"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, April 27, 2017

EPUKA MUHURI WA SHETANI

Kutoka 21:2-6 " Ukimnunua MTUMWA wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako HURU bure.
3 Kwamba aliingia kwako peke yake tu, atatoka hivyo peke yake; kwamba ameoa, mkewe atatoka aende pamoja naye.
4 Kwamba ni bwana wake aliyempa huyo mke, naye amemzalia wana, wa kiume au wa kike; yule mke na wanawe watakuwa ni mali ya bwana wake, naye mume atatoka peke yake.
5 Lakini huyo mtumwa AKISEMA WAZIWAZI, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; SITAKI MIMI KUTOKA NIWE HURU;
6 ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake ATALITOBOA SIKIO LAKE KWA UMA; ndipo ATAMTUMIKIA SIKU ZOTE. "

JE! UNAJUA JAMBO GANI LITAMPATA MTU YULE, ALIYESIKIA UKWELI HALAFU HATAKI KUBADILIKA?
 
Biblia inaeleza wazi kabisa kulingana na maandiko hayo hapo juu, Mtumwa yule aliyetangaziwa uhuru wake baada ya kutumika miaka 6 akakataa (Yaani akaona ni vyema kuendelea katika utumwa wake.). Jambo linalotokea ni hili bwana wake huyo mtumwa atachukua sindano na kutoboa SIKIO lake, kuwa kama MUHURI wa kukataa kuwekwa huru, Hivyo basi huyo mtumwa atamtumikia bwana wake milele, Na kama tunavyofahamu sikio likishatobolewa haliwezi kurejea tena katika hali yake ya kwanza. Na ndio maana ilikuwa inatumika kama ISHARA YA MAPATANO(MUHURI).


Vivyo hivyo kwa wanadamu wa leo, Kristo alikuja kututangazia uhuru wetu kutoka katika UTUMWA WA DHAMBI kulingana na

 mathayo 11:28-29 (Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; "), 
 Kwasababu Bwana Yesu alisema Yohana 8:34-36" ....Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. "
 
 Bwana Yesu pia alisema maneno haya luka 4:18-19" Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma KUWATANGAZIA WAFUNGWA KUFUNGULIWA KWAO, Na vipofu kupata kuona tena, KUWAACHA HURU WALIOSETWA,Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. "


Kwahiyo injili ililetwa  kwetu mahususi kwa kutuweka HURU mbali na dhambi. Hapo anaposema "kuutangaza  mwaka wa Bwana uliokubaliwa" akiwa na maana kuwa ndio mwaka wa maachilio, ule mwaka wa saba ( Kwa maana mahali pengine anasema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa. 2 wakoritho 6:2). Kwahiyo tunaona MBIU YA MAACHILIO IMESHAPIGWA watu wote wawe HURU kwa YESU KRISTO BWANA. Lakini  cha kusikitisha wapo baadhi ya watumwa (watumwa wa dhambi), wanakataa kuupokea uhuru WAO waliotangaziwa na Bwana wanapenda kuendelea kumtumikia bwana wao shetani ambaye hapo mwanzo alikuwa anawatumikisha na kuwatesa. Embu tuitazame hii mihuri inampataje mtu.


MUHURI WA MUNGU:
Mungu anao MUHURI wake, na shetani pia anao muhuri wake kwa watoto wake. Wale waliokubali kuwekwa huru na BWANA wanatiwa MUHURI WA MUNGU nao ni ROHO MTAKATIFU kulingana na waefeso 4:30"(Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa MUHURI hata siku ya ukombozi). , na pia biblia inasema katika 2 Wakoritho 3:17 .. walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. ". Kwahiyo unaona unapoukubali UHURU Mungu anakupa zawadi ya kupokea Roho Mtakatifu kama Muhuri wa uhuru wako. Lakini kama hauna Roho wa Mungu wewe bado ni mtumwa wa dhambi na UNAJUA MSHAHARA WA DHAMBI NI MAUTI. Warumi 8:9"....Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. "


MUHURI WA SHETANI:
Kwa wale waliokataa uhuru kwa makusudi angali wakijua kabisa wapo kwenye utumwa na wangepaswa wawe huru, lakini wakapenda kumtumikia bwana wao shetani katika dhambi zao kuliko kumtumikia Mungu nao pia wanatiwa MUHURI. Na mihuri hiyo YA SHETANI wanatiwa katika MASIKIO YA MIOYO YAO, maana yake ni hii HAWATAKUWA TENA NA NEEMA YA MUNGU JUU YA MAISHA YAO!,baada ya kuisikia injili na kuikataa Haiwezekani wao kumgeukia Mungu tena, Hata waelezweje injili hawawezi kusikia tena wageuke hao wameshakuwa mali halali ya shetani. Hii ni hatari sana tuwe makini tunaposikia wito wa Mungu.


Na huu muhuri wa shetani mpaka sasa hivi unaendelea kuwapiga watu, leo hii umeshaisikia injili mara ngapi, umehubiriwa uache uzinzi mara ngapi ewe kijana ewe binti,? umehubiriwa utubu dhambi zako mara ngapi? lakini umekuwa wa kwanza kufanya mizaha? umehubiriwa uache ulevi mara ngapi? unavuta sigara, unaangalia pornoghaphy, unafanya mustarbation, binti unasagana, umekuwa shoga kijana, unaenda kwa waganga, unajifurahisha katika anasa na miziki ya kidunia, mwanamke unavaa suruali, vimini, unapaka rangi kucha, kijana unanyoa mitindo isiyofaa na kusuka nywele ,na tatoo kwenye mwili wako, wanawake usengenyaji na umbea, mtukanaji, unajichanganya na watu waovu kwa jinsi isivyopasa, unachati nao mambo maovu, huku ukijua kabisa watu wanaoyafanya hayo wataishia katika jehanum ya moto, JE! UNADHANI NEEMA YA MUNGU ITAENDELEA KUDUMU JUU YAKO MILELE?. Mungu hadhihakiwi apandacho mtu ndicho atakachokivuna. Tutawezaje kupona tusipouthamini wokovu mkuu namna hii?.


