"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, January 29, 2018

ANGALIA JINSI USIKIAVYO:

Bwana alituweka duniani kila mmoja wetu tumzalie matunda, na kuna matunda ya aina mbili

1) Matunda ya Haki: (wafilipi 1:11, wagalatia 5:22) nayo ni upendo, furaha, utu wema, kiasi, uvumilivu, upole, amani, fadhili, n.k. ambayo kwa ujumla tunaita ni UTAKATIFU.

2) Matunda ya kazi ya Mungu: Ambayo ni kuwavuta watu wa Kristo, kwa njia mbalimbali za kuhubiri, kufundisha, na kuhudumu, nk.


Biblia mahali pengine imefananisha matunda haya yote kama "TALANTA". Tukisoma mfano Bwana Yesu aliowapa wanafunzi wake kwenye
 Mathayo 25:14-30"
14 Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake.
15 Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.
16 Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano.
17 Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida.
18 Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.
19 Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao.
20 Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida.
21 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
22 Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.
23 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.
24 Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;
25 basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.
26 Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;
27 basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.
28 Basi, mnyang'anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.
29 KWA MAANA KILA MWENYE KITU ATAPEWA, NA KUONGEZEWA TELE; LAKINI ASIYE NA KITU, HATA KILE ALICHO NACHO ATANYANG'ANYWA.
30 Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno."


Mfano huu ni dhahiri unajulikana kuwa moja kwa moja unalenga katika kuifanya kazi ya Mungu kwa karama mtu aliyopewa, kama amepewa karama ya aulimu, au amepewa karama ya kichungaji, au karama ya kinabii au uinjilisti au nyingine yoyote ni jukumu lake kuitumia kuwavuta watu kwa Kristo ili siku ile Bwana atakapokuja na kumuuliza mtu huyo umemzalishia vingapi aweze kumpa vya kwake na vya ziada.


Lakini pia tafsiri kuu ya mfano huu, TALANTA haimaanishi karama peke yake, bali pia hata KILE MTU ANACHOSIKIA ni talanta. Unapohubiriwa NENO la Mungu hiyo ni talanta imepandwa moyoni mwako na Bwana ataihitaji ya kwake pamoja na ya ziada katika siku ile ya hukumu kwa yote uliyoyasikia.

Kama ukisoma kwa makini mstari wa 29 unasema "Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa."

Mstari huu huu umejieleza zaidi kwenye 
Mathayo 13:2-13" unasema..."Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani.
3 Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.
4 Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;
5 nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina;
6 na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka.
7 Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga;
8 nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.
9 Mwenye masikio na asikie.
10 Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano?
11 Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.
12 KWA MAANA YE YOTE MWENYE KITU ATAPEWA, NAYE ATAZIDISHIWA TELE; LAKINI YE YOTE ASIYE NA KITU, HATA KILE ALICHONACHO ATANYANG'ANYWA.
13 Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. "

Bwana Yesu mara nyingi alipokuwa akiwafundisha makutano, hakuzungumza nao moja kwa moja, kwa kufafanua mambo, bali kama kwa njia ya mafumbo, hivyo wengi walikuwa wakitoka na maswali mengi kichwani, au wengine hawakumuelewa kabisa, na wengine walimwona kama vile mtunga hadhithi tu zisizo na maana, lakini alifanya hivyo kwa makusudi ili ajue ni wangapi walio tayari kujifunza , na ndio maana tunaona baada ya kumaliza ile mifano ni kikundi cha watu wachache tu(wanafunzi wake) kati ya maelfu kilichoenda kumuuliza tafsiri ya ile mifano yote aliyokuwa anazungumza, na ndipo hapo anapowafunua macho yao na kuwaelewesha tafsiri ya mifano ile na kuponyeka roho zao, bali wale wengine waliosalia ambao hawakutaka kujifunza zaidi kwao ilikuwa ni kama hadhithi tu. Na mahali popote Bwana alipokuwa akifundisha kwenye makutano mengi hiyo ndiyo ilikuwa desturi yake. Na ndivyo anavyofanya hata sasa.

