"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, January 26, 2017

MASWALI YALIYOULIZWA NA MAJIBU YAKE: SEHEMU YA 10


SWALI 1: Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi?

JIBU: Tukisoma;

Mathayo 12:25-32 " Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo.
25 Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama.
26 Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?
27 Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu.
28 Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.
29 Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake.
30 Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
31 Kwa sababu hiyo nawaambia, KILA DHAMBI, NA KILA NENO LA KUFURU, watasamehewa wanadamu, ILA KWA KUMKUFURU ROHO HAWATASAMEHEWA.
32 Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. "

Tunavyosoma mistari hiyo tunaona kabisa wale Mafarisayo  walikuwa wanajua Bwana Yesu  ni kweli alikuwa anatoa pepo, na kutenda mambo yote  kwa uweza wa  Roho wa Mungu, lakini wao kwa ajili ya wivu, na kwa tamaa zao wenyewe,ili tu wawavutie watu kwao, wakakusudia kwa makusudi kabisa, wawageuze watu mioyo ili watu wasimuamini Bwana Yesu,wawaamini wao, na ndipo wakaanza kutoa maneno ya makufuru wanawaambia watu kuwa BWANA anatoa pepo kwa uwezo wa belzebuli mkuu wa Pepo angali ndani ya mioyo yao walikuwa wanajua kabisa anachofanya ni kwa uweza wa Roho wa Mungu.

  Ukweli wa jambo hilo unajidhihirisha   kwa Nikodemo ambaye naye alikuwa ni mmoja wa wale  mafarisayo alipomwendea Yesu usiku na kumwambia

Yohana 3:1-2"Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi.
2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, RABI, "TWAJUA" YA KUWA U MWALIMU, UMETOKA KWA MUNGU; KWA MAANA HAKUNA MTU AWEZAYE KUZIFANYA ISHARA HIZI UZIFANYAZO WEWE, ISIPOKUWA MUNGU YU PAMOJA NAYE. "

kwahiyo unaona walikuwa wanajua kabisa lakini kwa ajili ya wivu wakaanza kuzusha maneno ya uongo juu ya kazi ya Roho wa Mungu, sasa huko ndiko kumkufuru Roho Mtakatifu. hivyo basi Bwana Yesu alitoa angalizo tunapozitazama kazi za Mungu, pale mtu mwenye Roho wa Mungu anatenda kazi za Mungu kweli  huku tunajua ni Mungu ndiye anayefanya kazi ndani yake, na kuanza kusema yule ni mchawi, au anatumia uchawi, au mshirikina, au tapeli, au mwizi, ili tu watu wasiziamini kazi za Mungu au vinginevyo, au unaanza kuzusha propaganda za uongo juu yake, pengine kwa kusudi la kumkomoa! hapo ndugu utakuwa unajimaliza mwenyewe. (Ni kweli si watumishi wote ni wa Mungu,hao ni sawa kuufunua uovu wao). Lakini Hapa tunamzungumzia yule unayemfahamu kabisa ni mtumishi wa BWANA,..wewe hujui umewakosesha wangapi, ambao kwa kupitia yeye, watu wengi wangeokolewa? kufanya hivyo ni hatari sana tuwe makini.

Hivyo hii dhambi unawahusu wale wanaozipinga kazi za Mungu kwa makusudi kabisa(Mfano wa mafarisayo). Hao kwao hakuna msamaha, hawawezi tena kutubu hata iweje wanachongojea ni ziwa la moto.

Lakini shetani naye anapenda kulitumia hili neno kuwafunga watu wajione kuwa wamemkufuru Roho Mtakatifu na kwamba dhambi zao hazisameheki hata wafanyeje,

Hii inakuja sana sana kwa watu waliowachanga ki-imani, kuna shuhuda nyingi za watu waliofungwa na shetani kwa namna hiyo wakidhani kuwa dhambi zao hazisameheki, kuna watu wamekata tamaa wanajiona kwa wingi wa dhambi zao, Mungu hawezi kuwasemehe tena, pengine wameua, wametoa mimba sana, n.k, Sasa jambo la namna hii likija katika mawazo yako likatae linatoka kwa yule mwovu kukufanya wewe ujione kuwa Mungu hawezi kukusamehe umemkufuru, hivyo usijisumbue kutubu kwasababu Mungu hatakusikiliza.

Kumbuka kama tulivyosema Dhambi hii inakaa kwa wale watu ambao ndani yao mioyo ya toba imekufa, au hofu ya Mungu haipo tena kwao, watu waliojikinai, wanaompinga Mungu katika fikra zao japo kuwa walimjua Mungu na uweza wake wote, wanazipotosha kazi za Mungu kwa makusudi kwa faida zao wenyewe,ili wawavute watu kwao, au wawe washirika wao na sio kwa Mungu. Hivyo basi kitendo tu cha wewe kuwa na hii hofu ya kumwogopa Mungu ujue Roho wa Mungu anatenda kazi ndani yako na hayo mawazo ya kwamba umemkufuru Roho Mtakatifu yapinge huyo ni adui ndio moja ya njia zake hizo ili usiufikie wokovu  na anapenda kuwatesa watu wengi katika andiko hili.

SWALI 2: Je!  Kuna dhambi kubwa na ndogo, na kama hakuna je! Mtu aliyeua na aliyetukana je watapata adhabu sawa?

JIBU: Dhambi ni dhambi iwe kubwa au ndogo, zote ni kosa, biblia inasema. 

