale wengine waliosalia ambao hawakutaka kujifunza zaidi kwao ilikuwa ni kama hadhithi tu. Na mahali popote Bwana alipokuwa akifundisha kwenye makutano mengi hiyo ndiyo ilikuwa desturi yake. Na ndivyo anavyofanya hata sasa.

Jambo la kujifunza ni kwamba hawa wanafunzi walipopewa talanta za Neno la Mungu mikononi mwao kwa ile mifano, hawakuenda kuichimbia chini(yaani kuridhika na mifano ile), badala yake walikwenda kuifanyia biashara ili wanufaike, pale walipokwenda kumuuliza Bwana tafsiri ya mifano ile. Na hao ndio pekee waliozidi kuimarika na kukua kiroho siku baada ya siku kwa kuzijua siri za Mungu, wakifananishwa na mbegu zile zilizotupwa katika udongo mzuri, zilizozaa moja 30, nyingine 60 na nyingine 100, lakini wale wengine walifananishwa na zile mbegu zilizoangukia njiani, na kwenye miamba na kwenye miiba ndege walipopita wakazila, jua lilipokuwa kali zikaungua, na mwamba ulipokuwa mgumu zikasinyaa kwa kukosa mizizi hawakuzalisha chochote.

Hawa ni mfano ya watu wasiotumia talanta zao vizuri (yaani kusikia NENO la Mungu), wale wa kwenye njia ndio wale wanaosikia Neno la Mungu kila siku likihubiriwa lakini wanalizembea kulitendea kazi au pengine hawajalielewa vizuri, kwao limekuja tu kama fumbo badala waendelee kutafuta kujua zaidi wao wanaliacha , maana biblia inasema "kila atafutaye ataona" kama ulivyo mfano wa wale makutano ambao mwisho wa siku shetani anapata nafasi ya kulichukua mioyoni mwao na kulisahau, ni mara ngapi umesikia ukihubiriwa Neno la Mungu ubadilike lakini haubadiliki?, umefundishwa usivae vimini, hata kama haujalielewa au linakuchanganya je! ulishawahi kukaa na kumuuliza Mungu una maana gani kukataza mwanamke kuvaa suruali au kuweka make-up na kuvaa vimini??. Hiyo TALANTA uliyopewa na Mungu kwa kuhubiriwa umeitumiaje??..Ni dhahiri kuwa umeifukia chini na katika siku ile ya Hukumu utatoa hesabu yake.

Umehubiriwa mara nyingi uache uasherati, ulevi, usengenyaji, ushirikina, lakini huachi ulishawahi kukaa na kwenda kukufanyia kazi hicho ulichoambiwa? kumbuka hiyo ni talanta uliyopewa kwa kuhubiriwa Injili itatakwa na ya ziada siku ile ya hukumu.

Umefundishwa utukanaji, wizi, uvutaji sigara, utoaji mimba,usagaji, kutazama pornoghaphy, musterbation ni dhambi, talanta hizi zote zilipandwa ndani ya moyo wako kwa mafundisho mbalimbali uliyoyasikia ya Neno la Mungu, pengine mengi yalikuacha njia panda lakini je! ulishawahi kutenga muda na kwenda kumuuliza Mungu au kutaka kujua zaidi kama ni kweli au sio kweli, lakini umepuuzia kama yale makutano yalivyofanya. TALANTA hiyo itatakwa siku ile ya Hukumu.

Umesikia Neno la Mungu limepiga kelele masikioni mwako kwamba kuabudu sanamu, kusali rozari, mafundisho ya kwenda toharani na ibada za wafu ni mafundisho potofu yanayawapeleka mamilioni kuzimu, pengine uliposikia mara ya kwanza kwako ilikuwa kama ni kitendawili lakini je! ulishawahi kutenga Muda na kumuuliza Mungu je! mambo hayo ni kweli kuliko kupuuzia au kubisha, Kumbuka hiyo ni TALANTA ambayo Bwana alikupa moyoni mwako na usipoizalisha utaulizwa katika ile siku ya Hukumu.


Lakini kama ungependa kujifunza na kuyatendea kazi yale unayohubiriwa au kufundishwa..Bwana anasema: "KWA MAANA YE YOTE MWENYE KITU ATAPEWA, NAYE ATAZIDISHIWA TELE;". Hivyo ungejikuta hata yale uliyokuwa huyajui Bwana anakuongezea na mengine mengi, Neno la Mungu linajifunua kwako , na kujikuta unaimarika kiroho siku baada ya siku.