Jambo la kujifunza ni kwamba hawa wanafunzi walipopewa talanta za Neno la Mungu mikononi mwao kwa ile mifano, hawakuenda kuichimbia chini(yaani kuridhika na mifano ile), badala yake walikwenda kuifanyia biashara ili wanufaike, pale walipokwenda kumuuliza Bwana tafsiri ya mifano ile. Na hao ndio pekee waliozidi kuimarika na kukua kiroho siku baada ya siku kwa kuzijua siri za Mungu, wakifananishwa na mbegu zile zilizotupwa katika udongo mzuri, zilizozaa moja 30, nyingine 60 na nyingine 100, lakini wale wengine walifananishwa na zile mbegu zilizoangukia njiani, na kwenye miamba na kwenye miiba ndege walipopita wakazila, jua lilipokuwa kali zikaungua, na mwamba ulipokuwa mgumu zikasinyaa kwa kukosa mizizi hawakuzalisha chochote.

Hawa ni mfano ya watu wasiotumia talanta zao vizuri (yaani kusikia NENO la Mungu), wale wa kwenye njia ndio wale wanaosikia Neno la Mungu kila siku likihubiriwa lakini wanalizembea kulitendea kazi au pengine hawajalielewa vizuri, kwao limekuja tu kama fumbo badala waendelee kutafuta kujua zaidi wao wanaliacha , maana biblia inasema "kila atafutaye ataona" kama ulivyo mfano wa wale makutano ambao mwisho wa siku shetani anapata nafasi ya kulichukua mioyoni mwao na kulisahau, ni mara ngapi umesikia ukihubiriwa Neno la Mungu ubadilike lakini haubadiliki?, umefundishwa usivae vimini, hata kama haujalielewa au linakuchanganya je! ulishawahi kukaa na kumuuliza Mungu una maana gani kukataza mwanamke kuvaa suruali au kuweka make-up na kuvaa vimini??. Hiyo TALANTA uliyopewa na Mungu kwa kuhubiriwa umeitumiaje??..Ni dhahiri kuwa umeifukia chini na katika siku ile ya Hukumu utatoa hesabu yake.

Umehubiriwa mara nyingi uache uasherati, ulevi, usengenyaji, ushirikina, lakini huachi ulishawahi kukaa na kwenda kukufanyia kazi hicho ulichoambiwa? kumbuka hiyo ni talanta uliyopewa kwa kuhubiriwa Injili itatakwa na ya ziada siku ile ya hukumu.

Umefundishwa utukanaji, wizi, uvutaji sigara, utoaji mimba,usagaji, kutazama pornoghaphy, musterbation ni dhambi, talanta hizi zote zilipandwa ndani ya moyo wako kwa mafundisho mbalimbali uliyoyasikia ya Neno la Mungu, pengine mengi yalikuacha njia panda lakini je! ulishawahi kutenga muda na kwenda kumuuliza Mungu au kutaka kujua zaidi kama ni kweli au sio kweli, lakini umepuuzia kama yale makutano yalivyofanya. TALANTA hiyo itatakwa siku ile ya Hukumu.

Umesikia Neno la Mungu limepiga kelele masikioni mwako kwamba kuabudu sanamu, kusali rozari, mafundisho ya kwenda toharani na ibada za wafu ni mafundisho potofu yanayawapeleka mamilioni kuzimu, pengine uliposikia mara ya kwanza kwako ilikuwa kama ni kitendawili lakini je! ulishawahi kutenga Muda na kumuuliza Mungu je! mambo hayo ni kweli kuliko kupuuzia au kubisha, Kumbuka hiyo ni TALANTA ambayo Bwana alikupa moyoni mwako na usipoizalisha utaulizwa katika ile siku ya Hukumu.


Lakini kama ungependa kujifunza na kuyatendea kazi yale unayohubiriwa au kufundishwa..Bwana anasema: "KWA MAANA YE YOTE MWENYE KITU ATAPEWA, NAYE ATAZIDISHIWA TELE;". Hivyo ungejikuta hata yale uliyokuwa huyajui Bwana anakuongezea na mengine mengi, Neno la Mungu linajifunua kwako , na kujikuta unaimarika kiroho siku baada ya siku.

Kwahiyo cha muhimu sana ni kuzingatia "kile unachokisikia" na kukifanyia kazi kwa bidii adui asije akakichukua hata hicho kidogo Mungu alichokupa neema ya kukisikia kikapotea moyoni mwako. Kwasababu alisema...

Marko 4:24 ... ANGALIENI MSIKIALO; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.
25 Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. "
Maombi yangu ni uanze kukitendea kazi kile ulichokisikia tangu zamani, ili atakapokuja aone matunda ya kusikia kwako Neno lake.

Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment