"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, April 25, 2017

UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?

Mathayo 7:15 "Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?
17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
19 Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni.
20 Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.
21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. "
Kuna watu wanasema usizihubiri hizi habari, we fundisha TU watu watubu wawe wakristo inatosha ndiyo kazi yako!. Swali ni je! ukishakuwa mkristo ndio mwisho wa safari?, unahitaji kukua na ndio safari inapoanzia  na sio inaishia. Hivyo basi unahitaji chakula ili ukue, na ujue ni chakula gani unapaswa ukile, maana vyakula ni vingi vijengavyo na vibomoavyo, Hivyo ni kuwa makini kujua ni chakula kipi ule na kipi usile kwa usalama wa roho yako na hatma yako ya milele.

Tunaishi katika kipindi cha hatari ambacho hakijawahi hata kutokea katika vizazi vyote vya nyuma, ambacho kina mchanganyiko mkubwa wa MANABII WA UONGO NA MANABII WA KWELI, Na wote wanafanya kazi moja ya KUVUNA ROHO ZA WATU, aidha kuzipeleka kuzimu au mbinguni, ni kipindi cha hatari sana tunachoishi. Ni muhimu kufahamu unavunwa upande gani, ili usije ukajikuta unadondokea sehemu ambayo haujatarajia.


UPOTOFU ULIOPO SASA:
Jambo kubwa linalowachanganya watu wengi ni kuona pale mtu anayejiita mtumishi wa Mungu halafu bado ni mwasherati, mtukanaji, mlevi, anapenda anasa, na bado miujiza inatendeka na yeye, anafufua wafu, anaombea watu wanaponywa, anatabiri na unabii unakuja kutimia, ananena kwa lugha n.k. kiasi ambacho kinamfanya mtu mchanga ashindwe kuelewa inawezekanikaje huyu mtumishi anafanya mambo ya kidunia lakini bado ishara na miujiza zinatendeka na yeye, Na wala hatumii uchawi ila  anatumia jina la YESU na nguvu za Mungu zinashuka. "HII NI SIRI" na ni jukumu kwa kila mkristo anayethamini maisha yake ya kiroho kufahamu..kumbuka (kuna wanaotumia nguvu za giza kutenda miujiza, siwazungumzii hao, hao ni rahisi kuwagundua lakini nawazungumzia wale wanaotumia nguvu za Mungu ambao ni ngumu kuwatambua.)


Tusome, mstari ufuatao unawazungumzia hao wanaotumia nguvu za Mungu ; kumb.13:1-5"
1 Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,
2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;
3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.
4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.
5 Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya Bwana, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru Bwana, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako. "

Unaona hapo? Huyo nabii hapo katoa unabii kwa uweza wa nguvu za Mungu na ikatokea, lakini anawafundisha watu waende kinyume na maagizo ya Mungu. Vivyo hivyo na hata sasa katika kipindi hichi cha mwisho Mungu ameamua kuachia mvua yake (UPAKO) kwa watu wote waovu na wema kutujaribu sisi kama TUNAMPENDA BWANA NA KUYASHIKA MANENO YAKE AU LA!. 
 Mtu anaweza akaja kwako na kutoa unabii na ukatimia na kufufua wafu, na kuponya wagonjwa lakini akafundisha injili nyingine akakwambia  ulevi ni sawa, wanawake kwenda na mitindo ya kisasa ni sawa (anasema Mungu haangalii mavazi anaangalia roho ), akakufundisha kuupenda ulimwengu ni sawa, kuoa wake wengi ni sawa, Dunia haiishi leo wala kesho kula maisha, kuwa na pesa nyingi ndio kigezo cha kubarikiwa na Mungu, Mungu siku zote ni Mungu mzuri na hawezi kuwahukumu watu aliowaumba. n.k. na bado mtu huyo akatoa mapepo na kufufua wafu. Na wewe kwasababu NENO na kumpenda Mungu hakupo ndani yako, ukadhani anazungumza ukweli au katumwa na Mungu kwasababu tu! ametoa unabii ukatokea, NDUGU USIDANGANYIKE UMEPOTEA!! .  Biblia inasema jiepushe na huyo mtu, CHUKUA TAHADHARI KWA USALAMA WA MAISHA YAKO..KIMBIA! HARAKA SANA NI BWANA NDIYE ANAYEKUJARIBU KUONA KAMA UNAMPENDA KWELI NA KULIFUATA NENO LAKE AU LA!
 
Leo hii wewe unayejiita mkristo unapenda injili za kufarijiwa tu! siku zote unapendwa kuambiwa "ALL IS WELL" ulimwengu hautakuja kuteketezwa,tunaishi chini ya neema, mafundisho unayoyapenda wewe ni KUTABIRIWA MAFANIKIO TU!. Lakini fahamu jambo moja BWANA YESU hakuacha enzi na mamlaka mbinguni ili aje kutufia sisi mlabani tuwe MABILIONEA, bali kwa ajili ya dhambi zetu.(hicho ndicho kiini cha injili) yeye mwenyewe alizungumza ..mathayo 16:24-27

" Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.
25 Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.
26 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 
Leo mkristo anadai anamfuata YESU, lakini kigezo cha kumfuata YESU ni kuwa na MSALABA wako, sasa wewe MSALABA WAKO UKO WAPI?, Jihadhari na haya mafundisho ya uongo yanawapeleka maelfu wa waaminio kuzimu kila siku pasipo wao kujua.