Kwahiyo cha muhimu sana ni kuzingatia "kile unachokisikia" na kukifanyia kazi kwa bidii adui asije akakichukua hata hicho kidogo Mungu alichokupa neema ya kukisikia kikapotea moyoni mwako. Kwasababu alisema...

Marko 4:24 ... ANGALIENI MSIKIALO; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.
25 Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. "
Maombi yangu ni uanze kukitendea kazi kile ulichokisikia tangu zamani, ili atakapokuja aone matunda ya kusikia kwako Neno lake.

Mungu akubariki.

Friday, January 26, 2018

KAMA MWIZI USIKU WA MANANE:


Kama tunavyofahamu wakati wa usiku kabla hatujalala, huwa ni lazima tufunge milango yetu yote, kwa makufuli na makomeo, na hii sio kwasababu tunapenda kujifungia tu hapana! bali ni kujiweka katika hali ya usalama dhidi ya WEZI usiku, Kwasababu hatujui ni wakati gani wataingia na kuleta madhara. Hii ni desturi kwa kila mtu,hakuna mtu asiyefahamu kuwa anapaswa kufunga milango yake wakati wa usiku.

Lakini pamoja na hayo kufunga mlango tu na kwenda kulala haitoshi, kwasababu mwizi anajua kabisa akienda atakutana na changamoto ya milango kufungwa hivyo atakuwa amekwisha jipanga kwa njia mbadala ili kuhakikisha kuwa zoezi lake la kuiba linafanikiwa kikamilifu, hivyo ni dhahiri kuwa atakuwa na vifaa husika vya kuvunjia nyumba.

Kwahiyo ili mwenye nyumba aweze kunusuru mali zake au roho yake sio tu KUBANA MILANGO yake bali anapaswa pia AKESHE, Kwasababu mwizi hawezi kuharibu kama mwenye nyumba yupo macho. Hivyo dawa pekee ya kudhibiti wizi usiku ni kubana milango pamoja na KUKESHA.
Ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Bwana Yesu Kristo,akifananisha kuja kwake na kama ujio wa mwizi wakati wa usiku alisema ...

Mathayo 24:40-44" Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;
41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.
43 Lakini fahamuni neno hili; KAMA MWENYE NYUMBA ANGALIIJUA ILE ZAMU MWIVI ATAKAYOKUJA, ANGALIKESHA, wala asingaliiacha nyumba yake KUVUNJWA. "
44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa damu yuaja.


Tukisoma pia katika Marko 13:32 Bwana Yesu alisema maneno haya: Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.
33 Angalieni, KESHENI, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.
34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.
35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, KWAMBA NI JIONI, AU KWAMBA NI USIKU WA MANANE,au AWIKAPO JIMBI, au ASUBUHI;
36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.
37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, KESHENI. "

Kumbuka hapo Bwana Yesu hakusema "fungeni milango" bali alisema "kesheni" kwasababu inajulikana ni wajibu wa kila mtu kufunga milango yake, na kufunga milango ina maana kujiona umeokoka lakini maisha yako hayaendani na ukristo,umebatizwa na unaenda kanisani lakini umelala katika roho(vuguvugu), nje milango imefungwa lakini ndani umelala kwasababu hiyo basi mwizi atakapokuja hautajua lolote. Mkristo aliyeridhika na dhehebu lake au mapokeo yake lakini hazingatii mambo ya muhimu yanayohusiana na wokovu wake na maisha yake ya umilele ni sawa na mtu aliyejifungia na kulala usingizi.

Dunia sasa hivi ipo katika GIZA NENE SANA ikiashiria kwamba huu ni wakati wa USIKU na ndio wakati uliokaribia wa BWANA kurudi tena, kuongezeka kwa maovu ulimwenguni kama vile anasa,ulevi,uasherati uliokithiri hususani katika ulimwengu huu wa sasa wa utandawazi,mauaji,uchawi,rushwa,dhuluma, kupenda ulimwengu zaidi ya Mungu,n.k. vinawafanya watu wazidi KULALA usingizi wa mauti, na jinsi giza linavyozidi kuongezeka ndivyo wakristo nao wanavyozidi kushawishika kulala.