Unashindwa kuona jinsi unavyozidi kutiwa ule MUHURI wa shetani? kwa kuukataa uhuru wako ambao BWANA aliokutangazia pale KALVARI?. Maana kama unasikia sauti ya Mungu kila siku ikisema moyoni mwako UTUBU lakini unaipuuzia nakwambia ukweli utafika wakati HAUTAKAA UISIKIE TENA NDANI YAKO!!, Na unajua ni kitu gani kitaenda kukutokea? Ni kwamba utafika wakati utaona mambo yote kuwa ni sawa, kuwa ulevi ni sawa,utaona uasherati hauna ubaya wowote, Mungu aliyetuumba hawezi kutuhukumu, hautaamini tena kama kuna jehanamu, utaishia kuwaona watumishi wote wa Mungu ni waongo, utaishia kuukosoa kila siku ukristo na biblia ukisema hayo mambo ni ya kale, Utaanza kujiona kuwa ni haki yako kuishi unavyotaka hata kujichubua, kubadili maumbile, kuvaa unavyotaka ni sawa, Utajiona kutukana ni sehemu tu ya maisha ya binadamu hakuna kosa lolote kwasababu Roho Wa Mungu hayupo tena ndani yako kwasababu UMESHATIWA MUHURI, utaanza kuona kujipenda mwenyewe ni sawa, Kutazama pornography na kufanya musturabation ni sehemu maisha ya kila mwanadamu ukijidanganya kuwa Mungu hawezi kumuhukumu mtu kwa kufanya hivyo, unajikuta unaanza kupenda kufuatilia mafundisho ya mashetani kuliko mafundisho ya Mungu, Biblia hutaki kusoma kusoma lakini habari za freemasons, na zi kichawi, na filamu pamoja na vitabu kama , harryporter, twightlight, vampires,n.k. ndivyo vinavyokuvutia kusoma na kuangalia, jiulize ni roho gani inakuendesha? n.k.


Ndugu ukishaanza kuona dalili ya mambo kama hayo yanakuja ndani yako, jua kabisa neema ya Mungu ndivyo inavyoondoka kwako kidogo kidogo na ndo unavyoupokea MUHURI wa shetani hivyo, maana jua tu wewe unayeisikia injili kila siku unaambiwa utubu hautaki, neema yako haiwezi kuwa sawa na mtu yule ambaye hajawahi kusikia  injili kabisa. soma mstari ufuatao; 


2 thesalonike 2:10-12 " na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.
11 KWAHIYO MUNGU AWALETEA NGUVU YA UPOTEVU, WAUAMINI UONGO;
12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu. "
Kwahiyo ndugu maneno hayo hayakuogopeshi??  TUBU! yamkini hii sauti ya upole inayokuambia kila siku utubu bado inaendelea KULIA NDANI YAKO! ..itii na ugeuke maana upo katika HATARI, Maana hiyo sauti haitadumu milele ndani yako. Na ikishaondoka hakutakuwa na njia ya kurudi tena. YAANI MOYO WA KUTUBU hautakuwepo tena ndani yako utafanana na hao watu unaowaona huko ulimwenguni watendao matendo ya giza si kana kwamba hawasikii au hawakusikia injili  hapana lakini mioyo yao imeshatiwa MUHURI, hawatakaa wasikie tena na kubadilika, ndugu usifanane nao. Mtii Mungu tubu dhambi zako muda umeenda sana kuliko unavyofikiria.Yesu yupo mlangoni kurudi.
 Maana biblia inasema...

 ufunuo 22:10 "Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia. MWENYE KUDHULUMU NA AZIDI KUDHULUMU; na MWENYE UCHAFU AZIDI KUWA MCHAFU; na MWENYE HAKI AZIDI KUFANYA HAKI; na MTAKATIFU NA AZIDI KUTAKASWA.Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. "
Naomba umalizie kwa kuyatafakari maneno yafuatayo ujue hatma ya WALIOUKATAA UHURU WAO KUTOKA KWA BWANA;
Warumi 1:24" Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.
25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.
26 HIVYO MUNGU ALIWAACHA WAFUATE TAMAA ZAO ZA AIBU, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;
27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, WAKAPATA NAFSINI MWAO MALIPO YA UPOTEVU WAO YALIYO HAKI YAO.
28 NA KAMA WALIVYOKATAA KUWA NA MUNGU KATIKA FAHAMU ZAO, MUNGU ALIWAACHA WAFUATE AKILI ZAO ZISIZOFAA, WAYAFANYE YASIYOWAPASA.

29 Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya,
30 wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao,
31 wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema;
32 AMBAO WAKIJUA SANA HUKUMU YA HAKI YA MUNGU, YA KWAMBA WAYATENDAYO HAYO, WAMESTAHILI MAUTI, WANATENDA HAYO, WALA SI HIVYO TU, BALI WANAKUBALIANA NAO WAYATENDAYO.

Tuesday, April 25, 2017

UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?

Mathayo 7:15 "Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?
17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.
20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.
21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. "
Kuna watu wanasema usizihubiri hizi habari, we fundisha TU watu watubu wawe wakristo inatosha ndiyo kazi yako!. Swali ni je! ukishakuwa mkristo ndio mwisho wa safari?, unahitaji kukua na ndio safari inapoanzia  na sio inaishia. Hivyo basi unahitaji chakula ili ukue, na ujue ni chakula gani unapaswa ukile, maana vyakula ni vingi vijengavyo na vibomoavyo, Hivyo ni kuwa makini kujua ni chakula kipi ule na kipi usile kwa usalama wa roho yako na hatma yako ya milele.

Tunaishi katika kipindi cha hatari ambacho hakijawahi hata kutokea katika vizazi vyote vya nyuma, ambacho kina mchanganyiko mkubwa wa MANABII WA UONGO NA MANABII WA KWELI, Na wote wanafanya kazi moja ya KUVUNA ROHO ZA WATU, aidha kuzipeleka kuzimu au mbinguni, ni kipindi cha hatari sana tunachoishi. Ni muhimu kufahamu unavunwa upande gani, ili usije ukajikuta unadondokea sehemu ambayo haujatarajia.


UPOTOFU ULIOPO SASA:
Jambo kubwa linalowachanganya watu wengi ni kuona pale mtu anayejiita mtumishi wa Mungu halafu bado ni mwasherati, mtukanaji, mlevi, anapenda anasa, na bado miujiza inatendeka na yeye, anafufua wafu, anaombea watu wanaponywa, anatabiri na unabii unakuja kutimia, ananena kwa lugha n.k. kiasi ambacho kinamfanya mtu mchanga ashindwe kuelewa inawezekanikaje huyu mtumishi anafanya mambo ya kidunia lakini bado ishara na miujiza zinatendeka na yeye, Na wala hatumii uchawi ila  anatumia jina la YESU na nguvu za Mungu zinashuka. "HII NI SIRI" na ni jukumu kwa kila mkristo anayethamini maisha yake ya kiroho kufahamu..kumbuka (kuna wanaotumia nguvu za giza kutenda miujiza, siwazungumzii hao, hao ni rahisi kuwagundua lakini nawazungumzia wale wanaotumia nguvu za Mungu ambao ni ngumu kuwatambua.)


Tusome, mstari ufuatao unawazungumzia hao wanaotumia nguvu za Mungu ; kumb.13:1-5"
1 Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,
2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;
3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.
4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.
5 Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya Bwana, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru Bwana, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako. "

Unaona hapo? Huyo nabii hapo katoa unabii kwa uweza wa nguvu za Mungu na ikatokea, lakini anawafundisha watu waende kinyume na maagizo ya Mungu. Vivyo hivyo na hata sasa katika kipindi hichi cha mwisho Mungu ameamua kuachia mvua yake (UPAKO) kwa watu wote waovu na wema kutujaribu sisi kama TUNAMPENDA BWANA NA KUYASHIKA MANENO YAKE AU LA!. 
 Mtu anaweza akaja kwako na kutoa unabii na ukatimia na kufufua wafu, na kuponya wagonjwa lakini akafundisha injili nyingine akakwambia  ulevi ni sawa, wanawake kwenda na mitindo ya kisasa ni sawa (anasema Mungu haangalii mavazi anaangalia roho ), akakufundisha kuupenda ulimwengu ni sawa, kuoa wake wengi ni sawa, Dunia haiishi leo wala kesho kula maisha, kuwa na pesa nyingi ndio kigezo cha kubarikiwa na Mungu, Mungu siku zote ni Mungu mzuri na hawezi kuwahukumu watu aliowaumba. n.k. na bado mtu huyo akatoa mapepo na kufufua wafu. Na wewe kwasababu NENO na kumpenda Mungu hakupo ndani yako, ukadhani anazungumza ukweli au katumwa na Mungu kwasababu tu! ametoa unabii ukatokea, NDUGU USIDANGANYIKE UMEPOTEA!! .  Biblia inasema jiepushe na huyo mtu, CHUKUA TAHADHARI KWA USALAMA WA MAISHA YAKO..KIMBIA! HARAKA SANA NI BWANA NDIYE ANAYEKUJARIBU KUONA KAMA UNAMPENDA KWELI NA KULIFUATA NENO LAKE AU LA!
 
Leo hii wewe unayejiita mkristo unapenda injili za kufarijiwa tu! siku zote unapendwa kuambiwa "ALL IS WELL" ulimwengu hautakuja kuteketezwa,tunaishi chini ya neema, mafundisho unayoyapenda wewe ni KUTABIRIWA MAFANIKIO TU!. Lakini fahamu jambo moja BWANA YESU hakuacha enzi na mamlaka mbinguni ili aje kutufia sisi mlabani tuwe MABILIONEA, bali kwa ajili ya dhambi zetu.(hicho ndicho kiini cha injili) yeye mwenyewe alizungumza ..mathayo 16:24-27

" Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.
25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.
26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 
Leo mkristo anadai anamfuata YESU, lakini kigezo cha kumfuata YESU ni kuwa na MSALABA wako, sasa wewe MSALABA WAKO UKO WAPI?, Jihadhari na haya mafundisho ya uongo yanawapeleka maelfu wa waaminio kuzimu kila siku pasipo wao kujua.