Hawa manabii wa uongo, Bwana Yesu alisema tutawatambua kwa  MATUNDA YAO na sio kwa upako wao, kwasababu Mungu anaweza akamtumia mtu kama chombo tu cha kuazima akishamaliza shughuli nacho anakiacha, mfano tunaona Mungu alimtumia Punda kuongea na Nabii Balaamu kumpa ujumbe, lakini baada ya punda kutoa ujumbe alirudia katika hali yake ya kawaida ya upunda, vivyo hivyo na Balaamu mwenyewe alikuwa ni MCHAWI lakini Mungu alimtumia yeye kuwabariki Israeli, (hesabu 22:21-29), Na pia Mungu aliwatumia wale manabii 400 kumdanganya mfalme Ahabu kwasababu Mungu alikuwa amekusudia mabaya juu yake. (1 wafalme 22:6). Kwahiyo kuwa na upako mtu kuona maono, au kuwa nabii, au kunena kwa lugha au kuponya au kufanya miujiza yoyote ile, sio kigezo cha huyo mtu kuwa NABII WA MUNGU. Tutatawatambua kwa matunda yao (AMBAYO NI NENO LA MUNGU). Nabii wa ni yule anayekuja na ishara pamoja na NENO lakini lililokuu ni NENO.


Kipime mtu anachokuambia je! kinaendana na NENO la Mungu? kama hakiendani na NENO la Mungu weka kando haijalishi anawashirika wengi kiasi gani, au anakubalika kiasi gani, au kanisa ni kubwa kiasi gani, au anaupako kiasi gani. KIMBIA! HILO NI SINAGOGI LA SHETANI!.. 


  • Ukiona unadumu kwenye mafundisho yanayokupeleka wewe kuutazama ulimwengu kuliko kumtazama KRISTO! KIMBIA!  KWA USALAMA WA MAISHA YAKO!!.
  • Ukiona unahubiriwa injili za mafanikio tu! Haufundishwi kufikia toba, au utakatifu maana biblia inasema pasipo huo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu (waebrania 12:14). KIMBIA!
  • Ukiona unahubiriwa injili ya kutoa tu! kutoa tu! toa zaka, panda mbegu, n.k. Lakini NENO halihubiriwi, ONDOKA HAPO! Bwana Yesu alisema hivi..mathayo 23:23-24"Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. VIONGOZI VIPOFU, WENYE KUCHUJA MBU NA KUMEZA NGAMIA. " ...KIMBIA! JIOKOE NAFSI YAKO.
  • Ukiona unaenda katika nyumba ya Mungu, hauhubiriwi NENO bali SIASA, usitazame nyuma hata kama kuna miujiza inatendeka kiasi gani....KIMBIA KAMA UNAIPENDA NAFSI YAKO!
  • Ukiona kiongozi wako wa dini, Anaelekeza watu kwake, na sio kwa KRISTO, anajisifu na kujitukuza yeye, utukufu wa Mungu anauchukua yeye.Hapo  hapana tofauti na ibada za sanamu, fahamu kuwa unamwabudu mtu na sio Mungu, isaya 42:8" Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu. ".usimsikilize nabii huyo biblia inasema hivyo... KIMBIA!
Jiulize Wewe unayejiita mkristo  tangu ulipoamini, maisha yako ya kiroho yamesonga mbele kiasi gani. utakuwaje mkristo halafu biblia husomi!??  sasa utawatambuaje manabii wa uongo au manabii wa ukweli kwa namna hiyo watakapokujia na mafundisho yao??. Utakuwa unapelekwa na kila upepo unaokuja wa elimu yoyote. Maana njia pekee ya kumpima nabii wa uongo au Nabii wa ukweli ni kwa NENO TU!. Na sio kitu kingine. Jijengee kila siku tabia ya kusoma NENO na kuomba. Hizi ni nyakati za hatari tunaishi zile zilizotabiriwa kuwa watatokea manabii na makristo wengi wa uongo nao watawadanganya wengi yamkini hata walio wateule. Kumbuka ni wateule ndio wanaozungumziwa hapo kuwa wanaweza wakadanganywa sasa jiulize wewe ambaye sio mteule utaonekania wapi? wewe ndio hautaelewa chochote kinachoendelea utaishia kuwashangilia na kuwasifia kama Bwana Yesu alivyotabiri juu ya manabii wa uongo.


2 Petro 1:10" Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe."
KWAHIYO NDUGU HUU NI WAKATI WA MUNGU KUTUJARIBU SISI KAMA TUNAMPENDA YEYE NA KULISHIKA NENO LAKE AU LA!. Biblia inasema, MPENDE BWANA MUNGU WAKO, KWA MOYO WAKO WOTE, KWA ROHO YAKO YOTE, KWA NGUVU ZAKO ZOTE, NA KWA AKILI ZAKO ZOTE.
 
Mungu hadhihakiwi usipoweza kufanya hivyo jua tu utaangukia kwenye huu mstari ufuatao;

2 Thesalonike 2:10-12"... na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.
11 KWAHIYO MUNGU AWALETEA NGUVU YA UPOTEVU, WAUAMINI UONGO;12  ILI WAHUKUMIWE WOTE ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu. "

MARAN ATHA!

No comments:

Post a Comment