Yakobo 2:10-11 "Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.
11 Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria. "

Unaona hapo? Kwahiyo mtu akitenda dhambi iwe kubwa au ndogo ataadhibiwa. lakini adhabu zitatofautiana huko waendako, kwasababu  Bwana Yesu pia alisema aliyeua kwa upanga atauawa kwa upanga, apandacho mtu ndicho atakachovuna. adhabu ya shetani haiwezi ikawa sawa na adhabu ya mwanadamu. Biblia inaeleza..

luka 12:47-48"Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, ATAPIGWA SANA.
48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, ATAPIGWA KIDOGO. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi. "

kwahiyo mapigo yanatofautiana kulingana na matendo ya mtu aliyoyatenda akiwa hapa duniani, ni kama tu vile thawabu zitavyotofautiana kwa mtu na mtu mbinguni kwa jinsi alivyotaabika katika kumtumikia Bwana vivyo hivyo na jehanamu adhabu zitatofautiana kulingana na dhambi mtu alizotenda akiwa ulimwenguni. Hivyo hatupaswi kuipima dhambi kwa namna yoyote, ni kukaa nayo mbali kwasababu  iwe ni kubwa au ndogo mshahara wake ni MAUTI, warumi 6:23.

SWALI 3:
Katika amri kumi za Mungu, Amri ya sita inasema "usiue" lakini sisi tunaua baadhi ya viumbe kwa ajili ya kitoweo n.k. sasa basi ni nini tunapaswa kuua na ni kipi hatupaswi kuua?

JIBU: tangu mwanzo haikuwa mapenzi ya Mungu sisi kuua kiumbe chochote kwa matumizi yoyote yale, lakini baada ya anguko Mungu aliyaruhusu hayo yatendeke kwa makusudi maalumu kama kwa ajili ya chakula, mavazi, na matumizi mengine yoyote ambayo ni halali. Na ndio maana tunaona hata baada ya Adamu kuasi Mungu alikuwa wakwanza kuwachinjia mwanakondoo na kuwavika ngozi yake kama mavazi. Na pia tunaona wanyama walichinjwa kwa ajili ya kumtolea Mungu sadaka ya kuteketezwa n.k.
Hivyo basi kwa kuua mnyama yeyote kwa ajili ya matumizi maalumu kama kwa chakula au vinginevyo sio dhambi lakini utakapomuua bila sababu yoyote maalumu, Mungu atakuhesabia makosa. kwahiyo hapo unaona kikubwa ni sababu(motive) ya wewe kumuua huyo mnyama. Utakuta mtu anamuua mnyama pasipo sababu yoyote na hana madhara yoyote katika jamii, wengine wanawaua wanyama kwasababu wanawachukia tu. Lakini kuna faida na thawabu nyingi tunapowahurumia wanyama na kuwatunza ikiwemo kuongezewa siku za kuishi soma;
kumbukumbu 22:6" Kiota cha ndege kikitukia kuwa mbele yako njiani, katika mti wo wote, au chini, chenye makinda au mayai, naye koo ameatamia juu ya makinda, au juu ya mayai, usimtwae yule koo pamoja na makinda;
7 sharti umwache yule koo aende zake, lakini makinda waweza kuyatwaa uwe nayo; ili upate kufanikiwa, ufanye siku zako kuwa nyingi. " umeona kwa kufanya hivyo tu Mungu anakuongezea siku zako za kuishi.
lakini haya yote ya kuua, kuchinja n.k. Mungu ameyaruhusu kwa muda tu, tutakapokuja kutawala na Kristo hapa duniani kwa muda wa miaka 1000, mambo yote yatarejeshwa kama ilivyokuwa Edeni ya mwanzo, kutakuwa hakuna kuua wanyama. Na wanyama pia hawatauana tutaishi wote kwa amani. soma..
isaya 11:6-9 "  Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.
7 Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe.
8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.
9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari. " 

Na pia tukisoma warumi 8:19"19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.
20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini;
21 kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa."

kwahiyo haya mambo ya kuua wanyama ni ya muda tu. unaweza ukaua chochote (ila sio mtu), lakini kiwe ni kwasababu maalumu tu na si vinginevyo zaidi ya hapo ni dhambi. 
Mungu akubariki.

Tuesday, January 17, 2017

UZAO WA NYOKA.

Karibu tujifunze Neno la Mungu....Tumezoea kula vyakula vilaini, kila siku maziwa, , tutakua lini?? Ni vizuri tuanze kujifunza kula vyakula vigumu pia ili tukue tuzidi kumjua Kristo katika utimilifu wake wote, Leo tuutazame uzao wa nyoka mwanzo wake na ulipofikia sasa kwa msaada wa Kristo..

Mathayo 12:34 "Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake"
Mahali pengine Bwana Yesu alisema:
mathayo 23:31-33 "Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii.
32 Kijazeni basi kipimo cha baba zenu.
33 Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?"

   
Na Yohana mbatizaji aliyarudia haya maneno, tunayaona kwenye luka 3:7 " Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?" 


 
Maneno haya yanathibitisha kuwa uzao wa nyoka upo, na ndio umekuwa adui wa uzao wa Mungu tangu vizazi hata vizazi, Tuufatilie huu uzao wa nyoka umeanzia wapi, na chimbuko lake ni wapi, na ni akina nani hawa wanaitwa uzao wa nyoka?.

Tumeona jinsi mti wa uzima na mti wa ujuzi wa mema na mabaya una maana gani, kama hujafahamu soma somo nililoliandika kabla ya hili " MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA" ili tuteremke vizuri pamoja.


Tunafahamu kuwa kitendo kilichotendeka kwenye bustani ya Edeni ni kwamba Hawa alifanya uasherati na nyoka kisha akaenda kufanya na mume wake ikapelekea Hawa kubeba mimba ya watoto wawili mapacha wasiofanana, kila mmoja akiwa na baba yake tofauti, Habili baba yake akiwa ni Adamu na Kaini baba yake akiwa ni nyoka. 