Hawa manabii wa uongo, Bwana Yesu alisema tutawatambua kwa  MATUNDA YAO na sio kwa upako wao, kwasababu Mungu anaweza akamtumia mtu kama chombo tu cha kuazima akishamaliza shughuli nacho anakiacha, mfano tunaona Mungu alimtumia Punda kuongea na Nabii Balaamu kumpa ujumbe, lakini baada ya punda kutoa ujumbe alirudia katika hali yake ya kawaida ya upunda, vivyo hivyo na Balaamu mwenyewe alikuwa ni MCHAWI lakini Mungu alimtumia yeye kuwabariki Israeli, (hesabu 22:21-29), Na pia Mungu aliwatumia wale manabii 400 kumdanganya mfalme Ahabu kwasababu Mungu alikuwa amekusudia mabaya juu yake. (1 wafalme 22:6). Kwahiyo kuwa na upako mtu kuona maono, au kuwa nabii, au kunena kwa lugha au kuponya au kufanya miujiza yoyote ile, sio kigezo cha huyo mtu kuwa NABII WA MUNGU. Tutatawatambua kwa matunda yao (AMBAYO NI NENO LA MUNGU). Nabii wa ni yule anayekuja na ishara pamoja na NENO lakini lililokuu ni NENO.


Kipime mtu anachokuambia je! kinaendana na NENO la Mungu? kama hakiendani na NENO la Mungu weka kando haijalishi anawashirika wengi kiasi gani, au anakubalika kiasi gani, au kanisa ni kubwa kiasi gani, au anaupako kiasi gani. KIMBIA! HILO NI SINAGOGI LA SHETANI!.. 


  • Ukiona unadumu kwenye mafundisho yanayokupeleka wewe kuutazama ulimwengu kuliko kumtazama KRISTO! KIMBIA!  KWA USALAMA WA MAISHA YAKO!!.
  • Ukiona unahubiriwa injili za mafanikio tu! Haufundishwi kufikia toba, au utakatifu maana biblia inasema pasipo huo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu (waebrania 12:14). KIMBIA!
  • Ukiona unahubiriwa injili ya kutoa tu! kutoa tu! toa zaka, panda mbegu, n.k. Lakini NENO halihubiriwi, ONDOKA HAPO! Bwana Yesu alisema hivi..mathayo 23:23-24"Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. VIONGOZI VIPOFU, WENYE KUCHUJA MBU NA KUMEZA NGAMIA. " ...KIMBIA! JIOKOE NAFSI YAKO.
  • Ukiona unaenda katika nyumba ya Mungu, hauhubiriwi NENO bali SIASA, usitazame nyuma hata kama kuna miujiza inatendeka kiasi gani....KIMBIA KAMA UNAIPENDA NAFSI YAKO!
  • Ukiona kiongozi wako wa dini, Anaelekeza watu kwake, na sio kwa KRISTO, anajisifu na kujitukuza yeye, utukufu wa Mungu anauchukua yeye.Hapo  hapana tofauti na ibada za sanamu, fahamu kuwa unamwabudu mtu na sio Mungu, isaya 42:8" Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu. ".usimsikilize nabii huyo biblia inasema hivyo... KIMBIA!
Jiulize Wewe unayejiita mkristo  tangu ulipoamini, maisha yako ya kiroho yamesonga mbele kiasi gani. utakuwaje mkristo halafu biblia husomi!??  sasa utawatambuaje manabii wa uongo au manabii wa ukweli kwa namna hiyo watakapokujia na mafundisho yao??. Utakuwa unapelekwa na kila upepo unaokuja wa elimu yoyote. Maana njia pekee ya kumpima nabii wa uongo au Nabii wa ukweli ni kwa NENO TU!. Na sio kitu kingine. Jijengee kila siku tabia ya kusoma NENO na kuomba. Hizi ni nyakati za hatari tunaishi zile zilizotabiriwa kuwa watatokea manabii na makristo wengi wa uongo nao watawadanganya wengi yamkini hata walio wateule. Kumbuka ni wateule ndio wanaozungumziwa hapo kuwa wanaweza wakadanganywa sasa jiulize wewe ambaye sio mteule utaonekania wapi? wewe ndio hautaelewa chochote kinachoendelea utaishia kuwashangilia na kuwasifia kama Bwana Yesu alivyotabiri juu ya manabii wa uongo.


2 Petro 1:10" Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe."
KWAHIYO NDUGU HUU NI WAKATI WA MUNGU KUTUJARIBU SISI KAMA TUNAMPENDA YEYE NA KULISHIKA NENO LAKE AU LA!. Biblia inasema, MPENDE BWANA MUNGU WAKO, KWA MOYO WAKO WOTE, KWA ROHO YAKO YOTE, KWA NGUVU ZAKO ZOTE, NA KWA AKILI ZAKO ZOTE.
 
Mungu hadhihakiwi usipoweza kufanya hivyo jua tu utaangukia kwenye huu mstari ufuatao;

2 Thesalonike 2:10-12"... na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.
11 KWAHIYO MUNGU AWALETEA NGUVU YA UPOTEVU, WAUAMINI UONGO;12  ILI WAHUKUMIWE WOTE ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu. "

MARAN ATHA!

Monday, April 24, 2017

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?


Tukisoma kitabu cha mwanzo 1, Biblia inasema Hapo mwanzo, Mungu aliziumba mbingu na nchi. Lakini tunaona hakueleza aliumbaje umbaje hii mbingu na nchi yaani, miti, jua, mwezi, milima, wanyama, mwanadamu n.k.

Lakini tukija kusoma kwenye kitabu cha waebrania 11:3 tunaona

" Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri. "
 Kwahiyo siri inaonekana hapo ni kwamba mbingu na nchi ziliumbwa kwa NENO la Mungu.

Sasa swali linakuja hili NENO ni nini?
Tukisoma Yohana 1:1-3"
1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. "
Kwahiyo kulingana na mstari huu biblia inaeleza kuwa Neno lilikuwapo kwa Mungu, na lilikuwa ni Mungu, maana halisi ya "Neno" kulingana na tafsiri ya Kigiriki iliyotumika ni WAZO au NIA. Kwahiyo wazo lilikuwapo ndani ya Mungu, Na hivyo vitu vyote vilivyoumbwa vimetoka katika hilo wazo la Mungu mfano dunia, malaika, wanadamu, sayari, miti n.k. 

Mfano mzuri ni kama wewe kitu chochote ulichokitengeneza kama nyumba, kiti, meza, nguo, vilitoka kwanza katika wazo lako au nia yako. Hii ikiwa na maana kwamba kama usingekuwa na hilo wazo usingeviumba vitu hivyo vyote, Vivyo hivyo na kwa Mungu pia kama WAZO  lake (ambalo ni Neno lake) asingekuwa nalo hapo mwanzo asingeweza kuumba chochote.

Kwahiyo kabla ya mwanadamu kuasi hili NENO lilikuwa pamoja na mwanadamu, Mtu alikuwa na ushirika na Mungu kwa asilimia zote, kwasababu NENO lilikuwa ndani yake kama lilivyokuwa ndani ya Mungu kitu kilichomfanya mpaka mwanadamu kuonekana kuwa kama mfano wa Mungu, Adamu alikuwa na mamlaka yote duniani, kama vile YESU leo alivyo na mamlaka yote duniani na mbinguni biblia inasema hivyo. Na ndio maana utajua sababu ya Mungu kutuita sisi ni miungu duniani, Na yeye ni MUNGU WA miungu.
Lakini baada ya anguko Adamu aliyapoteza yote aliyokuwa nayo kwasababu alijitenga na NENO la Mungu kwa kutokutii. Hivyo yeye na NENO (nia ya Mungu) vikawa ni vitu viwili tofauti. Kuanzia wakati huo baada ya anguko, lile NENO likaanza kumtafuta tena mwanadamu limrudishe tena katika ile hali ya kuwa na mahusiano na Mungu na mamlaka yote aliyokuwa nayo kabla hajayapoteza. Na ndio maana kuna mahali Yesu alisema sio ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua nyinyi.

Sasa tangu huo wakati lile NENO likaanza kutafuta njia nyingi za kumrejesha mwanadamu, likaanza kuzungumza na wanadamu kwa kupitia MBINGU, nyota,sayari na kwa  vitu vya asili, kwa dhumuni la kumrejesha tu, lakini mwanadamu bado hakutaka kutega sikio lake kusikia.

Baadaye lile NENO likaanza kuzungumza kupitia watu, mfano manabii wa Mungu, tunaona manabii kama Henoko, Nuhu, Ibrahimu, Musa, Eliya, Danieli, Yeremia, Isaya n.k..lilisema nao kwa nguvu na kwa udhihirisho mwingi liliwapigia kelele wanadamu wamrudie Mungu, warudi  katika ule ushirika waliokuwa nao kwanza na Mungu. Lakini wanadamu bado hawakutega sikio lao kulisikia, zaidi ya yote waliwaua manabii waliotumwa kwalo.

Lakini japokuwa NENO hili limezungumza mara zote hizi kwa vizazi na vizazi kupitia vitu vya asili na manabii, bado ule uhusiano uliokusudiwa mwanadamu awe nao na Mungu wake haukufanikiwa kurejeshwa kwasababu ya ugumu wa mioyo ya wanadamu. 

Ndipo wakati ulipofika lile Neno likaona liuvae mwili, lije lenyewe katika mwili,liishi na wanadamu, lihubiri mambo yote lililohubiri ndani ya manabii na vitu vya asili kwa kusudi lile lile la  kumrejesha mwanadamu  kwa muumba wake. Hili jambo linazungumziwa kwenye..
Waebrania 1:1-2" Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. " ...Sasa umeona mwisho wa yote Neno limekuja kuzungumza na sisi kupitia nini? sio kanisa wa chochote bali mwana.

Hili NENO likajichagulia mwili unaoitwa YESU KRISTO, Haleluya! ni furaha kiasi gani Mungu alivyojirahisisha kwetu sisi ili tukae na hilo NENO kwa jinsi ya kimwili, likiongea, likifundisha, likijibu maswali, likitembea na sisi wazi kabisa, linafurahi na sisi, kitu ambacho hapo mwanzo ilikuwa ni ngumu kulielewa lizungumzapo lakini hapa lipo pamoja nasi (IMANUELI)..Embu tutazame mstari ufuatao;

 1 Yohana 1:1-3"
1 Lile lililokuwako tangu mwanzo, TULILOLISIKIA, TULILOLIONA kwa macho yetu, TULILOLITAZAMA, na mikono yetu IKALIPAPASA, kwa habari ya NENO la uzima;
2 (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);
3 hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. "
..Habari hiyo inaelezea lile NENO ambalo zamani lilikuwepo lakini sasa limefanyika mwili na lipo katikati yetu kama mwanadamu.

Hivyo basi BWANA YESU KRISTO alipokuja akaanza kutufundisha na kuturejesha katika utimilifu wote na Mungu tuliokuwa nao pale Edeni hata na zaidi ya pale.,Jambo la kwanza alilolifanya ni kutupatanisha sisi na Mungu kwa kumwaga damu yake kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu maana biblia inasema pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo (waebrania 9:22)

Na jambo la pili ni kutufanya sisi kuwa wana wa Mungu (miungu),
Yohana 1:12 "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; " Tukisoma 

2 wakoritho 5:18-19 "Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu NENO la upatanisho. "
Kama tulivyosema lile NENO ni wazo/nia ya MUNGU nalo ni Mungu, ikiwa na maana usiipotii nia ya Mungu haujamtii Mungu. Na nia ya Mungu ni nini? Ni kuturujesha sisi tuwe na mahusiano naye kama ilivyokuwa hapo mwanzo ili tumwabudu MUNGU katika Roho na Kweli. Na ndio maana WAZO/NIA yake iliuvaa mwili kwa dhumuni la kutuhubiria sisi tumgeukie Baba. Kwasababu hiyo basi Yesu Kristo ndiye NJIA, NA KWELI, NA UZIMA, MTU HAFIKI KWA BABA ISIPOKUWA KWA NJIA YAKE YEYE.(Yohana 14:6), alisema aliyeniona mimi amemwona BABA, usipomtii YESU KRISTO na kumwamini umeukataa mpango wa Mungu kwa wanadamu na viumbe vyake vyote kama shetani alivyofanya. 

Natumaini utakuwa umeshaiona sababu ya YESU KRISTO Kutokea ni nini?, ni hiyo hapo juu, Neno la Mungu liliuvaa mwili, kutuhubiria sisi na kuturejesha kwa Mungu wetu ili tumwabudu yeye katika roho na kweli. 

Wakolosai 2:9 "Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. "
Kwahiyo Mungu hana nafsi tatu, Nafsi ya Mungu ni moja tu. Mungu kuonekana katika mwili hakumfanyi yeye kuwa na nafsi tatu. Alifanya hivyo tu ili kutupatanisha sisi na yeye. Kama tusingeanguka katika dhambi kulikuwa hakuna haja ya yeye kuuvaa mwili na kuja duniani, Yeye ni Roho nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

NEEMA YA BWANA YESU KRISTO IWE PAMOJA NAWE!

FASHION! NI DHAMBI KWA BINTI ZA MUNGU.

                          (Sikiliza ujumbe huu utakusaidi kubadilisha maisha yako )


Bwana YESU ni yeye yule jana, na leo na hata milele hajabadilika wala hana kigeugeu, na NENO lake ni lile lile. Kama maandiko yanavyosema mwanamke wa kikristo anapaswa avae mavazi ya kujisitiri.(1timotheo 2:9) hilo Neno hata leo bado linaendelea kufanya kazi kwa binti za Mungu.

Leo hii vichaa wapo wengi mitaani tunawaona, lakini ni mara chache sana kumuona kichaa mwanamke akitembea uchi barabarani, ingawa vichaa wanaume ni rahisi kuwaona wakiwa uchi, lakini sio kwa wanawake vichaa utawakuta wamevaa matambara na kujisitiri mwili mzima japo ni vichaa. Je! ni kwanini iwe hivi?? Jibu ni Kwasababu uchi wa mwanamke ni wathamani zaidi kuliko wa mwanamume hivyo unastahili muda wote usitiriwe.

Lakini leo hii mwanamke mwenye akili timamu ambaye uchi wake unathamani ambaye angepaswa afunikwe, ndiye anayeongoza kwa kutembea uchi barabarani, SASA HAPO KICHAA NI NANI?  lakini mwanamume ambaye uchi wake usiokuwa na thamani nyingi utakuta kajisitiri, kafunika shingo yake kwa shati na tai, huwezi kuona mgongo wake uko wazi wala mapaja yake wazi akitembea barabarani, miguu yake imesitiriwa yote kwa viatu na soksi, ni mtu huyo ambaye uchi wake hauna thamani sana, Leo hii huwezi kuona mwanaume anaenda na vesti kazini, lakini hili jambo ni la kawaida kwa wanawake kutembea migongo wazi na vifua wazi hata sasa imekuwa kawaida mpaka kwenye sehemu za ibada.

Swali ni Je! roho gani ipo hapo katikati? jibu ni rahisi ni ile ile roho iliyokuwa kwa mwanamke Yezebeli wa kwa maana yeye ndiye mwanamke pekee aliyekuwa anapaka uso rangi katika biblia.Lakini tuna wadada hao hao ambao Bwana Yesu amewaambia yeye mwenyewe wasifanye  mambo kama hayo na wametii yaani, kujipodoa uso, kupaka wanja, kuvaa vimini, suruali, kaptura, vesti, tight, pedo, kupaka lipstick, kupachika kucha, wigi n.k. lakini cha ajabu utamkuta mdada mwingine anajiita mkristo na anadai  amepokea Roho Wa Mungu lakini bado anajiona salama kufanya vitu hivyo.

Jiulize ni roho gani iliyoko ndani yako? kwanini YESU yule yule amkataze dada yule kufanya hivyo vitu na wewe asikukataze? jiulize sana, kama Roho wa Mungu kweli anakaa ndani yako atakushuhudia kwamba haya mambo hayafai na yanakupeleka kuzimu.

 Lakini kaa ukifahamu tu, wanawake wote wanaofanya hivyo sehemu yao ni katika lile ziwa la moto HIVI ASEMA BWANA.. (warumi 1).

Friday, April 14, 2017

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 13

 
SWALI 1: Je! ni sahihi mtu kuning'iniza  picha nyumbani mwako kama ya Yesu? maana imeandikwa kutoka 20:4 "Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. " Sasa naomba kufahamu kufanya hivyo ni makosa?