Sasa katikati ya kilele hichi cha maovu hapo ndipo Kristo atakaporudi, alisema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu watu walikuwa wakila na kunywa(ikiashiria kufanya anasa),walikuwa wakipanda na kujenga, hata siku ile ikawajilia kama ghafla, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adamu.

1Thesalonike 5:1 Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.
2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.
4 Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.
5 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.
6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.
7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.
8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu. "
Bwana Yesu pia alisema..
Ufunuo 16:15 "(Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.) ".

MAANA YA KUKESHA NI NINI?

Kukesha kunakozungumziwa ni KUKESHA KATIKA ROHO, kutokulala katika roho, kudumu katika utakatifu,huku matunda ya roho yakijidhihirisha upole,kiasi,upendo,uvumilivu,n.k pamoja na kuishi maisha ya kama mtu anayemngojea Bwana wake, kama msafiri duniani, asiyefanana na watu wa ulimwengu huu waliousingizini, huku macho yake yakitazama mambo ya mbinguni yanayokuja,

Utajisikiaje siku hiyo utakapoona wenzako wamekwenda kwenye unyakuo na wewe umebaki? ni uchungu usioneneka, mara nyingine Mungu anawaotesha watu ndoto kwamba unyakuo umepita na wenyewe wamebaki, hapo ni Mungu anajaribu kuwakumbusha watu kwamba maisha yao hayajakidhi vigezo vya kwenda mbinguni.Huu ni wakati wa kuamka usingizini biblia inasema..katika waefeso 5:14 "Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza."

Amka ndugu utoke katika usingizi wa wafu wa ulimwengu huu, uasherati ni usingizi,kiburi cha uzima ni usingizi,ulevi,sigara,anasa,fashion,ushirikina,usengenyaji,rushwa,ulawiti,utoaji mimba,wizi,utukanaji vyote hivi ni usingizi wa kiroho, na kumbuka siku Kristo atakapokuja kulichukua kanisa lake hawa hawatajua lolote badala yake watabaki hapa wakingojea ile SIKU KUU YA BWANA inayowaka kama tanuru ndivyo biblia inavyosema,

2 Petro 3:10 "Lakini siku ya Bwana ITAKUJA KAMA MWIVI; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.
11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo,IMEWAPASA NINYI KUWA WATU WA TABIA GANI KATIKA MWENENDO WENU MTAKATIFU NA UTAUWA,
12 mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? ".

Kwa kuwa sisi sote hatujui ni saa gani Bwana atakayokuja , ni wajibu wa kila mtu aliye mkristo kukesha kwa kuishi maisha ya uangalifu katika giza hili nene lililopo dunian sasa.

Mungu akubariki.

Thursday, January 25, 2018

BEI YA UFALME WA MBINGUNI:


Kuna gharama kubwa sana katika kuupata ufalme wa mbinguni kama Bwana Yesu alivyotangulia kusema kwenye Mathayo 11:12 "Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. " Hii ikiwa na maana kuwa ufalme wa mbinguni ni kitu kinachogombaniwa kwa nguvu na watakaokipata ni wachache. Na kumbuka NGUVU zinazozungumziwa hapo sio nguvu za kimwilini, Tukisoma..

Mathayo 13:44-46 "
44 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda AKAUZA ALIVYO NAVYO VYOTE, akalinunua shamba lile.
45 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;
46 naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda AKAUZA ALIVYO NAVYO VYOTE, akainunua. "Bwana Yesu alifananisha ufalme wa mbinguni na maisha yetu tunayoishi kila siku, kama tukisoma hiyo mifano hapo juu tunaona kuna mfanya biashara aliyekuwa anatafuta lulu nzuri ya thamani kubwa, na alipoiona akaipenda sana, pengine hakuwa na fedha za kutosha, kuinunua kutokana na gharama ya LULU hiyo ilivyokuwa na thamani kubwa, lakini kwasababu ni mfanya biashara, alitafakari sana, kwamba japo inauzwa kwa thamani nyingi, lakini akiipata ataweza kuiuza mahali pengine kwa gharama kubwa zaidi, Hivyo atarudisha fedha aliyoinunulia pamoja na faida nyingi juu yake. Kwasababu hiyo basi ilimpasa aende kuuza kila kitu alichokuwa nacho pengine hata nyumba yake, na miradi yake yote, ilimradi tu afikie kiwango kile cha pesa akainunue lulu ile yenye thamani kubwa.