Jambo hili linawezekana kibaolojia na ni jambo la kawaida linalotokea mara kwa mara duniani, kwamba mama mmoja ana uwezo wa kukutana kimwili na wanaume wawili tofauti na kusababisha kubeba mimba ya watoto wawili wa baba tofauti tazama picha hapa chini,





Ni dhahiri kuwa nyoka hakuwa kama jinsi tunavyomuona leo akitambaa kwa tumbo, hana mikono wala miguu bali alikuwa hivyo baada ya kulaaniwa, lakini kabla ya kulaaniwa alikuwa ni mnyama anayekaribiana sana na mwanadamu soma mwanzo 3:14, hivyo baada ya mwanadamu alikuwa anafuata nyoka kisha nyani, kisha wanyama wengine, kwahiyo nyoka alikuwa ana uwezo wa kuzungumza kama mwanadamu,kutafakari, na alikuwa na mikono na miguu miwili kama mtu, Mungu alimuumba kwa kusudi la kumsaidia mwanadamu katika shughuli zake za karibu na kama biblia inavyosema amelaaniwa kuliko wanyama wote ina maanisha alikuwa juu ya wanyama wote na alikuwa mwerevu mbali na wanyama wengine.


Lakini tunaona shetani baadaye alikuja kumwingia nyoka na kwenda kumdanganya Hawa asimtii Mungu ikapelekea kwenda kufanya kitendo cha uasherati. mwanzo 3:20 "Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai." biblia ilimwita Hawa kuwa mama wa wote walio hai lakini haikumwita Adamu baba wa wote walio hai. Hii ikiwa na maana kwamba wote walitoka kwa Hawa lakini sio wote waliotoka kwa Adamu.


Jambo linalowachanganya wengi ni pale mwanzo 1:4 inaposema"



1 Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana.
2 Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.
3 Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana."
Hapa tunaona Adamu alimjua Hawa mara moja tu, na sio mara mbili, maana alimzaa Kaini akamwongeza na Habili ni kitendo kimoja kimezaa watoto wawili ambao ni pacha wasiofanana,kitendo cha "kuongeza" hakimaanishi "kumjua" tena. Na pia tukichunguza kitabu cha mwanzo jinsi kilivyoandikwa matukio hayajakaa katika mfululizo, huwa kuna kwenda mbele na kurudi nyuma. kwamfano ..



*Kwenye sura ya kwanza Mungu aliziumba mbingu na nchi na miti na wanyama, na wanadamu huko huko(mwanamke na mwanaume) akamaliza kila kitu na siku ya 7 akapumzika,

* Lakini kwenye sura ya pili tunaona tena Mungu anamwumba Adamu tena kutoka ardhini, na Hawa akaja kumuumba baadaye kutoka kwa Adamu, kitendo ambacho tunajua kilishakamilika tangu sura ya kwanza, vivyo hivyo na mimea na wanyama, waliumbwa kutoka ardhini tena.


* Vivyo hivyo kwenye sura ya tatu inaeleza Adamu na Hawa walivyokula tunda na kufukuzwa katika bustani ya Edeni,

*Lakini sura ya nne inaelezea ni jinsi gani Adamu Alivyokula lile tunda kwa kumjua mkewe na kupata mimba na kuzaa watoto wawili.


Hivyo basi Kaini alipozaliwa alibeba tabia za baba yake nyoka na ndio maana tunaona tu baada ya kutoka bustanini alimwamkia ndugu yake na kumuua,hakuwa hata na muda wa kutubu, wivu na hasira vilimtawala hivyo tujiulize alivitolea wapi hivi? kwanini ndugu yake Habili hakuwa navyo jibu ni dhahiri kabisa alivibeba kutoka kwa baba yake nyoka, tunaona ni ile ile roho ya shetani ambayo ilitenda kazi ndani ya nyoka mwanzoni ndiyo inayotenda kazi ndani ya Kaini. 


Jambo hili hili tunaona likizidi kuendelea katika uzao wa Kaini, ukifuatilia vizuri utaona Lameki mzao wake alikuwa ni muuaji kushinda hata baba yake Kaini mwanzo 4:23-24"3 Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;
24 Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba.
" na pia tunaona tabia nyingine za kuoa wanawake wengi zilitokea katika huu uzao wa Kaini(ambao ni uzao wa nyoka). Lameki alioa wake wawili kitu ambacho Mungu hakumwagiza Adamu wala uzao wake wala hakikuonekana mahali popote katika uzao wa Mungu.


Pia tunaona huu uzao kutoka kwa baba yao Kaini Mungu aliwatia alama, baada ya Kaini kumuua ndugu yake


mwanzo 4:13-15 " Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.
14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.
15 Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. "

Kwahiyo hii alama Bwana aliyomtia Kaini sio alama kama chapa fulani kwenye mwili wake (tatoo) , Bali Mungu alimwongezea ukubwa wa mwili wake na akili nyingi (inteligency) yeye na uzao wake, tunaona katika kipindi cha Nuhu ule uzao wa Kaini ulikuwa ni wa watu wakubwa walioitwa "majitu (wanefili)" kwahiyo kwa ukubwa huu mtu yeyote asingeweza kupigana nao au kuwatishia, na kwenye upande wa akili tunaona katika mwanzo 4 wana wa Kaini walianza kuwa na ustaarabu mkubwa kwa haraka kama ugunduzi wa vyuma, shaba, ustadi wa vyombo vya miziki n.k.waliitwa watu hodari na wenye sifa wakati ule (soma mwanzo 6:4) inaelezea..wao ndio waliotengeneza mapiramidi ambayo yamesimama mpaka leo, kama tunavyojua hata leo taifa lenye ujuzi mwingi kwa teknolojia kubwa ni dhahiri kuwa taifa hilo litaogopeka na hakuna mtu atayakayedhubutu kwenda kulidhuru ndivyo ilivyokuwa kwa Kaini na uzao wake, Mungu alimpa ukubwa na ujuzi mwingi ambao ulikuwa kama ulinzi kwake ili mtu atakapomuona asimdhuru..


Lakini ule uzao mwingine wa Adamu ambao ni uzao wa Mungu wao walikuwa ni wafugaji tu na wakulima, na walikuwa ni wanadamu wenye miili ya kawaida. hawakuwa hodari katika nchi, mtazamo wao ulikuwa kwa Mungu na ndio maana tunaona walianza kuliitia tu jina la Mungu pale walipoanza kukaa katika nchi,

mwanzo 4:25-26" Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.
26 Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana. "

Tunaona katika kipindi hicho chote uzao wa Adamu ulikuwa dhahiri na unaonekana na uzao wa nyoka pia ulikuwa dhahiri na unajulikana kwa tabia na kwa kuutazama. Wana wa Adamu wote walikuwa wanaitwa ''WANA WA MUNGU'' na wana wa Kaini walikuwa wanaitwa "WANA WA BINADAMU" kulingana na
mwanzo 6:1-4 " Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,
2 wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.
3 Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.
4 Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile;tena ,baada ya hayo ,wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu,wakazaa nao wana;hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani ,watu wenye sifa. "
Kuna baadhi ya mitazamo inayosema kuwa hawa wana wa Mungu walikuwa ni malaika, na kwamba walikuja na kuzini na wanadamu, ndipo wakazaliwa wanefili lakini mtazamo huo sio kweli kwasababu, kwanza tunaona wanafili walikuwepo duniani kabla hata ya hao wana wa Mungu kuzini na binti za binadamu, na pia malaika hawana miili zile ni roho zitumikazo (waebrania 1:14), Hivyo hawawezi kukutana kimwili na wanadamu, lakini pia tunaona baada ya wana wa Mungu kuzini ni binti za binadamu Mungu aliwahukumu wanadamu na sio malaika kuonyesha kuwa wanadamu ndio waliohusika na hicho kitendo na sio malaika (mwanzo 6). tuendelee kujifunza..

 
Baada ya watu kuongezeka na kuwa wengi duniani, wana wa Mungu(uzao wa Adamu) waliwatamani binti za wanadamu(binti za Kaini) waliwaona ni wazuri, wenye mitindo ya kisasa, wanaopaka lipstick,wanaovalia nusu-uchi,wanaopaka wanja, wenye ujuzi wa kujipamba kwa manukato ya kila aina,waliojaa macho ya uasherati na ukahaba,wanaoenda na wakati(fashion) kwa mitindo ya kisasa huu ni mfano tu dhahiri wa wanawake tulionao sasa. Waliacha kwenda kuoa wake zao(binti za Mungu) ambao walikuwa ni wacha Mungu,wastaarabu, wanaojiheshimu kwa mavazi na tabia njema, mabikira, wasioendana na fashion za ulimwengu, lakini wao wakawaona kama washamba, hawafai, wakaenda kujitwalia binti za wanadamu wakazaa nao watoto Ikapelekea kuchanganya mbegu, wana wa Mungu wakaacha kumwangalia BWANA tena, wakaanza kuupenda ulimwengu kitu kilichomkasirisha sana Mungu na ndipo Bwana akaghairi na kusema Moyo wangu hautashindana na mwanadamu milele,basi maovu yakaendelea kuzidi kuwa mengi duniani, vitendo viovu, ukatili,ushoga,uuaji, usengenyaji, uzinzi, ulevi,rushwa kukawa hakuna tena wacha Mungu, Dunia ikaharibika sana, mambo yasiyofaa yaliujaza ulimwengu kama siku zetu hizi za leo, maana Bwana alisema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu ndivyo itakavyokuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu. Na ndipo hapo Mungu akakusudia kuiteketeza dunia katika gharika.


Lakini Nuhu ambaye alikuwa ni wa uzao wa Mungu (uzao wa Adamu) alipata neema, japo na yeye alikuwa na mke aliyechanganyikana na uzao wa Kaini, na kusababisha kupata watoto wale watatu waliochanganyikana Hamu,Shemu na Yafethi..Tunafahamu Bwana Mungu aliuangamiza ule uzao wote halisi wa nyoka kwenye gharika, Ule uzao wote uliondoka Hakukuwa tena na uzao halisi wa nyoka baada ya pale, lakini kutokana na kile kitendo cha kuchanganyikana mbegu kulisababisha na wana wa Mungu kubeba zile tabia za nyoka ndani yao, japo hawakutoka katika ule uzao wa nyoka. na ndio maana tunaona zile tabia ambazo zilikuwa kipindi cha nyuma zilianza kujidhihirisha tena katikati ya wale watoto, tunafahamu Hamu alikuja kuuona uchi wa baba yake,(kulala na mama yake) hii ni dhahiri kuwa haikuwa tabia ya uzao wa Mungu lakini kwasababu mbegu zimeshachanganyikana sio jambo la kushangaza vitendo kama hivyo vya wanyama kutokea maana wanyama ndio wanaolala na mama zao, hivyo kwa nje mtu anaweza akaonekana kuwa ni mwanadamu lakini ndani anayo ile asili (mbegu) ya nyoka.


Na tabia hizo hizo zikaendelea kwa vizazi vyote hadi kufikia wakati wa agano jipya Bwana Yesu Kristo alipoifichua hii "SIRI YA UASI " alipowaambia watu ni wa uzao wa nyoka, sasa unaona asili ya huu uzao wa nyoka umetokea wapi, mtu yeyote ambaye hajazaliwa mara ya pili haijalishi wewe ni nani una asili ya nyoka ndani yako fahamu tu wewe ni mzao wa nyoka, na mtu atauliza nitafahamuje kama mimi ni mzao wa Mungu au uzao wa nyoka? jibu ni rahisi kabisa kama haujazaliwa mara ya pili wewe ni mzao wa nyoka, na uzao wa nyoka wote utateketezwa kwenye lile ziwa liwakalo moto na kiberiti.


Mungu aliiumba mbegu halisi ya mwanadamu lakini baada ya Adamu kuiharibu ile mbegu halisi kwa kuichanganya na mbegu nyingine ikapelekea wote tuingie katika hali ya uharibifu na mauti, hivyo basi Mungu alimuumba Adamu wa pili yaani Yesu Kristo kwa mbegu nyingine isiyoweza kuchanganyikana ili tukizaliwa katika yeye tupate uzima wa milele 1 petro1:23"
Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele. " unaona jinsi ilivyo muhimu kuzaliwa mara ya pili?? Bwana Yesu alisema

yohana 3:3-5"
3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?
5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu."
  
Je! umabatizwa kwa maji na kwa Roho ipasavyo? kubatizwa kwa maji ni kuzamishwa na ni katika  jina la BWANA YESU KRISTO  kulingana na matendo 2:38, na pia unapaswa ubatizwe kwa Roho Mtakatifu(huko ndiko kuzaliwa mara ya pili) ambao huo ndio utimilifu na muhuri wa Mungu juu yako kulingana na waefeso 4:30, biblia inasema wote wasio na Roho wa Mungu hao sio wake warumi 8:9" Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake." kwa hiyo Roho wa Mungu tu peke yake ndiye anayeweza kutoa asili ya uzao wa nyoka ndani ya mioyo ya watu. usijidanganye kwa namna yoyote kuwa unatenda matendo mema, unaenda kanisani, unatoa fungu la 10,unasaidia yatima n.k ukidhani unampendeza Mungu, ndugu kama haujazaliwa mara ya pili kwa ubatizo wa Roho Mtakatifu hauwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni.

Maombi yangu ni wewe ujazwe ROHO MTAKATIFU,
naomba umalizie kwa kusoma kifungu kifuatacho:


Luka 11:9-13" Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
10 Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
11 Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?
12 Au akimwomba yai, atampa nge?
13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

Mungu akubariki.

 

Monday, January 16, 2017

MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA.

Mwanzo 2:8-9 "Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.
9 Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya".
Tukisoma katika mistari hii hapa juu, tunaona kabisa mwanzoni Mungu alipopanda bustani mashariki mwa Edeni Mungu aliiweka miti ya aina tatu bustanini nayo ni:
  • Kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa.
  • Mti wa uzima katikati ya bustani,
  • Na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
Hapa usichanganye hii ni miti aina tatu tofauti yenye tabia tatu tofauti tofauti, tukianzana na mti wa kwanza, 


  1. Kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa
Sasa mti wa aina hii unaozungumziwa hapa biblia inasema Mungu alichepusha katika ardhi ''KILA'' mti unaofaa kwa chakula, tunaona hili neno "KILA" linamaanisha ni miti mingi na sio mti mmoja, mfano wa miti hii ni  mapeasi, matofaa, maembe,mananasi, ndizi, mapasheni,mapapai n.k. hii ni miti aina ya kwanza ya mti ambayo Mungu aliichepusha katika ardhi kwa ajili ya chakula cha mwanadamu kumfaa kwa ajili ya mwili wake na mahitaji yake akiwa bustanini, yeye pamoja na wanyama wake wote Bwana aliompa. Adamu hakupewa masharti juu ya miti hii alikuwa na uhuru wa kula jinsi apendavyo na jinsi atakavyo kama biblia inavyosema. 

      2. Mti wa uzima katikati ya bustani.

Huu ni mti aina ya pili ambao Bwana aliuweka bustanini, tunaona kuwa mti wa pili na watatu imebeba tabia, na hii miti miwili ya mwisho ipo mmoja, mmoja tu. sio mingi kama ile aina ya kwanza ya mti, sasa huu mti wa uzima. Huu mti ulikuwa hauonekani kwa macho, kama miti mingine, na ulikuwa ni mti ambao ukila matunda yake (sio kula kwa mdomo) unapata uzima ambao umebeba ule uzima wa milele. Kwahiyo huu mti Mungu aliuweka kama hazina kwa Adamu endapo ikitokea wameupoteza ule uzima, waende kula matunda yake wapate uzima tena, Mungu kwa kujua kuwa mwanadamu baadaye atapoteza uzima aliuumba huu mti kuwa kama akiba ya tiba baadaye. Na huu mti Adamu hakuwa na matumizi nao kwasababu tayari alikuwa na uzima wa milele ndani yake.

Lakini tunaona baadaye Adamu alipodondoka kwenye dhambi na kupoteza uzima ndani yake alitamani kwenda kula matunda ya mti wa uzima lakini njia yake ilikuwa imeshafungwa ikilindwa mpaka wakati ulioamuriwa wa hiyo njia kufunguliwa ufike.kwahiyo ilipasa mwanadamu aijue hiyo njia ni ipi. soma mwanzo 3:24.  kuanzia hapo wanadamu ndipo walipoanza kufa na kuanza kutafuta suluhisho la kuishi milele tena, na ndipo hapo wanadamu walipoanza kuliitia jina la BWANA, mwanzo 4:26

  Lakini sasa sisi tunaoishi wakati huu wa neema tunajua NJIA ni ipi?... na huo MTI WA UZIMA  ni nani?... na MATUNDA yake ni nini?..na tunajua sio mwingine zaidi ya BWANA wetu YESU KRISTO mwokozi wetu Haleluya!! .Kwa ufafanuzi mfupi wa jambo hili tusome maandiko yafuatayo...

  Yohana 14:6" Yesu akamwambia, Mimi ndimi NJIA, na KWELI, na UZIMA; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi." Unaona hapo!?? hakuna njia yoyote sisi tunaweza kumfikia Baba kama ilivyokuwa hapo mwanzo kabla ya Adamu kuasi isipokuwa kwa njia ya YESU tu!    na pia tena ukisoma
 Yohana 6:47-51" Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna UZIMA WA MILELE.
48 Mimi ndimi chakula cha uzima.
49 Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa.
50 Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife.
51 Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ATAISHI MILELE. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu."

  Maandiko hayo hapo juu  yanaonyesha wazi kabisa kuwa hakuna uzima wa milele mahali pengine popote nje ya BWANA YESU KRISTO, matunda ya porini siku zote hayajawahi kumpa mtu uzima wa milele, kwahiyo mtazamo wa kuwa matunda ya mti wa uzima ni matunda yafananayo na ya mwituni sio sahihi,(ni kukosa tu Roho ya mafunuo) kwasababu matunda ya kawaida hayawezi kutupa sisi uzima wa milele, biblia inasema hakuna wokovu wowote nje ya Yesu Kristo, Hivyo basi maana ya kula matunda ya mti wa uzima ni kulitafakari na kuliamini NENO la Bwana Yesu tu, na kusafishwa kwa damu yake ambaye yeye ndiye huo mti wa uzima. Na hili NENO la Mungu ndilo liletalo Utii,Upendo,Amani,Uvumilivu,Fadhili,Kiasi,Utakatifu,Utu wema,Hekima,Haki n.k. 

Wagalitia 5:22" Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria".


   3.Mti wa ujuzi wa mema na mabaya.
Kama tulivyouona mti wa pili, haukuwa mti wa kawaida kama ule wa kwanza, ndivyo ulivyo na huu pia, mti huu nao upo mmoja na umebeba tabia ya kipekee kwamba ukila matunda yake, utapata maarifa ya ujuzi wa mema na mabaya na ndio mti pekee Mungu aliomkataza mwanadamu asiule, alimwambia kabisa siku atakapokula tu matunda ya mti ule atakufa hakika. Lakini mwanadamu alikaidi  akala na ikapelekea hata sisi wote tukaingia katika hali ya laana ambayo tunayo mpaka sasa, lakini ashukuriwe Mungu njia ya mti wa uzima (YESU KRISTO) imeshafunguliwa tunao ukombozi wetu.

Huu mti asili yake ni mauti, na mauti inaletwa na shetani, kama vile uzima unavyoletwa na Yesu Kristo vivyo hivyo mauti inaletwa na shetani. Kwahiyo huu mti alikuwa ni "shetani" mwenyewe, na matunda yake ni "kwenda kinyume na NENO la Mungu" ndio huko unazaliwa uongo,uasherati,uuaji,ulevi,wizi,ulafi,sanamu,ufisadi,wivu, usengenyaji, n.k. ambayo mwisho wake ni mauti.

sasa kilichotendeka Edeni. shetani ambaye ndio ule mti wa ujuzi wa mema na mabaya, alimwingia nyoka. na nyoka akaenda kumdanganya Hawa kwa mafundisho yake ya uongo aliyoyatoa kwa baba yake shetani. kumbuka Mungu alimwonya mwanadamu adumu katika maagizo yake, asitafute maarifa mengine nje na Neno lake, lakini kwa kuwa shetani alijua mwanadamu anapenda maarifa ambayo Mungu alimkataza mwanadamu asiyatafute, na shetani siku zote ni mpingamizi wa Mungu hivyo alimjaribu katika hayo hayo, ndipo alipomwingia nyoka, na kumshawishi Hawa kutokumtii Mungu. na njia shetani aliyotumia ni ushawishi wa kufanya uasherati, kwa maana nyoka alimwambia ukila matunda haya utafanana na Mungu ukijua mema na mabaya. kumbuka kuwa nyoka hakuwa mnyama "reptilia" kama tunavyomwona leo, bali alikuwa ni mnyama anayekaribiana sana na mwanadamu, alikuwa na uwezo wa kuongea, kutafakari, alikuwa anatembea kwa miguu miwili, kwa ufupi alikuwa kama mtumwa wa mwanadamu.Baada ya kulaaniwa ndipo alipotembea kwa matumbo, na kula mavumbi.


nyoka alikuwa mnyama aliyekuwa anakaribiana sana na mwanadamu, mbali na wanyama wengine, katika wanyama wanaokaribiana na mwanadamu, alikuwa akitoka nyani anafuata nyoka kisha mwanadamu. tazama picha juu.


Kwahiyo baada ya nyoka kuingiwa na shetani na kwenda kufanya uzinzi na Hawa, Hawa naye akaenda kumpa tunda (kuzini) na mumewe, ikapelekea Hawa kubeba mimba ya mapacha wawili wasiofanana, akamzaa Habili na Kaini kila mmoja akiwa na baba yake. Baba yake Habili alikuwa ni Adamu na baba yake Kaini alikuwa ni nyoka. kumbuka nyoka hakuwa kama nyoka tunayemwona leo.(kwa ufafanuzi mrefu fuatilia somo langu liitwalo UZAO WA NYOKA.)

Tujue kuwa kitendo cha kula matunda ya porini kama peasi, embe au papai, hakuwezi kumfanya mtu ajione kuwa uchi, na kama walikula matunda yale kwa midomo hiyo midomo ndiyo ingetakiwa ilaaniwe na sio viungo vya uzazi, tunaona kabisa baada ya kula tunda (kuzini) walikimbilia kwenda kujifunika sehemu zao za siri, kiashirio kuwa hizo sehemu zao ndizo zilizohusika katika tendo lile.
Ni dhahiri kabisa kuwa mwanadamu ni vigumu kushawishika kwa matunda ya porini, kwa sababu alikuwa na matunda mengine mengi kwanini sasa aende kula lile la katikati ya bustani ya Edeni? Jibu ni dhahiri kuwa ni dhambi ile ile ya asili ambayo shetani alifahamu atampata nayo mwanadamu kirahisi na ndiyo hiyo hiyo anayowapata nayo wanadamu hata leo na hii sio nyingine bali ni dhambi ya uasherati.

Mungu ni yeye yule jana, na leo na hata milele, alichokichukia Edeni ndio hicho hicho anakichukia hata leo. Kama ilikuwa kula tunda kama tunda la kawaida ni makosa angeendelea kukichukia na kukikemea hicho kitu mpaka leo. lakini ni dhambi ya uasherati Mungu anayoichukia hata leo na ndiyo inayowaangusha watu wengi, kwa wanaojiita wakristo na wasio wakristo. kwahiyo hili tunda la kutokuliamini neno la Mungu (ambalo kwa mara ya kwanza shetani alilitangaza kwa kivuli cha uzinzi) hadi leo watu wanalila hili tunda. kama vile tu watu wa Mungu wanavyoendelea kula matunda ya mti wa uzima (kama tulivyosema ni kuliamini na kuliishi Neno la Mungu)  ili wapate uzima wa milele vivyo hivyo hadi leo watu wanaendelea kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya kama uasherati, n.k. kwa ajili ya mauti yao wenyewe. Akipandacho mtu ndicho atakachovuna.