JIBU: kwa kulijibu hili swali tumalizie kusoma mstari huo..

 kutoka 20:4-5" Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.
5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,"

Sasa tunaona katika huo mstari wa tano msisitizo umewekwa pale katika neon “USIVISUJUDIE WALA KUVITUMIKIA”, lakini sio kuwa na picha yoyote kama ya  Yesu nyumbani mwako ni vibaya hapana! unaweza kuweka picha yoyote upendayo ilimradi iwe ni njema, maana tukisema tusiweke picha yoyote basi hata tunaponing'iniza picha zetu wenyewe ukutani majumbani mwetu tunafanya vibaya kwasababu maandiko yanasema usijifanyie mfano wa kitu chochote sio tu kilicho juu mbinguni bali hata kilichopo chini duniani. unaona hapo msisitizo ni kwamba unapoweka picha yoyote au sanamu yoyote hupaswi kuiabudu  wala kuisujudia kwa kufanya hivyo ni machukizo makubwa mbele za Mungu. Lakini leo hii kuna baadhi ya watu,na dini na madhehebu yanaabudu sanamu za Yesu na bikira Mariamu au watakatifu waliokufa kale hao ni dhahiri kuwa wanamwabudu shetani aidha kwa kujua au kwa kutokujua. Kwahiyo hakuna shida yoyote kuweka picha ilimradi isihusishwe na mambo yoyote ya ibada mfano wa kuabudiwa au kusujudiwa.




SWALI 2: Naomba ufafanuzi wa huu mstari Yohana 11:25-26"  Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? " hususani hapo anaposema (naye kila aishiye na kuniamini mimi hatakufa kabisa hata milele.) ana maana gani?

JIBU :
Tunajua Yesu Kristo ndio ule mti wa uzima uliozungumziwa katika bustani ya Edeni kule mwanzo kwamba ukila matunda yake utaishi milele, na matunda yake leo hii tunayajua ni NENO lake, na neno lake ndio UZIMA wenyewe na siku zote palipo na uzima hapana kifo. 

Tukichunguza katika mstari huo tunaona Bwana Yesu alizungumza kwa watu wa aina mbili tofauti,


Aina ya kwanza: ni "yeye aniaminiye mimi ajapokufa atakuwa anaishi". Hili ni kundi ambalo linajumuisha watu wote waliomwamini Bwana watakaokufa watakuwa wanaendelea kuishi katika paradiso wakingojea ufufuo wa mwisho lakini kundi hili halikufanikiwa kufikia utimilifu wa imani ya kumwamini Mwana wa Mungu, hivyo basi itawapasa wafe lakini kwa kuwa walimwamini Mungu kwa sehemu ya imani watakuwa wanaendelea kuishi huko paradiso. Na ni watu wengi leo hii wanakufa katika hali hii.


Aina ya pili : "naye kila aishiye na kuniamini mimi hatakufa kabisa hata milele". Hili ni kundi lililofikia imani timilifu ya kumwamini na kumjua sana mwana wa Mungu inayozungumziwa katika kitabu cha...

 (waefeso 4:13”hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; )

hata kufikia hatua ya kushinda kifo na mauti. Mfano wa watu kama hawa tunawaona kama Henoko, Eliya, na kanisa ambalo litakuja kunyakuliwa siku ya mwisho. Hata leo hii inawezekana mtu kutokuonja mauti kabisa tukimwamini mwana wa Mungu (YESU KRISTO) katika utimilifu wote, tutachukuliwa juu hatutakufa kama  ilivyokuwa kwa Eliya na Henoko, maana biblia inasema Eliya alikuwa ni mtu mwenye tabia sawa na sisi lakini kwa bidiii na kwa imani akachukuliwa juu. Mahali pengine Bwana Yesu alisema katika...
 Yohana 8:51-54 "Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele.
52 Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng'amua ya kuwa una pepo. Ibrahimu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele.
53 Wewe u mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani?
54 Yesu akajibu, Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu. " mstari huu unaelezea jinsi Bwana alivyokuwa akijaribu kuwaeleza juu ya jambo hili lakini wayahudi hawakutaka kulipokea.
Sehemu nyingine Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake, mathayo 16:28"Amin, nawaambieni, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake. " leo hii zipo shuhuda nyingi duniani za watu waliochukuliwa na Bwana pasipo kuonja mauti lakini shetani anataka kuwafanya watu waamini kuwa hilo jambo haliwezekani kwamba ni manabii tu wa zamani ndio walikuwa na uwezo wa kufanya hivyo siku hizi hayo mambo hamna. usidanganyike katika kila kizazi Bwana ana watu wake wanaoshinda. Hivyo maneno haya yanatupa changamoto ya sisi kuongeza uhusiano wetu na Mungu kwasababu hata kanisa litakalokuja kunyakuliwa halitaonja mauti na ni lazima liwe na hiyo imani swali je! wewe unayo? kama hauna ndio wakati wa kuitafuta sasa maana Bwana Yesu mwenyewe alisema luka 18:8”......walakini atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” kwahiyo ni lazima aione imani kwanza ndipo aje hivyo tuitafute hii imani vinginevyo hatutakwenda kwenye unyakuo kumbuka ni Kristo anayetungojea sisi tuwe wakamilifu ndipo aje kutuchukua na sio sisi tunayemngojea yeye.

Mungu akubariki.

Tuesday, April 11, 2017

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 12

SWALI: Watumishi naomba kuuliza..ni nani anatawala dunia kati ya Mungu na shetani? Na kama ni Mungu anayetawala kwa nini kuna matukio ya kutisha kama ajali mbaya za magari,ndege,mafuriko kama ya Japan kama Mungu ndiye anayetawala kwanini hayazuii anaacha yanaua watu??? Na ukisoma mathayo 4:1 na kuendelea unasoma shetani anamwambia Yesu dunia ni Mali yake, na Kuna  tofauti gani kati ya dunia na ulimwengu nisaidie?

