"Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake...ufunuo 16:15"

Tuesday, January 17, 2017

UZAO WA NYOKA.

Karibu tujifunze Neno la Mungu....Tumezoea kula vyakula vilaini, kila siku maziwa, , tutakua lini?? Ni vizuri tuanze kujifunza kula vyakula vigumu pia ili tukue tuzidi kumjua Kristo katika utimilifu wake wote, Leo tuutazame uzao wa nyoka mwanzo wake na ulipofikia sasa kwa msaada wa Kristo..

Mathayo 12:34 "Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake"
Mahali pengine Bwana Yesu alisema:
mathayo 23:31-33 "Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii.
32 Kijazeni basi kipimo cha baba zenu.
33 Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?"

   
Na Yohana mbatizaji aliyarudia haya maneno, tunayaona kwenye luka 3:7 " Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?" 


 
Maneno haya yanathibitisha kuwa uzao wa nyoka upo, na ndio umekuwa adui wa uzao wa Mungu tangu vizazi hata vizazi, Tuufatilie huu uzao wa nyoka umeanzia wapi, na chimbuko lake ni wapi, na ni akina nani hawa wanaitwa uzao wa nyoka?.

Tumeona jinsi mti wa uzima na mti wa ujuzi wa mema na mabaya una maana gani, kama hujafahamu soma somo nililoliandika kabla ya hili " MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA" ili tuteremke vizuri pamoja.


Tunafahamu kuwa kitendo kilichotendeka kwenye bustani ya Edeni ni kwamba Hawa alifanya uasherati na nyoka kisha akaenda kufanya na mume wake ikapelekea Hawa kubeba mimba ya watoto wawili mapacha wasiofanana, kila mmoja akiwa na baba yake tofauti, Habili baba yake akiwa ni Adamu na Kaini baba yake akiwa ni nyoka. 


Jambo hili linawezekana kibaolojia na ni jambo la kawaida linalotokea mara kwa mara duniani, kwamba mama mmoja ana uwezo wa kukutana kimwili na wanaume wawili tofauti na kusababisha kubeba mimba ya watoto wawili wa baba tofauti tazama picha hapa chini,

Ni dhahiri kuwa nyoka hakuwa kama jinsi tunavyomuona leo akitambaa kwa tumbo, hana mikono wala miguu bali alikuwa hivyo baada ya kulaaniwa, lakini kabla ya kulaaniwa alikuwa ni mnyama anayekaribiana sana na mwanadamu soma mwanzo 3:14, hivyo baada ya mwanadamu alikuwa anafuata nyoka kisha nyani, kisha wanyama wengine, kwahiyo nyoka alikuwa ana uwezo wa kuzungumza kama mwanadamu,kutafakari, na alikuwa na mikono na miguu miwili kama mtu, Mungu alimuumba kwa kusudi la kumsaidia mwanadamu katika shughuli zake za karibu na kama biblia inavyosema amelaaniwa kuliko wanyama wote ina maanisha alikuwa juu ya wanyama wote na alikuwa mwerevu mbali na wanyama wengine.


Lakini tunaona shetani baadaye alikuja kumwingia nyoka na kwenda kumdanganya Hawa asimtii Mungu ikapelekea kwenda kufanya kitendo cha uasherati. mwanzo 3:20 "Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai." biblia ilimwita Hawa kuwa mama wa wote walio hai lakini haikumwita Adamu baba wa wote walio hai. Hii ikiwa na maana kwamba wote walitoka kwa Hawa lakini sio wote waliotoka kwa Adamu.