Kwahiyo ndugu jambo lile lile lililotendeka Edeni linaendelea kutendeka hadi leo, je! unakula matunda ya ule mti wa ujuzi wa mema na mabaya huku ukijua kabisa Mungu amekataza usiyale ambayo tunayajua matunda yake ndiyo haya, uasherati, na mengine ni uongo, ulevi,ufisadi, usengenyaji, ushoga, ulafi, anasa, kuupenda ulimwengu, wizi, rushwa, tamaa mbaya, chuki, wivu, n.k. unafahamu kabisa mwisho wa haya ni mauti kama Mungu alivyosema pale Edeni, siku utakapokula matunda hayo utakufa hakika. Apple haliwezi likakufanya ufe! na biblia inasema mshahara wa dhambi ni mauti. Kimbilia kwa Yesu sasa ukale matunda ya Mti wa uzima, upate uzima wa milele, Bwana Yesu alisema itakufaidia nini uupate ulimwengu mzima na kupata hasara ya nafsi yako au utatoa nini badala ya nafsi yako. Kuzimu ipo, tazama miti miwili ipo mbele yako, chagua moja MTI WA UZIMA au MTI WA MAUTI. 

warumi 6:16 Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.

 Chaguo lipo kwako. Wakati umekwenda sana na mlango wa neema unakaribia kufungwa, je! umejiweka tayari.?? Umejazwa Roho Mtakatifu,??

Neema ya Mungu iwe pamoja nawe.

Thursday, January 12, 2017

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

Mathayo 24:32-35 " 32 Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu;
33 nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.
34 Amin, nawaambia, KIZAZI HIKI HAKITAPITA, hata hayo yote yatakapotimia.
35 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. 


Mambo haya Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake walipokuawa wameketi katika mlima wa Mizeituni, akiwaonya mambo yatakayokuja kutokea siku za mwisho kabla ya kurudi kwake, yakaandikwa kwaajili yetu sisi tusiwe gizani ili wakati huo ukifika mambo hayo yasitujie  kama mwivi. Yapo mambo mengi Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake kama tunavyoyaona katika vitabu vya injili na vitabu vingine kuhusu siku za  mwisho zitakavyokuja kuwa.

Lakini katika kitabu cha mathayo 24 Bwana Yesu alisema katika siku za mwisho kutatokea vita na matetesi ya vita (mathayo 24:6), Hii ni sahihi hivi vita tumekuwa tukiviona vikipiganwa kwa karne na karne kati ya mataifa na mataifa, lakini vita vingi na vikubwa vimekuja kukithiri zaidi katika karne ya 20 na 21,tunaona mfano wa vita vya kwanza (1914-1918) na vya pili vya dunia (1939-1945) ambavyo vimesababisha mauaji ya mamilioni ya watu ulimwenguni kote, kitu ambacho hata hakijawahi kuonekana katika historia ya vizazi vyote vya nyuma., lakini Bwana alieleza wazi  yatakapoanza kutokea haya msitishwe ule mwisho bado,alisema kuwa huo ndio mwanzo wa utungu.

Bwana Yesu alisema pia siku za mwisho kutakuwa na njaa (mwilini na rohoni), matetemeko ya nchi, kutakuwa na magonjwa mengi, mambo ambayo tumekuwa tukiyaona kila kukicha matetemeko kila mahali, magonjwa mapya yanazuka kila siku((kama cancer, kisukari,presha,zika,ukimwi,ebola,sars,kimeta, n.k) ambayo hayakuwepo katika vizazi vya zamani, lakini haya yote Bwana Yesu pia  alisema ni mwanzo wa utungu, kwamba ule mwisho unakaribia lakini bado haujafika.

Jambo lingine Bwana Yesu alilolisema ni kuwa manabii na makristo wengi wa uwongo watatokea na kuwadanganya wengi, Kila mtu anafahamu kama tunavyowaona leo mafundisho mengi ya uwongo yamezagaa kila mahali, alisema pia upendo wa wengi utapoa, ni dhahiri kabisa upendo(shauku) ya watu kumpenda Mungu na kupendana wao kwa wao imetoweka,na tamaa mbaya za ulimwengu huu zimewasonga watu na kumsahau Muumba wao, alisema pia watu watakuwa wakijipenda wenyewe, wakisalitiana na kuchukiana.

Aliwaambia wanafanzi wake pia,
luka 21:20-24  " Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia.
21 Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.
22 Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.
23 Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.
24 Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia.".
 Hili jambo lilitimia kama lilivyo mwaka 70AD pale majeshi ya Rumi yalipouzunguka mji wa Yerusalemu na kuharibu mji na hekalu kuliteketeza kwa moto, na wayahudi wote waliokuwa wamesalia Yerusalemu walitawanywa katika mataifa yote duniani hivyo basi Izraeli wakawa wageni katika mataifa mengine, mpaka Mungu alipowarejesha tena nchini kwao mwaka 1948 kuwa kama taifa huru tena linalojitegemea.

Mwisho  Bwana Yesu alisema habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. 

Lakini hapa kuna jambo kuu na la muhimu sana tunatakiwa tulione,
 Tukisoma katika mathayo 24:32-35 na  Luka  21:29-33 inasema "29 Akawaambia mfano; Utazameni mtini na miti mingine yote.
30 Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu.
31 Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu.
32 Amin, nawaambieni, KIZAZI HIKI HAKITAPITA, HATA HAYO YOTE YATIMIE.
33 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe. 

