"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Thursday, January 26, 2017

MASWALI YALIYOULIZWA NA MAJIBU YAKE: SEHEMU YA 10


SWALI 1: Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi?

JIBU: Tukisoma;

Mathayo 12:25-32 " Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo.
25 Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama.
26 Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?
27 Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu.
28 Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.
29 Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake.
30 Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
31 Kwa sababu hiyo nawaambia, KILA DHAMBI, NA KILA NENO LA KUFURU, watasamehewa wanadamu, ILA KWA KUMKUFURU ROHO HAWATASAMEHEWA.
32 Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. "

Tunavyosoma mistari hiyo tunaona kabisa wale Mafarisayo  walikuwa wanajua Bwana Yesu  ni kweli alikuwa anatoa pepo, na kutenda mambo yote  kwa uweza wa  Roho wa Mungu, lakini wao kwa ajili ya wivu, na kwa tamaa zao wenyewe,ili tu wawavutie watu kwao, wakakusudia kwa makusudi kabisa, wawageuze watu mioyo ili watu wasimuamini Bwana Yesu,wawaamini wao, na ndipo wakaanza kutoa maneno ya makufuru wanawaambia watu kuwa BWANA anatoa pepo kwa uwezo wa belzebuli mkuu wa Pepo angali ndani ya mioyo yao walikuwa wanajua kabisa anachofanya ni kwa uweza wa Roho wa Mungu.

  Ukweli wa jambo hilo unajidhihirisha   kwa Nikodemo ambaye naye alikuwa ni mmoja wa wale  mafarisayo alipomwendea Yesu usiku na kumwambia

Yohana 3:1-2"Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi.
2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, RABI, "TWAJUA" YA KUWA U MWALIMU, UMETOKA KWA MUNGU; KWA MAANA HAKUNA MTU AWEZAYE KUZIFANYA ISHARA HIZI UZIFANYAZO WEWE, ISIPOKUWA MUNGU YU PAMOJA NAYE. "

kwahiyo unaona walikuwa wanajua kabisa lakini kwa ajili ya wivu wakaanza kuzusha maneno ya uongo juu ya kazi ya Roho wa Mungu, sasa huko ndiko kumkufuru Roho Mtakatifu. hivyo basi Bwana Yesu alitoa angalizo tunapozitazama kazi za Mungu, pale mtu mwenye Roho wa Mungu anatenda kazi za Mungu kweli  huku tunajua ni Mungu ndiye anayefanya kazi ndani yake, na kuanza kusema yule ni mchawi, au anatumia uchawi, au mshirikina, au tapeli, au mwizi, ili tu watu wasiziamini kazi za Mungu au vinginevyo, au unaanza kuzusha propaganda za uongo juu yake, pengine kwa kusudi la kumkomoa! hapo ndugu utakuwa unajimaliza mwenyewe. (Ni kweli si watumishi wote ni wa Mungu,hao ni sawa kuufunua uovu wao). Lakini Hapa tunamzungumzia yule unayemfahamu kabisa ni mtumishi wa BWANA,..wewe hujui umewakosesha wangapi, ambao kwa kupitia yeye, watu wengi wangeokolewa? kufanya hivyo ni hatari sana tuwe makini.

Hivyo hii dhambi unawahusu wale wanaozipinga kazi za Mungu kwa makusudi kabisa(Mfano wa mafarisayo). Hao kwao hakuna msamaha, hawawezi tena kutubu hata iweje wanachongojea ni ziwa la moto.

Lakini shetani naye anapenda kulitumia hili neno kuwafunga watu wajione kuwa wamemkufuru Roho Mtakatifu na kwamba dhambi zao hazisameheki hata wafanyeje,

Hii inakuja sana sana kwa watu waliowachanga ki-imani, kuna shuhuda nyingi za watu waliofungwa na shetani kwa namna hiyo wakidhani kuwa dhambi zao hazisameheki, kuna watu wamekata tamaa wanajiona kwa wingi wa dhambi zao, Mungu hawezi kuwasemehe tena, pengine wameua, wametoa mimba sana, n.k, Sasa jambo la namna hii likija katika mawazo yako likatae linatoka kwa yule mwovu kukufanya wewe ujione kuwa Mungu hawezi kukusamehe umemkufuru, hivyo usijisumbue kutubu kwasababu Mungu hatakusikiliza.

Kumbuka kama tulivyosema Dhambi hii inakaa kwa wale watu ambao ndani yao mioyo ya toba imekufa, au hofu ya Mungu haipo tena kwao, watu waliojikinai, wanaompinga Mungu katika fikra zao japo kuwa walimjua Mungu na uweza wake wote, wanazipotosha kazi za Mungu kwa makusudi kwa faida zao wenyewe,ili wawavute watu kwao, au wawe washirika wao na sio kwa Mungu. Hivyo basi kitendo tu cha wewe kuwa na hii hofu ya kumwogopa Mungu ujue Roho wa Mungu anatenda kazi ndani yako na hayo mawazo ya kwamba umemkufuru Roho Mtakatifu yapinge huyo ni adui ndio moja ya njia zake hizo ili usiufikie wokovu  na anapenda kuwatesa watu wengi katika andiko hili.