Labda pengine alivyodhamiria kufanya hivyo, alionekana mwendawazimu mbele za watu kuuza mali alizozitaabikia kwa muda mrefu, lakini kwasababu ni mfanya biashara alifahamu ni kitu gani anafanya.

Vivyo hivyo na yule mwingine aliyeona hazina iliyositirika katika shamba na kwenda kuuza vyote alivyonavyo hakuwa mwendawazimu, pengine aliiona ALMASI imejichimbia katika kiwanja cha jirani yake, hivyo ili aweze kuipata ni sharti kile kiwanja kiwe chake, ili awe na ruksa ya kuifukua, sasa kwa ujanja, akaenda kumshawishi mwenye kiwanja amuuzie hata kwa bei mara 10 ya bei halisi ya kiwanja kile ili aweze kukipata kwa haraka na bila ya usumbufu , kwa kuwa mtu huyo anajua ni kitu gani anachokifanya, akaamua akauze kila kitu alichokuwa nacho, pengine mifugo yake, au majumba yake, au magari yake, na kama fedha isingetosha angeweza hata kwenda kukopa ili atimize lengo lake la kupata kiwanja kile.

Lakini kwa namna ya kawaida watu wangemuona kama amelogwa, au amerukwa na akili, kugharimikia kitu kisichokuwa na faida, lakini yeye hakuona tu kiwanja, bali aliuona UTAJIRI mkubwa zaidi ya kile kiwanja.

Mifano hiyo hiyo inatufundisha sisi kama wanadamu, HATUTAWEZA KUUPATA UFALME WA MBINGUNI, KAMA BADO HATUJAJUA THAMANI YAKE. Kumbuka yule mfanyabiasha hakuona tu lulu bali aliona thamani kubwa iliyopo ndani ya lulu, ndiyo ikamgharimu kuuza kila kitu, vivyo hivyo na yule aliyenunua shamba, hakuona tu shamba, bali aliona thamani ya kitu kilichokuwa kimejificha ndani ya lile shamba na ndipo gharama za kukipata hicho kitu zinajitokeza.

Na katika ufalme wa mbinguni, usiuone tu ufalme wa mbinguni halafu basi, bali tazama thamani na utajiri ulioko ndani ya huo ufalme, ukishalifahamu hilo au kupata ufunuo huo utakuwa na nguvu za kuchukuliana na gharama zozote utakazokumbana nazo kwa furaha zote.

Tukirudi kwa kijana mmoja aliyeitwa Musa, tunaona alizaliwa katika makasri ya kifalme ya FARAO, aliyekuwa msomi, na mtawala mwenye cheo, pamoja na mali nyingi, lakini ilifika wakati neema za Mungu ilifunguliwa machoni pake,na kuuona uzuri ulio katika ufalme wa mbinguni, hivyo kwa furaha yote aliamua kuuza kila kitu alichokuwa nacho ili aupate ,alidharau elimu yake ya kipagani, alidharau cheo chake kama mfalme mrithi, alidharau anasa na fahari alizokuwa anazipata katika jumba la kifalme, ili tu aupate ufalme usioharibika wa mbinguni..
 
 Mtume Paulo aliandika katika.Wabrania 11:24 Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;
25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;
26 AKIHESABU YA KUWA KUSHUTUMIWA KWAKE KRISTO NI UTAJIRI MKUU KULIKO HAZINA ZA MISRI; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.
27 Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana. "

Tunaona hapo Musa alihesabu kushutumiwa kwake Kristo ni Utajiri mkuu kuliko hazina zote za Misri, ilimpasa AUZE baadhi ya mambo, ili aweze KUUNUNUA ufalme wa mbinguni, aliuona utajiri mkubwa huko mbeleni kuliko hazina zote za Misri, Ilimpasa auze umaarufu wake, ilimpasa auze anasa zake, ilimpasa auze ujana wake, ilimpasa auze kiburi chake, ilimpasa auze fashion zake, ilimpasa auze majigambo yake na ujuzi wake, ilimpasa auze dhuluma yake, ili aweze kufikia viwango vya kuununua ule UFALME WA MBINGUNI.