Jambo linalowachanganya wengi ni pale mwanzo 1:4 inaposema"1 Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana.
2 Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.
3 Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana."
Hapa tunaona Adamu alimjua Hawa mara moja tu, na sio mara mbili, maana alimzaa Kaini akamwongeza na Habili ni kitendo kimoja kimezaa watoto wawili ambao ni pacha wasiofanana,kitendo cha "kuongeza" hakimaanishi "kumjua" tena. Na pia tukichunguza kitabu cha mwanzo jinsi kilivyoandikwa matukio hayajakaa katika mfululizo, huwa kuna kwenda mbele na kurudi nyuma. kwamfano ..*Kwenye sura ya kwanza Mungu aliziumba mbingu na nchi na miti na wanyama, na wanadamu huko huko(mwanamke na mwanaume) akamaliza kila kitu na siku ya 7 akapumzika,

* Lakini kwenye sura ya pili tunaona tena Mungu anamwumba Adamu tena kutoka ardhini, na Hawa akaja kumuumba baadaye kutoka kwa Adamu, kitendo ambacho tunajua kilishakamilika tangu sura ya kwanza, vivyo hivyo na mimea na wanyama, waliumbwa kutoka ardhini tena.


* Vivyo hivyo kwenye sura ya tatu inaeleza Adamu na Hawa walivyokula tunda na kufukuzwa katika bustani ya Edeni,

*Lakini sura ya nne inaelezea ni jinsi gani Adamu Alivyokula lile tunda kwa kumjua mkewe na kupata mimba na kuzaa watoto wawili.


Hivyo basi Kaini alipozaliwa alibeba tabia za baba yake nyoka na ndio maana tunaona tu baada ya kutoka bustanini alimwamkia ndugu yake na kumuua,hakuwa hata na muda wa kutubu, wivu na hasira vilimtawala hivyo tujiulize alivitolea wapi hivi? kwanini ndugu yake Habili hakuwa navyo jibu ni dhahiri kabisa alivibeba kutoka kwa baba yake nyoka, tunaona ni ile ile roho ya shetani ambayo ilitenda kazi ndani ya nyoka mwanzoni ndiyo inayotenda kazi ndani ya Kaini. 


Jambo hili hili tunaona likizidi kuendelea katika uzao wa Kaini, ukifuatilia vizuri utaona Lameki mzao wake alikuwa ni muuaji kushinda hata baba yake Kaini mwanzo 4:23-24"3 Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;
24 Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba.
" na pia tunaona tabia nyingine za kuoa wanawake wengi zilitokea katika huu uzao wa Kaini(ambao ni uzao wa nyoka). Lameki alioa wake wawili kitu ambacho Mungu hakumwagiza Adamu wala uzao wake wala hakikuonekana mahali popote katika uzao wa Mungu.


Pia tunaona huu uzao kutoka kwa baba yao Kaini Mungu aliwatia alama, baada ya Kaini kumuua ndugu yake


mwanzo 4:13-15 " Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.
14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.
15 Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. "

Kwahiyo hii alama Bwana aliyomtia Kaini sio alama kama chapa fulani kwenye mwili wake (tatoo) , Bali Mungu alimwongezea ukubwa wa mwili wake na akili nyingi (inteligency) yeye na uzao wake, tunaona katika kipindi cha Nuhu ule uzao wa Kaini ulikuwa ni wa watu wakubwa walioitwa "majitu (wanefili)" kwahiyo kwa ukubwa huu mtu yeyote asingeweza kupigana nao au kuwatishia, na kwenye upande wa akili tunaona katika mwanzo 4 wana wa Kaini walianza kuwa na ustaarabu mkubwa kwa haraka kama ugunduzi wa vyuma, shaba, ustadi wa vyombo vya miziki n.k.waliitwa watu hodari na wenye sifa wakati ule (soma mwanzo 6:4) inaelezea..wao ndio waliotengeneza mapiramidi ambayo yamesimama mpaka leo, kama tunavyojua hata leo taifa lenye ujuzi mwingi kwa teknolojia kubwa ni dhahiri kuwa taifa hilo litaogopeka na hakuna mtu atayakayedhubutu kwenda kulidhuru ndivyo ilivyokuwa kwa Kaini na uzao wake, Mungu alimpa ukubwa na ujuzi mwingi ambao ulikuwa kama ulinzi kwake ili mtu atakapomuona asimdhuru..