SWALI 2: Je!  Kuna dhambi kubwa na ndogo, na kama hakuna je! Mtu aliyeua na aliyetukana je watapata adhabu sawa?

JIBU: Dhambi ni dhambi iwe kubwa au ndogo, zote ni kosa, biblia inasema. 

Yakobo 2:10-11 "Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.
11 Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria. "

Unaona hapo? Kwahiyo mtu akitenda dhambi iwe kubwa au ndogo ataadhibiwa. lakini adhabu zitatofautiana huko waendako, kwasababu  Bwana Yesu pia alisema aliyeua kwa upanga atauawa kwa upanga, apandacho mtu ndicho atakachovuna. adhabu ya shetani haiwezi ikawa sawa na adhabu ya mwanadamu. Biblia inaeleza..

luka 12:47-48"Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, ATAPIGWA SANA.
48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, ATAPIGWA KIDOGO. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi. "

kwahiyo mapigo yanatofautiana kulingana na matendo ya mtu aliyoyatenda akiwa hapa duniani, ni kama tu vile thawabu zitavyotofautiana kwa mtu na mtu mbinguni kwa jinsi alivyotaabika katika kumtumikia Bwana vivyo hivyo na jehanamu adhabu zitatofautiana kulingana na dhambi mtu alizotenda akiwa ulimwenguni. Hivyo hatupaswi kuipima dhambi kwa namna yoyote, ni kukaa nayo mbali kwasababu  iwe ni kubwa au ndogo mshahara wake ni MAUTI, warumi 6:23.

SWALI 3:
Katika amri kumi za Mungu, Amri ya sita inasema "usiue" lakini sisi tunaua baadhi ya viumbe kwa ajili ya kitoweo n.k. sasa basi ni nini tunapaswa kuua na ni kipi hatupaswi kuua?

JIBU: tangu mwanzo haikuwa mapenzi ya Mungu sisi kuua kiumbe chochote kwa matumizi yoyote yale, lakini baada ya anguko Mungu aliyaruhusu hayo yatendeke kwa makusudi maalumu kama kwa ajili ya chakula, mavazi, na matumizi mengine yoyote ambayo ni halali. Na ndio maana tunaona hata baada ya Adamu kuasi Mungu alikuwa wakwanza kuwachinjia mwanakondoo na kuwavika ngozi yake kama mavazi. Na pia tunaona wanyama walichinjwa kwa ajili ya kumtolea Mungu sadaka ya kuteketezwa n.k.
Hivyo basi kwa kuua mnyama yeyote kwa ajili ya matumizi maalumu kama kwa chakula au vinginevyo sio dhambi lakini utakapomuua bila sababu yoyote maalumu, Mungu atakuhesabia makosa. kwahiyo hapo unaona kikubwa ni sababu(motive) ya wewe kumuua huyo mnyama. Utakuta mtu anamuua mnyama pasipo sababu yoyote na hana madhara yoyote katika jamii, wengine wanawaua wanyama kwasababu wanawachukia tu. Lakini kuna faida na thawabu nyingi tunapowahurumia wanyama na kuwatunza ikiwemo kuongezewa siku za kuishi soma;
kumbukumbu 22:6" Kiota cha ndege kikitukia kuwa mbele yako njiani, katika mti wo wote, au chini, chenye makinda au mayai, naye koo ameatamia juu ya makinda, au juu ya mayai, usimtwae yule koo pamoja na makinda;
7 sharti umwache yule koo aende zake, lakini makinda waweza kuyatwaa uwe nayo; ili upate kufanikiwa, ufanye siku zako kuwa nyingi. " umeona kwa kufanya hivyo tu Mungu anakuongezea siku zako za kuishi.
lakini haya yote ya kuua, kuchinja n.k. Mungu ameyaruhusu kwa muda tu, tutakapokuja kutawala na Kristo hapa duniani kwa muda wa miaka 1000, mambo yote yatarejeshwa kama ilivyokuwa Edeni ya mwanzo, kutakuwa hakuna kuua wanyama. Na wanyama pia hawatauana tutaishi wote kwa amani. soma..
isaya 11:6-9 "  Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.
7 Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe.
8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.
9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari. " 

Na pia tukisoma warumi 8:19"19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu.
20 Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye atiyevitiisha katika tumaini;
21 kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
22 Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa."

kwahiyo haya mambo ya kuua wanyama ni ya muda tu. unaweza ukaua chochote (ila sio mtu), lakini kiwe ni kwasababu maalumu tu na si vinginevyo zaidi ya hapo ni dhambi. 
Mungu akubariki.

No comments:

Post a Comment