Vivyo hivyo na mtume Paulo mwenyewe aliingia gharama hizo hizo..ukisoma Wafilipi 3:7-8 inasema.." Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama "MAVI" ili nipate Kristo; "
 
Paulo ambaye alikuwa ni msomi mwenye cheo na kiburi alihesabu mambo yote kuwa kama mavi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni, kumbuka kilichomfanya achukue uamuzi huo sio tu kwasababu ni neno "ufalme wa mbinguni" , hapana bali ni UTAJIRI aliouna angeupata katika huo ufalme.Na kwa kufunuliwa na Roho Paulo alifika wakati na kusema
 warumi 8:
18 Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama UTUKUFU ULE UTAKAOFUNULIWA KWETU.
19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.

Hivyo ndugu fungua macho yako uone thamani na utajiri mkubwa ulio katika huo ufalme, ndipo utakapoona sababu ya kuacha kila kitu kisichompendeza Mungu kwa furaha zote na kumwandamia Mungu kwa hali zote,. Kumbuka thawabu za UFALME WA MBINGUNI, zitakazokuja huko ni mambo mazuri ambayo biblia inasema katika..1Wakoritho 2:9 "lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. ", pia usisahau, kutakuwa na wafalme na wenye mamlaka kubwa, pamoja na makuhani wa Mungu hawa watakaa pamoja na Kristo na kuhudumu pamoja naye, na huko watakuwepo pia watu wa kawaida tu, thawabu zitatofautiana sana, na ni milele, ikiwa na maana kuwa kama wewe ni mdogo kule utabaki hivyo hivyo milele, na kama wewe ni mfalme kule utadumu mfalme milele, na Bwana wetu YESU KRISTO akiwa kama MFALME WA WAFALME. 
Jina la BWANA YESU LIBARIKIWE.

Kuna wakati mitume walimuuliza Bwana..Mathayo 19:27 "Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. "

Hivyo wale watakaoketi karibu na Bwana ni wale tu, walioona thamani na kuingia gharama za kuununua ufalme wa mbinguni, je! ufalme huu unathamani gani kwako? , wewe mwanamke hauwezi ukaacha fashion na kuvaa hivyo vimini na suruali, kwasababu hauoni faida yoyote ya kuacha kufanya hivyo, mwanamume hauwezi kuacha pombe na sigara kwasababu kwako ni sawasawa ni biashara isiyo na faida, hauwezi kuacha uasherati, wizi kwasababu faida ya ile LULU(UFALME WA MBINGUNI) haijafunuliwa machoni pako. Laiti ungeifahamu thamani ya LULU usingefanya hivyo.

Lakini kumbuka wana wa Mungu, sio wajinga kuwaona wanauza mambo ya ulimwengu huu sasa ivi ili wanunue mambo ya ulimwengu unaokuja, ni kwasababu wanaona mbele, na kujipenda na wanapenda maisha ndio maana wanatafuta maisha ya milele yanayodumu, na wanapenda furaha zaidi hata ya wewe unayejiona unajistarehesha katika anasa za ulimwengu huu.

Kanisa tunaloishi ndilo la mwisho linalojulikana kama LAODIKIA kulingana na Kalenda ya Mungu, na ujumbe wetu tuliopewa umeandikwa katika kitabu cha Ufunuo 3:14 unasomeka hivi..
 
"Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, UNUNUE KWANGU DHAHABU ILIYOSAFISHWA KWA MOTO, UPATE KUWA TAJIRI, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona."
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. "

Bwana ametupa shauri tukanunue dhahabu kwake tupate kuwa matajiri, kumbuka ili KUNUNUA lazima TUUZE yote maovu tulionayo ili tuweze kukidhi viwango vya kuupata ufalme wa mbinguni. Maombi yangu ni Bwana akupe neema ya kuona THAMANI YA UFALME WA MBINGUNI kwasababu UFALME WA MBINGUNI unapatikana kwa nguvu, na wenye nguvu ndio wanaouteka.

Mungu akubariki.

Monday, January 22, 2018

MAELEZO JUU YA UFUNUO 22:

Bwana wetu YESU KRISTO apewe sifa, Karibu katika mfululizo wa mwendelezo wa kitabu cha ufunuo leo tukiwa katika sura ya 22 na ya mwisho, Tusome..

    Mlango 22

1 Kisha akanionyesha MTO WA MAJI YA UZIMA, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo,
2 katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo MTI WA UZIMA, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.
3 Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia;
4 nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao.
5 Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele.
6 Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi.