Lakini ule uzao mwingine wa Adamu ambao ni uzao wa Mungu wao walikuwa ni wafugaji tu na wakulima, na walikuwa ni wanadamu wenye miili ya kawaida. hawakuwa hodari katika nchi, mtazamo wao ulikuwa kwa Mungu na ndio maana tunaona walianza kuliitia tu jina la Mungu pale walipoanza kukaa katika nchi,

mwanzo 4:25-26" Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.
26 Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana. "

Tunaona katika kipindi hicho chote uzao wa Adamu ulikuwa dhahiri na unaonekana na uzao wa nyoka pia ulikuwa dhahiri na unajulikana kwa tabia na kwa kuutazama. Wana wa Adamu wote walikuwa wanaitwa ''WANA WA MUNGU'' na wana wa Kaini walikuwa wanaitwa "WANA WA BINADAMU" kulingana na
mwanzo 6:1-4 " Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,
2 wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.
3 Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.
4 Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile;tena ,baada ya hayo ,wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu,wakazaa nao wana;hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani ,watu wenye sifa. "
Kuna baadhi ya mitazamo inayosema kuwa hawa wana wa Mungu walikuwa ni malaika, na kwamba walikuja na kuzini na wanadamu, ndipo wakazaliwa wanefili lakini mtazamo huo sio kweli kwasababu, kwanza tunaona wanafili walikuwepo duniani kabla hata ya hao wana wa Mungu kuzini na binti za binadamu, na pia malaika hawana miili zile ni roho zitumikazo (waebrania 1:14), Hivyo hawawezi kukutana kimwili na wanadamu, lakini pia tunaona baada ya wana wa Mungu kuzini ni binti za binadamu Mungu aliwahukumu wanadamu na sio malaika kuonyesha kuwa wanadamu ndio waliohusika na hicho kitendo na sio malaika (mwanzo 6). tuendelee kujifunza..

 
Baada ya watu kuongezeka na kuwa wengi duniani, wana wa Mungu(uzao wa Adamu) waliwatamani binti za wanadamu(binti za Kaini) waliwaona ni wazuri, wenye mitindo ya kisasa, wanaopaka lipstick,wanaovalia nusu-uchi,wanaopaka wanja, wenye ujuzi wa kujipamba kwa manukato ya kila aina,waliojaa macho ya uasherati na ukahaba,wanaoenda na wakati(fashion) kwa mitindo ya kisasa huu ni mfano tu dhahiri wa wanawake tulionao sasa. Waliacha kwenda kuoa wake zao(binti za Mungu) ambao walikuwa ni wacha Mungu,wastaarabu, wanaojiheshimu kwa mavazi na tabia njema, mabikira, wasioendana na fashion za ulimwengu, lakini wao wakawaona kama washamba, hawafai, wakaenda kujitwalia binti za wanadamu wakazaa nao watoto Ikapelekea kuchanganya mbegu, wana wa Mungu wakaacha kumwangalia BWANA tena, wakaanza kuupenda ulimwengu kitu kilichomkasirisha sana Mungu na ndipo Bwana akaghairi na kusema Moyo wangu hautashindana na mwanadamu milele,basi maovu yakaendelea kuzidi kuwa mengi duniani, vitendo viovu, ukatili,ushoga,uuaji, usengenyaji, uzinzi, ulevi,rushwa kukawa hakuna tena wacha Mungu, Dunia ikaharibika sana, mambo yasiyofaa yaliujaza ulimwengu kama siku zetu hizi za leo, maana Bwana alisema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu ndivyo itakavyokuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu. Na ndipo hapo Mungu akakusudia kuiteketeza dunia katika gharika.


