"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Monday, April 24, 2017

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?


Tukisoma kitabu cha mwanzo 1, Biblia inasema Hapo mwanzo, Mungu aliziumba mbingu na nchi. Lakini tunaona hakueleza aliumbaje umbaje hii mbingu na nchi yaani, miti, jua, mwezi, milima, wanyama, mwanadamu n.k.

Lakini tukija kusoma kwenye kitabu cha waebrania 11:3 tunaona

" Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri. "
 Kwahiyo siri inaonekana hapo ni kwamba mbingu na nchi ziliumbwa kwa NENO la Mungu.

Sasa swali linakuja hili NENO ni nini?
Tukisoma Yohana 1:1-3"
1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. "
Kwahiyo kulingana na mstari huu biblia inaeleza kuwa Neno lilikuwapo kwa Mungu, na lilikuwa ni Mungu, maana halisi ya "Neno" kulingana na tafsiri ya Kigiriki iliyotumika ni WAZO au NIA. Kwahiyo wazo lilikuwapo ndani ya Mungu, Na hivyo vitu vyote vilivyoumbwa vimetoka katika hilo wazo la Mungu mfano dunia, malaika, wanadamu, sayari, miti n.k. 

Mfano mzuri ni kama wewe kitu chochote ulichokitengeneza kama nyumba, kiti, meza, nguo, vilitoka kwanza katika wazo lako au nia yako. Hii ikiwa na maana kwamba kama usingekuwa na hilo wazo usingeviumba vitu hivyo vyote, Vivyo hivyo na kwa Mungu pia kama WAZO  lake (ambalo ni Neno lake) asingekuwa nalo hapo mwanzo asingeweza kuumba chochote.

Kwahiyo kabla ya mwanadamu kuasi hili NENO lilikuwa pamoja na mwanadamu, Mtu alikuwa na ushirika na Mungu kwa asilimia zote, kwasababu NENO lilikuwa ndani yake kama lilivyokuwa ndani ya Mungu kitu kilichomfanya mpaka mwanadamu kuonekana kuwa kama mfano wa Mungu, Adamu alikuwa na mamlaka yote duniani, kama vile YESU leo alivyo na mamlaka yote duniani na mbinguni biblia inasema hivyo. Na ndio maana utajua sababu ya Mungu kutuita sisi ni miungu duniani, Na yeye ni MUNGU WA miungu.
Lakini baada ya anguko Adamu aliyapoteza yote aliyokuwa nayo kwasababu alijitenga na NENO la Mungu kwa kutokutii. Hivyo yeye na NENO (nia ya Mungu) vikawa ni vitu viwili tofauti. Kuanzia wakati huo baada ya anguko, lile NENO likaanza kumtafuta tena mwanadamu limrudishe tena katika ile hali ya kuwa na mahusiano na Mungu na mamlaka yote aliyokuwa nayo kabla hajayapoteza. Na ndio maana kuna mahali Yesu alisema sio ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua nyinyi.

Sasa tangu huo wakati lile NENO likaanza kutafuta njia nyingi za kumrejesha mwanadamu, likaanza kuzungumza na wanadamu kwa kupitia MBINGU, nyota,sayari na kwa  vitu vya asili, kwa dhumuni la kumrejesha tu, lakini mwanadamu bado hakutaka kutega sikio lake kusikia.

Baadaye lile NENO likaanza kuzungumza kupitia watu, mfano manabii wa Mungu, tunaona manabii kama Henoko, Nuhu, Ibrahimu, Musa, Eliya, Danieli, Yeremia, Isaya n.k..lilisema nao kwa nguvu na kwa udhihirisho mwingi liliwapigia kelele wanadamu wamrudie Mungu, warudi  katika ule ushirika waliokuwa nao kwanza na Mungu. Lakini wanadamu bado hawakutega sikio lao kulisikia, zaidi ya yote waliwaua manabii waliotumwa kwalo.

Lakini japokuwa NENO hili limezungumza mara zote hizi kwa vizazi na vizazi kupitia vitu vya asili na manabii, bado ule uhusiano uliokusudiwa mwanadamu awe nao na Mungu wake haukufanikiwa kurejeshwa kwasababu ya ugumu wa mioyo ya wanadamu. 

Ndipo wakati ulipofika lile Neno likaona liuvae mwili, lije lenyewe katika mwili,liishi na wanadamu, lihubiri mambo yote lililohubiri ndani ya manabii na vitu vya asili kwa kusudi lile lile la  kumrejesha mwanadamu  kwa muumba wake. Hili jambo linazungumziwa kwenye..
Waebrania 1:1-2" Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. " ...Sasa umeona mwisho wa yote Neno limekuja kuzungumza na sisi kupitia nini? sio kanisa wa chochote bali mwana.

Hili NENO likajichagulia mwili unaoitwa YESU KRISTO, Haleluya! ni furaha kiasi gani Mungu alivyojirahisisha kwetu sisi ili tukae na hilo NENO kwa jinsi ya kimwili, likiongea, likifundisha, likijibu maswali, likitembea na sisi wazi kabisa, linafurahi na sisi, kitu ambacho hapo mwanzo ilikuwa ni ngumu kulielewa lizungumzapo lakini hapa lipo pamoja nasi (IMANUELI)..Embu tutazame mstari ufuatao;

 1 Yohana 1:1-3"
1 Lile lililokuwako tangu mwanzo, TULILOLISIKIA, TULILOLIONA kwa macho yetu, TULILOLITAZAMA, na mikono yetu IKALIPAPASA, kwa habari ya NENO la uzima;
2 (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);
3 hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. "
..Habari hiyo inaelezea lile NENO ambalo zamani lilikuwepo lakini sasa limefanyika mwili na lipo katikati yetu kama mwanadamu.

Hivyo basi BWANA YESU KRISTO alipokuja akaanza kutufundisha na kuturejesha katika utimilifu wote na Mungu tuliokuwa nao pale Edeni hata na zaidi ya pale.,Jambo la kwanza alilolifanya ni kutupatanisha sisi na Mungu kwa kumwaga damu yake kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu maana biblia inasema pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo (waebrania 9:22)

Na jambo la pili ni kutufanya sisi kuwa wana wa Mungu (miungu),
Yohana 1:12 "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; " Tukisoma 

2 wakoritho 5:18-19 "Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu NENO la upatanisho. "
Kama tulivyosema lile NENO ni wazo/nia ya MUNGU nalo ni Mungu, ikiwa na maana usiipotii nia ya Mungu haujamtii Mungu. Na nia ya Mungu ni nini? Ni kuturujesha sisi tuwe na mahusiano naye kama ilivyokuwa hapo mwanzo ili tumwabudu MUNGU katika Roho na Kweli. Na ndio maana WAZO/NIA yake iliuvaa mwili kwa dhumuni la kutuhubiria sisi tumgeukie Baba. Kwasababu hiyo basi Yesu Kristo ndiye NJIA, NA KWELI, NA UZIMA, MTU HAFIKI KWA BABA ISIPOKUWA KWA NJIA YAKE YEYE.(Yohana 14:6), alisema aliyeniona mimi amemwona BABA, usipomtii YESU KRISTO na kumwamini umeukataa mpango wa Mungu kwa wanadamu na viumbe vyake vyote kama shetani alivyofanya. 

Natumaini utakuwa umeshaiona sababu ya YESU KRISTO Kutokea ni nini?, ni hiyo hapo juu, Neno la Mungu liliuvaa mwili, kutuhubiria sisi na kuturejesha kwa Mungu wetu ili tumwabudu yeye katika roho na kweli. 

Wakolosai 2:9 "Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. "
Kwahiyo Mungu hana nafsi tatu, Nafsi ya Mungu ni moja tu. Mungu kuonekana katika mwili hakumfanyi yeye kuwa na nafsi tatu. Alifanya hivyo tu ili kutupatanisha sisi na yeye. Kama tusingeanguka katika dhambi kulikuwa hakuna haja ya yeye kuuvaa mwili na kuja duniani, Yeye ni Roho nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

NEEMA YA BWANA YESU KRISTO IWE PAMOJA NAWE!

No comments:

Post a Comment