Tukirejea kidogo kwenye historia ya Edeni, tunafahamu kuwa katikati ya Bustani, kulikuwa na ule mti wa uzima, na pia kulikuwa na mto kando ya mti wa uzima ambao ulikuwa unaitilia bustani yote maji, na kisha baada ya hapo uligawanyika na kuwa vichwa 4 (Mwanzo 2),ambavyo vilikwenda kuimwagilia dunia yote. Hivyo tunajua kuwa ule mti wa uzima, haukuwa mti kama mti wa matunda ya asili kama vile zabibu au peasi, la! bali ulikuwa ni mti wa rohoni, ambao matunda yake mtu akila anapata uzima wa milele, vyakula vya mwilini haviwezi kumpa mtu uzima wa milele, ukisoma kwa makini pale utaona Mungu alichepusha miti ya aina tatu: wa kwanza ulikuwa ni kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa(haya ndio matunda ya asili kama vile zabibu, embe, tufaa, n.k.)..aina ya pili ni mti wa uzima, na aina ya tatu ni mti wa ujuzi wa mema na mabaya,(Mwanzo 2:9), sasa hii miti aina 2 za mwisho ni miti ya rohoni.

Hivyo ule "mti wa uzima" ulikuwa ni NENO LA MUNGU ambao ndio baadaye ulikuja kuuvaa mwili ukaitwa YESU KRISTO, Sasa hili NENO LA MUNGU ndilo lililokuwa sheria na maagizo yote ambayo Adamu na Hawa walipewa na Mungu ili wakidumu katika hayo waishi milele. Hivyo pale Edeni Adamu na Hawa walikula matunda ya kawaida ya asili pamoja na maji ya asili kuwapa uzima miili yao, lakini pia walikula chakula cha rohoni (Matunda ya mti wa uzima), na maji ya rohoni, kuwapa uzima katika roho zao.

Lakini baada ya Adamu kuasi(kukaidi sheria ya MUNGU) tunaona njia ya mti wa uzima ilifungwa(kumbuka mti wenyewe haukuondolewa), ilipofika wakati uliokusudiwa ile njia ilifunguliwa tena, na tunajua huyu si mwingine zaidi ya BWANA wetu YESU KRISTO, Yohana 14:6"Yesu akamwambia, Mimi ndimi NJIA, na kweli, na UZIMA; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. "
Hivyo YESU KRISTO ni NENO/maagizo yale yale ya Mungu yaliyouvaa mwili.

Yeye ndiye ule mti wa uzima, na pia ndio anayetoa yale maji ya uzima.
 
 ukisoma Yohana 4:14"
13 Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena;
14 walakini ye yote atakayekunywa MAJI YALE nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia UZIMA WA MILELE. "
 
Sasa tukirudi juu, katika kitabu cha UFUNUO, tunasoma..
 
1 Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo,
2 katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo MTI WA UZIMA, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.

Hapa tunaona mto wa maji ya uzima unaonekana ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha mwanakondoo, kumbuka kama tulivyosoma katika sura iliyopita kwamba katika ile Yerusalemu mpya(ambayo ni BIBI-ARUSI) ndipo patakapokuwa makao ya Mungu(Ufunuo 21:3-4"Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, TAZAMA, MASKANI YA MUNGU NI PAMOJA NA WANADAMU, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. ), hivyo kiti chake cha enzi cha Mungu kitakuwepo huko, Na MTI wa UZIMA pamoja na mto wa maji wa uzima utatokea huko.

Kwahiyo bibi-arusi wa Kristo ambaye ndo ile Yerusalemu mpya na ndio watu wale wote watakaoshinda kutoka katika nyakati mbalimbali za Kanisa, Kama Bwana Yesu alivyoahidi katika Ufunuo 2:7 "Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu. "
Hii Ikiwa na maana kuwa wale watakaoshinda tu ndio watakula mema yote na kuzishiriki baraka zote ambazo Mungu alimwahidia YESU KRISTO atakapokuja kuumiliki ulimwengu, Yaani kwa lugha rahisi hawa watu watakatifu watafanana na YESU KRISTO mwenyewe. Kwa kuwa maisha yao walipokuwa hapa duniani yalifanana sana na mwana wa Mungu, hivyo watavuna walichokipanda kwa kula matunda yake.(yaani matunda ya mti wa uzima-YESU KRISTO mwenyewe.)