Lakini Nuhu ambaye alikuwa ni wa uzao wa Mungu (uzao wa Adamu) alipata neema, japo na yeye alikuwa na mke aliyechanganyikana na uzao wa Kaini, na kusababisha kupata watoto wale watatu waliochanganyikana Hamu,Shemu na Yafethi..Tunafahamu Bwana Mungu aliuangamiza ule uzao wote halisi wa nyoka kwenye gharika, Ule uzao wote uliondoka Hakukuwa tena na uzao halisi wa nyoka baada ya pale, lakini kutokana na kile kitendo cha kuchanganyikana mbegu kulisababisha na wana wa Mungu kubeba zile tabia za nyoka ndani yao, japo hawakutoka katika ule uzao wa nyoka. na ndio maana tunaona zile tabia ambazo zilikuwa kipindi cha nyuma zilianza kujidhihirisha tena katikati ya wale watoto, tunafahamu Hamu alikuja kuuona uchi wa baba yake,(kulala na mama yake) hii ni dhahiri kuwa haikuwa tabia ya uzao wa Mungu lakini kwasababu mbegu zimeshachanganyikana sio jambo la kushangaza vitendo kama hivyo vya wanyama kutokea maana wanyama ndio wanaolala na mama zao, hivyo kwa nje mtu anaweza akaonekana kuwa ni mwanadamu lakini ndani anayo ile asili (mbegu) ya nyoka.


Na tabia hizo hizo zikaendelea kwa vizazi vyote hadi kufikia wakati wa agano jipya Bwana Yesu Kristo alipoifichua hii "SIRI YA UASI " alipowaambia watu ni wa uzao wa nyoka, sasa unaona asili ya huu uzao wa nyoka umetokea wapi, mtu yeyote ambaye hajazaliwa mara ya pili haijalishi wewe ni nani una asili ya nyoka ndani yako fahamu tu wewe ni mzao wa nyoka, na mtu atauliza nitafahamuje kama mimi ni mzao wa Mungu au uzao wa nyoka? jibu ni rahisi kabisa kama haujazaliwa mara ya pili wewe ni mzao wa nyoka, na uzao wa nyoka wote utateketezwa kwenye lile ziwa liwakalo moto na kiberiti.


Mungu aliiumba mbegu halisi ya mwanadamu lakini baada ya Adamu kuiharibu ile mbegu halisi kwa kuichanganya na mbegu nyingine ikapelekea wote tuingie katika hali ya uharibifu na mauti, hivyo basi Mungu alimuumba Adamu wa pili yaani Yesu Kristo kwa mbegu nyingine isiyoweza kuchanganyikana ili tukizaliwa katika yeye tupate uzima wa milele 1 petro1:23"
Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele. " unaona jinsi ilivyo muhimu kuzaliwa mara ya pili?? Bwana Yesu alisema

yohana 3:3-5"
3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?
5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu."
  
Je! umabatizwa kwa maji na kwa Roho ipasavyo? kubatizwa kwa maji ni kuzamishwa na ni katika  jina la BWANA YESU KRISTO  kulingana na matendo 2:38, na pia unapaswa ubatizwe kwa Roho Mtakatifu(huko ndiko kuzaliwa mara ya pili) ambao huo ndio utimilifu na muhuri wa Mungu juu yako kulingana na waefeso 4:30, biblia inasema wote wasio na Roho wa Mungu hao sio wake warumi 8:9" Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake." kwa hiyo Roho wa Mungu tu peke yake ndiye anayeweza kutoa asili ya uzao wa nyoka ndani ya mioyo ya watu. usijidanganye kwa namna yoyote kuwa unatenda matendo mema, unaenda kanisani, unatoa fungu la 10,unasaidia yatima n.k ukidhani unampendeza Mungu, ndugu kama haujazaliwa mara ya pili kwa ubatizo wa Roho Mtakatifu hauwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni.

Maombi yangu ni wewe ujazwe ROHO MTAKATIFU,
naomba umalizie kwa kusoma kifungu kifuatacho:


Luka 11:9-13" Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
10 Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
11 Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?
12 Au akimwomba yai, atampa nge?
13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

Mungu akubariki.

 

5 comments:

 1. Nimebarikiwa sana Mwalimu. Natamani nikufahamu sana. +255716724193 Wakili/ Mwl.Lenhardt Kyamba

  ReplyDelete
 2. Mtumishi unajua asante sana Mungu akulinde

  ReplyDelete
 3. Amen naguswa na mafundisho Yako .

  ReplyDelete
  Replies
  1. Ubarikiwe Sana mtumishi wa Bwana

   Delete