 Alisema kwa mtini jifunzeni, "Mtini" siku zote kwenye biblia unawakilisha Taifa la Izraeli,(soma yeremia 24), na aliposema utazameni mtini na miti mingine,hii miti mingine ni mataifa mengine, sasa aliposema mtini utakapoanza  kuchipua alikuwa na maana Taifa la Israel kuzaliwa tena upya baada ya kukaa katika mataifa mbalimbali kwa muda mrefu. Tunaona jambo hili lilitimia mwaka 1948 pale Izraeli waliporejea katika nchi yao wenyewe kama ilivyotabiriwa na Bwana, hiyo ndiyo maana ya kuchipuka kwa Izraeli. Hivyo basi kuanzia huo mwaka wa 1948 mpaka sasa tunaona mataifa mengi yalianza kupata uhuru wao ikiwemo mataifa karibu yote ya Afrika, baadhi ya Asia na Marekani ya kusini hii inatimiza ule unabii Yesu aliosema mjifunze pia  kwa miti mingine (miti mingine ni sisi mataifa mengine mbali na Izraeli).

Taifa la Izraeli likisherekea siku ya uhuru wao 1948


Sasa baada ya mtini kuchipuka(Izraeli) hapo ndipo Bwana aliposema  "Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe."

Hichi kizazi kinachozungumziwa hapa sio kile kizazi cha Yesu alichokuwa anazungumza nacho, bali ni kile kizazi kilichoshuhudia Izraeli ikichipuka yaani Izraeli kuwa Taifa huru tena kama ilivyokuwa hapo mwanzo zaidi ya miaka 2500 iliyopita.

Na kizazi kilichoshuhudia hayo ni kuanzia watu waliozaliwa mwaka 1948 na kuendelea hadi sasa, kwahiyo tumeshafahamu kuwa kizazi cha wale waliozaliwa mwaka 1948 Bwana Yesu ndicho alichosema hakitapita. Na tunajua kizazi mpaka kitoweke kabisa katika dunia ni miaka 100,kwa dunia ya sasa, tukiangalia tangu mwaka 1948 hadi leo ni miaka 69 imeshapita, na hapa Bwana Yesu alisema kizazi hiki hakitapita hakusema kitatimia ndio mwisho uje bali alisema hakitapita, kwahiyo hii ina maanisha hapa hapa katikati kabla ya kufikia hicho kipindi cha kizazi kutoweka Bwana Yesu Kristo atakuwa ameshakuja, ni wazi kabisa wengi waliozaliwa chini ya mwaka 1948 ni asilimia 7% tu inayoishi duniani sasa (kwa mujibu wa takwimu za dunia), kwahiyo hili rika la hawa watu linakaribia kupotea, lakini Bwana Yesu Kristo aliapa kuwa hili rika halitapita,

aliweka msisitizo kabisa akasema Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe."..

Na baada ya hapo ndipo Bwana Yesu aliposema mtakapoona hayo yanaanza kutokea tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu, kwa hiyo ndugu tambua hilo wewe unayesema bado sana Yesu kurudi, wewe ambaye unasitasita kwenye mawazo mawili, maneno haya yanaonyesha wazi kabisa kuwa kuja kwa Bwana kuko mlangoni, Baada ya hayo maneno Bwana Yesu Kristo alimalizia kwa kusema 
" Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
35 kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima.
36 Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu."

Bwana Yesu Kristo hakutoa muda wala saa ya kuja kwake lakini alitupa majira kwamba yatakapokuja yasitujie kama mwivi au kama mtego unasavyo, je! wewe ambaye unatambua kabisa tunaishi katika kizazi ambacho tutashuhudia kuja kwa Yesu Kristo mara ya pili, umejiwekaje tayari, umebatizwa kweli kwa Roho Mtakatifu?? umeufanya imara kweli uteule wako na wito wako? Bwana Yesu akija leo una uhakika wa kwenda naye??.

Huu ni wakati wa wale wanawali werevu kutengeneza taa zao kwenda kumlaki Bwana Yesu, je! na wewe una uhakika kuwa taa yako iko sawa?? Tambua ya kuwa Bwana akija leo na taa yako haipo sawa utabaki hapa na kuingia katika ile dhiki kuu? Kumbuka ujumbe huu unakuhusu wewe mkristo unayesema umeokoka, kumbuka wale walikuwa wote ni wanawali na wote walikuwa wanamsubiria Bwana wao isipokuwa watano walikuwa werevu na watano walikuwa wapumbavu (mathayo 25) kwahiyo hao wanawali  10 wote ni wakristo na sio watu wasioamini, fahamu tu uchungu utakuwa kwa wale ambao walidhani wangeenda katika unyakuo lakini wakabaki, na sio wale wasioamini, hivyo ndivyo itakavyowakuta wakristo wote ambao ni vuguvugu sasa wanachofahamu tu ni madhehebu yao lakini hawataki kumjua Kristo katika neno lake, hawataki kujazwa Roho Mtakatifu ili awaongoze katika kweli yote uteule wao uwe wa uhakika, Roho Mtakatifu ndio muhuri wa Mungu (waefeso 4:30) pasipo Roho Mtakatifu hakuna unyakuo. je! wewe ni mmoja wa wanawali mwerevu au mpumbavu? wanawali wote werevu wanajivunia kuwa wakristo wa NENO na sio wakristo wa madhehebu, wanawali wapumbavu wanaona aibu kuitwa wakristo, wanajivunia madhehebu ukimwuliza yeye ni nani atakwambia mimi ni mlutheri,mkatoliki,msabato,mbranhamite,m-eagt,morovian., hawafahamu jambo lingine lolote nje ya madhehebu  yao, ukiwaambia biblia inasema hivi wanasema dhehebu letu halifundishi hilo, 

Lakini BWANA YESU KRISTO leo anatuita tuwe WANAWALI WEREVU(SAFI).....na ujumbe tulionao sasa kwa wakati wetu ni ufunuo 18:4 "4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake. Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake."   Jihadhari na mafundisho ya uongo.

Ndugu tubu, mgeukie Bwana muda ndio huu, usidanganyike na mafundisho yanayosema kuwa Kristo bado sana kurudi.

Mungu akubariki!