Lakini pia majani yatakuwa ni ya kuwaponya mataifa, kama tunavyofahamu mti wowote wa matunda, kwa mfano mti wa mwembe, huwezi ukala majani, ukasema, huu mwembe ni mzuri pengine yanaweza kukusaidia kama dawa ukiyatwanga, au kuongeza tu virutubisho fulani mwilini, lakini anayekula EMBE ndie anayejua uzuri wa mwembe, Vivyo hivyo kwa YESU KRISTO yeye kama mti wa UZIMA matunda yake watakayoyafurahia aliyopewa na BABA yake ni BIBI-ARUSI tu, wengine wote watamfahamu YESU katika sehemu ya matawi yake, kama biblia inavyosema yatakuwa ni kwa ajili ya kuwaponya tu, waendelee kuishi milele, lakini BIBI-ARUSI atakuwa na vyote.

Kama ilivyokuwa katika bustani ya Edeni mto ulitoka katika bustani na kusambaa duniani kote, vivyo hivyo na huu mto utokao katika kiti cha Enzi cha mwanakondoo katika ile YERUSALEMU MPYA, maji yake yatasambaa ulimwenguni kote kuwanywesha mataifa, ikiwa na maana kuwa yale maji ya uzima ambayo chanzo chake ni YESU KRISTO, kwa kupitia bibi-arusi wake, yataenea duniani kote kwa kufandisha mataifa kanuni zote za Mungu na utukufu wake.

Hivyo hawa watu ambao wanaaunda huu mji Yerusalemu mpya, watakuwa wametawanyika duniani kote . Unaona uzuri wa kuwa bibi-arusi wa Kristo? Kama dunia ya leo ni wasomi tu, ndio wanaotoa mwongozo wa mataifa ya dunia na kupewa kipaumbele, vivyo hivyo na kule ni BIBI-ARUSI tu, ndiye atakayetawala na KRISTO, na litakuwa ni kundi dogo, ni kwa wale watakaoshinda tu!

Tukiendelea..

Ufunuo 22:7-21 
"7 Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.
8 Nami Yohana ndimi niliyeyasikia na kuyaona mambo hayo. Na hapo nilipoyasikia na kuyaona nalianguka, ili nisujudu mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionyesha hayo.
9 Naye akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako, na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu.
10 Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.
11 Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.
12 Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.
13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.
14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.

Ndugu hapa Bwana anatoa angalizo, Hili neno "TAZAMA NAJA UPESI" ..na thawabu yangu ipo mkononi mwangu kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo, Linaonyesha kwamba wakati umeisha, je! wewe kazi yako ni ipi?, je! umeipima thawabu yako?, je! unastahili kuitwa bibi-arusi ?, je! kazi yako inakupeleka mbinguni au kuzimu?.
 
maana hapa anaendelea kusema...

15 Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.
16 Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung'aa ya asubuhi.
17 Na "ROHO na BIBI-ARUSI" wasema, NJOO! Naye asikiaye na aseme, NJOO! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.

Huu ni wakati wako wewe mkristo uliyevuguvugu, kimbilia kwenye chemchemi ya maji ya uzima unywe maji yaliyo hai na ufue nguo zako, ufanyike kiumbe kipya, wakati umeisha Bwana yu karibu kurudi. Mungu alishamtuma mjumbe wake kwa kanisa letu la mwisho linaloitwa LAODIKIA , mjumbe huyu anaitwa WILLIAM MARRION BRANHAM, na ujumbe unaotangaza kuja kwa pili kwa Kristo, Hivyo ni vyema kujua kalenda ya Mungu na ujumbe wa Mungu kwa wakati unaoishi. Kwa kulijua hilo utaishi maisha ya uangalifu tukijua kuwa BWANA wetu yu karibu kurudi kumchukua bibi-arusi wake safi asiye na hila wala mawaa.

Bwana anaendelea kusema...

18 Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
19 Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20 Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu.
21 Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.
Huu ni wakati wa kupiga mbio kweli kweli tuhakikishe hatukosi kuwa katika hiyo YERUSALEMU MPYA bibi-arusi wa Kristo ambayo Bwana anaendelea kuiandaa hadi sasa, na watakaokuwa huko ni kundi dogo, biblia inasema..

Waebrania Mlango 12:
1 Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu,
2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
3 Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. "

Amen.

Maran Atha!