JIBU:
Dunia yote ni ya Mungu ukisoma;

 zaburi 24: 1-2 "1 Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.
2 Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya mito ya maji aliithibitisha. "

Na pia Bwana Yesu Kristo baada ya kufufuka kwake aliwaambia wanafunzi wake
 mathayo 28:18"Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. "
Kwahiyo kwa maandiko hayo tunaona kabisa dunia yote inamilikiwa na Mungu na wala sio shetani, lakini "dunia sio ulimwengu". Huu ulimwengu ndio mali ya shetani na ndio yeye anayeumiliki na kitakachokuja kuteketezwa sio dunia bali ni ulimwengu huu mbovu wa shetani ambao ni milki yake..
Tofauti kati ya dunia na ulimwengu ni hii;

  • Dunia ni vitu vyote vya kijeografia unavyoviona vya asili kama mabara, bahari, miti, milima, hewa, ardhi, mito,mabonde, visiwa, n.k.
  • Na Ulimwengu ni ustaarabu uliobuniwa na aidha Mungu au shetani ili kuifanya dunia iwe ni mahali pa kuishi. mfano. elimu, burudani, miziki, utawala, uchumi, mahakama,Milki, fahari, uchukuzi, n.k. Na ndio maana kwenye mathayo 4 shetani alimwambia Bwana Yesu nitakupa ulimwengu wote na fahari yake ukianguka kunisujudia.
Kwahiyo dunia itadumu siku zote, lakini ustaarabu uliowekwa na shetani utaangamizwa (ulimwengu) utabaki tu ule uliowekwa na Mungu, na hata hivyo 99% ya ustarabu uliopo duniani leo unakaliwa na shetani na ndio maana siku ya Bwana itaharibu ustaarabu wote wa shetani na kuleta ustaarabu mpya wa Kristo hapa duniani huo ndio utakaodumu milele na  utakaokuwa katika ule utawala wa miaka 1000 ufunuo 19 & 20.
Na sababu ya Mungu kuruhusu mambo mabaya kutokea kama ajali, vimbunga, mafuriko ni kwasababu ya mambo maovu ya huu ulimwengu yaliyopo kama umwagaji damu, rushwa, uasherati, ulevi, uaribifu wa mazingira, ushoga, vita, n.k. mambo kama haya huaribu dunia husababisha gadhabu ya Mungu kumwaga juu ya nchi.

Sunday, April 9, 2017

MASWALI NA MAJIBU: SEHEMU YA 11


SWALI: Ufunuo 20:7  "Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;
8 naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.
9 Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala."
 Je!, hawa watu ambao shetani atawashawishi kuishambulia kambi ya watakatifu watatoka wapi wakati katika ule utawala wa miaka 1000 hakukuwa na waovu?
JIBU: Katika utawala wa miaka 1000 biblia inarekodi kuwa wenye dhambi watakuwepo, lakini dhambi  haitatawala dunia kwasababu mkuu wa ulimwengu ule atakuwa ni MFALME WA AMANI yaani Yesu Kristo, tofauti na dunia ya sasa ambayo mkuu wa ulimwengu huu ni shetani. Dhambi na wenye dhambi watakuja kuondolewa wote mara tu baada hukumu ya kile kiti cheupe cha Mungu ambayo itakuja baada ya utawala wa miaka 1000 kuisha. Kwahiyo kama vile biblia inavyosema Kristo atatawala kwa fimbo ya chuma pamoja na sisi  ukisoma..
ufunuo 2:26-27" Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,
27 naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu. "
(fimbo ya chuma inamaana >> ni utii chini ya kila kitakachoamriwa pasipo majadiliano wala mahojiano, kwa atakayekaidi atalazimika kutumikia adhabu kali ). Hautakuwa utawala wa kimabavu bali ni wa amani na utaratibu lakini kwa watakaokuwa wanaenda kinyume na sheria ya Mfalme na watakatifu wake wataangukia laana, soma zekaria 14 yote inaelezea adhabu zitakazowakuta mataifa wasiokwenda kumwabudu mfalme mwaka kwa mwaka Yerusalemu,
  pia isaya 65:17-20" 17 Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.
18 Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.
19 Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza.
20 Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. "
Hivyo tunaona atakayetawaliwa hapo kwa fimbo ya chuma sio mkristo bali watakuwa ni watu wengine watakaokuja kuzaliwa ndani ya huo utawala wa miaka 1000. Maana ile siku ya mwisho ya Bwana atakayokuja pamoja na sisi kuuharibu ulimwengu wa sasa haitamaliza watu wote bali kuna watu wachache watakaosalia,soma
 Isaya 13:9-13"  Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.
10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.
11 Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;
12 nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri.
13 Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali. "
hao ndio watakaopata neema ya kuingia katika utawala wa miaka 1000 katika miili yao ya asili(hawa ndio watakaokuwa wakizaa na kuzaliana) lakini sisi tutakao kuja na Kristo kutakuwa hakuna kuzaa wala kuzaliana kwa sababu tutakuwa na ile miili ya utukufu iliyotoka mbinguni,
 Na baadhi ya hawa watu  baadaye shetani atakapokuja kufunguliwa kuwajaribu ndio watakaotaka kufanya vita dhidi ya watakatifu, kama biblia inavyosema moto utashuka kutoka mbinguni na kuwameza wote. ndipo hukumu ya kiti cheupe itafuata ambapo waovu wote watahukumiwa na kutupwa katika ziwa la moto pamoja na shetani na kisha tutaingia katika umilele ambapo dhambi haitakuwepo wala waovu.

Thursday, April 6, 2017

JUMBE KATIKA VITABU ZILIZOREKODIWA ZA NDUGU WILLIAM BRANHAM



MAELEZO YA JINSI YA KU-DOWNLOAD
  • Bofya ''download'' rangi ya pinki chini.
  •  kisha upande wa juu kulia wa ukurasa utaona alama ifuatayo ibofye kwa ku-download